Mji uliochongwa katika Mwamba huko Jordan unajulikana kama mji wa Petra yaani Mwamba
Utangulizi:
Ilikuwa mwaka wa 1763 wakati
Mchungaji Rev.Augustus Montague Toplady,
Muhubiri wa Injili kutoka kijiji cha Blagdon Huko Mendip Hill Uingereza,
alipokuwa akisafiri kwa shughuli za injili, alikumbwa na dhoruba kali sana
njiani alijaribu kutafuta hifadhi katika moja ya miamba na kufanikiwa kuwa salama
na ndipo baadaye alitunga wimbo MWAMBA
WENYE IMARA au MWAMBA ULIOPASUKA
ambao ni moja ya nyimbo kuu na za Muhimu sana kwa waanglikan na umekuwa maarufu
katika tenzi za rohoni namba 58 na nyimbo za injili 30, wimbo huu ulichapishwa
kwa mara ya kwanza mwaka 1775 na gazeti moja la injili lililojulikana kama The
gospel Magazine. Wimbo ulipendwa sana na Prince Albert ambaye aliagiza wimbo
huo upigwe siku atakapokufa na ndipo ukawa maarufu sana wakati wa misiba hata
ingawaje wimbo huu unamzunguzia Yesu kama Mwamba.
Mwamba wenye imara,
Kwako nitajificha,
Maji hayo na damu,
Yaliyotoka humu,
Hunisafi na
dhambi,
Hunifanya mshindi.
Kwa kazi zote pia,
Sitimizi sheria,
Nijapofanya bidii,
Nikilia na kudhii,
Hayaishi makosa,
Ndiwe wa kuokoa.
Sina cha mkononi,
Naja msalabani,
nili tupu, Nivike,
Ni mnyonge,
nishike,
Nili mchafu naja,
Nioshe nisijafa.
Nikungojapo chini,
Na kwenda
kaburini,
Nipaapo mbinguni,
Na kukwona enzini,
Roho yangu na iwe,
Rahani mwako wewe.
Mtunzi wa wimbo huu aliokoa
maisha yake katika mwamba! Na kwa vile alikuwa muhubiri alielewa wazi kuwa
Mwamba ulimwakilisha Yesu Kristo, Katika majira haya ya Pasaka ni muhimu kwetu
kurudi katika maandiko na kutafakari kwa kina kwa nini Yesu anaitwa Mwamba?
Watakatifu waliotutangulia walimfananisha Mungu na mwamba.
Biblia inamtaja wazi Mungu wetu
kuwa ni Mwamba wa wokovu wetu
1. Zaburi ya 18:2 Bwana
ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu
ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
2. Zaburi ya 62:1-2 Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu
hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu
na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.
3. Zaburi ya 95: 1 Njoni, tumwimbie Bwana, Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Neno mwamba katika Biblia ya
Kiebrania linatajwa kwa maneno makuu mawili yaani TSUR ambalo maana yake ni gema au pande kubwa la jiwe, na neno
lingine ni SELA ambalo maana yake ni
mlima au Jabali au ngome ya Jiwe, Kiyunani ni Peter na Petra
Kwa hivyo Biblia inapomtaja
Kristo kama Mwamba inamaanisha SELA
au PETRA Kila mmoja wetu anaweza
kujua ujasiri anaojisikia akiwa juu ya mwamba unapokuwa juu ya mwamba au juu ya
jabali unaweza kukaa kwa ujasiri, unaweza kurukaruka na hakuna wa kukubabaisha,
mwamba huwa hautikisiki, haung’oki, hauogopi dhoruba na kama mtu atashindana na
mwamba atavunjika vunjika na kama mtu ataangukiwa na mwamba atasagwasagwa!
Hakuna njia nyingine yoyote
ambayo kwa hiyo tunaweza kuwa salama isipokuwa kumtegemea Yesu tu mtuni wa
wimbo alionyesha kuwa ni kwa Damu yake yesu tu tunaweza kuwa salama, kwake
tunaweza kujificha na kuutegemea ushidni, kazi njema , na matendo mema hayawezi
kutuokoa ni zawadi ya Yesu Kristo pekee aliyekufa msalabani kwaajili yetu ndio
inayoweza kututhibitishia usalama wetu, kwa jambo lolote lile ni lazima tuweke
tegemeo letu kwa Bwana Yesu
Tunaweza kukutana na dhuruba za
aina mbalimbali zenye kuhuzunisha Magonjwa na mateso, Matatizo ya kifedha na
kiuchumi, Matatizo ya kifamilia, Huzuni na kukata tamaa jambo kubwa na la
msingi la kufanya ni kumwangalia Yesu ni kumtegemea ni kujificha kwake yeye
ndio nguvu yetu, na kimbilio letu ndiye mwamba imara
Yeye aliahidi kuwa atalijenga
kanisa lake juu ya mwamba na wala malango ya kuzimu hayatalishinda, ushindi ni
wetu kama tu tutajificha na kuutegemea Mwamba.
Mathayo 16: 13-18 “Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza
wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema,
Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo
wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena
mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu
akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia,
Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali
Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba
huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni