Alhamisi, 18 Novemba 2021

Alipita katikati yao Akaenda zake!


Luka 4:16-30Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe. Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu.Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye ALIPITA KATIKATI yao, akaenda zake.”



Utangulizi:

Moja ya maswala ya kushangaza sana ambayo huwa tunayasoma katika maandiko na kisha yakatuacha aidha hatujaelewa, au yakatushangaza sana ni pamoja na muujiza huu, wa Yesu kupita kati kati ya  waliokuwa wamejaa ghadhabu na wamepania kummaliza, lakini wakashangaa kuwa ametoweka katika mazingira ya kutatanisha!

Hii sio mara ya kwanza  tunasoma katika maandiko ya kwamba Yesu amewahi kuwepo au kupita kati kati ya watu  tena watu waliojaa ghadhabu na hasira ili wamdhibiti na kumwangamiza  na bado yeye akapita kati kati yao  bila wao kutambua  na kwenda zake waandishi wengi wa injili wanapata taabu namna ya kuelezea tukio hili na hivyo kuwafanya wasomaji wao kushindwa kuelewa au kupata kile kilichofanyika ona

 Yohana 8:48-59Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Je! Sisi hatusemi vema ya kwamba wewe u Msamaria, nawe una pepo?  Yesu akajibu, Mimi sina pepo; lakini mimi namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima yangu. Wala mimi siutafuti utukufu wangu; yuko mwenye kutafuta na kuhukumu. Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele. Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng'amua ya kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele. Wewe u mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani? Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu. Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nalishika. Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu? Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko. Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu AKAJIFICHA, akatoka hekaluni.”

Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia ya kiingereza ya King James katika maandiko au maneno AKAPITA KATI KATI YAO AKAENDA ZAKE yanasomeka katika Luka 4:30But HE PASSING THROUGH THE MIDST OF THEM and went his way” na Katika hali kama hiyo tena Yohana 8:59 andiko lile LAKINI YESU AKAJIFICHA, linasomeka kwa kiingereza “then took they up stones to cast him, BUT JESUS HID HIMSELF and went out of the temple, GOING THROUGH OF THEM and so passed byYohana 10:39 “Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao.” Kumkamata Yesu halikuwa jambo rahisi kama watu wengi wanavyoweza kudhani, Hapa huu ulikuwa ni muujiza wa wazi, aidha kwa mujibu wa wanatheolojia wengi, walipigwa upofu, au walipigwa gazi, au Yesu alitoweka kwa jinsi ya muujiza biblia ya kiyunani inatumia maneno haya “DIELTHON DIA MESOU EPOREUETO”  kwa kiingereza  “But Passing through their midst he went his way”  kwa hiyo neno EPOREUETO  ambalo kiingereza klinasomeka “WENT HIS WAY”  pia linasomeka kama  “TRAVERSE” ambalo tafasiri yake inaweza kusomeka kama KUTOKOMEA, kama vile kitu kinapopotelea mwisho wa mto, au ndege inapopaa na ikapotelea angani, au meli inavyosafiri na kutokomea nje ya upeo wa macho ya kibinadamu kwa hiyo ukiangalia kwa undani sana swala hili utaweza kuona “HE BECAME INVISIBLE” yaani alitoweka na kuendelea na shughuli zake sehemu nyingine, kwa kukosa neno zuri la kuelezea ndio Yiohana anatumia neno kujificha au kutoweka mikononi mwao na Luka anaelezea vema kupita katikati yao na kwenda zake!

Katika maandiko hayo ya msingi utaweza kujiuliza maswali mengi kwamba ilikuwaje kuwaje Yesu, akapita kati ya watu waliokuwa wamekusudia kumdhuru, na kumuumiza, au inawezekanaje mtu ambaye watu wote wanamuangalia anajificha kama biblia ya Kiswahili ilivyotumia neno hilo kwenye injili ya Yohana na watu walikuwa wamekusudia kumkamata na kumtupa nje ya kilima wakiwa wamejaa ghadhabu?, watu wenye nguvu na ambao tayari walikuwa wamekwisha muweka mikononi mwao, ukweli ni kuwa kulikuwa na nguvu ya ziada na ya kiungu ya kupita kawaida ambayo wakati mwingine iliwafanya maadui wasimuone, yaani walipigwa upofu na kufanywa wasimtambue na hili lilikuwa ni jambo la kawaida kuweza kufanyika  mfano, angalia watu hawa:-

Luka 24:13-16 “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue.”

Mungu katika mpango wake anazo njia zake za kuwaficha wapendwa wake ili wasidhurike na hatari ya aina yoyote ile, Ndio maana tunapokuwa na Mungu hatupaswi kuogopa jambo lolote lile, hatupaswi kuogopa wingi wa majeshi ya maadui,  wala mipango mikakati ya adui zetu kutuangamiza na kututupilia mbali, tunapaswa, tu kufahamu kuwa kuna wakati Mungu yu aweza kuwapiga upofu maadui zetu na wasituone na kuwa tunaweza kupita katikati yao na kuendelea na shughuli zetu bila madhara, Mungu ameahidi kutuokoa na mitego yote ya adui ona Zaburi 124:6-7 “Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokokaMungu ameahidi kutuokoa kama nudge anavyonusurika katika mitego ya adui, Jambo alilolifanya Yesu Kristo ni jambo la kawaida sana lililoweza kufanywa na manabii hata katika agano la kale, Wakati wa nabii Elisha yeye alitafutwa na jeshi kubwa sana la nchi ya shamu, na walikwenda maalumu kwaajili ya kumtafuta Elisha, na Elisha alizungumza nao vizuri tu  na kuwalisha kisha akwaacha waende zao ona

2Wafalme 6:8-23 “Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala. Akasema, Enendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko Dothani. Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira mji ule pande zote. Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote. Na walipomtelemkia Elisha akamwomba Bwana, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha. Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria. Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, Bwana wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. Bwana akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria. Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige? Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao. Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli” 

Haijalishi kuwa leo mpendwa unapitia katika hali ya namna gani, inawezekana umebanwa kila upande, umezingirwa, na hali tata ambazo hujui utapenya vipi, kila kilicho kibaya kinakuandama na kukutafuta, adui wamejipanga kwamba wanakuharibia lakini leo nataka nikutie Moyo, ya kuwa upo muujiza wa kupita kati kati yao na kuenda zako, kwa amani, Muujiza huu unatuthibitishia ya kuwa adui hatatuona; Lakini sisi tutamuona na kuamua wapi pa kumpeleka na au wapi pa kupita, adui atadhani kuwa hatutaiona njia lakini Muuijza huu unatufundisha ya kuwa iko njia hata katikati ya kibano, ambacho kwa akili zako unaweza kudhani ya kuwa hutapenya lakini kwa neema ya Mungu utapenya, wiki hii kidato cha nne watakuwa na mitihani ya kitaifa na wengi wanaweza kuwa wanaogopa kwamba itakuwaje au wanafikiri itakuwaje hata wazazi wanaogopa na walimu vilevile tunawaza itakuwaje hofu inatufunika kana kwamba ule mtihani tunakwenda kufanya sisi, tunawaza tunavukaje? na pengine ibilisi amekusudia kukukwamisha na kukutupilia mbali ili kwamba historia yako isiwepo tena lakini nataka kukuthibitishia ya kuwa bwana anakusudia kukupitisha katikati ya mtihani huu wa kitaifa na uende zako Hekaluni ukamtukuze Mungu, hatupaswi kuogopa kwa sababu Mungu ana njia nyingi” atakusaidia. Na nafsi yako itaokoka katika mikono ya adui zako kwa namna ya kushangaza! 

Isaya 43:1-2 “Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.”  
   

Na Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!



Hakuna maoni: