Luka 13:1-5 “Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya
Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba
Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na
mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo
hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua,
mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?
Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa taarifa
(Habari) ni moja ya nyenzo yenye kubwa sana yenye kubeba maana zinazoweza
kujenga au kubomoa jamii, taarifa zina nguvu, zina nguvu zote mbili za kujenga
au kubomoa, Mungu ndiye mwanzilishi wa taarifa, Alipomuumba mwanadamu alimpa
taarifa ya namna na jinsi ya kuutawala ulimwengu alimweleza kama mtu huru namna
anavyoweza kuutumia ulimwengu na alimuelekeza namna nzuri ya kuutumia ulimwengu
lakini pia alimuonya kuwa kama atautumia ulimwengu vibaya angeweza kuleta
madhara makubwa kwa maisha yake na jamii yake yaani kifo. Taarifa inaweza kuwa
ndogo lakini kama ikitumika vibaya inaweza kuleta madhara makubwa sana kwa
jamii kama njiti ya kiberiti inavyoweza kuchoma msitu mzima!
Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati
za Biblia pia kulikuwa na namna ambavyo watu waliweza kupokea na kutoa taarifa
kama unavyoweza kuona katika kifungu hiki
Luka 13:1-5 “Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya
Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba
Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na
mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo
hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua,
mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?
Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”
Yesu alikuwa amepokea taarifa au
habari kuhusu Wagalilaya waliouawa vibaya na Pilato, na baada ya kupokea
taarifa hizi tunaona namna Yesu alivyozitumia taarifa hizo sasa kuwafundisha
watu wake somo kuhusu toba na pia akiunganisha na taarifa nyingine ya watu kumi
walioangukiwa na mnara huko siloamu, Kutoa na kupokea taarifa ni haki ya kila
jamii, Yesu aliitumia taarifa hii kwa sababu huenda aliamini au kulikuwa na
namna ya uthibitisho kuwa chanzo cha taarifa alichokipokea kilikuwa ni chanzo
cha kuaminika na kwa sababu hiyo taarifa alizozipokea zilikuwa na ukweli, na
hivyo alizitumia kufundisha kama mfano kwa jamii iliyomzunguka, Unapochunguza
kwa kina mafundisho ya Yesu Kristo utaweza kuona alikuwa na mifano mingi sana
na alikuwa na stori nyingi sana na khadithi nyingi sana na nyingi alizitumia
katika kuielimisha jamii na kuijenga kama jinsi Mungu anavyotaka.
Kutokana na kupanuka kwa
technolojia leo hii kumekuweko na vyanzo vingi sana vya kupokea na kutoa
habari, lakini ni jambo la kusikitisha sana kuwa jamii ya leo haizingatii
uadilifu katika swala zima la kupokea na kutoa habari, Mfano mzuri ni tukio la
hivi karibuni ambapo watangazaji/ waandishi wa habari wa TBC walifariki, lakini
wakati huo huo kulikuwa na taarifa za kufariki kwa Mtangazaji wa shirika hilo wa
habari za biashatra aliyeitwa “Gloria Maiko” aidha kabla ya kuenea kwa taarifa
hii kuhusu kufa kwake ilienea taarifa kuwa Gloria anaumwa sana tena ana ugonjwa
wa Corona, Mimi napenda habari, mimi ni mwana habari, mimi nimesoma
Introduction to jounalism, napenda kupata taarifa kwa sababu huwa pia natoa
taarifa yaani nazitumia kuijenga jamii, sio hivyo tu unaposoma chuo cha Biblia
kwaajili ya kazi ya uchungaji hausomei Biblia pekee unaandaliwa pia kuwa mwana
habari kwa sababu kanisa linaweza kuwa na gazeti, Kanisa linaweza kuandika
vitabu, kanisa linaweza kuwa na televisheni, kanisa linaweza kuwa na radio,
kanisa linaweza kuwa na ukurasa wa faceboo, instagram, blog na nyenzo nyingine
za utoaji wa taarifa kwa hiyo lazima watu wa Mungu wawe na angalau ufahamu
mdogo tu kuhusu upokeaji na utoaji wa habari, wakati huu nilisoma chanzo
kingine kuhusu Gloria kinasema hivi ngoja nikinukuu
“TBC1 tuliwaonya kukusanyika siku ya msiba wa
Marini Hassan hamkusikia! Haya leo Joseph Kambangwa mfanyakazi wenu kafa kwa
corona na maziko ni kesho saa 4 huko huko Mloganzila! **Gloria Maiko
(anatangazaga habari za biashara) yuko hoi ana dalili zote za corona! RIP
Kambangwa”
mwisho wa
kunukuu, angalia huyu ni mtu mwenye akili timamu, ni mtu ambaye jamii
inamtegemea, jamii inaamini labda katika hiki alichokisema lakini je habari hii
ilikuwa na malengo gani kwa jamii, ilikusudia nini kwa Gloria? Na kwa familia
yake, je ilikuwa inajenga au inabomoa? Kwa sababu baada ya kuenea kwa Taarifa
hii Gloria Maiko alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii akithibitisha kuwa yeye
yuko hai na wala haumwi! Lakini mwandishi anajisikiaje? Baada ya Gloria
mwenyewe kutokea je wale walioeneza katika mitandao ya kijamii na kutoa salamu
za astarehe kwa amani wanajisikiaje katika mioyo yao baada ya mtu mliyemzushia
kifo kujitokeza na kuonyesha yuko hai, nimetoa tu mfano huu lakini Jambo hili
limewahi kuwatokea wengi, hapa nchini hata Mheshimiwa Augustin Lyatonga Mrema
alizushiwa mara kadhaa mpaka alipojitokeza na kuionya jamii kuwa yeye ni mzima
na kuwa kuanzia sasa atawafungulia mashtaka watu wanaoanzisha uzushi huu, Huko
ulaya mambo ya aina hii yako sana lakini kwa mujibu wa tamaduni zao, Lakini
sisi ni Watanzania na wana Afrika Mashariki je mambo haya ni sawasawa? Je wale
waliosomea uandishi wa habari jambo hili ni sawa katika utoaji wa taarifa na
upokeaji, Je wale wanaozushia wenzao hujitokeza kuomba radhi? Je wanachukuliwa
hatua gani je ni aina gani ya jamii tunaijenga ya watu wanaosema ukweli au
jamii ya waongo? Mungu ametupa hekima na akili na maendeleo makubwa ya nyenzo
za utoaji wa taarifa lakini ni muhimu zikatumika kwaajili ya utukufu wa Mungu,
kwa wakristo tunaambiwa katika maandiko kwamba lolote tulifanyalo kwa neno au
kwa tendo tulifanye kwa utukufu wa Mungu ona
Wakolosai 3:17 “Na
kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu,
mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”
Swali kubwa
ambalo kila mwana jamii anapaswa kujiuliza na kuhoji ni kuwa kama Yesu
angekuwepo Duniani leo ni habari gani angeikubali na habari gani angeikataa na
je angetumiaje mitandai ya kijamii, na sisi vilevile tujiulize je tunapopata
habari ambazo hazina uhakika haziko sahihi, hazina utu, zina mitazamo hasi,
zinaupendeleo, na kama ni za uongo wanaozitoa hawawajibishwi, habari hazina
kiasi, na ziko kinyume na uadilifu je tungejisikiaje? Nafikiri wote tuna namna
ambavyo tunatarajia jinsi habari au taarifa inavyopaswa kuwa! Mkurugenzi wa
Maadili ya uandishi wa habari aitwaye Aidan White anasema ziko kanuni 400
ambazo wanahabari wanapaswa kuzizingatia lakini ziko kanuni 5 Muhimu zaidi
ambazo kila mwandishi na mtoa habari anapaswa kuzifuata bila kushindwa
1. Ukweli na Uhakika (Accuracy)
– “the quality or state of being correct or precise” Maana yake kila mtoa
habari na mpokea habari na mtawanya habari au taarifa anapaswa kuhakikisha kuwa
taarifa anayoitoa ina UKWELI na pia IMEHAKIKISHWA. Lakini pia kuzinagatia
kuwa habari inaweza kuwa ya ukweli na imehakikishwa lakini swali je ni wakati
muafaka kuitoa? Kwa sababu inaweza kuwa kweli na ya uhakika lakini wakati ukawa
hauruhusu kuisema au mazingira yakawa hayaruhusu kusema !, tunapohubiri injili
watu wa Mungu huwa hatuleti maneno ya kushawishi, watu wanapaswa kuziamini habari njema na za
kweli ili wapate kuamini na kuokolewa.
Isaya 53:1 ”Ni nani aliyesadiki
habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?” wale yenye ufundi wa kibinadamu tunapopeleka
habari njema tunapeleka habari ambazo ni za kweli na zinathibitishwa na Roho
Mtakatifu, ile Nguvu ya ukweli pekee inauwezo wa kuwaweka watu huru na kuiponya
jamii. Nyakati za Biblia watu waliwahi kueneza habari za uongo kwaajili ya
faida zao na hivyo ikafikiriwa kuwa Yesu aliibiwa na hakufufuka ona.
Mathayo 28:12-15 “Wakakusanyika
pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema,
Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa
tumelala.Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi
tutawaondolea wasiwasi.Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama
walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo”. Waandishi wa habari ni
kama manabii wanapaswa kutia habari za ukweli na uhakika ona Kumbukumbu la Torati 18:22
“Atakaponena
nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno
asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope”
Biblia liagiza kuwa kama
nabii atatia taarifa na akadai taarifa hiyo imetoka kwa Mungu na kumbe sivyo
yaani haikutimia yaani haina ukweli asiogopwe maana yake achukuliwe hatua, kwa
hiyo kama watu wanaotoa habari na habari zao zikawa sio za uhakika torati
inashauri wachukuliwe hatua katika agano la kale waliuawa, katika agano
jipya wanapaswa kuchukuliwa hatua, Yesu
angelikuwepo leo hangeweza kukubalia habari ambayo haijathibitishwa haina
ukweli na haijahakikishwa! Habari zisizo
za kweli zinaumiza mioyo ya watu na kubadili mtizamo wa mtu Habari za uongo
zinasumbua na kuiumiza jamii Yakobo alilia na kuomboleza kwa miaka mingi sana
baada ya kueletewa habari kuwa yusufu mwanae amekufa ona
Mwanzo 37:31-35 “Wakaitwaa kanzu
ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda
nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue
kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya
mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa.Yakobo akararua
mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe
wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa,
akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake
akamlilia”
Yusufu hakuwa amekufa kweli
lakini wana wa israel walimdanganya baba yao naye akaamini kuwa mwanaye Yusufu
amekufa lakini kumbe habari hii haikuwa sahihi Yakobo aliishi kwa huzuni kwa
miaka 13 akiwa na mtazamo kuwa mwanaye amekufa, Ni mpaka watoto wake tena
walipomletea habari kuwa mwanao Yusufu yuko hai ndipo Roho ya Yakobo
ilipofufuka kwa furaha
Mwanzo 45: 25-28 . “Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba
yao. Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika
nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. Wakamwambia
maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu,
ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka. Israeli akasema, Yatosha!
Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.”
Kumbe sasa tunaweza
kufahamu kuwa habari inaweza kuhuisha au kuua kwa msingi huo ni vema wakristo
wawe makini katika kutoa na kupeleka taarifa, Taarifa inauwezo wa kuua, Habari
inaweza kuwa ya kweli lakini lazima pia inagaliwe namna unavyoipeleka kwa
sababu ina nguvu inaweza kuua au kupoteza maisha ya mtu ona
1Samuel 4:10-17 “Wafilisti wakapigana
nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi
sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani
kwa miguu.Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana
wawili wa Eli, wakauawa. Basi, mtu mmoja wa Benyamini akapiga mbio kutoka mle
jeshini akafika Shilo siku ile ile, hali nguo zake zimeraruliwa, na mavumbi
kichwani mwake. Alipofika, tazama, Eli
alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka
kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji
wote ukalia. Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini
kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli.
Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka
hata asiweze kuona. Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini,
nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu?
Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti,
tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi,
wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa.”
2.
Huru –
Independence – yaani taarifa inapaswa kuwa ya haki isiyopendelea upande wowote, Kila mtoa habari na mpokea habari
anapaswa kuwa na mtizamo wa haki, hapaswi kuwa mwenye kupendelea upande fulani,
mfano kama ni kwa habari ya vyama vya siasa ni vema mtoa habari na mpokea
habari wakawa hawana mtazamo wa kisiasa au mtazamo wa siasa zinazofungamana na
upande fulani, taarifa itolewe kwa uwazi na kwa haki na ihaririwe kwa uwazi na
kwa haki, Maandiko yanatufundisha wale wanaomuamini Yesu kuwa imani yetu katika
Kristo isiwe kwaajili ya kupendelea watu
Yakobo 2:1 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa
utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu” unaona Yesu angelikuwepo leo hangeweza kupokea au kutoa
habari inayomkandamiza mtu fulani haki ingesimama, Wako watu ambao wanaweza
kutoa taarifa lakini kwaajili ya maslahi yao, kwa hiyo kanuni za kiandishi
zinataka watu wasipeleka taarifa kwaajili ya faida yao ona pia
Yuda 1:16 “Watu hawa ni wenye
kunung'unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena
maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.” Kila mpokea habari na mtuma habari hapaswi
kuwa na upendeleo anapaswa kutenda haki kama hakimu Mambo ya walawi 19:15 “Msitende yasiyo
haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali
utamhukumu jirani yako kwa haki.” Maandiko yanamtaka kila mmoja
kutenda haki kuhukumu kwa haki agizo hili sio kwa mahakimu pekee bali na kwa
wanaotoa taarifa na kupokea taarifa au kusambaza taarifa na
Kumbukumbu la Torati 1:16-17 “Nikawaagiza
wakati ule waamuzi wenu, nikawaambia, Sikizeni ninyi maneno kati ya ndugu zenu,
mkaamue kwa haki kati ya mtu na nduguye, na mgeni aliye pamoja naye. Msitazame
nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso
wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo
mniletee mimi, nami nitalisikiza.”
3. Usiyo na Masalahi nayo – Impartiality
kwa kiingereza neno hili maana yake “Impartiality
is a principle of justice holding that decisions should be based on objective
criteria, rather than on the basis of bias, prejudice, or preferring the
benefit to one person over another for improper reasons“ yaani kanuni ya haki
inayotaka maamuzi yafanyike kwa mujibu wa vigezo na sio kwa sababu mtu una
masalahi fulani, au ukungu fulani unaotaka mtu mmoja anufaike dhidi ya mwingine
kwa sababu zisizo sahihi, unapopokea au kutoa habari kwa makusudi maovu au kwa
uependeleo kwa Mungu hufai kuwa mtu wa haki, Yesu angekuwepo leo kwa habari ya
kupokea na kutoa habari angehukumu kwa haki Isaya 11:1-5 “Basi litatoka
chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa
matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya
shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa
katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake,
wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki
atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye
ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua
wabaya.Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia”
Mtoa habari au mpokea habari anapaswa kuwa mwaminifu na kuwa mtu wa haki,
wakati mwingine kwa sababu ya mitazamo fulani na hata kwaajili ya kupokea
rushwa tumepokea au kutoa habari kwa maslahi ya upande fulani kwa sababu
tunaletu jambo, Mungu hapendezwi na utaratibu huo na ndio maana hatua kali sana
zinapaswa kuchukuliwa endapo itabainika mwandishi kuwa ana dalili za kupokea
rushwa.
Nyakati za
Kanisa la Kwanza stephano aliuawa kwa sababu ya maslahi ya watu, na sio kwa
sababu alisema uongo Matendo 6:9-15 “Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la
Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia,
wakaondoka na kujadiliana na Stefano;
lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.
Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya
kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi,
wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi
wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa
patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo
Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.
Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake
kuwa kama uso wa malaika.” Stephano alihukumiwa na kuuawa kwa sababu
ya taarifa za uongo kwa masalahi ya watu wa dini kwa sababu hawakutaia kuambiwa
ukweli, kila mpokea taarifa na mtuma taarifa anapaswa kyuhakikisha kuwa anatoa
taarifa yenye kujenga jamii na sio kuua au kwa sababu ana maslahi nayo.
4. Taarifa yenye kujali utu – Sence of Humanity Ni muhimu
kufahamu kuwa biblia inasema usiue kuua kuko kwa namna nyingi sana unaweza kuua
kwa kutumia maneno, unamuua mtu kisiasa, umamuharibia mtu au unamchafua mtu
huku ni kuua mpokea habari au mtoa habari anapaswa kuhakikisha kuwa anajali
utu, ni dhambi kuandika, kupokea au kutoa habari yenye kudhuru, yenye kuharibu
ubinadamu wa mtu, au yenye kumvunjia mtu heshima hatupaswi kutoa habari wala
kusambaza habari au habari picha yenye kuharibu maisha ya wengine au
kudhalilisha, watu wasiojua kutumia mitandao ya kijamii wanapiga picha hata za
watu waliopata ajali mbaya na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii, katika
nchi nyingi zilizoendelea hata mwili wa Marehemu anapoagwa haupigwi picha,
Picha ya marehemu inayoruhusiwa kuonekana ni ile ambayo wanafamilia wataiweka
juu ya jeneza kwaajili ya kumbukumbu yake, nchi nyingi zawatu wasiostaraabika
utaona mtu aliyepasuka kichwa kwa ajali, waliovunjika miguu, mtu mwenye ulemavu
wa jabu na picha za kutisha sana zinarushwa kwenye mitandao ya kijamii, je
umewahi kujiuliza kwanini mtu akipata ajali watu hutoa nguo zao na kuufunika
mwili wa marehemu? Ni kwaajili ya kujali
utu, Mungu hawezi kukubali na kufurahia utu wa mtu udhalilishwe, kwa msingi huo
kila mtoa habari na mpokea habari namsambazaji anapaswa mno sana kuzingatia
utu, Yesu alikubali kifo cha aibu pale msalabani ili kutunza heshima ya mwanadamu,
natarajia kuona jamii iliyostaarabika ambayo haitarusha picha ya marehemu
yoyote akiwa na pamba puani, wala hata jeneza ikiwezekana na kama umefiwa weka
picha ya aliyefariki ikiwa katika hali ya ubora na usiiwekee “X” muonyehse mtu enzi za ubora wake,
sikitika kwa kumpoteza mtu huyo lakini usimdhalilishe nduguyo, aidha usisambaze
wala usizikubali picha za watu walio katika hali mbaya za ajali, mwanadamu
ameumbwa kwa sura na utukufu wa Mungu na lazima utu wa kila mtu uheshimiwe,
hali kadhalika picha za ngono na zenye kuonyesha uchi ni mwiko kwa watu
waadilifu, Mtu wa haki huwa hadhalilishi mtu mwingine. Mathayo 1:18-19 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama
yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba
kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa
haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.” Mtu wa haki
huwa hafanyi mambo kwa kusudi la kumuaibisha mtu mwingine hata kama mtu huyo ni
kweli amefanya jambo hilo Yesu angekuwepo leo hangekubali kupokea au kutoa
taarifa zinazodhalilisha utu wa mwanadamu ambao ni uumbaji wake.
5. Kuwajibika – accountability
- In ethics
and governance, accountability is answerability, Maana yake kila mtoa habari na
mpokea habari na msambaza habari wanapaswa kujua na kukubali kuwa wanawajibika
kwa habari wanazotoa au kusambaza, kwa msingi huo kama utatoa habari na
ikasababisha madhara au hata isiposababisha madhara ufahamu kuwa unatakiwa kuwa
na utayari wa kuijibia kuitolea maelezo na kuwa tayari kuomba radhi ikiwa
umekosea, au kukubali kukosoelewa na
kupokea maoni ya jamii kuhusiana na ulichokitoa au kukisema na ikiwezekana kuwa
tayari kushitakiwa mahakamani na hata kufungwa na au hata kuuawa na wale
watakaochukizwa na habari ulizozitoa Mfano 2Samuel
1:2-15 “hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu
kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake;
basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia. Daudi akamwambia,
Umetoka wapi? Akamwambia, Nimeokoka katika kambi ya Israeli. Daudi akamwambia,
Yalikwendaje? Tafadhali uniambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi
wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa.Daudi
akamwambia yule kijana aliyempa habari, Umejuaje ya kuwa Sauli na Yonathani
mwanawe wamekufa? Yule kijana aliyempa
habari akasema, Nalikuwapo kwa nasibu juu ya kilima cha Gilboa, na tazama,
Sauli alikuwa ameegemea fumo lake; na tazama, magari na wapanda farasi
wanamfuatia kwa kasi. Naye alipotazama nyuma, akaniona, akaniita. Nikajibu,
Mimi hapa. Akaniambia, U nani wewe? Nikamjibu, Mimi ni Mwamaleki. Akaniambia,
Tafadhali simama karibu nami, ukaniue, maana shida imenipata; kwa sababu roho
yangu ingali hai ndani yangu. Basi, nikasimama karibu naye, nikamwua, kwa
sababu nalijua hakika ya kuwa hawezi kupona baada ya kuanguka; kisha nikaitwaa
ile taji iliyokuwa kichwani mwake, na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, nami
nimevileta hapa kwa bwana wangu. Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua na
kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye; wakaomboleza, wakalia, wakafunga
hata jioni, kwa ajili ya Sauli, na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili
ya watu wa Bwana na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa
upanga. Naye Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Watoka wapi wewe?
Akajibu, Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki. Daudi akamwambia, Jinsi gani
hukuogopa kuunyosha mkono wako umwangamize masihi wa BWANA? Ndipo Daudi
akamwita mmoja wa vijana, akamwambia, Mwendee, ukamwangukie. Basi akampiga hata
akafa.”, kila habari unayoitoa ni muhimu kufahamu kuwa itakugharimu,
Kijana huyu alitoa habari iliyoweza kudhuru maisha yake, yeye alifikiri atapata
sifa kwa Daud lakini kifo cha Sauli na Jonathan haikuwa habari njema kwa Daud
na hivyo kijana huyu aliuawa, habari zinaweza kugharimu maisha yetu mbele za
Mungu na wanadamu, Yesu alisema kila neno lisilo na maana atakalolinena mwanadamu
atatoa hesabu yake Mathayo 12:36-37 “Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena
wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako
utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa” Yesu atakapokuja atawahukumu wazushi wote hapa
aliwaonya watu waliokuwa wakitoa habari zisizo sahihi kuhusu utendaji wa Yesu
Kristo, Yesu anatoa pepo kwa Roho wa Mungu wapotoshaji wakesema anatumia nguvu
za mkuu wa pepo Baalzebub, lazima ieleweke wazi kuwa watoa habari watawajibika
sio mbele za wanadamu tu na mbele za Mungu! Wote tunakumbuka kuwa Sababu ya
kifo cha Yohana Mbatizaji na kuwekwa kwake gerezani kulitokana na kupokea
habari na kuzitumia habari hizo kumkemea Mfalme Herode ona Mathayo 14:3-10 “Maana Herode alikuwa
amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa
Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye
alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii. Hata
ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya
watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote
atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na
mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya
viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru
apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani.” Watoa
habari wengi sana wameuawa na kupotezwa na kufunguliwa mashitaka duniani kwa
sababu ya utoaji habari, habari inaweza kuwa ya kweli na imethibitishwa lakini
kama haikuzingatia kanuni hii ya kuwajibika basi inaweza pia kugharimu maisha
yetu, mtoa habari mpokea habari na msambaza habari wanapaswa kuwa na uangalifu
mkubwa sana namna wanavyopeleka habari
Hitimisho!
Biola shaka kuna kitu umejifunza hapo sisi kama
wakristo ndio chumvi ya ulimwengu napenda kila mmoja wetu aelimike na kukubalia
kujifunza kuwa katika wakati huu wa utandawazi wakati ambapo kila mwanadamu
anauwezo wa kutoa taarifa, kupokea taarifa na kusambaza taarifa ni Muhuhimu
kwetu tukaacha kujisahau na kukumbuka kuwa ziko kanuni za neno la Mungu ambazo
zinatuongoza jinsi na namna ya kuitumia mitandao hii ya kijamii,
ninapohitimisha nataka kukukumbusha mambo kadhaa ya msingi yafuatayo:-
a. Tumia mitandao ya kijamii
kuhudumu kwa neno la Mungu na kusambaza habri njema za Yesu
b. Kumbuka kujitenga kwa muda
na mitandao ya kijamii na kwenda kuomba, Yesu wakati mwingine aliacha makutano
wengi sana na akajitenda kwenda kuomba.
c. Kumbuka kuwakumbusha watu
kutubu na kuishi maisha yanayompendeza Mungu, jitambue kuwa wewe ni mjenzi wa
jamii na hivyo kabla ya kutoa habari tulizozipokea hakikisha kuwa zitakuwa
zenye kujenga, kuonya kukemea kuelekeza na kukaribia kwa kusudi la mkujenga.
d. Kumbuka kutia moyo mambo
yaliyo mema kwa ku like na kuweka maoni yako na kukosoa vikali maovu na
kuonyesha wazi jambo au kitu usichopendezwa nacho tumia neno la Mungu
e. Tumia mitandao ya kijamii
kudumisha uhusiano na kutafuta amani na watu wote na sio kuharibu, hakikisha
nkuwa huondoki katika kusudi lako la matumizi ya mitandao, kama ni injili
injili,
f.
Tumia mitandao ya kijamii kuonyesha semina, mikutano ya neno
la Mungu na maswala muhimu ya kijamii onya karipia fundisha na jihadhari na
matapeli, uwe makini na taarifa zako, maadui wanaweza kutumia taarifa zako
kukudhuru wewe mwenyewe.
g. Zingatia kanuni husika
tulizojifunza na muombe Mungu ziwe kanuni muhimu katika maisha yako, asomaye na
afahamu, ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda,
Na.
Mchungaji Innocent Kamote
Mkuu
wa wajenzi mwenye hekima
0718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni