Jumatatu, 6 Mei 2024

Falsafa za Utumishi (Hekima za Utumishi).


Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”



 Pichani ni Reverend Innocent Samuel Kamote, aka. Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima

Utangulizi:

Leo tutachukua muda kuzungumzia miongozo inayoweza kutusaidia na kutukumbusha wajibu wetu kama wahudumu katika jamii, namna na jinsi inavyotupasa kuenenda miongoni mwa wale tunaowahudumia, kuwa Muhudumu wa jamii na hasa kiongozi wa kiimani, kisiasa na katika jamii kunahitaji neema ya Mungu, na nidhamu ya hali ya juu, na muongozo utakaotusaidia kuweza kuifanya huduma hii kwa unyenyekevu na ufanisi mkubwa tukimpendeza Mungu na wanadamu, hii ni muhimu sana kwetu kusudi tusiwe watu wa kukataliwa hususani na baba yetu wa Mbinguni.

1Wakorintho 9:25-27 “Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”

Falsafa za utumishi ni muongozo au dondoo zinazotusaidia kutupa picha ya utumishi wetu mzima kwa jamii, na kutusaidia kujua wajibu wetu kama viongozi namna na jinsi inavyotupasa kuenenda ili kutimiza kusudi letu kubwa ambalo Mungu ametupa kwaajili ya kuitumikia jamii, wajibu huo unahitaji nidhamu, nidhamu ambayo wanamichezo wanayo na huishika ili wapokee taji au kombe liharibikalo, na pia kwaajili ya kulinda umahiri wao wakati wanaposhiriki michezo, lakini sisi tunahitaji kujitia nidhamu ili tupokee taji isiyoharibika. Paulo anasema naye ana fanya zoezi  (Nidhamu ya kiroho) hilo kila siku la kujitia nidhamu ili hatimaye asijekuwa mtu wa kukataliwa, anataka kuwaongoza wengine lakini bila kuingia matatani na mwajiri wetu ambaye ni Mungu kwa hiyo ili jambo hili liweze kufanikiwa tunahitaji muongozo wa kutusaidia kuelewa sisi ni nani, tunapaswa kufanya nini, tunafanyaje na tunatimizaje kusudi zima la huduma ambayo Mungu ametupa kuwasaidia watu wake, tutajifunza somo hili Falsafa za Huduma kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

·         Maana ya Falsafa

·         Falsafa za utumishi        

Maana ya Falsafa:

Neno falsafa limetokana na Neno la kiingereza Philosophy  ambalo kwa asili ni neno la Kiyunani Philosophy yaani Muungangiko wa neno “Phileo” na “Sophia”  Phileo ni Upendo na Sophia ni Hekima  neno hili liligunduliwa na Mwanafalsafa wa kiyunani aliyejulikana kama Pythagoras  ambaye yeye alisema kwa kuwa Mungu ndiye Mwanzilishi wa Hekima basi ukimcha Mungu au ukimpenda Mungu utakuwa na hekima au maarifa, Neno Philosophy kwa hiyo ni kupenda Hekima,  au kwa ufupi ni Hekima tukilitohoa neno hilo tunapata neno Falsafa katika Kiswahili.  

Mithali 1:5-7 “mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia. Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao. Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.”

Kazi kubwa ya falsafa ni kutoa muongozo, na kutatua changamoto zozote zinazowakuta wanadamu kwa kutoa kweli zitakazodumu milele zikiwaongoza wanadamu kuishi na kutenda na kuenenda kwa busara, Falsafa inafanya kazi katika mazingira yote na pasipo falsafa jamii inapoteza muelekeo, kila jamii yenye maendeleo makubwa ni jamii iliyofuata falsafa iliyo bora, walijiwekea falsafa wakaifanyia kazi ikawaongoza na kuleta matokeo yanayokusudiwa!

Kwa hiyo katika somo hili tutakuwa tukijifunza sasa dondoo au falsafa za utumishi, yaani miongozo ambayo itatusaidia kama viongozi wa jamii, siasa na imani, kutupa hekima na akili ya namna ya kuwahudumia watu na watu hawa wakaridhika huku sisi nasi tukibaki kuwa salama katika utumishi wetu na huduma zetu.

Falsafa za utumishi.

# 1.  Kwaajili ya utukufu wa Mungu.

Utumishi wowote ule ambao Mungu ametupa, iwe ni katika siasa, au jamii au kanisa yaani kiimani kusudi lake kubwa ni ili Mungu atukuzwe, ili Mungu ainuliwe, ili sifa na utukufu na heshima zimrudie Mungu.

 

Isaya 43:7 “Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.”

 

Kila mtu duniani ameumbwa kwaajili ya utukufu wa Mungu, kwa hiyo viongozi wote wa kijamii, kisiasa na kiimani ni lazima tukumbuke kumpa Mungu utukufu, kuhakikisha ya kuwa kila tunalolifanya katika jamii kutoka moyoni tunalifanya kwaajili ya utukufu wa Mungu, Yesu aliwafundisha wanafunzi wake wakati wote kukumbuka kuwa wanapofanya jambo wajiambie nafsi zao kuwa wao ni watumishi tu wasio na faida

 

Luka 17:7-10 “Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.”

 

Mungu atakapokuwa anatoa hukumu yake kwa kazi zetu tulizozifanya hatahukumu si tu kwa kile tulichokifanya lakini atahukumu kwanini tunafanya, yaani nia yetu ya kufanya tunachokifanya.               

 

Katika nyakati zetu za leo tulizo nazo kumekuweko watu wanaotafuta kubeba utukufu kwa sababu zisizo hata na msingi, wakati Fulani Mke wangu alikwenda kuombewa na nabii mmoja ambaye alivuma sana katika mji wa Tanga, kwa hiyo mke wangu alikuwa na hitaji lake ambalo kimsingi mimi nalifahamu na Mungu alishasema na mimi kuhusu changamoto ya mke wangu hata kabla ya kumuoa, Lakini alishawishiwa na baba yangu mzazi kwenda kwa nabii huyo na kwa heshima ya baba yangu na hitaji la mke wangu nilimuacha aende, kwa nasibu baada ya maombezi ya nabii yule alimwambia mke wangu amlete mumewe, na kwa sababu ya kuheshimu watu wa Mungu niliamua kwenda kwa nabii yule, nilihudhuria ibada ambapo kulikuwa na ibada ya sifa na neno la utangulizi kabla nabii hajatokea, ibada ya sifa ilikuwa nzuri sana na kisha neno la Utangulizi, neno la utangulizi lilikuwa likiwaandaa waamini kukutana na nabii na kumuamini nabii, “hakuna shaka katika hilo kwa sababu neno linasema mwaminini Mungu nanyi mtathibitika waaminini manabii wake nanyi mtafanikiwa”  Lakini katika ibada ile maandiko mengi sana yalitumika kutuelekeza namna ya kumpokea nabii na kulikuwa na vitisho vingi sana ikiwa ni pamoja na maelekezo kuwa nabii akikuchagua kama anataka kukuhudumua utapiga magoti chini wakati wa kuzungumza naye, hayo hayakuwa na shida yoyote, ibada ile ya utangulizi iliisha na kisha nabii alikuja alikuwa ni kijana mdogo na ukilinganisha na umri wangu, alikuwa ameanza huduma miaka kama mitatu tu na mimi nikiwa katika huduma zaidi ya miaka 20 sina neno na umri wa kihuduma kwa sababu hayana msingi katika Kristo, lakini ibada ya kinabii ilipoisha nilitakiwa kwenda ofisini kuonana naye kwa sababu yeye ndiye aliniita, nilikuwa nimevaa suti yangu nyeusi safi sana na nabii alikuwa na shati lake na jinsi wala hakuwa amechomekea shati lile mimi nilivaa kiatu cheusi cha kupiga kiwi na nabii alikuwa na raba tu, hilo nalo halikuwa na shida, wakati nikielekea ofisini kwake niliambiwa na binti mdogo sana kwamba nivue viatu vyangu ninapokwenda ofisini kwa nabii, nilisita sana kwa sababu nabii mwenyewe alikuwa na viatu na aliingia navyo ofisini kwake na jingo lile halikuwa kanisa lingekuwa kanisa nadhani hakungekuwa na shida kuvua viatu, nimewahi kuvua viatu nilipotembelea msikiti wa wahindu kwa sababu nilipeleka wanafunzi wangu wa somo la dini za ulimwengu kujifunza Imani za watu mbalimbali hivyo kule haikuwa shida, kwani hata shekhe wa wahindu nay eye alivua viatu,  lakini kwa vile ni ofisi za watu na niliamuriwa kuvua viatu vyangu, nilivua viatu vyangu na kuingia, nilisalimiana naye na akanijulia hali na akaniuliza vipi mtumishi wa Mungu nilimueleza kuwa changamoto ya mke wangu ilitoka kwa Mungu na Mungu alishasema na mimi hata kabla sijamuoa, kwa hiyo hakuna nabii anaweza kuitangua! tulisalimiana na kisha tuliagana hakuthubutu hata kuniombea, kwa sababu na mimi nilimuomba Mungu upako na utishio mkubwa sana kwa hiyo aliniogopa, nilitoka na kuvaa viatu vyangu na nilipotoka katika mlango wa ofisi nilimkazia macho binti yule aliyeniambia nivue viatu, ilihali nabii mwenyewe yeye hakuvua viatu vyake, kisha nikaondoka zangu. Kitu nilichojifunza pale ni kuwa watu wanatishiwa sana ili watuone sisi watumishi wa Mungu kama malaika au kuwa sisi ni watu maalumu sana, wakati ukweli unabaki tu kuwa  sisi ni wanadamu ni watumwa wa Yesu Kristo tusio na faida watu wana mbwembwe nyingi sana, na makeke mengi ya kujitangaza wao kuliko Kristo, mimi nimelelewa kiroho Pale Mwenge kwa Akofu @Zachary Kakobe, tangu nikiwa Makongo secondary kidato cha pili, na kanisani nilikuwa nakaa viti vya mbele mstari wa kwanza kabisa  katika  ukumbi namba moja naujua UTISHO wa kimungu na mimi mwenyewe nimetembea na utisho wa kimungu kwa hiyo,  Na nilimuona Mchungaji wangu Kakobe akiwa na utisho na mimi haukunisumbua, ila pepo ndio walisumbuka, mimi mwenyewe naujua utisho wa Mungu na nimetembea nao, niliwahi kwenda hoteli moja na rafiki yangu na tukaongea na muhudumu aliyetuhudumia na kisha tulifurahi kwa huduma yake na hivyo tulitaka kumbariki wakati tunatamka Baraka kumuombea kumbe alikuwa na mapepo aliagunshwa chini na kupiga makelele nikamkemea pepo nab inti yule akawa huru, kumbuka ilikuwa tu hotelini,  sio ile mikwara ya kibinadamu, watu tunaomtumikia Mungu tuache vitimbi vyovyote vya kutafuta utukufu usio sahihi, tunaweza kujitengenezea mauti kwa sababu tu ya kuchukua utukufu wa Mungu au kutaka sifa kutoka kwa wanadamu, watu wote walionizidi umri mimi huwaamkia shikamoo, hata baada ya salamu za kidini, siwezi kumpigisha magoti mtu aliyenizidi umri, lakini naogopa pia magoti kwa sababu yameumbwa kwaajili ya ibada nayaona magoti ni kama mali ya Mungu, tusiharibu utumishi wetu kwa kujifanya kuwa sisi ji miungu watu au watu maalumu sana. Upako kama upo upo tu na kama hakuna hakuna

 

Matendo 12:20-23 “Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme. Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao.Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.”

 

Herode alikuwa kiongozi wa kisiasa katika jamii, alikuwa na mamlaka aliweza hata kuwafunga na kuwahukumu watu wa kanisa, siku moja alipokuwa akihutubia watu walishangilia hutuba yake wakasema si mwanadanu anayenena ni Mungu, akiwa katika mavazi yake ya kifahari, Malaika wa bwana alikuja kumpiga na stroke na akafa pale pale, Mungu anapokuweka katika nafasi yoyote ile kumbuka kujishusha na ukiona watu wanakusifia sana kataa sifa hizo zisizo na msingi, wakumbushe watu kuwa ni wajibu wangu/wetu kuwahudumia kwa sababu Mungu ameniweka niwahudumie, lakini kama tunafanya huduma hizi katika jamii na tukalewa sifa kiasi cha kujisahau kuwa sisi ni wanadamu tunaweza kupatwa na mabaya, Paulo Mtume na Barnaba walikataa kupokea ibada walirarua mavazi yao na kuwakumbusha watu kuwa wao sio Mungu, wao ni wanadamu kama walivyo wanadamu wengine wenye mwili na nyama  

 

Matendo 14:8-15 “Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda. Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng'ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;”

 

Kwa hiyo ni muhimu kukumbuka kuwa tunawahudumia watu wa Mungu, sisi ni watumishi wa Mungu yaani watumwa wa Mungu, hatuko kwaajili ya kutafuta mambo makubwa, kuhudumia watu ni wajibu wetu hatupaswi, kulazimisha kutafuta heshima Mungu mwenyewe atatuheshimu kadiri tunavyojitoa katika utumishi wetu, na kufanya kila tulifanyalo hakikisha ya kuwa unalifanya kwa utukufu wa Mungu na upendo.

 

 Yeremia 45:5 “Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema Bwana; lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.”

 

1Wakorintho 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.”

 

Yohana 12:26 “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.”

 

Kwa hiyo falsafa ya kiutumishi inatukumbusha kuwa wacha Mungu, inatukumbusha ubinadamu wetu sisi ni wadhaifu Mungu ni Muumba, kiumbe kamwe hakiwezi kulinganishwa na Mungu kwa sababu zozote zile, wakati wote hatunabudi kuhakikisha kuwa sisi tunapungua na Mungu anazidi.

 

Yohana 3:27-30 “Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua.”

 

Isaya 42:6-8 “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa. Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.”   

 

# 2.  Kwaajili ya kuwa Pamoja na Mungu

 

Moja ya sababu kubwa kwanini Mungu alimuumba mwanadamu, ilikuwa ni pamoja na kuwa na ushirika naye, Mungu anatamani sana kufanya kazi pamoja na mwanadamu duniani, ile dhana ya Mungu pamoja na wanadamu yaani Imanuel (Mungu Pamoja nasi) lilikuwa ni wazo la Mungu la zamani sana na ambalo lilihariiwa katika bustani ya Edeni baada ya anguko, baadaye Mungu atakuja kulitimiza mwisho wa nyakati.

 

Ufunuo 21:1-3 “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.”

 

Yesu Kristo alipokuwa anawachagua viongozi yaani mitume ambao wangekuwa wasaidizi wa kazi zake duniani mwandishi wa injili anaonyesha kuwa pamoja na kuwatuma wale mitume ambao ni viongozi moja ya maswala ya msingi ni pamoja na watu hao kuwa pamoja naye angalia mkazo wa neno wapate kuwa pamoja naye kama msingi kwa kwanza, kisha wafanye kazi yake, kisha wawe na mamlaka dhidi ya Pepo wabaya!

Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”

Hii maana yake ni nini?  Mungu anataka viongozi wa kisiasa na kijamii na kimani kuwa wenziwake maana yake wawe na ushirika wa kudumu pamoja na yeye, Kimsingi hatuwezi kuzaa matunda kama tunakuwa nje ya uwepo wa Mungu, Ili amani na uwiano wa kibnadamu ulio bora uwepo viongozi ni lazima wawe marafiki wa Mungu, (wawe wacha Mungu) Baba yetu Ibrahimu alikuwa rafiki yake Mungu, Daudi mfalme yule mkuu katika Israel aliyekuwa na mafanikio makubwa sana alikuwa katika moyo wa Mungu, kwa hiyo alipokuwa akiwaongoza watu mara kwa mara alihitaji ushauri kutoka kwa Mungu, alikuwa na manabii maalumu kwaajili ya kuyajua mapenzi ya Mungu, hali ya Daudi ya Kiroho iliathiri hali ya taifa zima japo alikuwa kiongozi wa Kisiasa kwa hiyo ni lazima tumtegemee Mungu, lazima tuwe na yeye kwaajili ya mafanikio yetu na maandiko yanaonyesha kuwa peke yetu hatuwezi lakini pamoja na Mungu tutatenda makuu

Yohana 15:4-5 “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”

Zaburi 60:11-12. “Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai. Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.”

Sasa ili kudumisha ushirika huo na Mungu viongozi wa kijamii, kiimani na kisiasa wanapaswa kuwa karibu na Mungu. Na ni kwa jinsi gani tunaweza kwa neno la Mungu na kwa maombi, huduma zetu zitakuwa na ukavu kama hatutakuwa na neno la Mungu na maombi, kwa hiyo huduma ya kudumu katika kuomba na kulihudumia neno haipaswi kupuuzwa kwa kila kiongozi anayetaka mafanikio makubwa katika uongozi wake

Matendo 6:2-4 “Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”

Yoshua 1:7-9 “Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”

1Wafalme 2:1-3. “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;”

Maandiko yanatuonyesha umuhimu wa neno la Mungu ambalo likijumuishwa na maombi  na utii litaleta mafanikio makubwa sana yatakayosaidia kuzalisha matunda yanayokusudiwa,  watu tunaowaongoza ni watu wa Mungu bila kujali wanatokea wapi, na sisi timewekwa na Mungu kuwahudumia hatuwezi kutumia fimbo ya kibinadamu kuwaongoza lakini tunaweza kuwaongoza tukijishikamanisha na mwenye watu wake ambaye ni Mungu mwenyewe, tulitumie neno la Mungu kuwaongoza, kuwaelekeza na kuwatendea haki, jamii inafurahi anapotawala mtu wa Mungu na jamii huugua atapotawala mtu muovu,  Mithali 29:2 “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua.” Hivyo kumcha Mungu ni lazima.

# 3.  Kwaajili ya kuwatumikia watu.

Kusudi kubwa la Mungu kuwachagua watu miongoni mwa watu wake ili kuwasimamia watu wengine kijamii, kisiasa na kiimani ni ili watu hao watumikiwe, wako viongozi kadhaa duniani ambao ni kama miungu watu, wako mbali sana na jamii, wako juu ya jamii, ni maboss na ili uwakute huna budi kupanda na ngazi, jamii inajua kuwa wanapaswa kuwaheshimu viongozi, wanaelewa lakini viongozi hawapaswi kuitafuta heshima hiyo na Yesu Kristo alituonyesha mfano kivitendo ya kuwa alikuja kuwatumikia watu

Marko 10:42-45 “Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

Wafilipi 2:5-11 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba

1Petro 5:1-3 “Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.”    

2Nyakati 10:6-8 “Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa? Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote. Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, waliosimama mbele yake.”           

Mafanikio makubwa  kwa viongozi wote waliofanikiwa ni wale ambao walikuwa ni viongozi watumishi, Yesu alifanikiwa sana na kuheshimika sana mbinguni na duniani kwa sababu ya moyo wake mkubwa wa unyenyekevu, na kujishusha na kuamua kuwatumikia watu, falsafa hii itafanya kazi kwa wafalme, makuhani na manabii namaanisha viongozi wote wa kijamii, kisiasa na kiimani. Tufuate njia na nyayo ya Bwana Yesu na tutaona aina ya uongozi wetu itakuwa nyepesi na Mungu ataweka mkono wake kutufanikisha., tuwatue watu mizigo yao, tutatue matatizo yao, tuwasikilize na tujihadhari kuwatwisha mizigo isiyo na sababu (Mfano katika nchi yetu kuna malalamiko ya kikokotoo, ambacho wabunge hakiwahusu, lakini wala kinaowahusu wanaumia na wanalia lakini hakuna mtu wa kuwasikiliza, viongozi wanaosimama kwaajili ya watu watasimama kuwatetea watu na sio kuwakandamiza)

#4.  Kwaajili ya Upendo:

Iko dhana potofu duniani ambayo imejengeka katika jamii kwamba watu wengi sana hudhani ya kuwa mtu anapokuwa kiongozi basi ameuchinja! Dhana hii ni ya kipumbavu kwa mtazamo wa Mungu, kwani jambo hili husababisha watu wautake uongozi na ama wanapokuwa viongozi wawe na ubinafsi, tamaa ya fedha na ushindani, nia ya kweli inayokubaliwa na Mungu katika swala zima la uongozi ni upendo na huruma, na sio kuwaendesha watu wa Mungu badala ya kuwaongoza, maandiko yanatuonyesha ya kuwa bila upendo kila kitu kinakuwa hakina maana

1Wakorintho 13:1-3 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.”

Upendo unapaswa kuongoza nia zetu za ndani za kuwatumikia watu, wakati ubinafsi unataka tuchukue, badala ya kutoa, kuwa waovu badala ya kuwa wema, kulazimisha badala ya kusihi, kuwaongoza watu kwa upendo kunahusisha uwazi, kuwa tayari kuwa baba mwenye huruma kwa jamii, au mama mwenye huruma, lazima tuwahurumie watu na kuwaongoza tukijua kuwa ni watu wa Mungu na sio watu wetu, Yesu kila alichokifanya kwa watu alikifanya kwa sababu aliongozwa na upendo. Aliwaona wanadamu kuwa ka amkondoo wa baba yake, na hivyo hakuwahi kuweka maslahi yake mbele hata siku moja moyo wake ulijali   

Mathayo 9:36-38 “Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”

Ni nini kinakusukuma kuwaongoza watu Mungu anachunguza moyo, na anaiona nia yako ya kuwatumikia watu basi iwapo nia yako ni njema hakikisha kuwa nia hiyo inadumu na tusibadilike mpaka mwisho.

# 5.  Kwa kuwezeshwa na Mungu            

Kuhudumia watu sio kazi nyepesi ni Mzigo, uongozi ni mzigo, viongozi hukutana na changamoto nyingi, shida za watu ni shida zao, maumivu ya watu ni maumivu yao, wanapoumia wao viongozi huumia, wanapopatwa na shida nao huweza kuhisi zile shida kama ni zao, kwa hiyo wajibu huo ni mlima, katika mpango wake Mungu viongozi wote wa kisiasa, kijamii na kiimani Mungu hakuwahi kuwatuma bila kuwapaka mafuta yaani bila nguvu za Roho Mtakatifu, Yesu Kristo alifanya wanafunzi wengi lakini aliandaa viongozi 12 na wengine 70, na wengie  120, na wengine 500, na kadhalika na hata baada ya mafunzo mengi ya nadharia na vitendo aliwataka wasiondoke bila ujazo wa Roho Mtakatifu.

Luka 24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Zakaria 4:6-7 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”

Roho Mtakatifu ni Mungu na anahusika na kitengo cha maongozi, hakuna kiongozi anaweza kuona mambo kuwa mepesi bila kuvikwa uwezo huu utokao juu, uwezo huu ndio unaomfanya kiongozi kuwa mtu mwingine, ndio unaomfanya kiongozi kubeba mzigo wa uongozi, ndio unaomfanya kiongozi kuwa na hekima, fahamu na ujuzi, na maarifa na uchaji wa Mungu na kuwa na mzigo wa kukataa udhalimu na uonevu wa watu, wafalme waamuzi na mashujaa wengi katika biblia waliifanya kazi waliyoifanya kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa juu yao

1Samuel 16:1-3,13. “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako”.  “Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”

Uweza, mamlaka na nguvu zako zitakazokurahisishia kazi wakati unapoelekea kutekeleza majukumu yako ni Roho Mtakatifu kuwa juu yako, yeye ni nyenzo muhimu katika utumishi tulioitiwa, usifanye kazi mwenyewe hakikisha kuwa una nguvu za Mungu, dumisha uhusiano wako na Roho Mtakatifu atakusaidia kukabiliana na kila aina ya upinzani na kukupa hekima ambayo Mungu anaikusudia  na ndio maana nyakati za kanisa la kwanza wakati wote walizingatia sana kuwachagua viongozi ambao wana uhusiano mzuri na Roho Mtakatifu

Matendo 6:3-6 “Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao.”

Ningeweza kusema mengi na kutoa mifano Mingi lakini kila asomaye na ahafamu wote tunajua umuhimu wa Mungu Roho Mtakatifu katika utumishi wetu basi na tusimzimishe, tujiulize tu hapa duniani kuna kiongozi aliyekuwa bora kushinda Yesu Kristo? Na ikiwa Yesu Kristo tu alihitaji kuwa na Roho Wa Mungu juu yake kabla ya kufanya huduma  je sembuse wewe na mimi, hatuwezi kufika kokote bila yeye  watu hawa ni mali yake na Yeye ndiye Bwana wa mavuno yote tutakayoyafanya kwaajili ya kuhudumia watu ni matokeo ya nguvu hizo za uungu kuwa juu yetu

Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

# 6. Kwaajili ya kuufuata mfano wake

Zamani sana nilikuwa napenda sana kuwaweka watu Fulani ambao kwangu walikuwa ni mashujaa wa Imani kama mfano wangu wa kuwafuata, na ndivyo wengi tulivyo, tunaweza kuwataja hapa wahubiri wakubwa sana na kuwaita kama mfano wetu na wakati mwingine tukawaita baba zetu wa kiroho!, yako mafundisho pia siku hizi ambayo yanasisitiza kwamba kila mtu awe na baba wa kiroho na wakati mwingine tunaambiwa ni hatari sana kama mtu hana baba wa kiroho, maandiko hayako kinyume sana na  kuwa na baba wa kiroho lakini yako mazingira ambayo wakati mwingine yanaweza yakakunyima kuwa na hao  na ni hatari sana kuwa na baba wa kiroho mwanadamu, nadhani neno zuri ni kuwa na Mchungaji. Au mchungaji rafiki ambaye anaweza kukushauri, au Mchungaji mwenye umri uliozidi wako, kukuongoza na kukukosoa au kukukemea na kukuonya. Biblia haijawahi kutuagiza kuwa na baba wa kiroho, wala hajaituamuru wakristo kuitwa baba tunaambiwa tunaye baba mmoja tu aliye mbinguni, lakini maandiko yanataka tuwakumbuke waliotuongoza, na kuiga Imani yao, lakini kwa kuuchunguza sana mwenendo wao

Mathayo 23:8-12 “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.  Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.”

Waebrania 13:7 “Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.”

Kwanini kwa sababu wao ni binadamu, naweza nikajivunia mtu Fulani, lakini ukashangaa watu wanaomjua kwa ukaribu wakawa wanakushangaa, kwa sababu wote hao ni binadamu, Abrahamu anaitwa baba wa Imani kwa mujibu wa maandiko, lakini hata hivyo yako mambo tunaweza kujifunza kutoka kwake na mengine tunaona ubinadamu wake sasa nani anaweza kuwa kielelezo chetu katika huduma na utumishi wetu ni Yesu Kristo peke yake  kwa sababu yeye alijaribiwa katika mambo yote kama tujaribiwavyo lakini hakutenda dhambi. Kwa sababu yeye Peke yake ni mkamilifu nay eye pekee anafaa kuwa mfano wa kuigwa!

Zaburi 37:37 “Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani.”

Yakobo 3:1-2 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu”.

Waebrania 4:14-15 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.”

Yesu peke yake ndiye anayeweza kuwa mfano wetu, (rolemodel) yeye hana mapungufu katika idara yoyote ile na kwa sababu hiyo tunaweza kumfuata yeye, tuache kuwa na tabia ya kutukuza wanadamu kwa sababu hatuwezi kusoma nia zao wala mioyo yao, ni Mungu peke yake ndiye aujua moyo wa mwanadamu na tunaambiwa kuwa moyo wa mwanadamu una ugonjwa wa kufisha kwa hiyo Yesu na awe kielelezo chetu katika utumishi wetu, tabia na mwenendo, kiongozi wako wa mfano ni nani ni Yesu, huku tukiwaheshimu wale aliowaweka yeye katika mamlaka ili watuongoze, Yesu ndiye baba yetu wa kiroho.          

Yeremia 17:9-10 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”

# 7.  Kwa unyenyekevu

Nimekataza hapo juu kuwa na baba kwa sababu neno la Mungu linaeleza kuwa baba yetu ni mmoja tu Mathayo 23:8-12 “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.”  

Yesu alikataza wanafunzi wake kutokujiita Rabbi, baba, au viongozi, kwa sababu ya tabia ya mafarisayo ambao walijiita majina hayo kwa sababu ya kukosa unyenyekevu na kutaka kujikweza kwaajili ya kutaka heshima kwa watu, kwa hiyo ni lazima kuchukua tahadhari juu ya hilo,  Na nimekazia hapo juu ya kuwa Yesu ndiye mfano wetu pekee wa kuufuata, hata hivyo tunao viongozi wetu waliowekwa na Mungu, ambao ni wanadamu wanaotuongoza maandiko yanataka tuwaheshimu na kujitiisha chini yao hii kwa lugha ya kiingereza inaitwa Submission 

Waebrania 13:17 “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.” 1Wakorintho 14:32 “Na roho za manabii huwatii manabii.”         

Kama tunaufuta mfano wa Yesu Kristo kamwe hatutaacha kutii mamlaka, na kuzinyenyekea hiyo ndiyo kanuni ya mafanikio ya uongozi wetu ni lazima tujitiishe chini ya mamlaka zilizoko, katika maisha yake yote na huduma Yesu Kristo alijinyenyekeza kwa baba yake, kwa hiyo Kristo anatufundisha kutembea kwa unyenyekevu, hata wale wenye huduma zao binafsi wanapaswa kuwa na watu watakaowashauri, kuwakemea na kuwaonya, ni salama sana kuwa na mtu juu yetu anayetuangalia, mimi hujisikia salama sana nikifanya kazi chini ya mtu, lakini asiwe mtu katili, au mwenye wivu, sina hatari kwa mtu yeyote yule, na ninaweza kumnyenyekea mtu yeyote yule lakini sipendi kuonewa au kunyanyaswa,  isipokuwa kama Mungu amekutuma uninyanyase, huduma yako itakuwa na thamani kama utajinyenyekeza huku watu wakiheshimiana na sio kuvunjiana heshima. Kumbuka kuwa unyenyekevu sio ujinga. 

# 8.  kwaajili ya kujitoa dhabihu.                                             

Uthamani wa kitu chochote kile duniani na katika Imani unapimwa kwa jinsi mtu anavyoweza kujidhabihu, Ibrahimu alihesabiwa kuwa na haki baada ya kuwa radhi kumtoa sadaka mwanae wa ahadi Isaka huu ulikuwa moyo mkunjufu na ukarimu wa hali ya juu hakuna anayeweza kuuiga, Mungu peke yake alimuiga Ibrahimu kwa kuwa tayari kumtoa mwana wake wa pekee kwaajili ya ulimwengu, katika utumushi wetu kwa jamii, siasa, na Imani utagundua kuwa huduma inahitaji kujidhabihu, hii sio kazi ya kivivu kama watu fulani wanavyoweza kufikiri, unaweza kuvutiwa tu na watu Fulani katika huduma hata kutamani kuwa kama wao lakini chunguza sana mapito yao utagundua kuwa waligharimika sana au wanagharimika sana, mpaka kufikia hapo walipofika, ukitaka kuwa na huduma kama ya Paulo Mtume ukumbuke pia mapito yake kwa kweli sio vitu vya kutia moyo hata kidogo,  kuna gharana za kulipa,

 

2Wakorintho 2:21-33 “Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Walakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri. Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Ibrahimu? Na mimi pia. Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?  Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo. Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata;nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.”

 

Kazi ya huduma ina gharama zake na unapokuwa kiongozi ni lazima ukubali kulipa gharama hizo na ili ulipe lazima ukubali kujidhabihu, upweke, mbali na familia, kujinyima na kadhalika wakati mwingine tunachukua muda mwingi sana kuandaa jumbe kama hizi ambazo zinakuwa baraka kwa wengi, ujumbe unaoweza kuhubiriwa kwa dakika 45 wakati mwingine unaweza kugharimu kwa ufinyu masaa nane ya maandalizi, na masomo marefu huchukua wakati mwingine majuma kadhaa, wiki kadhaa, au siku nzima, inagharimu muda na kukaa katika computa kwa muda mrefu, kuchapa na kuandaa ni lazima ujitoe kama kuku anayelalia ili uweze kutotoa bila kujidhabihu wakati mwingine maisha ya huduma hayawezi kuwa rahisi.  Huduma pia inaambatana na vita, na wakati mwingine kusema vibaya, kutukana kusingiziwa, tunaweza hata kuambiwa kuwa ni freemason au unatumia nguvu za giza, au kutuhumiwa kuwa mzinzi, na kusingiziwa, mimi niliwahi kusingiziwa kuwa nilitaka kubaka, na sijawahi kuwaambia watu hao watubu kwangu au wakae kimya  wala sihitaji kujitakasa kwa wanadamu kwa sababu ni kawaida kutuhumiwa, ni kawaida kunenwa vibaya ni kawaida kuchafuliwa  na hatuwezi kumthibitishia kila mtu kuwa tuna wema isipokuwa Mungu ajuae mioyo ya watu, hakuna sababu ya kujibu lolote au kunyamazisha wanaotutukana au kusema vibaya, kwa sababu hiyo ni sehemu ya dhabihu ya kujitoa kwa Mungu, kunenwa vibaya na kusingiziwa ni sehemu ya utumishi wetu nah ii inakuja ili kutunyenyekesha na kwaajili ya Mungu kutuongezea neema nyingi zaidi.

 

1Wakorintho 4:9-13 “Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa.”

 

9 #.  Kwaajili ya kuwakamilisha Watakatifu

Ukuaji ni tabia ya kitu chochote chenye uhai, maendeleo ni dalili ya afya ya jamii yenye akili nzuri, kila kitu chenye uhai kinapaswa kukua, jamii ya watu wa Mungu wanapaswa kukua kiroho, kiidadi na kijiografia, ni kazi ya viongozi kuhakikisha kuwa hilo linatokea, na ndio maana Yesu aliweka huduma kadhaa ndani ya kanisa kwaajili ya ustawi wa jamii ya kanisa.

 

Waefeso 4:11-15 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.

 

Karama za huduma zimetolewa katika kanisa ambazo pia ni karama za maongozi ya kanisa ili kuwaandaaa watu wa Mungu kwaajili ya kazi njema, ili mwili wa Kristo ujengwe, kwa hiyo karama hizi na vipawa hivi sio njia ya kujinufaisha,lakini zimetolewa kwaajili ya ujenzi, ujenzi wa mwili wa Kristo, ni kwaajili tu ya kufaidiana kuufaidisha mwili wa Kristo

 

1Wakorintho 12:4-7 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.”

 

Karama hizi za huduma zimetolewa ili tuweze kuwasaidia wengine na kuwatumikia ili wakue, kwa hiyo sio huduma za kitawala ni huduma za kujenga, lengo lake kubwa ikiwa ni matokeo na matokeo hayo ni ukomavu katika tabia na mwenendo ili watu wawe kama Kristo, yaani Kristo aumbike katika tabia na mwenendo wetu na kumzalia matunda.

 

Kwa mujibu wa Paulo Mtume kuwakamilisha watakatifu ndio lengo kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, na sisi kama watu mishi wake ni muhimu kwetu kuhakikisha tunalifanyia kazi lengo hili, kuwakamilisha watakatifu maana yake ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanakuwa kiroho, na kuondoka katika uchanga na kukomaa, na hili ndio kusudi kubwa la karama za Huduma, hatujazaliwa kama wakamilifu, na hivyo tunapaswa kukulia neema na maarifa katika kumjua Mungu na Mwokozi wetu Yesu

 

2Petro 3:18a “Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.”

 

Kuwakamilisha watakatifu ni kitendo cha kuwaongoza watu wa Mungu katika kukua kiroho na kuishi maisha matakatifu, kuwasaidia kukua kiimani, kuwa na maarifa ya namna ya kuishi sawa na neno la Mungu,  na mafundisho yake,  kwa hiyo ili kukamilisha swala hili, Kufundisha, kutia moyo kusimamia nidhamu, na kuwasaidia waamini zaidi sana kuwapunguzia mizigo yao! Utatatua vipi changamoto zao kwa kuhubiri, na kufundisha na kuwaombea na kufanya semina mbalimbali, kuwafundisha kuomba, kufunga kujitiisha na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na jamii.

# 10.  kwaajili ya  kutoa hesabu

Waebrania 13:17 “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.”

Kazi hii ina hatima na hatima yake ni kutoa hesabu kwaajili ya kila kitu ambacho Mungu ametukabidhi, ikiwemo watu ambao Mungu ametupa

Yohana 17:11-13 “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao.”

Maandiko yanatufundisha ya kuwa tutawajibika tutatoa hesabu mbele za Mungu kama kaka na dada namna na jinsi tunavyohudumiana na kuuhudumia mwili wa Kristo, tunamuona Yesu Mwana wa Mungu akiwajibika kutoa hesabu ya wale aliopewa sisi nasi tutatoa hesabu ya namna tulivyoishi na namna tulivyochukuliana na wenzetu,

Warumi 14:11-13 “Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu. Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha.”

2Wakorintho 5:9-10 “Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye.Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”

Hivyo tunapoishi maisha ya huduma na utumishi lazima tuyakumbuke haya na kujua ya kuwa tutayatolea hesabu mbele za Mungu na mafanikio ya huduma zetu yanategemeana na namna na jinsi tunavyotembea katika falsafa hizo, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuyazingatia haya na kuzidi katika jina la Yesu Kristo amen!

Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima! 





Hakuna maoni: