Andiko : Zaburi 94:1-3
“1. Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi,
uangaze, 2. Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao. 3.
Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia?
Utangulizi:
Je wewe umewahi kuona watu
wakidhulumiwa? Umewahi kuona mahali haki haitendeki? Je hujawahi hata kusikia
mahali watu wakionewa, wakiteswa, wajane na yatima na hata wageni au wakimbizi
na wanyonge wakikandamizwa na kuonelewa huku wale wanaofanya dhuluma
wakishangilia na kufurahi? Na hata wakidharau kuweko kwa Mungu na utetezi wake?
Jambo hili ndio hali halisi
katika zaburi hii iliyoandikwa na Daudi, Hatuwezi kujua kuwa Daudi wakati huu
alikuwa ameshuhudia nini katika mazingira yake, lakini kile anachokizungumza na
kukililia katika zaburi hii kinafunua wazi aidha jambo ambalo amelishuhudia
katika uzoefu wake wa maisha ama limewahi kumkuta, vyovyote vile iwavyo maswala
haya yanaikumba hata jamii inayotuzunguka leo na Biblia hapa kupitia kinywa cha
Mfalme Daudi ambaye pia Roho wa Kinabii alikaa ndani yake kuna mswala kadhaa
muhimu ya kujifunza ambayo tutajifunza katika vipengele vifuatavyo:-
·
Kumuita Bwana kwaajili ya Haki (Zaburi ya 94:1-4)
·
Kushitaki kile wanachikifanya wadhalimu (Zaburi 94:5-7)
·
Kushangazwa na ujinga wa wadhalimu (Zaburi 94:8-11)
·
Baraka za kupitia katika magumu (Zaburi 94:12-13, 14-15)
·
Hatima ya kucheza na mwenye haki (Zaburi 94:16-23)
Kumuita Bwana kwaajili ya Haki (Zaburi ya
94:1-4)
Daudi anaiimba Zaburi hii katika
mtazamo wa watu wanaoonewa, wanoteswa na kudhulumiwa na kutokutendewa haki watu
hao wakimuangalia Mungu kama Jaji mkuu mwenye uwezo wa kutoa hukumu ya mwisho,
wakati wengine wote wameshindwa kutoa msaada, Daudi anamuonyesha Mungu kuwa
ndio mahakama ya juu zaidi tunayoweza kukata rufaa na tena mahakama hii ya juu
zaidi inauwezo wa kutulipia Kisasi, Daudi anamtaka Mungu huyu mwenye uwezo wa
kulipiza kisasi dhidi ya maadui zetu
aangaze, yaani aangalie kila kinachofanyika na kutoa haki
Wewe na mimi tumewahi kushuhudia
kile ambacho Daudi alikishuhudia na kukililia katika Zaburi hii, inawezekana
umewahi kushuhudia mume akifariki na kuacha mjane na yatima na Ndugu wa Mume
wakiingilia kati na kudhulumu mali za yatima na kumuacha mjane huyo akiwa
mikono mitupu wakiishi maisha ya dhiki, tumewahi kushuhudia wanawake wakorofi
wakipora mali za waume zao na kujimilikisha, ndugu jamaa na hata watoto
wakigombea hati za viwanja, kadi za magari, watu wakichongeana makazini na
kusababisha wenngine wafukuzwe kazi, na kushangilia mafanikio ya anguko la
mwingine, watu wakichafuana kwa faida na maslahi yao wenyewe na hila za aina
nyingi zikifanyika duniani zinazofanana na hayo
Biblia inatufundisha kuwa endapo
tumezulumiwa kila tunachokistahili na hakuna wa kututetea pako mahali ambapo
tunaweza kudai haki zetu, Yesu alifundisha kwa msisitizo kuhusu madai ya haki
zetu kwa Jaji mkuu wa majaji wote duniani, Mfalme wa wafalme mwenye uwezo sio
tu wa kutoa haki bali pia kulipiza kisasi kwa watakaotudhulumu
Luka 18: 1-8 “1. Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu
sikuzote, wala wasikate tamaa. 2. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani,
hamchi Mungu, wala hajali watu. 3. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke
mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. 4. Naye
kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala
sijali watu, 5. lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake,
asije akanichosha kwa kunijia daima. 6. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule
kadhi dhalimu. 7. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia
mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? 8. Nawaambia, atawapatia haki upesi;”
Daudi anamuomba Mungu haki iweze
kupatikana, Yesu anatufundisha kuendelea Kumuomba Mungu mpaka haki yetu iweze
kupatikana Yeye ni Jaji mkuu, ni Hakimu wa Dunia nzima, tunaweza kuimuendea
yeye kwa ujasiri atupatie haki yetu, hatuhitaji kulalamika Yuko Mungu wa kisasi
mwenye kuihukumu inchi na kuwapa stahili zao wenye kiburi, Yeye atawahukumu
watu wote na pia ndiye mwenye kulipiza kisasi kwa wadhalimu na ndiye anayeteua
majaji Warumi 13:4
Biblia inatufundisha kuwa
tunapodhulumiwa tumuombe Mungu na kumsihi aangazie kile kinachoendelea,
Hatupaswi kutumia njia yoyote ile yenye kutaka kujilipia kisasi wenyewe ni
muhimu kumuachia Mungu yeye ndiye atakayetulipia kisasi.
Warumi
12:19 “Wapenzi,
Msijilipizie kisasi, Bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa Kisasi
ni juu yangu mimi nitalipa anena Bwana”
Kushitaki kile wanachikifanya wadhalimu (Zaburi 94:5-7)
Daudi mwandishi wa Zaburi
anaendelea kumwambia Mungu kilie wanachokifanya wadhalimu, wote tunajua kuwa
Mungu anafahamu kila kinachoendelea lakini Daudi anataka kufafanua, kuchamganua
kile ambacho ameona kinaendelea na anataka Mungu akiangazie
“5. Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa
urithi wako; 6. Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima. 7. Nao husema,
Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.”
Daudi anaelezea jinsi sifa ya wadhalimu hao walivyo,
hawana huruma, wana kiburi na wanazungumza kwa kejeli na kiburi cha hali ya
juu, hawajali hata kile wanachokizungumza, wanazungumza vibaya na wengine, sio
watu wa dini wala hawamjali Mungu, wanajiamini wanajitegemea, wanavunja watu
mioyo, wanagawa watu, wanawaua watu,hawajali huyu mjana wala yatima,
wanajisemesha kuwa nani atatwatetea nani atawaokoa na uwezo walio nao ni
makatili, hawajali wageni wala wakimbizi, Daudi aliwasoma vema maadui hawa na
kuwaona jinsi walivyo wabaya na wakatili na alieleza Moyo wake kwa Mungu
kuwahusu, wako watu Duniani ni wabaya na hawana haya unaweza kujiuliza ni roho
ya namna gani waliyonayo na usipate majibu kwamba wanaongozwa na ibilisi au
vipi wakati mwingine unaweza kuona ukatiliwao unazidi hata ule wa ibilisi
mwenyewe Mungu atulinde na watu wa aina hii
Kushangazwa na ujinga wa wadhalimu (Zaburi 94:8-11)
“8. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini;
Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? 9. Aliyelitia sikio mahali pake
asisikie? Aliyelifanya jicho asione? 10.
Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue? 11. Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni
ubatili.”
Daudi anashangwazwa na jinsi
wadhalumu hao walivyojawa na roho ya udanganyifu wanafanya uovu mkubwa kwa
kujiamini kiasi cha kupofuka macho na kuwa wajinga na wasiofikiri wala kuwa na
akili Daudi anauzoefu kuwa Mungu Jaji mkuu atafanya kitu haiwezekani Yeye
aliyemuumba mwanadamu awe na sikio kisha yeye mwenyewe asisikie, Yeye
aliyemuumba mwanadamu kuwa na jicho kisha asiione yanayotendeka, yeye
anayeshikisha watu adabu asikemee udhalimu unaoendelea, yeye anayewafundisha
wanadamu sheria na jinsi iwapaswavyo kuenenda asijue uharibifu unaoendelea,
anahitimisha kuwa Mungu anayajua mawazo ya wanadamu na anatambua kuwa ni ya
ubatili
Wako watu wameharibika mioyo
kiasi cha kutokutambua kuwa yuko Mungu anayeona na kusikia, wako watu wanafanya
uovu kana kwamba wao ndio Miungu na hakuna awaye yote aliye juu yao, Daudi
anasema huu ni ujinga wa watu na unaweza kufanywa na watu wasiofikiri, tena
anawaita wapumbavu na anajiuliza ni lini watakapopata akili
Baraka za kupitia katika magumu (Zaburi 94:12-13, 14-15)
12. Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na
kumfundisha kwa sheria yako; 13. Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye
haki atakapochimbiwa shimo.14. Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala
hutauacha urithi wake, 15. Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu
wa moyo wataifuata.
Daudi anatumia mistari hii
kumuita heri mtu anayepitia katika majaribu kwake yeye kupitia katika hali
ngumu ni kuadibishwa na Mungu ni kufundishwa sheria na kanuni za Mungu na kuwa
hatima ya Mungu ni kuja kutupa starehe wakati wa mabaya na kuwa mwisho wa adui upon
a tutawaona adui zetu wakizikwa wakichimbiwa shimo, Daudi aonyesha ya kuwa
Mungu hatawatupa watu wake hawezi kutuacha maana kila anayemcha yeye ni urithi
wake, ana uhakika kuwa Mungu atafanya hukumu atarejea na haki itapatikana na waliowanyofu wa moyo
watanufaika nayo
Dhuluma zinazoendelea Duniani
hazitadumu, uko wakati Mungu atakomesha , atahukumu kwa haki na kuwasterehesha
wote walioonewa na mwisho wa wabaya tutauona Ndugu yangu kama asemavyo Daudi na
kama lisemavyo neno la Mungu Bwana hatawatupa watu wake hawezi kuuachia Urithi
wake
Hatima ya kucheza na mwenye haki (Zaburi 94:16-23)
16. Ni nani atakayesimama Kwa
ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu? 17.
Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye
kimya. 18. Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako
zilinitegemeza. 19. Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako
zaifurahisha roho yangu. 20. Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe,
Kitungacho madhara kwa njia ya sheria? 21. Huishambulia nafsi yake mwenye haki,
Na kuihukumu damu isiyo na hatia. 22. Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na
Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia. 23. Naye atawarudishia uovu wao,
Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza
Mwandishi wa zaburi anahitimisha
kwa kuuliza swali nani atasimama kunitetea dhidi ya adui zangu? Na ni
atanisaidia dhidi ya waovu au wadhalimu? Kisha anaonyesha kuwa Bwana ni Msaada
na kama asingelikuwa msaada waovu waneipoteza nafsi yake, Lakini fadhili za
Bwana ni njema na zilimtegemeza Mungu alifanyika faraja kubwa pamoja na udhalimu wanaoufanya Mungu
akikimbiliwa anakuwa mwamba na atawarudisha waovu hawezi kukaa nao kiti kimoja
atawaangamiza katika ubaya wao na hakika atawaangamiza
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu
anaona kila aina ya uonevu unaoendelea katika ulimwengu, inatupasa kukata rufaa
na kudai haki zetu kwa dua sala na maombi, Mungu atatutetea, ataingilia kati
jambo kubwa la msingi ni kumwambia mlipiza kisasi aangaze Tumuombe Mungu wa
kisasi aangaze amulike aangalkie aone atazame na kukemea kila aina ya ubaya ,
uovu na udhalimu wa watu walioota sugu
walioharibika mioyo wasiojali wanaodhulumu, wanaoibia watu wakidhani kuwa
hakuna utetezi dhidi ya wanyonge Bwana ana aliangalie jambo hilo na kulikemea
Katika Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!
+255718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni