Alhamisi, 30 Agosti 2018

Maisha Bila Mipaka!


Warumi 8:38 -39.Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,  wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”


Utangulizi:

Nick Vujicic ni moja ya walemavu ambaye alizaliwa akiwa hana miguu wala mikono na wataalamu wa kitabibu walishindwa kuelewa sababu kuu ya ulemavu wake na hata namna ya kumtibu, lakini kwa sasa amejipatia umaarufu mkubwa sana duniani kutokana na bidii kubwa aliyo nayo na mafanikio makubwa sana katika maisha akiwa hana viungo hivyo muhimu yeye mwenyewe anasema Namnukuu  I was born without arms or legs and given no medical reason for this condition. Faced with countless challenges and obstacles, God has given me the strength to surmount what others might call impossible.” “Nalizaliwa pasi na mikono wala miguu na sikupewa sababu za kitabibu za kuzaliwa hivyo, Nimekumbana na changamoto nyingi na vikwazo, Mungu amenitia nguvu kupambana na hali ngumu ambazo wengine walizishindwa” Ni mwanzilishi wa shirika liitwalo Life without Limbs na Mwinjilisi mkubwa sana Duniani na pia ni Motivational speaker  ambaye aliweza kupitia vikwazo na magumu na kuvishinda kwa nguvu na tumaini lililo katika Kristo Yesu.

Siri kubwa ya mafanikio ya Mlemavu huyu Duniani ni “Mungu alimtia Nguvu” Kumbe kwa Mungu hakuna lisilowezekana, tunaishi katika misuguano na kujikuta tumezingirwa na mipaka pande zote dunia ikikulazimisha kusalimu amri na kuishia hapo ulipoishia au hapo ulipokatia tamaa kwa sababu hujatambua chanzo  cha nguvu zako, kwa hiyo dunia na mazingira na vikwazo vimekukwamisha hapo ulipo umeambiwa haiwezekani, haitowezekana, huwezi lolote, hustahili kitu hutoweza, ndugu zako walishindwa, Mfupa uliomshinda fisi wewe mbwa utauweza wapi.

Siri ya mafanikio.

Siri ya mafanikio ya watu kama kina Nick Vujicic  na wengineo ambao tunawasoma katika maandiko ni NGUVU ZA MUNGU nyuma ya maisha yao, Maandiko ni ufunuo wa Nguvu za Mungu, unaposoma na kuona shuhuda za watu kama kina Yusufu kutoka gerezani na kuwa mtu mwenye mamlaka kubwa duniani ni Matokeo ya Nguvu za Mungu, Unaposoma habari za kusisimua za kina Daniel na Hekima kubwa walizokuwa nazo na uwezo mkubwa katika kupambanua mambo ni kuwa siri kubwa ni Nguvu za Mungu, Roho wa Mungu alikuwa juu yake, hii ndio siri iliyowafanya waonekane kuwa ni wa kipekee.

Kila mtu Duniani Mungu alimuumba kwa kusudi, na moja ya kusudi la kuumbwa kwako ni ili ufanikiwe na kuwa Baraka kubwa kwa wengine pia, Lakini ni nguvu ya Mungu kiasi gani unayohitaji ndiyo itakayoamua hatima ya maisha yako, wengi tunaishi maisha yenye mipaka Lakini Mungu hakukusudia iwe hiyo! Hata kidogo, Mungu ametupa Nyenzo ya kutusaidia kufikia kiwango kikubwa na cha juu cha mafanikio Nguvu hizo ni Roho Mtakatifu.

·         Mwanzo 41:38-40Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”

·         Daniel 5:10-12Basi malkia, kwa sababu ya maneno ya mfalme na ya wakuu wake, akaingia katika nyumba ya karamu; malkia akanena, akasema, Ee mfalme, uishi milele; fikira zako zisikufadhaishe; wala uso wako usibadilike. Yuko mtu katika ufalme wako, ambaye roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yake; na katika siku za baba yako nuru na ufahamu na hekima zilionekana ndani yake; na mfalme Nebukadreza, baba yako, naam, mfalme, baba yako, akamfanya kuwa mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu;      kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na kufungua mafundo, zilionekana katika Danieli huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danieli, naye ataionyesha tafsiri.” 

·         1Wakoritho 2:4-5Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu,  ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu”.

     Paulo hakuhubiri Falsafa, hakutumia ushawishi wa kiakili lakini alifanikiwa sana katika injili kuliko wote kwa sababu alikuwa na Nguvu za Mungu

Kuishi bila Nguvu za Mungu ni kujiweka katika hatari kubwa sana, lakini ili tuweze kuwa washindi ni lazima tuishi katika uwepo na nguvu za Mungu, Mungu alituleta Duniani kama watu maalumu, alitukomboa ili tuwe Makuhani na Wafalme na watawala wa Dunia Ufunuo 5:10ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.” Mwanadamu ni kiumbe cha thamani sana, Mungu amewadhimisha wanadamu kuliko malaika lakini ili tuweze kuwa na mafanikio Duniani na kuitawala kama wafalme na makuhani hatuna budi kujiungamanisha na Nguvu za Mungu, Mungu hafurahii kutuona tukiishi kwa mipaka kwa ujumla hatukuumbwa ili tuje kuteseka na kufungiwa duniani bali Mungu alikusudia tuitawale dunia na kila kilichomo Haya yanawezekana tu kama tutajiachilia katika nguvu za Mungu na Roho wake hakuna jambo litakaloshindikana kwetu Zekaria 4:6-7.Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”  Unaweza kuona sasa kama tunasumbuka katika Dunia hii, tumejawa hofu, tumejawa kukata tamaa, tumepoteza ujasiri, tunalia, tunaugua, tunaonewa kuna kitu hakiko sawa ni kwamba hatujatambua kuwa sisi ni akina nani na Mungu ametuandalia Nini? Yesu alianza kupata umaarufu mkubwa mara moja tu alipokaliwa na Roho wa Mungu na kumruhusu aongoze maisha yake 

Luka 4:1Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani14 Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando.” 

Yesu anarejea akiwa amejaa nguvu za Mungu, na tangu tukio hili utaweza kuona umaarufu wake ulienea katika nchi zote za kandokando ya Israel, Wanafunzi wa Yesu walikuwa waoga walijifungia chumbani kwa siku kadhaa lakini alipokuja Roho Mtakatifu mambo yalibadilika waliupindua ulimwengu, Bila Roho Mtakatifu, bila neema na bila nguvu za Mungu tutaendelea kuwa wanyonge na kuishi katika kiwango cha chini cha maisha bila mafanikio na maisha yenye mipaka mingi.

Katika Warumi 8:38-39Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,  wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Paulo Mtume anazungumza kwa ujasiri unaotokana na uzoefu wake akikazia kwa msisitizo mkubwa sana wa imani ya kitume kuwa yeye sasa kutokana na Mambo ambayo Mungu amemfunulia, kutokana na jinsi Mungu alivyoufunua upendo wake kwetu, yeye pamoja na wengine wote wenye kuamini Hakuna kitu kinaweza kututenga na upendo wa Kristo, Hili halitokani tu na ufunuo mkubwa alioupata bali kazi kubwa ambayo Mungu amewatendea wanadamu, kwa kutuchagua, kwa kutufanya kuwa wana wake, ametambua kuna usalama Mkubwa katika Kristo na kuwa ni vigumu sana jambo lingine lolote kupingana na kusudi la Mungu, hivyo yote yanayoogopewa na wanadamu hayawezi kuwa mpaka wa kututenganisha na Mungu

·         Kifo hakina ubavu – Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Maisha hayana ubavu– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Mamlaka hazina ubavu– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Serikali hazina ubavu– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Malaika au mashetani – Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Mamlaka na falme– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Mambo yaliyopo yaani sasa na yajayo– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake

Kama Nick ameweza kufanikiwa na hakuzaliwa akiwa na mikono wala miguu, bali kwa nguvu za Mungu ameweza kuwa mtu maarufu Duniani na kufanikiwa katika kuwatia moyo wengine wote, wanaofikiri kuwa wao si kitu, wanaofikiri kuwa hawawezi, Maandiko yanatutaka tuinue macho yetu na kumuangalia Mungu Nguvu zake zinatosha kutupeleka katika level nyingine na kutufanya tufanye mambo yasiyokuwa ya kawaida, Hakuna sababu ya kukata tamaa, tuitafute Nguvu ya Mungu, tuutafute upako na kufanya kazi zetu kwa bidii hakuna kitakachoweza kusimama na kuzuia kusudio la Mungu katika maisha yako, usikubali kukatishwa tamaa, usikubali hata kujikatisha tamaa, usikubali maneno yaliyonenwa juu yako, wao sio Mungu yuko Mungu mwenye uweza usio na mipaka hakuna wa kukuwekea mpaka Mungu amekupa uhuru wa kuyafurahi maisha katika nguvu zake, kaa katika hizo na utafurahia sana. Ziko sababu za kuishi maisha yasiyo na mipaka kutokana na upendo mkubwa sana wa Mungu wetu na mambo ambayo ametukarimia.

1.       Hakuna hukumu ya adhabu Rumi 8:1
2.       Roho wa aliyemfufua Kristo anaishi ndani yetu 11
3.       Roho anatuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa 26
4.       Mungu yuko upande wetu 31
5.       Aliweza kumtoa Yesu kwaajili yetu 32
6.       Hakuna wa kuwashitaki wateule 33
7.       Sisi ni washindi na zaidi ya kushinda 37

Nakuombea Mungu akuvike Nguvu zake ili usiishi katika mipaka uliyowekewa au kujiwekea Bali ujae nguvu za Mungu na uweza wake

Na. Mkuuwa wajenzi mwenye Hekima.
Rev. Innocent Kamote.

Jumatano, 29 Agosti 2018

Habari za Mapito ya Zamani!


Yeremia 6:16Bwana asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo.”



Kama Jamii yoyote itapoteza Historia, maana yake imepoteza Muelekeo” Rev Innocent Kamote Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Utangulizi. 

Ni muhimu kufahamu kuwa Maisha yetu hayawezi kuwa na furaha ya kweli kama mara kwa mara hatutajifunza kutokana na Historia, Historia ni mwalimu mkubwa sana wa kutusaidia kujua tunatoka wapi na tuko wapi na tunakwenda wapi, “Kama jamii yoyote itapoteza Historia, maana yake itapoteza muelekeo” Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima, Kwa msingi huo kuna umuhimu wa kujifunza kutokana na Historia, semi kadhaa za Kihistoria zinatusaidia kujua umuhimu wake
·         Historia sio mzigo katika kumbukumbu zetu bali ni Mwangaza wa Nafsi zetu lord Acton- History is not a burden on the memory but an illumination of the soul – Lord Action.
·         Mtu asiyejali Historia ni sawa na Kiziwi ni sawa na kipofu – Aldof Hittler  The man who has no sense of history, is like a man who has no ears or eyes. Adolf Hitler
·         Baada ya kufanya makosa au kuteseka, na kupoteza muelekeo Mtu mwenye akili huangalia nyayo zake – Napoleon - After making a mistake or suffering a misfortune, the man of genius always gets back on his feet. Napoleon
·         Tunasoma kutokakatika Historia kile ambacho Hatujakisoma katika Historia – Desmond Tutu - We learn from history that we don’t learn from history! Desmond Tutu
·         Raia wenzangu, Hatuwezi kuiepuka Historia Abrahamu Lincoln - Fellow citizens, we cannot escape history. Abraham Lincoln

Kama tunavyoweza kuona hapo juu, umuhimu wa Historia ni wazi kuwa neno la Mungu pia limeandikwa kwa makusudi ya kutukumbusha na kutufundisha kutokana na Historia Biblia inasema hivi :-  

1Wakoritho 10:1-11Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.” Kumbe kila mmoja anaweza kujifunza kitu kutokana na Historia.

Katika kifungu cha maandiko Yeremia 6:16 Mungu anatoa wito kwa wana wa Israel, yaani wayahudi kuuliza kwa habari za mapito ya zamani, yaani katika wakati huu kulikuwa na ukengeufu mkubwa na mmomonyoko mkubwa wa uadilifum watu walikuwa wakifuata njia zao wenyewe na hivyo walipoteza raha na amani ya kweli, Taifa, Kanisa, Jamii na kila mmoja anapaswa kuangalia njia zake na kujifunza kutokana na Historian a kuangalia njia za Zamani na kujikagua kama tuko sahihi au lah nini kimepoteza furaha tuliyokuwa nayo, ka sababu gani tupo hapo tulipo? Kwa nini hilo au lile linatokea? Nabii Yeremia alitumwa na Mungu kuwakubusha wayahudi kuifuata njia ile ili waweze kufanikiwa  

Yeremia 7:22-23Maana sikusema na baba zenu, wala sikuwaamuru kwa habari za sadaka za kuteketezwa na dhabihu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri; lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa.”       

Unaweza kuona iko njia ya mafanikio ambayo Mungu aliwaonyesha Israel Tangu zamani lakini wao walikuwa wamekaidi kuifuata na hivyo maisha yao yalijaa taabu na kukosa raha na amani,  Hakuna namna yoyote ambayo tunaweza kuwa na amani ya kweli endapo tutakuwa nje ya njia ya kweli au kama tumeiacha njia ya Mungu, Kama Mungu anatupenda kwa dhati anachokifanya ni kuwatuma watumishi wake manabii wake kutukumbusha kurudi katika njia, Mungu anataka watu wake wajifunze kutokana na Historia Israel walipofanya vema na kuzishika nzjia za Mungu Mungu aliwarudia na kuwa pamoja nao, lakini walipofanya mabaya Mungu aliwaacha na walipata tabu sana
Sisemi kwamba kila taabu inasababishwa na kuacha njia ya Mungu hapana lakini kuna raha kupitia taabu huku ukiwa na Mungu, na kuna utungu mkubwa kupitia taabu huku ukiwa umemuacha Mungu, Katika nyakati hizi tulizo nazo pia Mungu ametupa njia ya kuifuata 

Yohana 14:6Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” 

Linapotokea jambo Gumu la kuumiza na kukatisha tamaa ni muhimu kuangalia Habari ya mapito ya zamani, baba zetu na watakatifu waliotutangulia walifanya nini? Wao walimtegemea Mungu hawakuzitegemea akili zao wenyewe, walimuweka Mungu mbele, walimfamya Mungu kuwa kinga yao, walimfanya yeye kuwa mtetezi wao, walimfanya kuwa ngao yao, walimfanya kuwa tumaini lao, walimgeukia yeye na kwa sababu hiyo walipata raha nafsini mwao, Historia inaonyesha kuwa Yesu hajawahi kumuangusha mtu aliyemtegemea  

Mathayo 11:28-29Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

Yesu amewahakikishia raha wale wote wanaoshikamana naye, Hakuna namna unaweza kujikwamua katika jambo lolote bila ya Yesu, Taifa jamii na kanisa kama tunataka kufanikiwa basi tunapaswa kuangalia njia zetu kama tumekengeuka tukajifunze habari za mapito ya zamani na kuangalia kwamba tunaenenda sawasawa au hapana? Tumfanye Yesu kuwa tegemeo letu, ngao yetu, kimbilio letu, mwamba wetu, tumaini letu na tukimtegemea yeye na kutii maelekezo yake tutapata raha nafisni mwetu, 
Tenzi namba 16 Kumtegemea Mwokozi kwangu tamu kabisa…………..

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Jumatatu, 13 Agosti 2018

Bwana yu karibu na waliovunjika Moyo:-

Andiko la msingi: Zaburi 34:17-19Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”

 "Bwana yu Karibu na Waliovunjika Moyo, Na waliopondeka Roho Huwaokoa Zaburi 34:18"

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa tuwapo duniani wanadamu tunazungukwa na changamoto nyingi, kwa kawaida Mungu ameruhusu tuweze kupitia nchangamoto za aina mbalimbali kwa makusudi mbalimbali, aidha ya kutufundisha ama kutufanya tukue kiroho, kihekima na kimaadili lakini wakati mwingine kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, hata hivyo wakati tunapopitia changamoto hizo, mara kadhaa wanadamu huwa tunakata tamaa, na tunaweza kujiuliza kama hivi Mungu anaona kweli? Hivi Mungu yupo? Kama yupo kwa nini anaachia jambo kama hili, kwa nini hakuzuia, kwa nini hakunitahadharisha mapema? Mbona yuko kimya Hivi yeye yupo kweli?tunaweza kufikiri kuwa Mungu ametuacha.

Katika nyakati hizi ngumu ndio nyakati ambazo ni rahisi kumuwazia Mungu kwa upumbavu, yaani kumfikiria Mungu kwa namna isiyofaa,Watakatifu waliotutangulia waliokuwa na ujuzi kuhusu Mungu walifahamu kuwa wanadamu wana changamoto nyingi maandi yanasema hivi kupitia Ayubu;-

Ayubu 14: 1Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu.” 

Wote tunafahamu jinsi Ayubu alivyopitia majaribu na mateso Magumu lakini Biblia inatuambia kuwa Ayubu katika dhiki yake hakuwahi kumkufuru Mungu wala kumuwazia Mungu kwa upumbavu,

Ayubu 1:20-22Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.”

Hali kama hii ndio iliyomtokea mwandishi wa Zaburi hii, kwa mujibu wa masimulizi ya tamaduni za kiyahudi Zaburi hii imethibitika kuwa iliandikwa na Daudi, au moja ya viongozi wa kwaya wa Daudi, na mazingira ya uandishi wa zaburi hii ulitokana na tukio la Daudi kunusurika katika hatari mbaya iliyokuwa ikimkabili, Zaburi hii iliandikwa mara baada au kwa kusudi la kukumbuka namna Daudi alivyonusurika katika hatari ngumu katikati ya mfalme wa wafilisti alipokuwa akitafutwa na Sauli ili aweze kuuawa Katika Mazingira haya magumu Daudi aliweza kujifanya mwendawazimu ili kupata namna ya kuondoka mikononi kwa Akishi mfalme wa wafilisti.

1Samuel 21:10-15 Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi. Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema,Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi makumi elfu yake. Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi. Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakuna-kuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake. Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mwaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu? Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe hiki ili aonyeshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?

Ni katima Mazingira ya aina hii ndio Daudi alipoimba zaburi hii ya 34 akzizungumza maneno ya kushangaza sana hata baada ya tukio hili gumu namna hii Daudi aliweza kumsifu Mungu, alionyesha kuwa Mungu ni tumaini lake, hakutaka kulalamika alitaka watu wote wawe wanyenyekevu wamtumaini Mungu wamweleze shida zao na kuwa yeye atawaitikia kwa kuwa Ni Mungu aliye karibu na watu wake angalia maneno yake hiyo isiyo ndefu sana Zaburi 34:1-22

1. Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
2. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
3. Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
4. Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.
5. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya.
6. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.
7. Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
8. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.
9. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
10. Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.
11. Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha Bwana.
12. Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema?
13. Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.
14. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.
15. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao.
16. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
17. Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote.
18. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.
19. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.
20. Huihifadhi mifupa yake yote, Haukuvunjika hata mmoja.
21. Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.
22. Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.

Unaweza kuona hatupaswi kukata tamaa wala kuvunjika Moyo katika mazingira yoyote, katika hali Ngumu zinazotukabili Mungu na aendelee kuwa Mungu wetu, tusimuwazie kwa Upumbavu tuendelee kuuona mkono wake, na kumtegemea yeye katika hali zozote, tusinungunike, bali afadhali kumlilia yeye, 

Manunguniko yanaondoa Baraka za Mungu, Manunguniko, yanamkasirisha sana Mungu, badala ya kulalamika na kunung’unika ni afadhali kumlilia yeye na kumhimidi yeye Daudi anasema atamhimidi Bwana kila wakati maana yake katika hali yoyote na Mungu yu Karibu na waliovunjika moyo na wanaonyenyekea kwake yeye huwakomboa huwahurumia na kuitikia kilio chao.
Mungu aitikie kilio chako Ndugu yangu, Mungu na awe karibu nawe Mungu asikupungukie Mungu asikufanye ukufuru Usivunjike moyo, wakati unapopita katika Magumu, Mungu yuko Karibu, Mungu hajatutupa wala hajakutupa wewe anakujali yuko Karibu nawe mtafute wakati huu wa dhiki yako atakutokea nawe utasadiki ya kuwa Mungu amenituma nikuhakikishie kuwa Yuko Karibu nawe Bila shaka atakufuta Machozi yako leo, BWANA YU KARIBU NA WALIOVUNJIKA MOYO, NA WALIOPONDEKA ROHO HUWAOKOA.

Na. Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima