Jumapili, 28 Aprili 2019

Sitakupungukia wala sitakuacha!

Mstari wa Msingi: Yoshua 1:5-8 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako”.



Jumatatu ijayo kidato cha sita kote Nchini wanatarajia kuanza mitihani yao ya kumaliza Elimu ya juu ya sekondari, nafahamu sana katika wakati huu wengi watakuwa wana hofu kwamba mambo yatakuwaje japo kweli wengi wamejiandaa vizuri na hawana wasowasi kabisa kukabiliana na mtihani huo, lakini hata hivyo Mungu alinipa neno hili maalumu kwaajili yao kwamba “Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.” Kumbukumbu la Torati 31:8

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maisha wakati mwingine tutakabiliana na changamoto za aina mbalimbali, ziko changamoto nyingi lakini mojawapo ya changamoto kubwa ni pale unapodhani kuwa uko peke yako au unakabiliana na muda ambao utabaki mwenyewe na wakati huo utapaswa kutatua changamoto zinazokukabili ukiwa peke yako, Bila mtu aliyekuwa anakupa msaada wa karibu, Mungu alifanya kazi na Musa kwa kiwango kikubwa na cha ajabu, Mungu pia alifanya kazi na Yesu Kristo kwa uweza mkubwa na waajabu, Musa alipokuwa ameondoka Yoshua alibaki mwenyewe na hivyo alikuwa na mashaka makubwa kuwa itakuwaje endapo atakabiliwa na changamoto nzito zilizoko mbele yake, sio hivyo tu hata wakati Yesu anaondoka wanafunzi wake walikuwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba itakuwaje Jibu sahihi katika wakati huu lilikuwa ni kuwahakikishia kuwa nitakuwa pamoja nanyi, Mungu alimuhakikishia Yoshua kuwa atakuwa pamoja naye hatampungukia wala hatamuacha

Ni rahisi kwetu wanadamu tunapopita katika changamoto ngumu huku tukifikiri kuwa hakuna msaada ni rahisi kwetu kupiga kelele za kibinadamu kama zile alizopiga Yesu Kristo pale msalabani baada ya mateso mazito “Mungu wangu mungu wangu mbona umeniacha?” Mungu katika neno lake ameahidi mara kadhaa kwani anatujua vema umbo letu anajua udhaifu wetu na ameahidi kuwa hatatuacha kamwe, ushindi wetu katika maisha yetu unaanza na ujasiri huu kwamba Mungu yuko Pamoja nasi, Hatatuacha wala hatatupungukia.

Tunapokaribia kuingia katika vyumba vya mitihani wiki ijayo, ni kweli kuwa tutakaa wenyewe mbali na wenzetu mbali na walimu, tutakuwa tukikabiliana na maswali yaliyotungwa na watu tusiowajua sisi, wasio walimu wetu sisi na hivyo ni rahisi kuogopa mtihani kwa sababu tu umepewa jina la mtihani wa kitaifa, lakini hata ujapokuwa peke yako katika chumba chako cha mtihani kumbuka kuwa Bwana anatangulia mbele yako hatakuacha kabisa wala kukupungukia kabisa. Hakuna mtu alipewa wajibu wa kufanya na Mungu kisha Mungu asiwe pamoja nae, mmepewa wajibu wa kusoma kwa sasa na hilo ndio kusudi la Mungu kwaajili yenu katika kusudi hilo Bwana atakuwa pamoja nanyi, MSIOGOPE.

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; NA TAZAMA, MIMI NIPO PAMOJA NANYI SIKU ZOTE, HATA UKAMILIFU WA DAHARI

Hakuna maneno ya muhimu kama haya wakati tunakabiliana na changamoto yoyote mbeleni Mungu akikuambia kuwa yuko pamoja nawe tayari hii ni alama kubwa sana ya ushindi, lakini akikuambia kuwa hatakuacha wala nhatakupungukia ni zaidi ya ushindi, yeye atakuwa pamoja nawe ahadi hii imerejewa mara kadhaa katika maandiko kwa kusudi la kutuondolea woga na kutupa ujasiri na moyo wa kujiamini, kwamba atakuwa pamoja nasi, katikwa wakati wa msahaka na wasoiwasi kumbuka atakuwa pamoja nasi kwa uwepo mkubwa sana.

Mungu alimwambia Yakobo katika Mwanzo 28:11-17 “Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. NA TAZAMA, MIMI NIPO PAMOJA NAWE, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.

Mungu anataka tuwe na ujuzi huu, kwamba yuko pamoja nasi, ujuzi wa aina hii ukiwa wazi mbele yetu hatutaogopa, tutakuwa na ujasiri, kwamba hata iweje yuko Mungu ambaye ni Mchungaji mwema na hivyo hatutapungukiwa na kitu, kwa vyovyote vile hatatupungukia wala hatakuacha hata tujapopita katika uvuli wa mauti

Daudi alipoifahamu siri hii hakuogopa alimtegemea Mungu na alijua wazi kuwa Mungu ni Mchungaji wake na kwamba hatapungukiwa, wala hataogopa mabaya au vitisho kwa maana yeye yupo pamoja naye, Hofu ni adui mkubwa wa mafanikio yetu, wanafunzi wengi wenye akili na uwezo wanaweza kufanya vema siku zote lakini wanaweza kuharibu wakati wa mitihani kwa sababu shetani huwatia hofu huwaogopesha lakini leo Bwana amenituma nikuamnbie kuwa usiogope Bwana yu pamoja nawe

Zaburi 23: 1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana WEWE UPO PAMOJA NAMI, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.   Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.

Yoshua alichoambiwa na Mungu ni kuliamini neno lake tu, kwamba alisome, alitafakari na kulitii na kulifuata na kuwa akifanya hivyo haitakuja itokee amepungukiwa na kitu, Hutapungukiwa na kitu Yesu akikutuma, hii ni ahadi katika neno lake anapokuagiza Yesu hata kama huna kitu mfukoni hutapungukiwa 

Luka 22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!

Waebrania 13:5-6 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?

Jambo kubwa na la msingi ni kuamini neno lake, na kulitendea kazi, na ndio maana, Mungu alimwambia Yoshua aliangalie neno la kulitafakari na kulishika atafanikiwa katika kila alifanyalo na kila aendako na kuwa hakuna kiti au mtu atakayeweza kusimamam mbele yake siku zote za maisha yake, Hitler Dikteta mkubwa sana alikuwa ni mtu asiye na hofu askari wake pia hawakuogopa walikuwa watii mno kwa neno la Hitler kwa kiwango cha kufa lakini Hitler anasema alikuwa anaogopa mitihani, sisis hatupaswi kuogopa kwa sababu Mungu ameahidi kwamaba atakuwa pamoja nasi, hii ni ahadi yake kwetu, na ni neno lake kwetu tuamini tu na utaona mafanikio makubwa katika mitihani itakayoanza jumatatu ijayo ya tarehe 6/05/2019 Bwana hatakupungukia wala hatakuacha amini tu neno lake.

Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.

Sisi ni warithi wa Baraka zake Ibrahimu, Ibrahimu baba yetu wa imani alikuwa rafiki wa Mungu, Ibrahimu hakuishi maisha ya hofu Mungu alimtokea na kumwambia wazi kuwa yeye ni thawabu yake kubwa sana na Ngao yake

Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.

Baba katika jina la Yesu nawasogeza kidato cha sita nchi nzima nawaombea mtihani mwema, naamini neno lako litawafikia hata kama wengine wako shule za Bweni na hawajui Mungu amesema nao nini lakini mimi mtumwa wako kwa nenolako ulilonipa nawaombea wote uwe pamoja nao kama ulivyoahidi, katika neno lako, uwasaidie wote wanaokutegemea wewe Bwana nakuomba usiwaangushe ukawafanikishe na uwepo wako ukawe pamoja nao katika vyumba vyao vya mitihani kwaajili ya utukufu wako, asiwepo awaye yote wa kuwatisha wala kuwaingizia hofu, nawakinga kwa jina lako kutoka katika mashambulizi yote ya yule muovu nakusihi ukawe pamoja nao, Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai, Amen!

Na. Rev Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.

Hakuna maoni: