Luka 24:1-3 “Hata siku ya kwanza ya juma,
ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka
tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi, Wakaingia,
wasiuone mwili wa Bwana Yesu.”
Utangulizi:
Moja ya mambo ambayo wanadamu
wengi sana huyaogopa duniani ni pamoja na Kaburi, au eneo la makaburini, sehemu
nyingi sana duniani na katika jamii nyingi duniani kumekuwepo na hofu ya aina
Fulani ambapo watu huogopa sana kaburi au makaburini, lakini sio hivyo tu hata
pamoja na kuweko kwa hofu ya kifo, bado watu wengi wanahofia tukio la kuzikwa
wakifikiri ni moja ya tukio gumu, au wakidhani kuwa wanaweza kuzikwa wakiwa na
fahamu zao, au wakifikiri itakuwaje kama itatangazwa kuwa nimekufa kwa bahati
mbaya kisha nikashituka nikiwa kaburini hofu ya aina hii imekuwepo kwa miaka
mingi, katika lugha ya kiyunani (Greek)
hofu hii ya kisaikolojia kwa kiyunani inaitwa TAPHOPHOBIA neno hilo ni
neno la kiyunani lenye muunganiko wa maneno makuu mawili TAPHO – ambalo maana yake ni Kaburi (Grave) na PHOBIA – Maana
yake hofu, kwa hiyo neno TAPHOPHOBIA
maana yake ni hofu ya kaburi, kwa hiyo kimsingi watu wengi sana wanaogopa kifo
lakini hata hivyo ni ukweli uliowazi kuwa watu wengi wanaogopa zaidi kaburi,
kwa hiyo kuna hofu ya kifo na kuna hofu ya kaburi, au hofu ya kufikia mwisho!,
sasa basi ni muhimu kufahamu kuwa kufufuka kwa Yesu, sio tu kunatusaidia
kutokuogopa kifo lakini vilevile kunatusaidia kutokuogopa nguvu za kaburi au
kuzimu! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Kuzikwa kwa Yesu Kristo.
·
Umuhimu wa kaburi lililo wazi.
·
Kaburi liko wazi.
Kuzikwa kwa Yesu Kristo.!
Mara kadhaa tumezungumzia sana
kuhusu Mateso ya Bwana wetu Yesu, na huenda wahubiri wengi hawajawahi
kuzungumzia kuhusu kuzikwa kwa Yesu Kristo, lakini ni muhimu sana
kuuthibitishia ulimwengu kuwa Kristo alizikwa, kuzikwa kwa Yesu Kristo ni moja
ya jambo, Muhimu sana katika injili kwa sababu Manabii waliliona na kulitabiria pia kama walivyotabiria mambo
mengine.
Isaya 53:8-9 “Kwa kuonewa na kuhukumiwa
aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na
nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia
kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda
jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.”
Unaweza kuona Isaya nabii
aliyeishi miaka 700 kabla ya Kristo, alitabiri kuhusu kuzikwa yaani kufanyiwa
kaburi kwa Yesu Kristo, Hili ni jambo la msingi sana kama sehemu ya injili unapozungumzia
mateso ya Kristo na hata kufufuka kwake basi tukio la kuzikwa ni la muhimu na ni
sehemu ya injili ambayo hata Paulo Mtume alikabidhiwa ona
1Wakorintho 15:1-4 “Basi, ndugu zangu,
nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo
mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri
isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale
niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu,
kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya
tatu, kama yanenavyo maandiko;”
Unaweza kuona kumbe unabii na
injili vyote vinakazia swala zima la kuwa Yesu alizikwa, mtu akifa hilo ni
jambo lingine na akizikwa hilo ni jambo lingine, Neno kuzikwa katika kiingereza
linatumika neno “Burial” au “Interment” au “inhumation” ambalo maana yake ni hatua ya mwisho kabisa ya kuwepo
duniani kwa kuuweka mwili wa Mwanadamu chini au kuuchoma (Cremation) au kuufungia na kuhitimisha huzuni au huruma kwa
kumuweka mtu au mwili wake na kuufunika kabisa, kwa hiyo licha ya kufa ukizikwa
maana yake umetoweka kabisa, kibinadamu imethibitika na kukubalika kuwa huwezi
kuweko tena, Hivyo Yesu alizikwa maana yake ilithibitishwa kuwa hawezi kuweko
tena kabisa duniani, lakini na pamoja na tendo hilo, serikali ya kirumi iliweka
walinzi ili kuhakikisha kuwa pale alipozikwa hakuna kitu kinaweza kubatilika.
Kimsingi jamii inapomzika mtu maana yake imekubali kuwa asiweko tena kabisa
duniani! Sasa Yesu alizikwa lakini sio kuzikwa tu na ulinzi uliwekwa
kuhakikisha kuwa amezikika.
Mathayo 27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo
iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia
Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa
akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe
salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu,
Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato
akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda,
wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari
walinzi.”
Asee sio tu kuwa mtu amekufa hapa
lakini AMEZIKWA na hata maziko yake
yanawekewa ulinzi kwa siku tatu, kuhakikisha kuwa hafufuki mtu, ndio maana
katika nguvu ya injili hatuwezi kamwe kupuuzia swala la kuzikwa “ALITESWA, AKAFA AKAZIKWA…” Wako watu katika maisha yako sio tu
unapokuwa umesitawi inawapa shida sana, na watatamani uharibikiwe, upotee na
ikiwezekana historia yako ifutike na usambaratike kabisa wanaweza hata kulinda
hata taarifa zako zisisambae watakuchafua ikiwezekana usisimame milele hawa
wanataka kukufuta “inhumation” “Cremation”
kuhakikisha kuwa hauko tena hata tuta lako la kaburi lisiweko, ni kama kwa
kaburi la Colonel Muammar Gadafi, au
Osama Bin Laden wameuawa na makaburi yao yamefutika hawako kabisa,
waliochukizwa nao hawakutaka hata wazikwe katika hali ya kawaida, wawe
wamefutika hivyo ndivyo adui za Kristo Yesu walivyotaka iwe, kwa hiyo kuzikwa,
kutoweka kusahaulika ni sehemu ya injili unaposema Yesu aliteswa, akafa usiseme
tu akafufuka siku ya tatu kumbuka alizikwa!
Umuhimu wa Kaburi lililo wazi.
Kufufuka kwa Yesu Kristo ndio
moja ya muujiza Mkubwa sana katika ukristo, kama Yesu hangelifufuka imani yetu
ingekuwa ni imani potofu na ya hovyo kabisa kuliko zote, nisikilize ni kufufuka
kwa Yesu Kristo pekee kunakotuthibitishia uwezo wa Mungu kwamba hatuwezi kukata
tamaa katika jambo lolote lile, Kaburi lililo wazi ni ushahidi ulio wazi wa
kutimizwa kwa unabii wa Mfalme Daudi ya Kwamba Mungu hatamuacha Mtakatifu wake
aone uharibifu
Zaburi 16:10 “Maana hutakuachia kuzimu
nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.”
Kaburi lililo wazi ni ishara
iliyowazi ya ushindi unaobainisha kuwa Mungu anauwezo wa kufufua hata pale mtu
anapofikia hatua ya kuzikwa, Yesu yuko hai nani wazi kuwa nguvu ileile
iliyomfufua Yesu Kristo ina uwezo wa kufufua lolote katika maisha yetu ambalo
linaonekana kama linataka kufa na hata kama limekufa machoni pa watu, Bado ana
uwezo wa kulifufua.
Warumi 8:11 “Lakini, ikiwa Roho yake yeye
aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu
katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake
anayekaa ndani yenu”
Nyakati za zamani sana alama ya
wakristo ilikuwa sio msalaba ilikuwa ni kaburi lililowazi, kaburi lililo wazi
ni ishara ya kuwa Yesu amefufuka na kuwa Mauti haimuwezi, ni ishara kwetu kuwa
hakuna mtu anaweza kuifuta historia ya kuwepo kwa masihi, ni ushahidi kwetu
kuwa Mungu wetu yu hai na ana nguvu, ni ishara kwetu kuwa hata kama watu
watakukusudia ufutike hawataweza kukufuta wewe juu ya uso wa dunia, Kaburi
lilowazi ni ushahidi kuwa yuko mwenye mamlaka mmoja tu mwenye ufunguo ambao
akifunga hakuna afunguaye wala akifungua hakuna awezae kufunga mwenye mamlaka ya kufisha na kuhuuisha
ni Yesu pekee!
Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona,
nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu
yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami
nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo
za mauti, na za kuzimu.”
Kaburi liko wazi!
Msikilizaji wangu mpendwa
nimepewa mamlaka ya kukutangazia ya kuwa kaburi liko wazi, tutaweza kupitia
kila aina ya changamoto tuwapo duniani, kila aina ya mawimbi na mateso na
matukano na dharau za watu, watu wanaweza kupanga mikakati ya kishetani katika kuhakikisha
kuwa tunapotea na kutoweka na kuwa historia yetu inafagiliwa na kufutiliwa mbali
na tunazikwa na kaburi zetu zinawekewa muhuri kuhakikisha ya kuwa hatuchomoki
lakini nataka nikutangazie kuwa kaburi liko wazi, hakuna mahali ambako mkono wa
Mungu hauwezi kufika na kukuchomoa, alimezwa Yona na nyangumi na nyangumi
akamtapika, alimezwa Yesu na Kaburi na kaburi likamtapika, aliwekwa Danieli
katika tundu la simba na makanwa ya simba yakazuibwa, walitupwa Daniel, Shadrak
na Abednego na katika tanuri ya moto yaani kaburi la moto ili wafanyiwe “Cremation” lakini mauti ilishindikana
nakutangazia kwa jina la Yesu Kristo hakuna mauti katika kazi yako, hakuna
mauti katika masomo yako, hakuna mauti katika ndoa yako, hakuna mauti katika
biashara yako, hakuna mauti katika sifa zako, hakuna mauti katika familia yako
hakuna mauti kokote kule itakayokuweza! Ndio maana kaburi liko wazi, kaburi
lililo wazi ndio kiini cha injili inayotuthibitishia kuwa Yesu yu hai, mtetezi
wetu yu hai hajafa naye atasimama juu ya nchi apate kututetea, kila mauti inayokusudiwa,
katika kila sehemu ya maisha yako naitangazia kuwa Kaburi liko wazi, mwambie
shetani kaburi liko wazi, mwambie adui yako kaburi liko wazi, kaburi lililo
wazi ni ishara ya kuwa kuna maitumaini kila wakati na kuwa Mungu hatatuacha
tuone uharibifu wa namna yoyote! Na badala yake tutawaona adui zetu wakitoweka
kwa haraka.!
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni