Zaburi 23:1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina
lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa
maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza
mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe
changu kinafurika. Hakika wema na
fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana
milele.”
Utangulizi:
Moja ya zaburi maarufu zaidi
duniani labda kuliko zaburi zote ni zaburi ya 23, Zaburi hii imetumiwa sana na
Wayahudi na Wakristo katika ibada na maombi lakini vilevile kwaajili ya kujenga
imani, Kiini kikuu cha zaburi hii ni yale maneno Bwana ndiye Mchungaji wangu maneno haya yanazigusa jamii nyingi
sana Duniani, Hata huko Mesopotamia, Inasemekana kuwa Mfalme Hammurabi katika
mojawapo ya hutuba yake muhimu sana aliyowahi kuitoa alihitimisha kwa kusema “Mimi ndiye Mchungaji ninayehakikisha
usalama na mafanikio ya watu wangu, utawala wangu utakuwa wa haki, wenye nguvu
hawatawaonea wanyonge, na hata yatima na wajane watatendewa kwa haki”
maneno ya kiongozi huyu wa zamani sana yalikuwa maarufu na huenda yakawa
yalichangia mtunzi wa Zaburi hii kuyachanganua kwa kina katika uimbaji wake kwa
kusudi la kutambua uhusiano wake na Mungu.
Zaburi hii ina mistari michache
sana lakini yenye kubeba maana pana sana na hatuwezi kwa somo moja kama hivi
kugusia kila neno linalozungumziwa na zaburi hii, Hata hivyo leo Mwalimu mkuu
Roho Mtakatifu anatupeleka kuutazama mstari wa tano (5) katika zaburi hii ya (23)
ili tuweze kujifunza kile ambacho Mungu amekikusudia kwetu .
Katika Zaburi 23:5 Daudi anasema “WAANDAA MEZA
MBELE YANGU, MACHONI PA WATESI WANGU” maneno haya peke yake
yanaashiria uhusiano mkubwa sana na wa karibu ulioko kati yake na Mungu, lakini
sio hivyo tu mstari huu unafunua heshima kubwa sana ya kifalme ambayo mwandishi
anapewa na Mungu, kwani kumbuka kuwa anayeandaa meza hapa sio Daudi bali Mungu
anamuandalia Daudi meza hivyo kimsingi mahali hapa pana maana pana na kubwa
sana ambayo inaweza kumfaa kila mmoja wetu leo!
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
taratibu za kifalme, unapomualika mtu ambaye unamuheshimu sana katika utawala
wako basi mgeni huyo rasmi labda ni rais au mfalme wa taifa lingine kama
alikuja aidha kwa mazungumzo au kwa mualiko wa serikali yako au ziara ya
kuimarisha uhusiano basi inapofika jioni kiongozi huyo mualikwa huandaliwa
chakula maalumu ambacho huitwa dhifa ya kitaifa kwa kusudi la kusalimiana,
kubadilishana mawazo, kufarijiana, kutiana moyo kujenga mahusiano, kufurahi na
kisha kula pamoja, na unapokuwa umemualika kiongozi huyo mfalme au Rais
aliyemualika mfalme mwingine anapaswa vilevile kuhakikisha kuwa anatoa na
huduma zote ikiwemo ulinzi mkali na hata kama ana ulinzi wake, Kwa msingi hata
kama ana maadui katika taifa lake au mataifa yanayomzunguka hawawezi kumgusa
akiwemo katika himaya yako na itakuwa ni aibu kubwa sana kushindwa kuimarisha
ulinzi wa mgeni wako huyu wa heshima endapo atauawa mbele yako, Dhifa hii kwa
kawaida huonyesha kuwa umempa heshima ya juu sana mgeni wako! Na haya ni
maswala muhimu katika mambo ya kidiplomasia.
Mwaka 1969 Mwenyekiti wa chama
cha ukombozi wa Msumbiji Edward Mondlane aliuawa makao makuu ya chama cha
FRELIMO yaliyokuwa jijini Dar es salaam baada ya kuletewa kikapu cha zawadi ya kitabu
alichokuwa akikifungua kwenye nyumba ya rafiki yake wa kimarekani aliyeitwa
Betty King, bomu lililipuka na kumuaa na mpaka leo haujajulikana aliuawa na
nani ingawa inahisiwa ni wapinzani wa ukomonisti, hii inatufundisha kuwa mtu
anaweza kuuawa hata mahali anakodhania kuwa ni salama!
Mungu aliwahi kuwapa heshima ya
kidiplomasia na kuwaandalia meza wazee 74 wanaoheshimika sana katika Israel akiwemo
Musa na haruni ingawa maandiko hayaelezei kwa kina ilikuwaje kuwaje ona lakini
waliandaliwa meza mbinguni
Kutoka 24:9-11 “Ndipo akakwea juu, Musa, na
Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli;
wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu
iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye
hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu,
wakala na kunywa.”
Hii ilikuwa ni neema kubwa na
heshima ya juu zaidi kuwahi kutokea!, Daudi anaonyesha kuwa alikuwa ana
uhusiano na Mungu wa karibu mno na anadhihirisha wazi kuwa neema ya Mungu
ilikuwa juu yake kiasi cha kualikwa katika uwepo wa Mungu na kuandaliwa meza,
huku Mungu akimlinda dhidi ya adui zake na kumhakikishia usalama, huku akiendelea
kuonyesha wema wake kwake, Daudi alikuwa mtu wa vita kwa hiyo alikuwa na maadui
wengi sana, lakini kwa heshima hii aliyopewa na Mungu, hakuna adui anaweza
kumgusa watamuona tu maana ameketi kwenye meza ya mwenye nguvu na hakuna mtu wa
kumgusa kwa gharama yoyote.
Jambo hili pia vilevile licha ya
kumhusu Daudi, lakini pia linaihusu Israel yote, nchi ya mkanaani haikuwa ya
Israel kwa asili, lakini ilikuwa ni Mungu aliyemuahidi Ibrahimu kuwa atawapa,
kwa msingi huo basi Israel wamealikwa katika nchi ya Mkanaani, Mwenyeji wao ni
Mungu, Israel kule kaskazini inapakana na nchi ya Lebanon, na Syria, magharibi
inapakana na Jordan na kusini iko Misri na eneo la wafilisti pale Palestina (Ukanda
wa Gaza) kwa kawaida wote tunafahamu
namna na jinsi Israel inavyostawi na jinsi inavyokuwa na nguvu kubwa sana ya
kijeshi, huku tukifahamu kuwa inazungukwa na adui pande zote na ambao
wangetamani ifutwe mara moja, lakini wako salama kwa sababu wameandaliwa meza
machoni pa watesi wao mwenyeji aliyewaalika ni Mungu.
Jambo hili vilevile linaweza
likalihusu kanisa kwani kanisa limepewa kazi ngumu ya kuipeleka injili lakini
kwa mfano wa kondoo na mbwa mwitu, aliyetualika kuihubiri injili alisema
atakuwa pamoja nasi hata ukamilifu wa dahari. Haijalishi kuwa ni changamoto za
aina gani tunapitia yeye mwenyewe anajua kuwa ametutuma kama kondoo katikati ya
mbwa mwitu!.
Mathayo 10:16-20 “Angalieni, mimi nawatuma
kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu
wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na
katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na
wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo
watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile
mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani
yenu.”
Hata hivyo pamoja na hatari zote
zinazoweza kumzunguka mtu mmoja mmoja au Israel au kanisa au wewe kumbuka
Zaburi hii ya 23 ina maana panasana katika maisha yako yenyewe inaaanza kwa
kusema Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu, Na katika kuandaliwa
meza kumbuka kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye aliyekualika na ni yeye ndiye
aliyekuheshimisha kwa hiyo zaburi hii inataka tuwe na ujasiri uliopitiliza na
kutokuogopa!.
Zaburi hii inamtia nguvu kila
mmoja kujua ya kuwa Mungu yuko pamoja nasi, na kuwa hatutapungukiwa na kitu, na
kuwa lazima tuwe na ujuzi kuwa Mungu yuko pamoja nasi na kuwa hatatupungukia
wala hatatuacha, haijalishi tunapitia maswala gani magumu au laini hata yawe
mazingira yenye kutishia amani yetu na usalama wetu, Mungu atajishughulisha na
kutupatia mahitaji yetu huku akituhakikishia usalama wetu.
Wafilipi 4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni
kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo
Yesu.”
Mungu anapotuandalia meza kazi
yetu ni kusubiri tu, hatupaswi kuwa na wasiwasi kama ilivyo kwa wageni wengine
unatulia tu mwenyeji wako anajua unachohitaji na anaweza kukuuliza akuletee
kinywaji gani, unapokuwa unaandaliwa meza haupambani ukae wapi, haupambani ule
nini, haupambanii usalama wako ni yeye
aliyekualika anajua unayoyahitaji kwa msingi huo unapaswa kuwa na utulivu,
huwezi kujiandalia mwenyewe ni aibu
umealikwa sebuleni kwa mtu kisha unaanza kufungua friji, unaingia jikoni,
unaulizia matunda na kadhalika Hapana
haipaswi kuwa hivyo kwani yeye anayeandaa meza ataleta kila tunachiokihitaji,
Israel walipokuwa wanaalikwa katika inchi ya kanaani mwenyeji wao aliwapa maji,
aliwapa na mana wakala na aliwapa kware walipolilia.
Kutoka 16:14-16 “Na ulipoinuka ule umande
uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana,
kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini
hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA
amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho
kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo;
ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.”
Daudi kwa zaburi hii alikuwa
anamuamini Mungu ana ujasiri katika Mungu anamjua Mungu kuwa hawezi kumuangusha
yeye atatupa mahitaji yetu kwa kadiri ya neema ya uhitaji wetu maandiko yanaema
katika Waebrania 4:16 “Basi
na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema
ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”
Mungu ndiye mwenyeji
amemkaribisha mgeni kwenye dhifa maana yake ni nini kila kitu kimekwisha
kuandaliwa kwaajili yake, ni yeye ndiye aliyetupa mwaliko sisi sio wazamiaji,
hivyo tunamtegemea yeye kwa mahitaji yetu yote ya kimwili na kiroho na muhimu
zaidi atatulinda Mungu sio tu atatupatia kila tunachikihitaji katika ulimwengu
huu lakini kama Mungu atakuwa pamoja nasi milele
2Petro 1:3 “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu
umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita
kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.”
Kwa msingi huo Zaburi ya 23:5 inapandisha chati ya
mwamini ambaye amealikwa katika karamu ya mwana kondoo na katika uwepo wa Mungu
uhakika wa wema na fadhili za Mungu kutufuata siku zote za maisha yetu na kukaa
katika uwepo wake milele
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni