Wimbo ulio bora 1:5-6
“Mimi ni
mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri, Enyi binti za Yerusalemu, Mfano wa hema za
Kedari, Kama mapazia yake Sulemani. Msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi,
Kwa sababu jua limeniunguza. Wana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe
mlinzi wa mashamba ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda”
Utangulizi:
Maandiko
Matakatifu yanatufundisha maswala ya Msingi sana kuhusu Maisha, hususani katika
nyakati hizi za siku za mwisho ambapo watu wanajituma sana kutafuta maisha na
kufanya kazi zao kwa bidii ili waweze kukidhi haja ya mahitaji ya familia zao,
Katika nyakati hizi watu wengi sana wamekuwa wakifanya kazi sana (busy) kiasi
ambacho licha ya kufanikiwa sana katika maeneo mengine lakini wameharibikiwa na
kupoteza maswala ya msingi, au kupuuzia maswala ya muhimu sana katika maisha
yao.
Kifungu
cha maandiko tulichokisoma kinafaa kabisa kusomwa sambamba na kitabu cha Mithali 24:30-31 inayosema “Nalipita karibu na
shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili. Kumbe! Lote pia
limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.”
Somo
kubwa tunaloweza kulipata hapa ni onyo kuhusu kuwa :busy” katika maisha na
kusahau kushughulikia maswala ya msingi, tunaweza kujishughulisha sana na kazi,
na maswala yanayoonekana kuwa ya muhimu kwetu na tukasahau maswala muhimu na ya
msingi katika maisha yetu wenyewe, Katika mstari wa msingi tunaona mwandishi
akionyesha kulalamaika kwamba amekuwa mweusi mweusi ijapokuwa yeye ni mzuri,
lakini sababu kubwa ni kuwa amepigwa na jua kwa sababu ya kufanya kazi na
kujishughulisha na mambo ya wengine akitunza mashamba yao ya mizabibu kwa
kiwango ambacho yeye mwenyewe alikuwa anashindwa kushughulikia mambo yake na
hata ya shamba lake binafsi la mizabibu hapa ndio tutachukua muda kujifunza na
kuangalia kwa undani kwamba kuna nini ambacho maandiko yanataka kutufunza:-
Wajibu wa kufanya kazi tulizopewa!
Ni
muhimu kufahamu kuwa sisi ni watumishi wa Mungu, na kuwa ni Bwana ndiye
aliyetuchagua tumtumikie katika eneo ambalo ametuita kumtumikia ni neema kuu
kwa Mungu wetu kufanya kazi katika eneo ambalo Mungu amekupa kufanya ni Baraka
kubwa sana kwa vile huenda wengine wametamani kufanya unachokifanya lakini
hawakupata neema hiyo, kwa hiyo hatuna budi kumshukuru Mungu kwa wito
aliotuitia kwa kuwa ni wito wa ki Mungu (Divine
appointment) so kimsingi Mungu anataka sana tufanye kazi zetu kwa bidii,
kumbuka kuwa hatukuchagua kufanya hiki tunachokifanya kwa hiyari yetu wenyewe ila
Mungu alikusudia “Waliniweka niwe mlinzi”
ni wazi kuwa mtu huyu hakuchagua awe na hali ile alichaguliwa Mungu ndiye
anayechagua kwamba sisi tutimize wajibu gani hapa ulimwenguni Yohana 15:16 “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi
niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu
yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.”
Unaweza kuona kumbe ni Mungu aliyekusudia tuwepo katika wajibu huu tulio nao
sasa na sisi tumefanya vema kutii wito wake Mathayo 21:28 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea
yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la
mizabibu.” Unaona? Kila mmoja yuko katika shamba la mzabibu,
tumeitikiwa wito alioweka Mungu ndani yetu kutokana na upendo wake kwetu na
upendo wetu kwake tumetii , Shamba lako la mzabibu ni pale ambapo Mungu
amekuweka umtumikie nawe ni mtoto mwema kwa kuwa umetii na unafanya kazi kwa
bidii katika shamba lako la mizabibu uliloitiwa yaani:-
·
Kama ni mama wa Nyumbani shamba lako
la mizabubu ni pale Mungu alipokuweka kuhakikisha unailea familia yako na
kuongoza watoto wako katika njia iliyonyooka, unafanya wajibu wako wa kumlinda
mumeo kumtunza, kumpikia na kuhakikisha kuwa ana afya njema ili aweze kutiwa
moyo kutafuta kwaajili yako na familia yako.
·
Kama ni mwalimu utafanya yaliyo
wajibu wako wote kama mwalimu, utafundisha kwa bidii yako yote na kufanya kila
kilicho wajibu wako kuwaelimisha vijana, na kuwarithisha maadili na tamaduni na
uzalendo kwaajili ya taifa letu na faida ya kizazi kijacho utaifanya kazi hiyo
kwa bidi.
·
Mwanajeshi basi shamba lako la
mizabibu ni jeshini, kulinda na kulipigania taifa lako, utawalinda wananchi
wa-nchi yako, na kuhakikisha kuwa mipaka ya taifa lako iko salama na mipaka ya
majirani zako, na wakati wote utahakikisha unalinda na kuisimamia amani ya
dunia kwani umeyatoa maisha yako kwaajili ya jamii.
·
Daktari au muuguzi mlezi basi shamba
lako la mizabibu ni Hospitali, utawapenda na kuwahudumia wagonjwa kwa moyo wa
upendo ukijitoa kwa uaminifu na kutunza siri za wagonjwa wako, na kuwahudumia
kwa moyo wako wote ukiifanya kazi hii ya kuokoa uhai wao mpaka dakika za mwishi
isipokuwa tu pale ambapo Mungu ameingilia kati na kuchukua kiumbe wake, utatia
moyo na kuwapa pole waliopoteza ndugu yao kwa kuwa uwezo wako wa kibinadamu wa
kuokoa maisha yake umeishia hapo.
·
Muhubiri shamba lalo la mizabibu ni
injili, kwamba utahakikisha unalihubiri neno, kwa bidii, wakati unaofaa na usio
faa, utahakikisha kuwa injili inawafikiwawale wanaokuzunguka na eneo lile
ambalo mungu amekupa kumtumikia.
·
Mfanya biashara shamba lako la
mizabibu ni biashara ambazo Mungu amukupa uzifanye huko ndiko Mungu
alikokukusudia utumike na kumtumikia na kutimiza mapenzi yake.
·
Mwanafunzi wajibu wake nikusoma kwa
bidii, kujiandaa vema na kuhakikisha kuwa unapata maarifa yote ambayo serikali
na walimu wako wamekusudia uyapate, uwe tayari kufaulu pia mitihani yako na
kuwa tayari kukabiliana na changamoto za maisha mara baada ya kumaliza masomo
yako.
·
Kila mmoja kwa sehemu yake kazi
yoyote ile ni muhimu kukumbuka kuwa popote ulipo unamtumikia Mungu na kuwa
wapaswa kufanyakwa bidii kile ambacho Mungu amekupa kukifanya. Hayo yote ni
mapenzi ya Mungu kabisa.
Hatari inayomkabili mtunza mizabibu!
Wimbo uliobora 1:6b “Wana wa mamangu
walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa mashamba ya mizabibu; Bali shamba
langu mwenyewe sikulilinda”
Ni
muhimu kufahamu kuwa kuna hatari kubwa sana katika kujishughulisha na wajibu wa
kile ambacho Mungu amekusudia tukifanye na kwa urahisi sana tukasahau mambo ya
msingi, watu wengi sana kwa sababu ya kazi na kwa sababu ya biashara na masumbufu
ya maisha haya wamesahau kushughulikia maswala ya msingi ya ndani katika maisha
yao, kumbuka kuwa ni rahisi kuwapigia watu kiwi katika viatu vyao na
kuving’arisha lakini ukasahau kung’arisha cha kwako, ni rahisi kuwa mjenzi wa
majengo na ukajengea watu majengo ya kifahari na ukasahau kujenga ya kwako au
usiwe hata na kajumba, ni rahisi kulima vibarua na ukapalilia mashamba ya watu
wengine kisha kwako majani yakaota, ni rahisi pia kuwahubiri watu wengine
injili na kuwaelekeza katika neno la Mungu kisha wewe kuwa mtu wa kukataliwa,
hii ndio hatari kubwa sana kwa sababu hakuna mwajiri atakayekuhurumia duniani
(Kukasirikiwa) na akakupa nafasi ya kukuacha ufanye mambo yako, Israel kule
Misri walitumikishwa na walinyimwa kabisa muda wa kumuabudu Mungu, walifanya
kazi siku zote na hawakuwa na muda wa mapumziko wala muda wa kuwa na uhusiano
na Mungu ndivyo walivyofanywa na Farao kule Misri, mpaka walipofika Sinai ndipo
Mungu aliwakumbusha kupumzika na kufanya kazi siku sita na moja kuitoa kwaajili
ya Mungu Kutoka 1:13-14 “Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya
maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila
namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali”
unaona mfumo wa Dunia hii na hali
yake hauruhusu wala kutoa muda wa kushughulikia mambo yako ya muhimu na-ya
ndani kabisa Hali kama hii ilitokea Afrika wakati wa ukoloni, wakoloni
walifanya mambo kadhaa yenye kuwalazimisha waafrika waweze kuwa watumwa wao
wakati wa ukoloni na walime na kulipa kodi kwa matakwa ya wakoloni na kuwaminya
kiasi ambacho iliwalazimu waafrika na baba zetu kuona umuhimu na kuudai uhuru
wao.
1. Walitaifisha ardhi nzuri zenye rutuba – land alienation
2. Walibadilisha mfumo wa uchumi kutoka biashara ya kubadilishana
kwenda kwenye biashara kwa njia ya fedha – Money
economy
3. Waliwalazimisha raia kulipa kodi- Taxitation
4. Walianzisha mazao ya biashara – Cash crops
5. Waliwaajiri watu kwa ujira mdogo sana – Cheap labor
Kutokana
na mazingira ya aina hii, watu walipoteza uhuru wa kufanya mambo yao. Na ili
wapate fedha walilazimika kufanya kazi katika mashamba ya wakoloni au kuzalisha
mazao ya biashara ili wauze hali hii ilikuwa ngumu na kuwafanya wapoteze uhuru
wao na wasifanye mambo yao wenyewe, hali hii ni sawa na kulazimika kutunza
mashamba ya mizabibu ya watu wengine na kutokutunza mizabibu yao wenyewe, Dunia
na mfumo wake unakulazimisha ushughulike zaidi na mambo ya wengine kuliko mambo
yako ya msingi.
Kama
walimu tunaweza kufundisha watu na wakafanikiwa kwa kiwango kikubwa na
wakafaulu lakini nyumbani tukawa na watoto wetu au ndugu zetu wanafeli na
kudidimia kimasomo, ama tunaweza kukemea na kuchapa watoto wa wengine mpaka
wakabadilika kitabia wakawa watoto wazuri na hata wazazi wake wakakushukuru lakini
wetu wakatushinda wakawa ni watovu wa nidhamu wa hali ya juu.
Unaweza
kuwa Muhubiri na ukahubiri vema na kuwaelekeza watu njia ya Mungu lakini
ukasahahu kuwa na Muda wako binafsi na Mungu,ukasahau wajibu wa kuisimamia
nyumba yako vema ukawa na washirika wanaokutii lakini mke na watoto
wasiokuheshimu wala kukutii.
Unaweza
kuwa mshauri wa ndoa na mwalimu mzuri sana wa ndoa na ukasaidia ndoa za watu
wengi sana lakini ya kwako ikawa ni majanga, unaweza kuwafundisha watu kuomba
lakini wewe ukakosa nafasi ya kuomba japo kwa saa moja, unaweza kuwa mlinzi
mwema na askari mwema lakini ukashindwa kuilinda ndoa yako, ukashindwa
kuwatiisha watoto wako wakawa na heshima na adabu.
Unaweza
kuwashauri watu kwa habari ya afya au ukawa daktari mzuri, lakini wewe ukawa
una matatizo makubwa sana, Maandiko yanatulaumu kuwa tumeacha kuangalia mzabibu
wetu wenyewe
Nyakati
hizi tulizo nazo mambo yameharibika sana, kumekuweko na aina nyingi za
uharibifu katika maisha ya watu kutokana na kukosa malezi mazuri kutoka kwa
wazazi kutokana na wazazi kutokuwa na muda na watoto wao leo hii uzao wa ma-house
girl ndio unaotawala dunia au watoto wanalelewa katika vituo vya malezi au
shule za boarding zisizo na uadilifu wa kidini na kumruhusu shetani kuharibu
kabisa maisha ya kizazi hiki, wahubiri wengi wako busy na kazi wanazozifikiri
kuwa ni za Mungu na wamepoteza uhusiano wa karibu na Mungu, watu wanazunguka
huku na huko wakiwahubiri wengine lakini wao wamepoteza kabisa uelekeo, watu
wamekuwa busy na kazi na kusahau wajibu wao wa kujijenga wao binafsi, watu
hawana muda wa kusali, hawana Muda wa kusoma hata neno la Mungu na hata kukidhi
haja za tendo la ndoa kwa wanandoa wengi leo hii unasikia tu nimechoka
nimechoka kila kitu kinaparaganyika kwa sababu watu wamesahau kutunza shamba
lao la mizabibu, uko busy na maisha ya wengine yako je? Waimbaji wanashinda
studio kurekodi nyimbo zitakazoburudisha wengine na kuwajenga wengine na hata
kuokoa wengine lakini katika familia zao mambo yanaparaganyika Kiroho chako je,
nyumba yako je? Mke wako? Mume wako je ? watoto wako je? Maisha ya watu wengi
yameharibika na mashamba yao ya mizabibu yameota magugu kwa sababu wamesahau
wajibu wao wa kutunza mashamba yao ya mzabibu pia maisha yao ya binafsi, watu
wameshindwa hata kufanya mazoezi kwaajili ya afya zao, busy busy busy na
wamejawa na stresses kibao wamekuwa weusiwesu japokuwa wana uzuri ndani yao
lakini nini kimewaharibu wamesahau wajibu wao wa kuwa na Mungu binafsi, hali
inasikitisha mno sasa, watu wamesahau kushughulikia maswala muhimu
yanayowahusu, jua limewapiga wamepoteza uzuri wao wamechakaa na kuwa weusiwesui
sababu ya kutunza mashamba ya wengine na kusahahu mashamba yao ya mizabibu.
Mungu wangu! Hapa simaanishi kuwa zile
kazi tuzifanyazo sio za muhimu hapana lakini namaanisha unaporudi katika
maswala ya msingi unafanya nini kwaajili yako na kwaajili ya familia yako na
kwaajili ya maendeleo yako ya kimwili, kiakili, kiroho na kisaikolojia lakini
vilevile ya watu wale wa karibu wanaokuzunguka tunawezaje kuangalia mambo yetu?
Wajibu wa kutunza shamba lako la mzabibu.
1. Moyo wa
Kiasi – Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo
wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia;
tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”
ni muhimu kufahamu kuwa watu wengi
leo wanaharibikiwa kwa sababu ya kukosa moyo wa kiasi, neno kiasi maana yake ni “Self-control, au Displene” yaani ni swala la kujitia nidhamu, yaani mtu
anakosa kiasi, wako watu wengine wanakunywa pombe kiasi ambacho wanahatarisha
maisha yao na kazi zao na za wengine pia, ni abubu kufukuzwa kazi au kuitwa na
kiongozi wako na kuonywa kwa sababu ya ulevi, wengi siku hizi hawana muda wa
maongezi na watoto wao, wake zao na familia zao, kwani wanaporejea nyumbani
ndio wanapata wasaa wa kuoga na kula na kutulia wakifuatilia tamthilia za aina
mbalimbali, na wengine wanataka kila tathilia iliyo nzuri waifuatilie, watu
wako kwenye facebook, twiters, instergrams na mitandao mingine ya kijamii
wanajua kila kinachoendela lakini kama haitoshi hatra muda wa kazi wengine
wameshindwa kujicontrol na wamekuwa busy na simu zao, laptop zao wamekosa muda
wa kuwaweka sawa watot kuongea na
wapenzi wako na wengine huko huko wamenaswa na mapenzi yasiyo rasmi, tatizo
kubwa watu wameshindwa kuwa na kiasi na kujitia nidhamu.
2. Kuukomboa
wakati – Waefeso 5:15-16 “Basi angalieni sana jinsi
mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;
mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.” Maandiko yanatuonya kwamba tunapaswa kuenedna kwa hekima
katika nyakati hizi tilioznazo ambazo ni nyakati za uovu na kwamna inatupasa
kuenedna kwa kuukomboa wakati, Katika wakati huu ni muhimu kuyapa
kipaumbele mambo yaliyo ya muhimu na
kuyapa kipaumbele, inasemekana katika utafiti wa kitaalamu kuwa Marekani watu
hutumia wastani wa masaa 30 kwa wiki wakiangalia TV, katika zama hizi za uovu ni muhimu kupangilia
muda (time management) na kujipangia mambo ya kufanya, wapi utakuwa na marafiki
zako, wapi lini na muda gani utakuwa na familia zako, ni muda gani utaabudu na
kusoma neno la Mungu na kuomba na kufundisha familia yako na kusikiliza
mahubiri nakuhudhuria ibada, wengi
wameshindwa kutunza shamba lao wenyewe la mizabibu kwa sababu wamemezwa na
mifumo ya ulimwengu huu.
3. Ondoa kila
tawi lisilozaa Yohana 15:2 “Kila tawi ndani yangu
lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.” Lazima
ufanye Pruning yaani kuondoa maatawi yasiyozaa, matawi ambayo yatazuia matawi
yenye afya ya kuzaa matunda, lazima ujue na kukubali kuwa yako mambo yasiyofaa
katika maisha yetu yanahitaji kuachwa yanahitaji kuondolewa ili mambo yako
yaweze kufanikiwa, wako wengine wamebeba mizigo ya watu wengine wana uchungu
hawajasamehe, wengine wana uchungu na wake zao na watoto wao na waume zao na
wazazi wao maombi yao yanazuiliwa na hakuna mafanikio kwa sababu mzabibu wake
binafsi haujapaliliwa umesongwa hawajapogolea matawi ya muhimu ili mzabizu
uweze kukaa matunda kwa wakati wake, lazima umuombe Mungu aondoe pando
asilolipanda yeye Mathayo 5:29-30
4. Hakikisha kuwa unasafisha tawi lizaalo Yohana 15:2 “Kila tawi ndani
yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.”
Tawi lizaalo pia linapaswa kusafishwa,
wakati tawi lisilozaa huondolewa lizaalo linapaswa kusafishiwa 1Wakoritho 6:12 “Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote
vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa
kitu cho chote.” 1Wakoritho 10:23 “Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote
vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo.” Ni
muhimu kuhakikisha kuwa kila kitu kisichompendeza Mungu tunakiacha,
tunakitupilia mbali 2wakoritho 7:1 na 2Timotheo 2:19-22 lazima tufanye hayo ili
bwana atutumie.
5. Hakikisha
kuwa unajitunza na kujirutubisha
hii ni hali kama kumwagilia, kuwekea mbolea na katika udongo wa shamba lako,
hatuna budi kuhakikisha kuwa tunakuwa na Muda wa ukimya na Mungu, tunaomba,
Mathayo 6:6 tunasoma neno la Mungu 2Timotheo 2:15 ili kunufaisha roho zetu na
kustawisha uhusiano wetu na Mungu.
6. Hakikisha
kuwa unajilinda yaani kama tumechukua hatua za
kujitakasa na kuachana na dhambi na kujiimarisha katika neno la Mungu na
uhusuiano wetu na Mungu, sasa ni vema kwetu tukahakikisha kuwa tunalilinda
shamba letu la mizabibu hususani na mbeha wale wadogo waharibuo mizabibu Wimbo uliobora 2:15, vitu vinavyoharibu
na kutuondolea uwepo wa Mungu sio vile vikubwa bali ni vile tunavyovizarau na
kuviona vidogodvidogo Zaburi 139:23-24
Hatuna budi kumshukuru Mungu na kumfurahia kwa kila
alilolifanya kwaajili yetu na kila wajibu alioutupa kuutekeleza duniani, lakini
hatuna budi kuwa makini na kuhakikisha kuwa tunaendeleza maisha yetu ya kiroho
ya ndani ya familia zetu wakati tunaposhughulika na mengineyo, tuhakikisha
tunadumisha uhusiano wetu na Mungu na kufurahia uwepo wake kila iitwapo leo,
nasi tutakuwa na uzuri
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni