Alhamisi, 21 Machi 2019

Mtu atakayelitengeneza boma !



Ezekiel 22:30-31.Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika mpango wake wa ukombozi, hapendi kufanya mambo duniani bila kuwahusisha wenyeji wa dunia, Mungu huwa anatafuta mtu ili aweze kumtumia katika kuujenga ufalme wake, inapotokea kuwa Familia, ukoo, jamii au hata taifa limemtenda Mungu dhambi ni wajibu wa Mungu, kuikemea, kuonya na hata kuhukumu wale waliofanya uovu, hata hivyo Kabla ya Mungu kuhukumu pia huwa anatafuta mtu, ili yamkini aweze kumtumia mtu huyo kutoa Maonyo ili kwamba kama watu watatubu aweze kuwasamehe, hii ni kwa sababu yeye pia ni mwingi wa huruma na neema.

Ezekiel 22:30-31.Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.”

Katika kifungu hiki ambacho tunachukua Muda kujifunza leo, Tunaona Mungu akimueleza Mtumishi wake Ezekiel sababu za kuhukumiwa kwa utawala ya Yuda, na kufikia hatua ya Mungu kuliharibu taifa na hata kuruhusu vita na wao kuchukuliwa Mateka ni kwamba taifa lilipoteza watu wenye haki na waombezi, na waonyaji na wale waliokuwa na ushawishi wa kumuomba Mungu kwaajili ya watu hata Mungu akasikia.

A.     Hali ya taifa zima ilikuwa ni hali ya dhambi na watu walikuwa wameharibika

1.      Viongozi wa serikali walikuwa wameharibika sana
a.      Walifanya ufisadi na kupokea rushwa
b.      Makunani nao walikuwa wamejiingiza katika anasa za dunia na kuacha utumishi wao
c.       Watu wengi wa Mungu walijishughulisha na utafutaji mali, wakitafuta mali za ulimwengu
d.      Maswala ya ibada yalionekana kuwa ni ushamba, na kupoteza muda
e.      Walilitafasiri neno la Mungu kwa kusudi la kupata hekina na sio kuliamini
f.        Manabii wengi walikuwa hawakemei uovu bali waliwatabiria watu amani amani
g.      Walitabiri ushindi hata pale ambapo watu walikuwa wameshindwa vibaya kiroho
h.      Walitabiri amani wakati Mungu alikuwa amekusudia vita na hukumu
i.        Waliwatabiria watu kuwa na mali wakati Mungu alikusudia wawe mateka
j.        Watu walikosa Muongozo wa kiroho na walikuwa waliangukia katika 

B.      Mungu alikuwa anatafuta mtu atalayelitengeneza Boma na kusimama mahali palipobomoka

1.      Mungu ni mwingi wa rehema na neema angeweza kuwasamehe endapo angepatikana mtu wa kusimama mahali palipobomoka na kulitegeneza boma Yeremia 15:1Ndipo Bwana akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao.Mungu aliwakumbuka watu wenye haki walioweza kudumisha uhusiano wao na Mungu kiasi ambacho Mungu aliweza kuwasikiliza walipofanya maombezi kwaajili ya taifa na Mungu akasikia dua zao mfano Musa na Samuel, lakini kwa vile hakuona watu wa kiwango hicho aliweza kuwahukumu watu wake.

a.      Mungu hakupata watu au mtu wa kulitengeneza Boma, katika lugha ya kiingeza neno boma linasomeka kama “HEDGE” hii ni aina ya miti au maua magumu yaliyotumika kupandwa shambani au nyumbani kwa kusudi la kuweka uzio ili kuzuia uvamizi na uharibifu kwa mazao au uvamizi nyumbani au katika makazi yaliyokusudiwa kulindwa.

b.      Watu wanapofanya dhambi uzio huo unakuwa umebomoka katika ulimwengu wa roho na unaweza kuruhusu Hasira za Mungu kupita na kufanya uharibifu kwa hiyo ni lazima awepo MUOMBEZI, mtu atakayelia na kuomboleza kwaajili ya kuwaombea watu rehema kwa Mungu, ni aina hii ya watu ndio Mungu anawatafuta hapa Katika Yuda Mungu hakuwaona hao.

i.    Watu walikuwa busy na ujenzi wa makazi yao
ii.  Watu walikuwa wakijiimarisha kutafuta nguvu za kiuchumi na kujiongezea mapato
iii.Watu walijishughulisha na Mashamba yao, vyote havikuwa vitu vibaya lakini vitakuwa na faida gani kama Mungu ataruhusu Moto na uharibifu wa hukumu yake usambaratishe hayo yote na kwa kweli vilisambaratishwa.
c.       Mungu hakuona mtu na kwa sababu hiyo aliruhusu uharibifu kuiharibu Israel.

Hitimisho.

Ni muhimu kufahamu kuwa wanapokuwepo watu ambao Mungu anawaheshimu kwa kiwango cha Musa watu hao wana ushawishi mkubwa wa kuweza kumuomba Mungu au kumsihi Mungu kubadili maamuzi yake, Mara kadhaa Mungu alikusudia kuwafutilia Mbali wana wa Israel Pale walipomuudhi lakini Musa alisimama kwa nguvu na kumwambia Mungu HAPANA angalia  Zaburi 106:23 “Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.” Mungu anatafuta viongozi wa Kisiasa, viongozi wa dini na watu wacha Mungu watakaodumisha uhusiano wake na yeye na kuleta mapinduzi makubwa ya kijamii, kiroho na mabadiliko makubwa na kusababisha watu wamche Mungu na kumgeukia yeye, watakaoleta uamsho, wakataokomesha ufisadi, na kuifanya taifa kutembea katika uadilifu, Mungu anatafuta waombaji, watu watakaosimama kumshawishi aisamehe Familia, ukoo wako, taasisi yako kijiji chako na wilaya yako mkoa na taifa, wakikosekana watu wenye ushawishi wa iana hii katika Taifa lazima hasira ya Mungu itashuka na hukumu kubwa itafuata, Kama taifa halina viongozi wa kiserikali, waombaji na makuhani na manabii wanachekelea dhuluma ikifanyika, mizani zikivurugwa, haki zikipindishwa taifa lazimalitaanguka tu, Haki huinua taifa bali dhambi ni aibu ya watu wote, Hatuna budi kuhakikisha kuwa tunasimama katika zamu yetu kwa haki na kuliombea taifa.

Ni aibu Mungu kukosa waombaji, Mungu anapokosa waombaji katika jamii anaibomoa jamii hiyo na kuisambaratisha, anakuwa hana namna nyingine zaidi ya kuihukumu, Mungu anatoa wito wa watu kurudi magotini, kuomba kwa siri na kuwa watu wenye kuiombea jamii na taifa, watu wengi waombaji wametoweka Duniani leo na mambo yanakwenda Kombo, Mungu anatafuta mtu atakayesimama mahali palipobomoka na kulitengeneza Boma ili asiharibu Nchi.

*Rev. Innocent Kamote*
*Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima*.

Hakuna maoni: