2Timotheo 1:3-7.
“Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani
za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku
na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae
furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza
katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe
unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani
yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana
Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”
Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, usilie
;tazama,Simba aliye wa kabila ya Yuda,Shina la Daudi,Yeye ameshinda apate
kukifungua kile kitabu,na zile muhuri zake saba.” Ufunuo 5:5
Ni muhimu kufahamu kuwa Maandiko Matakatifu yanatufundisha kuwa kuna aina mbili za hofu, hofu ya kwanza ni hofu yenye manufaa, hofu yenye faida, aina hii ya hofu ndio inayotufanya tuogope kujiumiza, au tuogope kufanya mambo mabaya, na tuweze kumcha Mungu na kuogopa kutenda maovu hii ni hofu njema na yenye ufanisi, Lakini hofu ya pili ni hofu mbaya, aina hii ya hofu ni hofu yenye hasara ni hofu mbaya na ni roho hii ndio hofu ambayo maandiko yanatufundisha kuwa haitokani na Mungu ni hofu mbaya sana na ni hofu inayowafanya wengi waogope kuthubutu au kufanya jambo.
Hofu
ya Mungu.
Hofu ya Mungu huambatana pamoja na baraka nyingi na faida. Ni mwanzo
wa hekima na inaongoza kwa uelewa mzuri Zaburi
111: 10. “Kumcha
Bwana ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake
zakaa milele.” Pia unaweza kuona katika Mithali 1: 7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau
hekima na adabu”. Zaidi ya hayo, hofu ya Bwana inaongoza kwa maisha,
pumziko, amani, na ridhaa Mithali 19:23.
“Kumcha Bwana
huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya” kumcha bwana
kunaongeza Maisha ni chemichemi ya uzima inayoepusha na mauti Mithali 14:27 “Kumcha
Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti” Kwa
msingi huo hofu ya Mungu yaani lkumcha Mungu ni jambo muhimu sana katika maisha
ya mwanadamu na ndani yake Nguvu, upendo
na moyo wa kiasi hofu hii inafaida kubwa sana na biblia imewekea mkazo umuhimu
wa aina hii ya hofu.
Roho ya woga (Hofu isiyotokana na Mungu)
Katika mstari wa msingi
tuliousoma sasa Paulo mtume anaorodhesha aina nyingine ya Hofu na anamuieleza
Timotheo kuwa hofu hii haitokani na Mungu wala Mungu hatupi hofu ya aina hii na
zaidi sana anaiita hofu hii “ROHO YA WOGA” maana yake ni kuwa ainha hii ya hofu
ni dhahiri kuwa inatokana na shetani ni hofu mbaya 2
Timotheo 1: 7: "Kwa maana Mungu hakutupa roho ya
woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi."
Katika Biblia ya kiyunani neno
hili roho ya woga linaweza kutafasiriwa kama Hali ya kujiona Duni, “inferiority
complex” hili ni tatizo kubwa la
kisaikolojia linaloweza kuwapata hata watu wa Mungu, hata watu ambao wamekua
vizuri katika imani, lakini kwa vile ndani wanajiona duni basi wanafikiri kuwa
wao hawafai, wanaogopa, wanaogopa wanadamu, wanamuogopa shetani, wanaogopa ni
namna gani watazungumza mbele za watu, wanaogopa kukosea, wanaogopa kwa sababu
hawajui kiingereza vizuri, wanaogopa kwa sababu ya udhaifu fulani wa mwilini
ambao wanao, wanaogopa kwa sababu ya udhaifu katika roho zao, na kwa sababu
hiyo wanadhani kuwa hawataweza kufaa kwa namna yoyote kuwa watumishi wa Mungu,
wana jiona duni, wanajiona hawafai na hivyo wanajumlisha na kutoa na kupata
jawabu kuwa hawasytahili kuwa wachungaji, waisnjilisti au walimu, mitume na
manabii kwa sababu eti hawatoshi katika vipimo vya Mungu.
Hali ya aina hii ndio aliyokuwa
anaipitia Timotheo, aliwekwa kuwa mwangalizi wa Kanisa la Efeso, hili lilikuwa
moja ya Makanisa makubwa sana nyakati za kanisa la Kwanza, Na Timotheo alikuwa
tayari amekwisha chunga kanisa la Thesalonike, lakini Timotheo alikuwa ni
kijana mdogo, na alikuwa akiugua mara kwa mara lakini alitiwa moyo kwa uwepo wa
Paulo mtume, hofu ya aina hii bila shaka halikuwa tatizo kwa Timotheo lakini
Paulo alijua kuwa kwa vile Paulo alikuweko Duniani, aliweza kumtia moyo
Timotheo lakini sasa Paulo yuko gerezani na siku zake za kuondoka Duniani
zilikuwa zinakaribia na alijua kuwa kwa vyovyote vile Timotheo angeogopa au
angepoteza ujasiri na sasa anataka kumtia moyo kuwa asiogipe hofu ya aina hii
sio sehemu ya maisha ya mtu aliyeokoka.
Mungu hajatuita, tuwaogope
wanadamu, Mungu hajatuita, tuogope kusimama mbele ya umati mkubwa wa watu,
Mungu hajatuita tuwe waoga, Mungu hajatuita tuwe duni miongoni mwa wanadamu,
waluimu wa uongo na kazi za shetani na nguvu za giza kinyjme chake sisi tuna
Roho Mtakatifu, Roho wa Bwana, tuna roho ya nguvu, tuna roho ya hekima, tuna
roho ya uchaji wa Mungu, tuna roho ya Ushauri, tuna roho ya maarifa na ujuzi Isaya 11:1-2 “Basi
litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi
yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na
ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;”
Roho ya ya woga haitoki kwa Mungu.
Hata hivyo, wakati mwingine sisi
uhofu, wakati mwingine hii "roho ya woga"inatulemea, na kuishinda
tunapaswa kumwamini na kumpenda Mungu kabisa . "Hakuna hofu katika upendo. Lakini upendo kamili
unatoa nje hofu, kwa maana hofu inatumika na adhabu. Mtu mwenye woga hajafanywa
mkamilifu katika upendo "1
Yohana 4:18. Hakuna mtu mkamilifu, na Mungu anajua hilo. Mungu wakati mwingine hataondoa kabisa
madhaifu tuliyo nayo lakini badala yake atataka tumtegemee yeye hivyo hivyo
hivyo pamoja na udhaifu wetu naye ataleta utoshelevu wa neema na upendo wetu
kwetu kwaajili ya utukufu wake, kamwe usingije eti uwe mkamilifu kisha ndio
umtumikie Mungu, Biblia inatuhimiza wakati wote tusiogope, Roho ya Hofu ina
nguvu sana ya kuharibu vipawa na uwezo wa watu, na ndio maana Mungu anataka
tumuamini, bila kujali kuwa tuna umri mdogo, au hatuna elimu ya kutosha, au
hatujui kiingereza, au hatuna ujuzi na jambo fulani.
Isaya 41:10 inatuhimiza, "Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifahdaike, kwa
maana mimi ni Mungu wako, nitakutia nguvu, maana nitakusaidia, naam nitakushika
kwa mkono wa kuume wa haki yangu.“ Zaburi 56:11 "Nimemtumaini Mungu sitaogopa, mwanadamu atanitenda nini?"
Yeremia 1:5-8 “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka
tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa,
Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana
akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma
kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana
mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.”
Joshua 1:5-8 “Hapatakuwa mtu ye yote
atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa
pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala
sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu
hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na
ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa
mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate
kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako,
bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa
na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako,
kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si
mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike;
kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”
Mungu wakati wote atatoa neema
kwa kila aina ya ulemavu tulio nao anajazilizia, nimekutana na watu ambao
hawakusoma kabisa lakini wana akili za ajabu sana, Bibi yangu alikuwa ni moja
ya watu waliokosa elimu kabisa wakati wa Mkoloni, alitokea familia duni, lakini
yeye ndiye aliyekuwa analima na kulisha watu nyumbani, wenye fedha walikuwa
wakinunua mboga tu, lakini ugali na mahindi na mihogo bibi alileta kutoka
shambani, alisimamia watoto wake wote wakaenda shule na kuelimika na kuwa watu
wakubwa, leo tuna wanasiasa, wakubwa, tuna askari, tuna mainjinia, tuna pilisi,
tuna usalama wa taifa, tuna walimu, tuna madereva, tuna mafundi, mchundo,
waashi, lakini walilelewa na Bibi ambaye hakusoma Mungu atakupa neema katika
mapungufu uliyonayo, Usiogope simama na mtumikie Mungu kwa kile Mungu
alichoweka ndani yako Usiogope Mungu hakutupa Roho ya woga. Uwe na ushujaa Yesu
ni Simba wa kabila la Yuda tukiwa naye msituni hatupaswi kuhofia lolote.
“Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda,Shina la Daudi,Yeye ameshinda apate
kukifungua kile kitabu,na zile muhuri zake saba.” Ufunuo 5:5
Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.
0718990796.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni