Ijumaa, 29 Aprili 2016

Uamuzi wa Lutu!


Mwanzo 13:10-12.

“Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari.  Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao.  Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.”

 Ulimwengu wa sasa umekuwa kama Sodomana Gomorah

Kufanya uamuzi ni moja ya maswala ya msingi sana Duniani, kila mwanadamu mwenye akili timamu anapaswa kuelewa kuwa hakuna eneo makini duniani na linalohitaji busana na Neema ya Mungu kama linapokuja swala la kufanya maamuzi, ni lazima tutakutana na nyakati hizi ambazo tunapaswa kufanya maamuzi.

Iko habari moja ya kusismua iliyomuhusu Rais wa zamani wa Marekani Ronald Regan alipokuwa kijana mdogo alichukuliwa na shangazi yake katika mji wa New York ili amnunulie kiatu, kwa Kuchongesha, alipofika kwa fundi fundi alimuonyesha sampuli mbalimbali za viatu vingune vya Squqre na vingine vya kuchongoka Regan alivipenda vyote na hivyo alishindwa kuamua kwa haraka, Shangazi yake alimlipia na kazi ikawa imebaki kwa Regan na fundi alikuwa tayari kumtengenezea kiatu ambacho alichagua, Regan aliamua kurudi nyumbani na kuendelea kufikiri, na mwisho siku nyingi zilipita fundi aliipima miguu ya Regan na hatimaye aliamua kumchongea Regan kiatu kimoja cha kulia kikiwa kimechongoka na kushoto kikiwa square, kutokana na uamuzi huo wa fundi Regan hakukasirika alichukua viatu vile na kuviweka katika kumbukumbu zake na kusema “In this world if you will not Chose someone will chose for you” akiwa na maana Duniani usipofanya uamuzi mtu mwingine atakuamulia

Wote tunakubali kuwa uamuzi huamua hatima ya maisha yetu, Biblia imeonyesha katika maeneo mengi matokeo ya maamuzi na leo tunataka kuuangalia uamuzi wa Lutu

1.      Watu kadhaa katika maandiko wanatufundisha maswala mbalimbali ya msingi
a.       Kutoka kwa abrahamu tunajifunza thanmani ya Imani
b.      Kutoka kwa Yusufu Tunajifunza jinsi Mungu anavyojihusisha na maisha yetu
c.       Kutoka kwa Ayubu tunajifunza umuhimu wa Uvumilivu na saburi
d.      Kutoka kwa Lutu tunajifunza maswala makuu mawili
i.                    Umhuhimu wa kufanya maamuzi
ii.                  Umuhimu wa kufanya maamuzi sahii

2.      Maamuzi ya Lutu.
a.       Uhusiano wa lutu na Abrahamu ulikuwa wa baba mkubwa kwa baba mdogo Mw 12:15:13:1
b.      Wote walikuwa matajiri na Mungu aliwabariki kwa mali nyingi Mwa 13:2-5
c.       Kwa sababu ya mali zao kuongezeaka sana na wachungaji wao kuanza kugombana mali hizi ziliwalazimisha wao kuachana Mwanzo 13:6-9
d.      Abrahamu alimpa Lutu nafasi ya kwanza kuchagua ni wapi anataka kwenda?
e.       Huenda Lutu alipaswa kumuuliza Mungu aku Kumuuliza Baba yake mkubwa kwa vile alikuwa Nabii kumuongoza wapi pa kwenda? Lakini Lutu hakuuliza kwa Mungu wala kwa baba yake mkubwa, alizitumainia akili zake mwenyewe na kwa vila alukuwa mtu aliyepewa nafasi ya kwanza kuchagua alichagua Bonde zuri sana ambalo biblia inalisifia kuwa lilikuwa kama Bustani ya Mungu Mwanzo 13:10-12 ni muhimu kujigfunza kuwa maswala mengine tunayoyachagua yenye muonekano tunaoutaka sisi au kuupenda sisi au wenye kufikirika kuwa una faida kwetu unaweza kutuletea majuto taabu na huzuni nyingi katika siku zetu za maisha.

3.      Matokeo ya maamuzi ya Lutu
1.      Lutu alikutana na Vita Mwanzo 14:11
2.      Lutu alitekwa Mwanzo 14:12
3.      Aliteswa na kuumizwa na wakazi wa Sodoma kutokana na maisha yao yasiyo ya haki 2Petro 2:7-8, Mwanzo 19:1-11
4.      Lutu alipoteza kila alichokuwa nacho Mwanzo 19:15-16, 24-25
5.      Lutu alifiwa na mke wake mpendwa Mwanzo 19:17,26
6.      Lutu alianguka katika dhambi mbaya ya kuzini na Binti zake wa kuwazaa Mwanzo 19:30-36
Matokeo ya Uchaguzi wa Lutu ni lazima yatufunze na kutujengea kitu kuwa kama hatutafanya maamuzi sahii maisha yetu yanaweza kuharibika na kubaki magofu, baadhi ya maamuzi yana mchango mkubwa sana katika maisha yetu, ni muhimu kuwa makini katika maamuzi yetu kumbuka uamuzi wa Lutu ulikuwa ni wapi akaishi lakini uliweza kugharimu maisha yake Ingawa naamini naye alikuwa mtu wa Mungu, Biblia inamsifika katika Petro kuwa alikuwa mtu wa haki, lakini alihitimisha vibaya, tufanyeje? Unapokuja wakati wa kufanya uamuzi? Na je kama tumeshaingia katika maamuzi yasiyo sahii ni nini cha kufanya?

4.      Maamuzi yanayoweza kutuletea athari kubwa zaidi katika maisha yetu
a.      Kumuamini Yeu au kutokumuamini
·       Huu ni uamuzi muhimu sana na unaweza kuathiri maisha yetu Ukimuamini Yesu unaokoka na unakuwa na uhakika wa Uzima wa milele, lakini kitendo cha kumkataa Yeu pia kina athari kubwa sana unahukumiwa sasa na hata milele na milele
·         Kumuamini Yesu kunaamua ni wapi utakuweko Milele.
·      Kumuamini Yesu kutaathiri maamuzi yako mengine Yote utakayoyafanya katika maisha yako
b.      Uamuzi wa Kuoa au kuolewa
·      Huu nao ni uamuzi wa Busara sana unahitaji neema ya Mungu hapa watu wengi wamejuta sana, hata watu wa Mungu wakubwa na wenye upako wamelia na kujuta Ndoa ndio maisha, Ndoa ndio Furaha unapooa au kuolewa ndio umechagua mtu wa kuishinaye na kuzaa naye utakuwa karibu naye siku zote za maisha yako, huku mkiwa mmefungwa hamjui mtakufa lini na nani atatangulia, Bila kujali wewe ni nani Ndoa itaamua maisha yako na hali yako ya Kiroho, wako ambao baada ya kuoa huduma zimekufa, wamepata mikosi na matatizo ya aina mbalimbali, wengine wamefikia hatua hata ya kujiua kwa sababu ya ndoa
·    Ndoa itakuamulia utakuwa na watoto wa aina gani wanawake wanauwezo wa kugeuza moyo hata wa kiimani, Mfalme Sulemani aliyepewa Hekina nyingi sana na ufahamu wa hali ya juu moyo wake ulikengeuka kwa sababu ya wake zake aliowaoa.
·      Kuchagua mume au mke kutaamua kiwango cha furaha mtakayokuwa nayo siku zako zote na maisha yako yote
·         Unaweza kufikiri kwa haraka kuhusu talaka lakini fahamu ya kuwa utaongeza jeraha juu ya jeraha, Biblia inasema ukiacha ukaoa tena unazini na aliyeachwa akioa anazini, hii ni kwa sababu yoyote ile leo hii wakristo wengi sana wameoa watu walioachwa na walioachwa wengi wameolewa tena na kwa vile maswala hayo yanafanyika makanisani, wanajifariji kuwa huenda wako sawa lakini neno la Mungu litasimama vilevile Mungu hatakuhurumia kwa sababu ulikuwa ukiteseka katika ndoa yako ukaamua kuoa au kuolewa na mwanamume mwingine, Biblia inasema wewe unazini na hakuna mzinzi atakayeingia Mbinguni, Mungu analiangalia neno lake na hawezi kuruhusu lichujwe, iwe na Nabii, Mtume, Askofu au yeyote Yule hakuna mtu mwenye mamlaka juu ya Neno la Mungu, Neno ndio mamlaka ya mwisho Mathayo 19:3-10, Dunia ya leo imejaa watoto waliathiriwa kwa sababu walikosa malezi ya pande zote husika kwa usahii, wanawake wengi na wanaume wengi leo bila kujali wanaishi katika zinaa kwa namna nyepesi sana viwango vya maadili vimebomoka na hakuna mwenye kujali Heri kufanya maamuzi ya Busara leo.

c.       Kuchagua Marafiki.

·         Kama ilivyo kwa ndoa na marafaiki pia unahitaji kuwamakini rafiki yako ni nani rafiki anaweza kusababisha Baraka au laana katika maisha yako ukipata rafiki mzuri utabarikiwa Mithali 17:17
·         Lakini ukipata rafiki wabaya utapata hasara katika maisha yako, wako wengi wamesalitiana, wameumizana waliaminiana na wakatendana japo walikuwa marafiki, usifurahi tu kuwa na mtu unayefikiri kuwa ni rafiki bila kuwa makini ikiwezekana hata kumuuliza Mungu Nabii T.B Joshua alisema “ukiongeza chochote katika maisha yako Ongeza Maombi” bila shjaka lolote tunaloliongeza katika maisha yetu linafungua mlango wa shetani kutushambulia zaidi kuliko tunapokuwa wenyewe  ni vema kuwa na marafiki kwa sababu wanadamu hawakuumbwa wawe kisiwa lakini lazima tuwe na umakini wa kutosha katika kuchagua marafiki.Mithali 12:26: 1Wakoritho 15:33

d.      Kuchagua wapi utaishi
Nalo ni jambo muhimu Lutu aliponzwa na wapi pa kuishi na hili ndilo lilikuwa kosa lake alijengeza hema yake mpaka Sodoma na Gomora, matokeo ya uchaguzi wake yamekuwa somo kwetu, wewe nawe waweza kuwa somo kutokana na maamuzi yako, Mungu na atusaidie kwa neema yake asiwepo mtu wa kujuta katika jina la Yesu.

5.      Tunawezaje kufanya maamuzi sahii?
1.      Lazima tuombe hekima na muongozo wa Mungu Yakobo 1:5-8
2.   Tafuta Ushauri kwa wengine hasa wenye haki, hekima na utulivu Mithali 11:14,12:15, wako watu wengine wanajiamini sana na hawataki ushauri, wala kusikiliza wengine au kuuliza
3.      Jadili maswala ya kona watu wazima waliojifunza mengi na wenye uzoefu
4.      Tafuta hekima inayopatikana katika neno la Mungu hasa kitabu cha Mithali
5.      Lolote ufanyalo kwa neno au kwa tendo Fanya kwaajili ya Utukufu wa Mungu na sio kwa Mashindano Zaburi 37:5-6,23-26 Yakobo 4:14

6.      Tufanye nini tunapogundua kuwa tumefanya maamuzi mabaya
·         Fanya kama Lutu alivyofanya alikimbia kuondoka Sodoma na Gomora Biblia inasema wala msiifuatishe namna ya Dunia Hii
·         Fanya yaliyo ya haki bila kubakiza usiangalie nyuma kama mkewe Lutu
·         Fanya toba ya kweli mwambie Mungu nimekosa kabisa nisamehe
·         Kubali kumtumikia Mungu na kumuabudu
·         Sahau yaliyo nyuma na chuchumilia yaliyo mbele kama Paulo mtume
·         Kubali msamaha wa Mungu na amua kumuishia Mungu maisha yako yote
·         Fanya maamuzi ya Busara na Mungu atakutangulia katika mazingira mengine

Kama hujafanya maamuzi ya kumpokea Yesu ni afadhali uyafanye sasa na kumuishia yeye
Ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote

Hakuna maoni: