Ijumaa, 16 Februari 2018

HASIRA YA BWANA !



Zaburi 90:7-11Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima. Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.  Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, Kama miaka ile tuliyoona mabaya. Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na adhama yako kwa watoto wao. Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.” 



  • ·         Mifano ya kibiblia inayoonyesha kuweko kwa Hasira ya Mungu.
  • ·         Sababu ya kuweko kwa hasira ya Mungu.
  • ·         Hasira ya Mungu inafunuliwa namna gani.
  • ·         Hatima ya Hasira ya Mungu.
  • ·         Namna ya kujiokoa na hasira ya Mungu ijayo:


Utangulizi:

“Hasira ni hisia kali zinazotokea wakati jambo linalofikiriwa kuwa baya au lisilofaa au lisilola haki linapokuwa limetendeka” wanadamu kwa kawaida huwa wana hasira, Na hali kadhalika Mungu katika nyakati fulani fulani hufikia kiwango cha kutokuendelea kuwavumilia wanadamu pale wanapotenda yasiyopaswa! Neno la Mungu limejaa mifano mingi inayoonyesha juu ya hasira za Mungu pale wanadamu walipotenda kinyume na mapenzi yake!

Musa alifahamu kuwa Mungu ndiye aliyekuwa akiwaongoza wana wa Israel, aliona jinsi Mungu alivyowaokoa Israel kwa uweza mkubwa, kupitia mapigo yale 10 na vilevile namna alivyowaokoa Israel kwa kuwavusha bahari ya shamu na kumwangamiza Farao na majeshi yake yote kwa sababu walikuwa wakijaribu kupingana na mpango wake dhidi ya watoto wake na taifa lake teule, lakini vilevile Musa alishuhudia Mungu akiwaangamiza walwi 250 baada ya kuivuka bahari ya shamu, kwa hiyo sasa Musa alikuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu Hasira za Mungu.

Mifano ya kibiblia inayoonyesha kuweko kwa Hasira ya Mungu.

Mungu anapokasirika hufanya matukio ya kutisha sana hasira za Mungu huja pale wanadamu wanaposimama kinyume na mpango wake na kutaka kuvuruga makusudi yake na kuishi maisha ya dhambi, Mungu aliiharibu miji ya Sodoma na Gomora kwa sababu ya maisha mabaya na machafu., Mungu alimuhurumia Lutu tu na familia yake kwa sababu ya Haki, lakini wengine wote na mji mzima aliusambaratisha Maandiko yanaonyesha katika sehemu kadhaa jinsi Mungu anavyochukizwa na dhambi

·       Mapema sana wanadamu walipokuwa wakiongezeka juu ya uso wa dunia na kuacha njia za Mungu Mungu aliweza kuifunua Hasira yake takatifu na kuwafutilia mbali wanadamu wote juu ya uso wa nchi Mwanzo 6:1-8 “.Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.  BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu, wakazaa nao wana; hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.

·         Aidha Hasira takatifu ya Mungu ilifunuliwa pale wanadamu walipopingana na makusudi yake ya kutawanyika na kuijaza Dunia na hivyo Mungu alishuka na kuwachafulia usemi Mwanzo 11:1-9Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. Wakaambiana,Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa.  Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo BWANA alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko BWANA akawatawanya waende usoni pa nchi yote.

·         Hasira ya Munguiliweza kudhihirika pale watu wa miji ya Sodoma na Gomora walipoanza kufuata uchafu na kushiriki ngono za jinsia moja, Mungu aliteketeza kila kitu katika mji wa Sodoma na Gomora , waona watoto wao na mali zao na kila walichokuwa wakikimiliki Mwanzo 18:17-21 BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake. BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua”. Kumbuka kuwa watu wa Sodoma hawakuwa na Biblia hawakuwa na manabii wala viongozi wa dini lakini hiyo haikuwa tiketi ya Mungu kuwaacha watu waishi bila uadilifu, Mungu anataka watu waishi kwa uadilifu ili kuepuka hasira zake.

·         Hasira za Mungu zinafunuliwa katika kitabu cha kutoka Pale Kora, Dathan na Abiramu waliposhindana na Mtumishi wa Mungu Musa katika Hesabu 16:1-21Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana?  Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi; kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi Bwana ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za Bwana kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu Bwana atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi.

Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi; Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya Bwana, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha Bwana; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia? Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi; je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa? Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji. Musa akakasirika sana, akamwambia Bwana. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao. Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya Bwana kesho, wewe, na wao, na Haruni; mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za Bwana, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake. Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni. Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa Bwana ukatokea mbele ya mkutano wote. Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja.”

·         Hasira za Mungu ziliweza kuainishwa tena kwa wana wa Israel waliposhindwa kumuamini kwamba wataingia katikia nchi ya mkanaani  Hesabu 14:1-9Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.”

·         Wakati watu walipofanya dhambi ya manung’uniko kinyume na mpango wa Mungu Hasira za Mungu zliwaka na akaruhusu nyoka za moto kuwashughulikia Israel ingawa walikuwa watu wake Hesabu 21:4-6Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

·         Katika agano jipya tunaweza kuona Jnsi mtu aliyeitwa anania na Safira walivyoweza kufanya dhambi na hatimaye walijikuta wakifutiliwa mbali wote mtu na mke wake kwa sababu ya kulidanganya kanisa Matendo 5:1-10Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika.     Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe.Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.”

Sababu ya kuweko kwa hasira ya Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu ni Mungu wa haki, na moja ya malipo anayoyafanya kwa wanadamu wanapokuwa wameasi au kwenda kinyume naye biblia imeweka wazi kuwa mshahara wa dhambi ni mauti  na zawadi ya utii ni uzima wa milele Warumi 6:23Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Maandiko yanatuthibitishia wazi kuwa tukifanya dhambi yako malipo yanayotukabili Hesabu 32:23Lakini kama hamtaki kufanya neno hilo, ninyi mmefanya dhambi mbele za Bwana, nanyi jueni ya kwamba hiyo dhambi yenu itawapata hapana budi.” Hakuna mtu anaweza kufanya dhambi kisha akakwepa Hasira za Mungu, Ni kweli kuwa Mungu ana uvumilivu mkubwa lakini maandiko bado yanatuonya kwa uwazi kwamba dhambi huamsha hasira za Mungu.

Hasira ya Mungu inafunuliwa namna gani.

Ni muhimu kufahamu kuwa Hasira za Mungu zinafunuliwa mara kadhaa kupitia nyuso au uso wa watumishi wake na maneno ya watumishi wake au matendo ya watumishi wake, mara kadhaa utaweza kuona kimaandiko jambo lilipokuwa baya aidha lilimuuzi Mungu na mtumishi wake pia Hesabu 16:28-35Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba Bwana amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi Bwana hakunituma mimi. Lakini Bwana akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau Bwana Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. Kisha moto ukatoka kwa Bwana, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba.”

2Wafalme 1:1-17Ikawa, baada ya kufa kwake Ahabu, Moabu wakawaasi Israeli. Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka. Wale wajumbe wakarudi, na mfalme akawaambia, Mbona mmerudi? Wakamwambia, Mtu alitokea, akaonana nasi, akatuambia, Enendeni, rudini kwa mfalme yule aliyewatuma, mkamwambie, Bwana asema hivi Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi kwa ajili ya hayo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani? Wakamwambia, Alikuwa amevaa vazi la manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, Ndiye yule Eliya Mtishbi. Ndipo mfalme akatuma akida wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka.  Eliya akajibu, akamwambia yule akida wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Akatuma tena akida wa hamsini mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka upesi. Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Tena akatuma akida wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule akida wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako. Tazama, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawateketeza wale akida wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako. Malaika wa Bwana akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka pamoja naye hata kwa mfalme. Akamwambia, Bwana asema hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, uulize neno lake? Kwa hiyo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Basi akafa, sawasawa na neno la Bwana alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana.”

Yohana 2:14-16 “Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao;  akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara”.  
             
Hatima ya Hasira ya Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa hatima ya maswala yote haya ni kuwa Mungu ataifunua hasira yake kamili kwa wampingao katika jehanamu au ziwa la moto Zaburi 9:17Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.” Kuzimu ni mbali na huruma ya Mungu maelezo ya kawaida kuhusu kuzimu maana yake ni mahali ambapo pamejaa moto na salfa na makaa na mawe ya moto ni shimo lenye giza huko nafsi za wote waliomkataa Mungu kwa matendo yao watahifadhiwa wakiwa katika hali ya kifo milele na milele pamoja na mashetani, Biblia inaelezea kuwa huko kutakuwa na kilio na kusaga meno ni wazi kuwa Mungu anayaandika majina ya watu wake wanaomuheshimu na kushika amri zake katika kitabu cha uzima na kama mtu hataoonekana siku ile ya hukumu atatupwa katika ziwa la Moto Ufunuo 20:15Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”

Namna ya kujiokoa na hasira ya Mungu ijayo:

Biblia inaonyesha njia pekee ya kuikimbia hasira hii ni kuliitia jina la bwana ili tuokolewe Warumi 10:13kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.hatima ya kila mmoja wetu inategemeana na jinsi unavyoyatoa maisha yako kwa Yesu, kuliitia jina la Bwana maana yake ni kumuamini Yesu na kumuabudu na kuzishika njia zake na kufuata mafundisho yake na kuishi mbali na dhambi ambayo ndio husababisha hasira ya Mungu aidha dhambi mshahara wake ni Mauti Warumi 6:23, Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Njia pekee ya kujiokoa na na mauti hii ni sisi kumuamini Yesu Kristo na kumfanya kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu na kumuomba atuokoe na dhambi maana hii ndio kazi kubwa ya mwokozi Mathayo 1:21 “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao”

Tunaweza kuikwepa Hasira ya Bwana kwa toba na kumkimbilia Yeye, kumbuka kuwa Yeye ni mwaminifu kama tutajinyenyekeza kwake atatuangalia, katika Ghadhabu yake atakumbuka rehema, na kutusaidia, kama tukifanya dhambi kama watu wote tufanyavyo dhambi tusimkimbie Mungu bali tukimbilie kwa Mungu.

Ni muhimu kwetu tukajiokoa na kizazi hiki chenye ukaidi na uasi wa kila namna ili tuweze kuiepuka Hasira ya Mungu
Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa mbali na hasira ya Mungu katika Jina la Yesu.

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.!

Hakuna maoni: