1Wafalme 6:7. “Na nyumba ilipokuwa
ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala
shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa
ikijengwa nyumba.”
Utangulizi:
1Wafalme 6:7. “Na nyumba ilipokuwa
ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala
shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa
ikijengwa nyumba”
Moja ya mambo makubwa sana na ya
kushangaza ya zamani ni pamoja na teknolojia waliyoitumia katika ujenzi. Uwezo
wao na ustadi wao wa ujenzi ulikuwa ni wa hali ya juu sana, Hekalu la Suleimani
limeingia katika orodha ya moja ya maajabu makubwa ya kale ya Dunia kutokana na
ubora na uzuri wake, Ujenzi wake ulitawaliwa na utulivu mkubwa sana, tunasoma
kwamba wakati Hekalu la ibada lililokuwa linajengwa na Sulemani, wajenzi
walihakikisha kila pande la tofali linalohusika katika ujenzi, linachongwa
mbali na eneo la ujenzi huko kware (Mgodini walikochonga mawe) walikuwa makini
kuchonga kila jiwe kwa ufanisi mkubwa na jiwe lilipokuwa tayari, lilipelekwa
eneo la ujenzi wa Hekalu na likajengwa bila kelele yoyote kusikika.
Mawe yaliyotumika hayakuwa madogo
na wala hayakuwa na maruturutu yaani yalikuwa yamenyooka, waliyaleta mawe hayo
yalikuwa makubwa, yalikuwa ya thamani sana ambayo yalikwishachongwa mgodini ona:-
1Wafalme 5:17-18 “Mfalme akaamuru, nao
wakaleta mawe makubwa, mawe ya thamani, ili wauweke msingi wa nyumba kwa mawe
yaliyochongwa. Na waashi wa Sulemani na waashi wa Hiramu na Wagebali
wakayachonga, wakaweka tayari miti na mawe ya kuijenga nyumba.”
Mawe hayo ya thamani kubwa
yalichongwa na kuandaliwa mgodini, mbali na eneo la ujenzi, kisha yakaletwa
mjini wakayaweka tayari, Wajenzi wa Suleimani na Hiramu na Wagebali hawa
walikuwa wataalamu maalumu wa shughuli ya ujenzi huo wa Hekalu.
Katika namna zote mbili yaani
kimwili na kiroho, uzuri na ufahari na taratibu za ujenzi wa Hekalu ulikuwa ni
mradi unaosimamiwa na Roho Mtakatifu maandiko yako wazi kuwa sisi ni kazi ya Roho
Mtakatifu.
Waefeso 2:19-22 “Basi tangu sasa ninyi si
wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa
nyumbani mwake Mungu.Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo
Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa
vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi
mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”
Kila mtu aliyeokolewa ni hekalu
la Roho Mtakatifu, kila mmoja ana thamani kubwa sana wote tumechongwa kwa jinsi
ya kipekee mgodini na wote tumeletwa ili tuwe nyumba ya Mungu, na kuwa
tumuabudu yeye na kuishi kwa amani bila malumbano wala mafarakano, kwa sababu
kama mawe ya thamani kila mmoja lina thamani yake na linafaa kukaa pale lilipokusudiwa
ona
1Petro 2:4-5“Mmwendee yeye, jiwe lililo
hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi
nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu,
mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa
kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la
pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.”
1Wakorintho 3:16-17 “Hamjui ya kuwa ninyi
mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu
akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la
Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.”
1Wakorintho 6: 19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu
aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana
mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”
Kwa hiyo tunakubaliana na
maandiko kuwa kila aliyeokolewa ni Hekalu la Roho Mtakatifu na kwa umoja wetu
ni jengo la Mungu na kila mmoja ni jiwe la thamani lililochongwa kwa ustadi,
kutoka katika mgodi au kware ya giza iliyoko duniani na kuletwa na
kuungamanishwa na Yesu Kristo ambaye ni jiwe kuu la pembeni, jiwe la msingi,
hatujajichagua wenyewe bali ni Mungu ndiye aliyetuchagua na kutuleta katika jengo lake, ili tumtukuze
yeye na tena tumuabudu yeye na kumtumikia bila ya hofu yoyote.
Kwa nini hekalu halihitaji kelele?
Mungu amekusudia kutufanya sisi
kuwa watu wake, na amekusudia kutupa utulivu, kelele asili yake ni huko
mgodini, wakati wote unapotembelea mgodi au kware utasikia milipuko mikubwa ya
kuvunjwa kwa mawe na mafundi wakitumia makrasha au mashine maalumu za kuvunja
mawe, huko mafundi watayachonga mawe lakini yanapoletwa katika Hekalu yanakuwa tayari
yanafaa kwa ujenzi, kelele zinawakilisha maisha ya duniani, kelele
zinawakilisha taabu na uusumbufu wa kuwa nje ya uwepo wa Mungu, Kelele
zinawakilisha hofu, kelele zinawakilisha kuwa uwepo wa Mungu umetoweka, kelele
zinawakilisha hakuna ujenzi, bali kuna kuvunja vunja na kubomoa, na kuharibu.
Mahali kwenye hofu ya kifo, hofu
ya utumwa hofu ya uvamizi, hofu ya uharibifu, hofu za maisha, hofu ya njaa,
hofu ya kesho itakuwaje ni mahali penye
kelele ni nje ya uwepo wa Mungu sio
hekaluni, unapokuja kwenye uwepo wa Mungu Roho Mtakatifu tunapata utulivu wa
ajabu na amani na tunatengwa mbali na kelele. Mungu amekusudia kumtenga kila
mmoja wetu na kelele na kumpa kila mmoja wetu utulivu na amani.
Hutaogopa majeshi hodari
yatatapopanga vita kwaajili yako Bwana anajua kuwa wewe ni hekalu lake kwa hiyo
majeshi ya upinzani yatanyamazishwa, wakati wote Mungu Kama Mchungaji wetu
hutuongoza katika maji ya utulivu
Zaburi 23:1-2, “Bwana ndiye Mchungaji
wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabishi hunilaza, kando
ya maji ya utulivu huniongoza”
Israel walipomlilia Musa kwa
sababu ya Majeshi ya farao yaliyokuwa yakiwafuatia kwa nyuma ili kuwarejesha
tena utumwani, Musa alitoa unabii ya kuwa Bwana atawapigania nao watanyamaza
kimyaa! Mungu anafahamu ya kuwa wanadamu wanahitaji utuilivu wanahitaji ukimya!
Wanahitaji amani, wanahitaji kuwa mbali na hofu, wanahitaji maisha ya ushindi,
wanahitaji kuthibitishiwa kuwa watakuwa mbali na kelele za kila aina:-
Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu,
Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana
hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi,
nanyi mtanyamaza kimya ”
Mungu atakustarehesha katika
maskani yake utaburudishwa hata kutokee matetemeko, mafuriko sunami na
mabadiliko yoyote yale sisi tunaokimbilia kwa Mungu kamwe hakuna atakayeogopa
hakuna atakayetetemeshwa ukiwa katika uwepo wa Bwana ushindi unapatikana mapema
asubuhi tu
Zaburi 46:1-5 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada
utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi,
Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka,
Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji
wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu. Mungu yu katikati yake
hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.”
Wewe unapokuwa Hekalu la Mungu
huna sababu ya kupiga kelele, wala huna sababu ya kutikisika Mungu anafahamu
wazi kuwa tunahitaji utulivu, tunahitaji kuwa kimya kisha yeye ataleta
ukombozi, Daudi kila alipokuwa anakabiliwa na changamoto za aina mbalimbali
alikumbuka anapaswa kutulia kimyaaaa na Mungu huyu yeye mwenyewe atazimaliza
kelele
Zaburi 62:1-2 “Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu
wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu,
sitatikisika sana.”
Wanadamu hawapaswi kusumbuka,
kama umechoshwa na kelele za dunia umechoshwa na wavunja mawe, kelele za kware,
kelele za migodini wewe mfanye Bwana kuwa ndio mchungaji wako, utapata kila
aina ya utulivu, utaandaliwa meza mbele za adui zako machoni pa watesi wako,
hutakufa, hutaogopa mauti, utafarijiwa, utapata upako, nafsi yako itahuishwa,
Baraka zitafurika nawe utakaa nyumbani mwa Bwana milele yaani kwenye utulivu!
Zaburi:23:1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya
majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi
yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam,
nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe
upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele
yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe
changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha
yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”
Unapoona kelele maana yake nini?
Tunaweza kujibu kwa ufupi kuna
uharibifu, mtu mmoja alisema kwa kiingereza hivi nanukuu “Destructive work is noisy, constructive work is silent” Kazi ya
uharibufu ni ya kelele, na kazi ya ujenzi ni ya kimyakimya” Madhabahu ya Mungu
ilikusudiwa pawe mahali pa ibada na hivyo katika torati Mungu aliagiza
madhabahu isijengwe kwa kutumia chombo cha chuma yaani isichongwe! Kule
kuchongwa kungeleata kelele ambazo Mungu hakutaka kuzisikia kupitia madhabahu
yake au hekalu lake, kutumia chombo cha chuma kuichonga madhabahu au hekalu
kungeweza kulitia unajisi hekalu!
Kumbukumbu 27:5-6“Na huko umjengee
madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu
yake. Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa;
ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake;”
Kutoka 20:25 “Nawe ukinifanyia madhabahu ya
mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo
chako katika kuichonga umeitia unajisi.”
Kwa hiyo unapoona kelele Katika ujenzi wa hekalu maana yake ni kuwa;-
# Watu wameacha kufanya kazi waliyoitiwa wanafanya biashara nyingine
Marko 11:15-17 “Wakafika Yerusalemu, naye akaingia
ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya
hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala
hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. Akafundisha, akasema, Je!
Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi
mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.”
# Watu wakiwa mwilini, yaani udunia ukiingia, hekalu linakuwa na kelele
1Wakoritho 3:1-7 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na
watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na
watoto wachanga katika Kristo.Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa
kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi
ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si
watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana
hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je!
Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao
mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji;
bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali
Mungu akuzaye.”
#Watu wameingiwa na tamaa ona Yakobo 4:1-5 “Vita
vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa
zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na
kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa
kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili
mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni
kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui
wa Mungu. Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani
yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?”
# Kila mtu anapokuwa na nia yake 1Petro 3:8-13 “Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye
kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya,
au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili
mrithi baraka. Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie
ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende
mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye
haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya
watenda mabaya. Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?”
# Watu wema wanaposhikamana na waovu 2Wakoritho 6:14-18 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo
sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika
gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari?
Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano
gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye
hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao
nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni
kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami
nitawakaribisha. Nitakuwa
Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”
# Mbinguni hakutaingia chochote kilicho kinyonge
Ujenzi huu wa ajabu ambapo mawe
yalikuwa yakichongwa mbali, huko kware au mgodini, yaliletwa katika kiwanja cha
hekalu yakiwa yamekamilika unatukumbusha wazi kuwa shemu ya kuchongwa watu ni
hapa duniani, Roho Mtakatifu hufanya maandalizi ya kutuandaa na kutuchonga
tukiwa hapa Duniani, anatukarabati ndani na nje ili tufae kuwa chombo cha sifa
na ibada lakini zaidi kwamba baadaye
tuweze kufika Mbinguni ambako huko ni eneo la utulivu na hakuna kuchongwa tena
tutaingia tukiwa tumekamilishwa baada ya kupitia mchakato wa utakatifu duniani
kule mbinguni hakuna chochote kilicho kinyonge kitakachoingia,
Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili,
ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya
Kristo Yesu;”
kila mmoja anapaswa kujiweka
wakfu kwa maneno kama yale ambayo Suleimani aliyasema siku alipokuwa akiliweka
wakfu Hekalu, alisema
1Wafalme 8:13 Hakika nimekujengea nyumba ya
kukaa, iwe mahali pa makao yako milele. Meno ya kiingereza ya mstari huu ni
matamu zaidi kwani yanasema hivi “I have indeed built you exalted house,
a place for you to dwell in forever” Mungu anataka tuwe makazi yake milele.
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni