Jumatatu, 29 Juni 2020

Jinsi ya kushinda vikwazo ulimwenguni!

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.



Utangulizi:


Maisha yetu Duniani yamejaa yamejaa milima na mabonde, kila mwanadamu anapozaliwa duniani ni kama ameletwa ili aweze kupambana na changamoto mbalimbali, kuna nyakati za giza na kuna nyakati za nuru, Katika nyakati hizo za changamoto mbalimbali, wengi wetu tunaachwa na maumivu makubwa na mateso ya aina mbalimbali na wakati mwingine tunaweza kupoteza tumaini, wakati mwingine tunaweza kujiuliza hivi kweli Mungu yupo? Na kama yupo anaona haya tunayoyapitia? Tunaweza kujikuta tunakata tamaa na kuvunjiika moyo na  kupoteza imani kwa Mungu!, Kristo Yesu katika Yohana 14-16 alipokuwa anahitimisha safari yake ya kazi duniani alianza kuzungumza maswala kadhaa ynayoashiria dhiki itakayowapata wanafunzi wake neno analolitumia Yesu hapo ni TRIBULATION ambalo maana yake ni mateso, taabu, changamoto au vikwazo vya namna mbalimbali anaonyesha kuwa haya yapo kwa sababu tuko duniani kwa hiyo katika maisha ni lazima tukutane nayo na kuyakabli, kwa msingi huo kama watu wa Mungu hatupaswi kuvunjika moyo kutokana na vikwazo mbalimbali na badala yake hatuna budi kukabiliana navyo kwa imani na kuhakikisha tunatoboa anga jingine katika maisha haya hii ni kwa sababu Yesu ametuhakikishia ushindi siku zote za maisha yetu! Na adui yetu mkuu amekiwsha kushughulikiwa, Yesu sio tu ameushinda ulimwengu lakini pia ametuachia njia ambazo kwa hizo tunaweza kushinda vikwazo vyote! 1Petro 4:12 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.    

          
1.        Kumbuka  Hakuna jambo lililo gumu la Kumshinda Mungu

a.       Mwanzo 18:13-14 “BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.”  Abraham na Sara walikuwa wakitazamia kupata mtoto na muda mrefu sana ulipita hata wote wakawa wazee Sara akakoma katika siku zake za kawaida ya wanawake Hata Mungu alipowatokea na kuwaahidi kuwa watapata mtoto Sara alicheka sana bila shaka alifikiri inawezekanaje katika uzee kama ule yeye kupata mtoto Mungu alimjibu Abrahamu kuwa Hakuna neno lililo gumu la kumshinda Bwana !


b.      Hesabu 11:21-23 “Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu sita mia elfu waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima.  Je! Makundi ya kondoo na ng'ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha? Bwana akamwambia Musa, Je! Mkono wa Bwana umepungua urefu wake? Sasa utaona kwamba neno langu litatimizwa kwako, au sivyo.” Mungu alipokuwa amewaokoa wana wa Israel kutoka utumwani kule Misri alianza kuwalisha jangwani kwa chakula maalumu kutoka Mbinguni kiitwacho mana kwa muujiza hata hivyo wana wa Israel walianza kulalamika kuchoshwa na chakula hicho na wakaanza kumdai Musa awape nyama jambo hili lilionekana kama haliwezekani kwa Musa lakini Mungu aliahidi kuwa atauliza mkutano ule kwa nyama tena sio katika siku moja bali mwezi mzima mpaka wazikinai musa aliona kama jambo hili ni jambo lisilowezekana lakini Mungu alimjibu kuwa Hakuna lisilowezekana kwa Mungu!


c.       Yeremia 32:17 “Aa! Bwana MUNGU, tazama, wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza;” Hakuna jambo lolote lililo gumu asiloliweza Bwana Mungu wetu hivyo tunapokutana na changamoto za aina mbalimbali hatuna budi kuliitia jina la Bwana kwa imani tukijua ya kuwa Mungu wetu anaweza na atatusaidia na kutukomboa na kutupa ushindi katika hali yoyote tunayoipitia wengi tuliomtumaini alitusaidia na kutukomboa na kututoa katika kutazamia kwa adui yetu .


2.       Kumbuka shuhuda zake


Zaburi 124:1-8 “Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Israeli na aseme sasa, Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu; Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo. Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.Mwandishi wa zaburi hii amejaa shuhuda za Bwana anakumbuka matendo makuu ya Mungu na uwezo wake mkuwa wa kuwaokoa Israel anakumbuka hatari zote ambazo wana wa Israel walipitia na anakumbuka mashambulizi yote wana wa Israel waliyapitia jinsi walivyokusudiwa mabaya au kumezwa hai, anakumbuka hasira za adui zilivyokuwa mbaya sana juu yao lakini Mungu aliiokoa nafsi yake na watu wake anakumbuka kuwa Mungu ni msaada, siku zote tunapokabiliana na changamoto yoyote na jambo lolote lilolo gumu kumbuka shuhuda zake shuhuda za ushidi ndio zitakukumbusha kuwa Mungu ni nani na zitakufanya uione changamoto iliyoko mbele yako kuwa ndogo na kuwa itapita pia ona 1Samuel 17:32-37 “Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai. Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe.” Shuhuda za matendo makuu ya Mungu ni muhimu kwetu, mkumbuke Mungu alivyokushidnia katika mambo mengi makubwa na magumu na jua kuwa Mungu yuleyule aliyekusaidia katika 1 na 2 na 3 atakusaidia na hili unalokabiliana nalo!


3.       Kumbuka Neno la Mungu.

Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.” Neno la Mungu ni sauti ya Mungu lina mamlaka lina nguvu na ufunguo wa suluhu kubwa na nyingi ya maisha yetu, Hatuna budi kulisoma na kulitumia katika kila hali tunayokabiliana nalo, Neno la Mungu lina ahadi na ujumbe kwa kila hali unayokutana nayo duniani na kwa kila changamoto na vikwazo, tafuta ahadi za Mungu na kujifunza kuwa ni jinsi gani Mungu anaweza kutusaidia kupitia hali inayotunzunguka ndani ya neno kumejaa mifano ya jinsi Mungu alivyowasaidia wengine na wakaweza kupenya atakusaidia na wewe katika kila hali inayokukabili!



4.       Kumbuka Roho Mtakatifu.

Bwana Yesu alipokuwa akiwaaga wanafunzi wake na kuwajulisha kuwa watapitia vikwazo vingi, wengi wao walijawa na huzini na kiwewe, Yesu alikuwa anafahamu kuwa watapitia changamoto mbalimbali na kuwa wanahitaji msaada wake aliwaahidi kuwa Roho Mtakatifu atakuwa msaada ulio karibu na hivyo mara kwa mara aliwakumbusha kuwa atawaombea ili Baba aweze kuruhusu ujio wa Roho Mtakatifu ambaya atakuwa msaada ulio karibu kama Yesu mwenyewe ona :- Yohana 14:16-17, Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”  Ni kwa msingi huu nyakati za kanisa la kwanza waliweza kuwa washindi katika majaribu na shida za namna mbalimbali kwa sababu Roho Mtakatifu aliwatia nguvu kukabuiliana na changamoto hizo ona Matendo 4:1-10 “Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano.Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu,  na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu.Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Petro na Yohana waliweza kushinda vikwazo vilivyokuwa vinawakabili kwa sababu waklijaa Roho Mtakatifu, Roho wa bwana aliwasaidia kuwa na ujasiri na kulishuhudia neno la Mungu hata kwa viongozi wa dini waliokuwa wakaidi na waliokuwa kinyume cha Yesu na ndio maana wakati wote Katika nyakati za kanisa la kwanza Mitume na washirika walipotaka kuchagua viongozi moja ya sifa ilikuwa ni kujaa Roho Mtakatifu, kikwazo cha kulihubiri neno kilipowekwa wao waliomba na Mungu Roho Mtakatifu alikuwa juu yao na akawajaza tena na wakalihubiri neno lake kwa ujasiri ona  Matendo ya Mitume 4:23-31 “Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili?  Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta,ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.Kumbe basi tunamuhitaji sana Roho Mtakatifu Msaada ulio karibu kutusaidia wakati wa majaribu, vikwazo mtaabu na mateso pamoja na changamoto mbalimbali tunazokutana nazo katika maisha ulimwengu hautatuweza na magumu yake yote tukimtegemea Roho Mtakatifu na kumjaa yeye katika maisha yetu, kumbuka kuwa dhana hii ya msaada kutoka kwa Roho wa Bwana si ya kiagano jipya tu lakini katika agano la kale tunaona hususani katika kitabu cha waamuzi, pale Israel walipopata vipingamizi na kutumikiswa katika nchi ya kanaani na makabila yenye nguvu Mungu aliwainua waamuzi watu ambao aliwajaza Roho wake mtakatify na watu hao wakawa suluhu ya matatizo ya watu wao Munda hauwezi kutosha kumpitia kila mmoja wetu lakini angalia kwa mfanio maisha ya Samson moja ya waamuzi wakubwa sana na wa kipekee waliofaidika na uwepo wa Roho Mtakatifu nyakati za agano la kale ona  Waamuzi 13:24-25 “Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.kumbe Roho Mtakatifu ndani ya maisha ya mwamini ni msaada mkubwa sana wakati wa vikwazo na vipingamizi vya namna mbalimbali, kama unataka kufurahia maisha ya ushindi katika ulimwengu tulio nao tumuombe sana Mungu na kuishi maisha matakatifu ili tuwe na uhusiano ulio karibu na Mungu wetu Roho Mtakatifu, mara kadhaa tumeona katika maisha ya waamuzi na hasa Samsoni kwamba kila alipokutana na vikwzo Roho wa Mungu alikuja kwa nguvu juu yake na kumsaidia kushinda kikwazo Fulani mbele yake ona kwa mfano katika


Waamuzi 14:1-5 “Samsoni akatelemkia Timna, akaona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti. Kisha akapanda, akawaambia baba yake na mama yake, akasema, Nimemwona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti; basi mnipatie, nimwoe.Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana. Lakini baba yake na mama yake hawakujua ya kuwa jambo hili ni la Bwana; maana alitaka kisa juu ya Wafilisti. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli. Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.“   


Samsoni alipenda Mwanamke wa kifilisti na akazungumza na wazazi wake lakini walijaribu kumpinga mwisho wakakubaliana naye, Biblia inaonyesha kulikuwa na kusudi la Mungu nyuma yake hivyo Samsoni alimtaka mwanamke huyo na walikwenda yeye na baba yake na mama yake lakini njiani mwana simba akamuungurumia Samsoni, simba alisimama kama kikwako kwa Samsoni lakini kwa uweza wa Roho wa Bwana Samsoni alimpasua kama aposuavyo mwana Mbuzi, Roho wa Bwana atatutia nguvu na kutusaidia kila tunapokutana na vikwazo dhidi yetu.


Waamuzi 15:14-16 “Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo; Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfuunataka maisha ya ushindi fanya ushirika wa kudumu na Roho Mtakatifu jaa Roho Mtakatifu!,


5.       Kumbuka Neema


Ni muhimu kufahamu kuwa ujumbe wa biblia nzima hususani agano jipya la bwana wetu Yesu Kristo unahusiana na neema, ujumbe wa injili ni neema Mungu anaonyesha neema yake kwa kumleta Yesu Kristo katika maisha yetu, ameteseka msalabani kw niaba yetu kwa sababu sisi tusingeliweza, Mungu ametusaidia ametusaidia madhaifu yetu, Neema ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu kwa sababu hiyo basi hakuna tunaloweza kulifanikisha sisi wenyewe bila neema ya Mungu, 2Wakoritho 12:9 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.” Unaona neema ni nini neema ni msaada wa upendo na rehema unaotolewa na Mungu kwa wanadamu bila wao kuwa na jambo lolote la kumshawishi, ni uependeleo pasipo kustahili ni kuhesabika kuwa unastahili kupitia kazi ya Yesu Kristo msalabani, Neema ndio iinayotupa kibali hata cha kusogelea uwepo wa Mungu wakati wa maombi ona Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” Tunapokabiliana na changamoto zozote za maisha namna pekee ya kushinda changamoto hizo ni kuitumainia neema ya Mungu, kumbuka kuwa kuja kwa Yesu duniani ni pamoja na kutuletea neema ona Yohana 1:17  “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”  Tunaweza kuwa na maisha ya ajabu na upekee mkubwa sana duniani kama tutajaa neema Luka 1:26-30 “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.  Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Neema ya Mungu itaweka hofu zote mbali na wewe, neema ya Mungu itakupa fadhili ambazo kila mmoja anazitamani, ukiwa umejaa neema ahupaswi kuogopa, watu waliofahamu umuhimu wa neema mara kadhaa walimuomba Mungu wakimsifu na kujumuisha katika maombi yao kwamba Mungu wetu pamioja na mambo mengie amejaa neema Zaburi 103:8-10 “Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.” Kwa msingi huo wakati tunapopitia majaribu na changamoto za aina mbalimbali na jambo lolote lile ambalo kwalo twaliona kuwa ni kikwazo katika maisha yetu ni vema tukakumbuka neema ya Mungu, tukikaribie kiti chake cha rehema kwa ujarisi ili atupatie neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. Yesu alifanikiwa sana katika siku zako zote za maisha yake Duniani kwa sababu alikuwa amejaa neema ona Luka 2:40 “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.” Unaona ili maisha yetu yaweze kuwa na mafanikio ya kila namna tunahitaji neema neno neema katika kiibrania ni CHEN yaani maana yake fadhili, wema kupendelewa na kupewa thamani kubwa na Mungu, na kwa kiyunani neno neema ni CHARIS yaani Msukumo wa Mungu ndani yako unaona, kutokana na hali hii watu walioelewa umuhimu wa neema katika nyakati za agano jipya neema ilikuwa ni moja ya salamu yenye kutakiana Baraka za Mungu hebu jiombee neema kila unapokutana na changamoto na neema hiyo itakubeba!


6.       Kumbuka Imani               

Mara kwa mara Yesu aliwakemea sana wanafunzi wake kwa kutokuwa na imani, aliwaona kuwa hawataweza kukabuiliana na changamoto mbalimbali kama watakosa imani na kwa msingi huo linapokuja swala la kumuamini Mungu Yesu aliwataka wanafunzi wake wawe na imani Mungu hana furaha na mtu anayesita sita ona Waebrania 10:38-39 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.” Watu wote walioshinda changamoto za aina mbalimbali duniani walikuwa watu wa imani ona Waebrania 11:32-38 “Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.”  Imani ni silaha, imani ina nguvu kubwa sana na inatuwezesha kufanya mambo mengi na makubwa sana katika ulimwengu wa roho ona Mathayo 21:21-22 “Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng'oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.” Kwa msingi huo kila mwanafunzi wa Biblia anapaswa kuwa mtu wa imani, tukikosa imani kwa Mungu tutajikuta tunashindwa na kusababisha aibu kubwa katika maisha yetu, kamwe tusikubali kuwa watu wasio na imani amini Mungu ya kuwa atakufikisha katika jambo alilolikusudia katika maisha yako, kutokuamini ni machukizo mbele za Mungu na kunaweza kusababisha ukajikuta unaangamizwa au unakataliwa, Imani katika Mungu na ushindi itatupatia thawabu kubwa sana na tutafanikiwa!



7.       Kumbuka maombi.

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Wote tunafahamu kuwa Neno la Mungu limetufunza kivitendo kwamba maombi yana nguvu na uwezo mkubwa sana wa kubadilisha mambo, kila wakati Yesu na hata mitume walitutaka tukumbuke kuomba Petro alisema na tumtwike yeye fadhaa zetu zote maana anajishughulisha sana na mambo yetu  angalia katika 1Petro 5:6-7. “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.Unaona hii maana yake ni kuwa hatupaswi kusumbuka wala kufadhaika kazi yetu ni moja kila tunapokutana na changamoto za aina mbalimbali tukumbuke kuomba na tuingie kwenye maombi na kuliitia jina la Mungu wetu naye atatusikia tusijali kuwa nini kinanenwa juu yetu au tunatishiwa kwa kiwango gani sisi tukumbuke kuwa kuna majibu katika maombi, Nabii Daniel alikuwa moja wapo ya watu waliokutana na changamoto za aina mbalimbali katika maisha yake lakini alifahamu wazi kuwa dawa ya kuzishinda changamoto hizo ilikuwa ni kumuomba Mungu aliye hai ona katika  Daniel 6:10-11Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.” Tunajifunza pia katika maisha ya mfalme Hezekia alikuwa ni mfalme aliyemcha Mungu na kujaribu kwa kiwango Fulani kufuata njia za Daudi katika utawakla wake alipokutana na changamoto hata za kiafya aliuelekeza uso wake kwa Mungu bila kujali mazingira aliamini kuwa mazingira ya kuomba yatabadili kabisa hali inayomkabili bila kujali kuwa hatari ya kufa imetangazwa na nani ona  2Wafalme 20:1-6 “Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana akasema, Nakusihi, Bwana, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la Bwana likamjia, kusema, Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa Bwana. Tena, nitazizidisha siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.” Maombi yana uwezo mkubwa sana katika maisha yetu, kila aina ya dhiki, kikwazo au changamoto yoyote inaweza kusawazishwa kwa kupitia maombi. Ni kuomba ndiko kutakakotupa ufunguo wa tatizo letu lolote tunalolipitia, Hezekia alikuwa na uzoefu kuwa Mungu anaweza kumponya na janga lililokuwa likimkabili, kwa sababu hata alipopata vitisho kutoka kwa mfalme wa Ashuru aliliitia jina la Bwana kwenye maombi na Mungu alimsikia na kuingilia kati ona  2Nyakati 32:9-22 “Na baada ya hayo Senakeribu mfalme wa Ashuru, akatuma watumishi wake waende Yerusalemu, (naye alikuwapo mbele ya Lakishi, na uwezo wake wote pamoja naye,) kwa Hezekia, mfalme wa Yuda, na kwa Yuda wote waliokuwako Yerusalemu, kusema, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Mwatumainia nini hata mkae mkihusuriwa katika Yerusalemu? Siye Hezekia anayewashawishi, mtolewe kufa kwa njaa na kwa kiu, akisema, Bwana, Mungu wetu, atatuokoa na mkono wa mfalme wa Ashuru?  Si yeye Hezekia huyo aliyeondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaamuru Yuda na Yerusalemu, akisema, Abuduni mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtafukiza uvumba? Je! Ninyi hamjui mimi na baba zangu tuliyowafanyia watu wote wa nchi? Je! Miungu ya mataifa wa nchi iliweza kuokoa kwa lo lote nchi zao na mkono wangu? Ni yupi miongoni mwa miungu ya mataifa wale walioharibiwa kabisa na baba zangu, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, hata Mungu wenu aweze kuwaokoa ninyi na mkono wangu?  Basi sasa asiwadanganye Hezekia, wala asiwashawishi kwa hayo, wala msimwamini; kwa kuwa hapana mungu wa taifa lo lote, wala wa ufalme wo wote, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, au na mkono wa baba zangu; sembuse Mungu wenu atawaokoaje ninyi na mkono wangu? Na watumishi wake wakazidi kusema juu ya Bwana Mungu, na juu ya Hezekia, mtumishi wake.Tena akaandika waraka, kumtukana Bwana, Mungu wa Israeli, na kumwambia, akisema, Kama vile miungu ya mataifa wa nchi isivyowaokoa watu wao na mkono wangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hatawaokoa watu wake na mkono wangu. Wakawalilia kwa sauti kuu, kwa lugha ya Kiyahudi, watu wa Yerusalemu waliokuwako ukutani ili kuwaogofisha, na kuwafadhaisha; hata wapate kuutwaa mji. Wakamnenea Mungu wa Yerusalemu, kana kwamba kuitaja miungu ya mataifa wa nchi, iliyo kazi ya mikono ya watu. Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni. Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga. Ndivyo Bwana alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.Muda hungeweza kutosha kuweza kuonyesha nguvu ya maombi lakini shuhuda hizi chache katika maandiko na zitutoshe kuweza kuonyesha kuwa namna pekee ya kushinda vikwazo vya aina yoyote katika ulimwengu tulio nao ni pamoja na maombi, wakati wowowte tunapokutana na changamoto za aina yoyote ile na tuliitie jina la Bwana naye atatuokoa narudia tena changamoto za aina yoyote!



8.       Kumbuka unyenyekevu.

Moja ya njia ya Mungu ya kutuwezesha kushinda vikwazo na kutupatia neema ni kukumbuka unyenyekevu, Kutembea kwa unyenyekevu kuna faida kubwa sana katika maisha ya mwanadamu, Tatizo kubwa linaloonekana kwa watu wengi sana leo ni kujiamini kunakopitiliza kawaida, ni ukweli ulio wazi kuwa kokosa unyenyekevu kunaleta madhara makubwa sana kuliko unyenyekevu wenyewe, utafiti unaonyesha kuwa watu wanyenyekevu pia wana kiwango kikubwa sana cha self control yaani kujidhibiti, Biblia inatuelekeza na kutufundisha faida kadhaa za unyenyekevu.


a.       Unyenyekevu unaifanya neema ya Mungu kuwa kubwa kwetu Mithali 3:34 “Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema.” Kinyume cha unyenyekevu ni kiburi na tunapokuwa na kiburi na Mungu anatupinga na kuondoa neema yake kwetu


b.      Mungu huwapinga wenye kiburi ona 1Petro 5:5-6 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” 


c.       Kiburi huambatana na fedhea na aibu Mithali 11:2 “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.” 


d.      Unyenyekevu unakufanya uinuliwe juu sana na Mungu Wafilipi 2:6-11 “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba. Unyenyekevu sio ujinga ni hekima Mungu atatuinua wakati wa vikwazo kama tutakumbuka kutembea kwa unyenyekvu mbele zake na kujilinda na kiburi.



9.       Kumbuka uvumilivu.



Changamoto nyingine tunazokutana nazo duniani zinahitaji uvumilivu na subira, wakati mwingine itatuchukua muda mrefu kusubiria kutimizwa kwa ahadi za Mungu wetu katika maisha yetu kwa msingi huo tutajitaji uvumilivu, wengi wetu tunapenda kuona mambo yanatokea kwa haraka katika maisha yetu lakini Mungu anazo njia zake na mojawapo ni kututaka tutembee katika uvumilivu yako mabo mengine hayatokei kwa haraka mpaka tuwe na subira  neno uvumilivu katika kiingereza linatumika neno Persevearence  ambalo maana yake kwa kiingereza ni doing something despite of difficulty or delay in achieving success tunaweza kusema kwa Kiswahili ni hali ya kuendelea kuwa na subira bila kujali muda wala ugumu wa jambo katika kufikia mafanikio Waebrania 12:1-3 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.” Unaweza kuona neno la Mungu linatutaka kustahimili yaani kuvumilia wakati wote tunapopita katika vikwazo, magumu na majaribu ya aina mbalimbali tunapaswa kumuamini Mungu na kuendelea kuwa na subira bila kupoteza matumaini, Mungu anamengi ambayo ametuhifadhia na ana mpango wake kwa kila mtihani tunaoupitia na wakati mwingine kupitia magumu hayo atatokeza mema mbele yetu, Yakobo 5:10-11 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”      

      

10.   Kumbuka furaha.

Mojawapo ya kikwazo kikubwa sana cha mafanikio yetu ni kukubali kuhuzunika, huzuni inaathiri uwezo wetu wa kufikiri, inatufanya tukate tamaa na kufikiri kuwa mwisho umefika usikubali kutawaliwa na huzuni wakati wa changamoto unazozipitia, maandiko yanatutaka tuwe na furaha wakati tunapopitia changamoto za aina mbalimbali ona Yakobo 1:2-4  “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.” Endapo una adui usikubali kumuonyesha adui yako machozi, wakati wote mtegemee Mungu na hakikisha kuwa unafuraha siku zote hili ndio agizo la neno la Mungu Wafilipi 4:4 “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.



11.   Kumbuka Mapenzi ya Mungu.


Maisha hayako chini ya udhibiti wetu, kwa hivyo hatupaswi kijisumbua katika jambo lolote neno la Mungu linasema Mathayo 6:25-27 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Hatuna budi kujiachia katika mapenzi ya Mungu yako mambo ambayo hayako chini ya uwezo wetu yako kwenye mikono ya Mungu hatuwezi kuyadhibiti nsisi wenyewe kwa hiyo ni muhimu kwetu kumuachia Mungu ayashikilie na hayo ndio mapenzi yake, Mapenzi ya Mungu ni ngumu kuyatambua wakati mwingine na hayaelezeki wala huwezi kuuliza kwa nini lakini la msingi ni kuendelea kuamini kuwa Mungu yuko nyuma ya mambo kutusaidia na kutiokeza mema Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.  Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza. Mungu anajua makusudi na mapenzi yake kwa nini aruhusu kupitia unachokipitia yeye anajua kwa undani zaidi, na anajua lililosahihi pale atakapokuja kukufunulia mapenzi yake utakuja kuelewa ni kwanini aliruhusu alichokiruhusu katika maisha yako na kwa nini Mungu alikuacha upitie hilo kwa hivyo ni muhimu kwetu kukubali ilikuwa ni njia ya Mungu kupitia unachokipitia Mwanzo 50:15-20 “Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako.Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.” Angalia mapito yote ya Yusufu na kumbuka mapito aliyoyapitia na angalia mwisho wake ilikuwa njia ya Mungu kumfikisha hapo alipomfikisha kumbe ilikuwa ni njia ya Mungu kumleta katika ngazi hii japo Mungu alitumia njia mbaya ya ndugu zake kumleta hapo alipomleta



12.   Kumbuka kuto-kunungu’nika


Manung’uniko ni moja ya tabia ambayo inafunga Baraka za Mungu, au kuzichelewesha kwetu, Biblia inatutaka tuache kuning’unikiana sisi kwa sisi Yohana 6:43 “Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung'unike ninyi kwa ninyi.Manunguniko yanaweza kuleta adhabu kutoka kwa Mungu 1Wakoritho 10:10 “Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.” Mungu anachukizwa sana na Manung’uniko, manung’uniko kwa sababu manung’uniko kwake ni sawa na 

a.       Kukosa imani
b.      Kusahahu matendo ya Mungu
c.       Hayaondoai tatizo bali yanavunja moyo wengine
d.      Yanaleta ushuhuda mbaya
e.      Yanampa shetani  nafasi ya kulaumu 

Kwa kulijua hili neno la Mungu limetuonya tuacha kabisa kunung’unika na badala yake tumtukuze Mungu na kumshukuru kwa kila jambo, Mitume walikazia sana nyakati za kanisa la kwanza watu waache kunung’unika manung’uniko ni dhambi 

Wafilipi 2:13-15 “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”      
      
Yakobo 5:9 “Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango.” 

1Petro 4:8-11 “Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung'unika; kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.  Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.” Wana wa Israel mara kwa mara walijikosesha Baraka za Mungu kwa sababu ya manung’uniko yao, Manunguniko yanaweza kujibiwa lakini kwa kawaida yanajibiwa vibaya Hesabu 11:1-2 “Kisha hao watu walikuwa kama wanung'unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma.”


13.   Kumbuka Jina la Yesu.


1Samuel 17: 45 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.”  Moja ya siri kubwa sana aliyoitumia Daudi kupata ushindi dhidi ya Adui yake na wa taifa lake ni Jina la Bwana Mungu wa majeshi, Jina hili Nyakati za agano la kale lilikuwa limefichwa sana na lilikuwa ni siri kubwa mno, lakini katika nyakati za agano jipya jina hili tumepewa ni jina lanye kifurushi cha wokovu ni jina pekee linaloweza kumuokoa awaye yote atakayeliitia. Matendo 4:10-12jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”Jina la Yesu ni jina la kipekee sana na Mungu ametupa jina hili ili tuweze kulitumia kwaajili ya utukufu wake, tunapokutana na magumu na changamoto mbali mbali liko jina la Yesu, ni jina la pakee sana Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” Unaweza kuona Yesu mwenyewe amatuamuru kwamba kwa jina lake tunaweza kutatua matatizo na majaribu na changamoto za aina mbalimbali, Jina lake lina nguvu, na lina mamlaka kubwa sana ya kupambana na hali ngumu za namna yoyote, Jina hili ni ngome ambalo tunaweza kulitumainia na tukawa Salama Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.” Kwa kuhitimisha ni muhimu kufahamu kwamba jina la Yesu ni jina lililoinuliwa sana na lina uwezo mkubwa na kwa sababu hiyo zungumza kwa ujasiri na kwa mamlaka kwani jina hili ni silaha kubwa na hakuna vita utaishindwa ukilitumia jina la Yesu! 


14.   Kumbuka kujitenga/kujiepusha (to withdrw) 


Ni muhimu kufahamu kuwa mojawapo ya njia ya kujihami na vikwazo vya aina mbalimbali ni pamoja na kujitenga au kujitoa au kujiepusha njia kama hii inaweza wakati mwingine kutuletea amani na njia kama hii ilitumiwa pia na wazee wetu Abraham na Lutu ona  Mwanzo 13:2-13Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA. BWANA akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.” Unaweza kuona sio lazima ung’ang’ane kitu wakati mwingine kujiepusha kunaweza kuleta suluhu ya kudumu na amani ya kudumu miongoni mwa pande zenye migogoro, jiepushe, aidha maandiko yanatufunza namna Isaka naye alivyokuwa mtu mwema na mwenye kujiepusha na migogoro ya mara kwa mara, akiwa na Abimeleki, walfilistio mara kwa mara walidai kisima alichochimba Isaka  ni chao wakagombania lakini yeye alijiepusha na kuchimba kingine Mungu alimstawisha sana Mwanzo 26:16-22 “Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko.Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Tunaweza kuona kuwa wakati mwingine kujitoa kunaweza kuwa sababu ya kuepuka migogoro na kujiondoa katika changamoto kadhaaa kwa makusudi mema tu, Hili ni jambo la kawaida wanapoishi watu na wakati mwingine ikatokea tofauti tunaweza kuamua kujitioa kwa faida ya pande zote mbili na kwa kusudi la kumpa Mungu utukufu, Jambo hili halikuwahi kutokea kwa wazee wetu tu bali hata wakati wa mitume tena wenye sifa kubwa ona Matendo 15:36-40 “Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro. Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.Unaona wakati mwingine hakuna sababu ya kulazimisha mambo, Shamba la Mungu ni pan asana ni kubwa mmno tunaweza kuamua tu ukielekea kaskazini nitaenda kusini, ili amani iwepo na Mungu akapate kutukuzwa, hakuna sababu ya kumzunguka mtu wala kumtesa “make them happy by your absent if your presence makes them not happy” kama uwepo wako ni tatizo kwako wafanya wenye furaha kwa kuondoka kati yao, aidha pia yako maeneo mengine ambayo kwayo Biblia inatuonya kujitoa ili tusiweze kuharibu uhusiano wetu na Mungu Zaburi 1:1 “Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.” Wakati mwingine ili kujihadhari na vikwazo na majaribu na mapito mbalimbali njia sahihi inaweza kuwa kujitenga au kujihadhari au kuondoka Biblia inatutaka tujihadhari na watu wasioendenda kwa utaratibu 2Wathesalonike 3:6-7 “Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu. Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu;Biblia pia imeagiza kujitenga na watu wanaoleta mafarakano na wenye kukwaza watu Warumi 16:17 “Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao.Pia maandiko yanatutaka tujihadhari na kujiepusha na watu wasiotaka kufanya suluhu wasiotaka mapatano 2Timotheo 3:2-5 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.Pia Biblia inatutaka tujiepushe na jambo lolote lile ambalo haklina faida Tito 3:9 “Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana.” Kumbe basi kujiepusha ni mojawapo ya njia muhimu sana inayoweza kutusaidia kushinda vikwazo vya aina mbalimbali duniani, sio kila kitu kuwa ni lazima ukabiliane nacho vingine vinataka ujiepushe tu!         
                             

15.   Kumbuka kuridhika (To be Content)


Changamoto kubwa sana inayosumbua watu duniani ni kutokuridhika watu wengi wanasumbuliwa na tamaa kwa sababu wanataka kuwa zaidi ya kile walichojaaliwa na Mungu, sio vibaya kunai mambo makubwa lakini ni hatari sana kunai makuu kuliko ikupasavyo kunia, kuwania kuwa nafasi ya kwanza sio jambo baya, kuwania kupata division one sio jambo baya lakini kushindana na Mtu, katika maswala ya mali, fedha na cheo ni tamaa mbaya Warumi 12:1-8 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.”  Watu wengi sana nyakati za kanisa la kwanza walitaka kuwa kama Paulo Mtume, lakini yeye aliwaonya kuwa neema aliyopewa yeye ni tofauti, Mungu humpa kila mmoja karama kwa kadiri ya neema tama ya kuwa kama Fulani au kutaka kumzidi Fulani inaweza kutuletea mambo magumu mno kwa hivyo ni muhimu kuridhikana kile ulichonacho Mungu ameahidi kutokutuacha wala kutupungukia kwa hivyo na tumuombe yeye tuishi maisha ya kiasi Waebrania 13:5-6 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Kama tutaishi maisha yanayompendeza Mungu na tukaishai maisha ya kuridhika Biblia inasema kuna faida kubwa sana kuliko watu wanaotamkani kuwa na mali kwani wengi huangukia katika mitego ya aina mbalimbali 1Timotheo 6:6-11 “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole”. 


Ni muhimu kumsihi Mungu atufundishe kuwa na kiasi, Paulo mtume alifundishwa kuwa radhi katika hali zote hivyo hakukuwa na aina ya maisha yaliyombabaisha wako watu wengine hufa kwa sababu ya mali zao mioyo yao iko katika hizo, lakini kama maandiko yasemavyo hatukuja na kitu duniani wala hatutaondoka na kitu, tukiwanacho kisitupe kiburi wala mabadiliko wala kuinua mabega na tusipokuwa nacho tusimkufuru Mungu ona  Wafilipi 4:11-13 “Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”   

       
                                                                                     
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
0718990796

ikamote@yahoo.com

Maoni 3 :

Unknown alisema ...

Amina mtu wa Mungu kwa somo zuri. Ubarikiwe

Unknown alisema ...

Ubarikiwe sana kwa neno zuri

Bila jina alisema ...

Nashukuru sana kwa hili somo nzuri saaana tena lenye kutuleteya tena faraja katika maisha ya uchristo. Mungu azidi kuwezesha katika kipawa hiki piya akupe maisha marefu.