Jumatatu, 30 Julai 2018

Furaha timilifu!

Mstari wa Msingi: Yohana 16: 23 -24 Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; FURAHA YENU IWE TIMILIFU.”

 Je wewe hutegemea hali ya nje kama chanzo cha Furaha maishani mwako? Angalia kwamba Mungu ndio chanzo kikubwa cha furaha timilifu na sio vinginevyo

Utangulizi:

Maisha ya mwanadamu yanategemea sana kuwa na furaha ili yawe maisha, na mwanadamu siku zote anafanya kila kitu kwaajili ya furaha yake tuu. Furaha ndio kilele cha maisha ya mwanadamu, kila analolifanya mwanadamu lengo lake kuu ni kupata furaha.

Mathalani ukitoa msaada kwa mtu moyo huwa na furaha, ukipongezwa au kusifiwa kwa jambo fulani moyo huwa na furaha, ukiwa mshika ibada moyo huwa na furaha, ukiwa na mke mwema au mume mwema moyo huwa na furaha vilevile, ukiwa na watoto wazuri na wenye adabu na kujiheshimu, ukifanya kazi kwa ufanisi, ukipata malipo ya kazi yako au mshahara moyo huwa na furaha kadhalika, ukisikiliza mziki au filam ama picha na hata kusoma vitabu moyo huwa na furaha pia, Ukiwa na mafanikio makubwa, ukijenga nyumba, ukiwa na mashamba, ukinunua gari, ukipandishwa cheo, ukichumbiwa, ukiolewa, ukizaa mtoto, ukiwa na afya njema moyo huwa na furaha, ukipewa tuzo, ukishinda uchaguzi, ukimiliki kampuni na kufanikiwa Moyo huwa na furaha Lakini pamoja na hayo yooote bado utaweza kuona kuwa hakuna furaha iliyo timilifu, Je ni wapi tunaweza kuona na kuwa na furaha timilifu? 

Furaha nini?

Ni vigumu sana kuielezea furaha zaidi ya neno lenyewe furaha, Katika kiingereza neno linalotumika kuelezea furaha ni “JOY” ambalo katika lugha ya kiyunani ni “CHARA” linatamkwa “KHA-RAH” ambalo maana yake ni Hali ya kujaa raha katika nafsi kutokana na kufikia au kufanikiwa katika jambo fulani, hali ya kuwa na raha isiyo na mipaka kutokana na kutoshelezwa kwa nafsi.

Katika imani ya Kikristo tunaweza kusema ni Raha ya nafsi ndani ya mwamini anayopipata kama matokeo ya Neema na upendo wa Roho Mtakatifu kumuwezesha mtu huyo, kufurahia kuwa na uhusiano na Mungu na kumjua Yesu Kristo, Neno lake na makusudi yake na tumaini lililo ndani yake.

Je ni watu wangapi wana furaha?

Ukiulizwa swali je una furaha je unaweza kulijibu vipi? Ni swali gumu sana, kwani unaweza ukawa una furaha lakini unafahamu kuwa furaha hiyo haidumu milele. Labda una furaha kutokana na kuwa una familia nzuri, lakini kwa kina utaona kuwa furaha hiyo inategemea uwepo wa familia nzuri, na uwepo huo ukitenganishwa kwa vifo, maisha, mabadiliko mbalimbali basi furaha yake nayo inaisha. Hivyo kuna furaha za milele na furaha ya muda mfupi.

Kila mtu anapenda kuwa na furaha, na lengo kuu la maisha ni kuwa na furaha. Hata hivyo furaha ya watu wengi sana sio furaha timilifu kwa sababu furaha zao zinatawaliwa na hali ya nje ya maisha yao angalia mfano huu:-

Mtu moja alikuwa anamiliki nyumba nzuri sana ni nyumba ya thamani na ilikuwa yenye kupendeza na yenye mvuto mkubwa sana katika mji aliokuwa anaishi, na jamaa huyu aliipenda nyumba yake sana watu wengi waliwahi kumuendea na kumuomba awauzie hata kwa bei kubwa mara mbili ya thamani yake lakini alikataa, wakati fulani bwana huyu alisafiri na aliporejea aliikuta nyumba yake ikiwa inawaka moto mkubwa sana na hivyo alipatwa na huzuni kubwa mno! Mamia ya watu walikusanyika kwaajili ya kuangalia namna ya kusaidia kuuzima moto ule, lakini hakuna walichofanikiwa kukiokoa katika moto ule

Mara mwanae mkubwa alimjia na kumnongoneza sikioni, Baba usiogope, “Niliiuza nyumba hii jana na niliiuza kwa bei nzuri sana, bei ilikuwa nzuri kiasi ambacho nisingeliweza kukusubiri au kukutaarifu, Hivyo unisamehe bure tu baba”

Baba yule alivuta pumzi na kuzishusha akimshukuru Mungu kwani sasa amekuwa moja ya washuhudiaji wa ajali ile kama walivyo wengine,

Mara mwanae wa pili alikuja mbio akimkimbilia na kumbwambia baba unafanya nini uangalia nyumba yetu ikiwa inaungua? Baba alimjibu kijana yule kuwa tulia kwani kaka yako aliiuza tayari kwa bei nzuri, Kija ayule alimwambia baba yake kuwa tulichukua kiwango fulani tu cha fedha na sio zote hivyo nina mashaka kama yule aliyenunua atakubali kumalizia ilihali nyumba imeungua!
Yule baba alianza kulia tena, machozi ambayo mwanzoni alikuwa ameshasahau,Moyo wake ulianza kwenda mbio sana na nguvu zikaanza kumuishia alikuwa mwenye huzini kubwa sana, Mara mtoto wake wa tatu akaja na kumwambie Baba yule mtu aliyenunua nyumba yetu ni mtu mwema na mwaminifu na mwenye kutunza sana ahadi kwani nimetoka kuongea naye sasa na ameniambia “ Haijalishi kwamba nyumba imeungua au la Nyumba ni yangu na nitalipa kiwango chote cha fedha tulichopatana, kwa kuwa hakuna aliyejua kuwa nyumba itaungua, Kisha wote wakasimama wakiwa wametulia kama washuhudiaji wengine wakiangalia nyumba inayoungua bila wasiwasi wowote!
Tunajifunza nini kutokana na kisa hiki? Watu wengi sana wanajisikia kuwa wenye furaha kutokana na hali ya nje ya mambo na sio ya ndani na kwa sababu hiyo hawawezi kuwa na furaha ya kweli, furaha ya kibinadamu ya ya dunia hii ni yenye kuyumba kutokana na hali halisi ya kubadilika badilika kwa mambo, aidha furaha ya kweli haipatikani kwa kuwakosea wengine.

Wako watu wengine wanafikiri kuwa watakuwa wenye furaha kwa sababu ya kukandamiza wengine, kuwatesa, kuwatendea vibaya, kuwashitaki, kuwasengenya, na kuwakosea ni muhimu kufahamu kuwa watu wote wanahitaji furaha kwa sababu hiyo kama huwezi kuwasaidia wengine kuwa wenye furaha basi jitahidi usiwe sababu ya huzuni zao, furaha ya kweli hua kwa kuhakikisha kuwa wengine wana furaha kama wewe na sio kuwakosea. 

Faida za kuwa na furaha timilifu

Kwa mujibu wa wataalamu wa maswala ya saikolojia wanaeleza kuwa furaha ina faida kubwa sana
Zikiwemo

a. Inakulinda na magonjwa ya Moyo
b. Inaimarisha kinga za mwili
c. Inatupilia nje mikandamizo ya mawazo katika maisha
d. Inakulinda dhidi ya Magonjwa
e. Inarefusha maisha

Kitaalamu hata utungiswaji wa Mimba hutokea siku ambayo wana ndoa wote wamefurahi
Unawezaje kuwa na Furaha timilifu?

Kaa katika uwepo wa Mungu Zaburi 16:11Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.” Unaweza kuona maneno Mbele za uso wako ziko furaha tele yanamaanisha mbele za uwepo wa Mungu “Presence” kuna furaha tele, Musa alikuwa ni mtu aliyependa kukaa katika uwepo wa Mungu, alikaa uweponi mwa Munngu kiasi ambacho hakusikia njaa kwa siku 40 na hata aliporejea uso wake ulikuwa unangaa’ kiasi ambacho watu walishindwa kumtazama Kutoka 34:29-35Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao. Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo BWANA amemwambia katika mlima Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake. Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za BWANA kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa. Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.”

Usitawaliwe na hali ya nje.

Habakuki 3:17-18Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe; Walakini nitamfurahia Bwana Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.” Kwa mujibu wa Habakuki ni kuwa yeye atamfurahi Mungu bila kujali kuwa mtini haujachanua maua, au zabibu hazina matunda aku mzaituni haukuzaa au mashamba hayakutoa chakula au mazizi mifugo kutokuwa na kitu, Yeye bado atafurahi, hii ni wazi kuwa Mungu ndio chanzo cha furaha yetu na sio vinginevyo.

Dumu katika kuomba.

Kwa mujibu wa Yesu Kristo ukweli ni kuwa maombi yanasaidia kwa kiwango kikubwa sana kuketa firaha timilifu, kila amtu anapaswa kuomba, maombi ni muhimu sana, usiache kuomba Yohana 16: 23 -24Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; FURAHA YENU IWE TIMILIFU.”

Mwamini Mungu na Kumtegemea.

Warumi 15:13Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu.”, Imani katika Mungu na kumtegemea yeye kunaweza kutupa furaha timilifu.

Watumikie wengine Watu wanaowatumikia wengine huwa na furaha sana Duniani.

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Rev. Innocent Kamote

Hakuna maoni: