Jumatatu, 29 Aprili 2019

Imekwisha !



Yohana 19:28-30Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.  Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.


Utangulizi:
Mojawapo kati ya usemi wenye maana sana kati ya semi saba za Yesu alizozisema akiwa msalabani na ambazo zinatajwa katika sehemu mbalimbali za injili, moja ya usemi huo wa muhimu ni usemi wa sita wenye Neno IMEKWISHA  ambalo leo katika siku ya pasaka tutachukua muda kulijadili kwa undani na kupata maana iliyokusudiwa, maneno mengine kati ya maneno saba aliyoyasema Yesu msalabani ni pamoja na:-
·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34
·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43
·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27
·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46
·         Nina kiu Yohana 19:28
·         Imekwisha Yohana 19:30
·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46
Maana ya neno IMEKWISHA
Ni muhimu kufahamu kuwa Neno IMEKWISHA ambalo katika kiingereza kiingereza linasomeka “IT IS FINISHED  katika Biblia ya kiyunani yaani Kigiriki linasomeka kama “TETELESTAI  Neno hili ndio neno la Mwisho kabisa katika maneno aliyoyatamka Yesu pale msalabani kabla ya kutamka neno “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu” na kufariki dunia pale msalabani, Neno hili Imekwisha TETELESTAI limetokana na neno TELEO la kiyunani ambalo maana yake ni Kukamilisha kazi, kumaliza kazi, kutimiza kazi, to complete or to accomplish, neno hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu linazungumzia kumaliza kazi kwa furaha, au kwa mafanikio, utamu wa neno hili ni kama vile mtu anapokuwa amemaliza mtihani wa mwisho katika kozi ya mwisho, au mtihani wa mwisho kabisa wa kumaliza shule au chuo au kama vile mtu aliyekamilisha malipo ya mwisho ya ununuzi wa nyumba au gari, (Paid in Full) au kukamilisha kwa usahihi kile ulichowaza au kufikiri kuwa utakifanya na ukakifanya kwa usahihi kabisa, Kama vile Mungu alivyosema tazama kila kitu kimekuwa chema, well done, kazi imefanyika kwa ufasaha.

Lakini ni muhimu kufahamu kuwa neno hili IMEKWISHA liko katika wakati uliopita kwa namna linavyoonekana hapa  lakini katika kiyunani ni sentensi kamili Perfect tense na kwa sababu hiyo neno hili linapata umuhimu mkubwa kwa sababu lina maanisha imekwisha katika wakati uliopita, uliopo na ujao kwa msingi huo neno hili linaendelea kufanya kazi kila siku na kila wakati, Neno hili pia lilimaanisha kuwa kama kulikuwa na deni, basi deni hilo limelipwa milele, wale wamuaminio Yesu hawana wanachodaiwa, kama ilikuwa ni kesi imefutwa na hati za mashitaka zimeharibiwa kabisa Wakolosai 2:14-15 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo”.Neno hili ni kama kupewa ruhusa kutoka hospitalini baada ya kuugua kwa muda na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kila mtu akijua umekwisha kisha ukainuka tena ukiwa mzima wa afya. Ni neno muhimu sana katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu na wokovu wetu.

Umuhimu wa neno IMEKWISHA.

Yesu alipolia kwa sauti kuu IMEKWISHA alimaanisha katika wakati uliopita, sasa na itaendelea kuwa imekwisha hata baadaye. Kumbuka kuwa hakusema nimekwisha hii ingemaanisha kuwa ameshindwa na kifo, lakini alilia akisema IMEKWISHA! maana yake nimeikamilisha kwa ufasaha kazi niliyokuja kuifanya. Kwa msingi huo neno imekwisha lina maana ya hakuna kilichosazwa katika kazi ya ukombozi aliyokuja kuifanya na hivyo alikuwa akizungumza ukweli kuwa kila kitu kimekamilishwa sasa ni mambo gani Yesu aliyakamilisha yako mengi mno lakini baadhi ni pamoja na:-
1.       Alikamilisha kazi yote aliyokuwa ametumwa na baba yake kuja kuifanya duniani Yohana 17:4 “Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.

2.       Alikamilisha kazi ya kuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea Luka 19:10 “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

3.       Alikamilisha kazi ya kutukomboa sisi na adui zetu Luka 1:68-74 “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,

4.       Alikamilisha unabii katika torati na manabii uliozungumza kumuhusu yeye kwa unabii, ishara, alama na vivuli kuhusu ujio wake na kazi zake kutoka kitabu cha Mwanzo mpaka kitabu cha Malaki ambako kuna nabii zaidi ya 300 kuhusu Masihi Mwanzo 3:15 na Isaya 53

Kwa msingi huo hatupaswi tena kuteseka, kuwa watumwa, kukandamizwa, kuonewa, kuugua na kuteswa na magonjwa, kuwa watumwa wa dhambi na shetani, hatupaswi kumuogopa awaye yote, Nguvu za giza, na wachawi na washirikina na waganga, na mapepo na majini na mashetani na shetani hazina uwezo juu yetu kwa imani katika kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani, laana ya torati, na sheria, hatuna deni, hatuna deni la jana wala la leo wala la kesho kazi imekamilika yakikutokea majanga angalia msalaba kumbuka kazi iliyofanyika msalabani, kumbuka kuwa mwanaume huyu amemaliza amakamilisha kazi ya ukombozi huna hatia hata kidogo hakuna wa kukuhukumu, wewe hata kama ulikuwa na historia mbaya sana yeye anawweza kuifuta na kuiandika upya endapo utamwamini Bwan Yesu, Neno imekwisha ni neno lenye nguvu kama vile siku unapotangazwa uhuru wa taifa lililotawaliwa na wakoloni, tunapoadhimisha siku ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo yaani katika siku hii ya pasaka ni lazima tujikumbushe kuwa Yesu amekamilisha kazi ya kutuweka huru na kuvitangazia vifungo vinavyotuzunguka kwa kuvitangazia kuwa imekwisha, Mateso yamekwisha, kazi za shetani zimekwisha, majini na mapepo kazi zao zimekwisha kila aina ya vifungo na utumwa wa ibilisi ni lazima zisikie na kukumbuka kuwa imekwisha

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: