Alhamisi, 5 Agosti 2021

Vipawa vya Mungu!


Mstari wa Msingi:- 1Wakorithio 12:4-6 “4.Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. 5. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. 6. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.”



Utangulizi:

Leo tutachukua Muda kuzungumzia kwa kina na upana na urefu, ufahamu kuhusu vipawa vya Mungu, ambapo katika maandiko zinaitwa karama, Nyakati za Kanisa la kwanza vipawa au karama zilifanya kazi katika viwango vya juu sana na hivyo Mitume waliweza kuzungumzia ufahamu kuhusu karama au vipawa akiwemo mtume Paulo alipokuwa akiwandikia kanisa la Korintho ambalo lilikuwa na vipawa au karama vyingi sana ona 1Wakoritho 12:1 “Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu.” Paulo mtume alitaka watu wawe na ujuzi kuhusu vipawa vya Mungu au karama za rohoni, kwa msingi huo sisi nasi tunaishi katika nyakati ambapo karama na vipawa vya Mungu vinatenda kazi sana katika kanisa na hivyo ni muhimu kwetu kujua namna na jinsi vinavyotenda kazi: tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipendele kadhaa vifuatavyo:-


·         Tofauti ya neno vipawa na Karama

·         Makundi makuu matatu ya Karama

·         Karama za Roho Mtakatifu

·         Matumizi sahihi ya vipawa na karama:-


Tofauti ya neno vipawa na Karama.

Kwa kawaida neno vipawa na karama yote yana maana moja na yote hutolewa na Mungu, lakini neno kipoawa hutumika zaidi kwa uwezo wa asili na Karama hutumika zaidi kwa uwezo unaotokana na neema ya Mungu, kwa msingi huo katika kanisa na katika neno la Mungu, neema ya utendaji inayotokana na Mungu inaitwa karama neno hili limetokana na tafasiri ya neno la kiyunani CHARISMATA (KARAMA) NA VIPAWA vimetokana na neno la Kiingereza TALENT  sasa karama na vipawa hutofautiana katika namna ifuatayo

1.       Kipawa ni kipaji kinachiowekwa na Mungu ndani ya mtu Tangu siku ya kuzaliwa

Karama ni kipaji kinachowekwa na Mungu mara baada ya mtu kumuamini Yesu

2.       Kipawa kinaweza kurithiwa kutoka katika ukoo au wazazi

Karama inatolewa kwa neema ya Mungu kama apendavyo Mungu mwenyewe

3.       Kipawa kinapokelewa kwa kuzaliwa na kinakuja kwa asili

Karama inakuja kwa neema ya Mungu

4.       Vipawa vinaweza kutolewa kwa watu wote, waamini na wasioamini

Karama zinatolewa kwa mtu aliyemuamini Yesu tu

5.       Kipawa kinaweza kumpatia mtu faida kubwa sana, umarufu, fedha na kadhalika

Karama ziko kwaajili ya kumpa Mungu utukufu na kulijenga kanisa

6.       Kipawa kinaweza kuchochewa kwa mazoezi, kusomea na kujituma zaidi

Karama zinachochewa na hali ya mkao wa kiroho, maombi, kusoma neno la Mungu,ibada ushirika na kukua kiroho na mzigo wa kuwahudumia wengine

7.       Vipawa ni uweza wa Mungu ndani ya wanadamu bila kujali wanaamini nini au kama wanamuamini Yesu au la Mungu humpa yeyote tu kama apendavyo inaweza ikapitia katika vizalia Genetics vya kifamilia na kadhalika:- Mfano

 

a.       Yabali- Mwanzilishi wa kukaa katika Mahema na kufuga Mwanzo 4:20 Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.

b.      Yubali – Mwanzilishi wa kupiga vinubi na vinanda na filimbi Mwanzo 4: 21 Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.

c.       Tubal –Kaini Mfua vyuma na vyombo vya kukatia na shaba, Mwanzo 4:22 . Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.        

 

Karama zinapatikana kwa kuomba na vilevile kama Mungu mwenyewe atakavyo kwa kadiri ya wingi wa neema yake .

 

Kwa msingi huo tunapozungumzia vipawa vya Mungu, maana yake tunazungumzia Karama za Mungu, ni vipawa ambavyo asili yake sio uwezo wa kibinadamu bali asili yake ni Neema ya Mungu kwa makusudi ya kuujenga mwili wa Yesu Kristo yaani Kanisa lake ona

Warumi 12:6-8 “Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.”

Karama hizi zote hutolewa kwa kusudi la kuujenga mwili wa Kristo, au kwa kufaidiana  kwa maana nyingine ni kuwa Mungu hutoa vipawa na Karama kwa makusudi ya kusaidia wengine na si kwaajili yetu Binafsi 1Corithians 12:7 Biblia inasema “Lakini kila mmoja hupewa….Kwa kufaidiana

Makundi Makuu matatu ya Karama:

Tunapozungumzia sasa kuhusu Karama katika maandiko kuna Makundi makuu matatu ya karamaambazo hizi zinatoka kwa Mungu katika utatu wake yaani Mungu Baba, Mungu mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kwa hiyo kuna Karama mbalimbali katika kanisa kama zilivyoainishwa katika maandiko ona 1Wakoritho 12: 4-6 “4. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. 5. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. 6. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.” Unaona unapochunguza maandiko hayo utaweza kuona kuwa kuna tofauti za karama kwa maneno mengine kuna karama mbalimbali, kuna zinazotoka kwa Mungu Roho Mtakatifu, Kuna zinazotoka kwa Bwana yaani Yesu Mungungu mwana na kuna zinazotoka kwa Mungu yaani Mungu baba hivyo ni wazi kuwa kuna makundi makuu matatu ya karama

1.       Karama kutoka kwa Mungu Baba hizi zinaitwa karama za Masaidiano ambazo pia huitwa tofauti za kutenda kazi kwa kiyunani ni “DIAKONAI” GIFTS hizi ni karama za utendaji wa kazi mbali mbali katika kanisa zinaweza kuwa kwa waamini mbalimbali katama hizi zimetajwa katika Warumi 12:6-8 “6. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; 7. ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; 8. mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.”             

 

2.       Karama kutoka kwa Mungu mwana hizi zinaitwa Karama za huduma au tofauti za huduma hizi zinahusika pia na maongozi ya kanisa Administration Gifts kwa kiyunani zinaitwa ENERGEMATA” GIFTS hizi ni karama za maongozi na ujenzi wa kanisa zinatajwa katika Waefeso 4:11-1211. Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; 12. kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;”

 

3.       Karama kutoka kwa Mungu Roho Mtakatifu, hizi ndio maarufu sana duniani kama karama za roho ambazo zenyewe huusika na kuhudumia watu, karama hizi hutoa msaada mkubwa katika maisha ya kanisa nan je ya kanisa hizi huitwa kwa kiyunani CHARISMATA zinatajwa hivyo katika 1Wakoritho 12:8-11 “Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;

 

 

Karama za Roho Mtakatifu:

 

Karama za Roho zinagawanyika katika makundi makuu matatu na ziko tisa

a.       Karama za Uwezo (the gifts of Power)

 

i.                    Karama ya Imani au Neno la Mamlaka – faith or word of Authority

ii.                  Karama za Uponyaji – Healings Gifts

iii.                Karama za Matendo ya Miujiza – “the work of Miracles”

 

b.      Karama za Ufahamu (Revelations  Gifts)

 

i.                     Karama ya Neno la Hekima – The word (Message) of wisdom

ii.                  Karama ya neno la Maarifa – The word (Message) of Knowledge

iii.                Karama ya kupambanua Roho – Discerning of the spirits

 

c.       Karama za Usemi (Saying Gifts)

 

i.                    Karama ya Unabii – Prophecy

ii.                  Karama ya aina za Lugha- Diferrents Tongue

iii.                Karama ya tafasiri za Lugha – Interpreting of Language

Uchambuzi wa Makundi makuu matatu ya Karama za Roho Mtakatizu:-

Karama za Uweza

i.                    Karama ya Imani au Neno la mamlaka hii ni karama ya Roho Mtakatifu kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uwezo wa kunena maneno yenye Mamlaka na maneno hayo yakatimizwa au kusababisha muujiza

a.       Mfano Musa alisema Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya

b.      Elisha 2Wafalme 4:16-17 “Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo. Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia

c.       Eliya 1Wafalme 17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.”

d.      Nabii Yoshua Katika Yoshua 10:12-13 “Ndipo Yoshua akanena na Bwana katika siku hiyo ambayo Bwana aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao

e.      Petro katika Mlango Mzuri Matendo 3:1-10 “Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu

f.        Yesu alipousemea Mtini Marko 11:12-14 “Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Kisha Marko 11:20-22 “Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu.

ii.                  Karama za Uponyaji: Ni karama za Roho Mtakatifu kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uwezo wa kumuombea mtu mwenye ugonjwa au homa na kumuwezesha mtu huyo kupona kwa neema ya Mungu.

a.       Mfano Yesu aliponya wengi Mathayo 4:23-24 “Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya.”

b.      Wanafunzi wa Yesu wote Mathayo 10:1 “Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.”

c.       Petro alimponya ainea Matendo 9:33-34 “Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka.”       

iii.                Karama za Matendo ya Miujiza – Ni karama kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kwa uweza wa Roho Mtakatifu kuwa na Neema na uweza wa Mungu kumuombea mtu au mfu na kusababisha muujiza wa kupita kawaida kutokea mfano

a.       Paulo Mtume alitumiwa mno katika karama za matendo ya Miujiza Matendo ya Mitume 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”

b.      Yesu Kristo mwenyewe kwa Kulisha watu wengi kwa mikate michache Luka 9:13-17 “Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula. Kwa kuwa wanaume waliokuwako walipata kama elfu tano. Akawaambia wanafunzi wake, Waketisheni watu kwa safu, kila safu watu hamsini. Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano. Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili

c.       Yesu Kumfufua Mfu Luka 7:11-15 “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa.Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake

Karama za Ufahamu. (Revelations  Gifts)

Hili ni kundi la Karama za Roho kwa Mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa neema ya ufahamu wa ndani na wa kina kuhusu mambo, au maswala ya mtu kwa kusudi la kuleta suluhu inayokusudiwa, Karama hizi zaweza kuwa za kudumu, lakini pia zaweza kumjia mtu wakati wa kutatua tatizo

i.        Karama ya neno la Hekima 1Wakoritho 12:8Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; – Nikarama kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uwezo wa kutatua matatizo yanayojitokeza kwa mtu au katika jamii kwa kusudi la kuleta suluhu, Ni karama ya neema kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kumuwezesha mtu huyo wa kwenda nyuma ya tatizo au mbele ya tatizo na kunga’mua na kuweza kuleta suluhu au kuondoa utata

 

Karama hii inasaidia kushughulikia maswala kadhaa yafuatayo:-

·         Kufunua Makusudi ya Mungu – Purposes

·         Kufunua Mpango wa Mungu - Plan

·         Kufunua Mapenzi ya Mungu - will

·         Kufunua Mashauri ya Mungu - council

a.        Uwezo wa Kufasiri Ndoto Mwanzo 41:1-36Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto. Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema.  Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo.               

Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo. Farao aliwakasirikia watumwa wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari, mimi na mkuu wa waokaji. Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota.Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake. Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nalirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa. Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.     

Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto; na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini.Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu. Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono. Na walipokwisha kuwala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka. Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa. Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake.Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja.

Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba.Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.kwaYusuphu, Kupitia ndoto ya Farao Yusufu aliweza kutatua tatizo ambalo lingeikumba dunia ya wakati ule kwa njaa.”

b.      Uwezo wa kujua uovu uliofichika 2Wafalme 5:20-27 “Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama Bwana aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake. Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani? Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili. Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamshurutisha, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakayachukua mbele yake. Naye alipofika kilimani, alivitwaa mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao. Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi? Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.” Eliya aliweza kuona nuovu uliokuwa ukifanya na Mtumishi wake Gehazi

c.       Uwezo wa kujua Mapenzi na Mpango wa Mungu kuhusu Mambo yajayo Daniel 2:1-47, Daniel alitumiwa na Mungu Kufasiri Ndoto ya Nebuchadneza iliyohusu maswala yajayo.

d.      Uwezo wa kujua tukio lililoko mbele ya upeo wa Macho ya kibinadamu Marko 14:12-15 “Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka? Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini;atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni; na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu?Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni.” Yesu aliweza kuwaambia wanafunzi wake kuhusu mtu atakayewapatia Chumba cha Maandalizi kwaajili ya Pasaka

e.      Uwezo wa kujua mipango ya adui na kuidhibiti mapema kabla ya kupata madhara 2Nyakati 20:12-23 Elisha aliweza kumtahadharisha mfalme wake kuhusu mipango ya adui ya majeshi ya Washami.

ii.                   Karama ya Neno la Maarifa 1Wakoritho 12:8Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;” Karama ya neno la Maarifa Neno “Logos” the spoken word Neno linalosemwa, Maarifa ni “Gnosis” Knowing Kujua au kuvumbua, Hivyo Karama ya neno la Maarifa ni karama inayowekwa na Mungu Roho Mtakatifu kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uweza wa kiungu wa kuweza kujua Mazingira ya matatizo yanayowazunguka watu kwa kusudi la kuleta suluhu, Mfano:-

a.       Yohana 4:16-19Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!”

b.      Matendo 5:1-10 “Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali,akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.”

c.       Mungu alimfunulia Nuhu namna ya kujenga Safina Mwanzo 6:12-13 Na kuonya juu ya hatari itakayokuja kwa dunia

d.      Mungu alimfunulia Abrahamu kuhus Israel kwenda utumwani Misri Mwanzo 15:13-14

e.      Mungu alimfunulia Yusufu kwa Njia ya ndoto kuhusu kuwatawala Ndugu zake Mwanzo 37:5-9

f.        Mungu alimfunulia Yoshua Dhambi iliyofanyika kambini Yoshua 7:10-15

g.       Samuel aliweza kujua Punda waliopotea kuwa wamepatikana 1Samuel 9:20

h.      Nathan aliweza kuijua dhambi ya Daudi 2Samuel 12:1-7

i.        Mikaya aliona kushindwa na kuawa kwa Ahabu vitani 2Nyakati 1-47

j.        Mungu alimuonya Yusufu kuhusu mpango wa Herode dhidi ya Mtoto Yesu Mathayo 2:13

k.       Mungu alimfunulia Simeoni kuwa hatakufa mpaka atakapomuona Masihi Luka 2:26

l.        Mungu alimfunulia Anna kuwa Yesu ni Masihi Luka 2:38

m.    Yesu alizungumza habari za Nathanael  Tangu alipokuwa ameketi chini ya Mtini Yohana 1:45-51

n.      Nabii Agabo aliona njaa itakayoikumba Yerusalem Matendo 11:28

o.      Nabii Agabo aliona Mateso na kifungo cha Paulo Mtume  yatakayompata huko Yerusalem Matendo 21:10-11

p.      Paulo Mtume aliweza kuona hatari iliyoko safarini Matendo 27:10

iii.                  Karama ya kupambanua roho 1Wakoritho 12:10na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;” Ni karama kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kwa neema ya roho Mtakatifu kuwa na uwezo wa kujua ni roho ya aina gani inatenda kazi katik ya Roho wa Mungu, roho ya binadamu nay a shetani

a.       Yesu alijua roho iliyotenda kazi nyuma ya maneno ya Petro Mathayo 16:22-23 “ Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

b.      Yesu alijua roho iliyokuwa ikitenda kazi nyuma ya Yakobo na Yohana Luka 9:54-55 “Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]? Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]”

c.       Petro aliweza kumtambua Simon Mchawi kuwa yu katika uchungu Matendo 8:18-23 ” Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako.  Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu.”

d.      Paulo Mtume alimtambua Elima yule Mchawi na kumdhibiti Matendo 13:6-12” Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.”              

e.      Paulo Mtume alimtambua Pepo aliyekuwa ndani ya kijakazi kule Efeso Matendo 16:16-18 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.”

f.        Karama ya kupambanua Roho inatusaidia kujua ni roho gani inatenda kazi, sio kila roho inayotoa unabii au kufanya ishara na miujiza au hata kuzungumza unabii wa kweli inatokana na Mungu, maandiko yanatutaka tuzipime 1Yohana 4:1Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.

Kwa nini kuna umuhimu wa kuzipima roho kwa sababu ziko roho za uongo, yako mafundisho ya uongo, wako manabii wa uongo na kama kanisa tunapaswa kujua namna roho hizo zinavyotenda kazi na kuzipambanua ili kuweza kupata uhakiki wa mapenzi ya Mungu katika maisha yetu

 1Wafalme 22:19-24 “Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto. Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.  Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo. Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako

Ni muhimu kupima roho kwani siku za mwisho maandiko yanatuonya kuwa yako mafundisho ya mashetani, na fundisho pia au maneno katika maandiko huitwa roho Yohana 6:63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.” Unaweza kuona kumbe kama maneno ni roho hatuna budi kuwa na karama ya kupambanua roho ili kujua ni roho gani inatenda kazi kati ya roho ya kibinadamu, ya shetani na ya Mungu, Mungu haoni shani kuulizwa, mwanatheolojia aliyekamilika haoni shaka kuuliza sauti anayoisikia kama ni ya Mungu au ya mwanadamu tunahitaji karama ya kupambanua roho hususani katika nyakati hizi za mwisho

Paulo mtume alipotokewa na maono alihoji ni nani wewe Bwana ninayekuudhi na Yesu alijibu kuwa ni Mimi Yesu unayeniudhi, kumbuka alisikia sauti na mwanga mkali ulimulika na Mungu akasema naye Paulo alitaka kujua ni roho gani inasema naye ni maono gani anayaona yanatoka kwa Bwana yupi Matendo ya Mitume 9:1-5Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.  Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.”

Kwa msingi huo Kanisa ililiweze kujilinda na mafundisho ya mashetani na roho zidanganyazo hatuna budi kuhakikisha kuwa tunamuomba Mungu atupe kupambanua roho, katika kazi ya nabii karama ya kupambanua roho ni ya muhimu sana.         

Karama za Usemi:-

Karama za Usemi ni karama kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na neema ya Mungu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kutoa ujumbe wa kinabii, kuzungumza lugha asiyoifahamu na kutafasiri Lugha asiyoifahamu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu bila kutumia akili ya kibinadamu. Karama hizi zinatajwa katika 1Wakoritho 12:10. “na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;”

Karama hizi zinawekwa katika fungu moja kwa sababu zinahusisha kinywa

i.                    Karama ya Unabii – Prophecy

ii.                 Karama ya aina za Lugha- Diferrents Tongue

iii.               Karama ya tafasiri za Lugha – Interpreting of Language

 

Karama ya Unabii – Prophecy 1Wakoritho 12:10

Krama ya unabii ni karama kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uwezo wa kutangaza au kuzungumza mapenzi ya Mungu, au kutafasiri makusudi ya Mungu, na kuyafanya yajulikane kwa wahusika kwa kusudi la kuwajenga watu au kuwatia moyo, Karama hii haimfanyo mtu awe nabii, inngawa nabii anapaswa kuwa na karama hii, Karama hii pia sio lazima izungumzie maswala yajayo ingawa kuzungumzia mambo yajayo ni sehemu ya karama hii, kwa ufupi karama hii inahusu kuwajenga watu kuwatia moyo na kuwaelekeza katika mapenzi ya Mungu hususani katika wakati uliopo

Unabii kamwe haupaswi kutolewa kwa Mapenzi ya kibinadamu, bali unatoka kwa Mungu kwa kadiri ya neema ya Roho Mtakatifu anavojalia na kusukuma hilo kutendeka, 2Petro1:21 “Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” Ujumbe wa kinabii wakati wote utajihusisha na kujenga, kufariji, kutia moyo na kuelekeza mapenzi ya Mungu kwa watu wake na kanisa 1Wakoritho 14:3 “Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo.” Mifano ya karama za unabii

a.       Matendo 13:1-3Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao” Tunawezaje kujua hapa kuwa Roho Mtakatifu alisema? Ni wazi kuwa kanisa lilikuwa na manabii kama inavyoelezwa katika Mstari wa Kwanza na hivyo kupitia karama ya unabii Roho Mtakatifu alikuwa ameweka wazi Mapenzi yake kwa kanisa la Antiokia

b.      Mtumishi wa Mungu kama Timotheo alitambuaje kuwa amitwa katika utumishi ilikuwa ni kupitia unabii 1Timotheo 4:13-14Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha. Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee.”         

c.       Kusudi kuu la Karama ya unabii ni kujenga watu na sio kuwaumbua au kuwadhalilisha 1Wakoritho 14:4Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.”

Karama ya aina za Lugha – Ni karama ya neema ya Mungu kwa Mtu aliyeokoka inayowekwa na Roho Mtakatifu kumuwezesha mtu huyo kunena kwa lugha za wanadamu au malaika bila ya kutumia akili

a.       Mfano ni Katika Matendo 2:1-12Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?”

b.      Biblia inathibitisha kuwepo kwa Lugha za wanadamu na malaika 1wakoritho 13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.” Hata hivyo matukio ya kuzungumza lugha za wanadamu kwa uweza wa Roho Mtakatifu yameendelea kuwa nadra katika miaka ya kizazi chetu.

Karama ya tafasiri za Lugha – Ni karama ya neema inayowekwa na Mungu Roho Mtakatifu kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uwezo wa kuzungumza au kutafasiri lugha za wanadamu au malaika asizozijua au kujifunza bila kutumia akili

a.       Mfano ni Nabii Daniel aliweza kutafasiri Lugha ngeni iliyosumbua wengi Daniel 5:1-30Belshaza, mfalme, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya elfu hao. Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadreza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wapate kuvinywea.Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe.  Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana. Mfalme akalia kwa sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika ufalme.            

Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake. Ndipo mfalme Belshaza akahangaika sana, uso wake ukambadilika, na wakuu wake wakaona fadhaa. Basi malkia, kwa sababu ya maneno ya mfalme na ya wakuu wake, akaingia katika nyumba ya karamu; malkia akanena, akasema, Ee mfalme, uishi milele; fikira zako zisikufadhaishe; wala uso wako usibadilike. Yuko mtu katika ufalme wako, ambaye roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yake; na katika siku za baba yako nuru na ufahamu na hekima zilionekana ndani yake; na mfalme Nebukadreza, baba yako, naam, mfalme, baba yako, akamfanya kuwa mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na kufungua mafundo, zilionekana katika Danieli huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danieli, naye ataionyesha tafsiri. Ndipo Danieli akaletwa mbele ya mfalme. Na Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Je! Wewe ndiwe Danieli yule, aliye mmoja wa wana wa Yuda waliohamishwa, ambao mfalme, baba yangu, aliwaleta huku toka Yerusalemu? Nimesikia habari zako, kwamba roho ya miungu imo ndani yako, na kwamba nuru na ufahamu na akili bora zimeonekana kwako. Basi sasa, watu wenye hekima na wachawi wameletwa mbele yangu, wapate kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake; lakini hawakuweza kunijulisha tafsiri ya jambo hili.              

Lakini nimesikia habari zako, kwamba waweza kuleta tafsiri, na kufumbua mafumbo; haya! Kama ukiweza kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake, utavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utakuwa mtu wa tatu katika ufalme. Ndipo Danieli akajibu, akasema mbele ya mfalme; Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake.     

Kwa habari zako, Ee mfalme, Mungu Aliye juu alimpa Nebukadreza, baba yako, ufalme, na ukuu, na fahari, na utukufu; na kwa sababu ya ule ukuu aliompa, watu wa kabila zote, na mataifa, na lugha, wakatetemeka na kuogopa mbele yake; aliyetaka kumwua alimwua; na aliyetaka kumwacha hai, alimwacha hai; aliyetaka kumtukuza, alimtukuza; na aliyetaka kumshusha, alimshusha.Lakini moyo wake ulipoinuliwa, na roho yake ilipokuwa ngumu akatenda kwa kiburi, aliuzuliwa katika kiti chake cha enzi, nao wakamwondolea utukufu wake. Akafukuzwa mbali na wanadamu, moyo wake ukafanywa kuwa kama moyo wa mnyama, na makao yake yalikuwa pamoja na punda-mwitu; akalishwa majani kama ng'ombe, mwili wake ukalowa maji kwa umande wa mbinguni; hata alipojua ya kuwa Mungu Aliye juu ndiye anayetawala katika ufalme wa wanadamu, na ya kuwa humweka juu yake yeye amtakaye, awaye yote. Na wewe, mwanawe, Ee Belshaza, hukujinyenyekeza moyo wako, ijapokuwa ulijua hayo yote.     

Bali umejiinua juu ya Bwana wa mbingu; nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako; na wewe, na wakuu wako, na wake zako, na masuria wako, mmevinywea; nawe umeisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe; wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lo lote; na Mungu yule, ambaye pumzi yako i mkononi mwake, na njia zako zote ni zake, hukumtukuza. Ndipo kile kitanga cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake, na maandiko haya yameandikwa. Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI. Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi. Ndipo Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danieli mavazi ya rangi ya zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme. Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa.”

Matumizi sahihi ya vipawa na karama:-

Karama hazinunuliwi – wala haziuziwiMathayo 10:8 “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.” Matendo 8:18-20 “18. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, 19. Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. 20. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.”               

Karama hazipaswi kutumiwa kwa kudhalilisha watu wa Mungu – Karama za Mungu ni neema ya Mungu juu ya mwamini, hatupaswi kuzitumia Karama kwa kuzalilisha watu, mfano sio vema kumkanyaga mtu unapomuombea huko ni kukosa nidhamu biblia imeelekeza sehemu za kuombea Marko 16:17-18 “17. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; 18. watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Karama hazipaswi kutumika kwa chuki na kuligawa kanisa – Karama zinapaswa kutumika kwa upendo na sio kwaajili ya majivuno au kuligawa kanisa ukuaji wa kiroho wa mtu haupimwi kwa namna anavyotumiwa na Mungu unapimwa kwa upendo 1Wakoritho 12: 1-3. “1Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.  2. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. 3. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.

Karama hazipaswi kutumika kwa kiburi na majivuno – Lucifer alikuwa ni malaika mwenye kipaji kikubwa sana lakini alikataliwa na kutupwa kutoka mbinguni kwa sababu ya kiburi, Kanisa la nyakati za leo limepitia changamoto nyingi kwa sababu watu hawataki kuonywa na kuelekezwa kuwa na karama hakumaanishi kuwa hatupaswi kupokea ushauri  na maonyo kutoka kwa wengine au kujivuna kama ilivyokuwa kwa shetani tukiwa na kiburi Mungu ataruhusu aibu kubwa sana Ezekiel 28:14 -19 “14. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. 15. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. 16. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. 17. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. 18. Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao. 19. Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.               

Kadiri tunavyokuwa na vipawa vikubwa sana ndivyo tunavyotakiwa kuwa wanyenyekevu kwa kiwango kikubwa ili Mungu atukuzwe na kukututumia zaidi Wafilipi 2:3-9 Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima