Andiko la Msingi: Mathayo 4:3-4 “Mjaribu
akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe
mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa
kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu”.
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Katika majaribu ambayo Yesu amewahi kupitia,
Jaribu la kugeuza mawe kuwa mkate lilikuwa limekaa vizuri sana katika kumtega
Bwana Yesu ili atende dhambi, Jaribu hili ndilo ambalo lilikuwa na uwezo mkubwa
sana wa kufanikiwa, kwa sababu Yesu alikuwa amethibitishwa wazi na hadharani tena na Mungu mwenyewe kuwa yeye
ni Mwana wa Mungu Mathayo 3:17 “na tazama,
sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa
naye.” Na Hapa ni kama anapewa wakati
muafaka na mzuri wa kuonyesha kwamba yeye kweli ni mwana wa Mungu ulikuwa ni
wakati sahihi kabisa kwanza kumuonyesha shetani kuwa yeye ni nani, pili alikuwa
na njaa tena amechoka,tena ana uhitaji, tena yuko peke yake, tena masikini, na
ana uwezo wa kufanya muujiza na zaidi ya yoteni Mwana wa Mungu na uhitaji
ulikuweko ilikuwa ni kama ujinga kwamba hutumii mamlaka kubwa uliyonayo hivi
ndivyo shetani alivyokuwa akimjaribu Yesu, Yesu kama mwana wa Mungu ilikuwa ana
wajibu wa kutoa amri tu au kutamka neno tu na kuonyesha nguvu zake na angefanya
kusingelikuwa na tatizo.
Yesu alikuwa na uelewa Mkubwa sana alitambua kabisa kuwa anajaribiwa kama
Adamu wa Kwanza, Ili apoteze kibali kwa Mungu, Yesu alijua kuwa anapaswa
kulitii Neno la Mungu, na kufuata maelekezo ya Roho Mtakatifu Mpaka dakika ya
mwisho, kwa vile ndiye aliyemuongoza ili ajaribiwe, Kama Yesu angeshindwa
wokovu ungekuwa wa taabu sana, Utii wake ulikuwa unapimwa kama ulivyopimwa wa
Adamu, Adamu alishindwa kulitii neno la Mungu, na hivyo akaleta mauti, Yesu
aliweza kulitii neno la Mungu na hivyo akaletauzima
Jibu la Yesu kwa kweli lilikuwa tamu sana “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa
kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu” wote tunafahamu umuhimu wa Chakula kwamba hakuna
uhai bila kula, tunajua kuwa hatuwezi kustahimili maisha na shughuli zetu za
kila siku bila chakula, au maswala yanayotupatia Chakula, Lakini Yesu
alionyesha kuwa Mwanadamu hataishi kwa chakula tu, kuna jambo lingine muhimu
zaidi ambalo ni neno la Mungu, ni muhimu tu kujiuliza kwa nini neno la Mungu ni
Muhimu? Kuliko chakula?
1.
Neno la Mungu
lina Nguvu, lina uwezo mkubwa sana kama Moto na uwezo mkubwa sana kama nyundo
ya kuvunjia mawe Yeremia 23:28-29 “Nabii aliye na
ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu
kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na
kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”Mungu anaonyesha ya kuwa
Neno lake lina nguvu, ili maisha yetu yaweze kufanikiwa ni muhimu kuzungumza
neno katika kila aina ya jaribu na mapito tunayoyapitia, tafuta neno la Mungu
na lizungumze katika hali yoyote inayokukabili, tunaweza kuikabili haliyoyote
ile katika kwa kulitamkia neno.
2. Neno la Mungu ni Upanga wa kiroho Waebrania 4:12
“Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina
ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya
nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua
mawazo na makusudi ya moyo.”Neno la Mungu linasifiwa hapa kuwa lina
UHAI, LINA MGUVU, KALI KULIKO UPANGA UKATAO KUWILI,LINACHOMA, LINAWEZA
KUGAWANYA NAFSI, ROHO, VIUNGO, NA MOYO
Hivyo linaweza kutumika kuzima mishale yote ya adui na kila elimu
inayojiinua na Elimu ya Utukufu wa Mungu
3. Neno la Mungu ni kweli, Ukweli ni silaha yenye nguvu
kuliko silaha zozote, Shetani hutumia uongo kutushambulia lakini kweli ina
nguvu, kweli ni silaha kuu kwa mujibu wa Maandiko,Waefeso 6:10-14 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa
nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme
na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu
wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana
siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali
mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani” Kama
tunataka kuwa washindi wakati wote na kupata matokeo yaliyo thabiti hatuna budi
kuhakikisha kuwa tunasimama katika kweli ya Neno la Mungu, Neno la Mungu lina
uwezo wa kutakasa na kumfanya mtu wa Mungu akamilike Yohana 15:3, 17:17
4. Neno la Mungu ni Roho tena ni uzima Yohana 6:63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo
niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”Yesu alikuwa akimaanisha kuwa
Neno analotupa yeye lina uzweza linanufaisha roho na sio mwili, Torati ya Musa
ilikuwa na manufaa ya kimwili lakini Maneno na mafundisho ya Kristo yana
nufaisha roho yana uzima ndani yake, Biblia inaonyesha ya kuwa kila kitu
kitapia lakini neno la Mungu litasimama milele, ni neno la Milele, Kila mtu
anayetaka kufanikiwa katika jambo lolote anapaswa kuliishi neno, kuliangalia
neno, kulitazama neno, katika mazingira yoyote ishi kwa neno, Acha kuangalia
nafasi uliyonayo, uanafunzi ulionao, cheo ulicho nacho akili ulizo nazo, Uzima
wetu umewekwa katika neno, likitumika kwa halali shetani anajua kuwa lina nguvu
na analiogopa neno.
Hitimisho:
Kama Yesu angetii maneno ya shetani na kugeuza mawe kuwa mkate maana yake
angekuwa amelikataa neno la Mungu sawa na adamu na angekuwa ameyakubali maneno
ya shetani kama Eva
Kila mmoja wetu anapaswa kuishi sawasawa na neno la Mungu, kila siku
hatuna budi kuishi na sawa na neno la Mungu, Chakula cha siku moja tu
kinatosheleza mahitaji ya mwili usio wa Milele lakini neno la Mungu
linautoshelevu wa milele, Liseme neno. Liishi neno. Lihubiri neno litumikie
neno, litendee kazi neno, liamini neno, litumie neno la MUngu na utaona faida
kubwa sana katika maisha yetu, Mtu hataishi kwa Mkate tu Bali kwa kila neno
litokalo katika Kinywa cha Mungu.
Ushindi wa Yesu Kristo ulitokana na ufahamu wa neno, maisha yetu na
mafanikio yetu yamefungwa katika neno Yoshua 1:5-8 Biblia inasema “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku
zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa
pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa,
maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya
kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na
sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume,
au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali
yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na
maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha
ndipo utakapositawi sana.”
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni