Alhamisi, 2 Januari 2020

Sigara katika mpango wa Mungu!


Mstari  wa msingi: Yakobo 4:17Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia haizungumzi kwa uwazi sana au moja kwa moja kuhusu Matumizi ya sigara, bangi, unga, mirungi, shisha, ugoro  na madawa ya kulevya kwa ujumla katika namna iliyo wazi, Labda ni kwa sababu katika jamii na tamaduni za Israel hili halikuwa tatizo kwa nyakati zile, lakini hii haimaanishi kuwa Mungu anakubaliana na uvutaji wa sigara, bangi, mirungi au madawa yoyote ya kulevya, Badala yake Neno la Mungu lina kanuni na sheria zanazoweza kutuongoza katika kujiepusha ma mambo haya ambayo yameua na kuharibu watu wengi kwa karne nyingi sana huku jamii ikiwa imelikalia kimya swala hili!

Takwimu za haraka haraka zinaashiria kuwa sigara pekee au uvutaji unaua watu milioni saba kwa mwaka 7,000,000. Duniani kote, Na kuwa kama hatua za kijamii hazitachukuliwa kuna uwezekano wa idadi hii kupanda na kufikia  8,000,000. Kila mwaka ifikapo mwaka 2030.

Nchini Marekani pekee watu 480,000. Hufa kila mwaka kutokana na uvutaji wa sigara. Katika nchi ya Tanzania hakuna idadi kubwa ya watu walioripotiwa kufa kwa uvutaji wa sigara lakini takwimu zionaonyesha kuwa wanaume wapatao 244 hufa kila wiki, kwa athari zitokanazo na uvutaji na hivyo kwa mwaka ni wanaume 11,712. Je kanisa na viongozi wa dini wanalichukuliaje swala hili? Kama tutakuwa na ufahamu kuwa sigara pamoja na vitu vingine vinaharibu uhai kwa kiwango kikubwa ni lazima tutalikemea swala hili, “Yeye ajuaye kutenda mema wala hayatendi kwake huyo ni dhambi,” Katika karne iliyopita Duniani watu wapatao 100,000,000. Milioni mia moja walikufa kutokana na uvutaji wa sigara pekee!.
Kwa msingi huo ni muhimu kufahamu kuwa sigara ni muuaji hatari anayedhulumu uhai wa watu kimya kimya. Tutajifunza somo hili Sigara katika mpango wa Mungu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·        Maana ya uvutaji
·        Madhara ya uvutaji
·        Sigara katika mpango wa Mungu.



Maana ya uvutaji:
Uvutaji maana yake ni kitendo cha kuvuta hewa yenye tumbaku iliyochomwa kwa njia ya mdomo mpaka ndani ya mapafu na kuitoa nje, au kitendo cha kuiweka tumbaku iliyosagwa Ugolo katika fizi za mdomoni na kuitunza kwa muda na kuruhusu kilevi chake kupenya kwenye mishipa ya mfumo wa wa kusaga chakula na kuipeleka katika damu. Aidha siagara inapovutwa pia huchukuliwa kwa njia ya hewa kutoka kwenye mapafu na kuingizwa kwenye damu na pia kuufikia ubongo kwa haraka zaidi.
Tumbaku ina aina ya dawa ya kulevywa inayogeuza mwili kuwa tegemezi, na kuleta msisimko wenye kupunguza mkandamizo wa mawazo, dawa hii huitwa NICOTINE, Inapovutwa inaingizwa katika mfumo wa ubongo kwa haraka sana na inaweza kufanywa hivyo kwa kurudia tena na tena,  Mvuto mmoja tu kwa kawaida ni sawa na dose moja ya Nicotine kwa msingi huo mtu anayevuta sigara kwa siku nzima huweza kuzamisha dose zipatazo 200 kwa siku, Jambo ambalo ni sawa na kutumia dose kubwa sana ya Nicotine na kuifanya kuwa dawa inayotumika sana mwilini kuliko dawa nyingine zote. Kitendo cha kuendela kufanya hivyo kinakufanya uwe mlemavu tegemezi wa Nicotine (Nicotine uniquely Addictive) Jambo hili huweza kumpelekea mtumiaji kujisikia kama anaumwa au anajisikia vibaya endapo hatapata kiwango hicho cha nicotine cha kumtosheleza!. Hivyo mwili wa mtumiaji huwa mtumwa wa Nicotine unakuwa tegemezi.

Warumi 6:16Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.” 


Hata hivyo baadhi ya watu wanapingana na swala zima la kukataza uvutaji wa sigara kwa madai kuwa uvutaji sigara sio tatizo, wanajenga hoja kwamba kama uvutaji sigara ni tatizo mbona kuna watu wengi sana ambao wanakula vyakula hatarishi kwa afya zao? Na ambavyo pia vinaweza kuwafanya tegemezi na ni vibaya kwa miili yao, kwa mfano wako walioathirika na unywaji wa kahawa na chai kiasi ambacho hawawezi kujisikia vizuri mpaka wapate kikombe cha kahawa au chai, kama hili ndivyo lilivyo iweje mvuta sigara aonekane kuwa ana tatizo? Kahawa nao ni kinywaji chenye Nicotine kwa wingi! Na Chai pia ina Nicotine kwa kiasi fulani, hivyo wanaotumia je hawawi watumwa? Je is sawa na wavutaji wa sigara?

Wakristo wanapaswa kuitunza miili yao maana miili yao ni hekalu la Roho Mtakatifu ni wajibu wao kujitunza kutoka katika vitu vitakavyodhuru afya zao, ndio ni muhimu huwezi kuwa mkristo mzuri na ukahukumu jambo moja kuwa jema kisha lingine ukalifanya hapo utakuwa mnafiki! Lakini pamoja na hoja hii je Uvutaji unampa a sigara je Mungu Heshima? Nicotine ikiingia kwa njia ya mwilini haina madhara kama ikiingia kwa njia ya hewa na vifo vingi vimeripotiwa kitaalamu kusababishwa na Sigara na sio kahawa wala chai! Vitu na sumu zinazoingia kupitia tumboni huchujwa kwa umakini, kuliko kinachoingia moja kwa moja kwa njia ya hewa kama ilivyo kwa uvutaji wa sigara!

Hoja nyingine ni kuhusu kuwepo kwa watu wengi wa Mungu wanaovuta sigara, ukitembelea Israel njiani utaweza kuona vijana wengi askari wa kiyahudi wanavuta sigara! Lakini vilevile muhubiri maarufu C.H Spurgeon wa Uingereza mbona alikuwa mvuta sigara ? Ukweli ni kuwa kama Spurgeon alikuwa anavuta alikuwa akifanya makosa, alikuwa mtu wa Mungu na muhubiri na mwalimu mzuri ni sawa hii haiwezi kukanushika lakini vilevile hii haimaanishi kuwa matendo yake yote yalikuwa sawasawa! Uvutaji wa sigara una madhara makubwa katika mwili wa mwanadamu na Mungu hawezi kuachilia jambo hili, Mungu amemlinda mwanadamu mara kadhaa katika amri zake zote zikiwa na lengo la kumtakia maisha marefu yenye afya ili waweze kutimiza makusudi yake Duniani.

Madhara ya uvutaji wa Sigara!

Kama tulivyoona awali katika utangulizi kuwa sigara ina madhara makubwa sana katika maisha ya mwanadamu, tumbaku ina aina ya dawa ijulikanayo kama Nicotine ambayo husisimua na kupunguza migandamizo ya mawazo, Mvutaji anapovuta nicotine husafirishwa kwa njia ya hewa mpaka kwenye ubongo kwa haraka sana na kwa sababu hiyo endapo sigara itavutwa mara kwa mara kwa maana ya kuwa mvuto mmoja (Paff) ni sawa na dose moja ya nicotine na ikivutwa mara 200 maana yake ni sawa na matumizi makubwa kabisa ya dawa ya nicotine kwa siku jambo hili ni hatari na lina athari kubwa sana kwa afya zetu.

Biblia inaposema katika Warumi 6:16 Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.”

Inamaanisha kuwa mvuta sigara anakuwa mtumwa wa sigara kwa sababu amekuwa tegemezi wa sigara na hawezi kujisikia vizuri au kawaida bila kuivuta sigara kwa hiyo ni lazima ataitii kiu ya sigara na moja kwa moja anakuwa mtumwa wa kile anachokitii “addiction” Lakini sio hivyo tu Mungu anataka kila mmoja wetu awe mbali na jambo lolote lile linaloweza kuharibu maisha yake yaani jambo linaloathiri miili na roho zetu pia 

2Wakoritho 7:1Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu

Mungu yu ataka nasfi zetu, miili yetu na roho zetu ziwe safi mbele zake, hatuwezi kuyatoa maisha nyetu kwa Sigara, au kuwa watumwa wa sigara kisha huku tukadai kuwa sisi ni watumishi wa Mungu, hatuwezi kuwa tunaitii sigara kisha tukadai wakati huo huo kuwa tunamtii Mungu haiwezekani, Lazima tutambue kuwa Mungu anataka tumpe moyo wote

Luka 10:27 “Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.

·        Imethibitika kisayansi kuwa uvutaji wa sigara unaharibu karibu kila kiungo katika mwili wa mwanadamu na unaongeza kwa kiwango kikubwa uwezekano wa kufa, Matatizo makubwa ya kiafya kama Kansa ya mapafu, Magonjwa ya moyo, na hata TB (tuberculosis) kwa mujibu wa shirika la afya Duniani WHO vimathibitishwa kusababishwa kwa kiwango kikubwa na sigara na uvutaji

·        Moshi wa sigara una kemikali iitwayo Carcinogenic zaidi ya 50 ambayo sio nzuri na kwa mujibu wa The encyclopedia Britannica inaaminika kuwa asilimia 90 ya kansa ya mapafu duniani inasababishwa na uvutaji wa sigara, na pia huweza kusababisha kansa katika viungo vingine ikiwemo kansa yam domo, kansa ya mfumo wa hewa, kansa ya ini, kansa ya kongosho na kansa ya kibofu cha mkojo na uharibifu wa nyongo

·        Aidha moshi wa sigara una madhara makubwa zaidi kwa mtu asiyevuta aliye karibu na anayevuta kuliko hata mvutaji mwenyewe. Katika nchi nyingine, mabasi na kadhalika inakatazwa mtu kuvuta hadharani, sigara huweza kusababishja madhara yaleyale kwa asiyevuta jambo ambalo sio jema hata kidogo,  furaha yako binafsi haipaswi kuwa kero na madhara kwa watu wengine

1Wakoritho 10:24Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake.”

·        Tumbaku pia inachangia kwa kiwango kikubwa magonjwa ya mfumo wa hewa Respiratory diseases ikiwemo PNEUMONIA, NA INFLUENZA  na kwa watoto walio karibu na wavutaji wako katika hatari kubwa sana ya kupata ATHMA na KIFUA SUGU na kuathiri ukuaji wa mapafu na utendaji kazi wake

·        Wavitaji wa sigara wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo pamoja na kupooza STROKE  inasemekana ile CARBON MONOXIDE iliyomo katika moshi wa tumbaku inapenywa kwa urahisi katika mapafu na mfumo wa damu na kuathiri hewa ya OXYGEN, na kutokana na kupungua kwa hewa hiyo ya OXYGEN  inayosafirishwa na damu moyo hujikuta ukifanya kazi kubwa kusukuma hewa safi mwilini

·        Athari kwa wajawazito, kama mwanamke atakuwa anavuta sigara kisayansi kuna uwezekano mkubwa wa kuzaa mtoto njiti, au mwenye uzito hafifu, au matatizo fulani tangu kuzaliwa kwane na pia vichanga hao wanaweza kuwa na tatizo katika mfumo wao wa upumuaji, na wakati mwingine kusababisha kufa ghaflka kwa vichanga hao.





Sigara katika mpango wa Mungu!

Baada ya kuwa tumeona ukweli kwamba sigara zina madhara makubwa mno kwa mwili wa mwanadamu, na kuwa hakuna hasara yoyote mwanadamu anaweza kuipata kama ataacha sigara sasa ni vema kufikiri je ni mapenzi ya Mungu kwa watu wake kuvuta Sigara ? ni uwazi usiofichika kuwa sigara katika mpango au mapenzi ua Mungu haifai, Mungu hakubaliani na uharibifu huu na kwa sababu hiyo sigara ni dhambi, awaye yote anayevuta sigara anafanya dhambi kama alivyo mlevi, mwizi, mwesharati na mtenda dhambi mwingine yeyote tu huu ndio mpango wa Mungu, mtu anapomia Mungu na kutaka kuacha matendo yake maovu lazima akumbuke kuwa sigara nayo ni moja ya vitu ambavyo viko nje ya mpango wa Mungu.

1.      Mwili wako sio mali yako wewe umeazimwa ni mali ya Mungu, Hakuna faida yoyote ya kuvuta sigara, hakuna faida yoyote Ya kiafya badala yake kuna hasara kubwa kwa kuharibu mwili wako ambao ni mali ya Mungu, sigara ni mbaya sana kwa mwili wako na mapafu yako
·        1Wakoritho 6:19-20Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”

    
·        1Wakorithoi 3:16-17 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?  Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

   
·        Warumi 6:13 “wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki.”

2.      Usitiwe chini ya kitu chochote
Je sigara ina faida? Haina faida yoyote ni hatari kwa afya yako na inakushuhsia thamani, inaharibu fedha  na inaathiri familia yako, ina nicotine ambayo inakufanya uwe mtumwa wa sigara inakuweka chini ya utumwa wake umetiwa chini ya sigara, huwezi kuiacha ikiwa imekuathiri na inakutawala
·        1Wakoritho 6:12 “Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote.”
·        Warumi 6:16Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.”

3.      Sigara husababisha kifo, Kama tulivyoona kuwa ndio sababu kubwa ya kansa ya mapafu, na hivyo wanasatansi wanakubali kuwa uvutaji ni sawa na kujiua mwenyewe taratibu, katika amri za Mungu biblia inasema USIUE inawezekana hujiwekei kitanzi, wala hujiwekei bunduki kichwani lakini uvutaji ni sawa na kufanya hayo, unajiua mwenyewe kwa hivyo ni lazima ufikiri wewe mwenyewe kwamba sigara ina faida gani? Katika mwili wako na kisha fanya maamuzi

Kila mwanadamu anatamani kupendwa anatamani kukubalika Lakini wavutaji sigara hawakubaliki na watu wengi na hawapendwi na watu wengi kwa sababu ya kuvuta kwao sigara, wengi wa watu wanaovuta ni wale wanaokabilia na msongo wa mawazo, lakini badala ya kuondoa msongo huo wanajiua kwa kuvuta sigara , wavutaji wanaweza kupendwa, wanaweza kukubalika wanaweza kuwa huru kutoka katika migandamizo kwa kumuamini Mungu na kujitoa kumtumikia yeye, Mungu atakupa amani ya kweli nafuraha ya kweli na atakubadilisha mfumo wako mzima wa maisha ikiwa utayatoa maisha yako kwake na hivyo mtafute Mungu na uachane na dhambi hii ya uvutaji wa sigara
·        Kutoka 20:13 “Usiue.”
·        Yakobo 4:2 “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!”

4.      Swali Je mtu anaweza kusema kuwa anavuta kwa utukufu wa Mungu?
Neno la Mungu linatutaka kwamba lolote tulifanyalo kwa neno au kwa tendo tulifanye kwa utukufu wa Mungu,
·        1Wakoritho 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.”
·        Ni wazi kuwa uvutaji hauko katika mpango wa Mungu, sio tabia njema, inasemekana kitaalamu wavutaji wa Muda mrefu wako kwenye uwezekano wa kufa miaka 10 zaidi kabla ya miaka inayotarajiwa kuishi kwao na wakati mwingine hata mara mbili ya hiyo, ni muhimu kufahamu kuwa sio Mungu anayekusudia kila wakati mtu afikie mwisho lakini watu wenyewe pia wana nafasi ya kufikisha mwisho wao, mtindo wa maisha tunaojichagulia, na kusahau kwetu kuyatii maandiko kunaweza kutufanya tufe kabla ya wakati na tutawajibika kwa hilo
·        Muhubiri 7:17Usiwe mwovu kupita kiasi; Wala usiwe mpumbavu; Kwani ufe kabla ya wakati wako?  Maandiko yanakiri kuwa uovuo kupita kiasi na kuishi kipumbavu kunauwezekano mkubwa wa kufupisha maisha na ukafa kabla ya wakati wako
·        Mithali 10:27 “Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.
5.      Uvutaji wa sigara unawakwaza wengine? Jibu ni ndio
Watu wengi sana hawafurahii wavuta sigara, wala hawataki kukaa karibu nao, lakini vilevile kisayansi Moshi wa sigara unamuathiri asiyevuta kuliko mvutaji hususani kama ukiwa karibu naye na zaidi sana watoto wadogo huathiriwa kwa kiwango kikubwa, utafiti unaonyesha kuwa watu wengi hawatarajii kumuona mtu wanayemuheshimu akivuta Sigara, unaonaje kama ungeliambia kuwa Yesu pamoja na ubora wake wote aliokuwa nao alikuwa anavuta sana Sigara? Au unaonaje kama Mchungaji akimaliza kuhubiri kisha akakaa pembeni na kuwasha sigara yake na kuanza kuivuta? Je hili linaweza kuwa jambo sahihi moyoni mwako? Kwa msingi huo maandiko yanatutaka tuache kufanya mamboi ambayo mengine yanawakwaza wenzetu hata kama kwetu yako sahihi lakini kwaajili yaw engine tuachane nayo

·        Warumi 14:13 “Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha.”
·        1Wakoritho 8:9 “Lakini angalieni huu uwezo wenu usije ukawakwaza wale walio dhaifu.
·        1Wathesalonike 5:22 “jitengeni na ubaya wa kila namna.”

6.      Sigara huathiri zaidi asiyevuta kuliko anayevuta
Kama jinsi ambavyo tumeona awali na pia katika kipengele kilichotutangulia kuwa sigara humuathiri asiyefuta kuliko mvutaji, mvutaji huingiza moshi kwa kasi ya aina fulani na kisha huitoa kwa kasi fulani, asiyevuta huuvuta moshi ule katika hali yake ya kawaida ya kupumua na kuutoa kwa kiwango cha upumuaji wake hivyo moshi mwingi huingia katika mapafu ya mtu aliyeko karibu na mvutaji wa sigara kuliko mvutaji mwenyewe, na kwa sababu hiyo athari ileiloe anayoweza kuipata mvutaji humpata mtu asiye na hatia, hivyo kuvuta sigara mbele ya wasiovuta ni tabia ya ubinasfi na kutokujali wengine aidha ni kuwadhuru wengine na ni wazi kuwa mvutaji anapofanya hivyo amekosa upendo kwa wengine

·        Warumi 13:10 “Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.”

·        Yohana 13:34 “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.”

7.      Uvutaji wa sigara ni upotevu wa fedha
Biblia iko kinyume na matumizi ya fedha kwa kitu kisicho na maana angalia

·        Isaya 55:2 “Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono.

8.      Hakuna mzazi yeyote anayefurahia kijana wake aje kuwa mvutaji
Wazazi wote katika hali ya kawaida hata wa wale wanaovuta hawafurahii kuona vija na wao wakivuta, kuwa kijana wake anavuta huwa wanaumia na kusikitika sana ndivyo ilivyo kwa baba Yesu wa mbinguni.
·        Zaburi 139:13 “Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu.” 

  
·        Zaburi 139:17 “Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake!"   

9.      Wanaovuta sigara wanakwenda Motoni?
Sina mamlaka ya kusema kuwa unakwenda motoni sina, kwa kuvuta sigara? Unaweza kwenda motoni kwa kutokumuamini Yesu kristo, wako watu wengi wanampenda Mungu na wanakiri kuwa Yesu ni bwana, na wamekuwa waathirika wakubwa wa uvutaji waka katika mchakato wa kuacha tunawaombe wanabadilika wengine haraka wengine kidogo kidogo, Wokovu ni neema hauna sana kazi na matendo yetu, hatuokolewi kwa sababu ya matendo yetu bali ka neema 

Waefeso 2:1- 9. “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;        ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu.  Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.

Tunaokolewa kwa neema kwa kuiamini kazi iliyofanyika pale msalabani, kwa damu ya yesu tu, Yesu alishaichukua adhabu yetu, hakuna adhabu tena kwa aliye ndani ya Kristo, Lakini ukiisha kuokolewa na Kristo una wajibu wa kujitia chini ya nira yake na ukimpenda utazishika mari zake sasa basi Roho mtakatifu atakusaidia kutenda kazi ndani yako na kukuondolea kiu ya uovu ndani yako ikiwemo kuvuta sigara
Kama umeokoka hutafurahi wala hutakuwa na amani ya kutenda yasiyompendeza kwa hiyo lazima tukiri, tutubu na kupambana kwa neema yake kuishinda kiu ya sigara na atatusaidia

1Petro 2:24 “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.

1Yohana 1:9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.


Hitimisho.

Neema ya Mungu iko inatosha kabisa kutukamilisha na kutusaidia 2Wakoritho 12:9 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu”. Aidha Mungu ameweka njia kwa kila aina ya jaribu tukimuomba kwa bidii auatuoko na kila aina ya mwenendo wenye kubughudhi nasfi zetu

1Wakoritho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea”, ili mweze kustahimili. Neema ya Mungu iko kutusaidia katika yale tusiyoyaweza kwa nguvu zetu

Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”
Aidha pia unaweza kuwaona madaktari au watumishi wa Mungu kwa ushauri zaidi

Acha sigara, wenye viwanda na watengenezaji wenyewe pia wamekubali na kila pakiti ya sirgara imeandikwa Onyo Sigara ni hatari kwa Afya yako, lakini kama utakuwa mpumbavu ukafuata njia zako mwenyewe basi damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe na utawajibika mbele za Mungu, kwani huu ni ushauri tu na unatokana na hekima ya kimungu, uongezewe neema!
Mithali 12:15 “Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.”

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
0718990796

Hakuna maoni: