Jumatano, 16 Oktoba 2024

Kutoka Misri kwa ujeuri!


Kutoka 14:5-8 “Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote. Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”

 



Utangulizi:

Leo tutachukua Muda kutafakari kwa kusudi la kujifunza na kupandisha imani zetu kwanini maandiko yanasema Israel walitioka Misri kwa ujeuri? Jambo ambalo lilimfanya Farao kubadili mawazo na kuamua kuwafuatilia wana wa Israel baada ya kikao cha Dharula cha baraza la mawaziri na majeshi yake, kujadili kuwa imekuwaje wakawaachia Israel waende zao? Na wasiwatutumikie tena? Uchumi wao utasimamaje bila watumwa? Kazi zote ngumu za uzalishaji mali zitafanywa na nani? Kwanini tunawaachia watumwa waende kwa uhuru hata bila kupigana nao? Au kutumia nguvu kuwarejesha? Baada ya hoja nzito mswada ulipitishwa kuwa ni lazima watu hao warejeshwe utumwani vinginevyo tutapata hasara kubwa sana!

Kutoka 14:5-10 “Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote. Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA.”

Leo tunapojifunza somo hili Roho Mtakatifu ananiambia kuwa kuna watu watatoka kwa jeuri, wataondoka katika mateso yao kwa mkono ulionyooshwa wa Bwana, watafunguliwa vifungo vyao kwa nguvu na uweza wa Mungu wetu, watakombolewa kutoka katika mateso yao na maumivu yao na majonzi yao, na utumwa wa kila aina unaoyazinga maisha yao, na kila kitu chenye kusononesha maisha yako leo kitakuwa ndio mwisho wa utawala wake katika maisha yako nawe utaenda zako kwa jeuri, Nasema leo utatoka kwa ujeuri katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai haleluyaaa! Tutajifunza somo hili kutoka Misri kwa ujeuri kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya kutoka kwa jeuri

·         Nani ni sababu ya Jeuri yetu

·         Kutoka Misri kwa ujeuri

 

Maana ya kutoka kwa jeuri

Kutoka 14:8 “Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”

Katika kifungu hiki cha maandiko tunajifunza namna na jinsi Mungu alivyoingilia kati swala zima la mateso ya watu wake waliokuwa wanateseka kule Misri, Mungu alikuwa amechoshwa na utawala katili wa Farao, asiyekuwa na shukurani ambaye aliwatumia watumishi wake na wasimamizi wake kuwatesa wana wa Israel na kuwaletea msiba mkubwa na mateso makubwa kiasi ambacho waliugua na kumlilia Mungu.

Kutoka 3:7-9 “BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.”

Wote tunakumbuka namna Mungu alivyotekeleza mpango wake ambao mara kwa mara ulikuwa ukikataliwa na Farao vilevile kwa jeuri aliyokuwa nayo, akigoma kabisa kuwaachia wana wa Israel na kuwaongezea machungu na mateso makali zaidi huku akijaa kiburi na kujifanya hamtambui Bwana na kuwa watu hao wana kauli za uongo na ni wavivu hivyo akawakazia kazi ngumu zaidi.

Kutoka 5:1-9 “Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani.Farao akasema, BWANA ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui BWANA, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao. Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu BWANA, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga. Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu.Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe. Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo.”

Jambo hili liliwapa uchungu wana wa Israel zaidi, hali yao wakati wanadai uhuru wa ruhusa ilibadilika kuwa mbaya na chungu zaidi, Jambo lilopelekea sasa Mungu kuanza kumuadhibu Farao kwa mapigo mazito sana huku akiwapendelea wana wa Israel ambao walianza kupata faraja kwa kutokuguswa na mapigo mazito, mapigo yaliyendelea mpaka lilipofika pigo la kumi ambalo lilisababisha msiba mkubwa kuanzia kwa Farao mpaka kwa wanyama wao na watumwa wao wote kila mahali walifiwa na mzaliwa wa kwanza jambo lililopelekea kutoa ruhusa ya haraka haraka ili wana wa Israel waende zao wakamuabudu Mungu kwa uhuru na pasipo hofu! Mungu mwenye nguvu YHWH alijionyesha uwezo wake na kumtiisha mfalme mwenye kiburi awaachie watu wake ambao kimsingi nao waliondoka kwa mikogo sana waliondoka kwa furaha na walindoka Misri kwa ujeuri ni nini maana ya wana wa Israel kuondoka kwa Jeuri ambacho kimsingi kilimfanya Farao abadilishe maamuzi? Hilo ndilo jambo la msingi ambalo tunataka kujifunza kwa kila leo ili nasi tutoke kwa ujeuri katiika kila Nyanja ambayo ibilisi ameweka mkono wake! tuchunguze andiko hilo kwa kina tena !

Kutoka 14:8 “Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.”

Farao aliwafuta tena wana wa Israel kwa kiburi kwa sababu wana wa Israel walitoka kwa ujeuri ni nini hasa maana ya ujeuri unaozungumzwa hapo, kimsingi neno la kiebrania linalotumika hapo ni “Rûm” ambalo kimatamshi linatamkwa room neno hili lina maana pana zaidi kama nitakavyokuonyesha kwanza tafasiri nyingine za matoleo ya biblia ya kiingereza ili uweze kubaini misamiati tofauti tofauti upate kufaidika na maana halisi ya neno hilo:-

-          King James Version (KJV) – and the Lord hardened the heart of Pharaoh king of Egypt, and he pursued after the children of Israel, and the Children of Israel went out with and high hand

-          English Standard version (ESV) - and the Lord hardened the heart of Pharaoh King of Egypt, and he pursued after the people of Israel while the people of Israel were going out defiantly.

-          The Message Bible (MSG) – God made pharaoh king of Egypt stubborn, determined to chase the Israelites as they walked out on him even without looking Back.

-          God’s word translation (GW) – the Lord made pharaoh (the king of Egypt) stubborn that he pursued the Israelites, who were boldly leaving Egypt.

-          Holman Christian Standard Bible (CSB) – The Lord hardened the heart of Pharaoh king of Egypt and he pursued the Israelites, who were going triumphantly.   

Sikutaka kutumia matoleo mengine ambayo kimsingi yanaweza kuwa yamerudia neno mojawapo kama haya yaliyotumika hapo juu, hivyo nimechagua matoleo ambayo yametumia misamiati mbali mbali tofauti ili tuweze kujifunza kwa upana

1.       High – hand – Mkono ulionyooshwa, kwa nguvu kwa mamlaka, bila kujali hisia zao

2.       Defiantly. – Kwa lazima, kwa kuasi, bila kumtii au kumsikiliza Farao tena

3.       even without looking Back – Bila kutazama nyuma, moja kwa moja bila kujali wala kuhuzunikak

4.       boldly leaving – Kwa ujasiri, Bila kuogopa, bila hofu, ukijua uendako,

5.       triumphantly – Kwa shangwe, kwa furaha, kwa ushindi wa kufikia malengo

Rûm – Kwa ujeuri sasa maana yake kwa mkono wa Bwana ulionyooshwa, Kwa nguvu na mamlaka ya Mungu, wakati wao wanaomboleza kwa misiba, Israel anasonga mbele, Kwa lazima, kwa kuasi amri ya Farao, bila matakwa yake, bila kumsikiliza, bila kumtii, kwa kuinuliwa juu kulikopitiliza, bila kutazama nyuma, wala mpango wa kurejea tena, moja kwa moja bila kujali ya nyuma, kwa ujasiri, bila woga wowote, wakiwa wanajua kule wanakokwenda, sio kwa kubahatisha, kwa furaha na shangwe kwa mikogo, wakiwa na ushindi wa kufikia malengo, wakijivunia walioinuliwa sana, kwa uchangamfu sio kwa machozi. Kwa hiyo wana wa Israel kwao ilikuwa ni siku ya furaha kubwa sana kila mmoja ilikuwa ni shauku yake kuwa ni lini Bwana atakuja kuwatoa watoke katika hali waliyokuwa wakiipitia, walikuwa wamechoshwa na walikuwa sasa imani zao zimepanda sana, Israel walitoka si kwa jeuri yao bali walikuwa wamejaa matumaini, wametiwa nguvu, hawana hofu ya kurejea nyuma, Imani yao ilikuwa imepanda sana saababu kubwa ikiwa ni Mungu wao na namna alivyojifunua kwao kwa mkono wake uliohodari, mkono wa Bwana ulioonyooshwa, Bila hofu kwa ujasiri na kwa kujiamini.

Waebrania 11:27-29 “Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana. Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao.Kwa imani wakapita kati ya Bahari ya Shamu, kama katika nchi kavu; Wamisri walipojaribu kufanya vivyo wakatoswa.”

Nani ni sababu ya Jeuri yetu.

Israel walitoka kwa nguvu, kwa mamlaka na uthabiti mwingi kama tulivyojifunza hapo juu, sababu kubwa ya ujeuri huu haikuwa jeuri ya kibinadamu bali walikuwa wamejifunza jinsi Mungu alivyo mwema katika njia zake, kadiri alivyojifunua kwao kwa mapigo yale yote kumi, kila pigo lilikuwa ni shuhuda ya kuwa wanaye mtetezi ambaye hakuna anayeweza kupambana naye, ujeuri huu ulikuwa unatokana na nguvu alizonazo Mungu, Mungu wetu miujiza waliyokuwa wameiona ilikuwa imewapa imani thabiti kuwa wanaye Mkombozi, na hivyo hawakua na mashaka naye.

Wamisri pamoja na mfalme wao jeuri waliwasisitiza Israel kundoka maana hali yao ilikuwa mbaya na hawakujua kama watasalimika waliona kuwa wameisha wote hivyo waliwataka waondoke haraka

Kutoka 12:29-33 “Hata ikawa, usiku wa manane BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu. Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni BWANA kama mlivyosema.Twaeni kondoo zenu na ng'ombe zenu kama mlivyosema, enendeni zenu, mkanibariki mimi pia.Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote.”

Mungu alikuwa pamoja nao na wala hakuwaacha wakati wa mchana wala wakati wa usiku, hii iliwapa ujasiri mkubwa sana, Mungu aliwashughulikia vikali maadui wa Israel na alionekana wazi kwa nguzo ya wingu wakati wa mchana na alionekana wazi kwa nguzo ya moto wakati wa usiku na ni yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa akiwaongoza njia, Jambo hili liliwapa ujasiri mkubwa sana.

Kutoka 13:21-22. “BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.”

Hakuna jambo linatupa kiburi kama kujua ya kuwa Bwana yuko pamoja nasi, hakuna jambo linatupa ujasiri kama kujua Neno la Mungu linasema nini juu yetu, hakuna kitu kinatupa kujiamini kama kujua kuwa BWANA ni siri ya wokovu wetu, nuru yetu na ngao yetu, na ulinzi wetu, BWANA ni kila kitu kwetu hakuna jambo linatupa nguvu na mamlaka kama kujua ya kuwa Bwana anatupenda sana, na kuwa yuko upande wetu, hakuna jambo linatupa matumaini kama kujua ya kuwa Mungu ni mtetezi wetu na ya kuwa yuko hai, na yuko pamoja nasi kututetea na kutulinda na kutufunika !

Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”

Ayubu 19:25-27 “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu.”

Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Israel walipata Jeuri kwa sababu walijua kuwa Mungu ni Mungu anayesimamia neno lake, na agano lake akitamka kitu ni sheria, lazima kiwe, Mungu wetu ni mwaminifu na hatatuacha, wala hatatuangusha, andiko linasema na kila amwaminiye hatatahayari kamwe. Kama ni hivyo kwanini shetani asituone tuna jeuri, kwanini wapinzani wako wasikuone una jeuri? Kwanini wqasikuone una mikogo kwa sababu Bwana ndiye sababu yetu

Kutoka Misri kwa ujeuri

Neno la Mungu linatukumbusha ya kuwa Mungu ni mwaminifu katika kazi yake ya ukombozi, na kuwa yeye yuko tayari kumtoa kila mmoja katika hali yake ya utumwa, na kutupa ujasiri wa kusonga mbele, wala tusiwe na mashaka naye, kila changamoto unayokutana nayo na inayokutumikisha inataka kukuweka utumwani, na haitaki kukuachia kwa haraka kwa sababu inataka uwe mtumwa wa hali hiyo jambo kubwa la Msingi ni kukumbuka kuwa leo ni siku yako ya kutoka Misri kwa ujeuri, una shuhuda nyingi za jinsi Bwana alivyoyapigania maisha yako na  ya wengine kwa hiyo hauna sababu ya kuogopa au kulia na kuomboleza hata adui akijaribu kukufuata tena anachokitafuta kitampata, Farao alipojaribu kuwafuatia Israel kwa sababu walitoka kwa jeuri maandiko yanasema alifutiliwa mbali yeye na majeshi yake yote, katika biblia ya kiingereza inaonekana vizuri zaidi kuwa Farao pia alifutiliwa mbali kabisa na majeshi yake yote na hakubakia hai ona   

Zaburi 136:13-15 “Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akawavusha Israeli katikati yake; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.”

Psalm 136:13-15 “to him who divided the Red Sea asunder His love endures forever. And brought Israel through the midst of it, His love endure forever, BUT SWEPT Pharaoh and his army into the Red Sea; His love endure forever

Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Majeshi ya wamisri yalifutwa yote sawasawa na neno la Musa mtumishi wa Mungu hapo aliposema hawa mnaowaona leo hamtawaona tena milele, Mwandishi maarufu wa Historia ya wayahudi aitwaye Flavius Josephus alisema kuhusiana na tukio hili nanukuu “And thus did all these men perish, so that there was not one man left to be a messenger of this calamity to the rest of the Egyptians” kwa tafasiri yangu “Na wote wakaangamia hata kusiwepo hata mjumbe wa kuelezea yaliyowakuta wamisri” leo nataka utoke kwa ujasiri katika kila kifungo kinachokuonea, leo nataka kifungo kinachokuonea na kukandamiza kiwe mwisho, na usikione tena leo nataka utoke katika Misri inchi yako ya utumwa kwa ujeuri, utoke nje ya uonevu wa mashetani, nje ya magonjwa, nje ya huzuni, nje ya kila kinachopoteza tumaini la maisha yako, Nje ya utasa wako, nje ya kansa, nje ya tezi dume, nje ya magonjwa ya kizee, nje ya umasikini, nje ya uonevu wa wachawi, nje ya vifungo vya nguvu za giza, nje ya mashambulizi na uonevu wa ibilisi, leo nakutangazia kwa mamlaka niliyopepewa kama mtumishi wake kwa mafuta aliyonipaka kwayo nasema  Toka kwa imani ukimtegema Mungu na kufahamu ya kuwa hatakuangusha, mtegemee yeye katika maamuzi makubwa ya maisha, uwe na ujasiri unapopita katika dhiki na shida, kabiliana na majaribu yako kwa Imani ukijua wazi hatimaye Mwokozi atasimama karibu nawe na kukutoa katika hali unayoipitia na kamwe usitazame nyuma, toka kwa ujeuri mbele kwa mbele usitazame tena jaribu lako na nakuhakikishia halitakuwepo tena!, Bwana ameniambia kuwa fadhili zake ni za milele, ikiwa aliwaokoa wana wa Israel wakatoka kwa Jeuri, leo ni zamu yako kutoka kwa ujeuri katika hali iliyokusumbua kwa miaka mingi, katika jina la Yesu Kristo pokea, mahitaji yako, pokea uzima wako, pokea ukombozi wako, pokea uhai wako, nakufungua na kukuweka mbali na mauti katika jina la Yesu Kristo nakutamkia uzima kwa mamlaka niliyo nayo katika jina la Yesu, pepo achia wasomaji wangu, achilia wasikilizaji wangu, achilia watu wa Mungu katika jina la Yesu, Nakutangazia kutoka kwa Jeuri na kumuacha Shetani akijuta na kusikitika kwa kukuachia na akijaribu kukufuata ataangamia kama Farao katika jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai! Ramashakatariboso, saparatashanda, rimosakata free sakata lota fakaseta rimoso pa taratshatata parafata, katika jina la Yesu Amen!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Ijumaa, 11 Oktoba 2024

Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?


Yohana 6:65-69 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”




Utangulizi:

Je kuna watu wamewahi kukuacha na kuondoka katika maisha yako? Je kuna watu hawakupigii simu wala hawashughuliki tena na maisha yako? Je kuna watu mlikuwa karibu sana na siku hizi hawako karibu kama ilivyokuwa zamani? Je unahuzunika kwaajili yao? Je unalalamika kuwa hawakusalimii, hawatumi hata ujumbe na hawaulizi hata uko wapi na unafanya nini?, hawashughuliki hata kukusalimu?  kuna watu ulikuwa msaada mkubwa sana kwao, lakini sasa wako mbali na wewe? Je unahuzunika kwaajili yao? Kuna watu walikuwa faraja kubwa sana katika maisha yako, uliwapenda na wao wakakupenda, wakakufuata lakini sasa ni kama hawako na wewe, kuna wale mlisoma nao shule moja, darasa moja, kuna wale uliwasimamia harusi, kuna wale mlikuwa pamoja, mlicheza pamoja, kuna wale walikaa kwenu wakasomea kwenu, kuna wale ulisoma kwao ukakulia kwao, kuna wale ulikuwa msaada mkubwa kwao kiroho na kimwili na sasa ni kama hawataki kutambua mchango wako je unaumia kwaajili yao? Unalia kwaajili yao? Unasikitia kwaajili yao? Sikiliza wako watu ambao Mungu huwavuta kwetu na kuwaleta karibu nasi kwa makusudi maalumu, wako ambao Mungu amewaleta kwetu kama wenzi wetu, ndugu zetu, watoto wetu na ambao tunawafurahia hawa ni furaha yetu ni damu yetu ni watiifu kwetu hawawezi kutuacha kwa sababu Mungu alikusudia wawe nasi milele, kwa wakati mzuri na wakati mbaya, wako pamoja nasi hawana namna ya kujitoa kwetu, wao ni familia hawawezi kutuacha wala sisi hatuwezi kuwaacha. Lakini wako ambao Mungu huwaleta kwetu kwa sababu maalumu kama marafiki kwa kitambo, ni watu wema kwetu na wazuri kwetu lakini uko wakati ambao Mungu hufunga mlango na kuwaacha waende zao kwa sababu hawana shughuli kwetu tena, lile kusudi ambalo Mungu alikuwa amelikusudia kwa kuwaleta kwetu limeisha, Mlango umefungwa kwao kwaajili yetu, hawawezi tena kwenda unakoenda kwa hiyo Mungu hufunga mlango kwaajili yao, mchango wao wa kimwili na kiroho na kiushirika unakuwa umeishia hapo ambapo Mungu amekusudia uishie, huu ni ukweli ulio mchungu katika maisha, lakini hatuna budi kuukubali na kuujifunza na kujua kuwa ni mapenzi ya Mungu., Kama wana kazi nasi Mungu atawaleta tena Mara.

Muhubiri 3:1-8 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.”

Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na uhusiano uliofifia au uliokufa au ulioondoka na faida zake katika ufalme wa Mungu, tutajifunza namna unavyoweza kuelewa Mapenzi ya Mungu watu wanapokuacha na kuondoka zao katika maisha yako, Utajifunza namna na jinsi unavyopaswa kutokuhuzunika na kuwa na mashaka watu wanapokuacha na kukuona huna maana kwao, na kuona ya kuwa hawakuhitaji tena, hupaswi kulazimisha, wala hupaswi kujikomba komba, wewe umeumbwa kwa thamani kubwa sana  na; Ni Mungu tu aliyekuumba ndiye anayeijua thamani yako, kwa hiyo hatujifunzi kubomoa uhusiano hapa katika somo hili lakini tunajifunza kuwaachia watu wanaojiondoa katika maisha yetu wajiondoe, wataendelea kuwa rafiki zetu, na tutaendelea kuwapenda, lakini kama hawajihusishi na maisha yetu hatupaswi kuumia lazima ufikie wakati ukubali waende na ujue ya kuwa Mungu ameruhusu waende zao!, na kuna faida zake katika hilo, kwa hiyo hupaswi kulazimisha wakae, kwani unapojaribu kulazimisha kuwa na watu ambao wameshajiondoa katika maisha yako au Mungu amewaondoa katika maisha yako hii maana ni nini? Maana yake yake unajaribu kung’ang’ania, na kulazimisha kitu ambacho, Mungu ameshamalizana nacho katika maisha yako!, fahamu kuwa kila mtu ambaye Mungu alimleta kwako alimleta yeye kwa kusudi la kukujenga na kukupa changamoto na unapofika wakati mtu huyo au watu hao wanaondoka fahamu kuwa ni Mungu amewaondoa kwako kwa kusudi maalumu, kwa hiyo hupaswi kushangaa, kulalamika au kujifikiri kuwa una mapungufu na kulalamika na kuhuzunika na kulaani hapana!

Kifungu kile cha msingi tulichokisoma leo, ndicho ambacho kinabeba mafunuo yote ambayo Mungu amekusudia kutufundisha katika siku ya leo kwa mfumo wa kichambuzi (an Expository preachings) na tutakiangalia kupitia mstari kwa mstari tukizingatia vipengele husika katika somo hili hebu tukisome tena na kisha tutakifanyia uchambuzi wake

Yohana 6:65-69 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Tutajifunza somo hili “Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Mungu ndiye mwanzilishi wa uhusiano.

·         Maumivu ya kuvunjika kwa uhusiano.

·         Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?

 

Mungu ndiye mwanzilishi wa uhusiano

Yohana 6:65 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”

Katika kifungu hiki Yesu Kristo anatufunulia jambo ambalo sio tu linatokea katika maisha yake lakini vile vile linatokea katika maisha yetu kama watoto wa Mungu, Yesu alizungumza hili kuhusiana na wanafunzi wake akieleza kuwa hakuna mtu awezaye kuja kwake isipokuwa amejaliwa na baba yake wa Mbinguni, hili linatufunualia sisi nasi kuwa Ni Mungu ndiye anayeruhusu watu watukaribie na ni Mungu ndiye anayeruhusu watu waondoke,  Marafiki zetu wanaweza kuwa msaada mkubwa sana katika maisha yetu, wanaweza kutumiwa na Mungu kututia moyo, kutusaidia, kutujenga na kutupa ufahamu fulani katika safari zetu za kiroho na kimwili na kisaikolojia na kimakuzi, kwa hiyo marafiki ni neema ya Mungu, ni kupitia mahusiano ya kirafiki Mungu huwatumia marafiki kutuonyesha upendo, kutuonyesha namna na jinsi Mungu anavyojali, na hata kututia moyo na wakati mwingine huwatumia kutupa changamoto, kwa hiyo kila urafiki ni lazima utunzwe na kuchukuliwa kama zawadi ya Mungu katika maisha yetu na kuwa kupitia wao liko kusudi la Mungu, marafiki wengine huokoa maisha yetu kutoka katika maangamizi ya adui, wengine hutufundisha kuwa hata kama wako watu wanatuchukia bado wako ambao wanatuthamini sana na wanathamini mchango wetu na umuhimu wetu katika dunia hii, wengine hutusaidia kukua kiroho, na wengine tunawasaidia wao kukua kiroho na kadhalika kwa ujumla tunahitajiana na ndio maana tunahitaji ushirika.

1Samuel 18:1-5 “Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.”

Daudi hakukubalika sana kwa Sauli lakini hata hivyo mwana wa mfalme Yonathan alikuwa rafiki mwenye kufaa sana kwa Daudi, maandiko yanaeleza kuwa Yonathan alimkubali Daudi na na watu hawa walikuwa na agano la urafiki uliodumu sana hata baada ya maisha yao, ulikuwa ni urafiki wa kweli na wenye kufaa sana, ulikuwa ni urafiki wenye uhusiano wa kina kama uhusiano wa ndugu, Yonathan alikuwa mwelewa kwa rafiki yake Daudi, Yonathan aliyajua mapenzi ya Mungu yaliyokuwa juu ya Daudi, Yonathan hakuwa rafiki mwenye wivu wala hila, Yonathan alimtia moyo Daudi, alimpa mavazi ya kifalme aliyotumia mwenyewe, alimpa silaha, alimlinda alikuwa akimtakia mema, pamoja na kuwa baba wa Jonathan hakumpenda Daudi, alimchukia alimkusudia mabaya lakini haikuwa hivyo kwa Yonathan yeye alikuwa rafiki wa kweli. Na mtu ambaye aliangalia maslahi ya Mungu kwa upana. Hakuwahi kumponda wala kumchafulia sifa yake wala kutaka rafiki yake asipate kibali kwa mfalme, wakati wote Yonathan alikuwa faraja kubwa

1Samuel 19:4-6 “Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure?Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa.”

Kwa ujumla Yonathan alikuwa rafiki wa kweli kwa Daudi, alikuwa ni zaidi ya ndugu, alilinda uhai wa Daudi, na hakukubali maisha ya Daudi yawe hatarini wakati wote alitengeneza mazigira mazuri, ili raiki yake akubalike kwa baba yake asionekane kuwa muhalifu, alimtetea na kumtia Moyo na alimjulisha kuhusu hatari ambazo zingeweza kumkabili, kama tunataka kujifunza watu waliokuwa na urafiki wa dhati basi Daudi na Yonathani ni mfano wa kuigwa, Yonathani alikuwa ni rafiki aliyeambatana na Daudi na mwenye kufaa sana kuliko ndugu.

Mithali 18:24 “Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.”              

Marafiki zetu hawaji wenyewe kwetu huwa tunaletewa na Mungu na Mungu ndiye anayewavuta watu kuja kwetu, kama vile tu alivyowavuta wanafunzi kuja kwa Yesu Kristo, hakuna mtu awezaye kuja kwangu, isipokuwa amejaliwa na Baba yangu, Neno hilo kujaaliwa katika kiyunani linatumika neno “Didōmi” kimatamshi ni Did-o-mee ambalo maana yake “with the palm of hand” yaani ni tendo la Mungu kuushika mkono na kumleta mtu moja kwa moja na kushikisha katika kiganja cha mkono wa mwingine kama tu vile mtu anayemkabidhi bibi harusi kwa mumewe siku ya harusi yake, kwa hiyo Ni Mungu Baba ndiye anayetushika mkono na kutupeleka katika mikono ya Yesu, hali kadhalika ni Mungu ndiye anayewashika mkono wale waliokusudiwa kuwa rafiki zetu na kuwaleta katika mikono yetu, Kwa hiyo ni muhimu sana kutomchukulia kwa dharau mtu awaye yote anayetamani kuwa na urafiki na wewe kwa sababu kila unayeletewa au anayekujia analetwa kwako na Mungu kwa kusudi maalumu katika maisha yako na kwa ufalme wa Mungu, wakati wote watu wanapokuwa marafiki mioyo yao inaunganishwa kuwa kitu kimoja kwaajili ya mafanikio ya yule ambaye Mungu amemkusudia au kwa kufaidiana, na kila wakati Mungu huhakikisha kuwa pande zote mbili zinanufaika na urafiki huo, kwa hiyo wote mnajengana na kufaidiana kwani chuma hunoa chuma Mithali 27:17 “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.” Marafiki zetu huletwa kwetu na Mungu kwa kusudi la kutusaidia na sisi kuwasaidia na wakati mwingine kwajili ya kufaidiana, kama Barnaba na Sauli au Paulo

Matendo 9:26-28 “Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka.”

Maumivu ya kuvunjika kwa uhusiano.

Yohana 6:66 “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.”

Hata hivyo Pamoja na kuwa Mungu huwaleta watu karibu nasi kama tulivyojifunza kutoka kwa Bwana Yesu ni jambo la kusikitisha kuwa, kuna wakati  mwingine wengine wataondoka kama ilivyokuwa tu kwa Yesu, watu au wanafunzi wengi siku hiyo waliamua kuondoka tena biblia inasema wasiambatane naye tena, hapa ni kwa sababu walishindwa kupokea mafundisho yake magumu katika akili zao, jambo hili linatufunza ya kuwa si kila mtu anayeanza safari pamoja nasi atakuwa pamoja nasi mpaka mwisho, na wakati huu ni wakati wa maumivu makali sana hakuna jambo linaumiza kama kuvunjika kwa mahusiano, yawe ya ndoa, yawe na ushirika, yawe ya kichungaji, kazini na kadhalika, lakini Mungu huruhusu watu hao waende na huo ndio unakuwa mwisho wa stori yao katika maisha yetu, inauma sana na inaumiza sana lakini hatuna budi kukubali, kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristo ambapo wanafunzi wake walimuacha na hawakuambatana naye tena ndivyo ilivyo kwetu pia kuna kusudi kwa kila jambo katika maisha yetu,  wakati huo hakuna lolote tunaloweza kulifanya kuwafanya wabaki, Mungu tayari amekwisha kukusudia, wakuache wale wanaokupenda kwa dhati hawawezi kukuacha  watabaki na wewe iwe jua iwe mvua lakini wale ambao Mungu amekusudia waende wataenda tu hakua namna unaweza kulizuia hilo, hukuwaleta wewe kumbuka kwa hiyo  acha waende zao kwa amani, Kama Mungu ndiye aliyeamua waende hakuna unaloweza kulifanya wasiende?

Mungu ndiye mwenye funguo na mamlaka za kufunga na akifunga hakuna afunguaye, na akifungua hakuna anayeweza kufunga unaweza kujaribu kubembeleza na kujipendekeza kwa watu na ukajitahidi kuwapendeza na kufanya vizuri lakini kama Bwana hajaruhusu utakuwa unajisumbua bure, kile utakachokuwa unakitafuta ni kutafuta maumivu ya moyo tu, jaribu njia mpya na waache waende usiumie wala usikwazike ni Mungu ameruhusu, lazima tuamini kuwa Mungu ndiye anayedhibiti watu kuja na kuondoka katika maisha yetu na wengine huletwa kwetu kwa majira fulani tu kisha anawaondoa, unapoendelea kuwang’ang’ania watu ambao wamepoteza maana katika maisha yako maana yake unazuia kusonga kwako mbele au kukua katika kiwango kingine. Rafiki mimi ninajua uchungu wa kupoteza marafiki, ninapenda watu sana, sitaki kila ambaye amewahi kuwa rafiki yangu aniache, lakini uko wakati unalazimika kufanya hivyo, wako wapi uliosoma nao shule ya msingi, sekondari, vyuoni, na hata katika utumishi huu wako wapi? Wako wapi uliofanya nao kazi zamani,? Ulifika wakati waliondoka na Mungu aliwaficha na hukuweza kuwaona tena, kusudi la kuwepo kwao katika maisha yako lilikwisha kutimia na sasa Mungu anataka ufungue ukurasa mpya. Ona mfano wa maumivu yaliyomkuta Naomi:-

Ruthu 1:3-18 “Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Wakakaa huko yapata miaka kumi. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula. Basi akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; Bwana na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. Bwana na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako.Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa Bwana umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”

Tunasoma habari za Naomi, ambaye mumewe alifariki na kumuacha na watoto wawili ambao nao baadaye walioa, lakini vile vile walikufa katika nchi ya Moabu, kwa hiyo Naomi alibaki peke yake yeye na wakwe zake, Naomi aliamua kurudi kwao Yuda na aliwaeleza wakweze juu ya maamuzi yake mmoja aliitwa Orpa na mwingine Ruthu, Ruthu aliamua kubaki naye na Orpa aliamua kubaki katika inchi yake, wote walimpenda mkwe wao Naomi lakini Orpa aliamua kumbusu Naomi na kuondoka, Naomi hakuanza kulalamika kuwa Orpa anaondoka hata pamoja na wema wote aliomtendea na malezi yote aliyowapa Naomi alielewa kuwa huu ni msimu mpya ni msimu wa mabadiliko katika maisha kwa hiyo alikuwa na amani alipoachwa na Orpa alikubali kuwa Orpa aende na asiwe sehemu ya maisha yake tena, Mtu aliyekomaa kiroho/na kiufahamu huwaachia watu waende, unakubali Mungu awaondoe watu fulani katika maisha yako, Mungu ndiye anayefunga mlango au kufungua, lakini Ruthu aliamua kubaki na Naomi kwa gharama yoyote ile, hii ndio hali halisi, Yesu watu waliondoka na hakutikisika aliwauliza waliobaki naye je ninyi nanyi mwataka kuondoka? Aliendelea kuacha mlango wazi kwa kila anayetaka kumuacha, Naomi Orpa aliondoka ulikuwa wakati mgumu na wa maumivu makali sana, ulikuwa ni wakati mgumu ulikuwa ni wakati wa machozi lakini hakuna tunachoweza kufanya pale watu waliokuwa rafiki, waliokuwa ndugu waliokuwa jamaa zetu, waliokuwa wenzetu waliokuwa tunashinda nao, na kuzungumza nao wanapoamua kutuacha ni vema kukubali waende, Naomi alimbusu Orpa na kumuacha aende, kumbuka  hatuhitaji kufukuza mtu au kumaliza nao vibaya wala kuwa na uadui nao lakini sasa wanaondoka utafanya nini tuwaache waende zao kwa Amani huo ndio ukomavu wa kifikra na ukomavu kiroho na ujuzi, sio wewe tu utaacha wewe pia unaweza kuachwa na watu uliowapenda lakini wakawa hawakuhitaji tena huwezi kubadili pai isiwe 22/7  ni lazima ukubaliane na ukweli wa mambo hata kama ni mchungu kiasi gani waache waende! 

Yesu aliwahi kuwafundisha wanafunzi wake kuwa sio kila mahali watawakubali, ziko sehemu nyingine watu watakukataa hawatafungua mioyo yao kwako, watakukataa hawatakukaribisha unajua unachotakiwa kukifanya ni kukung’uta mavumbi ya miguu yako kisha enenda kule ambako watakukaribisha, hii sio kwa ugomvi ni sehemu ya kawaida kabisa katika maisha kwamba watu watakuja kwetu na kisha wataondoka na sisi halikadhalika.

Mathayo 10:13-14 “Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.”

Matendo 18:6-8 “Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.”

Usijisumbue na watu ambao hawakutaki, watu ambao hawaoni thamani yako, wala usijaribu kuwashawishi, endapo utafanya hivyo utajichelewesha na utajipatia fadhaa bure, Ni kweli Mungu anaweza kuwabadilisha  kama watatakiwa kukuunga mkono lakini kamwe usijaribu kujilazimisha kuungana na watu wasiotambua uthamani wako, damu ya kifalme ya Yesu Kristo inatitiririka katika mwili wako wewe sio wa kawaida wewe ni mali ya Mungu na ndio maana Mungu alikuokoa na amekuumba kwa sura na mfano wake kwa hiyo usiwashawishi watu wakukubali kama mioyo yao imefungwa, Mungu ameandaa watu tayari wanaotambua uthamani wako, inaweza kuwa inauma sana lakini ndio ukubwa achana nao waache waende, katika maisha yetu wako Orpa wengi lakini vile vile wako Ruthu wengi ambao wamepangiwa kutokutuacha watakaokaa nasi, na kuambatana nasi wanaoondoka ni kuwa Mungu amemalizana nao katika kusudi lao kwako na wanaobaki ni wale ambao Mungu anataka ushirikiane nao Baraka zako, wale walio kama Ruthu watabaki kuwa waaminifu kwako  na hawatakuacha daima, hatupaswi kumfukuza mtu wala kumpiga teke mtu lakini acha wao watupige teke na kutufukuza na hapo neema ya Mungu ya urafiki wetu kwao itakuwa imefikia ukingoni  inasikitisha inaumiza sana lakini huu ndio ukweli katika maisha.

Matendo 15:36-40 “Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro.Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.”

Paulo na Barnaba walikuwa marafiki, waliitwa pamoja  na Roho Mtakatifu katika kazi ya huduma, waliihubiri injili kwa pamoja kimsingi Barnaba alikuwa ni kama Mchungaji wa Paulo mtume, ni yeye ndiye aliyemtambulisha kwa mitume na ni yeye aliye mpeleka Antiokia, walizoeana sana, waliitwa kwa pamoja na Roho Mtakatifu kwa kazi ya umisheni, lakini ulifika wakati wakaachana haikuwa kwa lengo baya wala kwa ugomvi, lakini ulifika wakati ambapo Mungu alikusudia kila mmoja awe na njia yake hili ni jambo la kawaida sana katika maisha wao tofauti yao ilikuwa ni Marko, nadhani inawezekana Marko alijisikia vibaya maana Paulo alimuona ni mtu dhaifu, Lakini Barnaba aliona Marko anahitaji malezi tu kwa hiyo kulitokea tofauti na kulitokea matengano, Lakini Mungu ni mmoja, miaka mingi baadaye, Paulo aliutambua umuhimu wa Marko na aliomba aungane naye maana anamfaa kwa huduma! Angalia:-

2Timotheo 4:10-11 “Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.”

Paulo alimkumbuka Marko na kuagiza aletwe kwake kwa sababu ana faida nyingi sana kwa utumishi, kumbe kuna mtu anaweza asiwe na faida kwako leo, lakini akawa na faida kwako kesho, unaweza usimuhitaji mtu leo lakini ukamuhitaji mtu huyo kesho, Mungu ndiye anayehusika anaweza mtu asikufae kwa jua akakufaa kwa mfua na anaweza mtu asikufae kwa mvua akakufaa kwa jua hii ndio dunia ya Mola kwa hiyo tuheshimu mahuisiano sana  na kuyatunza isipokuwa pale to Mungu anapoamua huyu aende kule na huyu aje hapa kwa makusudi yake mema.

Wakati mwingine mafanikio yetu yanaweza kuwavuta watu wengi sana kwetu, na mapito yetu yanaweza kuwafanya wengi watukimbie, unapitia upweke? Wakati wa changamoto hakuna mtu wa kukutia moyo? Hii ilimpata Ayubu Maandiko yanasema watu wa nyumbani mwake walikuwa wengi sana ona

Ayubu 1:3 “Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, NA WATU WA NYUMBANI WENGI SANA; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.”

Unaona tunasoma kuwa watu wa nyumbani kwa Ayubu walikuwa wengi sana wakati wa mafanikio yake, lakini wakati wa dhiki yake watu wote walimuacha na kundoka zao, hata hivyo wakati wa mafanikio yake walirejea tena kwa wingi sana, hili nalo ni jambo la kawaida katika uanadamu kwa hiyo usivunjike moyo unapopitia upweke!  

Ayubu   42:10-12 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote Bwana aliouleta juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu.”

Wakati mwingine watu, na marafiki zako watakuacha kwa sababu tu unapita katika hali ngumu, lakini wanaweza kukurudia tena hali inapokuwa nzuri hili nayo ni jambo la kawaida katika maisha na hatuna budi kulielewa na kukubaliana nalo. Jambo kubwa la msingi ni kwamba mahusiano yanapaswa kutunzwa na kuwa na Amani na watu woe ni swala la smingi sana tuwapo duniani. lakini watu wanapoondolewa kwetu, tumshukuru Mungu kwaajili yao                                  

Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?

Yohana 6:67-69 “Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Yesu anatufundisha kuwa yeye alikuwa tayari kuwaacha watu waende zao, Kama wamechagua kwenda hakuwalazimisha kubaki nao lakini aliwapa uhuru wa kuondoka ili wafanye maamuzi yao wenyewe, waache waende zao kwa Amani, kama wamejisikia raha kuwa mbali na wewe wamejisikia Amani kukuacha acha waende! Na kama wamejisikia kubaki acha wabaki na wewe usiwalazimishe, kulazimisha watu wawe nawe wakati hawana Amani ya kuwa na wewe kutasababisha uchungu katika maisha yako, kukosa utulivu na majuto, lakini kama utawaacha waende watapata nafasi mpya na kujiamulia mambo yao wenyewe, wape watu uhuru wa kuamua  na Amani ya Mungu itaamua. Na huu ndio ukomavu wa kiroho, kiufahamu na kihekima. Let them go !

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

Amini katika kusudi la Mungu kwamba Mungu anaporuhusu watu waende zao na au wabaki na wewe ufahamu kuwa Mungu ana mpango mkubwa na mpya na kila mmoja, inaweza kuwa ngumu kuelewa lakini hatuna budi kuamini katika mpango wa Mungu kwa kuwa Mungu ni mwema, watu wanapoondoka katika maisha yako iwe kwa wema au kwa ubaya bado fahamu ya kuwa Mungu ana mpango mwema kwenu wote yeye huweza kuitumia njia yoyote ile katika kutokeza jambo lililo jema zaidi.

Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”              

Rafiki wa kweli ni yule atakayesimama na wewe hata katika hali ngumu, Petro na wale thenashara walichagua kubaki na Yesu, Petro alisema tuende wapi Bwana wewe una maneno ya uzima wa milele, wako marafiki watakaa na wewe kwa muda mfupi, au watajitokeza kwako katika wakati Fulani maalumu na kisha watakoma lakini marafiki kama Petro kwa Yesu Kristo watamaanisha kubaki na wewe, kwa hiyo ni Muhimu kutambua umuhimu wao na kumshukuru Mungu kwaajili yao. Wakati wote kumbuka kuwa uhusiano wowote ule uwe wa muda au ule wa kudumu una kitu cha kutufundisha katika maisha yetu, hatukutanishwi na watu kwa bahati mbaya, Mungu hakumuumba mwanadamu awe peke yake, tunahitajiana, Lakini Mungu huruhusu watu waje na kuondoka katika maisha yetu kwa kusudi maalumu,  jambo kubwa na la msingi ni sisi kuendelea kuwa waaminifu katika kila aina ya uhusiano ambao Mungu ametupa kumbuka mahusiano yanapovunjika inaleta maumivu makali sana lakini wale wanaoondoka waache waende na wale wanaobaki kaa nao kumbuka kuwa ni Mungu ndiye anayewashika mkono na kuwaleta kwetu kwa hiyo amini katika mchakato huo na utakubali ukweli huu mchungu katika maisha, wafurahie sana wale wote ambao Mungu anawaleta katika maisha yako ukijua kuwa ni sehemu ya mpango wa Mungu,  wakubali wale wote ambao Mungu ameruhusu waende zao mbali na wewe ukijua pia kuwa Mungu ana mpango mwema, thamini umuhimu na msingi wa marafiki  hususani wale wanaobaki kuwa waaminifu kwako hasa wakati wa majaribu na wakati wa mambo magumu, waheshimu wote wapende wakubali lakini usilazimishe mtu akupende au awe na wewe hii haimaanishi uwatendee watu kikatili hapana lakini jifunze kuwa kama Yesu, Yesu aliwahoji hata wale waliobaki je ninyi nanyi mwataka kuondoka?  

Hatima yako haiko mikononi mwa waliokuacha, wala Mungu haitaji lolote uliloliacha au chochote ulichopoteza kupitia marafiki walioondoka, jambo kubwa la msingi uwe na Amani lakini usilazimishe watu wakupende na kukubali au wakuamini, ukiona wamekuacha maana yake huwahitaji tena, wao sio sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha yako tena na Mungu ana mpango mwema na wewe na hata wale wanaokusema vibaya waache waseme, mimi nimewahi kusikia habari za mtu anayenisema vibaya na nikaonyeshwa sijawahi kumkataza wala kumbeleza aniseme vizuri, ninajua tu kuwa Mungu ameruhusu wawepo watu watakaonisema vizuri na wawepo watu watakaonisema vibaya wote wana faida katika mapenzi ya Mungu, wanaonisema vibaya wananisaidia nisiwe na kiburi, nikumbuke kuwa mimi ni mwanadamu na nizidi kunyenyekea na wale wanaofaidika na huduma yangu watamshukuru Mungu kwaajili yangu, sina muda wa kumbembeleza mtu asiniseme vibaya, siumii tena na wanaosema vibaya wala siwezi kutukuka watu wakinisifu, ninanyenyekea kwa Mungu kwa sababu mimi ni udongo tu, sikuja duniani kusifiwa, nimekuja duniani kutimiza kile ambacho Mungu amekikusudia katika maisha yangu na hivyo kile nitapangiwa na Mungu kukifanya nitakifanya, Petro alitambua ya kuwa Yesu ana maneno ya uzima wa milele, na ya kuwa ni Mtakatifu wa Mungu yaani ni Masihi.

Bwana ampe neema kila moja wetu kuelewa makusudi ya somo hili kwa kina na mapana na marefu katika jina la Yesu Amen!

 

Na. Rev Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Alhamisi, 10 Oktoba 2024

Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli!


1Timotheo 5:1-5 “Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.”




Utangulizi:


Moja ya maswala ambayo nyakati za kanisa la kwanza yalipewa kipaumbele sana ni pamoja na kuwahudumia wanawake waliokuwa wajane kwelikweli, Swala zima la kuwakumbuka wajane lilipewa uzito mkubwa sana katika kanisa la kwanza kuliko ilivyo katika nyakati za leo, na inawezekana moja ya sababu kubwa inayofanya kanisa la leo kujisahau ni pamoja na kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu somo hili, Lakini kwa neema ya Mungu, Roho Mtakatifu Mwalimu mkuu leo anataka kutukumbusha tena namna na jinsi ya kuwaheshimu wajane kama tutakavyoweza kujifunza kwa kina na mapana na marefu katika siku hii ya leo.


Yakobo 1:25-27 “Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai.Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.” 


Mungu anawajali sana wajane na kujihusisha sana na maisha yao na anatoa wito kwa kanisa lake na watu wake na jamii kufanya kitu kwaajili ya Wajane, Mungu aliwapa wajane kipaumbele kikubwa sana nyakati za agano la kale na kuwaweka katika uangalizi maalumu chini yake mwenyewe. 


Zaburi 68:4-6 “Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.”

 

Kutokuwafikiria wajane nyakati za kale kulifikiriwa kuwa ni moja ya sababu ya kuleta maovu na changamoto katika maisha yako, na ndio maana unaweza kuona Yakobo akifikiri ya kuwa dini ya kweli ni lazima ihusishe kuwaangalia au kuwajali yatima na kuangalia mahitaji yao, Ayubu aliwahi kusema hivi alipokuwa akijitetea sababu ya changamoto zilizompata katika maisha yake na rafiki zake nay eye akadhani kuwa labda ni moja ya sababu ya mateso yake:-


Ayubu 31:15-17 “Je! Huyo aliyenifanya mimi ndani ya tumbo, siye aliyemfanya na yeye? Si yeye mmoja aliyetufinyanga tumboni? Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, Au kama nimeyatia kiwi macho ya mwanamke mjane; Au kama nimekula tonge langu peke yangu, Mayatima wasipate kulila;”


Kwa hiyo ilieleweka wazi katika nyakati za waanzilishi wa Imani ya kuwa kutokuwajali yatima kunaleta mikosi na balaa kwa sababu kutokuwajali hao au kuwadhulumu na kutokuwapatia haki pamoja na yatima kunaweza kuwa sababu ya laana nyingi, na ndio maana utaweza kuona kuwa nyakati za kanisa la kwanza kulikuwepo na mgao maalumu wa mahitaji na chakula kwaajili ya wajane  na hali kadhalika utaweza kuona katika kifungu chetu cha msingi Paulo Mtume akimuagiza Timotheo kuwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.

Kumbukumbu 24:17-22 “Usipotoshe hukumu ya mgeni, wala ya yatima; wala usitwae mavazi ya mjane, yawe rehani; bali kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika Misri, Bwana, Mungu wako, akakukomboa huko; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako. Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane.Nawe kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.”


Kwa msingi huu leo tutachukua muda kujifunza sasa kwa kina na mapana na marefu namna na jinsi tunavyoweza kuwatambua na kuwatendea mema au kuwaheshimu wajane walio wajane kwelikweli na tutajifunza somo hili muhimu kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:-


Maana  ya neno Mjane 

Ufahamu kuhusu changamoto wanazokutana nazo wajane 

Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli


Maana ya neno Mjane


Neno mjane ambalo katika kiingereza linajulikana kama neno “widow” katika biblia ya kiibrania linatumika neno  “almānāh”   na katika maandiko ya kiyunani linatumika neno “Chēra”  yote yakiwa na maana ya Mwanamke aliyepoteza mume wake kwa sababu ya kifo na ambaye hajaolewa tena, Mwanamke aliyeachwa baada ya kifo cha mumewe, Mwanamke aliyebaki peke yake, ni mwanamke ambaye mumewe amafariki na ameachwa mwenyewe na kwa sababu hiyo anakutana na changamoto kadhaa wa kadhaa katika jamii, ni mwanamke aliyefiwa lakini anakabiliwa na mapungufu, anakabiliwa na uhitaji, hana ulinzi wala msaidizi, hana hali nzuri ya kiuchumi na kihisia anapitia mambo magumu. Kutokana na hali hiyo nyakati za agano la kale wajane waliwekwa katika kundi la watu wanaohitaji msaada kama wakimbizi, masikini na yatima, au pamoja na kundi la walawi, waliokuwa watumishi. 


Kumbukumbu 14:27-29 “na Mlawi aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja nawe. Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba Bwana, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo.”


Kuwajali wajane kama ilivyo kuwajali walawi, na yatima na wageni na masikini, katika maagizo ya Mungu kulikuwa kunafungua milango ya Baraka kubwa sana katika maisha ya wanadamu, maandiko yaaagiza kuwa watu hao waheshimiwe maana yake mtu asitumie nafasi ya ujane wao kuwadhulumu, kuwaonea na kuwafanyia jambo lolote lisilofaa, wakati mwingine katika hali ya ujane hivyo ziko mila na desturi mbaya miongni mwa jamii, na fikra potofu ambapo pia watu hao hufikiriwa kuwa wana nuksi, Mungu aliliona hilo na kulichungulia na anaweka katika utaratibu wa neno lake kuwa watu hao wapewe kipaumbele maalumu, aliwataka Israel hata wanapovuna chakula wabakize makombo ili yamkini watu hao duni wapate cha kuokoteza nyuma ya mashamba ya wenye uwezo. Pia Mungu aliweka sheria nyinginezo mbalimbali za kimila ili wajane warithiwe kwa kusudi la kuinua uzao wa Ndugu au kuwapa ulinzi na kadhalika hii yote ilikuwa ni kwa sababu ya kutafuta kuwatunza


Nyakati za kanisa la kwanza Mitume walikuwa na ufahamu kuhusu huduma kwa wajane na moja kwa moja tunaona nyakati za kanisa la kwanza kulikuwa na huduma maalumu ya chakula na mahitaji mengine na mgao wa kila siku kwaajili ya wajane 


Matendo 6:1-4 “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”

 

Ufahamu kuhusu changamoto wanazokutana nazo wajane 


Kabla ya kujifunza kwa kina na mapana na marefu, kwanini Mungu anawapa kipaumbele Wajane, ni muhimu kukumbuka kuwa wajane ni watu wanaopitia changamoto kadhaa wa kadhaa ambazo inawezekana watu wengi wakawa hawafahamu na au labda tu hatujawahi kutoa kipaumbele lakini mara tu baada ya mjane kupoteza mwenzi wake aliyeishi naye kwa muda mrefu, jambo ambalo linamuacha akiwa mpweke na mwenye msongo wa mawazo, na msiba unapoisha tu mjane huanza kujihisi kuwa ametelekezwa, au ametupwa na hapo ndipo neno la Mungu linatuagiza kujali na kutambua mahitaji yao na kuwatia moyo kwa kuwabebea mizigo wa moyoni.


Changamoto za kihisia – wote tunatambua kuwa hakuna jambo baya duniani kama kufiwa, linapokuja swala la msiba wewe lisikie kwingineko tu lakini omba Mungu lisikukute, kufiwa ni jambo zito zito zito mno, na kufiwa na mtu aliye karibu na mliyeishi naye kwa muda mrefu kunaacha mshituko mkubwa, simanzi nzito, kupoteza, upweke, kuachwa na kutelekezwa, linapokukuta swala la msiba wa mtu ambaye alikuwa ni kipenzi chako wa karibu haijalishi kuwa mlikuwa mkifarakana au kugombana ghafla unahisi kama umeadhibiwa, umeumbuka, ni kama una nuksi au dunia na Mungu amekukataa, hisia hizo zote zinakuwa juu ya mjane hata kama atakuwa ameachiwa mali nyingi kiasi gani, lakini kibinadamu linakuwa ni jeraha la kimaisha. 


Kutelekezwa katika kiingereza linatumika neno abandonment  ambalo maana yake ni  leaving someone or ending or stopping something usually forever, kumuacha mtu, au kumtupa, au kumalizana naye au kumaliza uhusiano na yeye, au kuacha kuwasiliana naye na kwa kawaida milele, hili ni tukio baya sana ambalo kimsingi Mungu hawezi kuthubutu kulifanya. 


Maombolezo 3:3-33 “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.” 


Kwa msingi huo inapotokea Mungu ameruhusu mwanadamu Fulani hasa mume kuondoka katika ulimwengu huu, mjane hupatwa na hisia za kutupwa, na hasa pale waombolezaji wanapoondoka na mfiwa anaanza kubaki mwenyewe, uhalisia wa msiba ndio unaanza, mfiwa anajikuta anajuta, anaanza kuhisi umuhimu wa yule aliyeonmdoka, pengo lake, na kama aliugua unaanza kuhisi kuwa labda ungempeleka hospitali Fulani ingekuwa kuna nafuu na kadhalika kwa hiyo simanzi huanza kuusonga moyo wa mjane. Kwa hiyo mara moja mwanamke anapofiwa na Mumewe watu wa Mungu hawana budi kujifunza namna ya kuwatetea wajane na kuwalinda jambo hili litawaletea Baraka kubwa sana


Isaya 1:16-17 “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.


Zekaria 7:9-10 “Bwana wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma; tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake.” 


Changamoto za kiuchumi -  Nyakati za Biblia kwa kiwango kikubwa sana au zamani wanawake wengi walikuwa wanawategema waume zao katika maswala ya kiuchumi, hata siku za leo pamoja na kuwa wanawake wengi wamepata mwamko mkubwa sana wa kujishughulisha hata hivyo bado ni jukumu la Mume kuitunza familia na kuitia moyo, kuisimamia kama kichwa cha nyumba na kama wanasaidiana ni njema sana sasa inapotokea mume amefariki bado inaleta mtikisiko mkubwa wa kiuchumi kwa mmoja anayesalia kwaajili ya kuitunza familia iliyobaki naye kwa hiyo changamoto za kiuchumi ni moja ya tatizo linalowakumba wajane, wanaweza kupoteza njia na namna ya kujikimu, na kwa sababu ni wanawake wakati mwingine hata kimila na desturi za baadhi ya watu wanaweza kuwaonea  na hata kutaka kuwadhulumu wanawake hao wajane  na ndio maana utaweza kuona Mungu aliweka sheria kali sana za kuwalinda wajane, kwani wakati mwingine pia walikabiliwa na madeni waliyoyaacha waume zao, au kupokonywa rasilimali na kadhalika  


Kutoka 22:22-24 “Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.


2Wafalme 4:1-7 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe,Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.” 


Aidha Mungu aliagiza kuhakikisha kuwa unawasaidia wajane kwa masazo ya chakula hasa wakati wa mavuno ili na wao waweze kuokoteza na kukidhi mahitaji yao, kwa lugha nyingine Mungu anataka tuwakarimu wajane, tusiende kwao mikono mitupu, tuwasaidie tuwabebe kiuchumi, lakini tuwakumbuke katika maisha


Kumbukumbu 24:19-21 “Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako. Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane.


Changamoto za upweke – Wajane katika namna mbalimbali huwa wanahisi kukumbwa na upweke, kuondokewa na ulinzi na heshima, wanahisi wametengwa na jamii kwa kiwango kikubwa, mabadiliko makubwa na ya ghafla katika hali ya ndoa yanaingiwa na giza,  na wakati mwingine katika jamii nyingine hufikiriwa kuwa ni mojawapo ya sababu ya vifo vya waume zao, na hivyo hulaumiwa  jambo hili na sababu nyinginezo zinaweza kuchangia wao kuhisi kutengwa na jamii, kuwa wapweke, na kutoa mwanya mdogo sana kati ya changamoto za kihisia na upweke na kuongeza madonda mwilini, wanawake wengine hufikiriwa kuwa na nuksi au kusababisha balaa na wakati mwingine wanaume wengine hufikiri kuwa mwanamke huyu ana nuksi na husababisha vifo vya wanaume wengine. 


Mwanzo 38:6-11 “Yuda akamwoza mke Eri, mzaliwa wake wa kwanza, na jina lake huyo mke ni Tamari. Naye Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mbaya machoni pa BWANA; na BWANA akamwua. Yuda akamwambia Onani, Uingie kwa mke wa nduguyo, ukamwoe, ukamwinulie nduguyo uzao. Onani alijua ya kwamba huo uzao hautakuwa wake, ikawa, alipoingia kwa mke wa nduguye, akamwagia chini asimpe nduguye uzao. Neno hili alilolifanya likawa baya machoni pa BWANA, basi akamwua yeye naye. Yuda akamwambia Tamari mkwewe, Ukae mjane nyumbani mwa baba yako hata Shela mwanangu atakapokuwa mtu mzima, maana alisema, Asipate kufa yeye kama nduguze. Basi Tamari akaenda, akakaa nyumbani mwa babaye.” 


Tamari alikuwa moja ya wahanga wa ujane, alifiwa na waume wawili na Yuda aliahidi kumuoza mwanae mwingine aitwaye Shela, hata hivyo hakufanya hivyo kwa hofu kuwa mwanamke huyu ana nuksi huenda atasababisha kifo cha mwanaye mdogo, kwa hiyo Tamari alijilipizia kisasi kwa kulala na Yuda mwenyewe na ndipo ukoo wa Masihi ulipotokea kwa kumzaa Peresi Zera kupitia Yuda mwenyewe badala ya watoto wake, ujane una mitihani mingi, wako wanaolenga mali zao, wako wanaowafikiria kuwa labda ni wagonjwa na wanawaogopa hata kuwaoa wakijiuliza waume zao wamekufaje, wako wanaowamendea wawatweze, na wako wanaowatamani kuwatumia tu kimwili kutokana na kujua upweke walionao 


Changamoto za kimalezi – Moja ya kazi ngumu sana kwa kina mama wajane ni malezi ya watoto, wote tunafahamu changamoto za kuwa mlezi peke yako, sauti ya mume ni sauti ya mamlaka ina nguvu katika makemeo ya watoto, haijalishi nani huwa ni mkali katika malezi lakini watoto hukaa vizuri sana wanapolelewa na pande zote mbili za wazazi, kwa hiyo kama wako watoto na mume amefariki mjane huwa na wakati mgumu sana wa kuwa mlezi pekee, kukabiliana na malimwengu inaweza kuwa rahisi kuliko kulea watoto peke yako  bila mwenzi wako,  watoto watahisi lile pengo ambalo baba yao angeweza kutosha,  yako mambo ambayo baba anaweza kuwa alikuwa mzuri katika hilo kwa hiyo mama atatakiwa kufanya mara dufu kuweza kuziba, hofu kubwa ikiwa kila mtoto atajihisi sasa ni kiongozi kwa nafsi yake na hivyo mwanamke huyu atabaki anapambana kuhakikisha kuwa kila kitu kina kaa mahali pake. Ni kwaajili ya haya Mungu mwenyewe alibeba jukumu la kuwa baba wa yatima na mwamuzi wa wajane. 


Zaburi 68:4-6. “Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu


Changamoto za kiroho – hali ya kupoteza mume huhesabika kama adhabu kubwa sana kwa mwanamke kwa hiyo wengi hugeuka kuwa wakali sana wakitetea maslahi yao na kwa Mungu wanakuwa na mgogoro naye, wanahisi Mungu amewaacha na kuwatelekeza hii ni fikira ya kawaida kwa wajane wengi na ndio maana Mungu akajiwahi katika maandiko kusimama kama mtetezi wao, wengi huwa na maswali mazito hata wakati wa Msiba huwa  wanalia huku wakimuuliza Mungu kwanini kwanini, huwa wanahoji kwanini Mungu achukue mume wake, kwa nini maisha yawe hivi au vile baada ya wao kupoteza mume?  Wanahisi kuwa maisha hayana maana na kupata maluwe luwe ya kiroho wengi huchanganyikiwa na kutokuwa sawasawa, ni ukweli ulio wazi kuwa wanapatwa na mshituko wa kiroho na kuwa katika wimbi kubwa la msongo wa mawazo, msongo wa mawazo wa mtu aliyefiwa na mume ni mara nne ya wale wenye ndoa yenye mgogoro, kama alimuombea sana mumewe amuokoe na mauti na bado akafa, mjane anaweza kumuona Mungu kuwa hana maana kabisa  na kama asipojengwa vema kiroho anaweza kupoteza uwepo wa Mungu nahata kuvamiwa na pepo kwa sababau ya kuelemewa na huzuni na vita ya kiroho. Wakati mwingine wajane hufikiri kuwa Mungu anawakumbusha dhambi zao walizozifanya zamani pale wanapopata majaribu mengine ili hali wao ni wajane


1Wafalme 17:17-22 “Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka.


Changamoto za kisaikolojia – Ni ukweli usiopingika ya kuwa wanawake wajane wanapitia changamoto nyingi sana za kisaikolojia, tafiti zinaonyesha hivyo japo kanisa linaweza lisiwe na utafiti wa kina au likawa linapuuzia hilo, lakini mgandamizo wa mawazo, mashaka, hofu  na ugumu wa maisha na kukosa tendo la ngono kunatengeneza changamoto kubwa na nyingi za kisaikolojia, wajane watateseka kijamii, kiutamaduni, kiimani,kimila, kiuchumi, kiroho na kisheria  na huku upande mwingine wakiwa hawana mume  wanayapitia haya kimya kimya wakati mwingine jamii ikiwa haina hata taarifa, wanakutana na unyanyasaji wa kisaikolojia wa aina mbalimbali licha ya maneno wanayokutana nayo, ukweli ni kuwa sio rahisi sana kujua wajane wanapitia changamoto gani mpaka uwe makini, hatuwezi kushughulikia kila kitu wanachopitia lakini angalau tunaweza kuwapunguzia.  Katika moja ya utafiti uliofanyika nchini kenya katika kaunti ya Kisumu wanawake 50 walifanyiwa utafiti wa kisayansi na kujulikana kuwa bila kujali kuwa waume zao walifariki katika namna ipi  wanawake hao waligundulika kuwa na changamoto ya fadhaa kubwa, kukosa msaada, maumivu makali ya ndani, maombolezo yasiyokoma, hofu na woga, utafiti huo uliotumia njia mchanganyiko za maswali,  na kuwahoji uso kwa uso, ukusanyaji wa taarifa  na tafiti za kiushauri tafiti hizo zilizofanywa na Atindabilal, Bamford, Adatara, Nauko na Obenwa mwaka wa 2014  ulibaini kuwa changamoto wanazokutana nazo wajane kisaikolojia na kuzinukuu kama walivyoorodhesha kwa kiingereza “mental and emotional challenges such as grief, loneliness, isolation, anxiety, low self – esteem, denial, withdraw, sexual unfulfillment and depressed moody, kwa tafasiri yangu wanapata changamoto za kiakili, kihisia, kumezwa na huzuni, upweke, kutengwa, kujitenga, wasiwasi, kutokujithamini, kujikataa, kukosa ngono, na hisia zenye msongo  kwa msingi huu kama matabibu wa kisaikolojia wanaweza kufanya utafiti huu na kugundua changamoto wanazozipitia wajane ukweli ni kuwa viongozi wa kiroho hususani watumishi wa Mungu wachungaji wanapaswa kujua pamoja na kanisa kuwa ujane sio tatizo dogo, na ndio maana nyakati za kanisa la kwanza lakini pia Mungu menyewe tumeona akijihusisha kutatua changamoto za wajane, dunia inakisiwa kuwa na wajane wapatao milioni 245 na kati ya hao wanaoishi kwenye umasikini wa kutupwa ni milioni 115 wengine wakiteseka kimila kama huko Nigeria ambako wengine huvamiwa na ndugu wa mume na wanachukua kila kilicho cha ndugu yao na kuwaacha wajane katika mazingira magumu sana kwahiyo unaweza kupata picha kuwa changamoto hii ni kubwa kwa kiasi gani, kwa hiyo kanisa haliwezi kukaa kimya na kuacha kuwa na huduma au kitengo na namna ya kuwahifadhi wajane sawa tu na mtazamo wa nyakati za kanisa la kwanza ulivyokua, tunaweza tusitimize mahitaji yao yote lakini tunaweza kuwapunguzia changamoto zao ili wasiwe na msiba juu ya msiba, Yesu alipunguza maumivu ya mwanamke mjane katika lango la mji wa Naini ambaye licha ya kuwa alifiwa na mumewe sasa watu wa mji walikuwa wakienda kumzika na mwanae wa pekee, hii ilikuwa huzuni juu ya huzuni ashukuriwe Mungu mwenye kujali, Yesu alimpunguzia mwanamke huyu majonzi  


Luka 7:11-16. “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.”


Sisi kama kanisa sasa tunaweza kufanya nini kwaajili ya kushughulika na changamoto hizi wanazokutana nazo wajane hili sasa linatuleta katika sehemu muhimu ya kutafakari kipengele cha tatu jinsi ya kuwahudumia wajane, na neno linalotumika ni kuwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.

Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli

1Timotheo 5:1-5 “Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.”

Ni muhimu kujiuliza kwanini Paulo mtume anamuagiza Timotheo kuwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli ni nini hasa maana yake? 

Kuwaheshimu – Neno kuwaheshimu kwa kiyunani hapa ni “timaō” ambalo maana yake ni “fix a valuation upon” yaani kuwapa uthamani, uwathamini, wawe wamekidhi vigezo, wawe wamefuzu, uwatambue “Give them a proper recognition” uwape heshima inayostahili, kwa hiyo Paulo mtume alikuwa anamuagiza Timotheo kama mwangalizi wa makanisa kule Efeso kuweka orodha yenye vigezo rasmi vya wajane wanaostahili kutambuliwa na kusaidiwa na kanisa wajane hao walijihusisha na huduma ya kanisa moja kwa moja baada ya kufiwa na waume zao, walijihusisha na maombi kanisani, wajane hao walikuwa ni wale ambao Paulo anawaita wajane kweli kweli yaani ni wajane wasio na mtu wa kuwasaidia, na wajane hao walipitia katika mchujo wenye vigezo kadhaa, na wamefuzu mtihani wa maisha ya uaminifu


Wajane kweli kweli - walikuwa ni wale wasiokuwa na watoto wala wajukuu wala ndugu wa kuwasaidia kabisa 

1Timotheo 5:3-4 “Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.”


Walikuwa ni wajane ambao wanamtegemea Mungu na wanaishi maisha ya maombi kazi yao ni kuomba kwaajili ya kanisa, wanamuombea mchungaji, na huduma zote za kikanisa  na hudumu katika huduma hiyo.

 

1Timotheo 5:5 “Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini Lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.”


Luka 2:36-38 “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.


Walikuwa ni wajane ambao waliishi maisha matakatifu na kujiepusha na lawama hawakuruhusu miili yao iwake tamaa na hawakuwa na mpango wa kuolewa tena bali waliishi maisha ya utauwa, tumaini lao ni Yesu. 


1Timotheo 5:5-7 “Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku. Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai.Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama.


Walikuwa ni wajane ambao sio wasichana sio wale wanaotamani kuolewa tena bali ni wajane ambao umri wao ni mkubwa na hawahitaji mume tena kwa hiyo Paulo alishauri ikiwezekana wawe na miaka sitini kwenda juu  na wale wanaojisikia kuolewa tena alisema waolewe wawe na nyumba zao.


1Timotheo 5:9-14 “Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja; naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema. Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa. Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.”


Kutumia vibaya mazingira magumu ya wajane – Kuwaheshimu wajane pia kulikuwa na maana ya kutoyatumia vibaya mazingira yao ya uhitaji kwa faida, Yesu Kristo aliwahi kuwalaumu Mafarisayo ambao kwa sababu za kidini waliyatumia mazingira yao ya kidini kuwatembelea wajane na kuonyesha kama wanawahurumia lakini wakiwa na nia ovu, au nia ya kutumia mazingira ya kidini kufunika uovu uliokuwa katika mioyo yao, na katika namna ya wazi walikuwa wakisali sala ndeefu sana ili kujiziba kwa jamii ya kuwa wanawajali wajane lakini kumbe walikuwa wanataka kuyatumia mazingira yao magumu kwa nia ovu, kwa hiyo katazo la Kristo ni kuwa mafarisayo walikuwa wanaonekana kama wanajali na kuheshimu sana wajane lakini ukweli ni kuwa walikuwa wanatumia mazingira magumu waliyo nayo wajane kwa faida zao, aidha kwaajili ya kupikiwa na kuhudumiwa ili wale, au kwaajili ya kupata tiba za kihisia kutoka kwa wajane hao, na mengine hatuyasemi kwa sababu Yesu mwenyewe hakuyasema, kwa hiyo utembeleo wao kwa nje ungeonekana kuwa ni wa kidini lakini kwa ndani walikuwa wanatengeneza mazigira ya kuleta faraja zisizokuwa za kiungu, kwa msingi huo watu wa Mungu hatupaswi kuwatumia wajane kwa misingi ya kufaidika kwetu kutoka kwao bali kwaajili ya utukufu wa Mungu, ukimtembelea Mjane huku ukiwa una nia nyingine mume wao ambaye ni Mungu anakuona!


Mathayo 23:14 “[Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.]

 

Hitimisho:


Neno la Mungu limeonyesha mkazo mkubwa sana na wa muhimu kuhusu kuwahudumia wajane na kuainisha kundi la wajane wanaopaswa kuhudumiwa lakini vile vile limetoa vigezo kwa wajane wanaojulikana katikia maandiko kama wajane walio wajane kweli kweli, Maandiko yanaelezea kuwa wao ni wa Muhimu na kwamba wanahitaji kupendwa, kujaliwa, kusaidiwa, kutiwa moyo na kulindwa, kwa kuwa kanisa tumepewa wajibu na agizo la Mungu ni pana uko umuhmu wa kutokulisahau jambo hili na hivyo Roho wa Mungu anataka tulikumbuke hili ili tuweze kujipatia Baraka zinazokusudiwa, kwa kuwajali na kushughulika nao tunajiweka katika nafasi ya Kristo inayoonyesha kuwa kanisa linajali, kwa hiyo pamoja na maagizo mengine hatupaswi kujisahau kama kanisa na kufumbia macho swala ambalo Mungu amelipa kipaumbele, Mungu mwenyewe amejionyesha kujishughulisha na wajane katika namna ya kipekee, Mungu aliwahudumia wajane kadhaa kwa miujiza mikubwa ili kutimiza mahitaji yao, wajane wakikuombea mtumishi wa Mungu, ujue ya kuwa Mungu anaheshimu sana maombi yao na kuwasikiliza sana, kila mtumishi wa Mungu anahitaji kuwa na waombezi wanaomuombea usiku na mchana unapofikiri kuhusu watu wa kukuombea maana yake unapaswa kuwafikiri wajane. Jicho na sikio la Mungu linawasikiliza sana kama tu endapo watasimama katika zamu yao. Kwa hiyo unaweza kuwa na timu ya maombi na kupa jina Ana binti Fanuel na ukawa na wajane wanaofanya kazi ya kuombea huduma mbalimbali lakini zaidi sana Mchungaji wa kanisa la mahali pamoja bila kusahau maombi ya wengine. 


Eliya alikaa pamoja na mjane wa sarepta, tukio ambalo hata Yesu alilithibitisha 1Wafalme 17:8-24 “Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya. Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la Bwana kinywani mwako ni kweli.”


Elisha alimhudumia mjane aliyekuwa na deni 2Wafalme 4:1-7 “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.”


Na Yesu alimuhudumia mjane aliyekuwa na msiba Luka 7:11-16 “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake.Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.”  

Wewe na mimi tunafanya nini kuhusu wajane wanaotuizungika katika jamii ya kanisa la mahali pamoja Uongezewe neema 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima