Jumatatu, 27 Februari 2023

Kufanyiwa nafasi wakati wa shida!



Zaburi 4:1-3 “Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu. Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo? Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo.”


Utangulizi:

Leo tutachukua Muda kujifunza kwa undani kuhusiana na kifungu hiki cha Zaburi 4:1-3, lakini hususani zaidi maneno Umenifanyizia nafasi wakati wa shida!  Maneno haya ni ya Muhimu sana kwetu kama yalivyokuwa ya muhimu sana wakati wa Mfalme Daudi mwana wa Yese Mbethelehemu alipokuwa akiandika maneno hayo!,  Wanatheolojia wengi sana wanafikiri kuwa huenda zaburi hii iliandikwa wakati wa mgogoro kati ya Daudi na mwanae Absalom, Lakini mimi nadhani kuwa Zaburi hii iliandikwa wakati Daudi alipokoswa koswa kuuawa na Mfalme Sauli kwa kutaka kupigwa mkuki mara kadhaa, hii ni kwa sababu Zaburi hii ni ya mapema zaidi kabla ya mgogoro wa Daudi na kijana wake Kipenzi Absalom! Hata hivyo kabla ya kuangalia kwa undani kifungu hiki ni muhimu kwetu kuligawa somo hili katika vipendele vitatu vifuatavyo:- 


·         Maana ya neno Nafasi

·         Maana ya kufanyiwa nafasi wakati wa shida

·         Kufanyiwa nafasi wakati wa shida 


Maana ya Neno nafasi

Neno nafasi linalotumika hapa lina maana pana sana inayohusiana na swala la kuokolewa katika mazingira magumu, tafasiri nyingi za kimaandiko zimetumika kulielezea neno hili katika maneno ya namna mbalimbali, mfano  King James Version imetumia neno “..Thou hast ENLARGED me when I was in distress” Biblia ya kiingereza ya English Standard Version imetumia neno “…You have given me RELIEF when I was in distress, New Language translation imetumia neno “…Oh God who DECLARE ME INNOCENT, FREE ME from my Troubles”  nyingine ijulikanayo kwa kifupi kama MSG imeandika namna hii “ …God take my side in a tight place” na nyingine imesema “…Free me from affliction  unaona unaposoma matoleo tofauti tofauti ya Biblia mbalimbali inatusaidia kupata maana halisi iliyokusudiwa kwa sababu neno NAFASI lililotumika kwenye Kiswahili linaweza kutunyima uwanja mpana wa kuelewa lile lililokusudiwa lakini kama unajua kiingereza kwa mbali sasa unatkuwa umeanza kufahamu kuwa Daudi alifanyiwa na Mungu tukio kubwa sana la WOKOVU,  Mungu ALIMKUZA baada ya kupitia shida, Mungu alimpa AHUENI baada ya kupitia shida, Mungu alimpa NAFUU baada ya kupitia dhiki, Mungu alimuhesabia HAKI, au KUWA HANA HATIA na kumuweka huru kutoka katika taabu,  unaona neno hilihilo ndilo alilolitumia Isaka alipokuwa akisumbuliwa na Wafilisti kuhusu visima vya baba yake kila alipochimba kisima walipata mgogoro na akwaachia, akachimba kingine wakaleta mgogoro akawaachia hatimaye pale walipoacha kumsumbua ndio akasema Bwana ametupa Nafasi, ahueni,  ona  


Mwanzo 26:18-25 “Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.  Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko  


unaona Isaka alipata changamoto kutoka kwa maadui zake hakupata nafuu, hakupata auhueni hakupata hata nafasi ya kumuabudu Mungu kwa kumjenge madhabahu maana maisha hayakuwa na utulivu kwa sababu alichukiwa kwa sababu alionewa wivu kwa sababu alifukuzwa kwa sababu waligombana sana sasa anapata kisima ambacho hakikugombewa na hapa anapaita REHOBOTH asili ya neno Nafasi katika lugha ya kiibrania  linakotokea neno REHOBOTH ni “RACHAB” kwa matamshi ni RAW-KHAB  au aliyeshinda changamoto kwa kiarabu RAQEEB.  Kila mwanadamu anahitaji utulivu, anahitaji nafasi, anahitaji usalama anahitaji kushinda changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo katikka maisha watu wanaweza kukuchukia pasipo sababu, unaweza kuandamwa hata na watu wenye nguvu sana, matajiri kuliko wewe, wenye mali kuliko wewe unaweza kuhisi uonevu kila mahali, unaweza kuionewa na kutafutwa na adui zako, magonjwa mateso, dhuluma bna changamoto za aina mbalimbali na unahitaji ufikie nafasi ambayo Mungu atakupa ahueni, atakupa nafasi, atakuondolea mashaka atakupa kuponyoka katika mikono ya adui hii ndio nafasi kwa ujumla inazungumzia wokovu katika kifurushi chake kamili tunahitaji nafasi! 

Maana ya kufanyiwa nafasi katika shida! 

Zaburi 4:1-3 “Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu. Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo? Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo.” 

Baada ya uchambuzi wa kina hapo juu kuhusu kufanyiwa nafasi, nadhani sasa unaweza kuelewa vema zaburi hii kuwa mtumishi wa Mungu Daudi alikuwa anapitia changamoto ya aina gani, narudia tena kusema wazi kuwa changamotio yake haikuwa wakati wa Absalom bali ni wazi kabisa ukiangalia maana ya chimbuko la Neno nafasi Daudi anayodai kufanyiwa na bwana ni wazi kuwa Daudi hapa anakumbuka nanma alivyoponyoka katika mikono ya Sauli, wakati wa vita na Absalom Daudi alikuwa ni Mfalme hivyo tayari alikuwa ana nafasi, alikuwa na majemadari wajuzi wa vita na wapelelezi wa kutosha pamoja na kuwa moyo wake ulibaki ukimtegema Mungu, Lakini wakati huu alikuwa mpiga kinubi tu, alikuwa masikini bado alikuwa akijifunza maswala ya utawala alikuwa mnyonge na eti mfalme anataka kumuua kwa kumpiga mkuki maandiko yanatuonyesha kuwa sio mara moja wala sio mara mbili na katika matukio yote hayo Mungu aliingilia kati 

1Samuel 18:9-14 “Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake.  Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye Bwana alikuwa pamoja naye.” 

1Samuel 19: 10-12 “Sauli akajaribu kumpiga Daudi hata ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule. Kisha Sauli akatuma wajumbe mpaka nyumbani kwa Daudi, ili wamvizie na kumwua asubuhi; naye Mikali, mkewe Daudi, akamwambia, akasema, Wewe usipojiponya nafsi yako usiku huu, kesho utauawa. Basi Mikali akamtelemsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka.” 

Ni ukweli ulio wazi kabisa kuwa ukiangalia asili ya kuchomoka kwa Daudi katika mikono ya Sauli ilifanywa na Mungu mwenyewe haikuwa akili ya Daudi,  ni mpaka Adui wa daudi walitambua ya kuwa Mungu yuko Pamoja naye, unajua kuna wakati watu wanaweza kukutafuta waklufanyie mabaya wanaweza kukusudia  mabaya dhidi yako, lakini kila wanapopanga mbinu zao na mikakati yao wanakuja kugundua kuwa unateleza kama samaki mbichi Mungu anakulinda na kukuepusha na kila kitu kibaya mpaka wanagundua ya kuwa Mungu yu Pamoja nawe!, umeona Adui wa Isaka walimfuata eee mwisho waalipogundua kuwa kila wakimdhulumu Bwana anamfanyia nafasi wakagundua kuwa Bwana yuko pamoja naye , na sauli vilevile alimuogopa Daudi kwa sababu alijua kuwa Bwana yuko pamoja naye 

Mwanzo 26: 26-30 “Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe  ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA.  Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa.” 

Unaona Mungu anapokufanyia nafasi anakupoa utulivu, anakubariki, anakupa amani, anakupatanisha na adui zako, anakupa kibali lakini ili nafasi iweze kupatikana ni lazima shida ziwepo, hatupendi kupita katika shida na mateso ya aina mbalimbali lakini Mungu huwa anaziruhusu kwa makusudi na mapenzi yake mema ili ziweze kutuinua na kuzalisha kitu kingine cha ziada katika maisha yetu 

Kufanyiwa nafasi wakati wa shida 

Ni muhimu kuwa na ufahamu wa kutosha kuwa kila changamoto unayoipitia haimaanishi kuwa Munghu hajajibu maombi yako, haimaanishi kuwa Mungu anakuhukumu kwa sababu umefanya dhambi, haimaanishi kuwa Munu hakujali lakini vyovyote ilivyo Mungu ndiye haki yetu, Na amemfanya Yesu Kristo kuwa haki yetu sisi hatuna haki yetu wenyewe, Lakini sio hivyo tu yeye ndiye Mwokozi nan i yeye ndiye mwenye haki ya kutuhukumu na sio mtu mwingine, unaweza kuwa unapitia changamoto, za aina mbalimbali na ukadhani kuwa umerogwa au Mungu amechukizwa naye au hayuko pamoja nawe inaweza kuwa una taabu kubwa sana zinakusonga adui mkubwa mara tatu zaidi yako, unatafutwa kuuawa, unajiona una nuksi, unajina una balaa, unajiona hufanikiwi unajiona umechelewa unaweza kuchoka na kujiuliza nini kinanitokea katika maisha yangu wengine wanaweza kudhani labda wameoa mwanamke mwenye mikosi au mwameolewa na abila lenye mikosi au balaa na unaweza kujiuliza maswala nini kinaendelea katika maisha yangu lakini dhiki zetu ni nafasi ni opportunity, Mungu anatupa  Nafasi itakayotupeleka katika ngazi nyingine na kutuinua, kutupa ahueni, kutupa nafuu, kutupa tahafifu, kutuponya kutuweka huru, kututangaza kuwa hatuna hatia kutupa raqeeb kutuweka panapo nafasi 

1Wakoritho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” 

Daudi alivumilia na kuliitia jina la Bwana katika dua zake na hatimaye Mungu alimpa upenyo, Leo nakutangazia na ninakutabiaria na ninatamka na kuzushuhudia mbingu na ardhi na kuziap[iza kwa jina la Yesu Kristo ya kwamba changamoto zako unazozipitia na shida unazipitia zikuletee mafanikio, zikuleteee amani na furaha, zikuletee Baraka, zikuletee tumaini, zikuletee nafuu, zikuleteee kibali, zikuletee ahueni, zikuletee uponyaji, zimletee Mungu utukufu, zikuletee kutoboa zikupatanishe na adui zako kumbuka kila wakati upitiapo shida kuna nafasi nasema kuna nafasi na Mungu ni mwaminifu! Utachanua katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: