Alhamisi, 30 Agosti 2018

Maisha Bila Mipaka!


Warumi 8:38 -39.Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,  wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”


Utangulizi:

Nick Vujicic ni moja ya walemavu ambaye alizaliwa akiwa hana miguu wala mikono na wataalamu wa kitabibu walishindwa kuelewa sababu kuu ya ulemavu wake na hata namna ya kumtibu, lakini kwa sasa amejipatia umaarufu mkubwa sana duniani kutokana na bidii kubwa aliyo nayo na mafanikio makubwa sana katika maisha akiwa hana viungo hivyo muhimu yeye mwenyewe anasema Namnukuu  I was born without arms or legs and given no medical reason for this condition. Faced with countless challenges and obstacles, God has given me the strength to surmount what others might call impossible.” “Nalizaliwa pasi na mikono wala miguu na sikupewa sababu za kitabibu za kuzaliwa hivyo, Nimekumbana na changamoto nyingi na vikwazo, Mungu amenitia nguvu kupambana na hali ngumu ambazo wengine walizishindwa” Ni mwanzilishi wa shirika liitwalo Life without Limbs na Mwinjilisi mkubwa sana Duniani na pia ni Motivational speaker  ambaye aliweza kupitia vikwazo na magumu na kuvishinda kwa nguvu na tumaini lililo katika Kristo Yesu.

Siri kubwa ya mafanikio ya Mlemavu huyu Duniani ni “Mungu alimtia Nguvu” Kumbe kwa Mungu hakuna lisilowezekana, tunaishi katika misuguano na kujikuta tumezingirwa na mipaka pande zote dunia ikikulazimisha kusalimu amri na kuishia hapo ulipoishia au hapo ulipokatia tamaa kwa sababu hujatambua chanzo  cha nguvu zako, kwa hiyo dunia na mazingira na vikwazo vimekukwamisha hapo ulipo umeambiwa haiwezekani, haitowezekana, huwezi lolote, hustahili kitu hutoweza, ndugu zako walishindwa, Mfupa uliomshinda fisi wewe mbwa utauweza wapi.

Siri ya mafanikio.

Siri ya mafanikio ya watu kama kina Nick Vujicic  na wengineo ambao tunawasoma katika maandiko ni NGUVU ZA MUNGU nyuma ya maisha yao, Maandiko ni ufunuo wa Nguvu za Mungu, unaposoma na kuona shuhuda za watu kama kina Yusufu kutoka gerezani na kuwa mtu mwenye mamlaka kubwa duniani ni Matokeo ya Nguvu za Mungu, Unaposoma habari za kusisimua za kina Daniel na Hekima kubwa walizokuwa nazo na uwezo mkubwa katika kupambanua mambo ni kuwa siri kubwa ni Nguvu za Mungu, Roho wa Mungu alikuwa juu yake, hii ndio siri iliyowafanya waonekane kuwa ni wa kipekee.

Kila mtu Duniani Mungu alimuumba kwa kusudi, na moja ya kusudi la kuumbwa kwako ni ili ufanikiwe na kuwa Baraka kubwa kwa wengine pia, Lakini ni nguvu ya Mungu kiasi gani unayohitaji ndiyo itakayoamua hatima ya maisha yako, wengi tunaishi maisha yenye mipaka Lakini Mungu hakukusudia iwe hiyo! Hata kidogo, Mungu ametupa Nyenzo ya kutusaidia kufikia kiwango kikubwa na cha juu cha mafanikio Nguvu hizo ni Roho Mtakatifu.

·         Mwanzo 41:38-40Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”

·         Daniel 5:10-12Basi malkia, kwa sababu ya maneno ya mfalme na ya wakuu wake, akaingia katika nyumba ya karamu; malkia akanena, akasema, Ee mfalme, uishi milele; fikira zako zisikufadhaishe; wala uso wako usibadilike. Yuko mtu katika ufalme wako, ambaye roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yake; na katika siku za baba yako nuru na ufahamu na hekima zilionekana ndani yake; na mfalme Nebukadreza, baba yako, naam, mfalme, baba yako, akamfanya kuwa mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu;      kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na kufungua mafundo, zilionekana katika Danieli huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danieli, naye ataionyesha tafsiri.” 

·         1Wakoritho 2:4-5Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu,  ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu”.

     Paulo hakuhubiri Falsafa, hakutumia ushawishi wa kiakili lakini alifanikiwa sana katika injili kuliko wote kwa sababu alikuwa na Nguvu za Mungu

Kuishi bila Nguvu za Mungu ni kujiweka katika hatari kubwa sana, lakini ili tuweze kuwa washindi ni lazima tuishi katika uwepo na nguvu za Mungu, Mungu alituleta Duniani kama watu maalumu, alitukomboa ili tuwe Makuhani na Wafalme na watawala wa Dunia Ufunuo 5:10ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.” Mwanadamu ni kiumbe cha thamani sana, Mungu amewadhimisha wanadamu kuliko malaika lakini ili tuweze kuwa na mafanikio Duniani na kuitawala kama wafalme na makuhani hatuna budi kujiungamanisha na Nguvu za Mungu, Mungu hafurahii kutuona tukiishi kwa mipaka kwa ujumla hatukuumbwa ili tuje kuteseka na kufungiwa duniani bali Mungu alikusudia tuitawale dunia na kila kilichomo Haya yanawezekana tu kama tutajiachilia katika nguvu za Mungu na Roho wake hakuna jambo litakaloshindikana kwetu Zekaria 4:6-7.Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”  Unaweza kuona sasa kama tunasumbuka katika Dunia hii, tumejawa hofu, tumejawa kukata tamaa, tumepoteza ujasiri, tunalia, tunaugua, tunaonewa kuna kitu hakiko sawa ni kwamba hatujatambua kuwa sisi ni akina nani na Mungu ametuandalia Nini? Yesu alianza kupata umaarufu mkubwa mara moja tu alipokaliwa na Roho wa Mungu na kumruhusu aongoze maisha yake 

Luka 4:1Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani14 Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando.” 

Yesu anarejea akiwa amejaa nguvu za Mungu, na tangu tukio hili utaweza kuona umaarufu wake ulienea katika nchi zote za kandokando ya Israel, Wanafunzi wa Yesu walikuwa waoga walijifungia chumbani kwa siku kadhaa lakini alipokuja Roho Mtakatifu mambo yalibadilika waliupindua ulimwengu, Bila Roho Mtakatifu, bila neema na bila nguvu za Mungu tutaendelea kuwa wanyonge na kuishi katika kiwango cha chini cha maisha bila mafanikio na maisha yenye mipaka mingi.

Katika Warumi 8:38-39Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,  wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Paulo Mtume anazungumza kwa ujasiri unaotokana na uzoefu wake akikazia kwa msisitizo mkubwa sana wa imani ya kitume kuwa yeye sasa kutokana na Mambo ambayo Mungu amemfunulia, kutokana na jinsi Mungu alivyoufunua upendo wake kwetu, yeye pamoja na wengine wote wenye kuamini Hakuna kitu kinaweza kututenga na upendo wa Kristo, Hili halitokani tu na ufunuo mkubwa alioupata bali kazi kubwa ambayo Mungu amewatendea wanadamu, kwa kutuchagua, kwa kutufanya kuwa wana wake, ametambua kuna usalama Mkubwa katika Kristo na kuwa ni vigumu sana jambo lingine lolote kupingana na kusudi la Mungu, hivyo yote yanayoogopewa na wanadamu hayawezi kuwa mpaka wa kututenganisha na Mungu

·         Kifo hakina ubavu – Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Maisha hayana ubavu– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Mamlaka hazina ubavu– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Serikali hazina ubavu– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Malaika au mashetani – Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Mamlaka na falme– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake
·         Mambo yaliyopo yaani sasa na yajayo– Haiwezi kuwa tishio la kuharibu kusudi la Mungu kwa sababu ya nguvu yake

Kama Nick ameweza kufanikiwa na hakuzaliwa akiwa na mikono wala miguu, bali kwa nguvu za Mungu ameweza kuwa mtu maarufu Duniani na kufanikiwa katika kuwatia moyo wengine wote, wanaofikiri kuwa wao si kitu, wanaofikiri kuwa hawawezi, Maandiko yanatutaka tuinue macho yetu na kumuangalia Mungu Nguvu zake zinatosha kutupeleka katika level nyingine na kutufanya tufanye mambo yasiyokuwa ya kawaida, Hakuna sababu ya kukata tamaa, tuitafute Nguvu ya Mungu, tuutafute upako na kufanya kazi zetu kwa bidii hakuna kitakachoweza kusimama na kuzuia kusudio la Mungu katika maisha yako, usikubali kukatishwa tamaa, usikubali hata kujikatisha tamaa, usikubali maneno yaliyonenwa juu yako, wao sio Mungu yuko Mungu mwenye uweza usio na mipaka hakuna wa kukuwekea mpaka Mungu amekupa uhuru wa kuyafurahi maisha katika nguvu zake, kaa katika hizo na utafurahia sana. Ziko sababu za kuishi maisha yasiyo na mipaka kutokana na upendo mkubwa sana wa Mungu wetu na mambo ambayo ametukarimia.

1.       Hakuna hukumu ya adhabu Rumi 8:1
2.       Roho wa aliyemfufua Kristo anaishi ndani yetu 11
3.       Roho anatuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa 26
4.       Mungu yuko upande wetu 31
5.       Aliweza kumtoa Yesu kwaajili yetu 32
6.       Hakuna wa kuwashitaki wateule 33
7.       Sisi ni washindi na zaidi ya kushinda 37

Nakuombea Mungu akuvike Nguvu zake ili usiishi katika mipaka uliyowekewa au kujiwekea Bali ujae nguvu za Mungu na uweza wake

Na. Mkuuwa wajenzi mwenye Hekima.
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: