Jumanne, 18 Aprili 2017

Malaika wa Pasaka!



Mstari wa Msingi: Marko 16:1-8, Mathayo 28:1-10

Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia. Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari.  Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.


              
Utangulizi:

Inaonekana wazi wakati wote Mungu anapokuwa na Tangazo muhimu sana kwa wanadamu, hutuma ujumbe wake kupitia Malaika, wakati mwingine Malaika wa habari muhimu alijitambulisha kwa jina na wakati mwingine Hakujitambulisha, vyovyote vile iwavyo malaika hao walileta ujumbe Muhimu kwa wanadamu mfano:- 

·         Mungu alituma Malaika kutangaza kuzaliwa kwa Samson Waamuzi 13
·         Mungu alituma Malaika kutangaza kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji Luka 1
·         Mungu alituma Malaika kutangaza kuzaliwa kwa Yesu Kristo Luka 2:8-11
·         Mungu alituma Malaika kushughulika na tatizo la Sodoma na Gomora Mwanzo 19
·         Mungu alimtuma Malaika wa Pasaka wakati wa Ukombozi wa wana wa Israel Misri 12:29

·     Na Mara hii Yesu anapofufuka Malaika wa Pasaka anakuja tena akiwa na ujumbe mzito ambao tutachukua Muda kuutafakari leo.

Malaika wa Pasaka anawatokea kinamama walikuja Kaburini wakiwa wamekata tamaa na wenye fadhaa kubwa sana, walitoka wakiwa hawajua hata ni nani atakayewaondolea jiwe waendelee na kazi ya kupaka mafuta mwili wa Yesu, lilikuwa ni jambo la hatari na lenye kuogopesha mno, lakini Malaika wa Pasaka alikuwa na ujumbe muhimu sana 

1.       Aliwaambia Msiogope.
Inawezekana kina mama waliokwenda Kaburini walishituka zaidi walipoona kijana huyu mwenye mavazi meupe, na waliogopa mno lakini ujumbe wa kwanza wanaoupokea kutoka kwa malaika wa pasaka ni kutokuogopa Mungu wakati wote anataka watu wake wasiogope na wawe na amani, wakati wote haijalishi tunazungukwa na mazingira ya namna gani, Malaika hakutaka kina mama na dunia nzima kwa ujumla itawaliwe na Hofu, hofu ni adui mkuu wa amani, kila mtu anayesheherekea Pasaka anapaswa kuwa Mbali na Hofu, Kama mauti ilimpata Yesu Kristo naye amefufuka hatupaswi kuogopa tena Milele Ufunuo 1:17-18, 2Timotheo 1:3, 8, Dunia ya leo imejawa na Hofu, Huko Syria hivi Karibuni Marekani imepiga Bomu kubwa sana kubwa mno, hali ya hofu inaongezeka , Hapa nchini kule Pwani Polisi kumi wameuawa ambao ni walizni wa amani nchini hii inaongeza Hofu, Kule Korea Kaskazini na Marekani wamekuwa na mikwara ya kustaajabisha wakitaka kupigana hali hizi zote zinaoneza hofu duniani na kuifanya Dunia isiwe mahali pa Amani ni lazima jitihada zifanyike katika kuhakikisha Amani inatawala Duniani na watu wanaondoka katika maisha ya hofu.

2.       Amefufuka Katika wafu.
Malaika anataka kuthibitisha kuwa Yesu alisulubiwa, na alikufa na kuwa amefufuka maana yake yu hai, Ufunuo 1:17-18 Yesu yu Hai milele na milele, kama kuna jambo ambalo shetani hapendi kulisikia ni ushahidi ulio wazi kuwa Yesu amefufuka, hii ndio tofauti yake na waanzilishi wote wa dini na falsafa mbalimbali duniani, wote waliandika historian a wakapita sivyo ilivyo kweke Yesu Kristo yeye yuko hai milele, ulikuwa ni ujumbe wa kutia moyo kwa kina mama hawa walikuwa wamenunua mafuta ya kuupaka mwili wa Yesu usizoe, aendelee kuwepokuwepo kaburini, Lakini Neno la malaika lilikuja kuondoa mashaka kwao na kuwajulisha kuwa hata mafuta yenu ya kumpaka Merehemu hayana kazi tena huyu mwanamume yu hai.Aidha malaika alikuwa amewakumbusha Maneno aliyoyasema Yesu kuwa atafufuka hii maana yake ni kuwa Yesu aliitimiza ahadi, viongozi wazuri ni wale wanaotimiza ahadi zao mara baada ya Uchaguzi kama ilivyo kwa Pombe Joseph Magufuli anatimiza ahadi nyingi sana alizowaahidi watanzania, lakini nitoe wito kwake kuendelea kudhibiti mfumo wa Bei ya chakula kwani imepanda mmno na kipato cha watanzania hakitoshelezi katika kukabiliana na kupanda kwa unga na vyakula vinginevyo.

3.       Hayuko Hapa
Malaika aliwaambia wanawake hawa wawe watalii wa kwanza wa kulitembelea Kaburi la Yesu lililotupu, aliwaambia Patazameni mahali walipomuweka, hata leo unaweza kwenda kupatazama mahali walipomuweka Hayupo tena, yuko Hai, Kaburi lake ni ushahidi wazi hata leo kuwa Yesu Kristo amefufuka na tayari yuko busy na majukumu ya kutuombea kama kuhani mkuu

4.       Nendeni Mkwawaambie wanafunzi wake na Petro
Habari njema kwa wanafunzi wote wa Yesu. Lakini pia maalumu kwa Petro, Petro na Yesu walikuwa tayari wameachana pabaya Petro alikuwa tayari amemkana Yesu Mara tatu wakati anasulubiwa Malaika ametumwa kulete ujumbe wa ufufuo kwa wanafunzi wote wa Yesu na maalumu kwa Petro pia, Mungu alitaka kuthibitisha kuwa ameshamsamehe Petro kabisa na kuwa sasa ana uhusiano naye mkubwa na wa kipekee zaidi, Habari njema za ufufuo zinawagusa hata wale ambao walikuwa wamemkana Yesu, Yesu kipakee anaonyesha kuhusika na rafiki zake wote na hata wale waliomkataa kivitendo na kwa kiapo

Malaika alikuwa na ujumbe uliobeba Kuondoa Hofu, Kuleta Matumaini, Msamaha na uthibitisho kuwa tutamuona Yesu aliyefufuka, Kila kiongozi wa kisiasa kuanzia ngazi ya kata anapaswa kuhakikisha wanainchi wanaishi mbali na Hofu, tuache kuwatisha wanainchi, Lazima kila kiongozi alete habari za matumaini na kututhibitishia hali halisi ya tumaini hilo Yesu alikuwa ni kiongozi aliyetoka tunmaini na alilithibitisha, aliposema yeye ni ufufuo na uzima alifuua wafu lakini pia alifufuka kwelikweli, aliweza kusamehe na kuwahesabu wale waliomkosea kama rafiki maalumu na sio maadui zake, viongozi wa leo hawapaswi kujenga hali ya uadui na raia wake, ahadi zake zilikuwa za kweli hakutoa matumaini hewa.

Na mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: