Jumatatu, 20 Februari 2023

Waoga katika ziwa liwakalo Moto!


Ufunuo 21:7-8 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya tabia ambayo inawakosesha watu wengi sana Baraka za kiungu ni Pamoja na tabia ya kuwa na WOGA, Mungu ameuweka woga kama moja wapo ya dhambi ya kwanza katika orodha ya watu watakaotupwa katika ziwa la Moto kutokana na kukosa ushindi wa kuingia Mbinguni, kama tunavyoweza kuona katika mstari wa Msingi

Ufunuo 21:7-8 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

Ni aina gani ya woga inazungumzwa hapo?  Katika Biblia ya kiingereza ya New international Version neno waoga linasomeka kama COWARDLY  au katika Matoleo mengine ya Biblia kama KJV neno linasomeka kama FEARFUL kwa mujibu wa Lugha ya asili iliyotumika kuandikia agano jipya neno la kiyunani linalotumika hapo ni DEILOS kimatamshi DILOS au DEOS maana yeke ni TIMID  ambalo tunaweza kulitafasiri kwa kiingereza kama a Person who is lacking Courage, au a person who lacks endure  dangerous au a person who fear unpleasant things kwa lugha yetu tunaweza kusema Mwoga ni mtu asiye na ujasiri, au mtu asiyeweza kuvumilia mambo magumu, au anayeogopa hatari, au kuogopa mambo yasiyopendeza au ya aibu,  watu wa aina hiyo utaweza kuona kuwa katika maandiko Mungu hakupenda kuwatumia, watu wa Mungu ni kama askari  na kila mara Mungu anapotuita katika ushirika nayeye huwa anatuagiza kwamba tusiogope, Mungu anajua namna ambavyo woga ni adui mkubwa sana na urithi wetu, woga ni adui wa maendeleo, watu wenye hofu huwa hawafanikiwi sio tu katika maisha haya lakini hata Mbinguni ni vigumu kuingia kama u mwoga!

Nyakati za Biblia Mungu alipowaita watu vitani alihakikisha kuwa waoga wote wanaondolewa kwenye orodha ya wapiganaji na waliobaki walikuwa ni wale waliokuwa na moyo wa ujasiri tu, na haikupaswa wao kuogopa chochote zaidi ya kuku mbuka tu kuwa Bwana yuko pamoja nao, ilikuwa ni lazima kila mwenye sababu zinazoonyesha kuwa hafai kwenda vitani aondolewe na wale waliokwenda walitiwa moyo na kuhani na kuelekea vitani wakiwa wana muamini Mungu tu ona

Kumbukumbu la Torati 20:1-9 “Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri. Na iwe, msongeapo mapiganoni, kuhani na akaribie na kusema na watu, awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao;  kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi. Na maakida na waseme na watu, na kuwaambia, Ni mtu gani aliye hapa aliyejenga nyumba mpya, wala hajaiweka wakfu? Aende akarudi nyumbani kwake, asije akafa mapiganoni, ikawekwa wakfu na mtu mwingine. Ni mtu gani aliye hapa aliyepanda shamba la mizabibu, wala hajatumia matunda yake? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, yakatumiwa na mtu mwingine matunda yake. Ni mtu gani aliye hapa aliyemposa mke wala hajaoa? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, huyo mwanamke akaolewa na mume mwingine. Tena maakida na waseme zaidi na watu, wawaambie, Ni mtu gani aliye hapa tena mwenye hofu na moyo mnyonge? Aende akarudi nyumbani kwake, isije mioyo ya nduguze ikayeyuka mfano wa moyo wake. Itakuwa hapo watakapokwisha wale maakida kusema na watu, na waweke majemadari wa majeshi juu ya watu.”

Mungu wakati wote aliwataka watu wake wawe na moyo wa ushujaa ona katika Yoshua 1:5-9 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”   

Yesu Kristo vile vile anawataka watu wake wawe na ujasiri na ndio maana wakati wote aliwataka wanafunzi wake wawe watu wenye kujikana nafsi lakini vilevile hakutupoa roho ya woga  ona


Luka 9:23-25 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?


Unaona wanajeshi wakati wote huwa hawayahesabu maisha yaio kuwa kitu, wanapokwenda vitani wanajua kuwa wako tayari kuyatoa maisha yao kwaajili ya taifa lao au kwaajili ya ndugu zao wanajua wazi kuwa unapokwenda vitani kuna kufa na kupona hivyo husimama kidete wakijionyesha kuwa wanaume, Kristo anataka kila mtu anayemfuata kuubeba msalaba wake na kumfuata kila siku, ziko changamoto za kila siku katika maisha yetu zinazohitaji imani yetu kwa Mungu na kwa msingi huo kamwe hatupaswi kuogopa ndio maana Mungu ametupa Roho Mtakatifu ili tuweze kukabiliana na hofu ya maisha haya ona


2Timotheo 1:7-9 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,”


Wakati wote ushindi wetu unapatikana kwa njia ya imani katika Mungu, kwa hiyo pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunamwamini Mungu kiasi kwamba tunamtegema yeye kiasi kwamba hatuogopi hatari ya aina yoyote, watu wanaoogopa aibu hawawezi kufanya biashara yenye mtaji mdogo, watu wanaoogopa mitihani wanaweza kufeli hata kama mitihani hiyo ni myepesi, woga unaweza kutukosesha ushindi, 

Nyakati za ikanisa la kwanza  wakati Yohana anaandika kitabu cha ufunuo ulikuwa ni wakati ambapo watu wanaomwamini Yesu kristo walikuwa wanauawa kwa kukatwa na misumeno, kwa kuchimwa moto kama mishumaa baada ya kumwagiwa lami, kwa kukatwa kiungo kimoja kimoja, kwa kuchunwa ngozi huku wakiwa hai, kwa kufunguliwa simba wenye njaa, kwa kusulubiwa na kutundikwa misalabani, kuuawa kwa mikuki na mambo mengine ulikuwa ni wakati mbaya na w mateso ya hali ya juu, katika wakati huu watu wengine walimkana Yesu na kuachiwa huru kwa sababu ndio lilikuwa sharti kubwa ukimkana Yesu unaachiwa huru, kwa hiyo kila Mkristo alipaswa kukubali kukabiliana na kila aina ya mateso atakayokutana nayo na kuvumilia kila hatari utakayokutana nayo na kufa kwaajili ya Kristo ilikuwa ni alama ya ushindi,  wale waliomkana Yesu kutakana na mitihani waliyokutana nayo waliitwa waoga na hawa waliwekwa katika orodha ya kwanza ya watu watakaotupwa katika ziwa la Moto! Kwa nini kwa sababu walimkana Yesu na kuihesabu damu aliyoimwaga kama kitu cha hovyo, wako watu wanaogopa kumkiri Yesu hadharani, wako watu wanamkataa Yesu kwa sababu ndugu zao baba zao na mama zao ni wa imani nyingine neno la Mungu linasema waoga wote sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto, Heri leo umkubali Yesu, heri leo upokee roho ya nguvu ya ujasiri na ya upendo, heri leo ukatae mashetani na mkizimu na majini na mapepo, heri leo ukiri Yesu katika njia zako zote! 

Woga wako ndio kizuizi cha muujiza wako!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

               

Hakuna maoni: