Mithali 14:34
“Haki huinua taifa; Bali
dhambi ni aibu ya watu wo wote.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa maandiko yanatupa siri
ya mafanikio makubwa sana katika maisha yetu ya kila siku na maisha ya kila mtu
na maisha ya taifa lolote lile kwamba; Ili tuweze kuwa na ustawi tunapaswa kuwa
watu wa haki, Mungu hawezi kumvumilia mtu au taifa lolote ikiwa watu wa taifa
hilo wataacha na uadilifu na kumkataa Mungu, siri ya nguvu na mafanikio ya mtu
watu jamii na taifa lolote iko katika kutenda uadilifu na kuyaishi mapenzi ya
Mungu na wala sio nguvu za kijeshi na uchumi, siri ya mafanikio ya kweli iko
kwenye uadilifu na kutenda haki, Taifa lolote likiandaa mipango na mikakati ya
kiadilifu na ya kumcha Mungu na kumuheshimu na kukaa katika uadilifu kila kitu
kitafanikiwa kwa mujibu wa maandiko Mithali 14:34 “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.” Tutajifunza somo hili Haki huinua taifa kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
1. Maana ya Taifa
2. Jinsi haki inavyoinua taifa na Dhambi inavyoleta aibu
3. Haki huinua taifa
Maana ya Taifa
Ni muhimu kufahamu kuwa katika maandiko lugha
inayotumika kumaanisha taifa inatumika katika maana pana sana unapoangalia maana
ya Taifa kwa kiingereza yaani Nation maana yake katika Dictionary inasomeka
hivi National means People who possess a common kinship, a social or
political group and simply a people, kwa kiyunani ni Ethnos au Ethinic, ni jamii
au watu wanaotokana na mtu, au kabila au dini au lugha na kadhalika, Kwa
mfano watu wanaweza kuzaliwa na baba mmoja na mama mmoja au hata wakawa mapacha
lakini katika jicho la kiungu hao wanaweza kuwa mataifa mawili tofauti na
kabila mbili tofauti unaona!
Mwanzo 25:21-23 “Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana
alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto
wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda
kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yamo tumboni mwako, Na kabila
mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari
kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo.”
Unaona na pia unaweza kuiona lugha ya aina hii
ikitumiwa na Yesu katika Mathayo 24:6-7 “Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita;
angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa
maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme;
kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali.”
Kwa msingi huo sasa Taifa linaweza kuwa ni
jamii ya watu wanaotokana na mtu mmoja mmoja, taifa ni watu wa karibu sana
wakati ufalme na ufalme inaweza kuwa ni mipaka ya kiserikali, kwa hiyo Mungu yu
aweza kumuona au kumuita mtu mmoja na mtu huyo akamfanya kuwa taifa, yaani kama
wewe ni mtenda haki na unampendeza Mungu wewe ni asili ya taifa Mungu yu aweza
kukufanya wewe kuwa taifa kubwa ona
Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi
yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi
nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na
kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye
akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”
Kwa msingi huo tunapozungumzia taifa
tunamzungumzia mtu mmoja mmoja, na jamii au kabila au kundi la watu wa aina
filani walio karibu sana hilo ndio taifa, na ufalme ni jamii ya watu
wanaopakana kiserikali, kwa hiyo kila mmoja anapaswa kuwa mtenda haki na kuishi
maisha ya kumcha Mungu kwa sababu Mungu hashindwi kukufanya wewe kuwa taifa kwa
sababu taifa linaanzia na mtu mmoja kama Mungu akipendezwa nawe anaweza
kukufanya kuwa taifa na kama Mungu akichukizwa nawe anaweza kukufuta ona
Kutoka 32:7-14 “BWANA akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako
uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha
ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na
kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa
katika nchi ya Misri. Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na
tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake
juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana
BWANA, Mungu wake, na kusema, BWANA, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu
wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu?
Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate
kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira
yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na
Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na
kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii
yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. Na BWANA
akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake” unaweza
kuona kwa msingi huo sasa swala la kutenda haki au kwa lugha nyingine nyepesi
kutembea katika mapenzi ya Mungu halianzi na mtu Fulani tu linaanza na wewe na
mimi
Jinsi haki inavyoinua taifa na Dhambi inavyoleta aibu
Maandiko sasa yanatuonyesha kupitia wana wa
Israel na maisha yao kwamba pale watu walipotenda haki na walipotembea katika
njia za Mungu, Mungu aliwafanya kuwa imara na pale watu walipoziacha njia za
Mungu, na kuyaacha mapenzi yake Mungu
aliwaacha waanguke katika mikono ya adui zao na kunyanyaswa vibaya ona kwa mfano
Waamuzi 2:11-23 “Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za
macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali.Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao,
aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya
miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao;
wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika. Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na
Maashtorethi. Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika
mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao
pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda
mkono wa Bwana ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama Bwana alivyosema, na kama
Bwana alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. Kisha Bwana akawainua waamuzi,
waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara. Lakini hawakuwasikiliza
hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine,
wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea
baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo. Na wakati Bwana
alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na
mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili
ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. Lakini ikawa,
wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao,
kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha
matendo yao, wala njia zao za ukaidi. Basi hasira ya Bwana ikawaka juu ya
Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu
nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; mimi nami tokea sasa
sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa; ili kwa njia
ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya Bwana kwenda
katika njia hiyo, au sivyo. Basi Bwana akawaacha mataifa yale, wala
hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.”
Unaweza kuona kwamba pale watu wa Mungu walipoziacha
njia za Mungu na kuishi kwa dhuluma na
wakajifanyia kila wanachokiona kuwa chema katika macho yao Mungu aliwadhibu vikali sana na kuwaacha
katika mikono ya adui zao ili washughulikiwe na wakati mwingine aliruhusu
wachukuliwe mateka na kwenda utumwani
na sio hivyo tu akliwaacha wadhalilike na kufedheheka nah ii ndio
aibu kubwa iliyokuwa inawapata pale wanapoacha njia za Mungu ambayo ndio haki
ya Mungu.
2Wafalme 17:6-12 “Katika mwaka wa kenda wa
Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka
Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika
miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda
dhambi juu ya Bwana, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke
chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea
sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria
za wafalme wa Israeli walizozifanya. Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri
mambo yasiyokuwa mema juu ya Bwana, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu
katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma.
Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila
mti wenye majani mabichi; wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu,
kama mataifa walivyofanya, ambao Bwana aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo
mabaya, ili wamkasirishe Bwana; wakatumikia sanamu, ambazo Bwana aliwakataza,
akasema, Msitende jambo hili.”
Pale Israel walipotubu na kucha dhambi zao na
kutembea katika mapenzi ya Mungu Mungu aliwasaidia aliwapa Mwokozi, alileta
ukombozi na kuwapa amani na kuondoa masumbufu yote
Waamuzi 3:9-11 “Kisha wana wa Israeli walipomlingana Bwana, Bwana
akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa
Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye akawa
mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo
Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake
ukamshinda Kushan-rishathaimu. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini.
Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.” Unaweza kuona hii ndio kanuni ya Mungu, Mungu hawezi
kukuinua na kukutumia katika hali ya uovu, hatunabudi kutubu, kujinyenyekesha
mbele za Mungu na kumlingana Mungu yaani kutembea katika njia zake tukifanya
hivyo hatutaingia katika aibu na fedhea ya aina yoyote ile na Mungu atakuwa
pamoja nasi na tutakuwa na uhakika wa ulinzi wa kudumu wala Bwana hatatuuza
tuumizwe na adui zetu
Haki huinua taifa
Mithali 14:15-34 “Mjinga huamini kila neno;
Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo. Mwenye hekima huogopa, akajitenga
na uovu; Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai. Yeye aonaye hasira upesi
atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa. Wajinga hurithi
upumbavu; Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa. Wabaya huinama mbele ya
wema, Na wasio haki malangoni mwao wenye haki. Maskini huchukiwa hata na jirani
yake; Bali tajiri ana rafiki wengi. Amdharauye mwenzake afanya dhambi; Bali
amhurumiaye maskini ana heri. Je! Hawakosi wawazao mabaya? Bali fadhili na
kweli zina wao wawazao mema. Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo
huleta hasara tu. Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni
upumbavu tu. Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu; Bali atoaye uongo
hudanganya. Kumcha Bwana ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio.
Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. Utukufu wa
mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.
Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza
upumbavu. Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; Bali husuda ni ubovu wa mifupa.
Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji
humheshimu. Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake; Bali mwenye
haki ana matumaini katika kufa kwake. Hekima hukaa katika moyo wake mwenye
ufahamu; Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika. Haki huinua taifa; Bali
dhambi ni aibu ya watu wo wote.”
Suleimani katika kitabu cha Mithali anaonyesha
wazi namna mtu mwenye haki anavyoweza kufanikiwa na namna watu waovu
wanavyoweza kujikuta katika mashaka kinachosisitizwa katika maandiko hapa ni
kwamba wale wanaomkataa Mungu na kuacha kutenda haki na kuendelea na uovu
wanafanya ujinga ambao utawaharibia maisha na wale wanaomkubali Mungu na njia
zake wanajipatia hekima na maarifa na
kujitengenezea ulinzi wa uhakika , kwa msingi huo neno la Mungu
linapozungumza kuhusu taifa linatuzungumzia wewe na mimi na baadaye jamii yetu
na jamii ya dunia kwa ujumla lakini kanuni hii inaanza kufanya kazi kwa mtu
mmoja mmoja
Mithali 3:5 -8 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako
wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye,
Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana,
ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.”
Ukiyajua hayo Heri wewe ukiyatenda!
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima