Jumatatu, 21 Agosti 2017

Kurudi nyuma kwao wajinga kutawauwa!


Mstari wa Msingi. Mithali 1:32-33 Biblia mahali hapo inasema;-

Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.”

Ni muhimu kuwa na ufahamu kuwa sio wakristo wote wanaopata neema ya kuzaliwa mara ya pili au kuokoka wanapata neema vilevile ya kuukulia wokovu, wengine wanarudi nyuma na hata kufa kiroho kutokana na sababu mbalimbali, wote tunafahamu kuwa ziko sababu mbalimbali za kwanini, watu  wanarudi nyuma na hatimaye kufa kiroho, lakini katika somo hili tutajaribu kuchambua chache kati ya hizo.

 
Hatari ya maisha ya upotevuni, tafadhali baki nyumbani rudi nyumbani



1.       KUKOSA MISINGI AU MIZIZI. 

Luka 8: 13 Biblia inasema Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga.” Ni muhimu kufahamu kuwa mara baada ya kuokolewa kila mtu aliyeokoka anapaswa kuhakikisha kuwa analifanyia kazi neno la Mungu na kujijengea juu ya msingi huu, kila mmoja anapaswa kuota mizizi na sio tu kuota lakini kuhakikisha kuwa mizizi yake inashuka chini sana, tatizo kuu la wakristo wengi sana wako katika kundi hili linalotajwa na Yesu Kristo kama watu au mioyo inayolipokea neno la Mungu kwa furaha lakini hawana mizizi, hawaendelei mbele wanadumaa na hatimaye kuiacha imani, Hawa pia wanaweza kufananishwa na mtu aliyejenga nyumba yake kwenye Mchanga Mathayo 7:24-27 “.Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.” Unaweza kuona tatizo kubwa la wapendwa wengi sio tu kulitendea kazi neno lakini hata kulielewa hawalielewi,wako wakristo ambao hata hawajui kwanini wanatoa sadaka, kwa nini wanahudhuria ibada katika kanisa wanalohudhuria, kwa nini wanaomba, kwa nini wanene kwa lugha? Na wakikutana na changamoto ndogo tu wanakwazika na kuchanganyikiwa, Hwawezi kuitetea imani, Hawana ujuzi wala uzoefu katika kutembea na Mungu ni wakristo ambao hawawezi kusema Mungu amezungumza name na wakikusikia kuwa unasema umezungumza na Mungu wanashangaa, hawana ushuhuda wao wenyewe.

Mkristo mwenye Misingi imara anapaswa kusimama mwenyewe haijalishi hata kama mtu aliyekuingiza katika ukristo amehama imani na kujiunga na imani potofu, yeye anaendelea kusimama kwa gharama yoyote, wazazi ndugu jamaa au rafiki wa karibu hawezi kubadilisha msimamo wa mtu mwenye mizizi, utashangaa kuona mtu aliyeokoka hajui hata tofauti ya Mashahidi wa Yehova na hata wasabato yeye kila aina ya fundisho na imani na kila aina ya upepo wa Elimu unamzoa tu!

Mkristo mwenye mizizi kamwe hawezi kuyumbishwa na jaribu la aina yoyote,taarifa mbaya kuhusu kiongozi wako wa kidini haiwezi kuwa sababu yaw ewe kuiacha imani, unaweza kuwepo kanisani lakini kama mimani yako haijajengwa kwenye misingi na haijaota mizizi ni rahisi kujikuta matatani, Dhambi za kiongozi wako wa kidini zinauhusiano gani na wokovu wako?uwapo duniani je unafikiri unaweza kumuacha Yesu kwa sababu ya dhambi ya kiongozi wako?mkristo anayeweza kumuacha Yesu kwa sababu ya tatizo la mtumwingine huyo hana misingi wala hajaota mizizi hajakomaa.

Mkristo aliyesimama vema ni yule ambaye amesimama hawezi kutikiswa na kurudi nyuma kwa wengine Yohana 6:66-69Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” 

Wanafunzi wa Yesu wenye msimamo kama Petro hawakuweza kuacha kuandamana na Yesu kwa sababu walitambua kuwa Yesu anao uzima wa milele, Mtu ambaye hajajengwa kwenye msingi na hana mizizi kwake ni rahisi kukata tamaa, ni vigumu kwake kupokea neno gumu na kusonga mbele kwao ni rahisi kukwazika tu na kungung’unika na kurudi nyuma Biblia haitutii moyo kumfuata kiongozi awaye yote anapokuwa amekengeuka badala yake inatutia moyo kumfuata Yesu au kumfuata kiongozi kama anamfuata Yesu pale anapokengeuka sisi tunasonga mbele na Yesu tu, tukimuombea yeye au kumuacha na ukengeufu wake Paulo mtume alisema tumfuate yeye kama anavyomfuata Kristo 1Wakoritho 11:1Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.” Ukiwa kiongozi wa kiroho ni rahisi sana washirika wako kukutii katika jambo lolote utakalowaamuru, wanakutii wanakuheshimu wanakusikiliza, lakini ni muhimu kuwafundisha washirika wetu kumfuata Yesu na sio mtu au dhehebu, wengi tumewaharibu washirika katika makanisa kwa sababu ya kuwaaminisha katika Dhehebu na katika mtu, badala ya Yesu na kuwafanya kuwa wanafunzi wa neno la Mungu, sisi watumishi wa Mungu ni binadamu na tunauwezekano mkubwa sana wa kufanya dhambi tena kubwa na za aibu tu, hivyo ni lazima ieleweke wazi kuwa kama tutawaambia washirika wetu kutenda jambo ambalo sio la kibiblia basi wawe na uwezo wa kusema hapana kubwa, na kama tutafundisha fundiso lisilo la kibiblia pia wawe na uwezo wa kutuambia Mchungaji, Mwinjilisti, Nabii, Mtume, Mwalimu na kadhalika je hili fundisho ni la msingi wa kibiblia?

Pasipo kuwajenga washirika katika kuwa wanafunzi wa Yesu kumepelekea baadhi ya watumishi wanafikia ngazi hata ya kuoga na mshirika kwa madai kuwa ni oga takatifu, wengine wameweza kuwaibia wakristo mali zao zote kwa kisingizio cha kumtolea Bwana, haya na mauchafu mengine mengi yanaweza kufanyika kwa sababu wakristo wengi wamedumaa kiroho na hawataki kujijenga juu ya msingi na kuota mizizi mikali katikia imani hivyo wanazolewa na kila mbwembwe za kila upepo wa kila elimu hata zile zisizo na uungu ndani yake!

Nikwa sababu kama Hizi Paulo alisema mnifuate mimi kama ninavyomfuata Kristo hii ni kwa sababu Paulo mtume alikuwa na uhakika wa mwenedo na tabia yake katika Kristo, alikuwa mwaminifu, wakristo ni lazima wajifunze neno la Mungu na kuwa na mizizi na kuwa ma misingi imara ya kutokuyumbishwa na aina yoyote ya ukiroho wa mtu, kumbuka kuwa kiongozi wa ngazi yoyote ya kiroho anaweza kukengeuka na kurudi nyuma, Je hatusomi katika maandiko kuwa Haruni aliruhusu makutano kuabudu sanamu Hapo Musa alipokuwa mlimani kuomba? Musa alipokawia mlimani je Israel wote hawakugeuka na kushindwa kusimama katika zamu yao  na kuabudu miungu ya sananu huku wakisema kuwa ndio mungu aliyewaokoa katika mikono ya Farao huko Misri? Ni wazi kuwa watu hawa walikuwa hawajajengeka katika imani, walikuwa hawana msingi na walikuwa hawana mizizi katika ujuzi wao binafsi na Mungu kumbuka kuwa Mungu si wa mkumbo, kila mmoja anapaswa kujijengea uzoefu binafsi katika kuwa na uhusiano wako na Mungu bila kufuata mkumbo.

Mtu mwenye misingi au mizizi hawezi kufuata mkumbo.

Wengi wa walioabudu sanamu Chini ya uongozi wa Haruni walikuwa ni watu waliofuata mkumbotu, wengi wa walioangamizwa jangwani walikuwa ni watu walionung’unika kwa sababu ya taarifa za wapelelezi, kumi waliokosa imani na hawakuwajali wawili waliokuwa na imanikwa Mungu, wengi pia wa waliomfuata mkumbo wakati Yesu anasulubiwa na kupiga kelele wakisema asulubiwe asulubiwe hawakuwa na msimamo wao thabiti bali walikuwa watu walifuata umati au mkumbo, kufuata mkumbo katika kutenda uovu ni tatizo kubwa sana kwa wakristo wa nyakati za leo hebu komaa kiroho, hebu kataa kudumaa, hebu kubali kuongozwa na neno na uote mzizi ya ujuzi wako mwenyewe mfanye Mungu kuwa Mungu wako na neno lake kuwa neno lako, usikubali kwenda kwa mkumbo Muombe Mungu akupe neema ya kusimama kwa miguu yako na uwe mkristo mwenye mizizi iliyozama sana chini katika imani.

2.       KUWA DEBE TUPU.

1Wakoritho 13:1Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.”
Biblia inazungumzia kuhusu debe la shaba linalolia na upatu uvumao upatu maana yake ni mwangwi,kwa ujumla biblia inazunguzmia utupu, bure kutokuwa na kitu, tunapozungumzia wakristo wenye hatari ya kurudi nyuma au ambao wamedumaa au wamesharudi nyuma inagwa wako kanisani biblia inazungumzia utupu wa kiroho, hii ni jamii ya wakristo tulionao leo makanisani bila kujali miaka yao ya wokovu, wala ngazi ya utumishi wako jambo kubwa la kujiuliza je wamejaa neno la Mungu,? Je wamejaa  Roho Mtakatifu? Wanaweza wakawa wananena kwa lugha lakini tujiulize ni nini faida yake? Je wana upendo? Wanaweza kuwa wana karama nyingi na wanatumika sana kuwaombea wengine lakini msingi wana nini katika Mungu?  Kuwa debe tupu la kiroho ni jambo la hatari sana katika maisha ya Ukristo

Shetani anapendezwa sana na nyumba iliyopambwa na kufagiliwa kisha iko tupu, unapokuwa ntupu kiroho shetani atatafuta vya kukujaza, Luka 11:24-26Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema,Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza”. 

Mkristo ambaye ni debe tupu ana maisha hatarishi shetani atatafuta kila namna ili aweze kuhakikisha kuwa anakujaza mambo yatakayokufanya uwe wa kawaida na kukurudisha nyuma, utajaa kila namna ya udunia ambayo hujawahi hata kuwa nayo kwa sababu, huna kitu, lazima mkristo awe mtu aliyejaa kitu na sio debe tupu

Matendo ya mitume 6:5a,8Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu” Unaona kumbe kama mkristo amekuwa debe tupu anakuwa na kelele tu hakuna kitu cha ziada katika maisha yake, hana imani, hajai roho, hana neema hana uwezo, wala nguvu za Mungu, wakristo ambao ni debe tupu na upatu uvumao ni wapiga kelele tu lakini hakuna kitu cha ziada maishani mwao,watapiga kelele za manunguniko, watapiga kelele za masengenyo, watapiga kelele za ugomvi, watapiga keleleza elimu zao na nchi walizotembelea lakini hawana kitu cha ziada , ni muhimu kukumbuka nini tunapaswa kukijaza katika maisha Yetu, ni lzaima tujaze neno la Mungu maishani mwetu na akilini mwetu, ni lazima tujae neema na kweli, nilazima tujae hekima ya Mungu, ni lazima tujae Roho Mtakatifu, ni lazima tujae nyimbo za injili,ni lazima tujae upendo na matendo, mema na kujaa upendo, tukatae kuwa tupu.
Kwani kinyume chake shetani atatujaza na matakwa yake na mapenzi yake.

3.       KUUPENDA ULIMWENGU.

2Timotheo 4:10Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia.” Kama mtu akikipenda kitu uko uwezekano mkubwa wa kukifuata, Dema aliupenda ulimwengu akaacha kufuatana na Paulo mtume anauendea ulimwengu, binti akimpenda kijana anaaacha wazazi wake na kuambatana na yule kijana kupenda kuna enda na nguvu ya kufuata au kuambatana

Kama ukiipenda dunia na tamaa zake, ukipenda fedha, ukipenda anasa, ukipenda wanawake au wanaume, na dunia yote kwa ujumla utavutwa na kile unachokipenda, Wakristo wanapaswa kutokuvutwa na kitu kingine nje ya Mungu, na neno lake, ni muhimu kupenda kile kilicho cha Muhimu ikiwa ni pamoja na Mungu, mkeo au mumeo na watoto nk kulingana na mapenzi ya Mungu kamwe usiruhusu aina nyingine ya upendo ulio kinyume na mapenzi ya Mungu, 1Yohana 2:15-16Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia”.

-          Kutokuipenda dunia maana yake ni nini ? kutokusahau kuwa dunia sio makazi yetu ya kudumu sisi ni wapitaji tu hatupaswi kujisahau na kufikiri tutaishi duniani milele hivyo ni lazima kuzingatia na kujiandaa kwa maandalizi ya makazi yetu ya milele mbinguni Wakolosai 3:1-2Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi” Lazima kila mkristo anayetaka kusonga mbele awe na muda wa kumtafakari Yesu Kristo, na kukumbuka kuwa kazi aliyoifanya msalabani sio ya bure, sio hilo tu lakini tunapaswa kuishi duniani kama wasafiri na sio watu wenye makazi Waebrania 11:9-10Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.”
-          Wala vilivyomo ndani yake au tamaa zake hapa biblia inazungumzia kila kinachoonekana kuwa raha katika dunia kinachoweza kutufunga ni lazima kujihadhari, hatupaswi kujitoa kwa vitu vilivyomo duniani ukilinganisha na jinsi tunavyopaswa kujitoa kwa vitu vya Mungu, kutokuutii mwili katika kila kinachohitajika nao 1Petro 2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.” 

-          Kutokufanya urafiki na waasiMtu akiipenda dunia kumpenda baba hakumo ndani yake” Yakobo 4:4 “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.” Aidha maandiko yanaonya vikali kufungiwa nira na wasioamini 2Wakoritho 6:14-18 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike

-           Aidha kupenda fedha kuliko Mungu au kuacha fedha itutawale maisha yetu, mfano tukiwa nayo na tukiwa hatuna hisia zetu zinakuwaje? 1Timotheo 6:6-10 “6. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”.

Ni hatari sana kupenda kwa tamaa, ni hatari kudharau kanuni za Mungu kwa sababu ya maswala ya ulimwengu huu, wako vijana wasichana ambao wanashauku na hamu kubwa sana ya kuolewa kiasi ambacho wako tayari kuvunja kanuni na sheria na kukubali kufanya lolote eti ili mradi waolewe, kupenda kitu kwa tamaa ni kuwa na shauku yenye nguvu kuelekea kitu hicho, ni tamaa ya kutaka kukifikia kitu hicho kwa namna isiyoweza kuzuilika tamaa ya aina hii haifugiki, watu wanaweza kufikia ngazi ya kutaka kushindana na wengine kwa sababu ya tamaa, tamaa ni shina la mabaya mengi hatuna budi kujihadhari nayo na kumpenda Mungu na kufanya kazi zetu kwa bidii kwa kadiri ya neema Mungu aliyotupa. Rafiki yangu mmoja mwimbaji wa nyimbo za Injili alikuwa akinisimulia jinsi kama mwimbaji mzuri wa nyimbo za injili na mrembo, mwenye umbile zuri, kiuno kizuri, na amejengeka kwa sifa zote za uzuri ananiambia mkuu wa wajenzi, majaribu ya kuinuliwa ni magumu sana mtu mmoja ananiambia nitakupa milioni 20 ukikubali kulala name kwa usiku mmoja tu. “I will give you 20 TZshs Million per one night of staying with me” Unaweza kuona je ungekuwa wewe ungechagua nini Hapo Fedha au Kumuacha Mungu, huu ndio ulimwengu. Ni lazima tumuombe Mungu atuokoe na tamaa za ulimwenguni katika sala ya bwana kula ile sentensi usitutie majaribuni lakini utuokoe na yule muovu hapa ndipo inapohitajika aina hii ya sala 2Petro1:4Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa”.

4.       UCHUNGU.

Waebrania 12: 14-15Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo”.

Uchungu uchungu uchungu umeharibu watu wengi sana, makanisani na kila mahali watu wameharibu mahusiano kwa sababu ya uchungu, wengine wamejitenga na kuiacha imani kwa sababu ya kufanyiwa mambo ya uchungu, wengine wamedai au kutoa talaka kwa sababu ya uchungu, wengine wameacha kazi kwa sababu ya kutendewa mambo machungu Biblia inataadharisha kuwa neema inaweza kupunguka, yaani ule uwezo wa kustahimili kwa sababu ya kutendewa machungu? Je kama Mkristo unapotendewa mambo machungu unafanya nini?  Wengine walianzisha madhehebu yao kwa sababu ya kukimbia kutendewa mambo machungu na wengine wamerudi nyuma kwa sababu ya kutendewa mambo machungu Biblia inatufundisha kuwa Yusufu alitendewa Machungu lakini kutokana na uvumilivu wake alipokea Baraka nyingi na kuwa mtawala dhidi ya ndugu zake  Mwanzo 49:22-26Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matawi yake yametanda ukutani.  Wapiga mishale walimtenda machungu, Wakamtupia, wakamwudhi, Lakini upinde wake ukakaa imara, Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye jiwe la Israeli, Naam, kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia; Kwa mibaraka ya mbinguni juu. Mibaraka ya vilindi vilivyo chini, Mibaraka ya maziwa, na ya mimba. Mibaraka ya baba yako Imepita mibaraka ya milima ya kale, Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele; Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliye mkuu kati ya ndugu zake”. Uchungu umeumiza wengi uko ushuhuda wa Pastor Dag Heward aliyeanzisha huduma yake kule Ghana anaeleza katika moja ya vitabu vyake sababu ya watu kuhama makanisa yao na kwenda kujiunga au kuanzisha mengine ni pamoja na watu kuwa na uchungu, Pastor Dag anasema wengine hawakuwahi hata kuhudhuria harusi yake ingawa aliwaalika, Nakumbuka mchungaji wangu Zacharia Kakobe wakati mwingine alikuwa akihudhuria mikutano ya wachungaji na kukaa pamoja nao alijikuta kila Mchungaji ameondoka na kuhama alipokuwa amekaa, wengi wlimuita npepo na wengine walisema anatumia nguvu za giza na wengine walimsema kuwa ni imani potofu, Niliwahi kuhudhuria kanisa moja na nilipojitambulisha kuwa mimi ni mshirika wa Full Gospel Bible Fellowship na tulipotoka ibadani hakuna mtu alinisalimia kwa mkono, wengi walikuwa wakinong’ona kuwa ametokea kanisa lenye imani potofu, je we umewahi kutendewa mambo machungu? Je umeweza kusamehe au unadhuru wengine kutokana na uchungu? Mchungaji wangu Msaidizi aliwahi kuzusha kuwa nilitaka kumbaka, na nikauhukumiwa na Askofu wangu wa jimbo kwa kutengwa miezi mitatu, ulipotimia wakati wa kufunguliwa nilimuendea Mchungaji na askofu wangu na kuomba anifungue lakini aliniambia kazi bado nakuongeza kifungo cha mwaka mmoja zaidi, ulikuwa ni wakati mgumu, nilinyimwa mshahara, familia iliteseka mke wangu aliuza maandazi, kanisa lilinipa elfu 50 tu kwa mwezi,nilipoteza haki zangu zote sikulipwa kipato chochote katika miaka tisa niliyolitumikia kanisa,  Nilijiuliza hivi kweli kuna wokovu? Hivi huu ndio Ukristo, Lakini Mungu Roho Mtakatifu aliniambia usiniache mimi nitakuwa pamoja nawe, nitakuwa ngao yako na thawabu yako kubwa sana nitakuongoza kila utakako kwenda, nilitiwa moyo tu kujua kuwa Mungu yuko name, huu ndio ulikuwa wakati rahisi kurudi nyuma, lakini misingi thabiti ya kujua neno na kujua kuwa askofu pia ni wanadamu ilinipa nguvu kusonga mbele, uchungu uchungu uchungu? Hatupaswi kurudi nyuma au kujiua kwa sababu ya uchungu badala yake na tusonge mbele, “Usimlaumu mtu yeyote katika maisha, watu wazuri watakupa furaha, watu wema watakufanya ukumbuke, watu wabaya watakupa uzoefu, na watu waovu watakufundisha adabu,” Hatuwezi kumuacha Yesu kwa sababu ya watu wabaya. Siku hizi ninauwezo wa kucheka watu wanaponitendea uchungu na kumwambia Mungu sasa kuna level gani nyingine unataka kunipeleka mzee najua una mazuri mengine zaidi hivyo ninafurahi.

5.       MAISHA YA DHAMBI.

Mfano wa mwana mpotevu ni mfano dhahiri wa mwana aliyetaka uhuru, aliyetaka kuishi kwa kujitegemea, mbali na sheria za nyumbani, mbali na kibano, mali na kupangiwa mbali na kuwaziwa, mbali na kuelekezwa,mbali na uwepo wa baba, mwana mpotevu alitaka kuwa huru kuishi maisha ya dhambi, hatuwezi kujua ushawishi huu ulitoka wapi, lakini huenda marafiki wabaya walichangia kumshauri vibaya Biblia inasema hivi Mithali 1:10Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali.” Maana yake ni kuwa kama u mcha Mungu ni muhimu kwako kuchukua hatua stahiki ya kuacha kuambatana na watu waovu wenye ushawishi, hatuwezikabisa kuhama ulimwenguni lakini ni muhimu kwako kuhakikisha kuwa unajihadhari na ushawishi utakaokurudisha tena katika kuishi maisha ya dhambi, au kuona kila kinachofanyika kuwa ni cha kawaida tu, 1Wakoritho 15:33Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema” ni Muhimu kufahamu kuwa katika biblia ya kiingereza neno mazungumzo linalotajwa hapo linasomeka hivi kwa mfano NIV na matoleo mengine ya kiingereza yanatumia neno “Bad Company” ambalo lingemaanisha marafiki wabaya,  kumbe wakati mwingine watu wanaweza kuishi maisha ya dhambi kutokana na mazingira yanayokuzunguka au kutokana na marafiki na ushawishi ili mkristo aweze kudumu katika imani ni lazima ahakikishe kuwa anavunja urafiki na watu waovu, Maisha ya dhambi yanaweza kuahribu ushirika wako na Mungu hiki ndicho kilichotokea kwa mwana mpotevu Luka 15: 11-19Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako” unaweza kuona katika mfano huu, maisha ya kutaka kuwa huru,ubinafsi na majaribio yenye kuhatarisha vinaweza kukuleta katika maisha yenye majuto sana Neema ya Mungu bado iko ni kwa toba ya kulia na kujuta kutoka moyoni tunaweza kurejea tena katika ushirika  na Mungu, ingawa ni vema zaidi kama hatutauvunja ushirika huo na kuendelea kushikamana na utimilifu wetu hata mwisho.

Wakristo wanaoishi katika maisha ya dhambi pia hawawezi kufurahia kanisa ambalo linakaza kukataza dhambi, hawawezi kujisikia salama kuweko mahali ambako dhambi zinakemewa,wanaweza kusema sihitaji kumsikia muhubiri huyu mwenye mahubiri ya kizamani,sitaki kumsikiliza Mchungaji yule na mambo yake ya kuvuana nguo hawataki kukemewa wanahitaji jumbe za kuwatia moyo tu ukianza kunyoosha wanakuchukia kama uko safi hutaogopa kukemewa ni muhimu kukubali kukemewa, kurudiwa na kuonywa hali hii ndio itakayotupeleka kwenye uzima Waebrania 12:4-10Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake”. Nimuhimu kufahamu kuwa kukemewa ni sehemu ya injili, kukemea zinaa, uongo, wizi, ujambazi, masengenyo, uchawi, uadui, ugomvi, uzushi, na kila aina ya uovu ni sehemu ya injili, kanisa lolote linalohubiri kweli bila kutia maji ni lazima waikemee dhambi, tabia endelevu ya kuishi katika dhambi itatupelekea katika kurudi nyuma na kupoteza neema ya Mungu.

6.       UONGO

Uwongo ni dhambi, watu wengi sana hujifunza kusema uongo tangu utoto, tunapookoka biblia inatutaka tuache kabisa uongo na kuambiana ukweli, Mwanzo 37:31-35Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia” Kabla ya mabadiliko makubwa wana wa Israel walikuwa waongo, waliweza hata kumdanganya baba yao kwa kupatana kwamba mtoto ameliwa na mnyama mkali, Israel alilia kwa siku nyingi kwa uchungu na masikitiko kumbe alikuwa amedanganywa nilikuwa nawaza inawezekanaje kutokuwa na huruma kwa  watoto wa mzee Yakobo walimuacha baba yao aamini uongo kwa muda mrefu walikula matanga na kuomboleza msiba ambao hawakuwa na uhakika nao, watu wa Mungu ni muhimu kukumbuka kutokudanganyana, kusema ukweli, na kuacha kusemezana uongo, Wakolosai 3: 9-10Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba”. Mungu ni mkweli hatupaswi kamwe kusema uongo, Afrika inafahamu sana uongo wa wamisionari waliokuja kuleta dini, walifundisha kuwa msiibe lakini wao walituibia madini, pembe za ndovu na mali nyingi sana zilizokuwepo Afrika wakati huo, hii ilisababisha baadhi ya maeneo afrika kuwa na ukristo mbaya, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu, Maisha ya wamishionari yanaangaliwa sana na wale wanao wahubiri, hivyo nilazima kuwa wakweli, watu wote waseme kweli biblia ni ya wote Mungu anachukizwa na uongo vilevile. “Kule Kenya Mzee Jomo Kenyata alisema walituletea Biblia lakini wao wakachukua ardhi yetu” kwa sababu ya mfano mbaya wa wakristo wamisionari waliotangulia Afrika imeathiriwa lakini sasa hakuna udhuru ni lazima tusimamem katika kweli bilamkuwa na visingizio  Mithali 6:16-17 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu”. Unaona ni muhimu kwetu tuakajifunza kuwa wakweli, kweli ni silaha mojawapo ya Mkristo kumshinda shetani Waefeso 6: 10 - 14. “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.  Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,” hatuwezi kuwa na nguvu na mamlaka kama tunasema uongo ni muhimu kwetu kujifunza na kukubali kubadilika na kuwa kweli katika maisha yetu ya Ukristo ni lazima tujihoji wenyewe je sisi ni waaminifu?,sisi ni wakweli? Je tunakubali kutubu tunapokosea? Je tunakasirika tunapoambiwa ukweli wakati umefika sasa wa kuacha kusema uongo na kusema kweli.

7.       KUASI 

Dhambi moja tu katika biblia inafananishwa na uchawi, dhambi hii ni dhambi ya kuasi,kuasi kwa ufupi ni kushindana na kupinzana na kupingana na mamlaka iliyoko, wakati wote vikundi vya aina hii vinavyopigana na serikali kwa sababu ya madai kadhaa kama mfano hapa Afrika vimepewa jina la waasi, Hali kadhalika watu waliomtii Mungu huitwa wana wa kutii na kinyume chake watu wanaomuasi Mungu huitwa wana wa kuasi 1Petro 1:14Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;” Biblia inawaita watoto wa Mungu kama watoto wa kutii lakini wakati mwingine hutokea watoto wa Mungu wakamuasi, uasi ni dhambi mbaya sana na inakwamisha watu kupata neema ya Mungu, uasi unaleta kukataliwa adhabu ya uasi au uhahini mara zote huwa ni kifo hakuna rehema kwa muasi 1Samuel 15:22-23Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.”  Unaweza kuona watu wanaweza kuasi makanisa yao na kuanzisha huduma, washirika wanaweza kuasi kanisa lao na kuhamia kanisa lingine, Wachungaji wanaweza kuasi na kufungua makanisa mengine, wachungaji wasaidizi wanaweza kuasi na kufanya mambo mengine, wana ndoa wanaweza kuasi na kutoka nje ya ndoa zao, na kupeana talaka, na kuolewa na waume au kuoa wake wengine, watoto wanaweza kuasi, wazazi wao, Mwana mpotevu pia anaweza kuingia katika kundi la kuasi, Absalom alimuasi babaye Daudi, Shimei,na Ahithofeli, shetani pia aliasi mbinguni uasi uliwanyima Israel nafasi ya kuingia kanaani , unapoasi sasa anayekuwa adui yako sasa sio shetani bali Mungu na Roho wake mtakatifu wanapigana nawe, uasi unaanzia moyoni, uasi unaambukiza na unaenea na kusambaa kwa haraka, Isaya 63:9-10Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale. Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao.” Kufanya uasi ni kujiweka katika wakati mgumu sana hatuwezi kupigana na Roho Mtakatifu kisha tukafikiri kuwa tunaweza kufanikiwa,  Katika ujuzi wa kimungu unapojikweza Mungu anakupinga na kuondoa neema yake kwako 1Petro 5:5-6Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” Mungu huwapinga wenye kiburi yaani waasi na kuwapa neema wanyenyekevu yaani watii, watu wengi sana wamepoteza neema ya Mungu kwa sababu ya kuasi , Uasi ndio dhambi kuu ya shetani. Hii inasababisha kurudi nyuma na hata kufa Kiroho na kutokufanikiwa. Mungu alikataa kabisa ombi la Musa na haruni kutaka kuiona Kanaani na mara kadhaa Mungu aliwakumbusha kosa lao la kuasi, Mungu anaweza kusahau dhambi zote lakini anakumbuka sana mtu anapoasi Bwana atupe neema ya kuachan na uasi na kuwa mbali nao katika jina la Yesu. Ukweli ni kuwa watu wengi katika biblia waliasi na walilipa gharama kubwa sana wengine walikufa Jangwani na Yona nabii alimezwa na Nyangumi Zaburi ya 68:6 Biblia inasema “Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu” Neno wakaidi hapo linatumika pia kama “the rebellious dwell in a dry land” yaani waasi Mungu huwapa waasi ukavu,jangwa, njaa wanakaukiwa kiroho uhusiano na Mungu unakufa na hakuna uamsho katika roho zao, wanaishi maisha ya huzuni na vifungo vya aina mbalimbali, ee Mungu tuokoe na dhambi ya uasi.

8.       UZEMBE/ UJINGA./UPUMBAVU.

Biblia ina maneno magumu sana kwa mtu aliyerudi nyuma anu kudumaa kiroho, hakuna maneno ya kutia moyo kwa mkristo anayemuacha Yesu, watu wengi sana wanapoishi maisha ya dhambi hujifikiri kuwa wao ni wajanja lakini biblia inamuita mtu anayerudi nyuma kama mjinga na mpumbavu mimi naita uzembe, Mithali 1: 32-33 “Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.” Unaweza kuona na Yesu anaongezea maneno magumu zaidi kwa mtu asiyelifanyia kazi neno lake anamuita Mpumbavu Mathayo 7:26-27 Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.” Mtu aliyeokolewa akiacha kujiandaa kwa maswala ya Mungu na akawa anaiwaza dunia kana kwamba atakaa humo milele biblia haina muda wa pongezi dhidi ya mtu huyo bali anaitwa mpumbavu Luka 12:16-21 16. “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.  Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.” Neno la Mungu halina lugha nyepesi kwa mtu anayerudi nyuma zaidi ya neno upumbavu na ujinga kumuacha Yesu na kuigeukia Dunia ni ujinga ni upumbavu mimi nasema ni uzembe wa hali ya juu 2Petro 2:20-22 Biblia inasema maneno magumu zaidi angalia “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni”.  Uwiii Mungu atusaidie Mithali ya kweli Mbwa anayekula matapishi yake mwenyewe au nguruwe aliyeoshwa kugaa gaa matopeni”

Ndugu nyangu kumbe kurudi nyuma ni upumbavu, ni ujinga ni kujikosesha Baraka za Mungu afadhali uendelee kukaa na Yesu, na kumshikilia kamwe usiwaze kumuacha ni afadhali uendelee kushikamana na Bwana endapo utetenda dhambi hakuna njia ya mkato tubu yeye ni mwaminifu lakini usimuasi Bwana na kurejea nyuma

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev.Innocent Kamote.

Hakuna maoni: