Luka 3:2-14 “wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu
lilimfikia Yohana, mwana wa Zakaria, jangwani. Akafika nchi yote iliyo karibu
na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, kama
ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya; Sauti ya mtu aliaye
nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Kila bonde
litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa
pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa; Na wote wenye mwili watauona wokovu
wa Mungu. Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi
wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi,
toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye
baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu
aweza kumwinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye
mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa
motoni. Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na
ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao
wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko
mlivyoamriwa. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini?
Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara
wenu.”
Utangulizi:
Moja ya manabii wa ajabu sana
ambao unaweza kujifunza habari zao na ukashangaa ni pamoja na na Nabii Yohana
mbatizaji, Huduma yake ya kinabii ilikuwa imejawa na kuwaandaa watu watubu,
kwaajili ya kumpokea Masihi, Ni wazi kuwa Masihi kwa namna anavyoelezewa na
maandiko ni kiongozi wa ngazi ya juu mno na ambaye sio wa kawaida na hivyo
Mungu aliona kuwa hawezi kupokelewa kienyeji bila mioyo ya watu kuandaliwa ili
iweze kustahimili ujio wa Masihi, kwa hiyo Mungu katika mpango wake alikusudia
kumtuma Yohana Mbatizaji nabii, Hili linadhihirishwa wazi na nabii Isaya miaka
700 kabla ya ujio wa Yesu, alitabiri juu ya ujio wa Yohana mbatizaji na huduma
yake ambayo ilikuwa na umuhimu mkubwa sana katika kuandaa mazingira ya kumpokea
Yesu Duniani ona:-
Isaya 40:3-5 “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye,
Itengenezeni nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.
Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka
patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa; Na utukufu wa Bwana
utafunuliwa, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana
kimenena haya.”
Unaweza kuona umuhimu wa nabii
huyu ulikuwa mkubwa mno, kwani alitumwa kuwaandaa watu watubu kabla ya huduma
ya masihi kwa kuwa masihi mwenyewe ndio wokovu wa Bwana utakaofunuliwa kwa watu
kwa jinsi ya Mwili, Masihi mwenyewe ni utukufu wa Mungu, na kwa sababu watu
wangemuona kwa macho yao ya mwili ilikuwa ni muhimu kuandaa mioyo yao ili macho
yao yauone wokovu wa Bwana na utukufu utakaofunuliwa kwa watu wote ona:-
Luka 2:25-32 “Na tazama, pale Yerusalemu
palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu,
akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa
ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa
Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto
Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,yeye mwenyewe
alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu
mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu
wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote;Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,
Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.”
Kuja kwa Masihi kuliambatana na
mahubiri mazito yaliyokuwa yakiwataka watu wawe na toba ya kweli iliyoambatana
na kuzaa matunda na kubatizwa ili kudhihirisha kuwa kweli watu wamebadilika na
wako tayari kumpokea Masihi, ilikuwa ni lazima jamii iwe na usafi wa moyo na
kuwa mioyo yao ilikuwa lazima iwe tayari kwaajili ya Mungu na kwaajili ya
wanadamu, Ili Yesu akute na atembelee jamii ilikuwa ni lazima njia isafishwe,
palipo na kilima pasawazishwe na kila mahali ambako hakuko sawa sawa ilikuwa ni
lazima pawe sawa, kila kikwazo ilikuwa ni lazima kiondolewe ili watu waweze
kuishuhudia neema ya Mungu maishani mwao, ilikuwa ni lazima watu wawe mbali na
uchungu, waondoe chuki dhidi ya Mungu, na maudhi na kero zote walizokuwa
wakiwafanyia wanadamu wenzao, Yohana aliwaonya juu ya hukumu ya Mungu
itakayokuja endapo kizazi kile hakitatubu, Hata hivyo ujumbe wa Yohana mbatizaji
ulikuwa na mtindo wenye kufurahisha sana kwa sababu watu walimwendea wakitubu
kwa kupitia kazi zao (professional), Mtindo wake wa kimaonyo na kimahubiri
unaonyesha wazi kuwa ni watu ndio walimuendea wenyewe wakitubu, na kuuliza
maswali, lakini sio hivyo watu walienda kimakundi kutokana na uhalisia wa kazi
zao na kila mmoja akitaka kujua kuwa afanyaje ili asimkwaze Mungu na jamii na
ndio maana swali kubwa la ujumbe huu ni *Na
sisi je tufanye nini?*
1.
Kwa
Jamii (Makutano) – Yohana mbatizaji alishangaaa kuona jamii kubwa ya watu wakikimbia
kwenda kutubu na hivyo aliiambia jamii waziwazi, Kwamba waondoe uchungu mioyoni
mwao Luka 3:7 “Basi,
aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni
nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?” Kitendo cha
kuwaita makutano kizazi cha nyoka kilimaanisha kuwa watu wengi walikuwa upande
wa shetani ambaye ndiye nyoka, lakini sio hivyo tu jamii ilikuwa na uchungu na
malalamiko ya kila aina, na sio hivyo tu ilikuwa ni jamii iliyojaa hila na
dhuluma na vilio vya kila aina, manung’uniko na hali ya kujiona kuwa
hawakufanyiwa sawa, watu ambao wakati wote hawana jema Yohana aliwaonya watu wa
namna hii Kuwa kamwe hawatafurahia uwepo wa Masihi, Na ujio wa Masihi hautakuwa
na maslahi wa jamii yenye uchungu, jamii yoyote yenye uchungu hata uwafanyie
nini hawatakuja kuridhika hata siku moja, hawatakuja kutoa shukurani, wakati
wote watalalamika, uwepo wa Mungu na Baraka za Mungu na Hazifanyi kazi kwa
jamii ambayo imejaa uchungu, Na ndio
maana Yoaha nanakiita kizazi cha nyoka!Uchungu wakati wote katika maisha
unapunguza sana neema ya Mungu, Maandiko yanatuonya kutokuwa na uchungu!
Waebrania 12:15 “mkiangalia
sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na
kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”
Yohana alikuwa
anaiona hukumu ya Mungu na kuwa mafanikio hayawezi kuja kwa jamii ambayo wakati
wote inalalamika tu au kwa jamii ambayo haitendeani mema au kwa jamii iliyojaa
dhuluma, wizi, ubabaishaji, na hila za kila aina au jamii ambayo hairushusu
hofu ya Mungu kutawala! Kama jamii
ina uchungu wa aina yoyote hicho ni kizazi cha nyoka!
Waefeso 4:31-32 “Uchungu
wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila
namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma,
mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.”
Kizazi cha nyoka
ni jamii iliyojawa na uchungu na uchungu ni sumu, ghadabu, hasira ni lazima
iondoke katika jamii, uovu na ubaya wa kila namna ni lazima uondoke katika
jamii ambayo inamtaka Masihi awe kiongozi wao, apite katikati yao aweze kuwa
Baraka na kuleta uponyaji, ni lazima iwe jamii inayojaliana na kufadhiliana
jamii ambayo imeacha umimi ubinafsi na uchoyo, Maandiko yanaitaka jamii kuondoa
uchungu kwa kujilinda na choyo na kufadhiliana ona
Luka 12:15 “Akawaambia,
Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu
vyake alivyo navyo.”
Si vema Yesu
akaja katika jamii na kuikuta ina sumu, ina uchungu, na hasira, ina ubaya ina
uovu, ina hali ya kutokusameheana au
isiyosamehe, jamii inayosingiziana, Yesu anaitaka jamii iwe na fadhili
na ndio maana Yohana mbatizaji aliiiambia jamii kama una cha ziada gawia wasio
nacho !
Luka 3:10-11 “Makutano
wakamwuliza, Tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na
ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo”
Jamii isiyo na
umimi itajifunza kutoa na kufadhiliana na itaachana na ubinafsi na kuangaliana wao
kwa wao, leo hii jamii haiko hivyo kila mtu ana uchungu na kila mtu yuko kwenye
kujikusanyia, kila mtu anangalia mambo yake na tumekuwa na jamii isiyo na
shukurani na bingwa wa kulalamika na kujenga hoja za malalamishi ndio
anaonekana shujaa katika jamii! Kama jamii ikiwa katika hali hiyo kweli hicho
ni kizazi cha nyoka na hakina budi kubadilika na kutoka katika hali ya kuwa
wana wa ibilisi na kuwa wana wa Mungu!
2.
Mafarisayo
na Masadukayo (Madhehebu mbalimbali) – Wakati wa Yohana mbatizaji na Yesu
pia kulikuwa na watu wa Madhehebu ya aina mbalimbali, madhehebu makubwa ya watu
waliokuwepo nyakati hizo walikuwa ni pamoja na Mafarisayo na masadukayo, hawa
walikuwa madhehbu maarufu sana nao waliposikia huduma ya Yohana mbatizaji
walimwendea na wakatubu kwa wingi lakini Yohana hakuwaacha bila maonyo watu wa
Madhehebu aliwaonya kuwa ni lazima waache kiburi cha kidini na kidhehebu,
lakini lazima waache kujihesabia haki, Mafarisayo na Masadukayo walijifikiri
kuwa wao ni madhehebu bora kwa sababu Ibrahimu ni baba yao Mbatizaji aliwaonya kwa
manenio haya ona:-
Mathayo 3:7-10 “Hata
alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake,
aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira
itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu
kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza
katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye
mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”
Mafarisayo na
masadukayo yalikuwa ni madhehebu makubwa nyakati za Yohana na Masihi, Mafarisayo
katika theolojia yao walikuwa wakiamini katika ufufuo wa wafu, waliamini katika
malaika na maono na walikubaliana na vitabu vya Musa na manabii, lakini
Masadukayo wao hawakuamini katika ufufuo, wala hawakuamini katika malaika na
maono na waliamini vitabu vitano vya Musa tu na hawakujali vitabu vya manabii,
kila mmoja alikuwa akijiona bora kutokana na madhehebu yake aliyokuwa nayo,Lakini
zaidi sana walidhani ya kuwa Mungu anawahesabia haki kwa vile wao ni wana wa
Ibrahimu, hata leo katika jamii zetu watu wanadhani kuwa kuwa na madhehebu ndio
kuuchinja, wananadi sana madhehebu yao kuliko kumnadi Yesu, Yohana Mbatizaji
aliwakazia akawaambia sikiliza Mungu anataka matunda yatokanayo na toba, Mungu
anataka watu waliotubu na kugeuka na kuacha dhambi, ishu sio kuwa mtoto wa
Ibrahimu kwa sababu Mungu anaweza kumuinulia Ibrahimu watoto hata kutoka katika
mawe, Hivyo Dhehebu lako sio ishu wala sio dili, dili ni Yesu, Dili ni Masihi,
dili ni toba ya kweli na mabadiliko, Mungu anataka matunda mazuri, hakuna
matunda mazuri mti huo utakatwa na kutupwa motoni:-
Wagalatia 5:19-24 “Basi
matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya
sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda,
ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama
nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo
hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani,
uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo
hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na
mawazo yake mabaya na tamaa zake.”
Wakati Yohana
akikazia kuwa shoka limekwisha kuwekwa tayari na ni moto tu unahusu watu wasio
na toba Paulo anaongezea kuwa watu wenye matunda yasiyofaa hawatauona ufalme wa
Mungu, Kama una dini nzuri watu wanataka kuona matendo yako na sio vinginevyo,
kama una dhehebu zuri watu wanataka kuona mabadiliko dini au dhehebu lako
halitusaidiii katika jamii Mungu anataka matunda kinyume cha hapo ni hukumu tu.
Wayahudi na waislamu na wakristo wanatokana na Imani ya Ibrahimu na wote
wanakiri kuwa Ibrahimu nabii ni baba yao wa imani, Ni muhimu kufahamu kuwa dini
na madhehebu hayatatusaidia kama hakuna matunda ya kweli na toba ya kweli
Yakobo 1:26-27 “Mtu
akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali
akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na
taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika
dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.”
Kwa msingi huo
Yohana aliionya jamii kuacha kujivunia dini zao na Madhehbu yao, wako watu
ambao wako tayari kufa kwaajili ya dini zao wanazing’ang’ania kama chapati na
hawana mpango na Yesu, na sio hivyo tu wanakiri ya kuwa wana dini lakini
matunda hayaonekani, kama watu wana dini ya kweli chuki inatoka wapi, majungu
yanatoka wapi, kiburi na dharau kinatoka wapi, fitina na majungu na
kujipendekeza kunatokea wapi? Mbona watu
hawajilindi na mawaa, mbona hawajilindi na dunia, mtu anakiri kuwa na dhehebu
safi lakini amejaaa viwango vya kidunia. Ni lazima watu watubu na kuzaa
matunda.Vinginevyo hukumu itamhusu kila mmoja bila kujali ana dhehebu au dini
nzuri kiasi gani!
3. Watoza ushuru - Luka 3:12-13 “Watoza ushuru nao wakaja
kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu
zaidi kuliko mlivyoamriwa.”
Kundi hili nalo
wakati wa Yohana mbatizaji lilijitokeza kutubu, hawa walikuwa ni watoza ushuru,
kundi hili liliagizwa kuacha dhuluma na kutoza zaidi ya kiwango kilichowekwa,
kundi hili lilikuwa ni kundi la watu wenye tamaa ya fedha na waliojilimbikizia
mali ka njia ya dhuluma, Dhambi yao kubwa ilikuwa ni kuzidisha na kutoza zaidi
ya jinsi ilivyoamuriwa ni watu waliokuwa
wamejaa dhuluma sana, waliwadhulumu wananchi lakini pia hawakufikisha mapato
serikalini, jamii ya watoza ushuru walihesabika kuwa hawana uzalendo na wala
wakati mwingine sio waaminifu na hawafikishi kile kiwango cha fedha
wanachokusanya au wakati mwingine walitoza juu ya kiwango kwa faida zao wenyewe!
Hwa pia waliongezea manung’uniko katika jamii na kwa wayahudi watu hawa
waliwekwa katika kundi la watu wenye dhambi sana, Kundi hili pia lilitakiwa
kuacha uovu wake na kujiandaa kumpokea Yesu
Luka
19:2-10 “Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake
Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa
akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa
watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate
kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama
juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani
mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu
walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.
Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa
maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.Yesu
akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa
Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
Watoza ushuru
walikuwa wamejitajirisha kupitia mali za dhuluma, na kuzidisha kiwango cha
fedha kilichowekwa, hawa Yohana mbatizaji aliwajibu walipo uliza na sisi je
tufanye nini aliwaambia wasitoze zaidi ya kiwango kilichowekwa, sehemu nyingi
sana leo hii kumekuweko na watu ambao wanatoza zaidi ya kiwango kilichowekwa,
unadhani kwanini serikali inapiga marufuku swala la twisheni kwa walimu? Kwa
sababu tayari ada zipo zimewekwa, lakini kwanini walimu wanafanya twisheni, kwa
nini wanachukua fedha ili wakufundishe pembeni pembeni, ada unayolipa
haiwatoshi? Kuna namna nyingi sana watu wanatoza zaidi ya kiwango kilichowekwa,
wako pia wafanya biashara ambao wanatoza
zaidi ya kiwango kinachokusudiwa na ukitaka kuwaweza we sema tu unadai risiti,
watakuambia kuna bei ya kuandika kwenye risiti na bei ya bila risiti, Kristo
hawezi kukubaliana na jamii ya watu yenye dhuluma ili aweze kuweka makazi
anahitaji watu watubu kama alivyofanya Zakayo, aliamua kutubu na kurudhisha kwa
jamii kile alichokusanya, wako watu wanakusanya na hawarudishi kwa jamii,
lakini vilevile hawafikishi serikalini kama kila aina ya ushuru ungekuwa
unafika inakotakiwa serikali ingekuwa imepiga hatua kubwa sana ya maendeleo,
watu wangeweza kunufaika na mataifa yao na nchi zao na huduma za kijamii bila
kuhitaji kukopa katika mataifa au mabenki, hakungekuwa na sababu ya kuinamia
mataifa mengine, kuhitaji msaada, watoza ushuru hali kadhalika walifanya kazi
za kubambikizia watu kodi nzito, kutishia kufunga biashara ugomvi na wafanya
biashara dhuluma na mambo mengine ya kusikitisha lakini hata hivyo wakitubu
Yesu atawapokea.
4.
Askari
– Luka 3:14 “Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi
nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena
mtoshewe na mshahara wenu”
Maandiko
hayaonyeshi kuwa kazi ya uaskari kuwa ni kazi mbaya au isiyofaa kwani ni wazi
Askari waliomjia Yohana mbatizaji hapa ilikuwa ndio mahali pa kuwaambia waache
kabisa kazi hiyo kama ingekuwa haifai, katika ulimwengu huu ulioharibika askari
ni wa Muhimu na wanahitajika kwa sababu kuna watu ni waizi, na bila kuweko
askari wakati mwingine ni ngumu kuitunza amani inayokusudiwa, Lazima askari
wawepo ili kukomesha umwagikaji mkubwa wa damu na kuzuia uhalifu, kulinda taifa
raia na mali zao na kuhakikisha usalama unakuwepo kila eneo, hivyo nabii
hakusema waache kazi hii lakini aliwaonya wasidhulumu mtu na wala wasishitaki
mtu kwa uongo kubambikizia watu kesi na kuwa watosheke na mishahara yao,Jaribu
hili ndilo lililokuwa likiwakabili askari na hasa jeshi la polisi ambao
walikuwa wakilinda usalama wa raia na mali zao katika mswala haya matatu kuna
mambo ya ksingi ya kujifunza kwetu kwa kila kitu walichojibiwa askari kupitia
Yohana mbatizaji.Sisi ni aksari tufanye nini:-
1. Msimdhulumu mtu.
Dhuluma kwa kiingereza maana yake ni “unrighteousness” au KAKIA kwa kiyunani yaani ni hali ya
kutokutenda haki, kutenda kwa ubaya, kutenda kwa kuumiza, kutenda bila kujali,
watu wengi sana hawatendi haki hususani askari na hata watu wasio askari,
lakini hata hivyo neno la Mungu linamtaka kila mtu atende haki kutokutenda haki kunaondoa neema ya
Mungu
Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;
nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi,
na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”
Kutokutenda haki sio mpango wa Mungu, Mungu alimwita
Abrahamu ili awafundishe watu wake kutenda haki, na hii ndio sababu kubwa kwa nini Mungu alimchagua Ibrahimu,
Mungu mwenyewe anaeleza:-
Mwanzo 18:17-19
“BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo
nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa
yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na
nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili
kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.”
Mungu hukasirishwa sana wanadamu wanapoacha kutenda
haki na kufadha udhalimu
Warumi 2:18 “Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na
toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya
haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa
saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika,
watapewa uzima wa milele; na wale
wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na
ghadhabu;”
Na ndio maana sasa katika mahubiri ya Yohana Mbatizaji
aliwataka askari kuhakikisha kuwa hawadhulumu mtu na hii ilikuwa ni agizo la
kwanza kwao haki huinua taifa bali dhambi ni aibu ya taifa zima !
2. Wala msimshitaki mtu kwa uongo:
Kushitaki watu kwa uongo ni moja ya dhambi kubwa sana
zinazofanywa na askari Katika Biblia mara kadhaa tumewahi kushuhudia watu
wakiuawa na kuhukumiwa kwa kusingiziwa makosa yasiyokuwa yao, siku hizi unaweza
kupewa kesi nzito kama Uhaini, unaweza kubambikiziwa ugaidi, au utakatishaji wa
fedha au uhujumu uchumi na kadhalika kesi ambazo zinaweza kukunyima dhamana na
ukajikuta unasota rumande Moja ya amri katika amri za Mungu ni pamoja na kutokushuhudia
uongo
Kutoka 20:16 “Usimshuhudie jirani yako uongo”. Ni wazi kuwa
kwa mujibu wa sheria za Musa kushuhudia uongo lilikuwa ni moja ya makosa mazito
na kama mtu anagebainika kutaka kumsingizia mtu uongo adhabu yake ilipaswa kuwa
sawa na kile alichokuwa akimshitaki mwenzi wake, waamuzi walitakiwa kuchunguza
ka makini sana kama mtu anatoa ushuhuda wa uongo kisha yeye anayeshuhudia uongo
alipaswa alipaswa kuhukumiwa katika kosa lileliole analolishuhudia ili mwenzake
ahukumiwe
Kumbukumbu la
torati 19:18-19 “nao waamuzi na watafute kwa bidii;
na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo
juu ya nduguye;ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo
utakavyoondoa uovu katikati yako”
Agizo la torati liliwataka waamuzi vilevile kutokumhurumia
mtu aliyewashitaki wengine kwa uongo yaani aliyetoa ushahidi wa uongo alitakiwa
asihurumiwe
Kumbukumbu la
torati 19:21 “Wala
jicho lako lisiwe na huruma; uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino,
mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.”
Awaye yote ambaye angemshitaki mtu kwa uongo au kutoa
ushahidi wa uongo kama alikuwa ana lengo la kumuumiza mwenzake waamuzi
wangebaini wangetakiwa kutokumhurumia mtu huyo na angehukumiwa sawa na kosa
alilokuwa akilitolea ushaidi wa uongo bila huruma, kwa hiyo unaweza kuona kwa
nini Yohana mbatizaji alikuwa mkali kwenye swala hili ni wazi kabisa ilikuwa ni
kosa kubwa na zito mbele ya macho ya Mungu kushuhudia uongo dhidi ya mtu
mwingine.
Ukiacha maamuzi yanayoweza kutolewa na waamuzi au
serikali, Mungu pia huingilia kati pale askari na watu wengine wowote
wanapoacha kutenda haki na kujaribu kumshitaki mtu kwa uongo, Kitabu cha Esta
ni mfano uliowazi wa mtu aliyeitwa Haman ambaye alikuwa mshauri wa Mfalme
Ahasuero alimshauri vibaya kwa makusudi ya kuwaangamiza wayahudi, hususani kwa
sababu ya chuki yake dhidi ya Mordekai, hii ikitokana na wivu mkubwa aliokuwa
nao dhidi yake unaweza kuona
Esta 5:9-14 “Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa
moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami
wala kutetemeka mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Walakini Hamani
akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi
mkewe. Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa
watoto wake, nayo mambo yote pia ambayo mfalme amemfanikisha katika hayo, na
jinsi alivyompandisha juu ya maakida na watumishi wa mfalme. Zaidi ya hayo
Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu ye yote pamoja na mfalme
katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa
naye pamoja na mfalme. Bali haya yote yanifaa nini, pindi nimwonapo yule
Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme? Basi Zereshi mkewe akamwambia,
na rafiki zake wote, Na ufanyizwe mti wa mikono hamsini urefu wake, na kesho
asubuhi useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa
kicheko pamoja na mfalme karamuni. Basi neno likampendeza Hamani, akaufanyiza
ule mti.” Unaweza
kuona pia.
Esta 6:4 “Mfalme akasema, Yupo nani behewani? Ikawa Hamani alikuwa
ameingia katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme, aseme na mfalme, ili kumtundika
Mordekai juu ya mti ule aliomwekea tayari.”
Esta 7:9-10 “Ndipo aliposema Harbona, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa
wale waliohudhuria mbele ya mfalme, Tazama, basi, mti wa mikono hamsini urefu
wake, Hamani aliomwekea tayari Mordekai, ambaye alinena vema kwa ajili ya
mfalme, upo umesimamishwa nyumbani kwa Hamani. Mfalme akasema, Mtundikeni juu
yake.Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu
ya mfalme ikatulia.”
Maandiko yanaonya kuwa wote wanaoshitaki wengine kwa
uongo wako chini ya hukumu ya Mungu na hukumu ileile wanayoikusudia kwa wenzao
itawapata wenyewe, wale waliomshitaki Daniel ili atupwe kwenye tundu la simba
walitafunwa wao, maandiko yanasema kila aliyechimba shimo aliingia mwenyewe
pia, Mungu hafuirahii udhalimu hata kidogo
Zaburi 5:4-6 “Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa
kwako; Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako; Unawachukia wote watendao
ubatili. Utawaharibu wasemao uongo; Bwana humzira mwuaji na mwenye hila”
Jambo la kushangaza ni kuwa wakati mwingine unaweza
kuona kuwa hata makanisani na sehemu zenye watu wanaodhaniwa kuwa watu wa Mungu
watu husingiziana, hubambikiziana kesi za uongo na kusababisha madhara makubwa wakati
mwingine unaweza kuumizwa na watu wanaoshuhudia uongo lakini Mungu anajua na
atakufariji kwa namna yake, Yesu alitambua kuwa wako watu wanashitakiwa kwa
kubambikiziwa kwa uongo kwa kutokusimama katika haki au kuisimamia kweli
Mathayo 5:11-12
“Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na
kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia;
kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii
waliokuwa kabla yenu”.
Haijalishi watu watatuzushia nini kwa uongo tumtegemee
Mungu, Mungu atatulipia tu unaweza kuzushiwa uongo na kubambikiziwa kesi mbaya
sana na ukaumia na kupata hasara lakini Mungu atakuja kufanya kitu
Zaburi
119:69-72 “Wenye kiburi wamenizulia uongo, Kwa moyo
wangu wote nitayashika mausia yako. Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Mimi
nimeifurahia sheria yako. Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza
amri zako. Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na
fedha.”
Ni jambo la kusikitisha sana kuona jamii ikiwa imejaa
watu ambao wanaweza kutunga jambo zito na gumu dhidi ya watu wengine na
kuwaharibia maisha, wahubiri wa haki ya Mungu kama ilivyo kwa Yohana mbatizaji,
asingeweza kuvumilia dhuluma katika jamii wala asingetaka Yesu Kristo aikute
dhuluma lakini kutokana na jamii iliyokuwa imejaa uovu hata Yesu mwenyewe
alishitakiwa kwa uongo na mafarisayo na Yesu Kristo aliposhutumiwa uongo alinyamaza
kimya wala hakujibu neno
Isaya 53:7-8 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa
chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo
Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa
aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na
nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.”
Unajua kwanini Yesu hakufunua kinywa chake kujitetea
dhidi ya washitaki wake, maandiko yalionyesha katika Torati kuwa ni jukumu la
Waamuzi kuamua na kuchunguza kwa makini kama mtu analeta ushahidi wa uongo na
ni jambo la kusikitisha kuwa Pilato pia alishindwa kufanya maamuzi ya hali na
kuachilia Yesu auawe huku ushahidi ukiwa wazi kuwa ni ushahidi wa uongo
Mathayo
27:22-26 “Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu
aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe. Akasema, Kwani? Ni ubaya gani
alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulibiwe. Basi Pilato
alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa
mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu
mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu
yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu. Ndipo akawafungulia Baraba; na
baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe.”
Kama unadhani kubambikizia mtu kesi na kumshitaki mtu
kwa uongo ni jambo jepesi ni lazima ujiohoji na uhoji kuwa ukiacha kusudi la
Mungu la mwokozi kufa pale msalabani kesi ya kubambikiziwa Yesu ilimwachaje
Mariamu mama yake? Na je ndugu zake Yesu na wanafunzi wake hii maana yake wale
wote waliomshitaki Yesu kwa uongo nao vilevile kwa sharia ya Musa walitakiwa
kusulubiwa lakini Yesu alitangaza sharia mpya ya msamaha ndio maana akawaombea
baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo ni kwaajili ya haya mahubiri ya
Yihana mbatizaji na makatazo yake yalikuwa ni ya muhimu sana kwa wanadamu na
jamii sio tu ya wakati ule bali hata naya wakati wa sasa.
3. Kutokutosheka na Mishahara –
Yohana aidha aliwajibu na kuwataka askari vilevile
kutosheka na mishahara yao, ni wazi kuwa kutokuridhika ni tatizo kubwa sana la
mwanadamu tangu anguko la mwanadamu lilipotokea hakuna kitu kinatosha wanadamu
wamekuwa na tamaa na miongoni mwao wakiwa askari kwa sababu wao kama walinda
usalama katika jamii wana nafasi ya kuona fursa mbalimbali na hivyo ni rahisi
kwao kama ilivyo vilevile kwa watu wengine kuingia katika mlango wa tamaa
hususani katika fedha na kuwa na roho ya kutokutosheka
1Timotheo 6:7-10
“Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka
na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao
watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo
na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana
shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali
wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”
Hali ya kutokuridhika na kuwa na tamaa kwa vyombo
ambavyo vinatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa haki au kwa mwanadamu
awaye yote ni tatizo la siku nyingi katika jamii mbalimbali hali hii huharibu
uhusiano wetu na Mungu na wanadamu na kuharibu hali ya kiroho, Mungu angehukumu
vilevile hali hii kwani hata zamani katika Israel ilikuwa ni njia ya matajiri
kujipatia utajiri kwa njia zilizoharamu maswala haya yalikemewa na manabii kama
Amosi, Mika na Yeremia Mfano katika kitabu cha Amos watu waliweza kuuza utu wa
watu kwa sababu ya jozi za viatu tu
Amosi 2:6b “Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Israeli,
naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye
haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu;”
Kwa msingi huo Yohana katika mahubiri yake alikuwa
akiitaka jamii hususani askari kuwa na shukrani kuridhika kwani moja ya matunda
ya ukomavu wa ubinadamu ni pamoja na kuridhika Lakini Mungu anawataka watu wake
kuitenda haki ili Baraka za Mungu ziweze kumiminika katika maisha yetu
Mika 6:8 “Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana
anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa
unyenyekevu na Mungu wako!”
Lazima jamii ikubaliane na maandiko kuwa unapaswa
ufike wakati turidhike na maandiko yanatufundisha kuwa kuridhika kuna faida
kubwa sana
1Timotheo 6:6-19 “Walakini utauwa pamoja na
kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi
kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini
hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi
zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na
uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo
wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu
mengi. Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa,
imani, upendo, saburi, upole. Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule
wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi. Nakuagiza
mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu,
aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato, kwamba uilinde amri
hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambako
yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke
yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana; ambaye yeye peke yake hapatikani na
mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu
aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.Walio
matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri
usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie
kwa furaha. Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa
mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo; huku wakijiwekea akiba iwe msingi
mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli”
Kwa mtindo huu utakubaliana nami kuwa Nabii Yohana
mbatizaji alikuwa Mtu aliyeibhubiri haki ya Mungu kwa konyooka bila kujali cheo
cha mtu yeye aliwaonya watu wote masikini kwa matajiri, wafalme na hata watumwa
akiwataka wote kuandaa njia ya masihi na kuwa tayari kwa mioyo iliyotubu mbele
za Mungu.kila mmoja hana budi kujiuliza nay
eye je anafanya nini katika nafasui yake! Na afanye ulio wajibu wake
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni