Mathayo 26:21-23. “Nao walipokuwa wakila,
alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza
kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono
wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti.”
Utangulizi:
Ndugu wapenzi leo kwa tuchukue
muda kwa undani sana kuzungumzia kwa kina na mapana na marefu juu ya maneno
haya ya msingi sana ya bwana wetu Yesu Kristo; Ufahamu kuhusu maneno haya ya
hekima utamsaidia kila mmoja wetu katika kupunguza huzuni au kujiepusha na
huzuni, zinazosababishwa na watu mbalimbali wanaotuzunguka hasa katika zamani
hizi za uovu!
Aidha ufahamu wa kina na mapana
kuhusu mstari huu au usemi huu wa muhimu sio tu utatusaidia kuweza kujilinda na
watu wenye nia ovu wanaoweza kuyaathiri maisha yetu na tabia zetu na kutufanya
kuwa na maisha mema au mabaya ya machungu au ya majuto lakini yatatusaidia kuwa
na tahadhari dhidi ya watu wanaotusogelea kwa ukaribu kama ni wema au wabaya,
Biblia inasema hivi kwa mfano katika
Mithali 18:24 “Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa
uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.”
Unaona maana yake nini kadiri
tunavyokuwa na marafiki wengi zaidi, au kwa kadiri tunavyokuwa maarufu zaidi
ndivyo tunavyojiweka katika hatari ya maangamizi zaidi, Maandiko yanatutaka
tuwe macho na dunia na kuielewa vema usiishi duniani kana kwamba ni mahali
salama sana, Dunia sio mahali salama hata kidogo, uwe umeoka uwe hujaokoka, uwe
mtu mwema usiwe mtu mwema, dunia sio rafiki yako, ni lazima uishi kwa
tahadhari!
Ni muhimu kufahamu na kuielewa
vema dunia na kuijua ikoje ili uweze kuishi kwa amani, Kanisa au watu wa Mungu
na pia watu wakarimu na wema, mara kadhaa wameshidhwa kuielewa dunia katika
upana wake na matokeo yake wamejikuta wakilizwa, watu wengi sana wewe ni
shahidi wamelizwa na watu waliokuwa karibu nao, wamelizwa na ndugu zao,
wamelizwa na marafiki zao, wamelizwa na waume zao, wamelizwa na wake zao
wamelizwa na watoto wao, wamelizwa na manabii, wamelizwa na maaskofu, wamelizwa
na mashehe, wamelizwa na waganga wa kienyeji, wamelizwa na wapenzi wao,
wamelizwa na wale waliowaamini na kuwaweka karibu na kuwapa siri zao kwa
nini? kwa sababu waliamini kila mtu na
kufikiri kuwa dunia ni mahali salama ni ndugu msomaji wangu ni makosa kufikiri hivyo !
Uishipo duniani ni lazima
ukumbuke nasema tena ni lazima ukumbuke kuwa wewe ni kama kondoo katikati ya
mbwa mwitu usisahau hilo
Mathayo 10:16 “Angalieni, mimi nawatuma kama
kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole
kama hua”
Haya ni maneno ya msingi sana ni
ya muhimu mno kuyakumbuka, duniani kuna wanyama wa aina mbili, wako wanaokula
majani na wako wanaokula nyama, wale wanaokula majani ni wapole sana na kazi
yao kubwa ni kula majani, na wale wanaokula nyama ni wakali sana kazi yao ni
kula wanyama wenzao, kama wewe ni mnayma unayekula majani unapokula majani ni
lazima uinue kichwa chako na kujilinda ili wale wanaokula nyama wasikukule
wewe, kwa sababu wakati wewe unakula nyasi kwa amani yuko mwindaji anaishi kwa
kukukula wewe! Mwenye masikio ya kusikia na alisikie neno hili!
Yeye aliyetia mkono wake katika kombe ndiye atakayenisaliti!
Mathayo 26:23, “Nao walipokuwa wakila, alisema,
Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza
mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja
nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti.”
Turudi sasa katika mstari huuwa
msingi ili kwamba tuweze kuuchambua sasa kwa kina na kujifunza kwanini Yesu
alisema maneno haya! Na yana maana gani? Bila shaka utafahamu kusudi la Mungu
kukufundisha jambo hili, Katika msatri huu kimsingi Yesu alikuwa akifundisha na
kuweka wazi kuwa ataingizwa matatani na mtu aliye karubu sana atasalitiwa na
mtu aliye rafiki, ataumizwa na mtu aliyemuamini sana ataumizwa na mtu aliyemjua
vema sana rafiki aliye karibu, mtu aliyekula pamoja naye mezani pake!
Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati
za Biblia na katika tamaduni za kiyahudi hususani wakati walipokuwa wanakaribia
sikukuu za Pasaka, walikuwa na desturi katika vyakula vyao kunakuwepo na chombo
kidogo kilichoitwa “KOMBE” chombo
hiki kilikuwa kinawekwa mboga chunguchungu zilizochanganywa na siki au
vinegar kwaajili ya kuongeza
ugwaduugwadu katika chakula “appetizers”
kule Tanga watu hutengeneza mbilimbi na kuzikatakata na kuweka pilipili na
kuanika juani na inageuka kuwa siki na wakati wa kula siki huletwa karibu na
kumiminwa katika kibakuli na kuchovya kwa kusudi la kula, kutokana na chombo
hiki kuwa ni chombo muhimu sana kila mtu alikuwa na chombo chake na sio rahisi
kushirikiana kuchovya katika chombo hicho, lakini kama mtu mmeshibana sana ni
rafiki yako wa karibu na unamuamini kiasi cha kutokuogopa mate yake basi
ungeweza kumruhusu achovyee kwenye chombo hicho unaweza kuona!
Kwa hiyo kimsingi, haikuwa lazima
sana kuwa Yuda aliyemsaliti Yesu au watu fulani walichovya katika KOMBE lakini Yesu alikuwa anazungumzia
ukaribu wa mtu atakaye msaliti kuwa ni yule ambaye alimuamini kwa kiwango cha
kuruhusu atowelee tonge katika chombo chake unaweza kuona!
Yesu alikuwa anatutahadharisha
kuwa shetani anaweza kumtumia mtu au watu waliokaribu kwa kiwango cha zaidi ya
rafiki, na kuwa kama hatutachukua tahadhari tunaweza kujikutabtukiletewa au
kufanyiwa madhara na watu waliokaribu au tuliowaamini kwa msingi huo ni vema
ukawa makini sio tu na jamambazo na matapeli lakini vilevile wale
wanaotuzunguka, watu wengi wana shuhuda za kuumizwa na wale walio karibu nao au
wale waliowaamini, watu waliosomea maswala ya human intellectual na human
intelligence wanasisitiza sana kuwa usimuamini mtu yeyote yule, wengi wamelizwa
kwa kuwaamini na kujimwaga kichwakichwa kwa watu waliokuwa karibu nawe!
Zaburi 41:9 “Msiri wangu tena niliyemtumaini,
Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.”
Lazima kila mwanadamu awe makini,
ni lazima tujifunze na kuelewa kuwa wako watu watakaoonekana wanatupenda katika
maisha yetu, wanaandamana nasi, wako nasi katika kila jambo jema na baya
wanaokana kuwa rafiki, wanaonekana kutoa msaada ulio karibu lakini wanatusaliti
wanatuuza kwa vipande thelathini vya fedha. Yuda alikuwa mwanafunzi muhimu
katika wanafunzi wa Bwana Yesu alipatikana kwa maombi kama ilivyo kwa wengine
Yesu alimuamini kwa kiwango cha kuwa mweka hazina wake
Yohana 12:4-6 “Basi Yuda Iskariote, mmojawapo
wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, Mbona marhamu hii
haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? Naye aliyasema hayo, si kwa
kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko,
akavichukua vilivyotiwa humo.”
Unaona Yesu alimuamini Yuda
alimchagua awe miongoni mwa wasaidizi wake lakini huyu ndiye aliyemsaliti, huyu
ndiye aliyemuingiza matatani na aliyemuingiza katika aibu kubwa sana na
kubadilisha historia ya maisha ya Yesu, ilikuwa ni jambo la kusikitisha mno!
Kaka zangu dada zangu Neno la
Mungu linatuonya kuwa tusimuamini mtu yeyote, sitaki unielewe vibaya kuhusu
kuwa na marafiki, sitaki uninukuu vibaya kuhusu watu wanaokuzunguka lakini Neno
la Mungu halidanganyi linasema ukweli na ukweli utabaki kuwa ukweli siku zote
usimuamini mtu awaye yote adui wa mtu ni
watu wa nyumbani mwake mwenyewe angalia katika
Mika 7:5-6 5. “Msimwamini rafiki, msimwekee
kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye
kifuani mwako asijue habari. Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti
huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye;
adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe”
Wako watu wamesalitiwa na rafiki
zao, na wasiri wao, na wale waliokuwa karibu nao, wako watu wameibiwa na
kutapeliwa kwa kuwaamini watu, wamejeruhiwa, na watu wa karibu zao, kwa
kuwamini, watu wameozwa wanawake bomu kwa ushauri wa wachungaji wao,kwa ushauri
wa wazazi wao, kwa ushauri wa shangazi zao, kwa ushauri wa rafiki zao, kwa
ushauri wa watu wao wakaribu waliowaamini watu wameachwa na wachumba zao
wakaolewa rafiki zao wa karibu waliowaamini, watu wamepinduliwa na mahause girl
waliowatoa vijijini wakawathaminisha, watu wamesalitiwa na wachumba zao wake
zao waliowasomesha, watu wameharibiwa
ndoa zao na wale waliokuwa karibu nao kama family friends, kuna vilio kila
mahali kuna misiba kila mahali kuna kesi za wizi wa kuamini wa makahamani na
polisi watu wakiwa wamedhulumiwa na watu waliowaamini, watu wameibiwa kwa njia
ya simu na matapeli waliotumia namba za watu wanaowaamini, yeye aliyetia mkono
wake katika kombe ndiye atakayenisaliti.
Wako watu wanaogopa leo kutoa
hata lifti ya gari zao kwa watu wema kutokana na mambo yaliyowakuta, wako
wachungaji walioumizwa na wale waliowaamini na kuwafanya kuwa wasaidizi wao,
wako walioumizwa na rafiki zao, wako walicholonga misheni za kuibiwa kupitia
rafiki zao, wako watu walikuja kugundua kuwa wake zao wamejenga mwakwao bila
wao kujua, wako watu wamechomekewa na kulea watoto wasiokuwa wao, wako watu
wamekodi teksi wakaibiwa, wako watu walomini nyumba za wageni wakaibiwa,
Nataka kuchukua nafasi hii
kukutia moyo wewe leo kuwa simama na Yesu, wanadamu waangalie mara mbilimbili,
jihadhari nao, wanapokusifia angalia, wanaokuzunguka kuwa makini nao yeye
aliyetia mkono wake katika kombe ndiye atakayenisaliti ni wale tuliowaamini kama
afamily friends ndio baadaye walitembea na wake zetu, waume zetu, wale
tuliowaamini kama ndugu wakalala katika vyumba na watoto wetu wa kiume ndio
waliowalawiti, wale tuliowaonyesha tuliyo nayo ndio waliochonga mchongo
tukaibiwa, wale waliotuoana tukitoa fedha bank ndio waliopigia simu majambazi.
Watu wanaoweza kuharibu maisha yetu na kuyapa mwelekeo mwingine ni wale
tuliowaamini, wako bodaboda wameuawa na hata kuporwa bodaboda zao wakifikiri
wamepakiza watu wazuri, wako watu wametoa lifti kwa nia njema kwa watu wenye
nia ovu na wakaingia matatani, wako watu wamepokea zawadi kwa watu waliowaamini
wakajikuta wanatapeliwa, wako waliolizwa kwa majina ya viongozi wa kisiasa
waliowaamini, Kanuni ya kibiblia inatutaka tusimuamini awaye yote kwa asilimia
100%.lakini tusiiishi kwa mashaka, Lakini tumuamini Mungu na kumuomba kila siku
katika sehemu ile muhimu Yesu alitufundisha “USITUTIE MAJARIBUNI LAKINI UTUOKOE NA YULE MUOVU” Mungu atupe kuwa
na macho ya rohoni na hekima na ujuzi kuhusu neno lake ili tusiwe miongoni mwa
watu watakaoumizwa kwa wale tuliowaamini Yeye aliyetia mkono wake katika kombe
ndiye atakayenisaliti.
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
0718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni