Jumatatu, 25 Aprili 2022

Yesu anaposimama katikati!


Yohana 20:19-23 “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika ubinadamu wetu, mara kadhaa tunaweza kuwa na wakati wa amani na vilevile tunaweza kuwa na wakati, tukapoteza amani na kuwa na mashaka kutokana na majaribu ya aina mbalimbali na changamoto za aina mbalimbali tunazokutana nazo, wakati mwingine tunaweza kujawa na hofu na mashaka hata kufikia kiwango cha kujifungia, kwa woga na hofu huku tukiwa hatujui hatima yetu, ni katika hali ya namna kama hiyo wanafunzi wa Yesu Kristo walikuwa na wakati mgumu sana wakati Yesu alipokamatwa na kuteswa kwa kusulubiwa na kufa na kuzikwa, kulikuwa na hali ya mashaka makubwa mno, huku taarifa za kufufuka kwake zikiwa bado hazijathibitika kwa uwazi kwa wanafunzi wote, lakini vilevile Bado kulikuwa na wasiwasi kama wayahudi watawaacha salama wanafunzi ama walianza na Kristo kisha wamalizie kundi lake hivyo walipoteza matumaini kabisa! Na kukata tamaa! Wakiwa katika hali kama hiyo maandiko yanasema Yesu akasimama katikati yao!, kumbe Yesu anaposimama katikati hali inakuwa tofauti, huyu ni Yesu aliyefufuka mara baada ya kusulubiwa na kufa na kuzikwa:-

o   Yesu akisimama katikati mahali ambapo watu wamepoteza tumaini, matumaini yanarejea

o   Yesu akisimama katikati mahali penye hofu hofu inaondoka

o   Yesu akisimama katikati mahali ambapo watu wamepoteza amani, amani inarejea

o   Yesu akisimama katikati mahali penye changamoto za aina mbalimbali, changamoto hizo zinatoweka

o   Yesu akisimama katikati wakati watu wanapopata shida na kuingilia kati, shida hizo zinaondoka

o   Yesu akisimama katikati anabadilisha hali ya mashaka na kuyaondoa kabisa, kwanini Yesu husimama katikati ni  kwa sababu anajali na kuguswa sana na mahitaji yetu:-

Maandiko yanasema na tumtwike yeye fadhaa zetu zote maana yeye hujishughulisha sana na mambo yetu,

1Petro 5:7” huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”


Ni muhimu kukumbuka hili ya kuwa Mungu wetu ni Mungu muelewa sana wakati mambo yanapoonekana kuwa ni yenye kuvunja moyo, yeye husimama katikati na kubadilisha hali ya hewa, Tuna Mungu anayejali, na mambo huwa tofauti wakati wote anapojitokeza,  wakati wa pasaka unapoadhimisha kufufuka kwa Yesu ni vema ukakumbuka kuwa Yesu aliyefufuka ni wa tofauti yeye anauwezo wa kuibuka katikati ya shida yako na kuyafanya mambo kuwa tofauti, Krito alipokuwa katika mwili alikuwa na tabia hiyohiyo ya kuingilia kati na kubadili hali ya hewa pale mambo yanapoharibika kwa wanadamu, Yesu anauwezo wa kubadilisha Msiba kuwa furaha, anauwezo wa kuhahirisha mazishi na kurudisha furaha na amani iliyopotea ona:-

Luka 7:11-16 “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.”

Yesu anauwezo wa kutuliza dhoruba ya aina yoyote itakayojitokeza katika maisha yetu na kutuondolea wasiwasi

Marko 4:36-41 “Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Yesu aliweza kuyafanya hao alipokuwa katika hali yake ya kawaida ya mwilini hapa duniani tena akiwa na mipaka katika Israel, Lakini Yesu aliyefufuka hana mipaka na haitaji mlango ufunguliwe yeye anauwezo wa kuingilia kati mahali popote pale na kufanya lolote lile iwe mashariki au magharibi, kasikazini au kusini yeye anaposimama katikati hubadilisha hali ya mambo:-

Yesu anaposimama katikati ya hali Fulani yeye anafanya nini kuna mambo ya kujifunza kutoka katika kifungu hiki

1.       Anaonyesha Makovu, unajua kwanini Yesu huonyesha makovu,? Mimi ninalo kovu Fulani katika mkono wangu wa kushoto ambalo nililipata Tarehe 01/05/2000 kule Dodoma nilipokuwa naelekea chuo cha biblia, nilivamiwa na majambaza zaidi ya nane na wakanikaba na kuniumiza kisha wakapora kila nilichokuwa nacho wakati huo nilipopoteza fahamu kwaajili ya uvamizi ule, kila ninapoliona lile kovu nakumbuka tukio lile na ninakumbuka namna Mungu alivyoniokoa na mauti, lakini kama Haitoshi Tarehe 01/05/2015 Binti yangu wa kwanza Irene alizaliwa hivyo kwenye Tarehe ile ambayo nilipaswa kukumbuka tukio baya sasa ninakumbuka tukio zuri la kuzaliwa kwa binti yangu, kovu lile limekuwa historia, Yesu aliwaonyesha makovu yake wanafunzi wake ili kwamba wajue kuwa mateso yake yamebaki historia tu, Yesu amefufuka yu hai haijalishi aliumizwa kwa kiwango gani,

 

Yohana 20:20 “Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.”

 

Mungu anajua hali unayoipitia na Yesu aliyefufuka anakuthibitishia kuwa hali unayoipitia itakuwa historia tu, Mungu atakufanyia muujiza mkubwa wa kupita kawaida kinyume kabisa na matarajio ya maadui zako, watuoenee wanavyoweza kutuonea, watutese wanavyoweza kututesa lakini hali yeyote unayoipitia sasa itakuwa Historia tu unaweza usiwe na majeraha na makovukatika mwili wako lakini unaweza kuwa na majeraha na makovu makubwa katika moyo wako, Yesu alityefufuka anapoonyesha makovu namaanisha mashaka yako na mateso yako na majeraha yako atayabadili kuwa historian a wewe utakuwa na kiwango kingine tunapoadhimisha kufufuka kwa Yesu tukumbuke pia kuwa atatuonyesha makovu yake nah ii ni sihara ya kuwa mauti na mateso na majeraha yetu yatabakia kuwa historia tu!.

 

2.       Anatangaza Amani, Ni muhimu kufahamu kuwa Mstari wa 19 na wa 21 Yesu anasema Amani iwe kwenu, hawa walikuwa wamepoteza amani, walikuwa na fadhaa, walikuwa na woga, walikuwa na hofu, Yesu alikuwa amewaambia mapema kuwa anawapa amani  na akarudia tena amani iwe kwenu!, kwa nini alifanya alitangaza vile ni kwa sababu alikuwa anataka kuwaondolea haki ya kuchanganyikiwa na hali ya hofu na woga ambao uliwaondolea amani, kumbuka amani hii ni maalumu kutoka kwa Mungu

 

Yohana 14:27 “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”

 

Amani itokayo kwa Mungu ni zawadi ni tofauti na amani ya dunia hii neno la kiebrania alilolitumia Yesu ni Shalom! Au Irene kwa kiyunani ambayo ni amani ya kipekee itokayo kwa Mungu, amani hii huilinda mioyo yetu kwa kiwango cha hali ya juu Paulo mtume anaiita amani hii kuwa inapita akili za kibinadamu amani hii inauwezo wa kutulinda na kutuhifadhi!

 

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

 

Amani ipitayo akili zote itatuhifadhi hii ni amani inayotumika kuhifadhi na kuilinda mioyo yetu isijeruhiwe hali yoyote ya kuchanganyikiwa na kutokuelewa kwamba hali itakuwaje hali hiyo na hofu hiyo inaondolewa na Yesu Kristo aliyefufuka, wanafunzi walikuwa wamejifungia na hawajui itakuwaje, walikuwa wamechanganyikiwa na hali ngumu ya kuuawa kwa Mwalimu wao kupitia mateso mazito lakini zaidi na habari tata ya kwamba Yesu yuko hai au la au mwili wake umeibiwa je amefufuka kwelikweli au hali ikoje? Kusimama katikati kwa Yesu kristo na kuwatangazia amani kuliondoa mashaka yote, Yesu atatuondolea mashaka yote yanayotukabili maishani.

 

3.       Yesu anatupa Mamlaka, Yohana 20:22-23 “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”.

 


Yesu anapoingilia kati anatupa mamlaka kupitia Roho wake Mtakatifu tunakuwa mawakili wa siri za Mungu kiasi ambacho tunaweza kuwapa watu mbingu au kuwanyima, kuruhusu wasamehewe dhambi au wasisamehewe, ni Roho Mtakatifu aliyekuja kubadilisha maisha ya watu kama Petro ambaye alitoka kumkana Yesu mara tatu siku chache zilizopita sasa ni jambo la kustaabisha kuwa anapewa mamlaka miongoni mwa waliopewa mamlaka na uweza na nguvu za Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu anatupa maisha ya ushindi na ujasiri anatupa kujiamini na uweza na mamlaka ya kutenda mambo makubwa na ya ajabu ni yeye atakayetupa ushindi katika siku zote za maisha yetu!

 

Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu anaposimama katikati, hofu zetu, katikati ya mashaka yetu, katikati ya changamoto zetu, katikati ya mateso yetu, katikati ya shida zetu, katikati ya vifungo vyetu, katikati ya mashaka yetu, katikati ya masomo yetu katikati ya jambo lolote lile maombi yetu yanajibiwa na kupata ufumbuzi lolote lile majibu ya maswali yetu katika maisha,  na Mungu anageuza kila kitu kwa njia ya kutisha, anajibu maombi, anafanya kwa wakati wake, anatikisa, anaweka huru anaokoa, anawezesha, anapatanisha anaweka mambo yote kuwa sawa, anavunja magereza, na minyororo analainisha malango yanafunguka ana anatetemesha na anaokoa!

Matendo 16:22-31 “Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”  

Namuomba Mungu asimame katikati katika maisha yako na kuleta majibu ya maombi yako na kukutana na haja ya moyo wako, wakati wote tunapopita katika changamoto za aina mbalimbali ni muhimu kwetu tukakumbuka kuliitia jina la Bwana na kumtwika yeye fadhaa zetu zote, naye ataingilia kati maisha yetu kwa kusimama katikati yetu na kutupa ufumbuzi wa mahitaji yetu ! uongezewe neema

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima


Hakuna maoni: