Jumanne, 27 Juni 2023

Jinsi ya kutengeneza Maji ya Baraka!


Ezekiel 36:25-27 “Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.”

 


 

Utangulizi:

 

Nyakati za siku hizi kumekuwepo na mfumuko mkubwa sana wa matumizi ya maji pamoja na mafuta katiika maombezi, na watu wengi sana wamekuwa wakijiuliza kulikoni kuhusu matumizi ya maji, mafuta na au chumvi katika maombezi na shughuli za utatuaji wa maswala kadhaa ya kiroho, Katika somo hili leo nazungumzia tu kuhusu matumizi ya maji katika maombezi, ambayo ni maarufu kama maji ya Baraka, au maji matakatifu.

 

Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa neno la Mungu liko kimyaa kuhusu namna maji ya Baraka au maji matakatifu na namna yanavyotumika leo, Maji yanayotajwa katika maandiko hususani agano jipya ni maji yanayohusika na ubatizo Mathayo 3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.”

 

Maandiko yanataja ubatizo wa maji kwa kusudi la toba, na hakuna ufafanuzi wowote kuhusu maji ya Baraka au maji matakatifu, Ubatizo wa maji mengi ni ishara ya kumkiri Bwana wetu Yesu kuwa bwana na mwokozi kwa kukubali hadharani kazi aliyoifanya pale msalabani kwa mateso yake, kifo na kuzikwa na kufufuka. Hicho ndicho kinaelezwa zaidi na kwa uwazi katika maandiko!

 

Swala la kunyunyizia maji ya Baraka au maji matakatifu kama tunavyoliona leo linaweza kufanana kliasi Fulani na ile dhana ya agano la kale la utakaso ambapo maji matakatifu yalitumika kutakasa vitu najisi endapo kimeguswa na kunajisiwa na mtu aliyevigusa aliyekuwa najisi, lakini pia maji matakatifu au maji ya Baraka yalitumika kama njia ya kuwatakasa watu waliokuwa najisi, kwa sababu mbalimbali ona mfano

 

Mambo ya walawi; 17:15 “Tena kila mtu atakayekula nyamafu, au nyama aliyeraruliwa na wanyama, kama ni mzalia, kama ni mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni; ndipo atakapokuwa safi.”

 

Hesabu 19:17-19 “Na kwa huyo aliye najisi watatwaa katika majivu ya kuchomwa kwake hiyo sadaka ya dhambi, na maji ya mtoni yatachanganywa na majivu katika chombo; kisha mtu mmoja aliye safi atatwaa hisopo, na kuitia katika hayo maji naye atayanyunyiza juu ya hema, na juu ya vyombo vyote, na juu ya watu waliokuwapo, na juu yake yeye aliyeugusa mfupa, au mtu aliyeuawa, au mzoga, au kaburi; na yule aliye safi atamnyunyiza huyo aliye najisi siku ya tatu, na siku ya saba; na katika siku ya saba atamtakasa; naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa safi jioni.”

 

Andiko la msingi ambalo nimelitumia katika utangulizi wa somo langu kwa kiwango Fulani linazungumzia kinabii kile ambacho Mungu amekitabiri kupitia nabii Ezekiel kuhusu kuwanyunyizia watu wake maji safi kwa kusudi la kuwaondolea vitu vibaya na kutafuta ushirika naye, kwa hiyo tunaweza kuona kuwa maji yalitumika kuwatakasa wanadamu, waliokuwa na magonjwa au waliokuwa najisi au kuweka wakfu vyombo vitakatifu, hivyo kwa kiwango Fulani tunaweza kuona tu kwa umbali kwamba maji yanahusishwa na utakaso lakini huduma kuhusu maji ya Baraka na maji ya matakatifu kama yanavyotumika leo bado biblia iko kimya!

 

Maji ya Baraka katika makanisa makubwa ya kale

 

Katika makanisa makubwa namaanisha kwa umri yaa ni makanisa ya asili kama Orthodox, Roman Catholic na Anglican yapo matumizi ya maji ya Baraka au maji matakatifu, hivyo kimsingi makanisa hayo yalikuwa na utaratibu wa kutumia maji hayo, bila kuweka wazi sana chanzo cha matumizi ya maji hayo, hata hivyo katika kanisa la Orthodox kwa mfano matumizi ya maji matakatifu yalikuwa au hufanyiika katika siku za jumamosi kuu, yaani jumamozi kabla ya sikukuu ya pasaka, na vilevile katika sikukuu ya Pentekoste, Makuhani huyafanyia maombi maji machache na chumvi kisha wanachanganya na kuruhusu maji hayo kuongezewa na maji mengine na kuyasambaza katika maeneo husika ya kanisa hususani sehemu za kuingilia milangoni, waamini wangeingia na kuchovya vidole vyao na kupiga ishara ya msalaba, kama maji hayo yakuongezea yangekuwa mengi zaidi kuliko yale yaliyobnarikiwa makuhani wangeiongeza maji zaidi baada ya kuandaa, uandaaji wenyewe unafanywa na makuhani, kwa kuombea maji pamoja na chumvi na kuyaombea ili yakutane na mahitaji ya watu ikiwa ni pamoja na kufukuza mapepo,kuponya magonjwa,kutakasa, kuondoa nuksi, mikosi na balaa, na kuleta neema isiyokusudiwa, juu ya watu, wao wanaamini tu kuwa maji matakatifu ni zawadi nzuri ambayo Mungu amewapa watu wake kwa kusudi la kuwatakasa watu wake kutoka katika changamoto mbalimbali za kila siku,  na kuhakikisha kuwa tunakuwa vizuri kila siku kama tutayatumia mara kwa mara, wao wanaamini kuwa maji ni sacrament  Neno Sacrament limetokana na neno la asili la kihispania Sacramento kwa kiingereza sacrament ni tukio la kidini au la kiishara kama ilivyo ubatizo au meza ya bwana linaloaminika kuwa linabeba neema ya Mungu na kuleta maana Fulani ya kiroho

 

A Sacrament is a religious ceremony or rituals that stand as baptism or Lord Supper held to be a means of divine grace to be a symbol of a certain spiritual reality

 

Kwa hiyo matumizi ya maji matakatifu, au maji ya Baraka kwa mujibu wa Orthodox unaendana na habari ya ubatizo wa maji mengi aliofanyiwa Yesu Kristo, kupitia Yohana Mbatizaji katika mto wa Yordani, kwa mujibu wa Orthodox ingawa Yohana alikuwa anabatiza kwa maji kama ishara ya toba dhidi ya dhambi, na watu walikwenda ili watubu dhambi zao, wanaamini kwa kuwa Yesu hakuwa na dhambi na alikuwa ni Mungu, wanaamini kuwa Yesu aliyabariki maji,  na wanayahesabu maji kuwa ni matakatifu na kuwa Yesu aliyatakasa na kwaasili maji yaliumbwa na Mungu kwa makusudi hayo yatumike pia kwa kazi zake za kutakasa! Roho Mtakatifu alitulia juu ya uso wa maji wakati waa uumbaji na hivyo maji ni sababu ya uwepo wa uzima katika mwili na roho

 

Mwanzo 1:2  Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.”      

 

Kwa mujibu wa kanisa Catholic wao maji ya Baraka au maji matakatifu wanayatumia kila siku na wanayaweka mlangoni mwa kanisa, wana wanaamini kuwa maji ya Baraka mwanzo ni yalitumiwa na watu walioabudu mwezi na yalitumiwa na makuhani wa dini za kienyeji walipokuwa wakiingia katika mahekalu yao, kwa hiyo swala la maji ya Baraka ni la asili ya dini za kipagani za waabudu miungu  na hasa mungu mwezi,  kwa mujibu wa kanuni ya 65 ya mkutano mkuu wa Constantinople (691). Na kwa mujibu wa Encyclopaedia ya wakatoliki inaeleza kuwa matumizi ya maji ya Baraka yalianza kutumika zaidi mnamo karne ya 19, pamoja na ukweli kuwa Agano jipya hakijasema chochote kuhusu matumizi ya maji, lakini waliitumia njia hii kama njia ya kuwashika wapagani na kuhakikisha kuwa wanaifuta ibada hiyo katika njia ya kipagani, kwa matumizi ya maandiko yanayoonyesha kuwa maji yanatakasa vilevile kama walivyokuwa wakiyatumia katika ibada zao za zamani.

 

Kanisa Anglikan wao hutumia maji vilevile kwa njia mbili, moja ikiwa ni kwa kuyaombea na kuchanganya na chumvi na kuyaweka katika milango ya kanisani ili washirika wanapoingia waweze kujibariki kupitia maji hayo, aidha pia kuhani wa kianglikan anaweza kupita katika baadhi ya ibada akiwanyunyizia maji, kama ishara ya kuwatakasa na washirika wangeitikia kwa kufanya ishara ya msalaba ili wakutane na mahitaji yao, tukio hili lilikuwa sawa na maombezi tu!

 

Wakatoliki na wanaamini kuwa tukio lolote ambalo linakufanya ujisikie ya kuwa Mungu yuko karibu nawe linapaswa kutiwa moyo  hii ni kwa mujibu wa Warumi 14:23  Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.”        Na pia

 

1Wakorintho 6:12 “Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote”.

               

Wanaamini kuwa kama jambo lolote ni jema katika kutufungamanisha na Mungu ni vema kulitunza, na akama linakwaza ni vema kulitupilia mbali, kwa hiyo ingawa maandiko hayajawahi kutoa maelekezo kuhusu matumizi ya maji ya Baraka kwa namna yoyote wana wanaona wayatumie tu japo sio agizo la kibiblia

 

Makanisa ya kiinjilisti na makanisa mengi ya kipentekoste sasa wamekuwa wakiyatumia maji vilevile kama makanisa makuu ya zamani, lakini sasa wao wamekuwa na msamiati mpya badala ya maji ya Baraka au maji matakatifu wao huyaita maji ya upako, matumizi haya ya maji ya upako yamepata mfumuko mkubwa wa kimatumizi katika dunia ya leo kuliko ilivyokua zamani na ni kwaajili ya haya ndio ilinipelekea kujaribu kufuatilia na kulifanyioa utafiti swala hili ili kuweza kuja na somo linaloweza kutusaidia katika kupanua ufahamu wetu kuhusu Maji ya Baraka na ikiwezekana tutengeneze wenyewe kama tunataka badala ya kuuziwa kwa vile pia yamekuwa na mfumuko mkubwa wa kibiashara na yamekuwa yakihusishwa katika kuuzwa

 

Jinsi ya kutumia maji ya Baraka.

 

Maji haya yanaombewa na kiongozi wa kiroho aliye na mamlaka ya kichungaji au kikuhani, au na mkristo yeyote anayeamini kwa maandalizi maalumu utakayoyaona baadaye katika kielelezo. Kuhani huyabariki maji hayo kwa kidole chake kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, baada ya maji kuwa tayari kwa kufuata hatua za maelekezo yaliyoko chini  katika somo hili  maji yatatumika aidha kwa kutumia ishara ya msalaba au kwa kunyunyizia watu katika ibada, yanaweza kutumika nyumbani, kwa kutakasa nyumba, kutakasa watu, kutakasa wanyama, kutakasa biashara, kutoa pepo, kuponya wagonjwa ulinzi,  kujipatia rehema za MUngu na matumizi mengine mengi zaidi kwa kadiri ya dhamiri inavyokushuhudia, wakati wote huwa unaweza kutumia jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu au moja kwa mojwa kwa jina la Yesu Kristo., unaweza kuyatumia kubariki familia, watoto, ndoa, wakati wanapoenda kulala usiku au asubuhi watu wanapoenda kazini na shuleni, kama sehemu inautembeleo wa kishetani kama shule au uchawi unaweza kutatumia maji ya Baraka au maji ya upako kwa jina linalotumika siku za karibuni.

 

Jinsi ya kutengeneza maji ya Baraka/ maji ya uapako

1.   Chukua maji safi na uyaweke katika bakuli safi la aluminium inayong’aa, yashikilie maji yako na kwa unyenyekevu mkubwa sema Ewe Mungu uliyeumba Nchi na ardhi na maji na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana nayabariki maji haya Katika jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu!.

 

2.   Chukua chumvi ya aina yoyote ile ya mawe au ya kawaida nyeupe au ya bahari, Omba kwa unyenyekevu mkubwa na kusema Ewe Mungu uliyeumba Nchi na ardhi na maji na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana naibariki chumvi hii Katika jina la baba na la mwana na la Roho Mtakatifu! 



3.   Chukua chimvi iliyoombewa sasa na utainyunyizia katika maji na pia utakoroga maji hayo ili yachanganyike na chumvi na utaichanganya kwa kutumia jina la Yesu au kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu!

 


 

4.   Sasa Mchanganyiko wa Maji ya Baraka uko tayari, lakini unasubiri dua maalumu ambayo utayaombea kwa kusema Baba wa Mbinguni, nayaweka maji haya wakfu katika jina la baba na Mwana na Roho Mtakatifu, Nikiomba kwa maji haya utakase kila kitakachoguswa na maji haya, utaondoa nuksi, mikosi na balaa na kila jicho baya na maneno mabaya dhidi ya kitakachoguswa na maji haya kiwe batili na manuizo yote ya kiganga na kichawi yaharibike,  nawe utakibariki kila kitakachoguswa na maji haya kwaajili ya utukufu wako ili wewe utukuzwe sawa na mapenzi yako Katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai amen!

 


Baada ya dua na maombi hayo na maandalizi hayo yote muhimu tayari una maji ya Baraka, una maji matakakatifu una maji ya upako na unaweza kuyatumia kwa sababu zozote zile kwa kusudi la kumpa Mungu utukufu, mashambani kwaajili ya mavuno, kwenye biashara kwaajili ya mafanikio, kazini, ofisini au maeneo unayohisi kuwa yamevamiwa kishirikina

 

Mafundisho haya ni kwawale tu wanaomini katika fundisho hilo au utamaduni huo, lakini wakati wote nguvu ya vifaa hivi vya kiroho ni jina la Yesu Kristo.

 

KUMBUKA: Mafundisho haya ya katika shule za kinabii na kama imani yako inakinzana usitilie maanani wala usifundishe kanisani kwako!

 

Na. Rev. Innocent Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Hakuna maoni: