Ijumaa, 28 Aprili 2017

Kazi za Roho Mtakatifu katika Kanisa!


Andiko la Msingi: Matendo 1:8Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”


 Hii hapo juu ni picha (symbol) ya Roho Mtakatifu na sio Roho Mtakatifu

Utangulizi.

Hali ya kanisa la leo imekuwa dhaifu kuliko Nyakati za kanisa la Kwanza, Kanisa lilikusudiwa na Mungu kuwa Chombo kikuuu cha ukombozi wa wanadamu Baada ya kazi njema iliyofanywa na Yesu Msalabani, Mungu analitegemea kanisa kuwa kama Waamuzi, watetezi, wakombozi, makuhani, wafalme na askari wa mstari wa mbele katika kuwatetea wanyonge, walioonewa na waliosetwa katika vifungo vya Ibilisi, na kukemea uovu, kuikosoa serikali na kuonyesha njia kwa ulimwengu!

Luka 4: 18-19Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Kanisa lilipaswa kufanya kazi hizo alkizozitaja Yesu na kuzitabiri Isaya hapo Juu, ikiwa Roho wa Mungu yuko juu yetu, ikiwa ametupaka Mafuta, lakini jiulize leo hii je kazi zinazofanywa na kanisa ndizo hizo hapo juu? Leo kanisa limejaa watu wengi wenye Stresses yaani migandamizo, lina watu wengi wasio waaminifu bila kujali kuwa wako ngazi gani za kiroho, yale ambayo zamani tulikuwa tunayaona na kuyashuhudia yakifanywa na watu tuliowaita Mataifa watu wasiomjua Mungu, tuliokuwa tukiwalilia waokolewe, wamjue Mungu wamgeukie Mungu sasa ndio yanafanywa na Kanisa, Je ni mara ngapi kanisa limekaa kimya watu wanapoonewa, Mauaji yanapotokea Duniani, vita vinavyoendelea, matishio ya umwagikaji wa damu na dhuluma za kila aina je leo ni nani anaifanya kazi hii? Nani anasimamia haki za binadamu zinazoendana sawa na Neno la Mungu? Kwa nini tumefikia hapa tulipofikia? Kuna na mambo mengi sana sitaki kuyazungumza hapa lakini wewe unayajua kuhusu hali ya kanisa la leo! Ni ya kushangaza, ni kweli ziko huduma za kinabii na mitume na miujiza ambayo inatendeka na najua inatendeka kwa nguvu za Roho Mtakatifu, lakini je uadilifu? Uko? Je Hakuna ulevi, uongo, picha za ngono, chuki, uadui, uchawi, ushirikina, masengenyo, uasherati na zinaa, je hatutoi muda mwingi kwa simu zetu, tablets, na laptop, zaidi kuliko kwa Mungu na familia zetu, hali ni mbaya mno sasa, Turudi kukazia kazi za Roho Mtakatifu ndani ya kanisa, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

1.       Roho Mtakatifu ni Nani?

2.       Kazi za Roho Mtakatifu Katika ya Kanisa

Roho Mtakatifu Ni nani?

Katika Maandiko Roho Mtakatifu anaelezewa vema kama Nafsi kamili  inayojitegemea yeye ni BWANA yaani ni Mungu 2Wakoritho 3:17-18 17. Basi 'Bwana' ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, Waebrania  9:14 Roho Mtakatifu ni wa Milele tunaelezwa katika maandiko “basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?” kuwepo milele ni sifa ya uungu, 1Petro 1:2, Roho Mtakatifu ni Mungu kama ilivyo kwa Baba na Mwana kwa msingi huo hatupaswi kumfikiri Roho mtakatifu kama nguvu tu au hamasa Fulani, ana sifa za nafsi anafikiri, Warumi 8:27 ana hisia Warumi 15:30 ana maamuzi 1Wakoritho 12:11 na ana uwezowa kupenda na kufurahia ushirika , alitumwa na Mungu Baba kuleta uwepo wa kiungu kwa washirika ili tufurahie ushirika wetu na Kristo Yohana 14:16-18,26, kwaajili ya hayo Kanisa linapaswa kukumbuka kuwa Roho ni Mungu na ni nafsi na nilazima tuhakikisha anaunganishwa mioyoni mwetu, na kuwa anastahili kuabudiwa kupendwa na kusikilizwa Marko 1:11

Kazi za Roho Mtakatifu katika Kanisa.

1.       Yeye ndio njia ya wokovu anayetushawishi kwa habari ya haki dhambi na hukumu Yohana 16:7-8 Sasa basi ni vigumu kwa kanisa kujisikia hukumu na kufa kwa dhamiri kama Roho Mtakatifu hapewi nafasi ya kutosha katika kuifanya kazi ya kutuhukumu kwa habari ya dhambi, kutuonyesha kuna hukumu kubwa ijayo endapo hatutatubu na kutushuhudia namna ya kutenda haki.
2.       Anafunua kweli kuhusu Kristo Yohana 14:16,26,
3.       Anatuzaa kwa upya Yohana 3:3-6
4.       Anatufanya washirika wa mwili wa Kristo 1Wakoritho 12:13
5.       Anatutakasa  Warumi 8:9, IWakoritho 6:19
6.       Anatuthibitishia kuwa sisi ni wana wa Mungu Warumi 8:16
7.       Anatusaidia katika kuabudu Matendo 8:26-27
8.       Anatufanya tumtukuze Yesu Kristo Wagalatia 5:22-23,1Petro
9.       Anazalisha neema ya Kristo inayotufanya tuwe na sifa zinazomtukuza Kristo Wagalatia 5:22-23, 1Petro 1:2
10.   Ni Mwalimu  na hutuongoza katika kweli yote  Yohana 16: 13, 14:26, 1Wakoritho 2:9-16
11.   Aanamfunua Yesu kwetu na kutuongoza katika kuwa na ushirika na Yeye Yohana 14:16-18,16:14
12.   Anapanda upendo wa Mungu siku zote ndani yetu  Warumi 5:5
13.   Anatupa Furaha faraja na msaada Yohana 14:16, 1Thesalonike 1:6
14.   Ni njia ya huduma na hututia nguvu kwaajili ya huduma, shuhuda na utangazaji wa Neno la Mungu Matendo 1:8, 4:31 na hutenda miujiza Matendo 2:43;3:2-8, 5:15, 6:8, 10:38
15.   Anatoa Karama za Roho kwa kusudi la kulijenga Kanisa 1Wakoritho 12-14
16.   Analijenga Kanisa Waefeso 2:22, anatia moyo kuabudu Wafilipi 3:3
17.   Anaongoza katika Umisheni Matendo 13:2, anateua waamini Matendo 20:28
18.   Anapaka Mafuta watumishi Matendo 2:4 1Wakoritho 2:4
 
Hitimisho!
Kama ikiwa Roho wa Mungu hufanya kazi hizo zote kanisa halipaswi kumdharau, upungufu mkubwa unaolikumba kanisa la leo unatokana na sababu tu za kumzimisha Roho Mtakatifu, Ni lazima kanisa limpe Roho Mtakatifu kipaumbele kama linataka kuwa hai nnapozungumza kanisa namaanisha kila mtu aliyeokolewa anayemwamini Yesu anapaswa kuzingatia haya ili Kazi za Mungu ziweze kufanyikakatika kiwango ambacho Mungu amekikusudia na sio chini ya kiwango.

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote. 0718990796

Maoni 2 :

Unknown alisema ...

Barikiwa Sana

Bila jina alisema ...

Amina endelea kuelimisha jamii