Jumanne, 27 Juni 2023

Inzi wanaposumbua Nyumba yako.


Kutoka 8:20-22 “BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.” 

 




Utangulizi:

Watu wengi sana huwa wanachukizwa sana na wakati mwingine wanapata hasira wanaposumbuliwa na Inzi katika nyumba zao, hii ni kwa sababu inzi katiika jamii nyingi wanahusishwa na uchafu, na wakati mwingine pia kusambaza magonjwa hivyo kimsingi inzi hawapendwi na ni machukizo kwa watu wengi sana duniani, wakati mwingine nzi wanaweza hata kutoa milio Fulani ya kuudhi au kujazana mahali, Jambo ambalo linakera na linaleta maudhi na wakati mwingine kuruka ruka katiika miili ya watu! Hata hivyo katika lugha ya kinabii inzi wanapotokea katika nyumba yako wana habari Fulani njema au mbaya ya kukupasha, katika ulimwengu wa kiroho, na hivyo ni muhimu kuwa na usikivu wa rohoni mainzi yanapotawala katika nyumba yako! Tutajifunza somo hili Inzi wanaposumbua nyumba yako kwa kuzingatia maeneo manne yafuatayo:-

i.                    Inzi katika mtazamo wa kibiblia

ii.                  Inzi wakiwa ni ishara njema

iii.                Inzi wakiwa ni ishara mbaya

iv.                 Mambo ya msingi yakupasayo kufanya

Inzi katika Mtazamo wa kibiblia

Hatunabudi kufahamu kuwa nzi ukiacha kwamba ni wadudu wa kawaida lakini pia wanatazamwa tofauti katika mtazamo wa kibiblia kwanza wanawakilisha malaika waovu au pepo wachafu, na dhana hii iko katika maandiko agano la kale na jipya ambapo hata mkuu wao aliitwa Beelzebubu ona mfano katika

Luka 11:14-15 “Naye alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.”

Katika kifungu hicho cha maandiko Wayahudi walimshutumu Yesu wakidhani ya kuwa anatumia nguvu za mkuu wa pepo Beelzebuli kutoa Pepo, kumbe yeye alitoa pepo kwa uweza wa Roho Mtakatifu na alifafanua kuwa shetani hawezi kumtoa shetani, sio kusudi langu kufafanua jambo hilo kwa undani kwani ninachikitaka hapa ni kufafanua tu huyu BEELZEBULI ni nani ?  Kimsingi jina hili Wayahudi walitoka nalo huko ukaldayo na hapa limeandikwa kwa lugha ya Kiyunani, kiyunani ni BEELZEBOUL ambalo tafasiri yake ni mkuu wa Pepo wachafu, au mfalme wa pepo wachafu jina ambalo kimsingi linamuhusu shetani,  aidha katika maandiko pia huko katika nchi ya wafilisti katika mji ulioitwa Ekron kulikuwa na mungu baali ambaye alikuwa anahusishwa na swala la kufukuza Inzi huyu aliitwa Baal-Zebub mungu wa Ekron ona katika

2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.”

Mungu huyu wa wafilisti aliitwa BAAL ZEBUBU jina ambalo kwa kiingereza humaanisha “BAAL OF FLIES”  yaani mungu wa mainzi, mungu huyu alisadikiwa kuwa na uwezo wa kufukuza mainzi, Hakuna uhakika sana kama kuna muununganiko wa kimaana kwa majina hayo na lile la agano jipya lakini huyu pia alikuwa ni shetani kwa hiyo bado tunaweza kuona Mapepo na mashatani yakihusishwa na mainzi, kwa sababu ya uchafu. Au jina lile pepo wachafu.

Huko Misri nako wakati wa hukumu ya Mungu dhidi ya Farao ili awaachie wana wa Israel Mungu aliipiga Misri kwa hukumu ya pigo la mainzi

Kutoka 8:20-22 “BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.”

Kimsingi pigo hili pia ilikuwa sio hukumu kwa Farao na wamisri tu bali pia kwa miungu ya wamisri, mungu aliyekuwa anahukumiwa hapa kwa wamisri ambao walikuwa na miungu wengi mmoja wapo ni  mungu aliyekuwa anajihusisha na kufukuza inzi, kwa uweza wa Mungu alikuwa akionyesha kuwa kama Mungu akiwatumia inzi kama sehemu ya hukumu miungu hiyo haiwezi kuzuia kusudi kuu likiwa lile lile Farao aweze kujua ya kuwa Yehova ndiye Mungu pekee duniani.

Kwa hiyo tunaweza kukubaliana wazi na wazo la kibiblia kuwa inzi wanawakilisha pepo wabaya na mkuu wao ni shetani, katika lugha ya kinabii, hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa kinabii inzi wa kawaida wanapoanza kuiandama nyumba yako huwa kunakuwa na maana za msingi za kiroho zinazowakilishwa maana hiyo inaweza kuwa ya hatari na mbaya au maonyo ya kutokupuuzia maeneo Fulani muhimu katika maisha yetu. Inzi kinabii pia wanawakilisha chuki, uovu, au lawama kwa sababu wanaruka ruka hovyo na kubughudhi watu, wanawakilisha pia tabia mbaya, kukosa kiasi na hisia mbaya, lakini pia wanawakilisha mambo mazuri kama tunavyoweza kujifunza katika vipengele vifuatavyo:-

Inzi wakiwa ni ishara njema

Inzi wakiwa na ishara njema huwa wanabeba maana zifuatazo:-

1.       Inzi wanashiria kuwa kuna mambo unapaswa kuyafanyia maamuzi magumu  - Inzi wanapokufuata futa katika nyumba yako wanakupa ujumbe kuwa kuna maamuzi magumu unapaswa kuyafanya ili kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yako, yako mambo aidha unapaswa kuachana nayo, au kuna jambo unapaswa kuliachia kabisa katika maisha yako, kama iko tabia mbaya ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa kuharibu maisha yako tabia hiyo iachwe mara moja, kama yuko mtu anakusababishia kufanya mambo mabaya mtu huyo uachane naye haraka, au mara moja, kuna ujumbe wanaokupa nzi kuwa kitu hicho kibaya kiondoke katika maisha yako, hivyo utapaswa kujitafakari na kuangalia ndani yako na mazingira yako na kile utagundua kuwa ni sababu ya wewe kutokuendelea au kuharibikiwa basi utapata jibu kuwa unatakiwa kukifukuzilia mbali kama vile tunavyotafuta kuachana na nzi, tahadhari hapa usichukue maamuzi bila kufikiri kwa kina na ukijisikilizia kwa ndani ndipo utagundua ni kitu gani watu au mtu gani mbaya anakusababishia mkwamo katika maisha kisha utatafuta njia mbadala za kuachana na jambo hilo kwa amani!

 

2.       Inzi wanakupa taarifa ya jambo jipya kutokea katika maisha yako – Ishara ya nzi sio tu wakati wote ni mbaya kama watu wanavyodhani lakini wanapokuandama inamaanisha kuwa kuwa kuna kitu kinaenda kuisha au kufikia mwisho katika maisha yako  na jambo jipya kabisa linaenda kutokea katika maisha yako, ni ishara ya kuisha kwa jambo Fulani katika maisha yako na kuanza kwa jambo jipya kabisa, hivyo kuwaona inzi wazi wazi kabisa au kwenye ndoto  ni ujumbe ambao unakueleza kuangalia jambo jipya kabisa katika maisha yako, a kulipokea vizuri kwani mabadiliko hayo yanaweza kuleta  nafasi usiyoitarajia.

 

3.       Inzi wanakupa taarifa ya kwamba kuna jambo linalokuondolea umakini - aidha unalijua au hulijui kama ni mtu aidha unamjua au humjui anakunyima usingizi, anakusumbua au ndio sababu ya kuharibikiwa kwako na kukuletea migandamizo katika moyo , unapoona inzi fikiria kwa kina kama kuna mtu katika maisha yako uwe unamjua au humjui anasababisha mabaya katika maisha yako iwe unajua au hujui, mtu huyo lazima umfanyie mkakati wa kumuacha au kuharibu nguvu anayoitumia kuharibu maisha yako mtu huyo aondoke au uache mawasiliano naye katika maisha yako kabisa. Kumbuka isiwe kwa ugomvi Mungu ametuita katiia mani.

 

4.       Inzi wana ujumbe kuwa kuna watu au mtu unampuuzia  kama unavyoona inzi wanapotusumbua huwa tunawapuuza, na kuwafukuza kwa dharau japo nzi hao hawataenda mbali na wataendelea kutusumbua hii ni ishara kuwa kuna watu wanakuhitaji lakini unawapuuzia hujawapa kipaumbele, ni mtu au watu wanaokupenda sana lakini umewapuuzia, au ni marafiki wa maana sana lakini umewapuuzia, inawezekana hata wakituma ujumbe unawapuuzia hujibu,  anza kujihoji kwa makini, na kwa uangalifu mkubwa kama umepuuzia na kuharibu urafiki na watu muhimu katika maisha yako au umeshindwakugundua umuhimu wa watu hao tunza na kurudisha urafiki haraka imarisha mahusiano na wote walio muhimu kwenye maisha yako

 

5.       Inzi wanakupa taarifa wazi kuwa unakabiliwa na hofu – Hofu hii ni hofu ya kupoteza mtu wa karibu sana umpendaye au kupoteza kazi, labda mambo hayaendi vizuri kazini na una mashaka ya kupoteza kazi hivyo kuna hofu inaanza kujengeka ndani yako, inzi wanakutaarifu kuhusu hofu yako ili uweze kujihami mapema kwa kufikiri kuondoka kazini au kutafuta kazi nyingine ambayo itaendana na hisia zako na kuachana na ile inayokupa mikandamizo ya moyo.

 

6.       Inzi wanawakilisha uwezo wako wa kukabiliana na mazingira – Inzi wanakupa ujumbe kwamba wewe sio wa kupuuzwa kuna nguvu kubwa ndani yako ya kukabiliana na mazingira nzi wanauwezo wa kuishi kokote na katika mazingira yoyote yawe mazuri au mabaya, wanauwezo wa kujipatia chakula hata katika mazingira yanayofikiriwa kuwa hayafai,  wana wanakupa ujumbe kuwa hata wakikutupa kama taka taka wewe ni hazina kwa wengine, inzi wanakupa ujumbe wa kufanikiwa, kuwa na vingi sana kuwa tajiri, kuwa na uwezo mkubwa wa kuhamasisha watu kuwa na uwezo wa kuishi katika mazingira hata ya kukataliwa, uwezo mkubwa wa kuvumilia magumu, huku ukiendelea na maisha na kujitafutia chakula , inzi wanakukumbusha kuwa wewe ni mtu mgumu sana  na unaweza kukabiliana na mazingira yoyote yanayobadilika, yawe mazuri au mabaya.

 

7.       Inzi wanakukumbusha kuwa una hasira -  na kwamba unatakiwa kumudu hasira yako, katika maisha, inzi hatuwezi kuwadhibiti sisi wenyewe  kwa msingi huo, hata hasira lazima tujifunze namna ya kuidhibiti ili isituletee madhara

Inzi wakiwa ni ishara mbaya

Inzi pia wana ujumbe mbaya na wa kuvunja moyo

1.       Inzi wanaujumbe wa kukutaarifu kuwa kuna jambo baya. – kuna jambo baya lisilopendeza, la kuudhi au lenye kuingilia mipango yako na kukuharibia kama vilevile tunavyoona inzi wakiwa wasumbufu, wenye maudhi na kutua tua katika mazingira tusiyoyapenda ndivyo wanavyoashiria kuwa kuna tukio litaingilia kati katika maisha yako kulete usumbufu, kukuharibia kukukatisha kukuudhi na kadhalika au jambo la kukuondolea amani, na au kukupa fadhaa, kiroho unajua nini unachopaswa kukifanya kuifuta hali hiyo.

 

2.       Inzi ni taarifa ya kifo – Kwa kawaida inzi pia wanapenda kitu kilichokufa au kilichooza au chenye harufu mbaya au shombo, nzi wanapoonekana katika ndoto au halisi wakiwa nyumbani kwako huashirikia kifo cha mtu aliye karibu sana na wewe ambaye hungependa afe  hata hivyo Inzi pia wana ishara ya ufufuo, kwa kuwa huzaliwa kama yai kisha buu kisha inzi hutokea kwa hiyo kuna ishara ya maisha mapya.

 

3.       Uwepo wa Inzi pia huashiria kuvunjika kwa mahusiano, - kwa hiyo watu wanapaswa kuzungumzia mahusiano yao ili ikiwezekana wayajenge kama wanaweza kuimarisha uhusiano wao na kila mmoja ajali hisia za mwenzake, kama watu hawataimarisha mahusiano yao ni dalili inayoonywa na nzi kuwa uhusiano unakwenda kuvunjika, inzi wanakupa ishara mbaya ya matukio mabaya ya kiroho, hivyo tunapowaona tunaweza kurekebisha hali ya mambo isiwe mbaya vinginevyo kitu kibaya kinakwenda kutokea na watu watafukuzana kama unavyofukuza inzi.

 

4.       Inzi wanashirikia haribiko – inaweza kuwa haribiko ambalo limekwishatokea au linalokwenda kutokea, labda ulikuwa ukifanya kazi na kuwafurahisha wanaokuzunguka na kukuajiri na umesahahu jambo muhimu sana unalotakiwa kulifanya sasa unapaswa kuangalia kile unachotakiwa kukifanyia kazi na kile kinachohusina na maisha yako, panga mipango yako mwenyewe na kaa katika hiyo ili uweze kufikia malengo, vunja malengo makubwa na angalia madogo ambayo unayamudu inaweza kuwa jambo sahihi kwako, kama unagundua kuwa umetoka katika mpango  anza kujipanga sasa panga mpango utakaokufaa ni rahisi kuwa kutokujisikia vizuri lakini itakusaidia kufanya mambo ya muhimu.

 

 

5.       Huwezi kufanya lolote – Inzi wanakupa ujumbe kuwa mambo yanayokutokea au yatakayokutokea  yako nje ya uwezo wako huwezi kuyadhibiti kinachokutokea kiko nje ya uwezo wako kama unavyoona inzi hujawaleta wewe unawaona tu na wanakuletea usumbufu ndivyo ilivyo katika maswala yanayokutokea au yatakayokutokea  kwa imani kumbuka tu kuwa Mungu anatawala.

Mambo ya msingi yakupasayo kufanya

Hakuna sababu ya kuogopa unapoona inzi katika nyumba yako, hawako hapo kwa makusudi ya kukutisha lakini wako hapo kukupa ujumbe kuhusu mambo yajayo, hivyo jipange jipe moyo kaa tayari kukabiliana na lolote litakalokusibu, weka moyo wako kwenye mipango yako, wasiliana na watu muhimu sana katika maisha yako, fanya kazi kwa bidii weka mahusiano yako vizuri, usiogope jambo baya wala taarifa mbaya jiandae kukabiliana na lolote gumu litakalokukabili, Muombe sana Mungu kwa kuahirisha mambo mabaya na kumshihi Mungu alete mambo mema siku zote za maisha yako, hakikisha kuwa unakuwa safi kwani kama jinsi ambavyo inzi wanavutiwa na uchafu, lisiwepo ovu katika maisha yako litakalokuchafua.

KUMBUKA. Mafundisho haya ya katika shule za kinabii na kama imani yako inakinzana usitilie maanani wala usifundishe kanisani kwako!

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: