Jumapili, 6 Machi 2022

Ngazi ya Yakobo:-


Mwanzo 28:10-19Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.”


Utangulizi:

Habari ya Ngazi ya Yakobo ni moja ya unabii ulio wazi kabisa kwamba kupitia Yakobo Mungu anakwenda kufanya jambo la maana sana kwa Dunia, ni ndoto iliyo wazi ya kuwa Mungu anakwenda kufanya njia ambayo kwa hiyo kutakuwa na uhusiano ulio wazi wa Mungu kwa watu wake kupitia Israel, Ni unabii ulio wazi kuwa Mungu amekusudia kupitisha jambo kwa Yakobo na kumfanya kuwa Baraka kwa dunia bila kujali kwamba amefanya nini katika maisha yake, Mungu katika maono haya au ndoto hii anamthibitishia Yakobo kwamba yuko pamoja naye na kuwa mapito yake sio mwisho wa kila kitu, Hatima ya maisha yetu haiamuliwi na nini tunakutana nacho katika maisha bali inaamuliwa na uhusiano wetu na Mungu, na ile kiu na hamu na shauku iliyoko ndani yetu inayotudhihirishia wazi kuwa tunampenda Mungu!, Kwa msingi huo basi leo tutachukua Muda kujifunza kwa undani na kwa kina na mapana na marefu, kuhusiana na somo hili Ngazi ya Yakobo, tukiwa na hamu na shauku ya kutaka kujua umuhimu wa Ngazi hii na maana yake kwa Yakobo na ujumbe wake kutoka kwa Mungu, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:-

·         Maisha kabla ya ndoto

·         Ndoto ya Yakobo

·         Maana ya ngazi ya Yakobo 


Maisha kabla ya Ndoto:

Kabla ya Ndoto yake Yakobo ambaye baadaye alikuja kuwa baba wa Taifa la Israel, alikuwa anakimbia kutoka mbele za uso wa ndugu yake Esau, sababu za kukimbia kwake zilitokana na makosa kadhaa aliyoyafanya kwa kaka yake, iko wazi kuwa wao walikuwa na ugomvi tangu tumboni

Mwanzo 25:21-23 “Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo.”

Ni wazi kuwa Mungu alikwisha kuonyesha mpango wake Tangu mwanzo ya kuwa atamtumia Yakobo katika mapenzy yake na Sio Esau, Hata hivyo watoto hawa walikuwa na mafarakano tangu tumboni, walikuwa ni kapacha wasiofanana na wenye mitazamo tofauti, ingawa Mungu alionyesha wazi kuwa atamchagua na kumtumia Yakobo, hata hivyo kulinganisha na tabia zao, Yakobo alikuwa mwenye hila na tabia mbaya sana ukilinganisha na Esau kaka yake kwani katika maisha yake baadaye alinunua kwa hila haki ya mzaliwa wa kwanza kutoka kwa ndugu yake ambaye naye alikuwa na mtazamo usiokuwa wa maana wa kutiokujua umuhimu wa Haki ya mzaliwa wa kwanza na kuuza kwa bei ya hovyo 

Mwanzo 25:27-34 “Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani. Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo. Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu.Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.”

Licha ya kununua kwa hila haki ya mzaliwa wa Kwanza, bado Yakobo aliendelea na tama yake ya kutamani maswala Muhimu ya kiungu ambayo esau alionekana kuyadharau, na hivyo Yakobo kwa mara nyingine alisaidiwa na mama yake walijaribu kwa kila namna, kumlaghai mzee Isaka na kufanikiwa kuchukua Baraka za Mzaliwa wa kwanza kutoka kwa Isaka ambaye yeye alikuwa amemkusudia Isaka, Yakobo tena na mama yake kwa hila walifanikiwa kumlaghai mzee Isaka na kuchukua Baraka hizo ambazo zilikuwa na umuhimu wa maswala ya kimwili na kiroho kwa Familia nzima  ona

Mwanzo 27:30-36 “Ikawa Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, na alipokuwa Yakobo ndiyo kwanza ametoka mbele ya Isaka, baba yake, mara Esau ndugu yake akaja kutoka katika kuwinda kwake. Naye pia amefanya chakula kitamu akamletea babaye, akamwambia baba yake. Babangu na aondoke, ale mawindo ya mwanawe, ili roho yako inibariki. Isaka, baba yake, akamwuliza, U nani wewe? Akasema, Mimi ni mwanao, Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Isaka akatetemeka tetemeko kuu sana, akasema, Ni nani basi yule aliyetwaa mawindo akaniletea? Nami nimekwisha kula kabla hujaja wewe, nikambariki; naam, naye atabarikiwa. Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikubwa cha uchungu sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu. Akasema, Nduguyo amekuja kwa hila, akauchukua mbaraka wako. Akasema, Je! Hakuitwa Yakobo kwa haki, maana amejitia mahali pangu mara mbili hizi? Alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua mbaraka wangu. Akasema, Je! Hukuniwekea na mimi mbaraka?

Tukio hili japo lilikuwa ni mpango wa Mungu lakini namna lilivyofanyika liliharibu kwa kiwango kikubwa mahusiano katika Familia ya Isaka, ambaye naye kimsingi ni mwana wa Ibrahimu na mrithi wa ahadi ile ya Abrahamu kufanywa taifa kubwa na Baraka kubwa sana kwa UlimwenguMwanzo 12:2 Kwa tendo la Yakobo kufanya hila hizo, kulipelekea uadui mkubwa kati ya Esau na Yakobo na kwa kweli Esau alikuwa amekusudia kumtenda mabaya Yakobo na kuwa angemuua mara tu baba yao atakapokuwa amekufa

Mwanzo 27:41 “Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.”

Jambo hili lilipelekea Isaka na Rebeka  kumruhusu Yakobo akimbie uhamishoni kwa mjomba wake Labani ili kwamba akajipatie mke huko lakini vilevile kuanza maisha mapya, Yakobo aliondoka katika hali ya wasiwasi mwingi na majonzi akiwa hana uhakika kuwa Mungu atafanya jambo, ama atatuimiza neno lake au atakuwa mwaminifu  kwa mtu ambaye kwa namna moja ama nyingine yeye mwenyewe amepoteza uaminifu, wote tunafahamu pale tunapokuwa tumefanya makosa makubwa sana wote tunajua kuwa japo tunampenda Mungu lakini wakati mwingine tumemkosea Mungu na kufanya mambo ya aibu na makubwa na mabaya ambayo kwayo tunaweza kudhani kuwa kila kitu kimeishia hapo, na kuwa yale yote ambayo tuliyatamkani na kuyafanya kwaajili ya Mungu huenda tusiyaone tena katika maisha yetu, wakati mwingine tunadhani kuwa hatuwezi tena kustahili Baraka za Mungu, tukiangalia mambo mabaya tuliyoyafanya, tunaweza kudhani kuwa tumepoyteza kibali kwa Mungu, tumepoteza upako, Mungu hatatutumia tena wala hatujali na wala hawezi kuzungumza na sisi, inaweza kuwa tumemkana Bwana tumefanya kinyume kabisa na neno lake, Yakobo alisababisha huzuni kubwa kwake, kwa kaka yake Mpendwa na pacha wake wa pekee, kwa baba yake ambaye ni mzee na yuko katika hali ya kufa, na mama yake aliyempenda sana sasa atamkosa na kukaa uhamishoni, ilikuwa ni hali ya kukatisha tamaa, kwamba badala ya kuona Baraka ambazo Mungu alizikusudia sasa yakobo anageuka kuwa mkimbizi na mtumwa anapoelekea kwa mjomba wake, akiwa njiani alichoka nadhani sio tu kwa sababu ya safari lakini pia kwa kuhuzunishwa na tafakari ya matendo yake ya kuhuzunisha na huzuni aliyowaachia wengine! Akiwa katika hali hii ndipo akapitiwa na usingizi mzito wa mawazo na kulala ! Hapa ndipo Mungu aliposema naye kwa njia ya Ndoto!

Ndoto ya Yakobo

Akiwa katika hali ya kufikiri na kutafakari, bila shaka utakubaliana nami kuwa haukuwa usiku mzuri kwa Yakobo hata kidogo, wewe na mimi tunafahamu tangu tulipokuwa wadogo pale tulipofanya makosa makubwa wakati mwingine baada ya kuadhibiwa au hata kabla ya kuadhibiwa tunafahamu usiku wetu unavyokuwa majuto mkaubwa yanavyotujia, mashaka makubwa yanavyotuvaa, na unajua kuwa unaweza usilale au unaweza kulala na usitamani kuamka na kama utaamka kosa lako linakuja na linakuwa la kwanza kulitafakari, majuto yanakuja unawaza  kwa nini nilifanya ujinga ule mkubwa, na unawaza kwa nini nimefanya vile laiti ningelijua, jaribu kuwaza na kukumbuka usiku ambao ulifanya makosa makubwa sana hutatamani jambo hilo ulikumbuke uatatamani hata kulifuta katika historia ya maisha yako, hiki ndio kilikuwa kinaendelea katika maisha ya Yakobo usiku ule, Yakobo alikuwa peke yake alikuwa anaelekea uhamishoni, usiku ule ulikuwa mzito na wenye kutisha usiku uliojawa na nyota nyingi na hakuna pa kupumzika Yakobo aliamua kuchukua jiwe ili ajipumzishe katika jiwe hilo kama ndio mto wa kulalia

 

Mwanzo 28:10-11 “Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale

Usingizi mzito ulimkabili Yakobo tena usingizi wa haraka ulikuwa ni usiku wa huzuni sana lakini ghafla usiku ule ulibadilishwa na kuwa usiku wa matumaini makubwa na usiku wa kipekee, usiku huu ulibadilishwa na Ndoto kutoka mbinguni na ndoto hii ilikuwa ndoto ya ajabu sana ndoto hii ilibadili mwelekeo wote wa mawazo ya Yakobo, ilikuwa ndoto ya matumaini makubwa sana ndoto hii ilikuwa hivi  

Mwanzo 28:12-15. “Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.” 

Ilikuwa ni ndoto iliyoleta uamsho mkubwa na matumaini makubwa katika maisha ya Yakobo yaliyokuwa muda mfupi uliopita amegubikwa na huzuni na kukosa matumaini lakini ndoto inabadili mwelekeo wa maisha yake, kila mmoja wetu katika maisha yake anapaswa kuacha kulalamika na kuhakikisha anakaa katika zamu yake akiisubiri ndoto yake itimie na ndoto hiyo haitasema uongo na itatimia kwa wakati wake, Yakobo alikuwa tu na muda wa kuisubiri ndoto hiyo itimie  kwa sababu ilikuwa ni ahadi ya Mungu mwenyewe ambaye ana sifa ya uaminifu!

Habakuki 2:1-3 “Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu. Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.”

Kila mmoja wetu anasubiri ndoto yake kutokana na majanga anayoyapitia ndoto itakayobadilisha mwelekeo wa maisha yako, maandiko yanatuahidi kuwa iko ndoto ambayo itakujia kwa wakati uliomariwa na ndoto hiyo inakuja hatraka, haisemi uongo wala haitakawia inafanya haraka kufika mwisho wake  ni lazima itakuja tu

Maana ya ngazi ya Yakobo

Ndoto kuhusu Ngazi ya Yakobo inahusu nini hasa?  Wana theolojia wengi sana wametafakari sana kuhusu maana ya ndoto hii lakini wameshindwa kupata majibu muafaka na kamili, Aidha katika commentary za Marabi wa Kiyahudi nao pia hawana tafasiri nzuri nay a kujitosheleza kuhusu ngazi hii, na wengine wamefikiri kuwa ngazi hii ni Yesu Kristo, Lakini ni wazi kwanza kabisa hili lilikuwa ni agano kati ya Mungu na Yakobo ya kuwa atamtumia na kuwa pamoja naye na kuwa kupitia yeye Mungu atafanya uhusiano na Yakobo na uhusiano huo utawaunganisha wanadamu wote na Mungu kupitia taifa la Israel  unaweza kuona, Hivyo ngazi ya Yakobo inafunua Neema ya Mungu inayotuunganisha na Yesu Kristo, isiyotokana na matendo yetu, lakini inatupa kibali cha kumdfikia Mungu kwa neema tu! Ona  

Mwanzo 28:12-15. “Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.” 

Ngazi ya Yakobo katika ndoto hii ilikuwa inawakilisha muungano “Connection” Kati ya Mungu na wanadamu, inaonyesha wazi kuwa Mungu anatamani katika maisha yake kuwa na uhusino maalumu na mwanadamu bila kujali kuwa mwanadamu huyo yukoje yeye anatamani sana angekuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mwanadamu, uhusiano huo haungeweza kuanzishwa na mwanadamu mwenyewe bali ni Mungu tu, Ni Mungu pakee awezaye kuuanzisha uhusiano huo, Uhusiano huo ni wa kiagano ni uhusiano wa neema hautokani na matendo yetu ya nyuma tuliyotena kwamba tulikuwa wema au wabaya lakini tunaokolewa kwa neema ona

Waefeso 2:1-9Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. nKwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;  wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”

 

Yakobo alikuwa anajua wazi kuwa ameharibu uhusiano na Mungu na wanadamu, ameharibu usiano wake na familia alikuwa akijifikiri kuwa yeye ndio basi tena lakini Hakujua kuwa iko ngazi inayoweza kumuunganisha yeye na Mungu, hii ilikuwa ngazi ya neema inayoweza kumuunganisha mwanadamu na Mungu, ambayo haingalii historia yetu ya nyuma bali inaangalia moyo wenye kiu na hamu na shauku ya kumtaka Mungu, Yakobo anaona wazi kabisa Mungu amesimama juu ya ngazi hiyo  huku malaika wake wakipanda na kushuka hii ilikuwa ni ahadi iliyowazi kuwa Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake hata pale inapotokea kuwa sisi tumepoteza tumaini na kuacha kumuamini yeye hubaki wa kuaminiwa

2Timotheo 2:13  Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.”

Hakuna mwingine anayeweza kuwa mpatanishi, kiunganishi, daraja lenye kuweza kumfukia Mungu isipokuwa Yesu Kristo yeye pakee ndiye anayeweza kumpatanisha mtu mwenye dhambi na Mungu na kufufua tena matumaini yaliyopotea kwa sababu ya makosa na dhambi zetu

1Timotheo 2:5 “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;

Ngazi ya Yakobo inawakilisha upatanisho kati ya Mungu na wanadamu, Ki msingi upatanisho huu ulifanywa na Yesu Kristo kristo pale msalabani hivyo kimsingi ngazi hii ya matumaini inayounganisha uhusiano wetu na Mungu inayosimama kama daraja au mahali palipobomoka kutupatanisha sisi na Mungu bila kujali historia yetu kuwa tulifanya nini huko nyuma ua tumeharibu kwa kiasi gani, NGAZI HII NI NEEMA YA MUNGU INAYOTUUNGANISHA KWAKE KUPITIA KAZI ALIYOIFANYA YESU PALE MSALABANI Kupitia Yakobo ambaye ndiye baadaye Israel kulitokea kabila 12 na mojawapo ikawa kabila la Yuda ambalo lilimleta maishi kwetu Mathayo 1;1-17  Yakobo ambaye alikuwa na makosa mengi katika familia yake kupitia ngazi hii anapewa ahadi na Mungu kuwa Mungu atamtumia kuwa Baraka kwa ulimwengu, ngazi hii ni ya kwetu sote haijalishi kuwa tumeharibu kiasi gani, Mungu wetu ni mwaminifu, Mungu ni kama alikuwa hajali Yakobo amefanya nini lakini Mungu alikuja kuonyesha ya kuwa amemkubali Yakobo kwa neema tu,  haijalishi anaweza kujikosoa kiasi gani lakini ahadi ya Mungu kutoka kwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo iko juu yake na kuwa Mungu atamlinda na kumuongoza  na kupitia yeye jamaa zote za Dunia watabarikiwa, Ngazi ya Yakobo ni uhusiano  wa neema ulioimarishwa kati ya Mungu na wanadamu kupitia Yesu Kristo, Huyu ndio njia na kweli na uzima ! Mungu anasema nasi na kuwasiliana nasi kwa njia ya Yesu Kristo na kwa neema yake, Pamoja na matendo yake Maovu Yakobo alipata neema ya kulibeba kusudi la Mungu na hata hivyo kwa kuwa Yakobo alipata neema ya kulibeba kusudi hilo Mungu hakumuacha awe na tabia mbaya bali alimbadilisha yeye mwenyewe baadaye na kuondoa jina la hila na kumuita Israel.

Waebrania 1:1-2 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu

Usinione hivi nilivyo mwenzio nina ngazi, ni ngazi hii inayoniunganisha na Yesu ndio inayonifanya niwe tofauti na wanadamu wengine, Ngazi hii ni neema ya Mungu, Roho Mtakatifu aliniambia Bwana alikuwa amesimama mwishoni juu ya ngazi hii na malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka, na kwa vyovyote vile Ngazi hii sio Kristo, Bali ngazi hii ni nyenzo inayotuunganisha na Kristo na akaniambia ngazi hii ni neema ya Mungu! Yakobo hakuwa mzuri, kimtazamo kama Esau, hakuna na akili kama Esau, hakuwa na nguvu kama Esau, tofauti zao ilikuwa Yakobo alitamani sana mambo ya Mungu na esau aliyadharau mambo ya Mungu na kwa kuwa Mungu hutazama moyo Yakobo alipata neema ya Mungu, na Mungu akafanya naye agano la neema, mwambie mwenzio nina ngazi na ngazi hii ni neema ya Mungu neema hii inaniunganisha na Kristo kule Mbinguni, ninalindwa nina ahadi nina nguvu kwa sina stresses tena siogopi kwa sababu nina neema!

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote



Hakuna maoni: