1 Wafalme 2:1-3 “
Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia
Sulemani mwanawe akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari,
ujionyeshe kuwa mwanamume, Uyashike mausia ya Bwana Mungu wako, uende katika
njia zake, uzishike sheroia zake na amri zake na hukumu zake, sawasawa na
ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ulifanyalo na
kila utazamako;”
Ni muhimu kujiuliza maswali kadhaa hasa kama wewe ni mwanamume kisha Baba
yako akakuusia au kukuambia Mwanangu “JIONYESHE KUWA MWANAMUME” hii ina maana
gani?
Katika jamii mbalimbali ikiwemo jamii zetu za kiafrika na Kiswahili tunazo
namna nyingi sana za kutiana moyo, na maneno yoyote ya kutiana moyo mengineyo
ni pamoja na kumwambie mtu Simama kiume, na kadhalika, katika jamii ya kimasai
kuonyesha uanamume ni pamoja na kutokulia na kuvumilia uchungu na ugumu wakati
wa kutahiriwa, Ngariba wa kimasai huwatairi vijana Morani bila ganzi na kila
kijana anapaswa kuonyesha ujasiri wa kuvumilia bila kulia akionyesha uanaume,
aidha kuua samba ilikuwa ni namna nyingine ya zamani sana katika jamii ya
kimasai yenye kudhihirisha uanaume.
Mfalme Sulemani:
Daudi anakaribia kufa na mwanaye Sulemani anapaswa kuchukua uongozi,
uongozi ni kazi ngumu sio kazi nyepesi inahitaji hekima, ujasiri na
kumtanguliza Mungu mbele lakini kubwa zaidi kusimama katika haki na kuonyesha
uhodari na ushujaa Daudi anamwambia Sulemani asimame kiume, aonyeshe uanaume,
ajionyeshe kuwa mwanamume, Kwa lugha na tamaduni za Kiyahudi au kiebrania nao
walikuwana maana zaidi ya kawaida walipoambiana onyesha uanaume!
Neno hilo Jionyeshe kuwa Mwanamume Kwa kiebrania Husomeka kama IYSH na
kwa Kiyunani Husomeka kama ANDRIZOMAI ambayo maana yake.
Mtu anayeweza kupambana wakati watu wengine wotewameshindwa! Mtu wa
mwisho mwenye kuleta ufumbuzi au ukombozi wakati mji unapovamiwa na kutekwa na
kila mtu anapoonyesha kushindwa, unapojitokeza kuleta suluhu wakati watu
wengine wote wamepoteza tumaini hapo ndipo mtu anapoitwa ameonyesha Uanamume
Kwa nini Daudi alimuagiza Sulemani
kusimama kiume?
1. Daudi mwenyewe alikuwa mtu shujaa, alionyesha uanaume wakati Israel wote
walipokuwa wakiogopa kumkabili Goliath yeye alijitokeza kutoa suluhu, sulemani
angeelewa vema kila ambacho baba yake alikuwa akimuagiza
2. Daudi mwenyewe alimpendeza Mungu na kuhakikisha kuwa Mungu yuko upande
wake wakati wote hata alipokosea alitubu na kubadilika kwa haraka ili Mungu awe
naye hakukubali kupoteza uwepo wa Roho Mtakatifu, alishika sheria za Mungu,
alijua kuwa ili Sulemani aweze kufanikiwa hana budi kuishika Sheria ya Mungu
3. Daudi alikuwa na uzoefu wa kupambana na changamoto mbalimbali na alikuwa
na ujuzi wa kuizima mishale ya adui, alijua namna ya kuwashughulikia adui zake,
kuwalipa mema walio wema na kuwashughulikia waovu au mafisadi na kutokuwaonea
haya wenye kudhulumu Mstari wa 4-9 unasema hivi
“ili Bwana
afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako
wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na
kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli. Na
zaidi ya hayo, umejua alivyonitenda Yoabu, mwana wa Seruya, yaani,
alivyowatenda majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri, mwana wa Neri,
na Amasa, mwana wa Yetheri, ambao aliwaua, na kuimwaga damu ya vita wakati wa
amani, akautia damu ya vita mshipi uliokuwa viunoni mwake, na viatu vilivyokuwa
miguuni mwake. Kwa hiyo ufanye kama ilivyo hekima yako, wala usimwachie mvi
zake kushukia Ahera kwa amani. Lakini
uwafanyie mema wana wa Barzilai Mgileadi, wawe miongoni mwao walao mezani pako;
kwa jinsi walivyonijilia nilipokuwa nimekimbia mbele ya Absalomu, ndugu yako.
Hata, angalia, yuko pamoja nawe Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu,
ndiye aliyenilaani kwa laana kuu siku ile nilipokwenda Mahanaimu; lakini
akashuka kunilaki kule Yordani, nami nikamwapia kwa Bwana, nikamwambia, Mimi
sitakuua kwa upanga. Basi kwa hiyo
usimwachilie, kwa kuwa wewe u mtu wa akili; nawe utajua ikupasayo umtendee, na
mvi zake utazishusha Ahera pamoja na damu.”
Kuonyesha uanaume kibiblia kuna maana ya kusimama katika uhodari wa
kuliangalia Neno la Mungu na kulishika, kuziangalia njia za Bwana kwa moyo wako
wote na kuhakikisha kuwa wale waliokutendea wema au waliowatendea wema baba
zako wanalipwa mema na wale waliotendea uovu baba zako wanashughulikiwa,
tafasiri hii katika mtazamo wa agano jipya yaweza kuwa sio sahii, kwa sababu
hatupaswi kulipa baya kwa baya au kuwatendea wema adui zetu. Lakini kisiasa ni
tafasiri sahii kwa vile kitabu cha wafalme ni kitabu cha viongozi, Kiongozi wa
kisiasa katika taifa letu na taifa lolote ni lazima amtangulize Mungu mbele,
lakini pia waliohusika na ufisadi nilazima ahakikishe kuwa wanashughulikiwa
ipaswavyo ili taifa liwezekuwa na amani.
Ahabu alikuweko katika serikali ya Daudi lakini aliuwa watu wawili
wasiokuwa na hatia, alikuwa ni shujaa lakini hangefaa kuwa kiongozi wakati wa
Sulemani angeleta laana kwa taifa kwa vile ana ufisadi moyoni mwake alitakiwa
ashughulikiwe, Shimei alimtukana Daudi, hata ingawa Daudi alikuwa amemsamehe, Utawala
wa Sulemani haungeweza kuwa wa amani kuendelea kupokea ushauri au kumfanyoia
mema mtu ambaye alimtukana baba yako aliyeweka misigingi ya kitaifa, ilikuwa
lazima shimei auawe halikadhalika alikuwa amemtukana masihi wa Bwana, huwezi
kumtukana masihi wa Bwana kisha ukawa salama hata kidogo ilikuwa lazima
ashughughulikiwe!
Katika kuyashughulikia haya yote kulihitaji Ushujaa, kulihitaji mtu
asimame kiume, na kutokukubali kuyumbishwa ili amani ipatikane. Bwana
angeufanya utawala wa Sulemani kuwa imara kama angeweza kuyashughulikia maagizo
hayo muhimu, Ni maombi yangu kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa John
Pombe Magufuli atasimama kiume na kuhakikisha kuwa anaiangalia katiba na
kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na utawala bora akimtanguliza Mungu na
kuwashughulikia mafisadi bila kuwaonea haya akifanya haya Mungu atauimarisha
utawala wake na sifa ambazo zimeanza kuenea Duniani kwaajili yake zitazidi mara
elfu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Ujumbe na Rev.
Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi
mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni