Kutoka 15:25-26 “Naye akamlilia BWANA;
BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi
akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko; akawaambia, Kwamba utaisikiza
kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na
kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu
yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa uponyaji wa
kimungu ni mojawapo ya sehemu muhimu sana ya Injili, Haiwezekani kwa namna
yoyote ile ukamuhubiri Yesu Kristo ukaacha huduma ya uponyaji, Huduma ya
uponyaji tangu zamani ilikuwa ni sehemu muhimu sana ya kazi ya uungu, Maandiko
yamejaa ahadi nyingi sana za Mungu kuhusu uponyaji, kile kifurushi cha wokovu
wa mwanadamu na ukombozi wa mwanadamu kinakwenda sambamba na uponyaji wa mwili
nafsi na roho, na kwa sababu hiyo uponyaji ni haki ya kila mwanadamu
anayehitaji msaada kutoka kwa Mungu kwaajili ya changamoto anayokutana nayo:-
Zaburi 103:2-5 “Ee nafsi yangu, umhimidi
Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya
magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na
rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;”
Mathayo 4:23-24 “Naye alikuwa akizunguka
katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari
Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na
habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi,
walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na
wenye kupooza; akawaponya.”
Kama huduma ya uponyaji ingekuwa
haina maana na si ya Muhimu kwa vyovyote vile mwana wa Adamu Yesu Kristo
asingejishughulisha na kazi ya kuhubiri habari njema na kufungua watu, Moja ya
sababu kubwa ya Mungu kuwapaka mafuta watumishi wake ni ili pia wawasaidie watu
kutoka katika udhaifu vifungo na magonjwa ya aina zote, kwa sababu hiyo watu
wote ni lazima wakumbuke kuwa Mungu anaponya, na yeye yuko tayari kufanya hivyo
na anawapaka mafuta watumishi wake ili pamoja na mambo mengine wafanye kazi ya
kuwafungua watu kutoka katika changamoto zao.
Luka 4:17-19 “Akapewa chuo cha nabii Isaya,
akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu,
Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti,
jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko
na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana
Mungu alikuwa pamoja naye”
Leo tutachukua muda kwa msingi
huo kujikumbusha tena msingi wa uponyaji wa kiungu na umuhimu wa huduma za
uponyaji na jinsi ya kuhakikishakuwa uponyaji inakuwa ni sehemu ya huduma ya
maisha yetu ya kila siku, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
·
Umuhimu
wa huduma ya uponyaji.
·
Vizuizi
vya nguvu za uponyaji.
·
Mimi
ndimi Bwana nikuponyaye.
Umuhimu wa Huduma ya Uponyaji:
Wokovu wa mwanadamu na ukombozi
wake unahusisha mwili nafsi na roho, na Mungu yuko tayari kuwasaidia wanadamu
wote katika changamoto zao ikiwa ni pamoja na kuwaponya magonjwa yao, Mungu
anataka tuwe na mafanikio yote ya kimwili na kiroho, na ndio maana unaweza
kuona kuwa katika huduma ya Kimasihi ya Yesu Kristo hakupuuzia uponyaji, Yesu
aliwaponya wagonjwa wote wenye changamoto za kila aina.
Mathayo 8:14-17 “Hata Yesu alipofika
nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani
hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata
kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake,
akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii
Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.”
Kristo Yesu alilipa kanisa au
wanafunzi wake mamlaka hii ya kuhubiri injili, kufundisha lakini alijumuisha
pia huduma ya kutoa pepo na kuponya magonjwa yote, maandiko yanaonyesha kuwa
mojawapo ya ishara ya kuwa tunamuamini Yesu, ni pamoja na kuombea wagonjwa na
kuwa nao watapata afya, kwa hiyo ikiwa tunamfuata Yesu ambaye ametupa
kielelezo, kwa sababu zozote zile hatuwezi kupuuzia moja kwa moja huduma za
uponyaji.
Mathayo 10:1, 7-8 “Akawaita wanafunzi wake
kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa
yote na udhaifu wa kila aina., 7-8. Na katika kuenenda kwenu, hubirini,
mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni
wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.”
Marko 6:7,13 “Akawaita wale Thenashara,
akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; 13 Wakatoa
pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.”
Luka 10:9 “waponyeni wagonjwa waliomo,
waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.” Marko 16:17-18 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina
langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa
kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa,
nao watapata afya.”
Kwa nini Yesu aliweka agizo la
kuhubiri injili pamoja na kazi ya uponyaji kwa kanisa na kuagiza wanafunzi na
kanisa kuifanya kazi hii ikiwa ni pamoja na kuihubiri injili? Hii ni kwa sababu
Yesu anajua kuwa magonjwa na madhaifu yanawasumbua wanadamu na kuwa magonjwa na
udhaifu wa kila aina ni kazi ya shetani, Magonjwa ni moja ya silaha ya ibilisi
kuwanyima wanadamu furaha na kuwatesa na kuwaonea, maandiko yanathibitisha kuwa
kila aina ya magonjwa na uonevu wowote wa kiafya ni kazi ya shetani. Na Yesu
alidhihirishwa ili azivunje kazi za ibilisi.
Luka 13:11-16 “ Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa
udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha
kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu
wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.
Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato,
akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni
mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akajibu
akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda
wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye
wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii,
haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?”
Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta
kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema
na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye”
1Yohana 3:8 “atendaye dhambi ni wa Ibilisi;
kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu
alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”
Kanisa linapaswa kuwa mstari wa
mbele katika kukemea na kukataa uonevu sio tu katika jamii lakini vile vile
katika miili ya wanadamu wanaoonewa na ibilisi, tangu nyakati za agano la kale
Mungu alikuwa akijihusisha na uponyaji wa watu wake, na katika nyakati za agano
jipya huduma za uponyaji ni muhimu sana, na zinaendelea, wote tunajua ya kuwa
Yesu Kristo ni yeye yule jana leo na hata milele na hivyo huduma hii
inaendelea, kazi ya ukombozi wa mwanadamu pale msalabani ilihusisha sio dhambi
zetu tu bali na magonjwa ambapo Yesu aliposulubiwa pia alikuwa akihusika na
kuharibu nguvu za magonjwa, alidhihirishwa ili azivinje kazi za ibilisi.
Isaya 53:4-5 “Hakika ameyachukua masikitiko
yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na
Mungu, na kuteswa.Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu
yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Mathayo 8:16-17 “Hata kulipokuwa jioni,
wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote
waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,
Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.”
Kwa hiyo neno la Mungu
linaonyesha wazi kuwa uponyaji ni sehemu ya mapenzi kamili ya Mungu, Mungu
aliponya katika wakati wa agano la kale na aliahidi kuwaponya watu wake,
akijiweka wazi kuwa yeye ni Bwana aponyaye, Yesu ni udhihirisho wa Mungu ulio
wazi, alipokuwa duniani alikuwa akifunua tabia ya uungu, na kutuonyesha mapenzi
ya Mungu baba, na hivyo yeye mwenyewe aliponya, na sio hivyo tu aliagiza
wanafunzi wake kuponya, na sio hivyo tu alitoa na vipawa na karama za uponyaji
na matendo ya miujiza kwa kanisa hii maana yake ni nini? Mbingu zinaona kuwa
uponyaji ni swala la Muhimu, kanisa likipuuzia huduma hii maana yake litakuwa
limempa nafasi na kibali shetani kuendelea kuwaonea watu, Agizo la Kristo
linatufundisha kuwa ni mapenzi ya Mungu kwa kila mtu kuponywa, Mfano wa Yesu
Kristo unatukumbusha kuwa huduma ya uponyaji ni sehemu muhimu ya injili, na
kuteseka kwake msalabani kunaonyesha umuhimu wa uponyaji wa mwanadamu, katika
nafsi, mwili na roho, kwa kupigwa kwake! Sisi tumeponywa ! kwa msingi huo kila mtumishi
wa Mungu anapaswa kujikumbusha kuwa huduma ya uponyaji ni sehemu ya kazi
tuliyopewa au kuitiwa na Mungu, ni sehemu ya agizo kuu, na ni wazi kuwa
tunamuamini Mungu aponyaye na ambaye yuko tayari kuwaponya watu wake hata sasa!
Katika mahitaji yao yote, kimwili,
kiroho, nafsi na uchumi.
Vizuizi vya nguvu za uponyaji
Ni muhimu kufahamu na kukumbuka
kuwa ni mapenzi ya Mungu kuwaponya watu wake, na kuwa Mungu yuko tayari
kuponya, lakini huduma hii ya uponyaji ina vizuizi kadhaa ambavyo ni muhimu kushughulika
navyo ili kanisa liweze kuwa makini na kujiepusha navyo, aidha shetani pia
anaweza kupingana na huduma za aina hii kwa sababu hataki watu wafunguliwe na
kwa sababu hiyo anaweza kutumia fahamu zetu zilizopotoka kuhakikisha kuwa
hatukumbuki kutoka kipaumbele kwa huduma za uponyaji, hata hivyo ninapokazia
swala zima la umuhimu wa huduma hii, ni muhimu kujikumbusha kuwa agizo la Mungu
ni pana sana na watumishi wa Mungu wanapaswa kutoa MLO KAMILI yaani “balance
diet” tunapoifanya kazi hii ya Mungu, yaani tuwe na kiasi katika
kuwahudumia watu, tuwahudumie kiakili, kimwili na kiroho. Tuwafundishe neno,
tuhudumie miili yao kwa huduma za kiponyaji, na sio vema kuelemea upande mmoja,
kwa hiyo huduma zetu zinahitaji mzani, kufundisha, kuhubiri, kutia moyo,
kushauri, kutembelea na huduma za maombezi na uponyaji. Kwa hiyo mpangilio wako wa ibada katika kanisa
lako ni wa muhimu, unaweza kuitumia siku ya maombi na maombezi kwa kazi za
uponyaji, na unaweza kuitumia siku ya mafundisho kufundisha watu Biblia yaani
neno la Mungu na unaweza kuitumia siku nyingine kwa kuimarisha watu, kumbuka
mitume walifundisha, waliomba, walifanya miujiza na walifundisha watu neno la
Mungu na kuhubiri, huduma yako isielemee upande mmoja kwa sababu vyote
vinahitajika kwa kusudi la kuwajenga watu, usifanye huduma ya maombezi tu
ukaaacha kuwaelekeza watu kwa Yesu, na kuwafunza. Sasa basi vizuizi vya
uponyaji ni vipi?
1.
Kutokuamini
- kumekuwepo na sababu nyingi sana zinaoainishwa kwa nini watu wengine
hawaponywi, lakini mojawapo ya sababu kubwa ni KUTOKUAMINI Kutokuamini pia
kunahusika katika hali ya kutokujibiwa maombi, tatizo la kutokuamini linaweza
kuwa kwa pande mbili anayekuombea na anayeombewa, Ni mapenzi ya Mungu watu kuponywa kwa sababu
hiyo kila anaemwendea Mungu kwaajili ya uponyaji ni lazima awe na Imani aaamini
kuwa Mungu yuko na yuko tayari kuponya na ataponya bila kutia shaka!
Yakobo 1:6-8 “Ila
na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la
bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama
yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana. Mtu wa nia mbili husita-sita
katika njia zake zote.”
Watu wanaotoa
huduma ya maombezi na watu wanaoombewa wanapaswa kuwa na imani ya kuwa ni
mapenzi ya Mungu kamili kwamba watu waponywe, na tunapoomba jambo lolote kwa imani
yaani kuliamini Neno la Mungu na kuwa na uhakikika kuwa uponyaji ni sehemu ya
haki yetu na ni sehemu ya mapenzi ya Mungu na kuwa Mungu anataka kutuponya
ufahamu huo pekee ni Imani tosha kuwa Mungu anaweza kutusaidia na hivyo ataleta
uponyaji wake, lakini tukiwa na shaka, tunajiwekea kizuizi cha kupokea kutoka
kwa Bwana.
Marko 9:23-24 23. “Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote
yawezekana kwake aaminiye. Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema,
Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.”
Mathayo 17:19-20 “Kisha
wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza
kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin,
nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu,
Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana
kwenu.”
2.
Kutokusamehe
– Wakati mwingine ni muhimu kuwafundisha kwanza wale wanaohitaji maombezi
umuhimu wa kusamehe, au umuhimu wa kutubu dhambi zetu, kama iko dhambi haijatubiwa au uko moyo ambao
una uchungu kiroho, uchungu na kutokusamehe kunamuweka mtu gerezani na kunampa
shetani haki ya kuendelea kukutesa na magonjwa yako!
Yohana 5:11-15 “Akawajibu,
Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende.
Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike, uende, ni nani? Lakini yule mtu
aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu
palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya
hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije
likakupata jambo lililo baya zaidi. Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari
Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima.”
Yakobo 5:15-16 “Na
kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa
amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na
kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa
bidii.”
Marko 11:24-25 “Kwa
sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea,
nayo yatakuwa yenu.Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu
ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.”
Watu wengi sana
wanatafuta uponyaji, na uponyaji ni kwaajili ya wanadamu wote, lakini
tunapomjia Mungu kwa uponyaji tunapaswa kuachilia, tunapaswa kuwasamehe
waliotukosea ili Mungu aweze kuturehemu, maombi yetu hayapaswi kuwa na mtu
tuliyemfungia moyoni, hayapaswi kuwa na mtu ambaye tuna kinyongo naye, lazima
tuhakikishwe kuwa tuko huru kabisa kutoka kwenye uchungu na wanadamu wenzetu,
tafadhali sana kusamehe ni kwaajili ya afya zetu, tusiposamehe sisi tunajiumiza
wenyewe. Na kujiacha kwenye gereza la
mateso ona :-
Mathayo 18:21-35 “Kisha
Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami
nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata
saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja
aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja
awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru
auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile
deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami
nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe
ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari
mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka
miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni,
hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka,
walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo
bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile
yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi
nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata
atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda
ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.”
Katika mfano huo
hapo juu unaohusiana na kusamehe, sehemu ya mwisho inaonyesha kuwa yile mtumwa
aliyeshindwa kusamehe, Bwana wake aliamuru kuwa apelekwe kwa watesaji, hata
atakapolipa deni ya mwisho maana yake hata atakapoweza kusamehe, au hata
atakapoweza kuachilia ndipo na yeye anaweza kuachiliwa, katika maswala ya
uponyaji ni wazi kuwa watu wenye uchungu na wanadamu wengine na wasiosamehe
hawawezi kupokea kitu kutoka kwa Mungu isipokuwa mpaka wamesamehe kwanza. Na
hiyo ni kanuni ya Mungu mwenyewe!
3. Kutokutii – Wale wanaofanya huduma za
maombezi watakubaliana nami kuwa Roho Mtakatifu huwa anatoa miongozo mbalimbali
jinsi na namna ya kuwahudumia watu, huduma za maombezi huwa hazina aina moja ya
kanuni, tangu zamani tunaona kuwa Mungu aliponya watu wake kwa jinsi na namna
mbalimbali kwa kupitia jina lake, wakati mwingine ili Mungu amponye mtu
inahitajika utii tu na kukubali kunyenyekea basi.
2Wafalme 5:1-3, 8-14 “1-3 Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu,
alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa
mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa
vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi,
wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye
akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa
pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake. 8-14 “Ikawa,
Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua
mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi
yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli. Basi
Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya
Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani
mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. Lakini Naamani
akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu,
na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake
mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari,
mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani
yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake
wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia
kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe,
uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na
neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama
ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.”
Luka 17:11-14 “Ikawa
walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na
Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye
ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa,
uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa
walipokuwa wakienda walitakasika.”
Yohana 9:6-11 “Alipokwisha
kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu
tope za macho, akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake,
Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona. Basi jirani zake, na wale
waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa
akiketi na kuomba? Wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini
amefanana naye. Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye. Basi wakamwambia, Macho yako
yalifumbuliwaje? Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka
macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata
kuona.”
Katika vifungu
hivyo utaweza kuona kuwa uponyaji unajitokeza kwa sababu ya maagizo,
walioponywa wote waliagizwa kitu cha kufanya, mmoja aliambiwa akajichovye
Jordani mara saba na mwingine alipakwa tope akaagizwa akanawe katika kisima
kiitwacho Siloamu na wakoma waliagizwa wakajionyeshe kwa makuhani, Kwa hiyo
Mungu anachotaka kukiona ni utii tu na kupitia utii wako analeta uponyaji, kwa
hiyo wakati wa huduma ya uponyaji Muhudumu sikiliza maelekezo ya Roho Mtakatifu
na muhudumiwa fuata maelekezo unayopewa na anayekuhudumia kwa utii wako
unapokea uponyaji. Maana yake ni nini kutokutii au kufuata maelekezo wakati
mwingine kunaweza kutunyima uponyaji. Kumbuka neno lile
…..Kwamba
utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea
mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi
sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA
nikuponyaye
4. Ndoa yenye mafarakano - wako wanandoa
ambao ugomvi kwao ni swala la kawaida sana wanagombana mno, Mafarakano ni moja
ya silaha muhimu sana anayoitumia shetani kuharibu ndoa, taasisi na kanisa,
shetani anapotaka kupigana na huduma iliyoko ndani yako anaanzia kwenye ndoa,
anatingisha kwenye ndoa lakini sio hivyo tu akitaka kukunyima miujiza, na
uponyaji mafarakano ni moja ya njia anayoitumia shetani kuondoa Baraka na
kukunyima kujibiwa maombi.
1Peter 3:6-7 “Kama
vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo
mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote. Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake
zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama
warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.”
Wanandoa wengine
pia wanatumia tendo la ndoa kama njia ya kuadhibiana na kutesana, kunyimana
tendo la ndoa kunaweza kukuletea balaa za kimwili na kiroho na kufungua mlango
wa shetani kupata nafasi na kuharibu taasisi ya ndoa na familia na kusababisha shetani apate mlango wa
kupenyeza mambo yake yakiwepo magonjwa, lakini sio hivyo tu kukufunga na
kukunyima uponyaji, kunyimana tendo la ndoa ni dhambi kwa sababu ni kinyume na
maagizo ya Mungu, pia kunavunja umoja ambao Mungu aliukusudia kwa wana ndoa na
kunatoa mlango mpana sana wa kusababisha majanga makubwa, ikiwa Yesu alisema
ole wake mtu yule asababishae makwazo, ni afadhali afungiwe jiwe kubwa shingoni
na kutoshwa baharini, maana yake kukoseshana kunakotokea kupitia tendo la Ndoa
kunaleta madhara yanayofanana na mauti, kubwa zaidi kunazuia uponyaji kwa
muhitaji wa maombezi.
1Wakorintho 7:3-5. “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki
yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri
juu ya mwili wake, bali mkewe.Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili
mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa
na kiasi kwenu.”
5.
Kushiriki
meza ya Bwana isivyostahili - watu
wafundishwe vizuri kuhusu meza ya Bwana na uwepo wa Mungu unaokuwepo kwenye
meza ya Bwana, meza ya Bwana ni mojawapo ya njia ya uponyaji, lakini watu
wakishiriki meza ya bwana bila kutubu dhambi, au bila kuipa heshima
inayostahili meza hiyo inaweza kusababisha magonjwa na magonjwa hayo yakawa
hayawezi kupona kwa maombezi wala njia nyinginezo
1Wakorintho 11:27-30 “Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha
Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini
mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na
kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa
sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha
wamelala.”
6.
Kutokuomba
– Yakobo 4:2 “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na
kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa
kuwa hamwombi!”
Kanuni ya kimaandiko
inatutaka tuombe, kila kitu tunachokihitaji, katika ulimwengu wa kiroho
kinapatikana kwa kuomba kwa hiyo katika huduma za uponyaji muhudumu anapaswa
kuwa na muda wa kuomba, omba karama za uponyaji, omba Mungu ajidhihirishe, omba
Mungu alithibitishe neno lake kwa ishara na maajabu, omba Mungu ishara na
miujiza itendeke kwa jina la mtumishi wake Yesu, lakini vile vile wanaoombewa wapate
muda wa kuomba, kumbuka Yesu aliwauliza watu aliowahudumia wakati mwingine
wataka nikufanyie nini, kwa hiyo muombewaji ana haki ya kuomba hata kwa ufupi,
ili kwamba Mungu aweze kumponya, zamani sana nilisoma kitabu kimoja kiitwacho
Edmundi John Mtu wa Mungu, Mtumishi huyu alikuwa ni mshirika wa kanisa la
Anglican ambaye Mungu alimtumia sana zamani, inasemekana alikuwa na undugu na
Askofu Sepeku wa kanisa la Anglican wakati huo, kiufupi Edmund alikuwa akifanya
maombezi siku za ijumaa katika makanisa na alikuwa akifunga siku ya ijumaa na wakati
huo huo aliwataka waliokuwa wanataka maombezi pia nao kufunga kwa hiyo yeye aliomba
kwaajili ya uponyaji na waombewaji waliomba kwaajili ya kuponywa na ulipofika
muda wa maombezi, Mungu alifanya miujiza Mikubwa sana na watu waliponywa sana,
kwa hiyo maombi ni nyenzo Muhimu sana kwaajili ya huduma za uponyaji, hamna
kitu kwa sababu hamuombi!
Matendo 4:29-31 “Basi
sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako
kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa
jina la mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali
pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la
Mungu kwa ujasiri.”
7.
Kuwepo
kwa nyenzo za utendaji wa ibilisi – ufunguliwaji wa uponyaji wa aina
mbalimbali hauko mbali sana na ufunguliwaji wa changamoto za kipepo, kuna
uhusiano Fulani wa uwepo wa ugonjwa na pepo kuna wakati ugonjwa Fulani unaweza
kuwepo kama dalili ya kuwepo kwa pepo wenye kusababisha aina hiyo hiyo ya
ugonjwa kwa mfano
Mathayo 22:12 “Wakati
ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu
akanena na kuona.”
Unaona huyu
alikuwa kipofu yaani haoni na pia alikuwa hasemi Sehemu nyingine anaonyeshwa
alikuwa bubu na kiziwi pia lakini Mathayo anaonyesha kwamba sababu hizo
zilisababishwa na Pepo na Yesu alipolikemea ewe pepo bubu na kiziwi toka mtu
huyu alipokea uponyaji wake wote
Marko 9:25-27 “Naye
Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu,
akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala
usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama
amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua
naye akasimama.”
Katika uponyaji
wa Mtu huyu Yesu anapolikemea pepo tunaona akiweka na amri wala usimuingie
tena, Yesu alikuwa anajua kuwa ni desturi na ni kawaida kuwa pepo wana tabia ya
kurudi tena na ndio maana sehemu nyingine Yesu alionya kuwa ili uponyaji wa mtu
uweze kuwa kamili, asiruhusu tena nyenyo za utendaji wa shetani, nyenzo hizo
Yesu aliziita mapambo na pia dhambi, hivi vikirudiwa tena vinampa haki shetani
ya kurudi tena na kusababisha tatizo endelevu au hata kuleta janga baya zaidi
Mathayo 12:43-45 “Pepo
mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa
kupumzika, asipate. Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata
akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda, akachukua pamoja naye
pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo;
na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo
itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya.”
Yohana 5:13-14 “Lakini
yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa
sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya
hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije
likakupata jambo lililo baya zaidi.”
Unaona kwa
msingi huo ili mtu aweze kupokea uponyaji kamili hana budi kuhakikisha kuwa anaondoa
mapambo na kuacha kuifanya dhambi iliyosababisha apatwe na ugonjwa huo mapambo
katia kiyunani linatumika neno Kosmeō kwa kiingereza Decoration ni lugha ya mficho aliyoitumia Yesu ikimaanisha nyenzo
za kishetani kama hirizi au vifaa vya kiganga na kichawi ambavyo ulipewa kama
njia ya ulinzi, pembe, chungu, hirizi, na kadhalika hivyo vinapaswa kuharibiwa
kwaajili ya uponyaji kamili wa kiungu, aidha kabla ya uponyaji au baada
vinginevyo utaweza kuona hali ile ya
kwanza ikijirudia rudia hii inaweza sana kuwahusu wale waliofunguliwa kutoka
kwenye mapepo. Na ndio maana watu wa Efeso walipolipokea neno walichoma vitu
vyote walivyokuwa wakivitumiwa kwa uganga na uchawi hata kama vilikuwa na
thamani
Matendo 19:18-19 “Na
wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu
wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao,
wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona
ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.”
Kwa hiyo uko
umuhimu wa kuharibu kila nyenzo za utendaji wa ibilisi, ili kutokumpa nafasi na
kibali cha kurudia vifaa vyake vya kiibada vinavyompa mamlaka ya kukuonea na
kukufikia tena na tena, jambo hili linampa Mungu nafasi ya kuifanya kazi kamili
ndani ya mwili wako, nafsi yako na roho yako kama mponyaji.
8. Vikwazo vya mitazamo ya Kitheolojia -
Mungu yuko tayari kuwaponya watu wake na ni mapenzi yake kamili kuponya, na
Mungu hana upendeleo yeye anajiita mimi ndimi Bwana nikuponyaye maana yake yeye
ni mponyaji, JEHOVAH RAPHA, watu
wanaumwa na Mungu anataka kuwaponya wote, Mungu hana upendeleo hawezi kumponya
huyu kisha akamuacha huyu, kama tumezingatia ukweli kuhusu neno lake na matakwa
yake yote ya uponyaji kwanini asikuponye?
Lakini moja ya changamoto kubwa sana katika huduma za uponyaji utaweza
kuona ni pamoja na vikwazo vya mitazamo
ya kitheolojia, na hasa wanatheolojia
waliosoma vyuo vya Biblia, unapofanya utafiti mdogo tu unaweza kugundua watu wengi
wanaotumiwa na Mungu katika huduma za uponyaji wengi wao sio wote ni wale ambao
labda hawajaenda vyuo vya biblia, Elimu tunazopata zinapaswa kuwa msingi wa
kutufungua macho zaidi, na kupanua uwezo wetu wa kuitawala dunia na kufanya
huduma zetu katika ubora unaokusudiwa, kwa bahati mbaya sana Elimu nyingi za dunia
zinawafunga watu katika boksi na kuwawekea mipaka, kwa hiyo utashangaa mtu
anakuja na somo lake KWANINI WENYE HAKI
WANATESEKA? Somo hilo litakupa
sababu kadhaa wa kadhaa zinazopelekea kuweko kwa mateso katika maisha ya
mwanadamu, ukiangalia kwa makini somo hilo ni kama linataka kutoa uhalali wa
watu kuteseka na wakati mwingine kufikiria kuwa labda ni mapenzi ya Mungu mtu
ateseke, kwa hiyo kunakuwepo na Labda tatizo hili limetokana na sababu hii au
ile labda labda zinakuwa nyingi sana, na ndio maana leo hii Dunia imekuwa na
magonjwa mengi sana, na watu wanateseka sana na nguvu za uponyaji katika
makanisa mengi zimepungua, na watu wanakabiliwa na changamoto nyingi na za aina
mbalimbali, pamoja na maendeleo makubwa
ya kisayansi katika tiba ya afya, bado watu wanateseka na sasa makanisani
tunashuhudia magonjwa makubwa sana na ya kutisha sasa yako kwa washirika na
wachungaji, sasa maelefu ya washirika na wakristo wanaumwa, siku hizi sio ajabu
kusikia, kansa, figo, sukari, presha, migandamizo ya mawazo, moyo, na michangamoto kibao iko makanisani, sababu
kubwa ni misimamo ya kitheolojia waliyo nayo watumishi wengi wa Mungu, watu
wanaweza kuja na neno la kukutia moyo tu
na kukuhurumia, na wakati mwingine
wakisema ugonjwa huu au tatizo hili ni mapenzi ya Mungu, na wengine utasikia
hakuna sababu ya kujiuliza kwa nini?, hii ni mpango wa Mungu na wengine utasikia ugonjwa huu ni mwiba, au
inawezekana ni Mungu anakunyenyekesha ili uwe karibu naye kwa hiyo Mungu
anaruhusu eti atulete karibu kupitia magonjwa na matatizo yaliyosababishwa na
wanadamu, Mungu asingejiita yeye ni Bwana mponyaji kama asingelikuwa na mpango
wa kutuponya, mojawapo ya sehemu ya Mungu kuonyesha upendo wake kwetu ni pamoja
na uponyaji, kwa hiyo mojawapo ya sababu kubwa sana wakristo kuteswa na
magonjwa leo inachangiwa na elimu zetu kuhusu Mungu, kama tukimuamini Mungu, na
kukumbuka ya kuwa aliahidi uponyaji na kuwa yeye si mtu hata aseme uongo
uponyaji wa wagonjwa itakuwa ni kama kupumua tu
Zaburi
103:3 “Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa
yako yote,” Hesabu 23:19 “Mungu si mtu,
aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo
amenena, hatalifikiliza? ”
Waebrania 6:16-18 “Maana
wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote
ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha. Katika neno hilo Mungu, akitaka
kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza
kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika,
ambavyo katika hivyo MUNGU HAWEZI KUSEMA UONGO, tupate faraja iliyo imara, sisi
tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu;”
Isaya 55:10-11 “Maana
kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali
huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na
mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa
changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa
katika mambo yale niliyolituma.”
Yeremia 1:11-12 “Tena
neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa
mlozi. Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu,
ili nilitimize.”
Maswala ya
uponyaji yako kwenye ahadi za Mungu kwetu, na kwa sababu hiyo yeye hawezi tu
kututia moyo kwenye neno lake kuhusu uponyaji kisha asifanye, kwa hiyo ni
lazima kwetu kuweka uwiano mzuriwa elimu zetu za kitheolojia katika kuamini
uponyaji wa kiungu, na tusiuchepushe kwa namna yoyote Mungu ni mponyaji na
ameahidi katika neno lake na hawezi kusema uongo!
Wanatheolojia
wengine wanaamini kuwa Maswala yote ya uponyaji wa kimiujiza yalikuwa zamani,
nyakati za mitume tu na kuwa siku hizi Mungu hashughuliki tena na uponyaji wa
kimiujiza kwa hiyo makanisa yao yana waamini ambao kwa miaka mingi sana wamekosa
kuona Mungu akishughulika na uponyaji wa kimiujiza,inasikitisha sana kuona kuna
ujinga mwingi sana wengine wanasoma hata maandiko yakionyesha kuwa Paulo mtume
aliacha Ndugu mmoja ambaye alikuwa anaumwa, wanaamini hata Paulo mwenyewe
alikuwa na tatizo ambalo Mungu hakumponya mwenyewe alilita mwiba wake ambao
unasadikiwa kuwa yalikuwa macho mabovu, vyovyote iwavyo kumbuka Paulo mtume
alijibiwa maombi yake Mungu alisema naye kuwa anaweza kumtumia kwa neema yake
bila kujali udhaifu aliokuwa nao ambao aliomba aponywe, lakini hii haimaanishi
hata kidogo kuwa Mungu haponyi, na wewe sio Paulo Mtume yeye alipewa mwiba huo
kusudi asijivune kwa sababu ya mafunuo makubwa sana aliyopewa ambayo wewe na
mimi hatuna !
2Timotheo 4:20 “Erasto
alikaa Korintho. Trofimo nalimwacha huko Mileto, hawezi.”
2Wakorintho 12:7-9 “Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo
nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna
kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba
kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika
katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa
Kristo ukae juu yangu.”
Wagalatia 4:13-15 “Lakini
mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa
mwili; na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa,
bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu. Ku wapi, basi, kule
kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho
yenu, mkanipa mimi.”
Kwa hiyo ujuzi
wetu wa kiungu (Theolojia) ina
nafasi kubwa sana katika utendaji wa huduma za uponyaji, kutokana na mitazamo
mbalimbali ya kitheolojia wako watu wanafaidika na uponyaji katika makanisa yao
na wako watu wasiofaidika na uponyaji katika makanisa yao kwanini ni kutokana
na jinsi mtu anavyomuwekea Mungu mipaka, na athari za namna anavyoamini na namna
anavyojaribu kulitendea kazi neno la Mungu au kile alichokisikia au
kuaminishwa, kama Imani yetu inasadiki katika swala la uponyaji wa kimungu basi
kumbuka ya kuwa Mungu anaponya hata sasa, na tuache woga wa kuombea wagonjwa,
nimefanya utafiti katika makanisa mengi sana siku hizi kuna janja janja nyingi
sana katika maombezi, watu wamepoteza ujasiri wa kufanya maombezi kwa waamini na hii ndio
inasababisha watu wasafiri kwenda mbali kutafuta uponyaji wa kiungu mbali sana badala
ya kupata msaada wa karibu kutoka kwa kwa watumishi wa Mungu walioko karibu
katika miji yao, kumbuka hapo ulipo Mungu amekuweka ili watu watafute msaada
kutoka hapo karibu na sio wasafiri mpaka mbali.
Mimi ndimi Bwana nikuponyaye
Kutoka 15:25-26 “Naye akamlilia BWANA;
BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi
akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko; akawaambia, Kwamba utaisikiza
kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na
kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu
yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye.”
Mimi Ndimi Bwana nikuponyaye!
Mungu anapojitambulisha kama mponyaji kwa wana wa Israel, anajifunua kwetu pia
watu wa mataifa kuwa yeye ni Mponyaji wa ulimwengu mzima na mponyaji wa kila
mtu, Yesu alipokuja duniani alikuja kufanya mapenzi ya baba yake, kwa sababu
hiyo alipokuwa akiponya pia alikuwa akifanya mapenzi ya Mungu, kwa sababu kila
kitu alichokifanya alikuwa ameandikiwa kukifanya, kwa hiyo uponyaji ni mapenzi
ya Mungu kamili.
Waebrania 10:5-7 “Kwa hiyo ajapo
ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari;
Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema,
Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako,
Mungu.”
Sisi nasi tunapaswa kufanya vile
vile kama Yesu alivyofanya, na Kristo aliahidi kuwa kazi alizozifanya sisi
tutafanya naam na kubwa kuliko hizo alizozifanya
Yohana 14:12-13 “Amin, amin, nawaambieni,
Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na
kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo
lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.”
Kwa hiyo uponyaji ni mapenzi kamili ya Mungu, Mungu anataka kutuponya, wako watu wengine wanaofikiria kuwa labda
huenda Mungu hataki kuwaponya, hii ni kwa sababu tu ya moyo wa kukata tamaa,
mkoma mmoja alimjia Yesu akiwa na ukoma wake, alifikiri ni mapenzi ya Mungu
yeye kuwa na ukoma, kwa sababu ukoma ulionekana kama ni pigo kutoka kwa Mungu,
hawakuwa wanajua kuwa mateso na magonjwa ni kazi ya shetani, Mungu katika wema
wake na upendo wake mkuu hawezi kutuadhibu kwa magonjwa kwa hiyo katika Kuomba
kwake aliomba kama ukitaka waweza kunitakasa na Yesu alipojibu kuwa nataka
takasika, alikuwa akionyesha kuwa anataka uponyaji na uzima kwa wote. Je Mungu anataka kukuponya? Jibu ni ndio Mungu
anataka kukuponya amini katika uponyaji wake
Marko 1:40-42 “Akaja kwake mtu mwenye
ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.
Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.
Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.”
Kwa hiyo swala la uponyaji sio
Mungu akitaka, hapana Mungu anataka ni mapenzi yake kumponya kila mtu, lakini
katika shughuli za uponyaji Mungu hutumia njia mbalimbali katika uponyaji kwa
jina lake hizi nazo ni muhimu kuzijua
1. Uponyaji kupitia neno la Mungu - njia
mojawapo ya kuleta uponyaji ni kupitia neno la Mungu, Neno la Mungu huwa
linaambatana na nguvu za uponyaji, Mungu anasema ya kuwa neno lake halitamrudia
bure na kuwa litatimiza mapenzi yake, kwa hiyo Mungu hulitumia neno lake
kusababisha uponyaji na kuwaondoa watu kutika katika maangamizo.
Isaya 55:10-11 “Maana
kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali
huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na
mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa
changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa
katika mambo yale niliyolituma.”
Zaburi 107:19-20 “Wakamlilia
Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya,
Huwatoa katika maangamizo yao.”
Uponyaji wa
kutumia neno la Mungu unafanyika kupitia ibada maalumu za maombezi, katika
ibada hiyo, ambayo inaweza kutanguliwa na sifa na kuabudu, kisha linakuja neno
la Mungu, neno hilo linakusudia kuelezea jinsi Mungu anavyowaponya watu wake,
litaonyesha nguvu za Mungu za uponyaji, na jinsi alivyoponya watu mbalimbali,
kwa hiyo wakati llikizungumzwa katika upako na uwepo wa Roho Mtakatifu Imani za
watu zitapanda kwa sababu Imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa
neno la Kristo Imani ya watu itapanda na watu watakuwa tayari kupokea uponyaji
na miujiza yao wakati wa maombezi.
Warumi 10:10,17 “Kwa
maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata
wokovu. 17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la
Kristo.”
Matendo 14:8-10 “Na
huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa
mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena;
ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa
sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.”
Neno la Mungu
linapohubiriwa katika mamlaka ya kutia moyo na kuinua Imani kwaajili ya
uponyaji linapandisha Imani ya wasikiaji na hivyo kusababisha uponyaji, kwa
hiyo baada ya neno la Mungu mtumishi anaweza kualika watu mbele au kupita
akiwasaidia na kuwaombea watu na utaweza kuona wakifunguliwa, huduma ya
uponyaji inakwenda sambamba na kufukuza pepo wenye kusababisha udhaifu wa namna
mbalimbali.
2.
Uponyaji
kwa kuwekea mikono – Kuwekea mikono wagonjwa ni moja ya sehemu ya njia ya
kufanya maombezi kwa wagonjwa na wakaweza kupokea uponyaji wao, njia hii ni ya
kimaandiko na ilifanywa na Kristo mwenyewe na imeahidiwa kwa waamini wote.
Luka 4:40-41 “Na
jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali
waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao
waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu.
Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo.”
Yesu Kristo
aliwaponya wagonjwa wengi sana kwa kuwawekea mikono, kwa msingi huo kuweka
mikono ni mojawapo ya njia sahihi ya kupitisha neema ya Mungu kwa watu wake
kutoka kwa watumishi wa Mungu, njia hii inakubalika sana kama njia ya upendo
kwa sababu unaweka mkono juu ya mgonjwa na kumuombea ukimtamkia afya njema kwa jina la Yesu. Ni njia inayokubaliwa na
wanatheolojia wengi Yesu aliitumia na kisha na yeye pia alituagiza kuitumia,
aliamini kuwa waamini wataweka mikono juu ya wagonjwa nao watapata afya
Marko 16:17-18 “Na
ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema
kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru
kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Tunapoweka
mikono juu ya mtu mwenyye udhaifu na kuanza kumuombea kwaajili ya muhusika
tunafanya hivyo tukiamini ya kuwa Roho wa Mungu atapitisha neema yake na kumpa
mgonjwa nafasi ya kupona, maombi hayo huambatana na kulitaja jina la Yesu,
tendo la uwekaji mikono pia hutumiwa na kanisa kama njia ya Kuruhusu Roho Mtakatifu
kupitisha neema yake sio tu ya uponyaji bali ya uongozi na pia kazi na majukumu
mbalimbali ya kikanisa
Matendo 6:5-6 “Neno hili likapendeza machoni pa mkutano
wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na
Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;
ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao
juu yao.”
Matendo 8:14-19 “Na
mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno
la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea
wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila
wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao
wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho
Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni
na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho
Mtakatifu.”
Matendo 13:1-3 “Na
huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni
Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa
ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia
Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa
kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao
juu yao, wakawaacha waende zao.”
Kuwekea mikono
sio tu ilikuwa kwaajili ya wagonjwa lakini pia ilikuwa njia ya kuwaombea watu
wapokee Roho Mtakatifu, na vile vile kuweka wakfu viongozi, kwa hiyo Mungu kwa
vile ni Roho hufanya kazi na wanadamu katika kuipitisha neema yake kupitia
mikono wanayoweka juu ya wagonjwa kwa makusudi ya kuleta afya, na vile vile
kwaajili ya kuombea neema nyinginezo, kama ujazo wa Roho, hekima, uongozi, busara
na kadhalika.
3.
Uponyaji
kwa njia ya Maombezi – Mungu ndiye mponyaji, uponyaji ni mali yake na
unatoka kwake hata hivyo Mungu huweza kuponya kupitia mawakala wake yaani
watumishi wake kwa sababu Mungu ni ROHO na hivyo sio rahisi kumuona kwa macho,
kwa hiyo kunapotokea changamoto Mungu huwatumia watumishi wake kwaajili ya
kuomba au kuombea na kwa mamlaka aliyowapa uponyaji hutokea
Mwanzo 20:17-18. “Ibrahimu
akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao
wakazaa wana. Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa
Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu.”
Mwanzo 25:21 “Isaka
akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA
akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.”
2Wafalme 20:4-7. “Ikawa,
kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la Bwana likamjia, kusema, Rudi,
ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako asema
hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya;
siku ya tatu utapanda nyumbani kwa Bwana. Tena, nitazizidisha siku zako, kiasi
cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme
wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Daudi,
mtumishi wangu. Naye Isaya akasema, Twaeni mkate wa tini. Wakautwaa, wakauweka
juu ya jipu, naye akapona.”
4.
Uponyaji
kwa njia ya Karama za Roho. – Katika kanisa Mungu ametoa karama za aina
mbalimbali kwaajili ya kuujenga mwili wa Kristo ziko karama nyingi, Paulo mtume
ametaja karama za Roho Mtakatifu kama tisa ambazo huwa tunazigawa katika
makundi makuu matatu.
·
Karama za
Usemi – Aina za lugha, tafasiri za lugha na Unabii
·
Karama za
Mafunuo – Neno la hekima, Neno la Maarifa na kupambanua roho
·
Karama za
Uweza – Neno la Imani/neno la Mamlaka, Miujiza, na Karama za uponyaji
Kwa kawaida
karama zinazohusika katika kuwahudumia watu kwa uponyaji ni karama za uweza
yaani Imani, Miujiza na Uponyaji, hizi ni karama zinazowekwa na Roho Mtakatifu
kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uwezo maalumu wa kuamini katika
Mungu na kuomba kwa Imani na kusababisha ukarabati katika mwili (Uponyaji) au
miujiza, somo kuhusu karama ni pana lakini
(mimi nataka kuzungumzia kwa ufupi sana za uweza) mtumishi mwenye Karama
hizi kwa kawaida anatumiwa na Mungu katika kiwango cha juu na cha tofauti katika kufanya kazi za kimiujiza na uponyaji,
kila mtu aliyeokoka anaweza kuombea mwingine na hata asiyeokoka anaweza kuomba
kwaajili ya mgonjwa na Mungu akajibu, hata hivyo mwenye karama anakuwa na
umaalumu zaidi katika kutumiwa na Mungu kwa eneo hilo zaidi ya wengine.
1Wakorintho 12:4-11 “Basi pana tofauti
za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni
yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule
azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa
kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la
maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na
mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya
miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za
lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo
mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.”
Kwa msingi huo
pamoja na kuwepo kwa uponyaji kwa njia ya maombezi, lakini wote tunakubaliana
ya kuwa Mungu kwa kutumia karama au watu aliowapa karama za uponyaji anaponya
watu wake, karama za Roho Mtakatifu ziko miongoni mwa mwili wa Kristo, watumishi
wa Mungu hawana budi kumuomba Mungu awape karama hizi kwaajili ya mahitaji ya
watu wetu walioko duniani na makanisani ambao wanahitaji uponyaji. Karama hizi unaweza kuzitaka na unaweza
kupewa kwa kuomba hata hivyo Mungu hutoa karama hizi kama apendavyo yeye
Mwenyewe.
1Wakorintho 12:31 “Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo
nawaonyesha njia iliyo bora” 1Wakorintho 12:11 “lakini
kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke
yake kama apendavyo yeye.”
5.
Uponyaji
kwa njia ya kupaka Mafuta - Uponyaji
kwa njia ya kupaka mafuta umekuwa maarufu sana katika nyakati za leo na
kuliacha kanisa likiwa katika vipande viwili, wale wanaopinga uponyaji kwa njia
ya kupaka mafuta na wale wanaokubali, Maandiko tangu mwanzo yanaonyesha kuwa
uponyaji wa kimungu haujawahi tu kuwa katika mfumo wa aina moja, hata karama za
uponyaji, haiitwi karama ya uponyaji inaitwa karama za Uponyaji kwa sababu ya
utendaji tofauti tofauti lakini kwa Roho Yeye yule mmoja, Biblia inasema nini
kuhusu uponyaji kwa njia ya kupaka mafuta? Hakuna ubaya kutumia mafuta katika
kumuombea Mgonjwa, mafuta yanatumika sana lakini Maombi ya Imani ndio njia ya
juu zaidi inayoleta uponyaji, Yesu alipowatuma wanafunzi wake katika maagizo
yake ya uponyaji aliagiza maswala kadhaa ikiwepo kuombea wagonjwa na kuwapaka
mafuta.
Marko 6:12-13 “Wakatoka,
wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi
waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.”
Yakobo 5:14-15. “Mtu
wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka
mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na
Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.”
Ni muhimu
kufahamu hata hivyo kuwa njia ya upakaji mafuta ni lazima ihusishe maombi na
mafuta haya ni yale yaliyotokana na zeituni, ambayo zamani yalitumika kuweka
wakfu viongozi, ili waweze kuwaokoa watu mafuta haya yaliwakilisha uwepo na
neema ya Roho Mtakatifu kwaajili ya kuharibu vifungo mbalimbali vya kikoloni na
kutoka kwa waonevu, na ndio maana Isaya alitabiri ushindi mkubwa wa Hezekia
dhidi ya wababiloni, kwamba kwaajili ya kutiwa kwake mafuta atavunja nira, ile
nira inavunjwa na Roho Mtakatifu ambaye aliwakilishwa na mafuta wakati wa agano
la kale.
Isaya 10:27 “Tena
itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake
shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.”
Yesu alipokuja
Duniani yeye ni mpakwa mafuta ndio masihi, hata hivyo yeye hakupakwa mafuta
halisi kutoka katika pembe au kichupa bali Mungu alimpaka mafuta yaani alimjaza
kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwa msaada kwa watu, kwa hiyo mafuta ni njia ya
kupitisha neema ya Mungu sawa tu na kuwekea mikono, hata hivyo Roho wa neema
anaweza kushusha neema bila hata ya kuwekea mikono au bila hata ya kupakwa
mafuta halisi.
Luka 4:18-19 “Roho
wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
Luka 3:21-22 “Ikawa,
watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu
zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua;
sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”
kimsingi huduma
hii inaweza kufanyika kwa wagonjwa wengine(hapa sio lazima wale ambao wako
kitandani) na inafanya kazi tatizo kubwa ni kuwa wale wanaokataa fundisho hili
hawajawahi kulitii hata mara moja wanapinga tu kwa sababu wameambukizwa
kipinga, au wana mtazamo mdogo katika theolojia zao kuhusu uponyaji kwa njia
hii ama na inawezekana wamekosa tu uzoefu au zoezi la kufanyia kazi hili (Exiperimental Theology) kama hii
haifanyi kazi jaribu uone paka watu mafuta omba na kukemea kwa jina la Yesu,
isipofanya kazi achana nayo, ikifanya
kazi endelea nayo haitakuwa umefanya dhambi Wathesalonike 5:21 “Jaribuni mambo yote;
lishikeni lililo jema;” iwapo jambo hili halitafanya kazi nimekaa
pale niite mzushi na ikifanya kazi tubu na uache kuanzia sasa kuwashutumu wale
wanaotumia mafuta katika uponyaji, kibiblia hata kuwekea mikono tu pekee ni
sawa na kuweka mafuta kwa sababu Mungu huitumia mikono kupitisha neema yake,
lakini wagonjwa wakiwa na imani wanaweza kupokea miujiza yao na uponyaji wao
bila kuwekewa mikono wala kupakwa mafuta, Mafuta zamani yalitumika kuweka wakfu
viongozi, na Roho wa Mungu alikuja juu yao, Mafuta yanatumika kuwaombea watoto
neema, kuweka wakfu makasisi katika makanisa yasiyo ya kipentekoste, pia
kuombea wagonjwa ambao hawawezi hata kuinuka
ndio maana unaweza kuona Lugha ya Yakobo Na awaite wazee… Lugha hii
awaite wazee akiwa hawezi maana yake inahusu zaidi mgonjwa aliyeteseka mno
kitandani, lakini hii haimaanishi kuwa isitumike kwa wagonjwa wengine, kumbuka
yakobo pia anasema Mtu wa kwenu amekuwa hawezi, kiingereza Is any sick amongo
you? Yaani yeyote ambaye anaumwa miongoni mwenu kwa hiyo kanisa lisitumie nguvu
sana kushindana na agizo hili, washirika wako watakuona mjinga pale unapokemea
mafuta ili hali wao wamehudumiwa kupitia mafuta na wanaendelea vizuri. Kitu
ambacho kanisa linaweza kukemea ni matumizi ya kupita kawaida ya mafuta au sura
ya kibiashara kupitia mafuta hayo, lakini kitheolojia ushahidi wa kimaandiko
unaonyesha kuwa hakuna shida kuyatumia mafuta katika kuombea wagonjwa kwa
sababu mafuta hayo yanapakwa kwa jina la Bwana Yesu na kimaandiko uko ushahidi
wa zaidi ya andiko moja,
Mathayo 18:16 “La,
kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya
mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike.”
2Wakorintho 13:1 “Hii
ndiyo mara ya tatu ya mimi kuja kwenu. Kwa vinywa vya mashahidi wawili au
watatu kila neno litathibitishwa.”
1Timotheo 5: 19 “Usikubali
mashitaka juu ya mzee, ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.”
Kwa mujibu wa
kanuni za kutafasiri maandiko, ni kwamba huwezi kufanya fundisho kwa kupitia
jambo ambalo limesemwa katika ushahidi wa mstari mmoja tu au tukio moja tu
ambalo halijajirudia mara mbili kwa hiyo kitaalamu matumizi ya mafuta kwa kuwa
yametajwa mara kadhaa katika maandiko ni halali, jambo ambalo linahitajika
katika kila kitu ni kiasi tu. Mtumishi aliyetumiwa sana na Mungu katika miujiza
na uponyaji T.L. Osborn katika kitabu
chake kiitwacho Healing the sick chapter 7 page 26 anaeleza kuhusu maombezi ya
kupaka mafuta kama Nanukuu “This is an unmistakably clear Promise of
healing for the sick” mwisho wa kunukuu kwa tafasiri yangu isiyo rasmi anasema “hii ni wazi au sahihi ahadi isiyo na dosari kwa
uponyaji wa wagonjwa” ni ahadi ya uhakika so bnafsi nakubaliana naye kuwa
hakuna shida kutumia mafuta kuwaombea waonjwa.
6. Uponyaji
kwa njia ya Hospital - Uponyaji wa hospitalini ni mojawapo ya
njia ambayo Mungu ameiweka kwa wanadamu wote, kupitia akili na maarifa ambayo
Mungu amewapa watu wake na uwezo mkubwa wa wanasayansi katika kufanya utafiti,
na kuvumbua madawa ya kisasa imekuwa ni njia ya uponyaji wa wanadamu ya
kawaida, Mungu anauwezo wa kuponya moja kwa moja kwa njia ya Imani, lakini pia
anaweza kutumia vyanzo vingine kama njia ya kuleta uzima, Katika historia ya kanisa la Kwanza Mtumishi
wa Mungu Timotheo alikuwa akisumbuliwa na vidonda vya tumbo, na kutokana na
taratibu za kitabibu za wakati ule Paulo alimshauri Timotheo kutumia mvinyo
kidogo
1Timotheo 5:23 “Tokea
sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na
magonjwa yakupatayo mara kwa mara.”
Aidha pia
Mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume na injili ya Luka, yaani Doctor Luka
ambaye alikuwa katika timu moja ya umisheni na Paulo Mtume mtu huyu alikuwa na
taaluma ya udaktari (tabibu) kwa Kiswahili cha zamani Wakolosai 4:14 “Luka, yule tabibu mpendwa,
na Dema, wanawasalimu.” Hii maana yake ni kuwa walikuwepo matabibu
wa kawaida na lugha ya matabibu ipo kwa wingi katika sehemu nyingi ikiashiria
walikuwepo na walikuwa wakifanya kazi za kitabibu, na ndio maana hata Yesu alitumia mifano ya
walio na afya hawahitaji tabibu
Mathayo 9:12 “Naye
aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.” Marko
2:17 “Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya
hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye
dhambi.”
7.
Uponyaji
kwa njia nyingine mbalimbali – Ziko njia nyingine mbalimbali ambazo
kimsingi haziwezi kutengenezewa fundisho kwa sababu hazina ushahidi wa maandiko
mengine, na hazina tukio la kujirudia rudia au hakuna ushahidi wa andiko zaidi
ya moja, lakini ni njia ambazo Mungu alizitumia kuponya watu naziweka hapa kwa faida
tu ya kuoanua ufahamu lakini sitoi idhini ya kutumiwa kwa njia hizo kwa sababu
hazithibitishwi mara zaidi ya mbili katika maandiko lakini iko haja ya kuzijua na kujifunza kwa kuwa zimetajwa
mara moja, tu katika maandiko.
a. Nyoka wa Shaba - Watu walikuwa
wamemuasi Mungu na manung’uniko na hivyo Mungu aliruhusu nyoka za Moto yaani
Nyoka wenye sumu, waliokuwa wakiwaadhibu, wakati watu walipotafuta suluhu Mungu
alimuelekeza Musa kuweka nyoka wa shaba, na ya kuwa kila atakayeumwa na nyoka
atapaswa kuangalia nyoka yule wa shaba, na angepata nafuu
Hesabu 21:8-9 “Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke
juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. Musa akafanya
nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu,
alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.”
Tunajua kuwa Nyoka huyu wa shaba alitumika kama alama
kivuli kuonyesha Kuwa Yesu atawaponya watu watakaomtazama yeye, lakini kwa
wakati huo ilikuwa ni ishara halisi ya uponyaji na Israel waliponywa kwa wakati
ule.
Yohana 3:14-17
“Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka
jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye
awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda
ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali
awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu
ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.”
b. Uponyaji kwa kutumia matope na mate –
Yohana 9:6-7 “Alipokwisha kusema hayo, alitema mate
chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho, akamwambia,
Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda
na kunawa; akarudi anaona.”
c. Uponyaji kwa kugusa upindo wa vazi (Talit) –
Luka 6:19 “Na makutano yote walikuwa wakitaka
kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote”. Marko
5:25-29 “Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda
wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa
vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa
mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa
vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi
ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule.”
d. Uponyaji kwa njia ya vitambaa na nguo –
Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono ya
Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo
zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”
e. Uponyaji kwa njia ya kivuli – Matendo 5:15
“hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na
kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake
kimwangukie mmojawapo wao.”
f.
Uponyaji
kwa njia ya Mkate wa tini – Isaya 38:21 “Maana
Isaya amesema, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.”
g. Uponyaji kwa njia ya chumvi – 2Wafalme
2:19-22 “Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia,
twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji
yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie
chumvi ndani yake. Wakamletea. Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa
ile chumvi humo ndani, akasema, Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya;
hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. Hivyo yale maji yakapona hata
leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.”
h. Uponyaji kwa njia ya kijiti – Kutoka 15:25
“Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye
akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu
huko, akawaonja huko;”
i.
Uponyaji
kwa njia ya tiba mbadala – Yeremia 51:8 “Babeli
umeanguka na kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake;
ili labda apate kuponywa.” Yeremia 8:21-22 “Kwa
sababu ya maumivu ya binti ya watu wangu nimeumia mimi; nimevaa kaniki;
ushangao umenishika. Je! Hapana zeri katika Gileadi? Huko hakuna tabibu? Mbona,
basi, haijarejea afya ya binti ya watu wangu?”
Hakuna jambo Muhimu katika maisha
ya mwanadamu kama Afya, Na ndio maana mwanadamu anaweza kufanya lolote
analoweza kulifanya ilimradi tu aweze kuwa na uzima, uzima wa afya ya mwili
ndio unaoamua ustawi wa kimwili nafsi na roho, shetani alikuwa na uhakika kuwa
mwanadamu akiguswa kwenye afya anauwezo hata wa kumkufuru Mungu ilimradi tu
atakuwa mzima,
Ayubu 2:4-6 “Shetani akamjibu Bwana, na
kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai
wake. Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye
atakukufuru mbele za uso wako.Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo
mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake.”
Marko 5:25-26 “Na mwanamke mmoja mwenye
kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya
matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo,
bali hali yake ilizidi kuwa mbaya”
Maandiko yanaonyesha kwamba
mwanadamu anaweza kutoa kila kitu alicho nacho endapo tu afya yake itaguswa,
Shetani alitoa hoja hiyo alipokuwa akizungumza na Mungu kuhusu Ayubu, na Marko
anatuonyesha mwanamke ilimgharimu vitu vyote alivyo navyo kwaajili ya uzima
wake, kwa hiyo unaweza kuona kuwa hakuna mwanadamu anayependa kuteseka, Na ndio
maana Mungu katika hekima yake ameahidi kuwaponya wanadamu, anajua umuhimu wa
afya kwa mwanadamu, yeye ni Mungu mwenye wivu mkubwa sana hataki watu watafute
msaada kwa waganga na wenye pepo wa utambuzi, jambo hilo linamuuzunisha sana.
Walawi 19:31 “Msiwaendee wenye pepo, wala
wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.”
2Wafalme 1:16-17 “Akamwambia, Bwana asema
hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni
kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, uulize Neno Lake? Kwa hiyo hutashuka
katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Basi akafa, sawasawa na
neno la Bwana alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika
mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye
hakuwa na mwana.”
Watu wanaweza kwenda kwa waganga
na wachawi au miungu kwa sababu tu ya kutafuta uponyaji na msaada, Mungu ni
Mungu mwenye wivu, hataki tutegemee miungu mingine wala wanadamu kwa hiyo
anapojitambulisha kuwa ni Mungu mponyaji, maana yae uponyaji ni swala la
uhakika, kwa Msingi huo na kwa namna yoyote ile kanisa halina budi kuutafuta
uso wa Mungu, uwepo wa Mungu, karama za uponyaji na miujiza kwa kusudi la
kuwasaidia watu kwa sababu Mungu yuko tayari na ahadi zake ni ndio na kweli
yeye si mtu hata aseme uongo.
Kwa habari ya njia za uponyaji
ambazo hazina andiko zaidi ya moja la ushahidi, kanuni za utafasiri maandiko
haziruhusu kutumia tukio ambalo halijajirudia zaidi ya mara mbili kutumika kama
fundisho lakini jambo la Msingi linaonyesha kuwa mwanadamu anauwezo wa kufanya
lolote waajili ya uzima wake na hivyo kanisa lisipokuwa msaada wanadamu hao
wanaweza kuutafuta msaada huo nje ya kanisa, au katika mikono ya watu wasiokuwa
salama kwao, Agizo la Yesu Kristo kwa kanisa ni pamoja na kuifanya kazi hii ya
kuwafungua watu, agizo hilo la Kristo limekataza kabisa kufanya biashara
kwaajili ya uponyaji.
Mathayo 10:7-8 “Na katika kuenenda kwenu,
hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni
wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.”
Kwa hiyo kibiblia ni marufuku
kuutumia uponyaji wa kiungu kama biashara kwa kuwa Mungu ndiye mponyaji mkuu na
huponya kwa kutumia wanadamu lakini wa jina lake na kwa nguvu zake, wala
wanaoponywa wenyewe bila kushurutishwa na Mtu wanaweza kuguswa na Mungu,
kumtumza mtumishi wa Mungu na kusaidia huduma yako kwa vile tu waliguswa
wenyewe kuona umuhimu wa huduma ya uponyaji, wako wanawake ambao waliisaidia
huduma ya Yesu kwa sababu walikumbuka tu jinsi Mungu alivyowarehemu kupitia
mtumishi wake lakini swala hilo sio sharti ni shukurani tu kwa wale ambao Mungu
amewatendea na kwa hiyari yao wenyewe
Luka 8:1-3 “Ikawa baada ya hayo alikuwa
akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema
ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha
wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu
aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake
Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.”
Wanawake wengi waliokuwa
wameponywa na Yesu, kutokana na kuelewa umuhimu wa huduma za uponyaji waliyatoa
maisha yao kumsaidia na kumtunza mtumishi wa Mungu kwa mali zao, walifanya
hivyo kwa hiyari yao na kwa mioyo yao na kwa shukurani zao, ili Yesu aendelee
kuwahudumia wengine, kwa hiyo waamini walioponywa na waliookolewa wanapaswa
kuwa na ufahamu kuwa ili kujitoa kufanya huduma hii watumishi wa Mungu
watahitaji muda mrefu, wa kuutafuta uso wa Mungu na uwepo wake na nguvu za
Mungu na hivyo watahitaji kutunzwa bila ya kutumia janja janja.
Rev. Innocent Mkombozi Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni