Yohana 8: 42 “Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda
mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu,
bali yeye ndiye aliyenituma.”
Utangulizi
Ni muhimu kwa kila mmoja wetu
kujiuliza je Mungu ni baba yetu? Ni muhimu kufahamu kuwa sio kila mmoja wetu
Mungu ni baba yake?, Yesu aliwahi kuwaambia ukweli mafarisayo na masadukayo
pamoja na waalimu wa Torati waliodhani kuwa Mungu ni Baba yao kwamba wao sio wa
Mungu, na aliwakemea kwa kuwaeleza wazi kuwa wao baba yao ni Ibilisi Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za
baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala
hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo,
husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”
Kama Mungu ni baba yetu tutampenda Yesu, tutamkubali Yesu, na tunaweza
kuthibitisha kwamba sisi ni wa baba katika njia kuu saba zifuatazo:-
1.
Tutamwanimi
yeye kama tunavyomwamini Mungu:-
Ni jambo la
kusikitisha kwamba Yesu alitoka kwa Mungu, lakini hata hivyo wakuu wa dini,
mafarisayo na masadukayo pamoja na waandishi yaani walimu wa torati hawakuwa
wamemwamini, huwezi kusema kuwa unampenda mtu, lakini hata hivyo humuamini,
kuamini kunaendana na kupenda Yesu anataka tumwamini yeye kwa kiwango kilekile
cha kumuamini Mungu Yohana 14:1 “Msifadhaike mioyoni
mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.”
Ishara kubwa ya
kwamba tunamkubali Yesu na kwamba tunamwamini Mungu na tunampenda ni pamoja na
kumuamini, na kama tunamwamini Yesu ni sawa na kuwa tumekubali zawadi kubwa
ambayo Mungu amewapa wanadamu kupitia yeye na hivyo tutampenda.
2.
Tutazitii
amri zake:-
Kiwango kikubwa
na cha juu zaidi cha upendo wetu kwa Yesu ni pamoja na kutii amri zake, Yesu
aliliweka wazi hili mapema tu ya kwamba kama Mungu ni baba yetu na amemtuma
mwanaye wa pekee sio tu ili tumwamini lakini vilevile tumsikilize yeye ni
ukweli ulio wazi kuwa Torati iliagiza kuwa Nabii huyu mkubwa aliyetumwa kwa
mfano wa Musa anapaswa kusikilizwa maana yake tumtii Kumbukumbu la Torati 18:15,18-19 “Bwana, Mungu wako,
atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni
yeye., Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami
nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.Hata
itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu,
nitalitaka kwake” Yesu alikuwa ndiye nabii yule ajaye aliyetabiriwa
na Musa katika torati na katika manabii na swala hili lilieleweka wazi Yohana 1:45. “Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia,
Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa
Yusufu, mtu wa Nazareti” ni ukweli ulio wazi kuwa ilieleweka kwamba
Yesu ndiye masihi lakini hata hivyo baadhi ya watu licha ya kuwa walikataa
kumuamini lakini pia hawakuzishika amri zake, Yesu anaweka wazi kuwa kama
tunampenda yeye basi tutazitii amri zake Yohana
14:15 “Mkinipenda,
mtazishika amri zangu” Unaona kama Mungu ni baba yetu tutamwanini
Yesu Kristo na tutazishika mari zake.Yesu hafurahii kuitwa Bwana na watu ambao
hawako tayari kuyatenda asemayo Luka
6:46 “Na kwa
nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?” unaona
Yesu kristo anahitaji kuaminiwa lakini vilevile kuyatii maagizo yake.
3.
Tutadumisha
Ushirika wetu na Yesu!
Ni muhimu
kufahamu kuwa uhusiano wetu na Mungu na bwana wetu Yesu Kristo ni uhusiano wa
kudumu, awaye yote ambaye atamwamini Yesu au aliyeamua kumfuata Yesu hana budi
kuhakikisha kuwa anashikamana na ushirika na Yesu bila kugeuka nyuma, Mungu
anatarajia uhusiano wetu nay eye uwe wenye kudumu, na hafurahii kugeuka nyuma,
kimsingi mtu anayemuacha Mungu biblia inamuita mtu mwenye moyo mbovu Waebrania 3:12-14 “Angalieni,
ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga
na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja
wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.
Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa
uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho;” Kuanza safari ya kumuamini
Yesu sio tatizo, watu wengi hulipokea neno kwa furaha na kumkubali Bwana yesu
kwa msisimko, lakini hata hivyo kuendelea kukaa ndani yake ndio jambo la muhimu
na zaidi ya umuhimu ni kustahimili mpaka mwisho na kuumaliza mwendo pamoja
naye, Mathayo 24:13 “Lakini mwenye
kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.” Unaweza kuona kwamba mtu anamalizaje hilo ndio jambo la muhimu,
Katika kutuongoza kuifuata imani Biblia inatutia moyo kuwaiga watu
waliotuongoza na kuiiga imani yao Waebrania
13:7 “Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza,
waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao,
iigeni imani yao.” Kumbe tunaweza
kuiiga imani ya kiongozi wetu, wachungaji wetu, mashemasi wetu wazee wetu,
maaskofu wetu na kadhalika lakini baada ya kuchunguza namna walivyohitimu
katika imani, Mungu anataka tudumishe uhusiano nay eye hata mwisho.
4.
Tutazinena
habari zake!
Hakuna namna
yoyote ambayo kwayo tunaweza kusema kuwa tunampenda Mungu na Yesu Kristo kama
hatuzisemi habari zake, Mitume walidhihirisha wazi kuwa wanampenda sio kwa
kunyamaza kimya bali walizinena habari zake
kila siku na kila mahali Matendo
5:41-42 “Nao
wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili
kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo. Na
kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri
habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.” Maandiko yanawasifia watu
wanaonena habari za Yesu kuwa ni watu wema na kuisifia miguu yao kuwa ni
mizuri, Yesu anataka tusambaze habari zake kwa watu wote ili waliitie jina lake
na kuokolewa Warumi 10:14-15 “Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye
wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa?
Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!”
Nyakati za kanisa la kwanza watu walimpenda sana Yesu na hivyo hawakuacha
kuzungumza habari zake kila walikokwenda hata pale walipotawanyika kwa sababu
ya dhiki bado walikuwa waaminifu kuelezea habari za Yesu Matendo 8:1-5 “Siku ile kukatukia adha kuu
ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya
Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.
Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli
akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na
kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko
wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri
Kristo.” Kama Mungu ni
baba yaetu tutampenda Yesu Kristo na kama tunampenda Yeu Kristo tutazungumza
habari zake, Biblia inatutaka tuwe tayari wakati wote na siku zote 1Petro 3:15 “Mwe tayari siku zote kumjibu
kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na
kwa hofu.”
Wote waliompenda Yesu walikuwa tayari kuzishuhudia habari zake na hawakuona
aibu.
5.
Tutakuwa
tayari kuteseka kwaajili yake
Kile
unachokipenda wakati mwingine unaweza kuwa tayari kukigharimikia, wazazi
wanatoa nguvu zao na muda wao kujinyima kwaajli ya watoto wao kwa vile
wanawapenda, wako watu ambao wako tayari kuyatoa maisha yao kwaajili ya
wapendwa wao, katika hali kama hii wote wanaompenda Yesu wote ambao Mungu ni
aba yao watakuwa tayari pia kuteseka kwaajili ya Yesu Kristo , Yeye alitupatia
zawadi kuu ya wokovu kwa njia ya Mateso
Waebrania 5:7-9 7. “Yeye, siku hizo za mwili wake,
alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja
na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na,
ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha
kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;”
unaweza kuona jinsi ambayo kiongozi mkuu wa wokovu wetu yaani Bwana Yesu
alikamilishwa kwa njia ya Mateso, kila mmoja wetu ambaye ameitwa kumwandama
Bwana ni lazima pia awe tayari kuteseka kwaajili yake kuwa ndani ya Yesu ni
kukubali mateso ni kujiunga na mateso
yake 2Timotheo 1:7-12 “7. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya
upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala
usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya
Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito
mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake
yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na
sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili
mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya
hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu. Kwa sababu hiyo nimepatikana
na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na
kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile.”
Unaweza kuona njia nyingine pekee yenye kuonyesha kuwa tunampenda Mungu na
kwamba Mungu ni baba yetu ni kukubali kushiriki mateso kwaajili ya injili yake.
6.
Tutatamani
kufanana naye.
Lengo kubwa la
neno la Mungu na mafundisho ya mitume ni sisi kuwa kama Yesu Kristo Wagalatia 4:19 “Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu
tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;” Unaona Kristo kuumbika ndani
yetu maana yake ni ile hali ya kukomaa na katika tabia na mwenendo na kufikia
hatua ya kuwa kama Yesu Kristo mwenyewe, hili ndilo kusudi kuu kama tunampenda
Yesu ni lazima tutafanana naye, mwelekeo na mkazo mkuu wa mitume na manabii ni
kuhakikisha kuwa tunawafuata wao kama wanavyomfuata Kristo 1Wakoritho 11:1 “Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.”
Watoto wakati wote hujifunza kwa kuigiza tunaweza kuwaigiza wazazi wetu katika
kila jambo liwe jema au baya, kwa sababu tunawapenda, sisi nasi kama tunampenda
Bwana Yesu tutamuiga katika kila eneo la tabia na mwenendo wake, kuitwa
wakristo kunatokana na mwenendo unaomfanania Yesu Kristo, Wakolosai 3:9-11 “Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja
na matendo yake; mkivaa utu
mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.
Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala
mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote.”
Unaona tunapaswa kuvaa utu mpya sawasawa na mfano wa yeye aliyetuumba, wakati
wote ni lazima tulenge kuwa kama Yesu na kufanana naye.
7.
Tutatamani
kumpendeza Yeye.
Ni muhimu kufahamu
kuwa watu wanaopendana hutamani sana kufurahishana, sisi nasi ni muhimu
kuhakikisha kuwa tunatamani kumpendeza Bwana wetu Yesu, yeye alitupenda upeo
nasi hatuna budi kumpenda 2Wakoritho
5:14-15 “Maana, upendo wa Kristo watubidisha; maana
tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote;
tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya
nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.”
Unaweza kuona haya ndio yalikuwa madai makubwa ya Bwana Yeye kuwa kila ambaye
Mungu ni baba yake angampenda yeye maana yeye ametoka kwa Baba Yohana
8: 42 “Yesu
akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka
kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye
aliyenituma.”
Hitimisho:
Ukweli ulio wazi ni kuwa kama mtu
hampenzi Yesu nasikitika kumjulisha mtu huyo kuwa maandiko yanasema amelaaniwa 1Wakoritho 16:22 “Mtu
awaye yote asiyempenda Bwana, na awe amelaaniwa. Maran atha.” Na kwa sababu hiyo hii kama humpendi Yesu Mungu sio
baba yako na kama Mungu sio baba yako wewe ni wa ibilisi na unawezaje kuwa
mwana wa Mungu ni kwa imani kupitia Yesu Kristo, Wagalatia 3:26 “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa
wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.” Ni kupitia yeye pekee tunaweza kumfikia Mungu na ndio
maana Yesu aliwataka viongozi wa dini kuelewa wazi kuwa hawana budi kumkubali
yeye endapo wanadai wanamjua Mungu lakini kama wanamkataa Yeye hawawezi kwa
njia yoyote kuwa wana wa Mungu.
“Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda
mimi”
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni