Jumatatu, 11 Septemba 2023

Wewe hutakuwa Mchukua habari leo!


2Samuel 18:19-21 “Basi Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akasema, Niende mbio sasa, nikampelekee mfalme habari, jinsi Bwana alivyomlipiza kisasi juu ya adui zake. Yoabu akamwambia, Wewe hutakuwa mchukua habari leo, siku nyingine utachukua habari; lakini leo hutachukua habari, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa. Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi mmoja, Nenda ukamwambie mfalme hayo uliyoyaona. Na huyo Mkushi akajiinamisha mbele ya Yoabu, akaenda zake mbio.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maisha yetu duniani, kuna umuhimu mkubwa sana wa kujua muda sahihi na wakati sahihi ya kufanya wajibu Fulani ambao Mungu ameukusudia kwetu, hakuna jambo zuri sana katika maisha kama kujua Mungu anataka tufanye nini na kwa wakati sahihi,

Muhubiri 3:11 “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.”

Unaona kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake, hii maana yake Mungu ndiye anayedhibiti maisha na ana wakati mkamilifu kwa kila jambo chini ya mbingu, kwa msingi hio maisha yao na maisha yangu yako katiia mikono ya Mungu na Mungu amelifanya kila jambo kuwa jema kwa wakati wake!, Hakuna jambo linaloweza kufanyika nje ya wakati

Wagalatia 4:4-5 “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.”

Unaweza kuona Mungu hufanya mambo kwa wakati tena wakati unapowadia utimilifu wa wakati alioukusudia, hakuna jambo linalotokea kwa bahati mbaya lakini wakati wote Mungu hutimiza makusudi yake kwa wakati, kwa hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kila mmoja wetu kujua mapenzi ya Mungu ili tujue tunafanya nini kwa wakati upi katika mapenzi na makusudi ya Mungu, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

*      Umuhimu wa kufanya mambo kwa wakati

*      Hasara ya kufanya mambo nje ya wakati

*      Wakati wa Mungu ndio wakati sahihi

Umuhimu wa kufanya mambo kwa wakati.

Ni muhimu kufahamu kuwa neno wakati linalotumika katika Maandiko ya kiyunani ni neno KRONOS  ambalo kwa kiingereza linapatikana neno CHRONOLOGY  ambalo maana yeke ni mpangilio wa muda na matukio katika wakati sahihi na maalumu, maana yake ni kuwa uko mtiririko wa matukio yanayotokea katika mpango wa Mungu kwa wakati na waka sio kwa bahati mbaya liwe jambo jema ama baya, mungu anajua na amekusudia kila kitu kwa wakati na kila tukio katika maisha yetu kwa wakati, kwa hiyo hakuna bahati mbaya katika maisha ya watu wa Mungu, kila jambo limeratibiwa na Mbingu zina taarifa ujuzi na utatuzi wa kila matukio katika maisha yetu. Tumejifunza kuwa Yesu alikuja kwa wakati na alifanya kila jambo kwa wakati na matukio yote katika maisha yake yalitokana na kile ambacho Mungu alikuwa amekikusudia kwa wakati huo

Luka 2:1-6 “Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia,”

Tunajifunza namna Mungu anavyofanya kazi katika namna ya kushangaza sana huku kila kitu kikiwa kimeratibiwa katika maisha yake wote tunakumbuka kuwa Nabii Mika alitabiri kuwa Masihi atazaliwa Bethelehemu

Mika 5:2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.

Lakini wakati wa kuzaliwa kwa Masihi ulipowadia wazazi wa Yesu Kristo walikuwa wanaishi Nazareth lakini mfalme wa kipagani Kaisari Augusto alitoa amri ya watu kuhesabiwa na kuwa kila mmoja alipaswa kwenda kuhesabiwa kwao, tamko hili lilimlazimisha Yusufu na mariam kutembea kama kilomita 130 hivi kutoka Nazareth kwenda Bathelehemu na katika kulitimiza hilo Yesu alizaliwa Bathelehemu,  kwa hiyo utakubaliana nami kuwa Mungu hufanya kila jambo kwa wakati wake

Alianza kuhubiri kwa wakati – Ona Marko 1:14-15 “Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.”  

Hakukubali kufanya mambo kwa shinikizo la watu kabla ya wakati wake – Yohana 7:3-6 “Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. Maana hata nduguze hawakumwamini. Basi Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo.”

Adui zake hawangeweza kumfanya lolote kama wakati wake bado – ona Yohana 7:30 “Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.”

Adui zake wangeweza kumkamata pale tu wakati wake ulipowadia ona Marko 14:41 “Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi.”    

Unaweza kuona tunajifunza kwamba kila jambo linalotokea katika maisha yetu tuwe tunajua au hatujui linatokea katika wakati ambao Mungu ameukusudia, kama wakati wa Mungu bado hawawezi kutufanya lolote, wakati wa Mungu ukifika wenye dhambi watatuonea, hakuna linalotokea kwa bahati Mbaya Mungu anajua kila kitu na kila jambo limetaribiwa katika maisha yetu, watu wengi sana huniambia mimi nifungue kanisa na wananipangia kabisa lakini mimi najua wakati, siwezi kufanya kama watu wafanyavyo au washaurivyo, Maisha yangu hayako katika uwezo wao wala mpango wao yeye aliyeniokoa anajua alicjikiweka ndani yangu ana anajua katika ulimwengu huu natakiwa kufanya nini na kwa wakati gani, nimechunga kanisa zaidi ya miaka 12, na nimefundisha vyo vya biblia kwa miaka 12 na nimekuwa mkuu wa shule ya seminary kwa miaka 10,  najua huduma iliyo ndani yangu na najua Yesu anavyotaka kunitumia,  najua matumiziz yangu sio kama matumizi ya mkumbo, kuna namna yangu ambayo kwayo Mungu hunitumia na ukifika wakati atafanya wala shihitaji ushauri wa kibinadamu, Mungu amekwisha kuniandikia kile ambacho ninapaswa kukifanya na wakati sahihi wa kufanya hilo upo, Ndugu zake Yesu walimshauri atoke akahubiri ili ajulikana Yesu alijua kuwa huo haukuwa wakti wake, hatufanyi mambo kwa sababu watu wanaona na kusema wala kwa sababu watu wanafikiri hiki ndicho tunapaswa kukifanya Mungu aliyemuita kila mmoja kwa wakati anajua ni wakati gani na ni muda gani atamtumia kila mmoja kwa majira yake na nyakati zake, hivyo wale ambao wanadhani wanaweza kunishauri au kunipangia cha kufanya nawaomba wakome kabisa kwani maisha yangu hayako katika ratiba zao!

Mtu anaweza kuja kwako na kukuuliza mbona huoi au mbona huelewi, ni kosa kubwa sana ni swali lenye maumivu makubwa kama wewe ndiye ambaye hujaolewa afu mtu anakuuliza dada mbona huolewi, mbiona muda unaenda, mbona wenzako wanaolewa wewe vipi!  Sasa utajioa mwenyewe? Lakini Mungu anajua wakati kwa wakati uliokusudiwa utaolewa tu hakuna jambo linalotokea kwa bahati mbaya, Katika Mwanzo 24 Abrahamu alimtuma mtumizi wake Eliazari aende kwa Nahori ndugu yake kwaajili ya kumtafutia Isaka mke yule Mtumishi aliomba maombi haya kwaajili ya kupata mke sahihi ona

Mwanzo 24:10-14 “Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori. Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji. Naye akasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu.”

Unaona wakati Eliazari anaomba dua hii Msichana ambaye Mungu alikuwa amekusudiwa kuolewa na isaka alifika kwa wakati na alikuwa mzuri na alifanya kama vile mtumishi wa Abrahamu alivyoomba na mtumishi wa Ibrahimu alijua mara moja kwamba huyu ndiye binti sahihi aliyekuja kwa wakati sahihi na kufanya jambo lililo sahihi na mwisho wa siku ndiye aliyefaa kuwa mke wa Isaka ona

Mwanzo 24:15 -27 “Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda. Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe.Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba BWANA ameifanikisha safari yake ama sivyo. Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu, akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda? Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni. Yule mtu akainama akamsujudu BWANA.  Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. BWANA akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu.”

Unaona Mungu anajua majira ya kila kitu duniani, ni Mungu mwema sana ni mzuri mno atafanya kila jambo kwa wakati wake, ni binti hajaolewa ataolewa kwa wakati wake, hivyo hatupaswi kusikitika au kulalamika kwa kila kitu kama kila kitu kiko katika udhibiti wa Mungu, utazaa, kwa wakati, utaolewa kwa wakati, utapandishwa cheo kwa wakati, utafanikiwa kwa wakati, utapata Amani kwa wakati, utainuliwa kwa wakati, utapata cha kufanya kwa wakati, utapata kazi kwa wakati, maisha yako yatabadilika kwa wakati, waambie adui zako ni swala la Muda tu kwa wakati wake Mungu atafanya kuile ambacho amekikusudia katika maisha yangu, kila jambo limeratibiwa katika makudui ya Mungu, hata mapito ninayoyapitia ni kwa wakati tu.

Hasara ya kufanya mambo nje ya wakati.

2Samuel 18:19-21 “Basi Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akasema, Niende mbio sasa, nikampelekee mfalme habari, jinsi Bwana alivyomlipiza kisasi juu ya adui zake. Yoabu akamwambia, Wewe hutakuwa mchukua habari leo, siku nyingine utachukua habari; lakini leo hutachukua habari, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa. Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi mmoja, Nenda ukamwambie mfalme hayo uliyoyaona. Na huyo Mkushi akajiinamisha mbele ya Yoabu, akaenda zake mbio.”

Ni muhimu kufahamu kuwa kama tulivyojifunza kuwa Mungu hufanya mambo kwa wakati wake na tena kwa wakati sahihi, lakini kutokna na tabia zetu wanadamu za kukosa uvumilivu wakati mwingine tumekuwa na kiherehere cha kuharakisha mambo kabla ya wakati, tukidhani kuwa tutapata heshima inayokusudiwa na kumbe badala yake inaweza kuwa aibu, Katika kifungu tulichokisoma hapo juu na ambacho ndio kifungu cha msingi katika somo letu, tunamuona mtu anayeitwa Ahimaasi, huyu alikuwa ni mjumbe wa Mfalme daudi anayehusika na kupeleka habari njema kwa mfalme kwa hiyo alizoeleka hivyo na kwa kweli alikuwa mtu mwenye mbio sana kwa hiyo alikuwa anauwezo wa kufikisha habari kwa haraka, lakini siku alipouawa Absalom, Yoabu hakumtuma yeye kupeleka habari, kwa sababu habari zilikuwa mbaya ni siku ambayo mtoto wa mfalme amekufa hivyo Yoabu alimtuma Mkushi (Mu Ethiopia) apelike habari kwa mfalme siku ile Lakini hata hivyo Ahimaasi alilazimisha sana awe mpeleka habari siku ile jambo ambalo halikumletea heshima kabisa kama ilivyokuwa wakati mwingine ona

2Samuel 18:20-33 “Yoabu akamwambia, Wewe hutakuwa mchukua habari leo, siku nyingine utachukua habari; lakini leo hutachukua habari, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa. Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi mmoja, Nenda ukamwambie mfalme hayo uliyoyaona. Na huyo Mkushi akajiinamisha mbele ya Yoabu, akaenda zake mbio. Ndipo Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akamwambia Yoabu mara ya pili, Haidhuru, tafadhali nipe ruhusa, nipige mbio na mimi nyuma ya huyo Mkushi. Naye Yoabu akasema, Mbona wewe unataka kupiga mbio, mwanangu, kwa maana hutapata kitu kwa habari hizo unazopeleka? Akasema, Haidhuru, nitapiga mbio. Akamwambia, Haya, piga mbio. Ndipo Ahimaasi akapiga mbio, akishika njia ya uwandani, akampita yule Mkushi. Basi Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili; mlinzi akapanda juu hata dari ya lile lango hata ukutani, akainua macho yake, akaangalia, na tazama, mtu anakuja mbio peke yake. Mlinzi akalia, akamwambia mfalme. Naye mfalme akasema, Kama yu peke yake, ana habari kinywani mwake. Akaja mbio, akakaribia. Kisha huyo mlinzi akaona mtu mwingine anapiga mbio; mlinzi akamwita bawabu, akasema, Angalia, mtu mwingine anakuja mbio peke yake. Mfalme akasema, Huyu naye analeta habari. Na huyo mlinzi akasema, Nionavyo mimi, kupiga mbio kwake yule wa kwanza ni kama kupiga mbio kwake Ahimaasi, mwana wa Sadoki. Naye mfalme akasema, Yeye ni mtu mwema, anakuja na habari njema. Ahimaasi akainua sauti yake, akamwambia mfalme, Amani. Akainama mbele ya mfalme kifudifudi, akasema, Ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyewatoa watu hao walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme. Mfalme akauliza, Je! Yule kijana, Absalomu, yu salama? Ahimaasi akajibu, Yoabu aliponituma mimi mtumishi wa mfalme, mimi mtumishi wako, naliona kishindo kikubwa, lakini sikujua sababu yake. Naye mfalme akasema, Geuka, usimame hapa. Akageuka, akasimama. Na tazama, yule Mkushi akafika; Mkushi akasema, Nina habari kwa bwana wangu mfalme; kwa maana Bwana amekulipizia kisasi leo juu ya hao wote walioinuka kupigana nawe. Naye mfalme akamwambia yule Mkushi, Yule kijana, Absalomu, je! Yu salama? Yule Mkushi akajibu, Adui za bwana wangu mfalme, na wote wainukao ili kukudhuru, na wawe kama alivyo yule kijana. Naye mfalme akataabika sana, akapanda juu, akaingia kile chumba kilichokuwa juu ya lango, akalia; na katika kwenda kwake alisema hivi, Mwanangu Absalomu! Ee mwanangu! Mwanangu Absalomu! Laiti ningalikufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu!”

Unaona Ahimaasi hakupata Heshima inayokusudiwa kwa siku ile kwa sababu hakujua wakati sahihi ambao Mungu huwa anamtumia, kimsingi hakuwa ameachishwa kuchukua habari, lakini Yoabu alijua kuwa siku ile haikuwa wakati sahihi wa yeye kuwa mchukua habari na hivyo alipata hasara, wako watu hutamani nafasi uliyo nayo uliyopewa na Mungu kwa majira na nyakati, wako tayari hata kufanya mapinduzi wakidhani ya kuwa wao wana mbio kuliko wewe labda wewe unaonekana uko polepole kama MKUSHI lakini hata wakipiga mbio hawatapata heshima inayokusudiwa kwa sababu Mungu hafanyi kwa sababu ya jitihada ya kibinadamu bali anafanya kulingana na mtu aliyemchagua yeye na kwa wakati alioukusudia ona 

Warumi 9:14-16 “Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”

Mungu huweka rehema zake kwa wale anaowachagua awatumie kwa wakati, wala sio kwa mtu atakaye au anayetamani, au ajuaye kupiga mbio bali yule ambaye Mungu ameamua kumrehemu mafanikio yoyote ambayo Mungu huyafanikisha kupitia watu huwa sio kwaajili ya akili au uwezo wa kibinadamu au maguvu na uwezo wa kukimbia no hapana Bali kuna rehema ya Mungu juu ya mtu ambaye Mungu amemchagua na kuamua kufanikisha mambo kwa mkono wake asomaye na afahamu, Mungu huonyesha hekima yake kwa kuchagua yale yaliyo manyionye, mapumbavu na yenye mapungufu ili kuonyesha kuwa Hekima ya kibinadamu haiwezi kufua dafu dhidi ya hekima ya Mungu

1Wakorintho 1:26-29 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.”  

Ahimaasi alipaswa kufahamu kuwa sio swala la mbio wala sio swala la uzoefu, wala bidi, alipaswa kukubaliana na Yoabu kuwa yeye hangefaa kuwa mchukua habari, katika siku ile jambo ambalo lingemletea Heshima lakini badala yake aliamua kukazana na kukimbia kuliko Mkushi, Ndugu zangu Hekima ya Mungu ni tofauti sana na Hekima ya kibinadamu, kuna hasara za kufanya mambo kabla ya wakati wa Mungu kwa sababu ya kutaka kufanya mambo nje ya wakati wa Mungu jambo hilo limewaponza watu wengi sana na utajikuta unaishi maisha ya majuto kila kitu kifanyike kwa wakati mkamilifu alioukusudia Mungu kumbuka wewe hutakuwa mchukua habari leo!, kama hujaitwa kwenye uchungaji hata kama unajua kuhubiri usikimbilie kuhubiri, usikimbilie kufanya huduma za kiimungu kabla ya wakati wako uliokusudiwa kwani kufanya hivyo kutakuletea kukosa heshima inayokusudiwa, usikimbilie kuchumbiwa tu ili mradi, usikimbilie lolote lile kabla ya wakati wa Mungu!  asomaye na afahamu !               

Wakati wa Mungu ndio wakati sahihi

Ni muhimu kila wakati kuutafuta uso wa Mungu ili tuweze kujua wakati sahihi wa kila jambo katika maisha yetu, na kama tumemuomba Mungu sana kuhusu jambo Fulani katika maisha yetu hatupaswi kamwe kukata tamaa, hata kama hali ya hewa inaonyesha kuwa mambo hayawezekani, mlango umefungwa kwa sababu ya fitina na majungu ya watu, unaona kuna ugumu kazini, unaona kuna shida kanisani, unaona kuna shida katika ndoa, unaona kuna shida katika uhusiano, unaona kuna mzigo mzito hali mbaya ya uchumi, mambo kuwa magumu, na changamoto zozote unazokutana nazo fahamu kuwa ni swala la Muda tu Mungu anaowakati sahihi kwa kila jambo katika maisha yako  na anajishughulisha sana na mambo yako, ana makusudi makubwa sana na maisha yako na kwa wakati wake atafanya

Ezekiel 12:21-25 “Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, ni mithali gani hii mliyo nayo katika nchi ya Israeli, mkisema, Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi. Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Nitaikomesha mithali hii, wasiitumie tena kama mithali katika Israeli; lakini uwaambie, Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote. Kwa maana hayatakuwapo tena maono yo yote ya ubatili, wala ubashiri wa kujipendekeza, katika nyumba ya Israeli. Maana mimi ni BWANA; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena; maana katika siku zenu, Ewe nyumba iliyoasi, nitalinena neno hilo na kulitimiza, asema Bwana MUNGU.”

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!     

Hakuna maoni: