Andiko la msingi: Zaburi 34:17-19 “Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na
waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini
Bwana humponya nayo yote.”
"Bwana yu Karibu na Waliovunjika Moyo, Na waliopondeka Roho Huwaokoa Zaburi 34:18"
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu
kuwa tuwapo duniani wanadamu tunazungukwa na changamoto nyingi, kwa
kawaida Mungu ameruhusu tuweze kupitia nchangamoto za aina mbalimbali
kwa makusudi mbalimbali, aidha ya kutufundisha ama kutufanya tukue
kiroho, kihekima na kimaadili lakini wakati mwingine kwa sababu
anazozijua yeye mwenyewe, hata hivyo wakati tunapopitia changamoto hizo,
mara kadhaa wanadamu huwa tunakata tamaa, na tunaweza kujiuliza kama
hivi Mungu anaona kweli? Hivi Mungu yupo? Kama yupo kwa nini anaachia
jambo kama hili, kwa nini hakuzuia, kwa nini hakunitahadharisha mapema?
Mbona yuko kimya Hivi yeye yupo kweli?tunaweza kufikiri kuwa Mungu
ametuacha.
Katika nyakati hizi ngumu ndio nyakati ambazo ni
rahisi kumuwazia Mungu kwa upumbavu, yaani kumfikiria Mungu kwa namna
isiyofaa,Watakatifu waliotutangulia waliokuwa na ujuzi kuhusu Mungu
walifahamu kuwa wanadamu wana changamoto nyingi maandi yanasema hivi
kupitia Ayubu;-
Ayubu 14: 1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke
Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu.”
Wote tunafahamu jinsi
Ayubu alivyopitia majaribu na mateso Magumu lakini Biblia inatuambia
kuwa Ayubu katika dhiki yake hakuwahi kumkufuru Mungu wala kumuwazia
Mungu kwa upumbavu,
Ayubu 1:20-22 “Ndipo Ayubu akainuka,
akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na
kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami
nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina
la Bwana na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi,
wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.”
Hali kama hii ndio
iliyomtokea mwandishi wa Zaburi hii, kwa mujibu wa masimulizi ya
tamaduni za kiyahudi Zaburi hii imethibitika kuwa iliandikwa na Daudi,
au moja ya viongozi wa kwaya wa Daudi, na mazingira ya uandishi wa
zaburi hii ulitokana na tukio la Daudi kunusurika katika hatari mbaya
iliyokuwa ikimkabili, Zaburi hii iliandikwa mara baada au kwa kusudi la
kukumbuka namna Daudi alivyonusurika katika hatari ngumu katikati ya
mfalme wa wafilisti alipokuwa akitafutwa na Sauli ili aweze kuuawa
Katika Mazingira haya magumu Daudi aliweza kujifanya mwendawazimu ili
kupata namna ya kuondoka mikononi kwa Akishi mfalme wa wafilisti.
1Samuel 21:10-15 “Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu
ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi. Nao watumishi wa Akishi
wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana
habari zake katika ngoma zao, kusema,Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi
makumi elfu yake. Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake,
akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi. Akaubadilisha mwenendo wake
mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakuna-kuna katika
mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake. Ndipo
huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mwaona ya kuwa mtu
huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu? Je! Mimi nina
haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe hiki ili aonyeshe wazimu
wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?”
Ni
katima Mazingira ya aina hii ndio Daudi alipoimba zaburi hii ya 34
akzizungumza maneno ya kushangaza sana hata baada ya tukio hili gumu
namna hii Daudi aliweza kumsifu Mungu, alionyesha kuwa Mungu ni tumaini
lake, hakutaka kulalamika alitaka watu wote wawe wanyenyekevu wamtumaini
Mungu wamweleze shida zao na kuwa yeye atawaitikia kwa kuwa Ni Mungu
aliye karibu na watu wake angalia maneno yake hiyo isiyo ndefu sana
Zaburi 34:1-22
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
2. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
3. Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
4. Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.
5. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya.
6. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.
7. Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
8. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.
9. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
10. Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.
11. Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha Bwana.
12. Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema?
13. Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.
14. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.
15. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao.
16. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
17. Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote.
18. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.
19. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.
20. Huihifadhi mifupa yake yote, Haukuvunjika hata mmoja.
21. Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.
22. Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.
Unaweza kuona hatupaswi kukata tamaa wala kuvunjika Moyo katika
mazingira yoyote, katika hali Ngumu zinazotukabili Mungu na aendelee
kuwa Mungu wetu, tusimuwazie kwa Upumbavu tuendelee kuuona mkono wake,
na kumtegemea yeye katika hali zozote, tusinungunike, bali afadhali
kumlilia yeye,
Manunguniko yanaondoa Baraka za Mungu,
Manunguniko, yanamkasirisha sana Mungu, badala ya kulalamika na
kunung’unika ni afadhali kumlilia yeye na kumhimidi yeye Daudi anasema
atamhimidi Bwana kila wakati maana yake katika hali yoyote na Mungu yu
Karibu na waliovunjika moyo na wanaonyenyekea kwake yeye huwakomboa
huwahurumia na kuitikia kilio chao.
Mungu aitikie kilio chako
Ndugu yangu, Mungu na awe karibu nawe Mungu asikupungukie Mungu
asikufanye ukufuru Usivunjike moyo, wakati unapopita katika Magumu,
Mungu yuko Karibu, Mungu hajatutupa wala hajakutupa wewe anakujali yuko
Karibu nawe mtafute wakati huu wa dhiki yako atakutokea nawe utasadiki
ya kuwa Mungu amenituma nikuhakikishie kuwa Yuko Karibu nawe Bila shaka
atakufuta Machozi yako leo, BWANA YU KARIBU NA WALIOVUNJIKA MOYO, NA
WALIOPONDEKA ROHO HUWAOKOA.
Na. Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni