Mstari wa Msingi: Ezekiel 37:1-3 “.Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye
akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo
limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na
mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza
kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe”.
Je! mifupa hii yaweza Kuishi?
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Wana wa
Israel walikuwa wameokolewa na Mungu kwa uweza mkubwa sana wote tunakumbuka jinsi
Mungu alivyomuadhibu farao kwa mapigo mazito chini ya mkono wa Mtumishi wake
Musa na Haruni, mpaka Mungu alivyojipatia taifa na kulistawisha katika nchi ya
mkanaani na kuwa na ustawi mkubwa sana chini ya waamuzi na wafalme. Hata hivyo
ni jambo la kusikitisha kuwa baada ya muda mfupi, walimuacha Mungu na kuabudu
miungu na kumpuuzia Mungu aliyewaokoa, ukweli ni kuwa walisahau historia nzima
na kugeukia njia zao, Hivyo Mungu aliruhusu waweze kwenda utumwani tena.
Mwaka kama wa 722BK na 586BK Mungu aliruhusu Israel kuchukuliwa uhamishoni
na Yuda kuchukuliwa uhamishoni Babeli chini ya utawala wa mfalme Nebuchadnezer,
Jeshi la Nebuchadnezer liliizingira Yerusalem na kuharibu na kusambaratisha
vibaya Hekalu lililokuwako Yerusalem na kulichoma moto kuwa majivu, na wayahudi
walichukuliwa kwenda Utumwani Babeli, hiki ndio kilikuwa kifo cha Taifa hili na
mwisho wa matumaini yao. Huu ulikuwa ni msiba mkubwa sana ambao haukuwa na
matumaini ya kuupoza.
Daniel 1:1-4 “Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa
Yuda, Nebukadreza mfalme wa Babeli,alikwenda Yerusalemu akauhusuru.Bwana
akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya
vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka
nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu
wake. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu
wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa
uzao wa kiungwana; vijana wasio na
mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye
kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia
awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.”
Katika wakati huu watu wazuri na vijana
wazuri na kila kitu kizuri kilichukuliwa utumwani Yerusalem ilibaki ukiwa huku
kukiwa hakuna matumaini tena, Ezekiel nabii alikuwa ni miongozi mwa watu
waliochukuliwa utumwani kwa mujibu wa historia.
Ni katika wakati huu sasa Ndipo
Mungu alimwambia nabii Ezekiel katika maono aweze kuangalia bonde hili lisilo
na matumaini, bonde lenye umauti usio na tumaini la kurejea tena na mifupa
ilikuwa imetapakaa na ni mikavu hakukuwa na matumaini ya uhai na ndipo Mungu
alipomuuliza Ezekiel swali hili Je mifupa hii mikavu yaweza kuishi?
Kwa ukweli maono haya yalikuwa
yanalihusu Taifa la Israel kwa wakati huo kwa sababu walikuwa wamekata tamaa,
walikuwa wamepoteza tumaini, waliona mauti na kujihisi kuwa ni kama
wamekatiliwa mbali Ezekiel 37:11 “Kisha akaniambia,
Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa
yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa.”ni
kweli kuwa hakukuwa na namna na jinsi ya kujiokoa kutoka katika msiba huo,
kwani watu wengi waliuawa na wengine walichukuliwa kwenda utumwani , Israel
iilikuwa tayari limegeuka kuwa bonde lisilo na uhani, na ni lenye mauti sisyo
na matumaini hii ilikuwa ni picha ya kukosekana kwa matumaini.
Tukio la jinsi hii lilijirudia
tena Israel waliporudi tena kutoka utumwani, walipata Hekalu na Yesu alikuja
lakinimnamo mwaka wa 70 hivi walitawanywa kotekote uhamishoni duniani na
hakukuwa na matumaini tena na hekalu lilibomolewa lakini ilipofika 1948 Israel
ilipata uhuru wake na kufanyika taifa tena Mungu ni mwaminifu kwa watu wake
Historia inatushuhudia.
Hali hii sio tu kuwa ilikuwa inaihusu
Israel wakati ule, lakini inawezekana ikawa inatuhusu sisi nasi katika siku hii
ya leo, inawezekana uko mahali hapa unaisikia sauti hii, au unasoma makala hii,
lakini ukiwa katika hali ya uzuni nzito inayokukabili, moyoni mwako ukiwa
umepoteza matumaini, huoni nuru mbele matumaini yako yamepotea, una vyeti
kadhaa vya madaktari, una shuhuda kadhaa za watu wenye tatizo kama lako na wote
mmeambia kuwa tatizo lako haliwezekani, inawezekana ni wachawi wameharibu ukoo
wenu, ni adui zako wamesema wale tumewaweza kwa hali hii hawachomoki tena,
hawainuki tena uko katika giza nene, inawezekana watu wakakuona una-smile
lakini Moyoni huna amani ya kweli, moyoni ni misiba, moyoni ni kukavu,
hufurahii uwepo wa Bwana, unalia kilio cha ndani unajiuliza matumaini yatatokea
wapi? Unajiuliza kehso itakuwaje? Unajiuliza nawezaje kukabiliana na aibu hii?
Kila kitu kimesambaratika hakuna matumaini ya kusimama tena, ndoto zako
zimeyeyuka? Mambo unayotaka ni kama hayaendi?
Namshukuru Mungu kwa Jibu
alilolitoa Ezekiel 37:3b “Nami nikajibu Ee
Bwana Mungu wajua wewe.” Ezekiel yuko katika Bonde lililojaa mifupa
mikavu tena iliyotawanyika na kwaakili za kibinadamu hakuna uwezekano wa kuweko
uzima wala ufufuo, ni vigumu kukubali hali halisi ya uzima hapa ni vigumu hata
kufariji we ungejibuje swali kama hili, Lakini jibu la nabii Ezekiel
linaonyesha kwa sehemu alijua kuwa Mungu anaweza kuwa anaelewa zaidi.
Ezekiel ni kama alikuwa anajua
kuwa Mungu anaelewa zaidi, ni yeye pekee anayeweza kuingilia kati na kufanya
kitu katika mazingira ambayo akili ya mwanadamu imefika mwisho, Ezekiel alikuwa
anajua kuwa Mungu anaweza kufanya lolote analolitaka, kwa Mungu hakuna
linaloshindikana, Mungu akitaka mifupa hii mikavu iiishi itaishi.
Mungu amenituma leo nikutangazie
kuwa yasiyowezekana kwa wanadamu, Kwa Mungu yanawezekana kwake liko tumaini
kubwa sana na hupaswi kukata tamaa, kila matumaini yanayofifia katika moyo wako
na ndoto zako Bwana anaweza kukuinua tena Ee bwana Mungu wajua wewe ilikuwa ni
sauti ya Ezekiel akimjibu Mungu ashukuriwe Mungu Ezekiel hakusema haiwezekani,
lakini alisema Mungu anajua liko tumaini katika yeye, atakufufua tena atakupa
uhai, kama alivyoipa Israel uhai, wa kisiasa na kiroho na kuliponya taifa lile
na kulilinda hata liko tena leo.
Mungu atakuinua tena, Simama tena
changamka usikae chini na kusikitika kuwa itakuwaje iko pumzi ya uhai leo,
Bwana atakuganga kwa upya, kila kilicho na uhai na kisicho na uhai kinasikia
neno la Mungu leo neno la Mungu linakuja kwako kama pumzi ya uhai nawe utajua
ya kuwa Bwana ndiye Mungu Ezekiel 37:4-6
“Akaniambia
tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno
la Bwana. Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi
ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama
iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi;
nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.”
Nakuomea ili kwamba Bwana afufue
na kurejeza matumaini yako kila yanakoonekana kufifia aku kufa katika jina la
Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai.
Ni matumaini yangu kuwa
umebarikiwa na ujumbe huu ningependa kupata maoni yako kama ujumbe huu
umekubariki, na ni imani yangu utakubariki, au utabariki washirika wako usisite
kumshukuru Mungu japo kwa ujumbe was sms
Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.
0718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni