Jumatatu, 27 Februari 2023

Kunyamaza mbele ya wakata Manyoya!


Isaya 53:7-11 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.  Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.  Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.”



Utangulizi;

Leo nataka kuzungumzia moja ya siri kubwa sana ya mafanikio yetu katika maisha ya kila siku na katika maisha yetu ya utumishi, katika uzoefu wangu wa maisha tangu utoto na nadhani hata kwa watoto wengine na mpaka tunakuwa huwa tumejengwa katika dhana ya kujifunza kujitetea  na kutokukubali kukaa kimya au kuonewa na mara nyingi sana watu huwa wanaweza kukuchochea usikubali kukaa kimya hasa unapoonewa na jamii inaweza kukuona wewe ni mjinga sana kama ulikuwa na uwezo wa kujitetea lakini wewe ukaamua kukaa kimya au kupoteza haki zako ni kama unaonekana wewe ni dhaifu, kwa hiyo mara kwa mara tunajifunza kujenga hioja za kujitetea lakini maandiko yanatufunza kanuni nyingine ya kipekee sana yenye nguvu mno katika maisha yetu na kanuni hii ni kutulia na kukaa kimya, hii ndio Kanuni iliyotumiwa na Mtu mkubwa zaidi aliyepata kuishi Yesu Kristo Mwana wa Mungu kama anavyoeleza Isaya wakati akiwa anaonewa yeye alitulia kama kondoo anavyoweza kutulia kwa wakatao manyoya ona

Isaya 53:7 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.“

Ufahamu kuhusu tendo la kukata manyoya

Kwa bahati mbaya sana Hapa kwetu Tanzania, hatuna jamii ya kondoo wa kukatwa manyoya, lakini katika nchi nyingi jamii ya kondoo wenye manyoa mengi wamekuwepo tangia miaka mingi sana ikiwemo katika Israel, na ndio maana Isaya aliyeishi miaka 700 kabla ya Kristo anaeleza jambo hili.

Kwa kawaida Kondoo wenye manyoya walikuwepo tangu zamani na miaka ya zamani sana swala la kukata manyoya lilikuwa ni swala la asili tu kondoo wenyewe wangeweza kujikwaruza kwenye miti na kuondoa uchafu na kujipunguza manyoya, lakini Manyoya ya kondoo yalipoanza kutumika kama bidhaa ya kutengeneza nguo, na shughuli nyingine wanadamu waliona wapandikize jamii ya kondoo watakaozalisha manyioya kwa wingi ili kupata faida na ndio kukawepo kondoo wenye manyoa maengi zaidi, kwa msingi huo manyoya haya yana faida kubwa sana kwa kondoo mwenyewe wakati wa baridi kuweza kukabiliana na hali joto la nchi manyoya huwasaidia kuwa salama wakati wa baridi na mara msimu wa baridi unapoisha, na kuanza msimu wa joto wakulima huwa na sherehe za kuwakata kndoo manyoya na kuvuna pamba nyingi inayotokana na kondoo, mwenye kondoo hupata faida lakini vilevile kondoo wanafaidika kuwa na afya nzuri na kujilinda na wadudu wanaoweza kusababisha magonjwa wakati wa joto, na hivyo kondoo hunyolewa kila mwaka mara moja angalau kwaajili ya haya , wakulima hufanya sherehe kubwa kama vile wamevuna mazao

1Samuel 25: 2-8 “Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu. Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi.”

Unaona ? kwa msingi huo ukataji kondoo manyoya lilikuwa ni tukio lililoeleweka vema sana katika jamii ya waisrael kuliko kwetu Afrika ya mashariki na  maeneo mengine duniani, na kwa bahati njema kwa vile kondoo walizoea zoezi hili na kama wanyama wenyewe walivyo wapole walikubali na kuonyesha ushirikiano wakati wa kunyolewa na hivyo hakukuwa na kamata kamata na mikiki mikiki wakati wa kunyolewa na kondoo walitulia na kunyamaza mbele ya wakata manyoya! 

Ni katika mazingira kama haya Nabii Isaya anatabiri na kuonyesha ushujaa na utulivu mkubwa sana aliokuwa nao Yesu wakati wa mateso yake yeye alionewa na aliwekewa hata na mashahidi wa uongo na waliyoyazungumza hayakuwa na ukweli lakini Kristo alinyamaza kimya ona

 

Mathayo 27:11-14 “Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema. Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno. Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia? Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana.         

Kuna kitu kikubwa cha kujifunza kutoka kwa Yesu, wakati wa mateso yake na wakati wa kuhukumiwa kwake watu walipeleka mashitaka ya uongo na kumsingizia mambo mengi lakini yeye hakujibu neno, pamoja na kushutumiwa kwa mambo mengio namna hiyo mpaka Hakimu alishangaa ni mshitakiwa gani huyu asiyejitetea alikaa kimya sawa na alivyotabiri isaya kuwa Yesu alikuwa kama kondoo kayika mikono ya wakata manyoya

Kunyamaza ni Nidhamu

Kwa asili hakuna mwanadamu anaweza kukubaliana na kuchafuliwa jina lake na wakati mwingine unaweza kulazimika kumlipa mtu fedha nyingi kama akikufungulia kesi za madai na kudai fidia ya kuchafuliwa jina, kila mtu anapenda jina zuri, kila mwanadamu anapenda heshima na hakuna mtu anayefurahia kudhalilishwa  au kuchafuliwa jina lake na heshima yake

Mithali 22:1 “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu.” Unana kimsingi mtu anapochafuliwa jina kuna vitu vinawaka sana moyoni na unaweza kujikuta unataka kujibu na kujitetea  lakini uwezo wa kunyamaza na kutulia huonyesha uwezo mkubwa sana wa kinidhamu ulionao,  watu wakati mwingine wanaweza kukuharibia jina, wanaweza kukusema vibaya wanaweza kuzungumza maneno ya uongo na uzushi mkubwa sana, wanaweza kutengeneza skendo, wanaweza kueleza matetesi, kukusengenya, kukuchafua kukusema vibaya , kueleza maswala mabaya ambayo wakati mwingine ni kama ynaweza kufanana na ukweli kabisa, watu wanaweza kujenga dhana mbaya sana kukuhusu, Katika maisha yangu nimefanya kazi mbalimbali za injili nimefundisha vyuo vya biblia kwa miaka karibu 12, nimekuwa mchungaji kiongozi kwa maiaka zaidi ya 22 nimekuwa mkuu wa shule na kuwasaidia wanafunzi kiroho na kitaaluma wakati mwingine nimewahi kusikia habari zangu zikizungumzwa sio za kazi ya injili niliyoifanya bali ya mambo mabaya yanayosaikiwa kuwa nimeyafanya,  watu wanazungumza mabaya kunihusu, sio jambo jepesi kukaa kimya, inahitaji nidhamu, nampenda sana Muhubiri Mtume Mwamposa moja ya vitu ninavyopenda kuhusu yeye sina cha kusema kuhusu huduma zake, kuhusu maji au mafuta lakini Muhubiri huyu huwa hajibu kitu chochote wala neno lolote la mtu yeyote anayemshutumu kwa jambo lolote  hii ni nidhamu ya hali ya juu je HUSIKII NI MAMBO MANGAPI WANAYOKUSHUHUDIA?  Aliuliza Liwali kwa Yesu lakini Bwana Yesu alikaa kimya kuna kanuni gani muhimu katika kukaa kimya nini tunaweza kujifunza kutoka kwa Yesu? Kuwa sisi ni safi au sio safi hiyo sio kazi yetu tuliyoitiwa Mungu ndiye atakayesimama kumtetea yule aliyemtuma, achilia haki zako katika mikono ya Mungu aliye hai, ni yeye ndiye atakayeamua kama wewe ni safi au la!  Mungu hajaagiza sisi kujihami, wala kujisafisha  maandiko yanaonyesha ya kuwa sisi tumeitwa kuwa jalala na kufanya kuwa takataka za dunia kuwa kama watu wa kuhukumiwa  Paulo mtume alisema nadhani kuwa sisi tuna wito huu wito wa kutukanwa, wito wa kusingiziwa, wito wa kusemwa vibaya wito wa kuonewa wito wa kuhukumiwa wito wa kuwafanya wenguine wafurahi, wito wa kudharaulika  ona 

1Wakorintho 4:9-13 “Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili;tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa.”

Unaona hatupaswi kujipanga kujibu hoja wako watu wanajua kujieleza kuliko sisi nakumbuka wako watu wanao uwezo wa kusema hata uongo ukaonekana kuwa kweli mimi binafsi sina uwezo huo mimi binafsi siwezi kesi mimi nikienda na mtu muongo kwenye kesi yeye atashinda sijazoea vikao vya fujo naweza vikao vya amani siwezi mimi kujitetea naweza kunyamaza kimya hata mbele ya wanaonishutumu na kunichukia hata bila sababu Mungu hakutuagiza kufanya hivyo Mungu ameagiza kulinda mioyo yetu tu

Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima

Swala la mimi ni mzuri au mbaya hiyo sio kazi yangu, mimi ni mwanadamu sijajiumba mwenyewe mwenye mzigo wake aliyeniita akaniokoa akanipa kazi hii ya injili  atajijua mwenyewe kama mimi ni dhaifu sio kazi yangu kuondoa udhaifu wangu ni kazi yake yeye aliyeniita wala sio kazi yangu kuwajibu wale wanaoshutumu kwani inawezekana pia Mungu akawatuma wafanya kazi ya kututukana tunapojaribu kujitetea inawezekana ndio tukaharibu zaidi watuite freemason au waseme lolote wanaloweza kulisema wewe fanya kile ulichoitiwa, kwa sababu kama tuko duniani ukiwanyamazisha hawa hawa watainuka so kazi ya kunyamazisha wanaotushutumu itafanywa na Mungu mwenyewe  ndio mimi ni kondoo tu kati ya wakata manyoya huenda Mungu amewatuma wanitukane hivi ndivyo alivyofanya Daudi wakati wa kushutumiwa kwake ona

2Samuel 16:5-11. “Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa!  Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu. Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya? Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza.”

Unaiona Daudi alikuwa ni mfalme tena ni askari na alikuwa akizunghukwa ma majemadari wakubwa wa vita alafu anatokea mtu anamtukana hana hata silaha anarusha mavumbi na kumshutumu, Abishai moja ya majemadari wa Daudi akasema huyu ni mbwa mfu anawezaje kumtukana mfalme tunaweza kumshughulikima mara moja Lakini Daudi akasema aaachiwe  Bwana amemtuma afanye hivyo! Oooh inahitaji uvumilivu mkubwa wako watu wametumwa watutukane watusengenye, watushutumu, watulaani, waseme sisi ni waongio, waseme sisi hatufai, waseme uongo na uzushi watupige vijembe, watudhulumu watunyanyase watuseme vibaya kaa kimya hao ni wakata manyoya tu! Wanafanya Pruning ili usipate magonjwa ili usijivune ili uendelee kumtegemea Mungu ili kuonyesha ukomavu wako na ili uweze kuwa na mbele nzuri unahitaji kuvumilia na unahitaji kukaa kimya !    

Kunyamaza mbele ya wakata Manyoya !

Unadhani unaweza kufanya nini kama watu hawakubali kukuelewa? Unadhani unaweza kutatua tatizo? Unadhani unaweza kujibadilisha ukawa kama wanavyotaka? Wamechagua kukuelewa hivyo lazimka ukubali na kuwa mkimyaaa wao hawauhsiki na maisha yako ya baadaye? Wala hawana nguvu ya kuamua hatima yako Mungu haweki hatima yetu katika mikono ya watu wapuuzi, wala mabaradhuri Mungu huweka hatima yetu katika mikono yake yeye ndiye aliyetuumba nan i yeye ndiye mwenye kusudi na sisi  na hakuna mtu anaweza kushindana na kusudi la Mungu na kile ambacho Mungu amekikusudia katika maisha yako hivyo nyamaza mbele ya wakata manyoya kazi yako ni kutimiza wajibu wako na lile kusudi ambalo kwalo Mungu amekuitia haijalishi watu watatuheshimu au watatudharau mwache Mungu afanye yake achana na watu wanaotaka uonekane mbaya pale kazini, shuleni mtaani na katika jamii wakati mwingine hawawezi kuonekana wazuri mpaka wakufanye wewe mzuri kuwa mbaya, wewe endelea na kazi uliyoitiwa, endele kufurahi, endelea kuwa na tabasamu, wao ni wakata manyoya tu, kazi ya kuotesha mengine ni ya Mungu nay ale wanayayafanya ni kwa faida yako kubwa sana , huitaji nguvu kubwa sana kushindana na wanaokupinga nadhani unahitaji nguvu kubwa sana kulinda moyo wako, Mungu anayo njia nzuri sana ya kukusafisha na kukuweka panapo nafasi, Mungu atashughulika mwenyewe wala hataachilia uonevu utamalaki

Zaburi 105:14-15. “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

Jukumu la kutokuacha au kuachilia tuonewe ni la Mungu mwenyewe, sisi tukae kimya mbele ya wakata manyoya Mungu ndiye atakayetuhesabia haki kwani ni yeye ndiye aliyetufia msalabani, ni yeye aliyeteseka kwa niaba yangu, ni yeye ndiye aliyeninunua kwa damu ya thamani, siwajibiki kwa mtu nawajibika kwa Mungu, sisemi na umbwa nasema na mwenye umbwa amabaye ni Mungu mwenyewe na kwa sababu hiyo tembea kifua mbele, tembea kwa ujasiri asikubughudhi mtu moyo wako aliyetuumba sisi ni Mungu, aliyetuokoa ni Mungu aliyetuita kwenye huduma ni Mungu anayetuelewa ni Mungu na anayetutetea ni Mungu kwa hiyo hakuna sababu ya moyo wako kuinama nyamaza kimya usiwajibu kitu wakata manyoya Mungu ndiye atakaye wajibu.

 

Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Faidha kubwa ya kunyamaza kimya mbele ya wakata manyoya ni kuwa Mungu mwenyewe atafanya kitu cha ziada kama alibyo tabiri Isaya ona

Isaya 53:10-12 “Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.              

Mungu alimuinua juu Kristo na kumuwadhimisha mno na kumkirimia jina lipitalo majina yote, kazi yetu sio lazima ikubalike na wanadamu kwa sababu sio wao waliotutuma, kazi yetu itathibitishwa na Mungu mwenyewe aliye hai hivyo tunapokutana na changamoto za aina mbalimbali hatuna budi kuhakikisha kuwa tunanyamaza kimya, tusijisafishe, tusilalamike tutulie kimya mbele za Mungu na kuendelea na majukumu yale ambayo Mungu ameyaweka mbele yetu na jitahidi uwe na amani moyoni mwako ukijua wazi ya kuwa Mungu ndiye anayehusika na maisha yetu kwa hali zote

Hakuna mwanadamu alisemwa vinaya kama Yesu, walisema amechanganyikiwa, walimwita ana pepo, walisema anatoa pepo kwa mkuu wa Pepo, Yeye aliendelea kuponya wagonjwa, kuwasaidia wenye shida kulisha wenye njaa na kuwafundisha wenye uhitaji, kwa sababu yako makundi ya watu waliamua kutokumuelewa na yeye aliwaacha, kumbuka Yusufu hakufanya kazi ya kujitetea kuhusu zinaa aliyosingiziwa na mke wa Potifa, kumbuka Nehemia aliendelea na kazi ya kuujenga ukuta pamoja na manenio mabaya kutoka kwa Tobia na Sanbalat na kazi ya Mungu ikakamilika je unadhani Mungu alikuwa hawaoni kina Tobia na Sanbalat? Je unadhani Mungu hangeweza kuwazuia ndugu yangu kama tumechagua maisha haya ya kumtumikia Mungu basi sisi ni kama Kondoo nayeye ndiye Mchungaji mwema na linapokuja swala la Mwenye Kondoo anataka kukata manyoya tutulie kimya mbele ya wakata manyoya!

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Hakuna maoni: