Luka 23:33-37 “Na walipofika mahali
paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja
upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, BABA, UWASAMEHE, KWA
KUWA HAWAJUI WATENDALO. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. Watu wakasimama
wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa
wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale
askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema,
Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe”
Utangulizi:
Mojawapo kati ya usemi wenye maana sana
kati ya semi saba za Yesu alizozisema akiwa msalabani na ambazo zinatajwa
katika sehemu mbalimbali za injili, ni pamoja ya usemi huo wa muhimu ni usemi
wa Kwanza wenye Neno BABA UWASAMEHE KWA
MAANA HAWAJUI WALITENDALO ambalo leo katika msimu huu wa pasaka tutachukua
muda kulijadili kwa undani na kupata maana Muhimu sana iliyokusudiwa, maneno
mengine kati ya maneno saba aliyoyasema Yesu msalabani ni pamoja na:-
1.
Baba uwasamehe kwa maana
hawajui walitendalo Luka 23:34
2.
Amin nakuambia leo hii utakuwa
pamoja nani peponi Luka 23:43
3.
Mama tazama mwanao, mwana
tazama mama yako Yohana 19:26-27
4.
Mungu wangu Mungu wangu mbona
umeniacha Mathayo 27:46
5.
Nina kiu Yohana 19:28
6.
Imekwisha Yohana 19:30
7.
Baba mikononi mwako naiweka
roho yangu Luka 23:46
BABA UWASAMEHE KWA MAANA HAWAJUI WALITENDALO.
Leo ni siku ya ijumaa kuu, ni
siku ambayo wakristo wote duniani, tunaungana katika kuadhimisha na kukumbuka
kusulubiwa kwa Yesu Kristo huko Golgota miaka zaidi ya 2000 iliyopita katika
siku hii basi basi sisi tutachukua Muda kuangalia usemi huu wa Kwanza katika
maneno saba yaliyozungumzwa na Yesu Pale Msalabani wakati wa mateso yake , Neno
hili ni miongoni mwa maneno saba ya Yesu akiwa matesoni ambayo yamekusanywa
kutoka maeneo mbalimbali ya vitabu vya injili na hili mojawapo tutaangalia
umuhimu wake katika msimu huu wa Pasaka. Hapa tunazungumzia Msamaha.
Kila mmoja wetu kwa namna moja
ama nyingine amewahi kujeruhiwa moyo na mtu mwingine, kila mmoja amewahi
kujeruhiwa na kuathiriwa kiakili, kihisia na hata kimwili, na kwa sababu hiyo
tunaweza kujawa na maumivu ya aina Fulani mioyoni mwetu, ama uchungu wa aina Fulani,
vyovyote vile iwavyo ukomavu wa kiroho katika maisha yetu ya ukristo unapimwa
na namna tunavyoweza kusamehe, uwezo wa kusamehe ukiwa pamoja nasi unatuwezesha kuishi kwa furaha na amani
duniani na huku tukiwa huru bila kifungo chochote endapo tutakuwa na uwezo wa
kusamehe wengine.
Yesu Kristo akiwa Msalabani
aliangalia chini na kutafakari katika hali ya ukimya akiwaangalia wote
waliokuwa wanahusika katika kumtesa, Askari ambao walisimamia mateso yake wakigawana
nguo yake kwa kuipigia kura, Yesu hakuwahi kutenda neno lolote ovu, siku zote
alikuwa akiwafundisha watu neno la Mungu na kuwaponya watu magonjwa yao,
aliwahudumia watu akifufua, akiponya, akilisha akihurumia na kurehemu, hata
hivyo kwajili ya wivu wakuu wa dini walikusudia kumuua, waliandaa mpango
mkakati wa kumuua, walitoa rushwa kwa Yuda ili aweze kumsaliti, waliandaa
mashahidi wa uongo ili wamshitaki, walimuweka katima mikono ya wenye dhambi ili
asulubiwe, hakimu aliyekuwepo alipindisha hukumu ilihali akijua wazi kuwa Yesu
hakuwa na hatia, zaidi ya yote aliamuru Yesu apigwe mijeledi
Yohana 19:1-6 “Basi ndipo Pilato alipomtwaa
Yesu, akampiga mijeledi. Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani,
wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa
Wayahudi! Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu
huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake. Ndipo
Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau.
Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu! Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi
wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulibishe! Msulibishe! Pilato
akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.”
Ni ukweli usiopingika kuwa Yesu
aliharibiwa sana kiasi ambacho ilikuwa ni ngumu kumtamani sawa kabisa na alivyotabiri
Isaya katika Isaya 53:2-5 “Maana alikua
mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo
wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa
na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu
humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika
ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa
amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,
Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa
kupigwa kwake sisi tumepona.”
Pamoja na mateso haya na suluba
kali pia walimfanyia dhihaka za namna nyingi, mateso yake yamerekodiwa na Mel
Gobson katika filamu yake ijulikanayo kama Passion of Jesus ambayo wayahudi
walipoiona kwa mara ya kwanza waliikataa na kusema kuwa inaweza kuchochea chuki
kati ya wakristo na wayahudi wakifikiri kuwa Mel Gibson ametia chumvi, lakini
kitaalamu Mel Gibson ameonyesha karibu robo tatu tu ya mateso halisi
aliyoyapata Kristo, mateso mengine :-
Yohana 19:23-24, “Nao askari
walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa
kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa
imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie
kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na
vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.”
Mathayo 27:27-31 “Ndipo askari wa liwali
wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima.Wakamvua nguo,
wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa
chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake,
wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate,
wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki,
wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.”
Wahalifu wawili waliokuwa kulia
kwake na kushoto kwake wakimshutumu,
Mathayo 27:44, “Pia wale wanyang'anyi waliosulibiwa
pamoja naye walimshutumu vile vile.” Viongozi wa dini waliofanya
fitina na kutengeneza ushahidi wa uongo na kushinikiza kwamba Yesu asulubiwe na
waliokuwa wakimdhihaki Mathayo 27:41-43,“Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja
na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.
Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea
Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa
Mungu”
Hakimu Pilato ambaye alifahamu
kabisa kuwa Yesu hakuwa na hatia, lakini akapindisha kesi haya yote na ile aina
ya mateso kwa mwana wa Mungu, kungeweza kwa namna yoyote ile kuleta hisia za
maumivu, uchungu, kinyongo, kisasi, ugumu wa moyo, hasira, ghadhabu, ubaridi,
kujihami na kuhakikisha kuwa unawashughulikia wote waliokutenda uovu, Lakini
Bwana Yesu anatangaza kusamehe na kuwaombea wakosaji wote kwa BABA KUWA WASAMEHEWE, Hali hii
inaashiria uwezo mkubwa wa ukomavu mkubwa wa kiroho aliokuwa nao Yesu wa
kutangaza Msamaha, ni ngazi ya juu sana ya Rehema na upendo, kwamba hata katika
hali ngumu kama hii ya kuteseka bado Yesu anatangaza Msamaha dhidi ya maadui
zake ! wote tunafahamu kuwa msamaha sio jambo rahisi, lakini katika msimu huu
wa Pasaka Bwana Yesu anatukumbusha kwamba tunapaswa kuachilia na kutangaza
msamaha kwa wote waliotukosea lakini vilevile kuwaomba radhi wale ambao
tumewakosea, wakati huu wa Kwaresma ni wakati wa kuachilia ni wakati wa
kusamehe ni wakati wa kuonyesha kuwa tumekomaa kiroho na kiakili na kuwa
kusamehe ndio njia ya juu kabisa ya kuonyesha tabia ya uungu na ukomavu wetu,
tusamehe.!
Kusamehe ni nini hasa?
Kusamehe ni kuachilia, unaachilia
mambio yaende, unaacha kuhesabu ubaya uliofanyiwa unaufunika kwa kuendelea
kupenda, unaacha kutafuta kulipa kisasi au nkulipiwa kisasi, unaondoa moyoni
mwako hali ya kumfikiri mtu aliyekukosea unajiweka huru mbali na kifungo cha
aina yoyote cha kuwa na mtu moyoni, unamuhurumia mtu, unachukuliana naye,
unamuhesabu kuwa yeye ni dhaifu, hivyo unamuachilia
Faida za kusamehe
·
Unadumisha mahusiano, mahusiano
yanakuwa mazuri, Ndoa inakuwa nzuri, unampata ndugu yako
·
Unaiweka akili yako kufikiri
mambo ya msingi na kuzungumza mambo ya msingi
·
Unajiweka huru kutoka kwenye
migandamizo na msongo wa mawazo
· Unakuwa na afya nzuri, unakuwa
mwenye furaha, hutakuwa na pressure, hutaugua magonjwa ya moyo, na unakuwa mtu
mwenye uwezio wa juu wa kujitambua
·
Kusamehe kunakufanya wewe nawe
usamehewe na Mungu
Mathayo 18:21-35 “Kisha
Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami
nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata
saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja
aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu
mmoja awiwaye talanta elfu kumi.Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru
auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile
deni.Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami
nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe
ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari
mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho.Basi mjoli wake akaanguka
miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini
hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli
wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana
wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa
mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa
kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika,
akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu
wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu
yake.”
Kutokusamehe hasara zake.
Hakuna sababu ya kuwabeba watu moyoni, hii hali kiroho
inakuweka wewe mwenyewe gerezani na kukunyima furaha, dua, sala, sadaka na maombi
yetu vinakutana na kikwazo kama hatujawasamehe wengine Mathayo 6:12 “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni
wetu.” Mathayo 6:14-15 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa
mbinguni atawasamehe ninyi.Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu
hatawasamehe ninyi makosa yenu” kuna hasara
nyingi sana za kiroho na kimwili kama watu hawatasamehe na kuna faida nyingi
sana kama watu watasamehe.Lakini kama mtu hatasamehe yafuatayo yatamkabili:-
·
Unakuwa na moyo wenye uchungu,
huwezi kufurahia mahusiano hata katika ndoa
·
Unakuwa na mawazo mabaya kwa
kudhani Fulani ni adui yako
·
Utakuwa na mgandamizo wa mawazo
·
Unafungua mlango wa kuvamiwa na
mapepo, unafukuza uwepo wa Mungu
·
Unazuia Baraka za Mungu na
kufanya ibada zako zikataliwe
Bwana na ampe neema kila Mmoja
wetu, kuwa na uwezo wa kusamehe ili tuweze kuwa wana wa Mungu sawasawa na
mafundisho ya Bwana wetu Yesu!
Na. Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni