Mathayo 17:14-20 “Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia
magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa
vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa
wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, ENYI KIZAZI
KISICHOAMINI, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana
nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu.
Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile.
Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi
hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa
maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia
mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno
lisilowezekana kwenu.”
Imani binafsi ambayo
haionekani kufanya kitu wakati wa matatizo hiyo sio Imani sahihi –W.
Willberfoce
Utangulizi:
Mungu anamtarajia kila mwanadamu,
aliyeitwa naye kuwa mwenye uwezo wa kuleta suluhu kwa matatizo yanayoizunguka
jamii yake, Kusudi kubwa la Mungu kulichagua kanisa ilikuwa ili kanisa liweze
kuwa na majibu ya changamoto zote katika jamii, Mungu anataka watu wenye
uhodari, wanaoweza kutatua matatizo yanayoikabili jamii, alipokaa na wanafunzi
wake alikuwa na matarajio ya jinsi hii hii, Lakini kama ilivyo kwa jamii ya leo
na kanisa la leo, Wanafunzi wake pia walishindwa kutatua na kumaliza changamoto
zilizowasilishwa kwao na mtu mmoja katika jamii.
Katika Mistari ya msingi tunaona Wanafunzi
wa Yesu wanaletewa kijana wa Pekee na Mzee mmoja, kijana huyu anateswa na
Mapepo na kumtupa kila wakati, na ni lazima alimjeruhi, Baba wa mtoto ameingiwa
na mashaka makubwa kwani anakosa tumaini anaona atapoteza kijana wake wa pekee
ambaye shetani anamsumbua, Swala hili linatokea kuwa kitu cha kusikitisha kwa
wanafunzi wa Yesu na inakuwa ni aibu kuwa wanashindwa kutatua tatizo hili, Yesu
hakuweko karibu wakati huu alikuwa pamoja na wanafunzi watatu Petro, Yakobo na
Yohana, Hivyo wanafunzi tisa wanajaribu
kutoa pepo wanashindwa hii ilikuwa mbele ya umati mkubwa wa watu, Tatizo
halikuwa jipya kwa vile Walikutana na changamoto kama hii na Yesu aliitatua
Marko 1:23-27 “Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao
mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa
Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu
akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa,
akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema,
Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao
wamtii!” na pia Marko 5:1-9 “Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya
Wagerasi. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye
ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;
makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza
kumfunga tena, hata kwa minyororo;kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa
pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala
hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Na sikuzote, usiku na mchana,
alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. Na
alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina
nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa
sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina
langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi”
Lakini vilevile Yesu alishawapa
Mamlaka ya kufanya kazi hii Mathayo 10:1, Lakini hapa wanashindwa, Yesu
anatokea na kila mmoja ana furaha kwani Yesu aliweza kutatua tatizo, lakini
wanafunzi wa Yesu hawakuweza kutatua tatizo lililokuweko, Swali kuu linazaliwa
nao, Yesu anajibu kwa kukemea Enyi kizazi kisichoamiana.
Kwanini sisi hatukuweza kumtoa?
Yesu hakuwaambia kuwa tatizo liko
kwenye mioyo yenu, Tatizo haikuwa kwamba kuna kanuni fulani haijatumika, Maana
wengine mpaka wayaimbie Pambio mapepo kwanza, Tatizo sio kuwa hawakuwa na
bidii, au kuwa hawana uzoefu, au hawakujaribu sana, wala sio kwa sababu
hawakuwa na nguvu za uuongu ndani yao hapana, Yesu anawaambia ni” kwa sababu ya
Upungufu wa Imani yenu”
Math 17:20 “Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu.
Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali
mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako
neno lisilowezekana kwenu.”
Kanisa linapaswa kuelewa kanuni
za utendaji wa Mungu
1. Mungu hufanya miitikio yeke kwa Mtu
anayemwamini, watu wanaomwamini Mungu wanaitwa “Risk takers” watu wenye
uwezo wa kufanya maamuzi magumu, ni wenye ujasiri wa kutatua matatizo pasipo
hofu ni watu ambao hawana shaka ni watu ambao wanamuamini Mungu na uwezo wake
na hivyo kuchukua hatua za hatarishi, Ibrahimu, Musa, Joshua, Daniel na wengine
wote walimuamini Mungu Waebrania 11:6
Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Neno la Mungu linasema Waebrania 11:6 “Lakini pasipo
imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini
kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”
2.
Mungu
anataka tumuamini na kumtegemea Kama tunataka kuona kazi zake zikitendeka
kwetu
haijalishi tatizo ni baya kiasi gani au kubwa kiasi gani lakini nini
kinaendelea moyoni mwako? Kinachoendelea ndani yako ni cha muhimu kuliko
kinachotokea nje yako, Moyo wako unakuawaje unapokutana na changamoto, je
unaogopa? Au una ujasiri ukijua kuwa Mungu yuko pamoja nawe hupaswi kuogopa,
Yesu hajali ukuu wa tatizo, kuwa limeanza tangu utoto, au ni la ukoo mzima au
limelishinda taifa zima Yesu haogopi hilo wala haangalii hilo, haijalishi
Madaktari wanasemaje, Mzee alipomuona Yesu alimwambia ukiweza unaweza kutusaidia,
Yesu alishangazwa na mashaka makubwa aliyokuwa nayo baba yule, kweli ilikuwa ni
kizazi kisichoamini, Ukiweza? Yesu alimjibu Yote yawezekana kwake aaminiye Marko 9:22-23 “Na
mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza
neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia. Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote
yawezekana kwake aaminiye”.
3. Mzee aliomba Naamini nisaidie kutokuamini
kwangu, zinapotokea changamoto, hatupaswi kuangalia ukubwa wa changamoto, uweza wa changamoto au muda wa changamoto bali
tunapaswa kumsihi Mungu atuongezee imani aondoe mashaka ndani yetu, wakati
tunapokabiliana na changamoto zozote acha kuwaangalia wanadamu, acha kuangalia
ukubwa wa tatizo, acha kuangalia umati wa watu, acha kufadhaika Muamini Mungu
muamini na Bwana Yesu kila kitu kitakuwa shwari.
4. Ni imani kiasi gani inahitajika kwetu? Kimsingi
kwa vile tatizo lilikuwa kubwa na lina historia ya kutisha basi wanafunzi
walifikiri wanahitaji kuwa na imani kubwa sana
na hivyo labda jibu sahihi la Yesu lingekuwa kwamba kwa vile tatizo ni
kubwa basi mnahitaji imani kubwa sana au kuongezewa imani, Lakini ni dhahiri
wanafunzi wa Yesu na hata mzee yule hawakuwa na imani kabisa, walijifikiri kuwa
wao ni watu maalumu, Yesu alisisitiza kuwa na imani na sio kuhusu size au
kipimo cha imani, Ni lazima tumuamini Mungu kwa kiwango cha juu sana na kuacha
kujiamini sisi, tusiangalie umaarufu wa dhehebu letu, muda wa kutembea na Yesu,
umaalumu wa aina ya huduma uliyo nayo, uzoefu katika huduma, uwezo wetu wa
kumtii Mungu au sheria za Mungu bali namna na jinsi unavyomtegemea Mungu chini
ya neema yake, Lazima tumwangalie yeye kwa kuwa yeye Hashindwi kitu Luka 1:37 “kwa
kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”
Enyi Kizazi kisichoamini.
Mara nyingi
tunaweza kuona kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kizazi kilichopita na kizazi cha
leo kwa sababu ya imani, Inaonekana kama Mungu aliwatumia sana wazee wetu
kuliko anavyotumia watu leo, Matamanio ya Mungu ni kuona watu wakimtumaini
Mungu kwa uzito zaidi nyakati za leo na kutumiwa na Mungu kwa kiwango kikubwa
katika nyakati za leo kuliko zamani, lakini shida Kubwa ni Hiki kizazi
kisichoamini, Yesu alikemea Enyi Kizazi kisichoamini, Mungu anajua kuwa
matatizo ya dunia hii na shuda zinazoukabili ulimwengu zinaweza kutatuliwa na
watu waliamuamini na wanaomtumaini Mungu sio katika kutoa pepo tu bali kutatua
matatizo ya wanadamu.
-
William
Wilberforce – Alizaliwa 24 August 1759 – 29 July 1833 alikuwa
mwanasiasa huko Uingereza na alijulikana kama kiongozi mwenye ushawishi
aliyeendesha mpango wa kukomesha Biashara ya utumwa, alikuwa ni mbunge wa jimbo
la Yorkshire kati ya mwaka 1784 – 1812, mwaka 1785 aliokoka na kumuamini Yesu kuwa Bwana na Mwokozi, jambo ambalo
lilimpelekea kubadilika kabisa katika mtazamo wake wa maisha na kusukumwa katika kupinga na kukomesha
biashara ya utumwa, alipata elimu yake katika chuo cha ST Johns College cha
Cambridge.
-
Elisha
aliweza kutatua Matatizo ya Mjane mmoja katika jamii yake na kukomesha kabisa
tatizo lililokuwepo kwa Neema ya Mungu “ 2Wafalme 4:1-7”
-
Dunia ina matatizo Mengi yanayohitaji ufumbuzi
leo, Utunzaji wa Mazingira, Matumizi
mazuri ya ardhi, uwepo wa kemikali hatarishi, ugaidi, magonjwa,
umasikini, shida za kisiasa, uongozi, uchumi, maji, ukame, ubaguzi, mauaji,
kutekwa, ujangili, wizi, ujambazi, uchawi, uadui, Mafarakano, talaka, watoto wa
mitaani, Elimu duni, picha za ngono, na kadhalika, Yesu anataka watu wote
wamuamini Mungu na kutumia uhusiano walio nao nay eye kwa imani katika kutatua
matatizo ya watu, Hatuwezi kumtumia yesu Kristo kwa kutafuta umaarufu naye
akakubali, Kila msomi anayesoma shule ya seminary anapaswa kuwa mtu atakayekuja
kutatua matatizo ulimwenguni na kuleta mabadiliko kwa jina la Yesu.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni