2Samuel 13:11-13 “Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa.”
Utangulizi
Mojawapo ya tatizo ambalo
limeleta majuto makubwa sana duniani na kuwaingiza wanadamu wengi kwenye
changamoto mbalimbali ni pamoja na Upumbavu!, amini usiamini upumbavu
umegharimu maisha ya watu wengi sana, na ni kupitia upumbavu aidha wa kwetu
wenyewe au wa mtu mwingine, wengi wetu tumejikuta katika matatizo na changamoto
zilizogharimu maswala kadhaa katika maisha, na ndio maana unaweza kuona
maandiko matakatifu yakisisitiza sana umuhimu wa kuitafuta hekima kwa gharama
yoyote ile kwa sababu hekima ni bora sana kuliko madini yoyote yale ya thamani
zikiwemo rubi au marijani, Hekima inasimama kama njia ya kutusaidia kuvuka
katika dunia hii salama.
Mithali 8:10-11 “Pokea mafundisho yangu,
wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi. Maana hekima ni bora kuliko
marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.”
Kwa msingi huo tunapojifunza somo
hili lenye kichwa “Wewe nawe utakuwa
kama mmoja wa wapumbavu?” Maana yake ni nini? Maana yake leo tutazungumzia
kwa kina na mapana na marefu jinsi tunavyoweza kukwepa kufanya upumbavu tukiwa
hapa duniani na hatimaye kuona umuhimu wa kumuomba Mungu na kuifuata njia ya
Hekima ili tuweze kufanikiwa katika maisha haya na yale yajayo, tutajifunza somo hili Wewe
nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu ? kwa kuzingatia vipengele vitatu
viafuatavyo:-
·
Maana ya
neno Upumbavu
·
Wewe nawe
utakuwa kama mmoja wa wapumbavu?
·
Chagua
Hekima!
Maana ya neno Upumbavu
Neno upumbavu katika lugha ya
kiingereza linaelezewa kwa misamiati mingi sana kama vile fool, lacking of good sense, lacking of good judgement, unwise, stupid,
silly, Idiotic, na kadhalika, lakini neno maarufu sana linalotumika katika
Biblia hususani agano la kale ambalo limeletwa kwetu kwa lugha ya kiebrania ni
neno nãbhãl neno hilo kimsingi katika tamaduni za
kiebrania linachukuliwa kama mtu aliyekosa hekima au mtu aliyepuuzia hekima,
mtu asiye na uadilifu, mtu baradhuli, mtu muovu, mtu mbaya, mtu asiyetenda
haki, mtu mwenye kuaibisha, mtu anayezungumza pumba, au mtu asiye muungwana,
aliekosa uungwana au asiyefunzwa uungwana, mtu wa hila, asiye na akili, au mtu
mwenye akili na hekima akifanya jambo la kushangaza kinyume na akili yake au
hekima au njia ya Mungu, kwa hiyo katika mtazamo wa kiungu kufanya upumbavu ni
kufanya jambo ambali liko kinyume na neno.
Isaya 32:5-8 “Mpumbavu hataitwa tena
mwungwana, wala ayari hatasemwa kwamba ni karimu. Maana mpumbavu atanena yaliyo
upumbavu, na moyo wake utafanya maovu, ili kutenda hila na kusema yasiyo kweli
juu ya Bwana, ili kuziacha nafsi za watu wenye njaa hazina kitu, na kukikomesha
kinywaji chake mwenye kiu. Tena vyombo vyake ayari ni vibaya; hutunga hila
mbaya, ili kuwaangamiza wanyonge kwa maneno ya uongo, mtu mhitaji ajaposema
maneno yenye haki. Bali mwungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana
mambo ya kiungwana.”
Kwa hiyo katika maandiko, mtu
asipofikiri katika kutenda kwake, au akifanya maamuzi mabaya na hata kufikiri
vibaya maana yake ametenda kwa upumbavu, na jambo hilo linaweza kutugharimu
katika maisha yetu kimwili na kiroho.
2Samuel 24:9-10 “Naye Yoabu akamtolea
mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta
panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu. Ndipo moyo wake
Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana,
Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee
mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.”
Kwa hiyo lugha upumbavu katika
maandiko inaweza kuwa na upana wa kiharibiko zaidi ya kukosa maarifa, au
ukosefu wa ustaarabu na kama mwanadamu hatakuwa makini mtu awaye yote yule, wa
ngazi yoyote ile anaweza kujikuta anafanya upumbavu! Bwana ampe neema kila
mmoja wetu ili tusiwe miongoni mwa watu watakaofanya upumbavu na kujutia katika
maisha yetu, Katika jina la Yesu Kristo ameen!
Wewe nawe utakuwa
kama mmoja wa wapumbavu?
Wakati wowote ule tunapofanya
jambo ambalo limeagizwa katika neno la Mungu na lina uhusiano na uadilifu hapo
tunatenda kwa hekima, na wakati wowote ule tunapofanya jambo ambalo liko
kinyume na mapenzi ya Mungu na swala zima la uvunjifu wa uadilifu maana yake
tunakuwa tumetenda kwa upumbavu, kwa hiyo upumbavu ni dhambi, upumbavu ni
ujinga na upumbavu unaweza kutuweka pabaya, upumbavu unaweza kuyagharimu maisha
yetu na ya wengine, na kwa kweli tukiruhusu, wivu, chuki, choyo, ubinafsi,
kupenda fedha, kupenda madaraka, kujivuna kutembea kwa kiburi, na kadhalika na
hayo yakatawala nafsi zetu ni rahisi sana kujikuta tumefanya upumbavu, kwa hiyo
utaweza kuona kuwa dhambi na upumbavu ni mapacha wanaotembea kwa ukaribu
sana na tuwapo duniani tunapaswa kujihadhari sana tusifanye
upumbavu, ili tuweze kuishi kwa Amani.
Katika andiko letu la Msingi,
ambalo Roho Mtakatifu Mwalimu mkuu alinipa na ndiko nilikopata kichwa cha
ujumbe wa somo hili, tunasoma habari za Amnoni kijana aliyejawa na tamaa na
kumpenda dada yake waliozaliwa mama tofauti lakini kwa baba mmoja, kijana huyu
alimtamani sana dada yake na kiasi ambacho aliandaa njama za kutaka kumbaka,
dada huyu alimshauri vizuri kwamba kama unanipenda unaweza kuzungumza na mfalme
baba yao na hatakuzuia kunioa, lakini yeye akizidiwa na tamaa aliendelea na
mpango wake wa kutaka kumbaka, dada yake aliyeonekana kuwa na busara sana alimshauri
kuwa kwa kutumia njia anayotaka kuitumia atakuwa kama mojawapo ya wapumbavu
katika Israel, yaani licha ya kuwa amefanya dhambi lakini atakuwa amefanya upumbavu,
hii maana yake ni nini? wakati wote tunapoacha kutumia busara katika jambo
lolote lile na tukaachia hisia zetu na tamaa ya mioyo yetu ituongoze maana yake
au kinyume chake tunachagua njia ya kipumbavu na swali hili litatuhusu wewe
nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu?, maandiko matakatifu yamejaa mifano mingi
ya watu waliotenda kwa upumbavu ambayo sisi hatupaswi kuiigia, kwani
yaliandikwa kwa kusudi la kutupa hekima sisi tunaoishi miisho ya zamani hizi ili
tusifanye upumbavu, kwa mfano:-
1.
Ukiwaza
moyoni kuwa hakuna Mungu – Maandiko yanaonya kuwa sio kusema tu lakini mtu
awaye yote ambaye anawaza moyoni mwake kuwa hakuna Mungu kibiblia huyo ni
mpumbavu, hajishughulishi kumtafuta Mungu, haamini kama Mungu yupo, huyo ni mtenda
maovu, awaye yote yule ambaye anaishi kana kwamba hakuna Mungu naye ni
mpumbavu, wote wanaoishi kwa ukaidi wakikataa miongozo ya Mungu, wakilikataa
neno la Mungu, wakiwa hawamtafuti Mungu na wanaishi sawa tu mawazo yao hao
wanakuwa wamekengeuka na jumla yaw azo la kimungu kwao katika maandiko ni kuwa
wamepumbazika.
Zaburi 14:1-3 “Mpumbavu
amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo,
Hakuna atendaye mema. Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama
yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja,
Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.”
Zaburi 53:1-3 “Mpumbavu
amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wametenda uovu wa ufisadi na kuchukiza, Hakuna
atendaye mema. Toka mbinguni MUNGU aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu
mwenye akili, Amtafutaye Mungu.Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna
atendaye mema, La! Hata mmoja.”
2.
Anayeshauri
mtu amwache Mungu – Wako watu ambao katika namna ya kushangaza sana
wanaweza kukushauri umwache Mungu, au utafute msaada kwa miungu mingine kwa
sababu ya changamoto unazozipitia na misimamo yako katika kumuamini Mungu mtu
anayefanya hivyo au kutoa ushauri wa namna hiyo katika maandiko anatajwa kama
mtu anayezungumza upumbavu au pumba. Aidha mtu awaye yeto akikubali kuyategemea
mawazo yake na njia zake au njia za kibinadamu huyu naye anatenda kwa upumbavu
Ayubu 2:7-10 “Basi
Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu
wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi
majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu
wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa
hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi
tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo
yake.”
3.
Kuondoka
bila kuaga – Umekaa na mtu kwa muda mrefu katika maisha yako, au mahali
ambapo ulikuwa unafanya kazi, alafu ukaamua kuondoka bila kuaga, au kutokumuaga
baba yako wa kiroho, na kuamua kutoroka, bila kuagana kwa Amani na kubarikiana
tendo hilo kadhalika linaweza kuwa sio dhambi lakini sio la kiungwana wala kistaarabu kwa hivyo katika maandiko
ukilifanya unahesabika kuwa umefanya upumbavu.
Mwanzo 31:26-28 “Labani
akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama
mateka waliotwaliwa kwa upanga. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala
hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na
kinubi? Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda
upumbavu.”
4.
Kulala
na binti ya watu kabla ya kumchumbia au kumuoa – kimaandiko unapolala na binti
ya watu na ukambikiri, kabla ya kumuoa kwa madai kuwa utamuoa baadaye jambo la
namna hii ni la kipumbavu katika tamaduni za kimaandiko na Israel. Huwezi kuishi
kama mwana ndoa kabla ya ndoa kwa kufanya hivyo unajidhihirisha namna ambavyo
umekosa adabu, umekosa heshima, umekosa maarifa huna hekima na umefanya
upumbavu.
Mwanzo 34:1-7 “Basi
Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi.
Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye,
akambikiri. Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu
msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. Shekemu akamwambia
Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. Basi Yakobo
akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na
wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hata walipokuja. Akatoka Hamori,
babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye. Wanawe Yakobo waliposikia hayo,
wakaja kutoka nyikani; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu
amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu
kutendeka.”
5.
Kumdhalilisha
mwanamke – tendo la mtu kumuoa mwanamke aliye bikira, kisha akafika ndani
na ukamchukia kisha kumsingizia kuwa eti hakuwa na ubikira tendo la
kumdhalilisha na kumuaibisha mwanamke katika Israel na katika swala zima la
uadilifu ni kutenda upumbavu.
Kumbukumbu 22:13-21 “Mtu akitwaa mke, akamwingilia na kumchukia, kisha
akamshitaki mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke
huyu, nami nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira; ndipo babaye yule
kijana na mamaye watakapotwaa alama za yule kijana za ubikira, wawatolee wazee
wa mji langoni; na baba yake yule kijana awaambie wazee, Mwanamume huyu nilimpa
binti yangu awe mkewe, naye amchukia; angalieni, amemwekea mambo ya aibu,
asema, Sikuona kwa binti yako alama za ubikira, nazo hizi ndizo alama za binti
yangu za ubikira. Na wayakunjue yale mavazi mbele ya wazee wa mji. Basi wazee
wa mji ule na wamtwae yule mtu mume na kumrudi, wamtoze shekeli mia za fedha,
wampe babaye yule kijana, kwa kuwa amemzulia jina baya mwanamwali wa Israeli;
naye awe mkewe; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote. Lakini likiwa ni kweli
neno hili, la kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira; na wamtoe nje
yule kijana mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa
mawe hata afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya
ukahaba katika nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.”
6.
Awaye
yote anayeiba – Maandiko matakatifu yanaagiza kuwa tusiibe, lakini sio
hivyo tu kila mmoja anaagizwa kuyatii maagizo ya Bwana na kulishika agano lake,
kufanya jambo kinyume na hayo ni kufanya upumbavu, mtu anayeiba ni mpumbavu, amechagua
njia isiyo ya kiungwana.
Yoshua 7:11-15 “Israeli
wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa
baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia
pamoja na vitu vyao wenyewe. Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya
adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa
pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.
Haya! Inuka, uwatakase watu, ukaseme, Jitakaseni, mwe tayari kesho; maana
Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kitu kilichowekwa wakfu kiko katikati
yako, Ee Israeli; huwezi kusimama mbele ya adui zako, hata mtakapokiondoa kile
mlicho nacho kilichowekwa wakfu. Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa
kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa Bwana itakaribia jamaa
kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa Bwana itakaribia nyumba kwa nyumba; na
nyumba ile atakayoitwaa Bwana itakaribia mtu kwa mtu. Tena itakuwa ya kwamba
yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa
moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la Bwana, na
kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli.”
7.
Kumbaka
mwanamke - Kumbaka mwanamke na kumuingilia
kinyume cha maumbile, sio tu kuwa ni dhambi, lakini vilevie ni upumbavu, katika
jamii, jambo hilo ni uovu ambao sio tu utakugharimu kufunguliwa mashitaka na
kufungwa lakini kwa Mungu ni dhambi na ni uovu katika jamii.
Waamuzi 20:4-6 “Huyo
Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifikilia
Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria yangu, ili tulale. Nao watu waume wa
Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa
usiku; walidhani kuniua, na suria wangu wakamtenza nguvu, hata amekufa.Basi
nikamtwaa huyo suria yangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote
ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika
Israeli.”
8.
Tamaa
na kutaka kulawiti ni upumbavu – jamii inapokuwa na watu ambao wanaona kuwa
mapenzi ya jinsia moja kama jambo la kawaida maana yake jamii hiyo
imepumbazika, usagaji ni upumbavu, ulawiti ni upumbavu, usagaji ni upumbavu, ni
kukosa akili ni kukosa hekima kwa hiyo ukiiangalia dunia ya leo na swala zima
la maovu yanayohusiana na ulawiti na tamaa ya aina hiyo utaweza kuwa na picha
halisi kuwa watu hata pamoja na kuwa na elimu kubwa hivyo na marifa kuongezeka,
dunia imekuwa na wapumbavu wengi sana.
Waamuzi 19:23-25 “Naye
mtu mwenye nyumba akawatokea hapo nje, na kuwaambia, La, sivyo, ndugu zangu
nawasihi msifanye uovu jinsi hii; kwa kuwa mtu huyu ameingia ndani ya nyumba
yangu, msifanye upumbavu huu. Tazama, binti yangu yupo hapa, ni mwanamwali, na
suria wake huyo mtu; nitawaleta hapa nje sasa nanyi watwezeni, na kuwatenda
hayo myaonayo kuwa ni mema; lakini mtu huyu msimtende jambo la upumbavu namna
hii. Lakini hao watu hawakukubali kumsikia; basi mtu huyo akamshika suria wake,
na kumleta nje kwao; nao wakamjua, na kumtenda uovu usiku kucha hata asubuhi
kisha kulipoanza kupambauka wakamwacha aende zake.”
Warumi 1:21-28 “kwa
sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali
walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena
kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na
uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya
wanyama, na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za
mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana
waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala
ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao
za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya
asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili,
wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo
ya upotevu wao yaliyo haki yao.Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu
zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.”
9.
Kuropoka
– nadhani umewahi kuishi na watu wanaoropoka, na utakuwa unajua madhara ya
kuropoka, kuropoka ni kuzungumza kitu bila kufikiri, wako watu yaani kitakachomjia
kichwani tu anakitekeleza kwa kusema au kuandika sms isiyofaa, unaweza kutuma
ujumbe usiofaa kwa mke wa mtu, mume wa mtu, unaweza kuropoka mambo ya watu au
siri za watu, au kutokwa na maneno yasiyo na maana kama mtu hana nidhamu katika
kuzungumza kwake maana yake anashindwa kuudhibiti ulimi wake naye anaitwa
mpumbavu
Mithali 14:3 “Katika
kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi, Bali midomo ya wenye hekima
huwahifadhi.”
Mithali 12:15-16 “Njia
ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima
husikiliza shauri. Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu
husitiri aibu.”
10.
Kufanya
dhambi – Kufanya dhambi ya aina yoyote ile kibiblia ilihesabika kuwa ni
kufanya upumbavu, kwani kila dhambi licha ya kuwa uko msamaha wa Mungu na
rehema zake lakini kwa kuwa Mungu ni mwenye haki wakati mwingine matokeo ya
dhambi yanaweza kuendeleza madhara makubwa nje ya msamaha wa Mungu, mfano
ukifanya uasherati ukapata mimba, na ukatubu kwa uasherati ule utasamehewa
lakini mimba haitayeyuka kwa hiyo ulipaswa kufikiri kabla ya kutenda na kwa
kutokufikiri umefanya upumbavu. Na au ukapata ukimwi, rehema za Mungu zinaweza
kuwepo lakini na virusi vinaendelea kuwepo kwa sababu ulifanya upumbavu,
hukutoa nafasi ya kufikiri kwa kina madhara unayoweza kuyapata. Kwa hiyo ni
muhimu kukumbuka ya kuwa dhambi ina madhara yake na madhara yake ni mabaya sana
katika maisha ya watu wote
Zaburi 38:3-5 “Hamna
uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani
mwangu Kwa sababu ya hatia zangu. Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa,
Kama mzigo mzito zimenilemea mno. Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya
upumbavu wangu.”
Zaburi 69:3-5 “Nimechoka
kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja Mungu
wangu. Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao
kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi
nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua. Ee Mungu, unajua upumbavu wangu,
Wala hukufichwa dhambi yangu.”
11.
Ukiruhusu
hasira kukutawala – wako watu ambao kupitia hasira wamefanya mambo ya
kijinga na kipumbavu na baadaye kujilaumu au kupata majuto, maandiko yanatutaka
kujidhibiti, kujitia nidhamu, badala ya kujisifia kuwa wewe una hasira,
hakikisha unajinidhamu kushindwa kufanya hivyo ni kuruhusu upumbavu.
Muhubiri 7:4-9 “Moyo
wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo
nyumbani mwa furaha. Heri kusikia laumu ya wenye hekima, Kuliko mtu kusikia
wimbo wa wapumbavu; Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria, Ndivyo kilivyo
kicheko cha mpumbavu. Hayo nayo ni ubatili. Kweli jeuri humpumbaza mwenye
hekima, Na rushwa huuharibu ufahamu. Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na
mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi. Usifanye haraka kukasirika
rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.”
12.
Kumtendea
maovu mtu ambaye hana nia mbaya na wewe – wako watu wengine kwa sababu ya
wivu tu wenye uchungu wanaweza kukutendea mabaya, au wanaweza kukusudia kutenda
mabaya kwa watu ambao hawana nia wala wazo la kuwadhuru, kufanya jambo la namna
hiyo ni machukizo sio kwa Mungu tu lakini ni upumbavu, kutafuta na kutaka
kumdhuru mtu ambaye hana mpango wala nia ya kukudhuru.
1Samuel 26:18-21. “Akasema,
Bwana wangu ananiwinda mimi mtumishi wake kwa sababu gani? Nimefanya nini mimi?
Ni uovu gani nilio nao mkononi mwangu? Basi sasa, nakusihi, bwana wangu,
mfalme, na asikie maneno ya mtumishi wake. Ikiwa ni Bwana aliyekuondokesha juu
yangu, na akubali sadaka; bali ikiwa ni wanadamu, na walaaniwe mbele za Bwana;
kwa sababu wamenifukuza leo, nisishikamane na urithi wa Bwana, wakisema,
Enenda, katumikie miungu mingine.Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na
uso wa Bwana; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama
vile mtu awindavyo kware mlimani.Ndipo Sauli akasema, Nimekosa; rudi, Daudi,
mwanangu; maana sitakudhuru tena, kwa kuwa maisha yangu yalikuwa na thamani
machoni pako leo; angalia, nimetenda upumbavu, nimekosa sana.”
13.
Mtu
anayefikiria maovu na mwenye mizaha - Maandiko yanataja vitu kadhaa
vinavyomchukiza Mungu, ikiwa ni pamoja na moyo uwazao mabaya, yaani maswala
hayo ni machukizo kwa Mungu, maana yake kule kufikiri na kuwaza namna ya
kufanya maovu, ni kufikiri na kufanya dhambi hayo yanawekwa katika kundi moja
la machukizo kwa Mungu, ambayo kimsingi nayo yanaitwa upumbavu katika maandiko
kwa sababu moyoni ndiko chanzo cha kila kitu kibaya kwa hiyo kufikiri au kuwaza
maovu ni kuwaza upumbavu na zaidi sana ikiwa ni pamoja na mizaha, kwa hiyo kila
mmoja wetu ajichunge fikira zake na kujihadhari za mizaha.
Mithali 6:16-19 “Kuna
vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya
kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao
mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;Shahidi wa uongo asemaye
uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.”
Mithali 24:9 “Fikira
za mpumbavu ni dhambi, Na mwenye mzaha huwachukiza watu.”
14.
Mtu
anayelipa maovu badala ya mema – kwa maana nyingine ni watu wasio na
shukurani, wako watu ambao unaweza kuwatendea mema na kisha ukahitaji fadhili
ndogo tu kutoka kwao lakini wakakulipa mabaya badala ya mema mfano wa aina hii
ya upumbavu ndio uliofanywa na mtu mwenye kuitwa nabali ambayo ndio tafasiri ya
somo hili Nabali maana yake mpumbavu ambaye alioa mwanamke muungwana au mwenye
akili.
1Samuel 25:2-26 “Na
huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli;
naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye
alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa
Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye
akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu
katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu. Basi Daudi akasikia huko
nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake. Daudi
akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli,
na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu
aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote
ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako;
haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa
kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao
watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia
katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape
watumwa wako na mwanao Daudi. Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia
Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la Daudi, kisha wakanyamaza. Naye
Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana
wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake!
Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu
niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu
ambao siwajui wametoka wapi? Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao,
wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno hayo yote. Kisha Daudi
akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga
kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma
yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo
vyao.Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema,
Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu,
naye akawatukana. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata
dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao,
tulipokuwako mavueni; watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote
tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda;
kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote;
kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye. Ndipo
Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai,
na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada
mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.
Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi
nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali. Ikawa, alipokuwa amepanda punda
wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa
wakishuka kumkabili; naye akawakuta. Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure
nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho
chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema. Mungu naye
awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake
hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi. Ndipo hapo Abigaili
alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi
kifulifuli, akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu,
bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene
masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana
wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama
lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao;
lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. Basi
sasa, bwana wangu, aishivyo Bwana, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa Bwana
amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa
adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali.”
15.
Mwanamke
asiye na hekima – Biblia aidha pia ina maonyo mengi kuhusu mwanamke mcha
Mungu, na mwenye hekima kuwa ni mwanamke anayeweza kusimamia nyumba yake
vizuri, na maandiko yanaonyesha kuwa kama mwanamke hamchi Mungu nyumba yake haiwezi
kusimama mwanamke asiye mcha Mungu anaweza kuhesabika kama mkaidi, asiyetaka
kumtii Mumewe, hafundishiki, mbishi, mbinafsi, anayetawala nyumba, mchoyo kwa
tendo la ndoa na anayeamua kumkomoa mumewe kwa tendo hilo, mvivu wa ibada,
hajishushi, mumewe akipanda naye anapanda juu zaidi, anayependa usingizi, Mmbeya,
hafanyi kazi kwa mikono yake mwenyewe, na majukumu ya mke anayapuuzia na
kupenda starehe nyingine utaongezea mwenyewe mwanamke wa aina hiyo ndiye
anayefikiriwa kuwa hana hekima na hivyo maandiko yanamuita mpumbavu.
Mithali 14:1-2 “Kila
mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa
mikono yake mwenyewe. Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha Bwana; Bali aliye
mkaidi katika njia zake humdharau.”
Mithali 9:13-17 “Mwanamke
mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu.Hukaa mlangoni pa nyumba yake,
Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka, Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao
moja kwa moja katika njia zao. Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia
mtu aliyepungukiwa na akili, Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa
siri hupendeza.”
Mithali 21:9 “Ni
afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na
mwanamke mgomvi.”
Mithali 21:19 “Ni
afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.”
Mithali 25:24 “Ni
afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na
mwanamke mgomvi.”
16.
Kutokumjua
Mungu wala njia zake – Watu wanaweza
kuwa na maarifa ya aina nyingine mfano maarifa ya kupanga ubaya, kufanya maovu,
kutekeleza majungu, kuharibu mahusiano, lakini hawana maarifa wala akili ya
kumtafuta Mungu, ziko nguvu za uovu ambazo watu wanazifanya ambazo kama
zingeelekezwa katika kumtafuta Mungu na kuongeza maarifa ya kumjua Mungu watu
wangekuwa mbali sana
Yeremia 4:22 “Kwa
maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili,
wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda
mema hawana maarifa.”
17.
Wanaoamini
Manabii wa uongo – Wako manabii ambao kazi yao kubwa ni kuzungumza maneno
ya kufariji watu, ilihali wakati mwingine suluhu ya uponyaji wa watu hao ni
kuwaambia tu watubu dhambi zao, ziko changamoto nyingi sana duniani
zinazosababishwa na dhambi kuliko hata wachawi na laana za ukoo, wakati
mwingine mtu akisamehewa dhambi zake na uponyaji wake unakuja kama neno lake
lisemavyo, akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, waambie watu
kosa lao badala ya kuona maono ya ubatili na upumbavu, manabii wa uongo huona
maono ya kipumbavu na hivyo kuzuia kuponywa kwako.
Maombolezo 2:13-14 “Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini, Ee Binti Yerusalemu?
Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji, Ee bikira binti Sayuni? Kwa maana
uvunjifu wako ni mkuu kama bahari, Ni nani awezaye kukuponya? Manabii wako
wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako,
Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili
yako Na sababu za kuhamishwa.”
18.
Kutokulifanyia
kazi neno la Mungu – kama watu wengi tungekuwa tunalitii neno la Mungu
tungekuwa na mafanikio makubwa sana na ustawi mkubwa sana katika maswala yote
ya mwili na roho lakini kwa bahati mbaya sana kulitii neno la Mungu limekuwa
jambo gumu kwa kizazi hiki hata kama watu wanatii wengi huchagua maswala kadhaa
ya kuyatii lakini neno la Mungu linatukumbusha kuyatii maagizo yote na
kuyafanyia kazi maneno ya Mungu.
Yakobo 1:22-24 “Lakini
iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi
zenu.Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni
kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda
zake, mara akasahau jinsi alivyo.”
Mathayo 7:24-27 “Basi
kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye
akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja,
pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa
juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na
mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko
yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa
kubwa.”
19.
Kujilinganisha
na wengine – Katika maisha haya Mungu amemuumba kila mwanadamu akiwa na
baraka tofauti na karama na vipawa tofauti, kwa hiyo kimaandiko mwanadamua
anyejilinganisha na mwingine au kuipima nafsi yake akiilinganisha nay a mtu
mwingine mtu huyo hana akili na ni mpumbavu, kwa mujibu wa maandiko, hatupaswi
kamwe kujilinganisha na wengine kwa sababu kila mwanadamu Mungu amemuumba kwa
namna na jinsi ya aina yake kwa uhodari mkubwa!
2Wakorintho 10:11-18 “Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo
kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo. Kwa
kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala
kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na
wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili. Lakini sisi hatutajisifu
zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani,
kadiri ya kufika hata kwenu. Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu,
kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu
katika injili ya Kristo; wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika
taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo,
tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada; hata kuihubiri
Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha
mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa. Lakini, Yeye ajisifuye, na
ajisifu katika Bwana. Maana mtu mwenye kukubaliwa si yeye ajisifuye, bali yeye
asifiwaye na Bwana.”
20.
Kutokujitayarisha
kwa Mungu - watu wote duniani
wanapaswa kujiandaa kwaajili ya kukutana na Mungu, na kujiandaa kwaajili ya
ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo mara ya pili duniani, na kunyakuliwa kwa kanisa,
kuishi maisha ya vuguvugu na kujidanganya kunaweza kuja kutuletea majuto na
kilio na kusaga meno, Yesu mara kadhaa alisisitiza jamii kujiandaa kwaajili ya
Mungu na awaye yote ambaye atakosa mbingu atakuwa amekosa kwaajili ya upumbavu,
Bwana amtunze kila mmoja wetu asiikose mbingu katika jina la Yesu Kristo.
Luka 12:16-21 “Akawaambia
mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza
kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno
yangu. Akasema, Nitafanya hivi;
nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka
yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema
vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.
Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na
vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi
yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”
Mathayo 25:1-13 “Ndipo
ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka
kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye
busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja
nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa
zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini
usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.
Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao. Wale wapumbavu
wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na
ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.Na hao walipokuwa
wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye
arusini; mlango ukafungwa.Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema,
Bwana, Bwana, utufungulie. Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.”
Chagua Hekima!
Tungeweza kuchambua maswala mengi
sana yanayozungumzia upumbavu lakini muda usingelitosha, ni ukweli ulio wazi ya
kuwa maandiko yanatuonyesha wazi kuwa upumbavu ni tatizo na janga zito sana
kuliko hata dhambi zenyewe, kwani hakuna dhambi ambayo utaifanya na isiwe kuwa
hukufanya upumbavu, ziko tabia mbaya nyingi sana ambazo mtu akizitenda
kimaandiko anaitwa amefanya upumbavu, swali kubwa la kujiuliza Je wewe nawe utakuwa kama mmoja wa
wapumbavu? Kama hutaki neno la Mungu linatushauri kuchagua hekima na hii
ndio namna ya kuchagua hekima.
a.
Hekima
ya kweli inapatikana kwa kumcha Mungu – Mithali 1:7 “Kumcha
Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu”.
b.
Uko
umuhimu wa kumuomba Mungu hekima – Yakobo 1:5-6
“Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na
aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.Ila
na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la
bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.”
2Nyakati 1:7-12 “Usiku
ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani
akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha
mimi badala yake. Basi sasa, Ee Bwana Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi
neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya
nchi. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu
hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi? Naye
Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala
hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala
hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate
kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa;
nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme
wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.”
c.
Hekima
ni ulinzi – ukiwa na hekima hakuna kitu kitaharibika kila kitu
kitarahisishwa kama vile fedha ilivyo ulinzi hekima itatuhifadhi zaidi kuliko
fedha, tutapunguza kuharibikiwa endapo tutachagua hekima, Hekima ni njema
hekima ni bora.
Muhubiri 7:11-12 “Hekima
ni njema, mfano wa urithi; Naam, nayo ni bora kwao walionao jua. Kwa maana
hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya
kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.”
d.
Chagua
Hekima – Mithali 8:4-11 “Enyi watu, nawaita ninyi;
Na sauti yangu ni kwa wanadamu.Enyi wajinga, fahamuni werevu, Nanyi wapumbavu,
mpate moyo wa kufahamu. Sikieni, maana nitasema yaliyo mazuri, Na kufumbua
midomo yangu kutakuwa maadili. Maana kinywa changu kitasema kweli, Na uovu ni
chukizo kwa midomo yangu. Maneno yote ya kinywa changu yana haki; Hapana hata
neno lililopotoka au la ukaidi. Yote humwelea yule afahamuye, Yote huelekea
mbele yao waliopata maarifa.Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa
kuliko dhahabu safi. Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote
vinavyotamanika havilingani nayo.”
Ni muhimu kujikumbusha tena ya
kuwa kukosa hekima ni gharama kubwa sana, kwani kinyume cha kukosa hekima ni
kuwa mpumbavu, kila unachokiona duniani hakiendi vizuri ni kwa sababu watu
walifanya upumbavu, upumbavu ni gharama kubwa sana na umewagharimu wengi,
majuto makubwa sana duniani yamechangiwa na upumbavu uliofanywa na watu, sisi
kama watu wa Mungu tunapaswa kumuomba Mungu atupe akili, atupe hekima ili
tusifanye upumbavu, ambao unaweza kuja kuyagharimu maisha yetu na maisha ya
wengine, maandiko yanatutaka tutembee na wenye hekima nasi tutakuwa na hiyo
hekima.
Mithali 13:20 “Enenda pamoja na wenye
hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.”
Ni mwenye hekima gani ambaye
unaweza kuambatana naye au kwenda naye naye atakuambukiza hekima? Kwa kawaida
wenye hekima pia huishi maisha matakatifu na ni nani aliye mtakatifu ni Yesu
Kristo ambaye yeye anaitwa Hekima yetu yeye ni mkuu kuliko Suleimani na ana
hekima kuliko Sulemani.
1Wakorintho 1:20-24 “Yu wapi mwenye hekima?
Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya
hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia
isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa
upuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na
Wayunani wanatafuta hekima;bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa
Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa
Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.”
Mathayo 12:41-42 “Watu wa Ninawi watasimama
siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa;
kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko
Yona. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki,
naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho
za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”
Kwa kuwa Yesu ndiye hekima yetu
natoa ushauri kama maandiko yasemavyo, mpokee Yesu aliye hekima yetu ili kwamba
uweze kuishi maisha ya neema na kujifunza kuwa kama yeye na kuishi maisha
yasiyo na majuto chagua hekima mchague Yesu.Kumchagua Yesu ni Kuchagua hekima,
na kuishi sawa na neno la Mungu ni kufuata njia ya Hekima, Bwana ampe neema kila
mmoja wetu kuishi na kuenenda kwa hekima katika jina la Yesu Kristo ameen.
Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.