Andiko la Msingi: Matendo 10:15 “Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na
Mungu, usiviite wewe najisi.”
Ni muhimu
kufahamu kwamba tunaishi katika nyakati za mwisho sana ambazo zina mawimbi
mengi makubwa na ya kutisha ya uharibifu katika jamii, tunaweza kwa sehemu
kuita nyakati hizi kuwa ni nyakati nzuri sana lakini kwa upande mwingine ni
nyakati mbaya sana, kwa vile Dunia imeshuhudia mfumuko mkubwa sana wa maendeleo
ya sayansi na teknolojia, elimu ujuzi na uvumbuzi umepiga hatua kwa kiwango
kikubwa sana, Hapo tunaweza kusema kuwa dunia imekuwa nzuri imeendelea, lakini hata hivyo dunia imeshuhudia mmomonyoko
mkubwa wa uadilifu na uvunjwaji mkubwa wa haki za kibinadamu katika mtazamo wa
Mungu, moja ya matukio yenye kuhatarisha amani ya dunia na kukuza chuki
miongoni mwa jamii ni pamoja na ubaguzi wa rangi na wa kimadaraja kwa aina
binadamu, Makusudi makubwa ya somo hili ni kuwaita watu kurudi katika haki na
upendo na kutokomeza maswala yote ya kibaguzi duniani.Tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia maswala kadhaa yafuatayo:-
·
Wajibu wa Kutenda haki.
·
Mungu Hakuichagua Israel kwa sababu walikuwa
bora kuliko wengine.
·
Vilivyotakaswa na Mungu usiviite wewe najisi.
·
Mashujaa waliosimama kupinga ubaguzi duniani.
Wajibu wa kutenda haki.
Neno la
Mungu katika vifungu kadhaa vya Biblia limekazia juu ya wajibu wa kutenda haki,
na kukataza maswala yoyote yenye uhusiano na kutokutenda haki, pamoja na
kukataza upendeleo kwa sababu zozote zile Walawi
19:15 “Msitende
yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye
nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki.” Mungu anapendezwa sana
na watu watendao haki, lakini vilevile anachukizwa mno na watu wasiotenda haki Mika 6:8 “ Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo
mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki na kupenda rehema na kwenda
kwa unyenyekevu na Mungu wako” Mtu anayetenda haki anabarikiwa
katika maandiko Zaburi 106:3 “Heri wazishikao
hukumu na kutenda haki siku zote” kinyume chake mtu asiyetenda haki
amelaaniwa katika maandiko Kumbukumbu
27:19 “Na
alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na
watu wote waseme Amina.” Kulaaniwa maana yake mambo mabaya yampate
mtu awaye yote asiyetenda haki unaweza kuona muda usingeliweza kutosha kuona
maandiko yanavyokazia swala zima la kutenda haki na kuhukumu sawasawa bila
sababu au upendeleo wa aina yoyote ule au kuchukua rushwa!
Mungu
anataka watu wajifunze kutenda Mema kutenda haki na kwahurumia wanaoonewa Isaya 1:17 “jifunzeni
kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima
haki yake; mteteeni mjane.” Kwa
msingi huo Biblia inapozungumzia kutenda haki maana yake ni kuwa swala lolote
la ubaguzi wa rangi au ubaguzi wa kijamii na kitamaduni unamaanisha kutokutenda
haki, Katika Mstari wetu wa msingi Mungu alikuwa akimkemea na Kumuandaa Petro
kwenda na kukubali kuwahudumia Mataifa ambao walikuwa wanahitaji injili na
kwamba Mungu alikuwa amewakubali, Mungu alikuwa anashughulika na Petro ambaye
ndani yake mila na tamaduni za kuwa Myahudi zilikuwa zimemfunga asiweze kuona
Mpango kamili wa Mapenzi ya Mungu kuhusu Mataifa, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe
najisi alikemewa Petro.
Mungu Hakuichagua Israel kwa sababu walikuwa
bora kuliko wengine.
Natambua
wazi kabisa kuwa Israel ni taifa teule, ni watu ambao Mungu alijifunga kwao kwa
kiapo na maagano aliyowaapia Baba zao Ibrahim, Isaka na Yakobo, naipenda Israel
ni taifa ambalo limemleta Masihi kwetu Yesu mwana wa Mungu aliye hai, najivunia
Israel naipenda Israel ni Mapenzi ya Mungu kuipenda Israel na kuiombea na
kuomba kwaajili ya Yerusalem, natambua
mapenzi ya Mungu dhidi ya Israel, tumejifunza mengi kutoka kwao na uadilifu pia
, Lakini maandiko yanakumbusha kuwa walichaguliwa kwa neema tu ni kwa neema ya
Mungu ili aweze kupitisha mpango wake kwao Mungu anaonyesha kuwa hakuwachagua
wao kwa sababu walikuwa bora zaidi ya mataifa mengine
Si kwa
sababu ya wingi Kumbukumbu 7:7-9
“Bwana
hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko
mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote; bali kwa sababu Bwana
anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu,
ndiyo sababu Bwana akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya
utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri. Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu
wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao
wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu;”
Si kwaajili
ya Haki au usafi wao Kumbukumbu 9:4-6
“Usiseme moyoni
mwako, Bwana, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni
kwa haki yangu alivyonitia Bwana niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu
wa mataifa haya Bwana awafukuza nje mbele yako. Si kwa haki yako, wala kwa
unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa
mataifa haya Bwana, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka
imara hilo neno Bwana alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Basi
jua ya kuwa Bwana, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki
yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu.”
Si kwa
sababu wao walikuwa bora Warumi 3:9
“Ni nini basi? Tu bora kuliko
wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani
ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi;”
Sio
kwaajili ya Matendo mema Tito 3:5
“si kwa sababu
ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa
kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;”
Vilivyotakaswa na Mungu usiviite wewe najisi.
Matendo 10:1-29 “Palikuwa
na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu
mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka
nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya
mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana,
akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako
zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa,
ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye
ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba
yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda. Na yule malaika aliyesema naye
akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani,
na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima; na alipokwisha
kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa. Hata siku ya pili, walipokuwa
wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata
saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa
wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka
kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake
walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege
wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana
sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili,
ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili
likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. Hata Petro
alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona,
wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni,
wakasimama mbele ya mlango, wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro
anakaa humo. Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako
watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi,
kwa maana ni mimi niliyewatuma. Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi
ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani? Wakasema, Kornelio akida, mtu
mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi,
alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate
kusikiliza maneno kwako. Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili,
Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa
wakafuatana naye. Siku ya pili yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa
akiwangojea, hali amekusanya jamaa zake na rafiki zake. Petro alipokuwa
akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia. Lakini Petro
akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu. Na katika kusema naye
akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika. Akawaambia, Ninyi mnajua ya
kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala
kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi.
Kwa sababu hiyo nalikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani
mliloniitia? ”
Ukifuatilia
mafundisho hayo hapo juu utaweza kuona kuwa Mungu alikuwa akishughulika na
Petro, Petro alikuwa moja ya wanafunzi wakuu wa Yesu Kristo, alitembea na Yesu
kwa muda mrefu alifundishwa mambo kadhaa kuhusu ufalme wa Mungu, Lakini sasa
Mungu anamfundisha Petro kitu kingine cha ziada, Mungu anataka kuvunja mipaka
ya mila na desturi na kidini na kikabila na rangi, Mungu anakataa kila aina ya
ubaguzi, Petro hengekuwa radhi kuwahubiri watu wa mataifa mengine hata ama watu
hao wanamkubali Mungu, Ni dhambi kuwabagua watu kwa sababu yoyote ile, Mungu
hana upendeleo, Yesu aliwafundisha wayahudi kwenda zaidi ya mazoea yao
aliwaambia kuwa Mungu baba huwapa jua lake na mvua yake wema na wabaya,
Ni wazi
kuwa Mungu anakataa ubaguzi wa aina yoyote, Ulimwengu tulionao sio ulimwengu wa
Mtu mmoja , Ni kweli kuwa Mungu amefanya mataifa ya aina mbali mbali na ni
kweli kuwa Mungu ameumba watu kwa rangi mbalimbali, na ni kweli yako mataifa
yameendelea sana kuliko mengine, wako watu wamefanikiwa sana kuliko wengine
hata hivyo Mungu anataka watu wote wapewe huduma sawa na haki sawa, hakuna mtu
asiyestahili injili, Petro alitakiwa kutoa injili kwa kila mtu na hivyo alipaswa
aingilkiane na tamaduni nyingine na kuwafikishia habari njema
Leo hii
sehemu mbalimbali duniani zimekuwa na utamaduni huu wa kizamani sana wa kupiga
marufuku watu wa jamii fulani wasiingie eneo fulani, au wasihubiri au wasijenge
makanisa yako mataifa ya kidini na hayataki mtu wa dini nyingine aingie huko Makanisani
kumekuweko na ubaguzi wa kikabila, watu wa kabila fulani, wana wabagua watu wa
kabisa lingine, au wanadhani kuwa wao ndio wenye hati miliki ya Mungu, wengine
wanabagua watu wengine kwa sababu sio wa Dini yao, dhehebu lao, kabila lao nchi
yao n.k huu ni utamaduni uliopitwa na wakati Mungu yuko kinyume na “racism”
Mungu yuko kinyume na madaraja, Mungu yuko kinyume na aina yoyote ile ya
ubaguzi, Vilivyotakaswa na Mungu usibiite wewe Najisi.
Mifano ya Mashujaa waliosimama kupinga ubaguzi
duniani.
Mwaka 2007
Umoja wa mataifa uliitangaza rasmi kuwa tarehe 2 kila mwezi wa kumi itakuwa ni
siku ya Kimataifa ya Kutokufanya Fujo, hii ilitangazwa kwa kusudi la kuenzi na
kukumbuka mwanzilishi wa maandamano ya amani ajulikanaye kama Mahatma Ghandi
ambaye anajulikana kwa kuiletea India Uhuru, na aliyekuwa na ushawishi mku bwa
wa kuwavuta watu kwenye maandamano ya amani, bila fujo duniani dhidi ya ukoloni
wa Kiingereza bila chuki dhidi yao licha ya kuwa walifanya ukoloni nchini kwao
Rosa Parks
(1913–2005)
Rosa Louise Parks anafikiriwa kuwa Ndiye
mama wa siku ya haki duniani huko Marekani, Yeye alijipatia umaarufu mkubwa kwa
kukataa kupisha siti ya kwenye basi kwa mtu mweupe huko Alabama mwaka 1955,
Jambo lililopelekea kukamatwa kwake, swala la mgomo wa kutokuachia siti au
kuingia katika hoteli za watu weupe na kula kwa lazima lilianzia huko Montgomer
na kuanza kuenea nchi nzima na katika majimbo ya kusini, Ujasiri wa Rosa
ulimpatia umaarufu na kuanza kubadili mitazamo kuhusu watu weusi huko Marekani
na kuanza kubadilisha mtazamo wa kihistoria, Rosa alikuwa mwanaharakati hata
kabla ya kugoma kupisha siti ya basi kwa mzungu, Mwaka 1930 alimpigania kijana
mmoja wa mweusi kati ya vijana weusi tisa walioshitakiwa kwa uongo kwamba
walimbaka mwanamke mweupe ndani ya treni karibu na Scottboro, Alabama, Parks na
mumewe Raymon Parks walifanya kazi katika shirika la umoja watu wasio weupe
colored, Baadaye alihamia Detroit Michigan na kuwa shemasi katika kanisa la
Methodist la watu weusi, alipewa Udaktari wa Heshima kwa degree 43 na mwaka
1996 Rais Clinton alimpa medali ya Uhuru Medal of Freedom.
Nelson Mandela (1918–2013)
Mpinga ubaguzi na
mwana mapinduzi aliyeyahamasisha mataifa kupinga vitendo vya kibaguzi,
alifungwa kwa kusingiziwa kuwa alitaka kuipindua serikali ya kibaguzi na
kuwekwa kizuizini, Mataifa mengi yalipiga kelele kwaajili yake, Baada ya kukaa
Gerezani kwa miaka 27 aliachiliwa mnamo mwaka 1990, Miaka mitatu baadaye
alipewa nishani ya Amani ya Nobel Yeye
pamoja na rais FW. De Klerk kwa kazi yao kubwa waliyoifanya huko Africa ya
kusini ya kuutokomeza ubaguzi wa rangi na sera zake, Mwaka 1994 Mandela
alitawazwa kuwa rais wa kwanza Mweusi mpaka mwaka 1999 alipoamua kung’atuka,
kutokana na umaarufu wake alipewa Heshimamkama Baba wa taifa aliyeleta
Democrasia ya kweli, wengine walimuita mpigania uhuru na wengine walimuita
Mwokozi, wengine walisema Washingtona na Lincolin walioungana pamoja ndani
yake.
Jimmy Carter (1924–)
Rais wa 39 wa Marekani,
aliacha Ofisi yake 1980, Mwaka 1982 yeye
na mkewe Rosalynn alianzisha Carter Center
Huko Atlanta ambayo misingi yake ilikuwa ni kusimamia haki za binadamu
hususani wanaaonewa na kuteseka, akilenga kutatua migogoro na kupata ufumbuzi,
kukuza uhuru na demokrasia na kutunza afya za watu
Center
yake ilianzisha mfuko wa usimamizi wa uchaguzi na kufanikiwa kusimamia chaguzi
za mataifa mbalimbali katika chaguzi zaidi ya 94, alihusika katika uhamasishaji
na ukuzaji wa demokrasia katika inchi za Ethiopia, Eritrea, Liberia, Sudan,
Uganda, Korean Peninsula, Haiti, Bosnia
and Herzegovina, na Mashariki ya kati
Alijishughulisha
na watu wenye kichaa, na kutia moyo viwango vya haki za binadamu katika jumuia
za kimataifa, alipigia kelele dhidi ya uonevu wa mtu moja moja mwenye haki
duniani na kwaajili ya haya mwaka 2002 kituo chake kilipewa Nishani ya Nobel
kwaajili ya kazi yake muhimu ya kutatua migogoro ya kimataifa na kutunza haki
za binadamu, kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.
Martin Luther King Jr. (1929–1968)
Mchungaji wa
Marekani, aliyekuwa kiongozi wa Waamerika wenye asili ya Afrika wenye kupigania
haki na usawa, Alijulikana sana kwa uwezo wake mkubwa wenye ushawishi na nguvu
akipinga ubaguzi wa rangi Nchini Marekani, alijulikana sana kwa uwezo wake wa
kushawishi na kuongoza maanadamano ya amani ya kupinga ubaguzi, Mwaka 1955
alikomesha ubaguzi wa rangi ndani ya mabasi, ilikuwa kama mkipanda basin a
mwafrika amekaa akija Mzungu unampisha, Kwa kipindi cha miaka 11 tangu
1957-1968 Martin Luther King alitembea zaidi ya mile milioni sita, na
kuzungumza katika hutuba mara 2500, alijitokeza kila eneo ambalo maswala ya
haki na ubaguzi yalijitokeza na kupinga kivitendo, akiwa na umri wa miaka 35
Martin Luther King JR alikuwa kijana wa kwanza kupokea Nishani ya Nobel
kutokana na umahiri wake, aliuawa na waliompinga kwa kupigwa risasi 1968.
14th Dalai Lama (1935–)
Mtawa wa Kibudha na
kiongozi wa Kiroho wa Tibet, anaitwa Tenzin Gyatso au Dalai Lama wa 14 yeye pia
aliwahi kupata nishani ya Nobel mnamo mwaka 1989, kwaajili ya kuendeleza
mapambano yasiyo ya uasi akitetea uhuru wa Tibet, Ameweza kusimamia amani na
kupinga mambo bila kumwagika damu hata wakati wa maswala magumu au katikati ya
hali ngumu amekuwa
akijishughulisha huku na huku kuhamashisha amani na kutokana na umahiri wake
amepewa Udaktari wa Heshima mara 150 akisifiwa kwa jumbe zake zenye kuhamasisha
amani na usawa. Uelewa na uwezo wa kuchukuliana na watu wa dini nyingine na
imani tofauti, huruma na uvumilivu, ameandika vitabu zaidi ya 110, na ana
wafuasi zaidi ya milioni saba katika mtandao wa twiter duniani unaweza kuona @DalaiLama.
Hitimisho
Kwa ujumla
Mungu anataka walimwengu waishi kwa amani bila ubaguzi wa aina yoyote, Pale mtu
anapojifikiri kwa namna yoyote kuwa Bora ukweli unabaki kuwa mtu huyo amejivuna
tu, ana kiburi na Mungu yuko kinyume na mtu mwenye kiburi, Ili dunia iishi kwa
amani ni lazima watu wache mambo ya kijinga, Kabila lako halina maana isipokuwa
ya utambulisho tu kama lilivyo jina lako, dini yako haina maana isipokuwa
kuonyesha mtazamo wako kuhusu Mungu au itikadi yako namna unavyomuona au
husiana na Mungu, Utajiri wako hauna maana dhidi ya uwakili wa malia ambao
Mungu amekuzawadia ili kukupima namna utakavyoishi na wengine, akili zako na
cheo chako hakina maana dhidi ya dhamna a ambayo Mungu amekupa ili akupime
utaitumiaje kwa upendo kuelekea wengine, rangi yako haina maana wala uzuri wako
hauna maana kama utatumika kuwa alama ya kiburi na majivuno
Lazima watu
wajifunze upenda na kutenda haki na kusimama katika kweli kwa gharama yoyote
Paulo Mtume alipingwa sana kwa sababu eti alikuwa akihubiri injili kwa watu
wanaodhaniwa kuwa hawafai 1Wakoritho
16:5-9 Lakini yeye aliwaona Mataifa kama mlango unaofaa mkubwa kwa injili.
Mpango wa Mungu ni kuwa dunia yote ipate kumjua Mungu na kujawa na utukufu wake
huku amani ikitawala ni kwaajili ya haya Yesu Kristo alikuja Isaya 11:1-9.
Rev.
Innocent Kamote.
Mkuu wa
wajenzi mwenye Hekima.
0718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni