Jumatatu, 27 Juni 2022

Imani ya kuhamisha Milima !


1Wakorintho 13:1-3 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.”



Utangulizi:

Imani imekuwa ni mojawapo ya jambo Muhimu sana ambalo limeelezewa kwa ajabu katika maandiko, Imani imetumiwa na mashujaa wote wa imani tunaowasoma katika maandiko kama nyenzo ya kipekee sana ambayo iliwaletea matokeo makubwa sana katika maisha yao

Waebrania 11:32-35 “Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora;”

Maandiko yanasema pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, mtu awaye yote anayemuendea Mungu ni lazima aamini kuwa Mungu yupo na kuwa huwapa thawabu wale wawamtafutao Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”     Kwa msingi huo basi ni muhimu kufahamu kuwa mashujaa wote wa imani tunaowasoma katika maandiko, pamoja na mambo mengine vilevile walimuamini Mungu katika kiwango cha imani ya juu sana kiasi cha kukubalika kwa Mungu, Abraham kwa mfano alipojaribiwa na Mungu kumtoa Isaka kwa imani alikubali, yeye aliamini ya kuha hata akimkata kichwa Mungu atamfufua tena kutoka kwa wafu na atarejea na mwanaye  Waebrania 11:17-19 “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee; naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.”

Aina za imani!

Katika agano jipya iko imani iokoayo, imani hii ni kumuamini Bwana Yesu kwa kukubali kazi aliyoifanya pale msalabani, na kwamba alikufa na kufufuka imani hii hutupa zawadi ya wokovu, imani hii kila mmoja anaweza kuipata kwa kumkubali Yesu kuwa bwana na mwokozi

Warumi 10:9-12 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;”

Vilevile iko imani inayotokana na kuwepo kwa karama ya Roho Mtakatifu, ambayo huitwa neno la Imani au neno la mamlaka hii imetajwa katika 1Wakoritho 12:4-11 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.” Karama ya imani ni karama kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uwezo wa kutamka neno na likawa au likasababisha muujiza mfano 1Wafalme 17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.” Hapa Eliya anatamka kwa neno la Mungu na kile anachokitamka kinakuwa vilevile, Elisha pia alitamka kuuzwa kwa chakula kwa bei nafuu wakati kulikuwa na njaa kali haijawahi kutokea njaa ambayo ilipelekea hata watu kula watoto wao 2Wafalme 6:24-30 24. “Ikawa baada ya hayo, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru Samaria. Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha. Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme.  Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni? Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho.Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake.”  Wakati hali halisi ikiwa ngumu kwa kiasi hicho Elisha anatamka kuwa kesho panapo saa hii chakula kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli ona 2Wafalme 7:1-10, “Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria. Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula. Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe?  Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu. Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha. Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme. Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha.”  Kisha ikawaje ona neno la Mungu alilolisema Elisha lilitimizwa vilevile kama alivyotamka 2Wafalme 7:16-20 “Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la Bwana. Naye mfalme akamweka yule akida, ambaye alitegemea mkono wake, awasimamie watu langoni; na watu wakamkanyaga langoni, akafa; kama alivyosema yule mtu wa Mungu, aliyenena hapo mfalme alipomshukia. Ikatukia kama vile yule mtu wa Mungu alivyomwambia mfalme, Vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, na kipimo cha unga mzuri kwa shekeli, ndivyo vitakavyokuwa kesho, panapo saa hii, katika lango la Samaria; na yule akida akamjibu mtu wa Mungu, akasema, Sasa tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akasema, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula. Ikampata vivyo hivyo, kwa kuwa watu wakamkanyaga langoni, akafa.”   

Mungu anatutaka tuwe na imani, tujiungamanishe naye katika kiwango cha kuwa na imani ya kuhamisha milima, kimsingi Mungu hafurahii sana kuona wakristo wanashindwa jambo, Yesu aliwakemea wanafunzi wake mara kwa mara kwa sababu walikuwa wanakosa imani hii

Mathayo17:15-20 “Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.”          

Sasa ni imani ya namna gani inahitajika ili kuhamisha milima Yesu anasema mkiwa na imani ndogo tu kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu ondoka hapa nao utaondoka huitaji imani kubwa sana unahitaji imani kidogo sana katika Mungu kukuletea ushindi na kutoa matamshi yenye mamlaka ya kiungu na mara moja utaweza kuona dunia ikishikishwa adabu

Mathayo 13:31-32 “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.”

Kumbe kiasi cha imani kinachohitajika ni kidogo tu nah ii ni kuonyesha kuwa watu wengi hawana imani, Mungu arupe kuwa na imani, Musa alikuwa mtu wa imani na alipokuwa akitamka jambo wakati mwingine hata kabla, hajaliomba Mbingu ziliweza kutekeleza matakwa yake ona:-

Hesabu 16:28-32 “Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba Bwana amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi Bwana hakunituma mimi. Lakini Bwana akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau Bwana Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote.”

Matamshi haya ya kimamlaka yatatuletea ukombozi, mkubwa sana katika maisha yetu Mungu ataifanya dunia ijuie na ifahamu ya kuwa yuko Mungu, mwenye nguvu na mamlaka nay a kuwa neno lake haliongopi kamwe, wakristo tuinuke na kuwa waombaji na kuitafuta mamlaka hii ili kushikisha adabu watu wasio na uelewa kuhusu Mungu

Ni milima ya namna gani inayozungumzwa hapa?

Niliwahi kumsikia mwanatheolojia mmoja mkubwa sana na msomi akizungumzia kuwa Yesu alipokuwa akizungumzia mlima au milima alikuwa akizungumzia mlima halisi au milima halisi, ni ukweli ulio wazi kuwa lugha inayozungumzwa kibiblia ni lugha ya kinabii,  na kinabii maandiko yanapozungumzia mlina yanamaanisha kikwazochochote kigumu, jambo lolote lililogumu, kwa hiyo inahitajika wazo la kinabii na kimaandiko kujua kuwa Yesu aliposema utahamisha mlima au Paulo mtume anapozungumzia imani ya kuhamisha milima wote kwa pamoja katika mioyo yao na jamii ya wale waliokuwa wakizungumza nao walielewa alikuwa anazungumzia vikwazo vinavyoinuka juu ya mtu, au jaribu au jambo gumu unaweza kuona, Milima hii ni vikwazo vya namna mbalimbali vinavyoweza kujitokeza katika maisha yetu, lolote linalozuia breakthrough au mpenyo katika maisha yako, upinzani, magonjwa, kifo, Magumu, yanayoonekana hayawezekani, na hali zenye utata katika maisha yetu hizi zote zinaweza kuitwa mlima ona

 Zakaria 4:6-7 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”

Unaona lugha ya kinabii kamwe haimaniishi kuwa mlima unaotajwa ni mlima halisia HAPANA Mungu hawezi kupinga ana kanuni yake ya kimaumbile kumbuka wakati anaumba ulimwengu alihitimisha kwa kusema tazama kila kitu ni chema, sisi tu nao uwezo wa kuchagua ni mahali gani pa kuishi unaweza kuamua kuishi bondeni au mlimani kwa kadiri ya uumbaji wa kiungu, hatusomi katika historia wala shuhuda kuwa kuna mtu aliweza kuondoa mlima mahali, lakini kwa lugha ya kinabii mlima ni changamoto ngumu zinazikinzana na maisha yetu ya kila siku

Isaya 40:3-5 “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa; Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.”

Unaona? milima hapa sio halisi ndugu zangu, milima inayotajwa hapa ni lugha ya mficho (Figurative) kama nilivyosema awali ni imani pekee ndiyo inayoweza kutuondolea mambo magumu ya kuyasawazisha hii maana yake yala yaliyoinuka juu yetu yanakuwa si kitu tena mbele yetu, kwa hiyo hakuna kitakachoweza kusimama mbele yako kutoka kwa mwaname au mwanamke kama utakuwa na imani

Marko 11:22-24 “Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.

Mathayo 21:21-22. “Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng'oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.”

Lugha hiyo pia ni lugha ya kukazia (hyperboles)kuonyesha namna na jinsi imani isivyoshindwa kitu na kuwa tunapomuamini Mungu na hata tunapomuomba Mungu kwa imani ni lazima tuamini na kusadiki kuwa lazima kutakuwepo matokeo makubwa sana.

Je imani yetu inaweza kuhamisha milima?

Ndio wakati wote tunapokuwa na imani imani hufanya mambo makubwa sana, lakini kuna maswala kadhaa ambayo yakikosekana katika maisha yetu tunaweza kuona mambo yakiwa ndivyo sivyo! Mathayo 17:14-21 1 “Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]

Wanafunzi wa Yesu walishindwa kumtoa pepo na Yesu aliwaonyesha sababu za kushindwa kwao, na kwanza aliwakemea mara kadhaa kwa sababu ya kukosa imani, kutia shaka, kuogopa jambo ambalo ni kinyume na imani.

Marko 4:40  Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?”

Marko 9:19 “Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.”

Mathayo 14:31 “Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?

hawakuwa na imani kabisa kuna maswala kadhaa ambayo yakikosekana kwako hutawexa kuona Baraka za kiutendaji katika imani

1.       Ukikosa imani

2.       Ukiacha kuomba

3.       Ukiacha kufunga

4.       Ukiacha kulitumia neno la Mungu

Siri kubwa ya ushindi na imani inayoweza kuleta matokeo inakaa katika maswala hayo niliyoyataja ukiwa na tabia hizo unaweza kuondoa mlima wowote unaoweza kujitokeza katika maisha yako, Mathayo 17:21 “[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]” Lakini kama inavyoelezwa katika maandiko ya kwamba silaha za vita vyetu zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome 2Wakoritho 10:4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) ni kukosa muda wa kuomba, kusoma neno la Mungu na kufunga ndiko kunakotuletea changamoto kuwa gumu katika maisha, tunapofanyia kazi maombi, neno na kufunga tunaifanya imani yetu kukomaa na kuwa kali sana  na kwa sababu hiyo hakuna mlima unaowezxa kusimamam mbele yetu neno la Mungu ambalo ni upanga war oho utarahisisha sana kazi yetu ya kuhamisha milima kwa haraka wakati wote Yesu alikema kukosekana kwa imani na mambo yanayoweza kuifanya imani kuwa imara ni hayo

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumapili, 19 Juni 2022

Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu !

Zaburi 23:1-6Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.  Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”



Utangulizi:

Moja ya zaburi maarufu zaidi duniani labda kuliko zaburi zote ni zaburi ya 23, Zaburi hii imetumiwa sana na Wayahudi na Wakristo katika ibada na maombi lakini vilevile kwaajili ya kujenga imani, Kiini kikuu cha zaburi hii ni yale maneno Bwana ndiye Mchungaji wangu maneno haya yanazigusa jamii nyingi sana Duniani, Hata huko Mesopotamia, Inasemekana kuwa Mfalme Hammurabi katika mojawapo ya hutuba yake muhimu sana aliyowahi kuitoa alihitimisha kwa kusema “Mimi ndiye Mchungaji ninayehakikisha usalama na mafanikio ya watu wangu, utawala wangu utakuwa wa haki, wenye nguvu hawatawaonea wanyonge, na hata yatima na wajane watatendewa kwa haki” maneno ya kiongozi huyu wa zamani sana yalikuwa maarufu na huenda yakawa yalichangia mtunzi wa Zaburi hii kuyachanganua kwa kina katika uimbaji wake kwa kusudi la kutambua uhusiano wake na Mungu.

Zaburi hii ina mistari michache sana lakini yenye kubeba maana pana sana na hatuwezi kwa somo moja kama hivi kugusia kila neno linalozungumziwa na zaburi hii, Hata hivyo leo Mwalimu mkuu Roho Mtakatifu anatupeleka kuutazama mstari wa tano (5) katika zaburi hii ya (23) ili tuweze kujifunza kile ambacho Mungu amekikusudia kwetu .

Katika Zaburi 23:5 Daudi anasema “WAANDAA MEZA MBELE YANGU, MACHONI PA WATESI WANGU maneno haya peke yake yanaashiria uhusiano mkubwa sana na wa karibu ulioko kati yake na Mungu, lakini sio hivyo tu mstari huu unafunua heshima kubwa sana ya kifalme ambayo mwandishi anapewa na Mungu, kwani kumbuka kuwa anayeandaa meza hapa sio Daudi bali Mungu anamuandalia Daudi meza hivyo kimsingi mahali hapa pana maana pana na kubwa sana ambayo inaweza kumfaa kila mmoja wetu leo!

Ni muhimu kufahamu kuwa katika taratibu za kifalme, unapomualika mtu ambaye unamuheshimu sana katika utawala wako basi mgeni huyo rasmi labda ni rais au mfalme wa taifa lingine kama alikuja aidha kwa mazungumzo au kwa mualiko wa serikali yako au ziara ya kuimarisha uhusiano basi inapofika jioni kiongozi huyo mualikwa huandaliwa chakula maalumu ambacho huitwa dhifa ya kitaifa kwa kusudi la kusalimiana, kubadilishana mawazo, kufarijiana, kutiana moyo kujenga mahusiano, kufurahi na kisha kula pamoja, na unapokuwa umemualika kiongozi huyo mfalme au Rais aliyemualika mfalme mwingine anapaswa vilevile kuhakikisha kuwa anatoa na huduma zote ikiwemo ulinzi mkali na hata kama ana ulinzi wake, Kwa msingi hata kama ana maadui katika taifa lake au mataifa yanayomzunguka hawawezi kumgusa akiwemo katika himaya yako na itakuwa ni aibu kubwa sana kushindwa kuimarisha ulinzi wa mgeni wako huyu wa heshima endapo atauawa mbele yako, Dhifa hii kwa kawaida huonyesha kuwa umempa heshima ya juu sana mgeni wako! Na haya ni maswala muhimu katika mambo ya kidiplomasia.

Mwaka 1969 Mwenyekiti wa chama cha ukombozi wa Msumbiji Edward Mondlane aliuawa makao makuu ya chama cha FRELIMO yaliyokuwa jijini Dar es salaam baada ya kuletewa kikapu cha zawadi ya kitabu alichokuwa akikifungua kwenye nyumba ya rafiki yake wa kimarekani aliyeitwa Betty King, bomu lililipuka na kumuaa na mpaka leo haujajulikana aliuawa na nani ingawa inahisiwa ni wapinzani wa ukomonisti, hii inatufundisha kuwa mtu anaweza kuuawa hata mahali anakodhania kuwa ni salama!

Mungu aliwahi kuwapa heshima ya kidiplomasia na kuwaandalia meza wazee 74 wanaoheshimika sana katika Israel akiwemo Musa na haruni ingawa maandiko hayaelezei kwa kina ilikuwaje kuwaje ona lakini waliandaliwa meza mbinguni

Kutoka 24:9-11 “Ndipo akakwea juu, Musa, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.”

Hii ilikuwa ni neema kubwa na heshima ya juu zaidi kuwahi kutokea!, Daudi anaonyesha kuwa alikuwa ana uhusiano na Mungu wa karibu mno na anadhihirisha wazi kuwa neema ya Mungu ilikuwa juu yake kiasi cha kualikwa katika uwepo wa Mungu na kuandaliwa meza, huku Mungu akimlinda dhidi ya adui zake  na kumhakikishia usalama, huku akiendelea kuonyesha wema wake kwake, Daudi alikuwa mtu wa vita kwa hiyo alikuwa na maadui wengi sana, lakini kwa heshima hii aliyopewa na Mungu, hakuna adui anaweza kumgusa watamuona tu maana ameketi kwenye meza ya mwenye nguvu na hakuna mtu wa kumgusa kwa gharama yoyote.

Jambo hili pia vilevile licha ya kumhusu Daudi, lakini pia linaihusu Israel yote, nchi ya mkanaani haikuwa ya Israel kwa asili, lakini ilikuwa ni Mungu aliyemuahidi Ibrahimu kuwa atawapa, kwa msingi huo basi Israel wamealikwa katika nchi ya Mkanaani, Mwenyeji wao ni Mungu, Israel kule kaskazini inapakana na nchi ya Lebanon, na Syria, magharibi inapakana na Jordan na kusini iko Misri na eneo la wafilisti pale Palestina (Ukanda wa Gaza) kwa kawaida  wote tunafahamu namna na jinsi Israel inavyostawi na jinsi inavyokuwa na nguvu kubwa sana ya kijeshi, huku tukifahamu kuwa inazungukwa na adui pande zote na ambao wangetamani ifutwe mara moja, lakini wako salama kwa sababu wameandaliwa meza machoni pa watesi wao mwenyeji aliyewaalika ni Mungu.

Jambo hili vilevile linaweza likalihusu kanisa kwani kanisa limepewa kazi ngumu ya kuipeleka injili lakini kwa mfano wa kondoo na mbwa mwitu, aliyetualika kuihubiri injili alisema atakuwa pamoja nasi hata ukamilifu wa dahari. Haijalishi kuwa ni changamoto za aina gani tunapitia yeye mwenyewe anajua kuwa ametutuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu!.

Mathayo 10:16-20 “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.”

Hata hivyo pamoja na hatari zote zinazoweza kumzunguka mtu mmoja mmoja au Israel au kanisa au wewe kumbuka Zaburi hii ya 23 ina maana panasana katika maisha yako yenyewe inaaanza kwa kusema Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu, Na katika kuandaliwa meza kumbuka kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye aliyekualika na ni yeye ndiye aliyekuheshimisha kwa hiyo zaburi hii inataka tuwe na ujasiri uliopitiliza na kutokuogopa!.

Zaburi hii inamtia nguvu kila mmoja kujua ya kuwa Mungu yuko pamoja nasi, na kuwa hatutapungukiwa na kitu, na kuwa lazima tuwe na ujuzi kuwa Mungu yuko pamoja nasi na kuwa hatatupungukia wala hatatuacha, haijalishi tunapitia maswala gani magumu au laini hata yawe mazingira yenye kutishia amani yetu na usalama wetu, Mungu atajishughulisha na kutupatia mahitaji yetu huku akituhakikishia usalama wetu.

Wafilipi 4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.”

Mungu anapotuandalia meza kazi yetu ni kusubiri tu, hatupaswi kuwa na wasiwasi kama ilivyo kwa wageni wengine unatulia tu mwenyeji wako anajua unachohitaji na anaweza kukuuliza akuletee kinywaji gani, unapokuwa unaandaliwa meza haupambani ukae wapi, haupambani ule nini,   haupambanii usalama wako ni yeye aliyekualika anajua unayoyahitaji kwa msingi huo unapaswa kuwa na utulivu, huwezi kujiandalia mwenyewe  ni aibu umealikwa sebuleni kwa mtu kisha unaanza kufungua friji, unaingia jikoni, unaulizia matunda na kadhalika  Hapana haipaswi kuwa hivyo kwani yeye anayeandaa meza ataleta kila tunachiokihitaji, Israel walipokuwa wanaalikwa katika inchi ya kanaani mwenyeji wao aliwapa maji, aliwapa na mana wakala na aliwapa kware walipolilia.

Kutoka 16:14-16 “Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.”

Daudi kwa zaburi hii alikuwa anamuamini Mungu ana ujasiri katika Mungu anamjua Mungu kuwa hawezi kumuangusha yeye atatupa mahitaji yetu kwa kadiri ya neema ya uhitaji wetu maandiko yanaema katika  Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

Mungu ndiye mwenyeji amemkaribisha mgeni kwenye dhifa maana yake ni nini kila kitu kimekwisha kuandaliwa kwaajili yake, ni yeye ndiye aliyetupa mwaliko sisi sio wazamiaji, hivyo tunamtegemea yeye kwa mahitaji yetu yote ya kimwili na kiroho na muhimu zaidi atatulinda Mungu sio tu atatupatia kila tunachikihitaji katika ulimwengu huu lakini kama Mungu atakuwa pamoja nasi milele

2Petro 1:3 “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.”

Kwa msingi huo Zaburi ya 23:5 inapandisha chati ya mwamini ambaye amealikwa katika karamu ya mwana kondoo na katika uwepo wa Mungu uhakika wa wema na fadhili za Mungu kutufuata siku zote za maisha yetu na kukaa katika uwepo wake milele

 

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumanne, 14 Juni 2022

Kaburi liko wazi!

Luka 24:1-3 “Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi, Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu.”


Utangulizi: 

Moja ya mambo ambayo wanadamu wengi sana huyaogopa duniani ni pamoja na Kaburi, au eneo la makaburini, sehemu nyingi sana duniani na katika jamii nyingi duniani kumekuwepo na hofu ya aina Fulani ambapo watu huogopa sana kaburi au makaburini, lakini sio hivyo tu hata pamoja na kuweko kwa hofu ya kifo, bado watu wengi wanahofia tukio la kuzikwa wakifikiri ni moja ya tukio gumu, au wakidhani kuwa wanaweza kuzikwa wakiwa na fahamu zao, au wakifikiri itakuwaje kama itatangazwa kuwa nimekufa kwa bahati mbaya kisha nikashituka nikiwa kaburini hofu ya aina hii imekuwepo kwa miaka mingi, katika lugha ya kiyunani (Greek) hofu hii ya kisaikolojia kwa kiyunani inaitwa TAPHOPHOBIA  neno hilo ni neno la kiyunani lenye muunganiko wa maneno makuu mawili TAPHO – ambalo maana yake ni Kaburi (Grave) na PHOBIA – Maana yake hofu, kwa hiyo neno TAPHOPHOBIA maana yake ni hofu ya kaburi, kwa hiyo kimsingi watu wengi sana wanaogopa kifo lakini hata hivyo ni ukweli uliowazi kuwa watu wengi wanaogopa zaidi kaburi, kwa hiyo kuna hofu ya kifo na kuna hofu ya kaburi, au hofu ya kufikia mwisho!, sasa basi ni muhimu kufahamu kuwa kufufuka kwa Yesu, sio tu kunatusaidia kutokuogopa kifo lakini vilevile kunatusaidia kutokuogopa nguvu za kaburi au kuzimu! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·        
  
Kuzikwa kwa Yesu Kristo.

·         Umuhimu wa kaburi lililo wazi.

·         Kaburi liko wazi.

Kuzikwa kwa Yesu Kristo.! 

Mara kadhaa tumezungumzia sana kuhusu Mateso ya Bwana wetu Yesu, na huenda wahubiri wengi hawajawahi kuzungumzia kuhusu kuzikwa kwa Yesu Kristo, lakini ni muhimu sana kuuthibitishia ulimwengu kuwa Kristo alizikwa, kuzikwa kwa Yesu Kristo ni moja ya jambo, Muhimu sana katika injili kwa sababu Manabii waliliona  na kulitabiria pia kama walivyotabiria mambo mengine. 

Isaya 53:8-9 “Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.” 

Unaweza kuona Isaya nabii aliyeishi miaka 700 kabla ya Kristo, alitabiri kuhusu kuzikwa yaani kufanyiwa kaburi kwa Yesu Kristo, Hili ni jambo la msingi sana kama sehemu ya injili unapozungumzia mateso ya Kristo na hata kufufuka kwake basi tukio la kuzikwa ni la muhimu na ni sehemu ya injili ambayo hata Paulo Mtume alikabidhiwa ona 

1Wakorintho 15:1-4 “Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko;” 

Unaweza kuona kumbe unabii na injili vyote vinakazia swala zima la kuwa Yesu alizikwa, mtu akifa hilo ni jambo lingine na akizikwa hilo ni jambo lingine, Neno kuzikwa katika kiingereza linatumika neno “Burial” au “Interment” au “inhumation” ambalo maana yake ni hatua ya mwisho kabisa ya kuwepo duniani kwa kuuweka mwili wa Mwanadamu chini au kuuchoma (Cremation) au kuufungia na kuhitimisha huzuni au huruma kwa kumuweka mtu au mwili wake na kuufunika kabisa, kwa hiyo licha ya kufa ukizikwa maana yake umetoweka kabisa, kibinadamu imethibitika na kukubalika kuwa huwezi kuweko tena, Hivyo Yesu alizikwa maana yake ilithibitishwa kuwa hawezi kuweko tena kabisa duniani, lakini na pamoja na tendo hilo, serikali ya kirumi iliweka walinzi ili kuhakikisha kuwa pale alipozikwa hakuna kitu kinaweza kubatilika. Kimsingi jamii inapomzika mtu maana yake imekubali kuwa asiweko tena kabisa duniani! Sasa Yesu alizikwa lakini sio kuzikwa tu na ulinzi uliwekwa kuhakikisha kuwa amezikika. 

Mathayo 27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.” 

Asee sio tu kuwa mtu amekufa hapa lakini AMEZIKWA na hata maziko yake yanawekewa ulinzi kwa siku tatu, kuhakikisha kuwa hafufuki mtu, ndio maana katika nguvu ya injili hatuwezi kamwe kupuuzia swala la kuzikwa “ALITESWA, AKAFA AKAZIKWA…”  Wako watu katika maisha yako sio tu unapokuwa umesitawi inawapa shida sana, na watatamani uharibikiwe, upotee na ikiwezekana historia yako ifutike na usambaratike kabisa wanaweza hata kulinda hata taarifa zako zisisambae watakuchafua ikiwezekana usisimame milele hawa wanataka kukufuta “inhumation” “Cremation” kuhakikisha kuwa hauko tena hata tuta lako la kaburi lisiweko, ni kama kwa kaburi la Colonel Muammar Gadafi, au Osama Bin Laden wameuawa na makaburi yao yamefutika hawako kabisa, waliochukizwa nao hawakutaka hata wazikwe katika hali ya kawaida, wawe wamefutika hivyo ndivyo adui za Kristo Yesu walivyotaka iwe, kwa hiyo kuzikwa, kutoweka kusahaulika ni sehemu ya injili unaposema Yesu aliteswa, akafa usiseme tu akafufuka siku ya tatu kumbuka alizikwa! 

Umuhimu wa Kaburi lililo wazi. 

Kufufuka kwa Yesu Kristo ndio moja ya muujiza Mkubwa sana katika ukristo, kama Yesu hangelifufuka imani yetu ingekuwa ni imani potofu na ya hovyo kabisa kuliko zote, nisikilize ni kufufuka kwa Yesu Kristo pekee kunakotuthibitishia uwezo wa Mungu kwamba hatuwezi kukata tamaa katika jambo lolote lile, Kaburi lililo wazi ni ushahidi ulio wazi wa kutimizwa kwa unabii wa Mfalme Daudi ya Kwamba Mungu hatamuacha Mtakatifu wake aone uharibifu

Zaburi 16:10 “Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.”

Kaburi lililo wazi ni ishara iliyowazi ya ushindi unaobainisha kuwa Mungu anauwezo wa kufufua hata pale mtu anapofikia hatua ya kuzikwa, Yesu yuko hai nani wazi kuwa nguvu ileile iliyomfufua Yesu Kristo ina uwezo wa kufufua lolote katika maisha yetu ambalo linaonekana kama linataka kufa na hata kama limekufa machoni pa watu, Bado ana uwezo wa kulifufua.

Warumi 8:11 “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu” 

Nyakati za zamani sana alama ya wakristo ilikuwa sio msalaba ilikuwa ni kaburi lililowazi, kaburi lililo wazi ni ishara ya kuwa Yesu amefufuka na kuwa Mauti haimuwezi, ni ishara kwetu kuwa hakuna mtu anaweza kuifuta historia ya kuwepo kwa masihi, ni ushahidi kwetu kuwa Mungu wetu yu hai na ana nguvu, ni ishara kwetu kuwa hata kama watu watakukusudia ufutike hawataweza kukufuta wewe juu ya uso wa dunia, Kaburi lilowazi ni ushahidi kuwa yuko mwenye mamlaka mmoja tu mwenye ufunguo ambao akifunga hakuna afunguaye wala akifungua hakuna awezae kufunga mwenye mamlaka ya kufisha na kuhuuisha ni Yesu pekee! 

Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.” 
     

Kaburi liko wazi!

Msikilizaji wangu mpendwa nimepewa mamlaka ya kukutangazia ya kuwa kaburi liko wazi, tutaweza kupitia kila aina ya changamoto tuwapo duniani, kila aina ya mawimbi na mateso na matukano na dharau za watu, watu wanaweza kupanga mikakati ya kishetani katika kuhakikisha kuwa tunapotea na kutoweka na kuwa historia yetu inafagiliwa na kufutiliwa mbali na tunazikwa na kaburi zetu zinawekewa muhuri kuhakikisha ya kuwa hatuchomoki lakini nataka nikutangazie kuwa kaburi liko wazi, hakuna mahali ambako mkono wa Mungu hauwezi kufika na kukuchomoa, alimezwa Yona na nyangumi na nyangumi akamtapika, alimezwa Yesu na Kaburi na kaburi likamtapika, aliwekwa Danieli katika tundu la simba na makanwa ya simba yakazuibwa, walitupwa Daniel, Shadrak na Abednego na katika tanuri ya moto yaani kaburi la moto ili wafanyiwe “Cremation” lakini mauti ilishindikana nakutangazia kwa jina la Yesu Kristo hakuna mauti katika kazi yako, hakuna mauti katika masomo yako, hakuna mauti katika ndoa yako, hakuna mauti katika biashara yako, hakuna mauti katika sifa zako, hakuna mauti katika familia yako hakuna mauti kokote kule itakayokuweza! Ndio maana kaburi liko wazi, kaburi lililo wazi ndio kiini cha injili inayotuthibitishia kuwa Yesu yu hai, mtetezi wetu yu hai hajafa naye atasimama juu ya nchi apate kututetea, kila mauti inayokusudiwa, katika kila sehemu ya maisha yako naitangazia kuwa Kaburi liko wazi, mwambie shetani kaburi liko wazi, mwambie adui yako kaburi liko wazi, kaburi lililo wazi ni ishara ya kuwa kuna maitumaini kila wakati na kuwa Mungu hatatuacha tuone uharibifu wa namna yoyote! Na badala yake tutawaona adui zetu wakitoweka kwa haraka.!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!