Jumatano, 13 Aprili 2022

Litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!


1Nyakati 13:9-12 “Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng'ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hata akafa pale pale mbele za Mungu. Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, NITAJILETEAJE SANDUKU LA MUNGU KWANGU?


Utangulizi:

Moja ya mazingira ya kusikitisha sana katika Historia ya maandiko ni Pamoja na historia ya kufa kwa kuhani aliyeitwa Uza kifo chake kimeelezewa kwa kina katika 1Nyakati 13:1-14, Kifo cha kuhani huyu kilikuwa ni matokeo ya uamuzi wa Daudi kulileta Sanduku la Agano la Mungu kutoka mji ulioitwa Kiriath Yearimu kuja Yerusalem mwendao wa miles kama kumi hivi (10). Sanduku lililetwa likiwa limebebwa kwenye mkokoteni uliokuwa ukikokotwa na ngombe!

Walipokuwa wakisafiri kuja Yerusalem ng’ombe wale walikunguwaa yaani walijikwaa na ikawa kama wanataka kuangusha Sanduku la agano, ndipo Uza aliyekuwa karibu na sanduku la agano la Mungu akanyoosha mkono wake kujaribu kulizuia ili lisianguke, Hasira za Mungu zikawaka na Bwana akampiga Uza kwa sababu ile na akafa mbele za Bwana pale pale, Jambo hili lilikuwa la kusikitisha sana na kila mmoja aliogopa Daudi naye aliogopa akajawa na uchungu sana akaliacha sanduku la Agano katika nyumba ya Obedi- Edom na akaanza kuwaza nitaliletaje Sanduku la Mungu kwangu! Ama linanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!

2Samuel 6:6-11 “Hata walipofika kwa uga ya Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng'ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu. Daudi akaona uchungu kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Bwana siku ile; akasema, LITANIJIAJE SANDUKU LA BWANA? Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Bwana akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye Bwana akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote.”

Wanatheolojia wengi sana hujiuliza sasa ni lipi kosa la Uza? Je Mungu hakuwa mwema kwa kumuua Uza lipi lilikuwa jema kuliacha sanduku la agano lianguke? Au kuzuia lisianguke? Kwanini Uza alikuwa akifanya jambo jema na Mungu akamkasirikia na kumuua? Kwanini, bila shaka kuna mambo ya msingi ya kujifunza katika tukio hili, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Ufahamu kuhusu Sanduku la Agano

·         Litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!

·         Mambo ya kujifunza katika tukio hili.

Ufahamu kuhusu Sanduku la Agano.

Sanduku la agano, ambalo pia huitwa Sanduku la ushuhuda au sanduku la Mungu, kilikuwa ni moja ya chombo muhimu sana na kitakatifu mno kwa wana wa Israel, Miongoni mwa Thamani zlizokuwa zikikaa katika hema la kukutania au hekaluni Chombo hiki kilijengwa wa mti wa mshita (Acacia)  na kufunikwa kawa dhahabu  kutokana na maelekezo ya Mungu kwa Musa, Ndani yake kulihifadhiwa mbao mbili za mawe zenye amri kumi zilizoandikwa na Mungu, mwenyewe na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka pamoja na kopo la dhahabu lenye mana iliyohifadhiwa, Chombo hiki juu kilikuwa na Makerubi wawili walioinamisha mbawa zao na kufunika kiti cha Rehema cha Mungu, na ni kutoka Hapo ndio mahali Mungu alikuwaakizungumza na Musa ona:-

Kutoka 25:10-22 “Nao na wafanye sanduku la mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote. Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili. Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu. Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa. Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa. Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.”               

Kimsingi kuna mambo mengi sana tunaweza kujifunza kutoka katika chombo hiki kitakatifu na cha thamani mno,mbao mbili za mawe zilizoandikwa Amri kumi zinatufundisha wazi kuwa Mungu ni Mungu wa Utaratibu, Fimbo ya haruni iliyochipuka inatufundisha kuwa Mungu anaheshimu itifaki uongozi aliouchagua, Kopo la dhahabu na ile mana iliyohifadhiwa inatufundhisha kuwa Mungu anashughulika na mahitaji yetu kila siku, kwa ujumla kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka katika chombo hiki lakini kwa leo itoshe tu kusema maana kuu hasa ya chombo hiki ilikuwa ni uwakilishi unaoonekana wa uwepo wa Mungu asiyeonekana, Chombo kiliwakilisha “UWEPO WA MUNGU” chombo hiki kilikuwa na uwezo mkubwa sana wa kusababisha Baraka na madhara, Baraka kama kitapewa heshima inayostahili na madhara endapo ukiukwaji wa Heshima yake utafanyika!

2Samuel 6:10-12 “Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Bwana akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye Bwana akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote. Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, Bwana ameibarikia nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe.”

Kutokana na tukio la kifo cha kuhani Uza watu waliingiwa na Hofu na Daudi pia alimuogopa Mungu siku ile lakini aliingiwa na uchungu sio wa kuchukizwa na Mungu lakini kujutia na kujiuliza imekuwaje Mungu akafanya vile! Hili lilimpa kujiuliza swali kubwa kuwa litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!

Litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!     

Swala kubwa hapa ni namnagani sanduku la Mungu litafika Yerusalem, kwani walipokuwa katika kulileta Ndio kuhani Uza akauawa na Mungu kwa kulinyooshea mkono Sanduku, na Daudi aliogopa sasa kulileta na alipoliacha kwa Obed- Edom mtu huyu ndani ya miezi mitatu tu alibarikiwa sana kwa nini hasa sanduku la agano lilishindwa kufika Yerusalem katika wakati uliokusudiwa na kusababisha madhara njiani?

Tukio linatukumbusha umuhimu wa kufuata maagizio ya Mungu na kufanya sawasawa na Mapenzi yake, Mungu alikuwa ametoa maagizo yaliyokuwa wazi namna na jinsi sanduku la agano linavyopaswa kubebwa katika Torati

Kutoka 25:14-15 “Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.”

Katika maelekezo ya ujenzi wake sanduku lilipaswa kuwa na vikuku ambavyo vingechomekwa miti ya dhahabu kwa kusudi la kuichomeka na kulibeba sanduku la agano mabegani mwa makuhani maalumu walioteuliwa kufanya kazi hiyo wengi wakiwa ni walawi na hususani kabila la walawi wa wakohathi

Hesabu 7:9 “Lakini hakuwapa wana wa Kohathi; maana, utumishi wa vile vitu vitakatifu ulikuwa ni wao; nao wakavichukua mabegani mwao.”

Daudi pamoja na kuhani Uza walisahahu kufuata maelekezo ya Mungu, na Mungu akamshughulikia Uza mara moja kwa kifo, jambo hili lilimfanya Daudi kumuogopa sana Mungu, Mungu yuko Sirius/Makini na maagizo yake, yeye alitaka Sanduku la agano liheshimiwe kwa kiwango kikubwa sana chochote ambacho Mungu amakitangaza kuwa ni kitakatifu hakipaswi kuchukuliwa kimzaha mzaha, Ulimwengu wa kiroho uwe wa giza au wa nuru unazingatia sana masharti wakati wote kama ukivunja mashari au miiko au kutokufuata maelekezo huwezi kutoboa! Ona madhara;-

1Samuel 6:19 “  Basi Bwana aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la Bwana, wapata watu sabini, na watu hamsini elfu; nao watu wakalalamika, kwa kuwa Bwana amewapiga watu kwa uuaji mkuu.”

Daudi alikuwa amejifunza kuwa ubebwaji wa sanduku la Mungu mwanzoni haukuwa umefuata maelekezo yake na sasa Daudi akawa amejifunza kupitia uchungu alioupata kwa kifo cha Uza ilikuwa ni lazima sanduku la Agano libebe Mabegani tena na makuhani kama Bwana alivyoagiza, wao walibeba kama wafilisti wasiomjua Mungu walivyolirudisha Sanduku la Agano

 1Nyakati 15:2 “Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua Bwana, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima. 15 Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, sawasawa na neno la Bwana.”

Walipofuata maelekezo ya Mungu kwa uaminifu ndipo walipokuwa na uwezo wa kulibeba sabduku la Bwana bila kusababisha madhara  na safari yao ikawa salama tofauti na mwenendo wao wa Mwanzo, watu wengi sana hawafanikiwi kwa sababu hawafuati maelekezo, huwezi kubeba uwepo wa Mungu kama Mungu hajakuchagua uubebe, Kama hujali kuhusu maelekezo na kufuata utaratibu hakuna mafanikio mahali popote ambapo watu hawafuati utaratibu Mungu ni Mungu wa utaratibu, Sanduku la agano litakujiaje ni kwa kufuata maelekezo, mafanikio katika maisha, kujibiwa maombi na kufurahia Baraka na uwepo wa Mungu vitatujia katika maisha yetu endapo tutakuwa makini kufuata maelekezo na kuyatii na kuacha kutumaini hekima yetu na ujuzi wetu wa kibinadamu.

Mambo ya kujifunza katika tukio hili.

Mungu ni mwema nani mwenye upendo mwingi sana na rehema zake ni kubwa kwa wanadamu lakini linapokuja swala la kutokufuata Maelekezo yake Mungu anachukizwa sana na yuko tayari hata kuahirisha mpango wake kwa mtu asiyefuata maelekezo, Endapo mtu anataka kufanikiwa katika njia za Mungu basi ni vema akafuata maelekezo.

·         UTII: 1Samuel 15:22-23 “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.”

 

Lazima wakati wote watu wajifunze, kukubali kujifunza sio dhambi, Yesu alikubali kujifunza Kabla ya kuwa Mwalimu mzuri na kiongozi mzuri alichukua Muda kukaa na walimu na aliuliza maswali  na hivyo tunamuona yeye baadaye anakuja kuwa kiongozi na mwalimu mwema na bora zaidi Duniani

 


·         KUJIFUNZA: Luka 2:52 “Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.”  Watu wengi sana wanaponzwa kwa sababu ya kujifikiri kuwa wanajua maandiko yanasema mtu akidhani ya kuwa anajua hajui bado kama impasavyo kujua ni lazima kila kitu tujifunze

 

1Wakoritho 8:2 “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.”

 

Daudi mwanzoni alikuwa hajui na alipokubali kujifunza akafanikiwa wako watu wanaona noma kujifunza wanafikiri kuwa watakuwa duni sana wakijifunza na kuuliza wanataka waonekane kuwa wanajua, Mungu hamfurahii mtu awayeyote anayekataa maarifa

 

Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.”

 

·         KUMTEGEMEA MUNGU SIO AKILI:  Mungu hapandezwi na mtu anayezitegemea akili zake mwenyewe, kutegemea akili zako mwenyewe ni kiburi, Kanuni ya Mungu inatutaka kuyatafuta mapenzi yake na kuyafuata tunapoanza kujifanya tuna akili na tunazitumainia akili zetu na hekima zetu basi madhara yake ni pamoja na kuharibikiwa Lazima tumtegemee Mungu katika njia zetu zote

 

Mitahli 3:5-8 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.”

 

Maandiko yanatuonya sana tuache kujiamini kupita kawaida na kufikiri kuwa yale tunayoyaona sisi ni sahihi wakati wote kumbe wakati mwingine yako kinyume na mapenzi ya Mungu, kujifikiri kuwa sisis ni smart mno tuko vizuri kichwani kunatupelekea kuumbuka kwa sababu tunaweza kudhani njie yetu ni sahihi kumbe njia ile ni njia ya mauti

 

Mithali 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”

 

Ilionekana ni sahihi kwa Uza kulinyooshea mkono Sanduku la agano ndio kwani ng’ombe walikuwa wamejikwaa na Sanduku lingeanguka isingekuwa vema machoni pa Uza ilikuwa ni sahihi lakini kumbe tukio hilo lingeleta mauti, Jambo linaweza kuonekana sahihi machoni pako lakini likawa sio sahihi machoni pa Mungu, kama mtu anataka kuufurahia uwepo wa Mungu, amani yake na uvumilivu wake hatuna budi klujifunza kutoka katika neno la Mungu na kulitendea kazi katika maisha yetu.

 

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Maoni 1 :

Matiko alisema ...

Ubarikiwe sana mtumishi wa Mungu aliye hai