Jumanne, 29 Machi 2022

Mbweha wadogo waiharibuo mizabibu


Wimbo uliobora 2:15 “Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.”


Utangulizi:

Kitabu cha wimbo uliobora ni mojawapo ya kitabu katika vitabu vijulikanavyo kama vitabu vya mashairi, vitabu vingine ni pamoja na Ayubu, Zaburi, Mithali, Muhubiri na kitabu hiki cha wimbo ulio bora, Katika vitabu hivi kuna mafunzo mengi sana ya hekima kuhusu maisha, na kwa kuwa ni vitabu vya mashairi wakati mwingine unaweza kukutana na lugha au misemo yenye kushangaza lakini yenye mafunzo muhimu sana kwa jamii!, kitabu cha wimbo ulio bora hata hivyo mashairi yake ni mashairi ya kimapenzi na ni mtu na mpenzi wake waliokuwa wakiimbiana na kujibizana, katikati ya mahaba yao wakaambiana maneno haya Wimbo Ulio Bora 2:15 “Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.” Kimsingi lugha hii ni lugha ya kimashairi na inatufunza mamswala ya msingi katika Nyanja nyingi za maisha katika maeneo mbalimbali, Wafasiri wengi wa maandiko na wanatheolojia wanakiri kuwa mahusiano haya ya kimapenzi yalikuwa ni kati ya kijana wa kifalme Suleimani na mwanamke Mshulami, hata hivyo kitheolojia wimbo huu unahusu vilevile mahusiano yaliyoko kati ya Yesu na Kanisa lake. Tunajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:- 

1.       Mbweha wadogo waiharibuo mizabibu!

2.       Maana ya mbweha wadogo waiharibuo Mizabibu


Mbweha wadogo waiharibuo mizabibu!

Nyakati za Biblia katika Isarael hasa kutokana na geographia ya nchi ya Kanaani au Israel Mbweha walijulikana kama wanyama wadogo waharibifu, hususani kwa sababu wao walijihusisha na kilimo ikiwemo kilimo cha mizabibu, Na wanyama hawa walikuwa miongoni mwa wanyama waharibifu kwa mizabibu hususani pale inapoanza kutoa maua au kuchanua !, inawezekana kuwa wako wanyama wengi wakubwa zaidi na waharibifu, kama ilivyo Afirka tembo wanaweza kuingia kwenye mashamba ya watu na wakafanya uharibifu mkubwa kwa dakika chache, Mashariki ya kati mashamba ya mizabizu yalikuwa yakizungushiwa wigo wa mawe ili kuyalinda na wanyama waharibifu na hivyo yalikuwa salama, ona

Marko 12:1-2 “Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu”.  

Lakini huenda hata hivyo Mbeha ndio walikuwa adui wakubwa wa mizabibu na labda zaidi sana wakati yakichanua maua. Lakini hata hivyo watu wengi waliwadharau mbweha kama wanayama wasi hatarishi sana, ukilinganisha na wengine, Kimsingi unapoiangali Biblia inaweza kumaanisha kuwa Mbweha alitumika pia au kuhesabiika miongoni mwa wanyama wanaoweza kutumika kwa uharibifu  na hivyo pamoja na kujilinda dhidi ya wanyama wengine wakubwa na waharibifu wakulima wa mizabibu hawakupaswa kabisa kuwadharau mbweha kwani nao wanachangia uharibifu hata kama watacheza cheza kwenye mashamba ya zabibu na kuangusha maua ambayo ndio asili ya kupata matunda, Ki biblia Mbweha ni mnyama aliyetumika kuonyesha hali ya uharibifu mfano Samsoni aliwatumia Mbweha kuchoma mashamba ya ngano ya wafililisti

Waamuzi 15:3-5 “Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru. Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili. Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni.”

Pia mbweha walitumika kama ishara ya dharau kubwa sana, kama kitu kilikuwa cha uongo, au chenye viwango vya chini sana au mtu mwoga kupita kawaida au chenya kuzuia mapenzi ya Mungu kilichodharaulika mno kama manabii wa uongo, au ujenzi ulio chini ya kiwango, au mtu mwoga kuliko kawaida manabii na watu wa nyakati za biblia walilitumia neno mbweha kwa kitu kilicho dharaulika mfano ona

Nehemia 4:1-5 “Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe. Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho; wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga.”

Ezekiel 13:1-4 “Kisha neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa.”

Luka 13:31-33 “Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.”              

Kwa hiyo suleimani na mpenzi wake walipokuwa wakiimbiana wimbo wa mapenzi na kuona kuwa penzi lao limechanua waliimbina na kupeana tahadhari kuwa watajilinda na maadui wakubwa wa mapenzi yao lakini fvilevile wasidharau maadui wadogo ambao nao wanaweza kuathiri pezni lao lisiweze kuzaa marunda, Maadui wakubwa wa mapenzi walifanannishwa na wanyama wakubwa huko Misri maadui wakubwa wa mapenzi walifananishwa na mamba, na Israel maadui wadogowadogo wa mapenzi walifananishwa na mbwea, kwa hiyo katika wimbo wao wa kimapenzi Suleimani hakutaka hata vitu vidogovidogo vinavyodhauliwa na watu,  wengi kwao visiharibu mapenzi yao kwa gharama yoyote wala viziwe tishio la mapenzi yao,  ili mahusiano yaweze kuwa imara kuna vitu vidogo vidogo vingi ambavyo havipaswi kupuuziwa, kwani vikipuuzwa navyo vinaweza kufifisha upendo, na vinaweza kuwa hatari sana hivyo wapendanao lazima wahakikishe kuwa wanajilinda dhidi ya maadui wakubwa na wale wadogowadogo ili kutunza mahusiano mema katika upendo wao,  Upendo haulindwi na kumnunulia mtu nguo pekee, au kumnunulia chakula, au kumtunza, au kumzalisha, au kumpa fedha ya saloon, au kumuachia fedha mezani, au kufanya kazi kwa bidii ili uitunze familia yako, au kushughulika sana katika tendo la ndoa au kumpa mumeo au mkeo kila siku, kuna vitu vidogovidogo sana ambavyo vinaweza kumfanya mwenzi wako ajisikie yuko peponi, leo hii watu wanagombana sana, hawasameheani, kila mmoja na simu yake, hakuna kupokeana, hakuna mazungumzo na vitu vingi ambavyo ni vya muhimu katika kujenga uhusiano hata hivyo kumbuka sitaki kuzungumzia mapenzi katika somo langu hili mimi nazungumzia maswala ya rohoni

Maana ya mbweha wadogo waiharibuo Mizabibu

Ni muhimu kufahamu kama tulivyosema awali kuwa Mbweha sio wanyama wakubwa sana wanaoweza kusababisha uharibifu mkubwa kama tembo au dubu na kadhalika, mbweha wana urefu wa inchi kama 20 na uzito kama wa kilo nane hivi, lakini tatizo lao kubwa ni kuwa wana uwezo wa kuharibu maua lakini pia kutafuna na kusababisha mzabibu kukauka na ukakosa matunda na ndio maana nyakati za Biblia licha ya kuwadharau mbweha lakini pia walikuwa na kampeni ya kuwakamata na kuwaua kabisa kutokana na uwezo wao mkubwa wa kusababisha uharibifu

Wimbo Ulio Bora 2:15 “Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.”

Jambo kubwa analolizungumza Suleimani hapa ni kuwa mapenzi yake na Mshulami ndio yanaanza kuchanua hivyo anatoa tahadhari kwa maswala ambayo kimsingi ynaweza kuleta uharibifu mkubwa katika mahusiano  yawe ya kimapenzi yawe na watu au na Mungu, watu wengi sana wanaompokea Yesu wanaweza kuwashinda maadui wakubwa wanaoonekana kwa nje wanaweza kuwa sio waizi, wanaweza kuwa sio wazinzi, wanaweza kuwa sio walevi, wanaweza kuwa hawaviti sigara, wanaweza kuwa sio wasengenyaji, wala sio wafitini, wala sio wachonganishi, wanaweza kuwa sio wenye tamaa ya fedha lakini kuna vitu ambavyo watu wengi wanavidharau, Maswala ambayo yanaharibu maisha yetu, na kuharibu ndoa zetu, yanayoharibu ushuhuda wetu, au yanayotutia gizani, yanayoharbu mahisiano wakati mwingine sio yale yanayoonekana kwa macho wakati mwingine ni yale yaliyoko mioyoni mwetu

1.       Ubinafsi -  wanadamu wengi sana wanasumbuliwa na ubinafsi, wanataka kujitukuza wenyewe, wanataka wao wenyewe ndio wabaki juu, wajitumikie wenyewe wajifurahishe wenyewe na wawe juu yaw engine tu  Biblia inaonyesha kuwa ni watu wachache sana ambao huangalia mambo ya wengine lakini wengi sana huangalia maslahi yao

 

2Timotheo 3:2-4 “Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;”

 

Kujipenda mwenyewe ni moja ya dhambi ambayo inaweza kuonekana kuwa ni ndogo lakini inaweza kusababisha madhara makubwa sana katika ndoa, familia na hata taifa au kanisa ni rahisi kufikiri kuwa ubinafsi sio tatizo lakini ni tatizo kubwa sana ambalo kwa hili wengi watakosa nafasi ya kuingia mbinguni hii ni ile hali ya mimi kwanza, mtu anaweza kuwa sio mzinzi, wala mlevi wala mwizo lakini akawa ni mbinafsi kuliko kawaida mchoyo anataka afanikiwe yeye tu

 

Luka 18:18-25 “Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

 

Tatizo kubwa la huyu tajiri ilikuwa iko dhambi ya choyo na umimi na ubinafsi ambayo yeye aliiona kama sio tatizo kubwa kwa sababu ameshika mari zote lakini kumbe alikuwa na mbweha anayeharibu mzabibu wake ambayo ni choyo na umimi na ubinafsi mkubwa kujikana nafsi sio jambo jepesi

 

Mathayo 16:24-26 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

 

Ubinafsi umeharibu maisha ya watu wengi duniani umeharibu mahusiano ya watu, umeharibu ndoa, umeharibu na kusababisha vita, mafarakano na migawanyiko mikubwa katika jamii, imeleta misiba mikubwa na hata vifo kwa sababu ya ubinafsi tu japo linaonekana ni jambo dogo

 

2.       Uchungu:

Watu wengi sana wanadhani ni haki wao kuwa na uchungu na hawaoni kuwa kuwa na uchungu ni dhambi inaonekana ndogo lakini ina madhara makubwa, kwa sababu ya uchungu na hofu mtu anajikuta akakosoa tu kila kitu au anakosoa mtu, linaweza lisiwe tatizo kubwa lakini biblia imaonya kwamba ni shina ambalo likiwemo ndani ya mtu linaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii

 

Waebrania 12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”

               

3.       Kutokusamehe:

 

Kusamehe ni swala la kutangaza msamaha kwa mtu mwingine, bila kujali amakukosea nini katika maandiko kibiblia msamaha wa Mungu unahusiana na dhambi zetu lakini ili tusamehewe na Mungu sharti lake ni kuwa lazima tuwasamehe wengine  kutokuwasamehe wengine kunakuweka katika magereza ngumu ya kukufanya nawe usisamehewe na Mungu

 

Mathayo 18:21-35 “Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.

 

Sio rahisi kusamehe lakini inahitajika neema ya Mungu, kuachia makosa ya aina mbalimbali ambayo tumetendewa na wenzetu watu wengi sana wanafikiri kuwa wa haki ya kutokusamehe wakidhani kuwa kununa kwao na kukasirika kwao ni halali kwa Mungu, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa mtu asiposamehe anaharibu kabisa maombi mfano katika sala ya Bwana

 

Mathayo 6: 12. “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.” Watu wengi kwaajili ya kutokusamehe wamepoteza kwa Mungu na wanadamu.

 

4.       Hasira

Hasira ni mojawapo ya udhaifu ambao watu wengi wanafikiri ni sifa kuwa nazo kumbe ni moja ya tabia mbaya sana, Mtu anayeweza kujizuia asikasirike ni mtu mwenye nguvu sana kuliko anayekasirika hovyo maandiko yanatuagiza kuwa tusiache jua likachwa kabla hatujaondoa hasira vifuani mwetu  andiko hili halitii moyo kuwa na hasira lakini linatia moyo kuhakikisha kuwa tunafanya mapatano na wale tuliowakosea kwa sababu ya hasira zetu kabla jua halijachwa  na kama tutashindwa kufanya hayo mapema tunampa shetani nafasi ya kupanda mbegu ya uchungu ambayo itakuwa na kuathiri wenguine

 

Waefeso 4:26-27 “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi.

 

Maandiko yanataka tuweke mbali na kuzifisha kabisa dhambi mbalimbali kubwa na nyinginezo tunazozidharau ikiwepo hasira na ghadhabu

 

Wakolosai 3:5-8 “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu. Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo. Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu

 

Ni hasira iliyomfanya Musa na Haruni kukataliwa na Mungu kuingia katika inchi ya mkanaani 


Hesabu 20:12 “Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa.”Hasira za Musa zikamfanya azungumze na kutenda mambo yasiyopasa ona 


Zaburi 106:32-33. “Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao, Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake.”Kutokana na kujaa ghadhabu Nabii Musa alimkosea Mungu na kupata hasara kwa kuzungumza na kutenda yasiyofaa watu wengi sana wamepata hasara kwa sababu ya hasira zilizowapelekea kutenda na kunena yasiyofaa hao ni mbweha wadogo wanaoharibu mizabibu

 

5.       Wivu.

 

Ni hali ya kutokujisikia vizuri kwa sababu ya mafanikio ya mtu mwingine, ubora wake, mafanikio yake na kibali chake au bahati yake wako watu wanaumia sana wanapoona wengine wamefanikiwa, wameolewa wao hawajaolewa, wamefanikiwa wao bado, wamefaulu wao wamefeli, wanakibali wao hawana, wanakubaliwa na Mungu wao hawana kitu na wanajisikia vibaya kiasi cha kukasirika kukosoa na hata kubeza ana wakati mwingine hata kuua kwa sababu ya wivu wenye uchungu ona

 

Mwanzo 4:3-5 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.”

 

Hali kama hii ilimtokea pia kaka mkubwa katika Mfano ule wa mwana mpotevu pale alipoona ndugu yake aliyepotea na akarudi japo alichukua mali za baba yake kama sehemu ya urithi unaomuangukia akaenda kuzitapanya na makahaba aliporejea baba yake alimpokea kwa furaha lakini kaka mkubwa aliposikia alisusa na kulaumu maamuzi ya baba yake

 

Luka 15:11-32 “Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;  lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”

 

Wako watu wana wivu wa ajabu sana kwa sababu wanachukizwa na neema ya Mungu iliyojuu yako hata wanaposikia umekosea wanatamani kama Mungu angekuua au kukutupilia mbali jehanamu ya moto, hawataki kabisa kuona Mungu amekurehemu na anaendelea kukubariki hii ni tabia mbaya sana na hawa ni mbweha waharibuo mzabimu, Bwana ampe neema kila mmoja kuwa mbali na wivu wenye uchungu katika jina la Yesu.

 

6.       Unafiki.

 

Watu wengi sana ni wanafiki, unafiki ni tabia ya kuigiza pretending Mungu hapandezwi na unafiki, kujipendekeza na kutaka sifa ili hali moyo wako uko mbali naye au na mapenzi yake 


Mathayo 15:7-9 “ Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.” 


Unafiki ni dhambi inayooenakana kuwa ni ya kawaida sana kwa watu wengi wanaodai kuwa wanamcha Mungu, bila kujua kuwa Mungu anachukizwa na jambo hili na Mungu alimuadhibu vikali Anania na mkewe kwa sababu ya dhambi ya unafiki 


Matendo ya mitume 5:1-10 “Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali,akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe.Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.”

 

Kwa hiyo utaweza kuona dhambi zile tunazazidharau na kuzifikiri kuwa ni ndogo zina athari kubwa sana katika kuharibu uhusiano wetu na Mungu na hivyo nazo Mungu anataka tuzishughulikie

 

7.       Choyo:

 

Maandiko yanatahadharisha sana kuhusu choyo, watu wengi sana ni wachoyo, na watu wengi sana wanapenda kujimilikisha vitu vingi wakifikiri kuwa kwa kuwa na vitu watakuwa na uzima Yesu aktika mafundisho yake alionya kuhusu choyo anasema katika Luka 12:15 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” Wako watu wana masanduku na nguo zimejaa kwenye begi zao masanduku mengine yamejaa mpaka zipu zimeachia au wanashundilia kwa miguu wakati wa kuyafunga lakini hawagawi Yesu akikolezea mungu mafundisho yake alionya kuwa sisi ni wapitaji tu katika ulimwengu huu na hivyio kujilimbikizia au mpango wa kujilimbikizia hautatufikisha kokote 


Luka 12:16-20 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.  Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?                


choyo ni moja ya mbweha wadogo na waharibifu, kuna choyo za aina nyingi, moja ya choyo maarufu sana katika mapenzi na inayokera na kuharibu mahusiano ni pamoja na kunyimana tendo la ndoa aina hii ya choyo imeharibu mapenzi sana na watu wengi wameachana kwa sababu wako wanaotumia fursa ya tendo la ndoa kuwekea mgomo na kuesa nafsi za wengine aina hii ya choyo imekemewa vikali katika maandiko 


1Wakoritho 7:1-5 “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.”  Neno la  Mungu linatahadharisha pia kuhusiana na jambo hili na ain azote za choyo Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kujilinda na choyo za aina mbalimbali ili tuwe na mahusiano imara kwa Mungu na wanadamu        

Athari za kutokukamata mbweha wadogo:-

-          Kunatokea kumzimisha Roho Mtakatifu Wathesalonike 5:19Msimzimishe Roho;”

-          Tunashindwa kuzaa matunda ya Roho Wagalatia 5:19-23 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

-          Tunapoteza furaha Zaburi 51:11-12Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.”

-          tunapoteza amani Wafilipi 4:7 “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

-          inaharibu uhusiano na Mungu 1Yohana 1:3 “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.”


-          Tunapoteza ujasiri katika maombi Warumi 8:26Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”

-          tunakuwa waoga 1Yohana 2:28Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake.”

Dhambi hizo tunazofikiri kuwa sio tatizo katika maisha yetu zinatuletea athari na kuharibu hali yetu ya kiroho na wakati mwingine kuturudisha nyuma na kuharibu uhusiano wetu na Yesu, hatuna budi kuhakikisha tunashughulikia maswala ya ndani tunayofafikiri kuwa ni madogo madogo na kumbe yanaharibu sana uhusiano wetu na Mungu, ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Rev. Innocent Samuel Kamote


Maoni 1 :

Unknown alisema ...

Mungu akubariki sana mchj kwa somo lililojaa baraka tele"Tukamatie mbweha,wale mbweha wadogo...."Ameni