Jumapili, 3 Oktoba 2021

Jilindeni na chachu ya Mafarisayo


Luka 12:1 “Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki.”


Utangulizi:

Mojawapo ya lengo kuu la kibiblia watu wanapojifunza neno la Mungu kupitia watumishi wa Mungu, ni kuhakikisha kuwa watu wote wanakua kiroho na kiadilifu kwa kumjua Yesu na kukua hata kufikia kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo

Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo

Kristo Yesu Bwana wetu katika mafundisho yake alikuwa na lengo la kumtaka kila Mwanafunzi wa Yesu afikie ngazi ya ukamilifu na kuwa kama baba yetu wa Mbinguni alivyo Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Haya ndio makusudi makuu ya mafundisho yetu kwamba mioyo yetu ifanywe imara ili iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu ona 1Wathesalonike 3:12-13 “Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.”

Kwa msingi huo basi, ili mioyo yetu iweze kuimarishwa, na sisi sote tuweze kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo, na mioyo yetu iweze kufanywa imara, ili tuwe watakatifu na watu wasio na lawama sio kwa wengine tu hata katika mioyo yetu mbele za Mungu, somo hili tunalojifunza leo ni moja ya masomo ya msingi sana katika kuwapata wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo. Kwa msingi huo basi tutajifunza somo hii jilindeni na chahu ya mafarisayo kwa kuzingatia vipengele sita vifuatavyo:-

  • Jilindeni na chachu ya Mafarisayo:-
  • Maana ya chachu ya mafarisayo:-
  • Chachu ya Mafarisayo ni tabia ya shetani:-
  • Chachu ya Mafarisayo ni jaribu la wanadamu wote:-
  • Madhra ya  Chachu ya Mafarisayo:-
  • Jinsi ya kujilinda na Chachu ya Mafarisayo:-

 

Jilindeni na Chachu ya Mafarisayo:-

Moja ya masomo ya muhimu sana ya Bwana Yesu kwa wanafunzi wake ilikuwa ni kujilinda na chachu, Neno hili Bwana Yesu alilirudia mara kwa mara katika injili kuonyesha jinsi alivyokuwa makini na swala hili ona Mathayo 16:6 “Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” Neno chachu kwa kifupi katika maandiko limetumika kuelezea Dhambi Wagalatia 5:7-9 “Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. Chachu kidogo huchachua donge zima.” Kwa hivyo kimsingi Yesu alikuwa anawaonya wanafunzi wake wajihadhari na dhambi ya mafarisayo au masadukayo ambayo ilikuwa ni unafiki,  Yesu alikuwa ameiona dhambi hii kuwa ni dhambi ya kuichukulia tahadhari, kwa sababu kwa kujua au kwa kutokujua Mafarisayo wengi na watu wengi wa dini walikumbwa na aina hii ya dhambi, Ni kwaajili ya haya maandiko yanawataka watu waliomwamini Yesu wawe tofauti. Wakiwa wamejaa, upendo, utokao katika moyo safi na imani isiyo na unafiki. 1Timotheo1:5 “Walakini mwisho wa agizo hilo ni upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na unafiki.” Sio hivyo tu utaweza kuona hata mitume waliwakumbusha wanafunzi wa nyakati za kanisa la kwanza kuwa mbali na uovu wa kila namna lakini pia na unafiki 1Petro 2:1 “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.”

Maana ya chachu ya mafarisayo:-

 

Sasa chachu ya mafarisayo inayotajwa hapa ni hii ni dhambi yao ya unafiki, Unafiki hasa ni nini? Neno linalotumika katika Biblia kuelezea unafiki ni “hypocrisy” – kwa kiyunani ni “Ypokrisia” – tafasiri yake kwa kiingereza ni The practice of claiming to have higher standard or more noble beliefs that the really case, unreality, pretending, kwa Kiswahili ni Hali ya kujionyesha au kujifanya kuwa uko kwenye kiwango cha juu sana au uko vizuri sana kiroho wakati hali halisi haiku hivyo, ni tabia ya kuigiza, ni hali ya kujidanganya mwenyewe, Dhambi hii inaweza kujifunua katika namna mbalimbali mfano Mtu anaweza akakusifia sana lakini moyoni akiwa na kusudi lingine

 

Marko 12:13-17 “Wakatuma kwake baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno. Hata walipofika walimwambia, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo? Tumpe, tusimpe? Naye, akijua unafiki wao, akawaambia, Mbona mmenijaribu? Nileteeni dinari niione. Wakaileta. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana.”

 

Mafarisayo walituma watu kwa Yesu, kwa kusudi la kumjaribu lakini tunawaona wakiwa wanajifanya kumsifia kumbe wakiwa na kusudi la kumleta pabaya, wako watu wa aina kama hizo wakati mwingine ukiona anakusifia tu ujue atakukopa, kwa hiyo unaweza kusifiwa kwa uwongo ili mtu aweze kutimiza maslahi yake

 

Mtu mnafiki pia hufanya jambo kwa kusudi la kuonekana na watu, ili asifiwe, au ili aonekane Mathayo 6:1-6 “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”     

 

Watu wanafiki, hufanya mambo kwa kusudi la kujionyesha tu, au kwa kusudi la kuonekana tu, au ili wasifiwe na watu  wanaweza hata kufanya jambo la kidini kama kusali au kufunga lakini sio kwa dhamiri ya kiungu, Mathayo 6:16-18 “Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”

 

Watu wanafiki huwa na utakatifu wanje tu, lakini ndani ni waovu kupindukia, utakatifu wao ni wa nje tu wao hufanya mambo kwa kusudi la kutaka kutazamwa na watu, au ili waonekane kuwa ni wema na wazuri na watu wakubwa sana  na hujiweka mbele sana katika kila kitu,

 

Mathayo 23:5-8 “Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi

 

Yesu alikemea vikali dhambi ya unafiki kwa sababu, ni udanganyifu wa njia ya nje lakini wanafiki wengi kwa ndani ni watu waliojaa uozo wa kila namna Mathayo 23:23-33 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki,na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. Kijazeni basi kipimo cha baba zenu. Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum? Yesu hakuwahi kuwa na huruma na wanafiki, wala hakuwa na lugha nyepesi ya kichungaji kwa wanafiki Yesu alikemea vikali na kuwaeleza watu waziwazi za uso, aliwapa makavu laivu, walitambua na kuthamini mchango wa Mtu baada ya kufa, lakini alipokuwa hai walihusika kuwaua, hii ndio tabia ya unafiki.

 

Wanafiki huona makosa ya wengine, nay a kwao wenyewe hawayaoni, Luka 6:41-42 “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.”

 

Watu wanafiki huwadharau watu wengine wakijifikiri kuwa wana ubora zaidi kuliko wengine laki mbele za Mungu wamekataliwa Luka 18:9-14 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

 

Yesu hata siku moja hakufanya jambo jema na kutaka kuonekana na watu, Marko 1:40-44 “Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.” Ni watu tu wasiotosha, au wasio jitosheleza kisaikolojia ambao wanataka wakifanya jambo wajulikane, waonekane, na watu, ijulikana wema ambao wameufanya, tabia ya aina hiyo ndio huitwa Tabia ya kinafiki.

 

Mtu mnafiki anaweza kuonyesha kuwa anakupenda usoni kumbe moyoni anatamani ufe, uharibikiwe, ushindwe, uchanganyikiwe na kadhalika, Kaini alimwambia ndugu yake twende uwandani kana kwamba wanakwenda bichi kupunga upepo kumbe moyoni amekusudia kumdhuru Mwanzo 4:8-10 “Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.”

 

Mtu mmnafiki anaweza kuonekana kuwa anakuhug anakukumbatia anakukubali kumbe amekuuza Luka 22:48 “Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu?”mtu mnafiki anaweza kakakubusu kumbe ameshakuuza, wakati wote wanatafuta hila na namna ya kufanya, kuharibu.      

 

Chachu ya Mafarisayo ni tabia ya shetani:-

 

Chachu ya Mafarisayo au dhambi ya mafarisayo ambayo ni Unafiki ni tabia ya shetani yeye ndiye mnafiki wa kwanza, Alionekana yuko bise akimsifu Mungu lakini moyoni alikuwa anatamani kuwa kama Mungu Isaya 14:12-15Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.”  Shetani alionekana Mbinguni akijishughulisha na kazi za Mungu, lakini kumbe moyoni alikuwa mnafiki, na hata leo watumishi wake wote hutembea katika tabia yake ya kinafiki 2Wakoritho 11:13-15 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.”   

Chachu ya Mafarisayo ni jaribu la wanadamu wote:-

 

Chachu ya mafarisayo Ambayo ni unafiki ni jaribu la wanadamu wote bila kujali kuwa mtu yuko ngazi gani ya kiroho anaweza kuchukuliwa na dhambi hii, awe ni mtume nabii na kadhalika dhambi hii inantafuta mtu awaye yote Petro wakati fulani aliwahi kujaribiwa na dhambi hii na mtume Paulo akamkemea mbele ya wote Wagalatia 2:11-14 1Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu. Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao. Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi?         

 

Madhara ya Chachu ya Mafarisayo:-

 

Chachu ya mafarisayio yaani ndhambi hii ya unafiki, Yesu aliikemea vikali sana na kuwaonya wanafunzi wake kwanza kuwa wajilinde na dhambi hii ka sababu Yesu alifahamu kuwa ndio dhambi itakayowapeleka wengi motoni Yesu alionyesha kuwa moja ya makundi ya watu watakaopata adhabu ni pamoja na wanafiki  Mathayo 24:48-51 “Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”

 

Ukiacha kuwa wanafiki watahukumiwa na kupewa adhabu kali lakini vilevile wanafiki ndio wanaofanya imani ya bwana wetu Yesu Kristo itukanwe kwa sababu wanawafungia watu, wasiuone ufalme wa Mungu huku na wao wenyewe hawaingii ona Mathayo 23:13, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.,15 Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe.”

 

Unafiki utaleta aibu kubwa sana siku ya hukumu heri kila mmoja atubu sasa Muhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.”

Jinsi ya kujilinda na chahu ya mafarisayo:-

Kila mmoja atubie dhambi hii na kuhakikisha kuwa anakuwa mkweli ndani nan je maandiko ynasema Afichaye dhambi zake hatafanikiwa, Bali aziungamaye na kuziacha atapata rehema Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Hakuna maoni: